Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Posts Tagged ‘Tanzania

Vitabu 53 nilivyosoma mwaka 2016

with 7 comments

Vitabu 53 nilivyosoma mwaka 2016

Zitto Kabwe

The Strongman: Vladimir Putin and struggle for Russia – Augus Roxburgh

The Strongman: Vladimir Putin and struggle for Russia – Augus Roxburgh

Mwaka 2016 nimesoma vitabu 53. Nimeongeza vitabu nilivyosoma tofauti na mwaka 2015 lakini sikuweza kufikia idadi ya mwaka 2014 ambapo nilisoma vitabu 56. Hiyo ndio rekodi ya juu zaidi tangu nilipoanza kuorodhesha vitabu nilivyosoma mnamo mwaka 2012. Mwaka 2013 niliorodhesha vitabu vichache zaidi nilivyosoma.

Mafanikio makubwa ya mwaka huu ni kuongeza vitabu vya Riwaya (fiction), ingawa mtaona mwandishi mmoja, Jeffrey Archer amejitokeza sana kuliko wengine. Hiyo ni kutokana na kusoma kazi yake moja nzuri na yenye mafunzo mengi sana kwa wanasiasa iitwayo First Among Equals. Kazi hiyo ilinifungua macho na kuanza kusoma Clifton Chronicles (vitabu 7) na kufuatia mapendekezo ya wanaonifuata kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram niliweza kupata vitabu vingine vya mwandishi huyu. Kwangu mimi Bwana Jeffrey Archer ni Mwandishi wa Riwaya Bora wa Mwaka 2016.

Licha kutaka kuanza na Gavana Ben Bernanke, nilijikuta naanza na vitabu kuhusu Russia na Rais wa nchi hiyo Vladimir Putin. Msukumo huo ulitokana na namna nilivyomsoma Mtawala mpya wa Tanzania Rais John Magufuli kulinganisha na Kiongozi wa zamani wa nchi yetu Rais Jakaya Kikwete. Kitabu nilichoanza nacho mwaka 2016 ni The Strongman: Vladimir Putin and the Struggle for Russia kilichoandikwa na Angus Roxburgh. Baada ya kusoma kitabu hiki nilijikuta ninanunua vitabu vingi kuhusu Urusi, Putin, Udikteta, Demokrasia na Maendeleo ili kuweza kuelewa mwelekeo wa Siasa za Tanzania za sasa. Vitabu hivyo vimenisaidia sana kujua namna ya kutafsiri watawala wapya kiasi cha kuunda neno Dikteta Mamboleo (neo-dictatorship) na kuipa tafsiri yake mnamo tarehe 29 Septemba 2016; kwamba Dikteta Mamboleo ni mtawala ambaye ana uzalendo usio tiliwa shaka na anahangaika kuleta maendeleo ya nchi yake lakini hataki kuhojiwa kwa namna yeyote ile.

Mwaka 2016 pia ulinifunua kuhusu uwezo mkubwa na umahiri wa wachapishaji wa Vitabu wa ndani. Nilipata fursa adhimu ya kuzungumza na Mzee Walter Bgoya wa Mkuki na Nyota Publishers. Vitabu kadhaa nilivyosoma katika orodha ya mwaka huu vimechapishwa na Mkuki na Nyota. Nilijifunza mengi mapya ya historia ya nchi yetu na Afrika nzima. Juzuu za masimulizi ya Ukombozi wa Kusini mwa Afrika nilizipata kutoka Mkuki na Nyota na humo nilipata mambo mapya mengi sana. Kisa kimoja kinachonichekesha kila nikumbukapo ni hadithi ya Rais Khama (baba) wa Botswana alivyobeba machungwa kwenye ndege kumletea zawadi Mwalimu Nyerere akimtania kuwa sera zake za Ujamaa zilileta njaa nchini.

Mwaka huu ninawawekea mapema vitabu nilivyosoma tofauti na miaka iliyopita kwa sababu kwa uwezo wake Manani sitaweza kusoma vitabu vingine baada ya leo kwani nitakuwa na majukumu ya malezi. Karibu kwenye orodha ya vitabu vyangu mwaka 2016.

  1. The Strongman: Vladimir Putin and struggle for Russia – Augus Roxburgh
  2. Putin’s Progress – Peter Truscott
  3. The Putin Mystique: Inside Russia’s Power Cult – Anna Arutunyan
  4. The Invention of Russia: The Journey from Gorbachev’s Freedom to Putin’s War – Arkady Ostrovsky
  5. I am going to Ruin Their Lives: Inside Putin’s War on Russian Opposition – Marc Bennet
  6. Red Notice: How I became Putin’s no 1 enemy: Bill Browell
  7. Ruling Russia: Authoritarianism from the Revolution to Putin – William Zimmerman
  8. Dictator’s Learning Curve: Inside the global debate for Democracy – William Dobson
  9. Dictator’s Handbook: Why bad behavior is almost good politics – Bruce Buener de Mesquita and Alastair Smith
  10. Dictator – Tom Cain
  11. The Warlord- James Steel
  12. Tanzania: A Political Economy ( 2nd Ed ) – Andrew Coulson
  13. Thieves of the State: Why corruption threatens global security – Sarah Chayes
  14. How to Run A Country – Marcus Tullius Cicero
  15. The End of Karma: Hope and fury among India’s young – Somini Sengupta
  16. The Hidden Wealth of Nations: The scourge of tax havens – Gabriel Zucman
  17. Mystery of Capital – Hernando De Soto
  18. So long a letter – Mariama Ba ( Special thanks to January Makamba for recommending this to Bunge Readers’ Club )
  19. The Fifth Mountain – Paulo Coelho
  20. First Among Equals – J. Archer
  21. Kane and Abel – J. Archer
  22. Best Kept Secret – J. Archer
  23. The Sins of the Father – J. Archer
  24. Only Time Will Tell – J. Archer
  25. Shall we Tell the President – J. Archer
  26. Mightier Than The Sword – J. Archer
  27. The Fourth Estate – J. Archer
  28. Honour Among Thieves – J. Archer
  29. Cometh The Hour – J. Archer
  30. This was a Man – J. Archer
  31. The New Collected Short Stories – J. Archer
  32. Building a Peaceful Nation – Bjerk
  33. Burundi Peace Dialogue- Pierre Buyoya
  34. Burundi: The Biography of a small African Nation – Nigel Weltt
  35. The Thabo Mbeki I know – ed. Sifiso Mxolisi and Miranda Staydom (Special Thanks to Amb. Ami Mpungwe, a contributor to the very book)
  36. Clinton Cash – Peter Schweizer
  37. Connectography: Mapping the Global Network Revolution – Parag Khanna
  38. The Rohingyas: Inside Myanmar’s Hidden Genocide – Azeem Ibrahim
  39. Stringer: A Reporter’s Journey in the Congo – Anjan Sundaram
  40. Uchambuzi wa Sera, Uongozi na Maslahi ya Watanzania – CSL Chachage
  41. Haki, Amani na Maendeleo: Nafasi na Wajibu wa Mahakama Tanzania – S J Bwana
  42. Wanawake wa TANU – Susan Geiger (a special thanks to my wife for bringing this home)
  43. African Socialism or Socialist Africa – A M Babu ( Special Thanks to Dr. Khamis Kigwangalla for suggesting it to Bunge Readers Club and Ezekiel Kamwaga who lent it to me )
  44. The Courage to Act – Ben Bernanke
  45. The Litigators – John Grisham
  46. White Lioness – Henning Mankell
  47. The Dogs of Riga – H. Mankell
  48. Fifth Woman – H. Mankell
  49. Kennedy’s Brain – H. Mankell
  50. Treachorous Paradise – H. Mankell
  51. Harusi ya Dogoli – Athumani Mauya
  52. Mlinzi Mkuu wa Mwalimu Nyerere – Peter Bwimbo
  53. The Hashim Mbita Project: Southern African Liberation Struggles Contemporaneous documents ( 1960 – 1994 Volumes 1, 3, 5, 6 & 7 ) – Ed. A J Temu and J N Tembe

Written by zittokabwe

December 20, 2016 at 6:01 PM

UCHAMBUZI WA BAJETI YA SERIKALI 2016/17 @ACTWazalendo @zittokabwe

with 2 comments

Written by zittokabwe

June 13, 2016 at 12:06 PM

ACT WAZALENDO TABORA DECLARATION(ABRIDGED ENGLISH VERSION) @ACTWazalendo

with 2 comments

Written by zittokabwe

June 17, 2015 at 5:14 PM

Yaliyojificha kuporomoka kwa shilingi dhidi ya Dola ya Marekani Shilingi inahujumiwa na Mabenki?

with one comment

Yaliyojificha kuporomoka kwa shilingi dhidi ya Dola ya Marekani

Shilingi inahujumiwa na Mabenki? – Zitto Kabwe[1]

Katika ukurasa wangu wa facebook mnamo tarehe 25 Aprili 2015 niliandika kuhusu sababu za shilingi kuporomoka thamani na majawabu ya namna ya kurejesha thamani halisi ya sarafu yetu. Nilieleza “Shilingi kuporomoka dhidi ya dola na kuvuka 1$/2000TS kunasababishwa na sababu kadhaa 1) Woga wa uchaguzi na hivyo Dola nyingi kutoingia nchini (FDI etc) kusikilizia Serikali ijayo inaundwaje 2) Woga wa uchaguzi na hivyo matajiri kununua dola kwa kasi (too many Tshs chasing too few $) ili kuzificha (hoard) nje 3) kutouza mazao nje na kuagiza bidhaa nyingi kutoka nje ( current account deficit) 4) Benki Kuu kutoachia $ nyingi kwenye soko kutokana na akiba ya fedha za kigeni kupungua 5) Kuongezeka kwa huduma ya Deni la Taifa ambapo malipo ni kwa fedha za kigeni kwa madeni yaliyo wiva.

Niliendelea kushauri majawabu “Suluhisho 1) Benki Kuu kuachia $ za kutosha kwenye soko katika muda mfupi na wa kati (Mwezi Februari BoT ilifanya hivi na kuongeza $64 milioni kwneye soko bila mafanikio[2] 2) Kuongeza mauzo nje hasa ukizingatia kwa sasa ‘our exports becomes cheaper vis a vis foreign exchange) 3) Malipo ya kodi ya Ongezeko la Mtaji kutoka BG (Shell transaction ) na Ophir (Pavilion transaction), malipo haya kwa fedha za kigeni 4) Punguza kununua vitu vya anasa kutoka nje 5) Unafuu wa huduma kwa Deni la Taifa ( Debt relief ) 6) Punguza ujazo wa fedha nchini (mop tshs out)”.

Mjadala mkali umeendelea kuhusu suala hili katika majukwaa mbali mbali. Ni dhahiri kuporomoka kwa shilingi kunaathiri sana Watanzania wa ngazi ya kati hasa wafanyabiashara wa kati wenye kununua huduma na bidhaa kutoka nje. Wenye viwanda wanaotegemea malighafi kutoka nje gharama zao za uzalishaji zimeongezeka zaidi na hivyo kuhatarisha uzalishaji mali nchini. Licha ya kwamba kuporomoka kwa shilingi kunafanya bidhaa zetu za kuuza nje kuwa rahisi, lakini huchukua muda kuzalisha bidhaa hizo na hasa kilimo kuweza kufaidika hali hiyo. Kwa hiyo ni faida kwa nchi kwa sasa kuwa na sarafu stahmilivu ( stable) iliyojengwa kwenye misingi imara ya Uchumi. Hata hivyo, inaonekana kuwa sarafu ya Tanzania inahujumiwa. Kuporomoka kwa Shilingi katika wiki za hivi karibuni sio matokeo ya nguvu za soko bali ni matokeo ya hujuma ( currency manipulations).

Mabenki makubwa ya kigeni nchini, inasemekana, katika miezi ya karibuni yamefanya currency manipulations na kupelekea dola chache kukimbizwa na shilingi nyingi na hivyo bei ya dola kupanda bei. Hii inatokana na ukweli kwamba Benki zetu kubwa tatu zinazoongoza zinaendeshwa na wageni. Inasemekana biashara hii hufanyika kati ya matawi ya Benki za kigeni hapa nchini na makao makuu yao. Kuporomoka kwa shilingi kunakotokea hivi sasa hakuendani na kuporomoka kwa miaka ya nyuma kipindi kama hiki (ambacho ki kawaida ni miezi shilingi hushuka thamani kwa sababu ya watalii kuwa wachache na mauzo ya bidhaa nje kuwa madogo sana). Wastani wa miaka 10 iliyopita inaonyesha kuwa kipindi hiki shilingi hushuka kwa kati ya 8% mpaka 13% na sio kuporomoka kwa zaidi ya 20% kulikotokea hivi sasa. Kwa mfano mwaka 2011 miezi kama hii ( Februari – Mei) Shilingi iliporomoka kutoka shs 1,380 kwa dola 1 mpaka shs 1,570 sawa na mporomoko wa 12%. Hata hivyo kuanzia mwaka huo mpaka mwaka 2014 shilingi imekuwa ikishuka thamani kwa kiwango kidogo sana. Mwaka 2013 thamani ya shilingi ilishuka kwa wastani wa asilimia 1.7 tu.

Uchambuzi huu wa thamani ya sarafu yetu unaonyesha kuwa kuna zaidi ya nguvu ya soko kunakotokana na mauzo yetu nje kuwa machache. Vile vile kupanda kwa thamani ya dola ya marekani duniani hakutoshi kuelezea mporomoko huu wa kasi wa shilingi kuanzia mwezi Disemba mwaka 2014 mpaka sasa. Tuhuma za mabenki kuwa yanahujumu shilingi (currency manipulations) zaweza kuwa na ukweli.

Vile vile, inasemekana kumekuwa na utoroshaji mkubwa wa dola kutoka nchini kwenda nje ya nchi. Utoroshaji huu unafanyika kupitia wasafiri wanaopita ukumbi wa VIP uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es Salaam. Utoroshwaji huu unatokana na hofu isiyo ya msingi kwamba uchaguzi utakuwa na vurugu. Utoroshwaji wa fedha ni kinyume sheria zetu. Sheria zetu za fedha za kigeni zinazuia mtu kubeba zaidi ya dola 10,000 za kimarekani zikiwa taslimu, kuingia nazo nchini au kutoka nazo nchini. Tafiti za haraka zinaonyesha kuwa huu umekuwa ni utaratibu wa kawaida kila mwaka wa uchaguzi tangu mfumo wa vyama vingi uanze.

Benki Kuu ya Tanzania inapaswa kuchukua hatua zifuatazo;

  1. Kufanya uchunguzi wa kushtukiza mara moja dhidi ya benki zote za kigeni zilizopo hapa nchini. Uchunguzi huu utazame biashara ya fedha za kigeni ya benki hizi kwa lengo la kuzuia ‘ currency manipulations’ na kuchukua hatua madhubuti dhidi ya Benki yeyote itakayokutwa imehujumu biashara ya fedha za kigeni kwa lengo la kushusha thamani ya shilingi dhidi ya dola za kimarekani.
  2. Jeshi la Polisi na kitengo cha kuzuia utoroshaji wa fedha ( anti money laundering unit) kufanya ukaguzi wa lazima wa watu wote wanaosafiri kwenda nje ikiwemo wanaopita sehemu ya watu mashuhuri (VIP Lounge) ili kudhibiti utoroshaji wa fedha za kigeni kwenda ughaibuni.
  3. Watanzania tufikirie upya nafasi ya Mabenki katika uchumi wa nchi na kufanya maamuzi magumu ya kurejesha baadhi ya Benki katika umiliki mpana zaidi wa Watanzania. Kwa malengo ya muda wa kati, Benki kubwa 3 nchini ilazimu kuwa na umiliki unaozidi 51% wa Watanzania. Bila ya kushika mabenki nchi itachezewa sana.
  4. Suluhiho la kudumu la sarafu stahmilivu ni kuongeza uzalishaji wa bidhaa za kuuza nje ya nchi na kupunguza manunuzi ya bidhaa kutoka nje. Urari wa Biashara wa Tanzania umepanuka kutoka $1bn mwaka 2004 mpaka $6bn mwaka 2013 (BOT 2013) kutokana manunuzi yetu nje kukua kwa kasi kutoka $2.5bn mpaka $11bn wakati mauzo yetu nje yakikua kwa kasi ndogo kutoka $1.4bn mpaka $5bn katika kipindi hicho. Isingekuwa uimara katika urari katika uwekezaji na uhamisho wa mitaji, Tanzania ingekuwa na sarafu yenye thamani sawa na takataka. Serikali ihimize uzalishaji mali mashambani na viwandani na kuuza nje biadhaa zilizoongezwa thamani. Zama za kutegemea dhahabu zimekwisha na sio endelevu. Turudi kwenye misingi: Bidhaa za Kilimo na Viwanda.

Tutaendelea kufuatilia thamani ya shilingi mpaka ifikapo mwezi Julai ambapo ndipo kipindi kigumu kwa shilingi huwa kihistoria. Hatua zilizoainishwa zisipotazamwa na mamlaka tajwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani yaweza kufikia tshs 3000!

[1] Zitto Kabwe ni Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo. Amepata kuwa Waziri Kivuli wa Fedha na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya PAC

[2] Benki Kuu kuingiza $ kwenye soko kuna hatarisha kupunguza Akiba ya fedha za Kigeni. Kutokana na ujinai unaoendelea kwenye soko la fedha za kigeni nchini, BoT kuendelea kumwaga fedha za kigeni inaweza kuwa ni mkakati wa kudumu wa wanaofaidika na ‘currency manipulations’. Kushinikiza Benki Kuu kuendelea kubomoa foreign reserve ni kutokuona mbali na kujaribu kujiridhisha kwa kutibu dalili za ugonjwa badala ya ugonjwa wenyewe.

Written by zittokabwe

May 3, 2015 at 10:40 AM

Katiba ya ACT-Wazalendo Kama Ilivyopitishwa Na Mkutano Mkuu 29Machi15

with 19 comments

Alliance for Change and Transparency

(ACT-Wazalendo)

Chama cha Wazalendo

KATIBA

TOLEO LA 2015

View this document on Scribd

Turejeshe nchi yetu Tanzania!-Hotuba ya Mzalendo Zitto Kabwe #ACTWazalendo @ACTWazalendo

with 10 comments

Turejeshe nchi yetu Tanzania!

Turejeshe nchi yetu Tanzania!

Turejeshe nchi yetu Tanzania!

Watanzania wenzangu, wageni waalikwa

Nawashukuru kwa kuwa pamoja nasi siku hii ya kihistoria.

Karibu Miaka 54 iliyopita tulipopata uhuru, Muasisi na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa kijana mwenye umri wa miaka 39, mwenye matumaini makubwa na taifa jipya na alikuwa na ndoto! Ndoto yake ilikuwa imejikita katika kuhakikisha taifa letu litakuwa taifa lisilo na umaskini, dhiki, ufukara; taifa lisilo na tofauti kubwa kati ya maskini na tajiri; taifa lenye usawa, haki na maendeleo, ambapo watoto wote wanasoma shule bila kujali kipato cha mzazi; taifa ambalo wananchi wake wanamiliki uchumi wao.

Ndoto hii aliiamini kwa dhati na wananchi wote walikubali na kuota nae ndoto hii. Alilisimamia kwa maneno na vitendo kupitia Azimio la Arusha, sera zake na uongozi wake wa kizalendo. Mpaka mauti ilipomkuta aliamini katika misingi hii aliyojitahidi kuturithisha. Lakini miaka 16 baada ya kifo chake, ndoto yake imeyeyuka!

Tulilonalo ni jinamizi alilolihofu Nyerere.

Leo hii:
Watanzania wachache wameondoka katika unyonge na dhiki.
Watanzania wengi bado wapo katika hali ya dhiki.
Watanzania wachache wameshikilia uchumi: Warasimu, Wanasiasa na Matajiri wachache wenye mitaji.
Watanzania wengi bado kama Mwalimu Nyerere alivyosema “wananyonywa kiasi cha kutosha; wanapuuzwa kiasi cha kutosha”.
Ndoto ya Mwalimu Nyerere bado haijawafikia wananchi.

Sasa ndio wakati wa mabadiliko ya kimapinduzi.

Sasa ndio wakati wa kujenga Uchumi shirikishi ambao utaruhusu kila mwananchi kupata fursa ya kuboresha maisha yake;

Sasa ndio wakati dola imara ipate nafasi ya kusimamia uchumi;

Sasa ndio wakati kwa wananchi kuwa na uhuru wa kweli wa mawazo, fikra, kushirikiana, kuabudu;
Sasa ndio wakati wananchi kuwa na nguvu ya kuwawajibisha viongozi wao;

Sasa ndio wakati wetu watanzania kujirithisha upya nchi yetu!

Huu ndio wakati wa kubomoa uchumi wa kinyonyaji na kifisadi na kujenga uchumi wa wananchi. Haya ndio mabadiliko ya kimapinduzi tunayoyataka. Hii ndiyo ilikuwa ndoto ya Mwalimu Nyerere, na muda umefika wananchi turejeshe nchi mikononi mwetu!
Haya yamekuwa mawazo yangu kwa muda mrefu kwa sababu mimi ni zao la ndoto ya Mwalimu Nyerere. Nililelewa na mama yangu mzazi pekee mwenye ulemavu; nimeanza kusoma shule ya msingi nikiwa naenda peku. Lakini kutokana na kufaulu mitihani vizuri, sikuhitaji kuwa tajiri kusoma mpaka chuo kikuu. Leo hii kutokana na elimu bora niliyoipata bure, nimesafiri na kufika katika nchi zaidi ya 70; nikiwa kama kiongozi nimekutana na kubadilishana mawazo na watu muhimu duniani kama vile wakuu wa nchi. Sio mimi peke yangu bali tupo maelfu tuliofaidika na mfumo huu. Lakini muhimu kupita yote, nimeweza kutumikia wananchi wa Kigoma na watanzania bungeni kwa miaka 10. Kama hii si ndoto iliyokuja kuwa kweli, ni nini?

Zitto Zuberi Kabwe angezaliwa mwaka 2000, angekuwa kijana ambaye hajakamilisha elimu yake, haelewi lugha za kigeni kama kiingereza, hana ujuzi wowote na kama Mungu angeendelea kuninyima kipaji cha kuimba kama sasa ningeshindwa hata kutoka kama Diamond na Mwana FA! Mwalimu Nyerere asingepigania ndoto yake miaka ya 60 na 70, ningekuwa kama mamilioni ya vijana leo ambao wanahangaika kutafuta ajira na kipato bila ujuzi na elimu.

Na ndiyo maana siku ya leo ni muhimu kwangu. Nina furaha na heshima kubwa kuwa katika familia yangu mpya ya kisiasa. Familia inayoaamini katika itikadi, misingi na tunu ninazoziamini.

Nimezungumza mara kadhaa kuhusu sababu za kujiunga na chama hiki. Chama cha Wazalendo ACT- Tanzania inaongozwa na misingi ya Uzalendo, Demokarsia, Uhuru wa fikra na matendo, Utu, Usawa, Uadilifu, Uwazi, Uwajibikaji na Umoja katika kila kitu. Chama hiki ni cha wananchi si wenyenchi wa sasa waliojimilikisha taifa. Chama hiki ni cha watanzania wote bila kujali kabila, dini, jinsia, rangi ya ngozi au hali ya ulemavu!
Tunapojadili wananchi kujimilikisha upya nchi yetu ni kupitia usimamizi wa sheria utakaohakikisha kuwa kuna uwazi na uwajibikaji wa viongozi. Uwazi tunaouamini ni ule utakaohakikisha kila mwananchi anapata taarifa za fedha zao, mikataba ambayo Serikali inaingia kwa niaba yao na taarifa za maslahi, mali na madeni ya viongozi wao. Tunataka uwazi katika uendeshaji wa Serikali na sisi tutaanza na uwazi katika uendeshaji wa chama chetu. Tunataka wananchi sio tu wajione kuwa sehemu ya uendeshaji wa nchi yao, bali pia wawe sehemu ya uendeshaji wa nchi yao.

Tunataka uwazi utakaoruhusu uhuru wa mawazo na uhuru wa wananchi kujieleza bila kuhofu Serikali kuwachukulia hatua kwa kutoa mawazo yao. Ndio maana ACT Wazalendo tunapinga vikali miswada ya sheria ambayo Serikali ya CCM imeiwasilisha bungeni katika mkutano unaoendelea. Miswada hii kama vile muswada wa Haki ya kupata taarifa, vyombo vya habari na ule wa makosa ya mtandao, inalenga kuminya na kunyima haki za wananchi kuwasiliana kwa uhuru na kutoa mawazo yao kama inavyoainishwa katika katiba ya nchi.

Tunapojadili wananchi kurejesha taifa mikononi mwao tunazungumzia uwajibikaji. Ripoti ya Tume ya Marekebisho ya Katiba ilieleza moja ya sababu kubwa ya kushamiri rushwa, ufisadi na ubadhirifu nchini ni nanukuu ‘kukosekana kwa mfumo madhubuti wa uwajibikaji’ nchini kwetu. Sababu kubwa ya ACT Wazalendo kupinga Katiba inayopendekezwa ni kwamba Katiba hiyo imechakachua nia hii ya kuweka mfumo wa uwajibikaji. Ndio maana tunawaambia wananchi waikatae Katiba hiyo kwa nguvu zao zote! Katiba inayoepndekezwa inastahili kadi nyekundu, tuikatae na kura ya hapana!
Iwapo wananchi hawawezi kuwawajibisha viongozi kwa matendo yao hatuwezi kujenga jamii ya watu wanaoheshimiana na kutii sheria za nchi.

Kila Mtanzania bila ya kujali cheo chake ni lazima awe chini ya sheria. Uwajibikaji ni lazima uanze na viongozi. Mnajua kuwa katika maisha yangu ya kisiasa hili ndio limekuwa jukwaa langu. Kwa bahati mbaya tunaishi katika kipindi ambacho wanasiasa wengi wamekuwa wakikumbwa na kashfa mbalimbali za kifisadi na matokeo yake inajengwa picha kuwa kila mwanasiasa ni fisadi. Mfumo wa Uwajibikaji wenye uwazi utasaidia wananchi kutofautisha wanasiasa wanaosimamia maslahi ya umma na wale wanaosimamia maslahi yao binafsi na vyama vyao vya siasa.

Mwungwana ni vitendo; nimewajibisha watu kwenye Buzwagi na mikataba ya madini, kwenye matumizi mabaya ya fedha za umma na juzi juzi kwenye akaunti ya Tegeta Escrow. Lakini matukio haya machache hayatoshi kujenga mfumo madhubuti wa Uwajibikaji. Ni lazima kufanya mapinduzi ya mfumo mzima wa uchumi wa nchi yetu na kujenga mfumo mpya unaohudumia kila Mtanzania na ambao kila Mtanzania anajivunia kuujenga. Hatuwezi kuwa Taifa linaloshikiliwa na vikundi vya wafanyabishara wachache na wanasiasa wanaofadhiliwa na wafanyabishara hao.

ACT Wazalendo inataka kujenga Taifa ambalo viongozi wake wanawajibika kwa wananchi. Hii ndio fikra tunayotaka kurejesha. Hizi ndizo siasa zilizoasisi Taifa letu. Hatuna budi, ni lazima kurudi kwenye misingi na kuanza upya!
Kwa sababu ACT Wazalendo imejikita kwenye misingi hii, tumelihuisha Azimio la Arusha.

Sio tu tumeweka miiko ya uongozi lakini pia tumetunga kanuni za kutekeleza miiko hiyo na kuifanya kuwa sehemu ya Katiba ya chama chetu. Hitaji moja kubwa la Kanuni zetu za Maadili ni kutaka kila Kiongozi wa ACT Wazalendo kuweka hadharani Maslahi yake, Mali na Madeni yake.

Katika chama hiki huo ndio utamaduni wa kisiasa tunaotaka kuujenga. Kutenda tunachohubiri hata kabla ya kuingia kwenye uongozi wa Dola.

Chama cha ACT Wazalendo kimeelekeza kikanuni kwamba kila Kiongozi wa chama lazima atangaze Mali zake na Madeni yake. Kila Kiongozi lazima aweke wazi maslahi yake ya kibiashara na mengineyo wazi ili kila anapotenda au kusema jambo wananchi wajue maslahi aliyonayo au la katika suala husika. Viongozi wote wa kitaifa wa ACT Wazalendo wamefanya hivyo na tutaweka saini zetu mbele yenu kama mashahidi. Naomba Mwanasheria wetu aje hapa tutekeleze matakwa haya ya kikanuni.

Fomu hizi zitakuwa kwenye tovuti ya chama ndani ya muda mfupi ujao ili kila mtanzaina aone. Kila Kiongozi wa Chama ambaye Miiko ya Uongozi inamtaja anapaswa kuwa amejaza fomu hizi na kuziwasilisha kwa Katibu wa Kamati ya Uadilifu katika ifikapo tarehe 30 Juni 2015. Tunapopinga Viongozi wa Umma kufanya Biashara na Serikali na hivyo kuwa na mgongano wa kimaslahi na kushamiri kwa ufisadi, hivyo hivyo tunapinga Viongozi wa Chama chetu kufanya Biashara na Chama. Ni Marufuku Serikali kugeuzwa kuwa genge la watu wachache wanaopora rasilimali za Umma. Uadilifu tunaoutaka Serikalini ni lazima uanzie kwetu tunaohubiri.

Tutafanya haya kwa kubadilisha siasa zetu kuelekea kwenye masuala yanayowahusu wananchi; Wakulima, Wafanyakazi, Wafanyabiashara ndogo ndogo, Vijana, Wanawake na Wazee wetu.

Tunataka kurejesha nchi yetu Tanzania kwa kujenga uchumi wa wote. Tunaporejea kwenye Azimio, hatusemi tunakwenda kutaifisha kila kitu na Serikali kuendesha shughuli zote za kiuchumi. Tunaheshimu na kuthamini sekta binafsi na mchango wake katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo. Tunamaanisha kuwa ni lazima Dola isimamie uchumi. Sio kazi ya Serikali kufanya biashara. Lakini tunamaanisha kuwa ni lazima kurekebisha baadhi ya makosa yaliyofanyika kwenye ubinafsishaji na hususan ubinafsishaji holela uliofanyika kwenye sekta ya Kilimo na kupora ardhi ya wananchi wetu na kuwageuza kuwa manamba kwenye ardhi yao wenyewe.

Tunataka kutomokeza ukwepaji kodi.

Tanzania inapoteza 15% ya makusanyo katika forodha kwa sababu ya ukwepaji wa kodi. Hii ni sawa na tshs 490 bilioni kwa mwaka, fedha ambazo zingeweza kuchangia wananchi milioni 4 kwenye hifadhi ya Jamii. Tanzania inapoteza takribani tshs 2 trilioni kila mwaka kwenye misamaha ya kodi. Hii ni fedha ambayo ingeweza kujenga reli mpya ya kati ya kisasa kutoka Dar mpaka Mwanza na Kigoma ndani ya miaka mitatu. Ili kuondoa upotevu huu ni lazima kupanua wigo wa kodi, kurahisisha kodi, kupunguza baadhi ya kodi kama ( PAYE) na kutumia teknolojia kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi.

Vile vile ni muhimu kuimarisha mfumo wetu wa kodi za kimataifa ili kuzuia utoroshaji mkubwa unaofanywa na makampuni ya kigeni. Ili tujitegemee kama Taifa ni lazima kukusanya mapato ya ndani ya kutosha. Ili kukusanya mapato ya ndani ya kutosha ni lazima kuweka mazingira mazuri ya biashara hasa kwa wafanyabishara ndogo ndogo kwani ndio wazalishaji wakubwa wa ajira.

Kwa Vijana, Taifa hili ni lenu. Asilimia 75 ya Watanzania wapo chini ya miaka 40. Asilimia 65 ya wapiga kura wapo chini ya miaka 40. Nusu ya Watanzania ni watoto chini ya miaka 18. Kurejesha nchi kwenye misingi ni wajibu wa kujenga maisha yenu. Haikubaliki Vijana kuwa mzigo kwa wazazi kwa sababu tu uchumi hauzalishi ajira za kutosha. ACT Wazalendo ndio jukwaa lenu la kufanya mapinduzi ya mfumo wa uchumi ili kujenga uchumi shirikishi unaozalisha ajira. ACT Wazalendo inataka kuwajengea mfumo wa hifadhi ya jamii ambapo mtakapokuwa Wazee msipate tabu za pensheni na matibabu wanazopata Wazee wetu hivi sasa. Shiriki kujijengea Taifa litakalohakikisha maisha yako ya sasa nay a baadae na ya kizazi kijacho.

Kwa Wanawake, Ninyi ndio mhimili wa Taifa hili, wazalishaji wakuu na walezi wa Taifa letu. Kurejesha nchi kwenye misingi ni wajibu wa kutambua nafasi yenu stahili katika jamii. Nikiwa nimelelewa na Mwanamke mwenye ulemavu na mpiganaji wa kweli wa haki za wananchi walio pembezoni, sina namna kutoa heshima yangu zaidi ya kuongoza chama chenye misingi thabiti ya kumkomboa mwanamke. Msitarajie watu wengine kuwapigania mnapaswa kuchukua hatua kupitia jukwaa hili la ACT Wazalendo.

Kwa wafanyabishara, ninyi ndio mnachochea shughuli za Uchumi na kuzalisha ajira. Kuanzia kwa wamiliki wa maduka madogo mitaani mpaka kwa mameneja wa maduka makubwa; kutoka kwa wachuuzi na mama lishe mpaka kwa wamiliki wa viwanda na biashara; mnaamka kila siku asubuhi kujenga Taifa hili kwa kuzalisha mali na huduma. Baadhi yenu ambao mnamiliki viwanda, mashirika makubwa na kutoa ajira kwa maelfu ya wananchi, mmeanza mkiwa mnashona viatu na sare za shule, au mkitengeneza na kuuza mkate. Mmepata utajiri wenu na mali zenu kwa juhudi na jasho lenu na kutokana na fursa za kiuchumi zilizokuwepo kipindi hicho ambacho hakikuangalia dini, kabila, uwezo wa kifedha au rangi ya ngozi. ACT Wazalendo inataka kuwawekea mazingira bora ya biashara halali lakini pia kuhakikisha mnalipa kodi zenu na kutonyonya wafanyakazi wenu. Tunataka kuwawekea mfumo rahisi wa kodi, wenye kueleweka na unaowapa motisha kuzalisha zaidi ili kuongeza ajira zaidi na kupanua Pato la Taifa. Msipotimiza wajibu wenu biashara zenu hazitashamiri. Kurudi kwenye misingi ya Taifa hili ni kurejesha maadili katika biashara zenu.

Kwa Wakulima, Wafugaji na Wavuvi, ninyi ndio mnaolilisha Taifa letu na kuleta fedha nyingi za kigeni kupitia mauzo nje. Kwa miongo mitatu sera za nchi zimewaweka pembeni na hivyo uchumi wenu kusinyaa. Viwanda vyote vya kusindika mazao yenu vimeuzwa kwa bei ya kutupwa licha ya kwamba jasho lenu ndio lilitumika kuvijenga. Miundombinu ya barabara, maji, umeme na mawasiliano haiwafikii ili muweze kupata masoko. Hamna hifadhi ya jamii wala bima ya mazao yenu. Ardhi yenu wamepewa wawekezaji na mnakodishiwa, mnapanga kwenye ardhi yenu wenyewe. Mmeachwa mkijihangaikia. Kurejesha nchi kwenye misingi kutawarudishia heshima yenu katika nchi yetu. ACT Wazalendo ndio jukwaa sahihi kwenu kuhakikisha kuwa tunajenga uchumi shirikishi ambao mtafaidika na jasho lenu. Hamna cha kupoteza isipokuwa minyororo ya kinyonyaji.

Kwa Watanzania wote mnaonisikiliza leo, katika ukumbi huu na popote mlipo kupitia vyombo vya habari, mnamo mwaka 1978 Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitangaza vita dhidi ya nduli Idi Amini na kusema;

“Tutampiga. Sababu za kumpiga tunazo, nia tunayo, uwezo wa kumpiga tunao”.

Tanzania ipo katika vita hivi sasa.
Vita dhidi ya Ufisadi,
vita dhidi ya uporaji wa rasilimali zetu,
vita dhidi ya Siasa chafu.
Vita dhidi ya Uchumi wa kinyonyaji.
Vita dhidi ya kuporomoka kwa Utaifa wetu.

Tunapaswa kufanya jambo moja tu, nalo ni kupigana vita hizi. Ni vita kwa ajili ya kurejesha ndoto tuliyoota miaka 54 iliyopita na Muasisi wetu Mwalimu Julius Nyerere. Tunataka kurejesha nchi kwa wananchi, tunataka kujimilikisha nchi yetu. Wananchi wawe WENYE nchi! Tutimize ndoto yetu ya kuona;

Tanzania yenye Dola madhubuti,

Tanzania yenye Wananchi wenye mwamko,

Tanzania yenye sekta binafsi iliyochangamka,

Tanzania yenye uchumi unaonufaisha watu wote.

Sababu tunazo, nia tunayo na uwezo tunao. Twendeni tukajenge Chama kitakachorejesha misingi ya Taifa letu.

Asanteni sana

Mzalendo Zitto Kabwe

Written by zittokabwe

March 29, 2015 at 3:39 PM

Ifahamu ACT

with 16 comments

Written by TeamZitto

March 23, 2015 at 10:24 AM

Uwajibikaji, Changamoto na Uweledi wa Kamati ya PAC

with 5 comments

Uwajibikaji, Changamoto na Uweledi wa Kamati ya PAC

Mfumo thabiti wa Uwajibikaji ni moja ya jawabu muhimu sana katika kuhakikisha Taifa linaondokana na ufisadi na masuala mengine yanayorudisha nyuma maendeleo ya Tanzania. Kazi za mwisho za Kamati ya PAC katika Bunge la Kumi zilisheheni mambo mengi muhimu katika mchakato endelevu wa ujenzi wa mfumo thabiti wa uwajibikaji nchini kwetu.

Taarifa ya Mwaka iliyojadiliwa na kupitishwa na Bunge wiki iliyopita ndio ilikuwa taarifa yetu ya mwisho katika Bunge hili. Kama kawaida mwaka 2015 ulianza kwa ziara za kukagua miradi na hatimaye kukutana na maafisa masuuli wa Wizara na Mashirika ya Umma ili kukagua mahesabu yao na kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya wakaguzi na Kamati.

Kipindi hiki ni muhimu sana kwangu kwani kwa vyovyote vile ni kazi yangu ya mwisho kufanya kama Mwenyekiti wa PAC, nafasi niliyoichukua mwezi Machi mwaka 2013. Kabla ya hapo nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) kuanzia Februari mwaka 2008 mpaka Februari mwaka 2013. Katika Maisha yangu ya miaka 10 Bungeni, nimetumikia uongozi wa kamati hizi kwa miaka Saba na Nusu. Hata hivyo leo natafakari kazi ya wiki nne tu na nilichojifunza katika siku hizo.

Wiki ya Kwanza, tulitembelea miradi ya njia za Reli na Mashamba ya Miwa ili kuongeza uzalishaji wa Sukari nchini. Tulikwenda mkoani Morogoro katika Wilaya za Kilosa na Kilombero. Tulijulishwa kuhusu mahitaji ya fedha nyingi katika ujenzi wa Reli ya Kati ambapo ili kukarabati mtandao Reli iliyopo zinahitajika jumla ya shilingi 500 bilioni kwa miaka mitatu mfululizo ($800m). Vilevile zinahitajika dola za Kimarekani $6 bilioni kujenga reli mpya ya kisasa (standard gauge). Wiki mbili baada ya kumaliza ziara hiyo, niliona picha ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akikagua ujenzi wa Reli ya kisasa nchini humo. Nilipoangalia picha yangu na wajumbe wenzangu katika kijireli chetu, nilicheka kicheko cha huzuni sana. Nimejifunza kwamba nchi yetu inaweza kusonga mbele iwapo tu tutaamua kujinyima baadhi ya maeneo ili kuendelea kwenye maeneo mengine. Fedha inayopotea katika kutoa misamaha ya kodi (tshs 1.9 trilioni ) peke yake, kwa mwaka mmoja inamaliza ukarabati wa Reli yote ( Kigoma – Tabora – Dar es Salaam na Tabora – Mwanza ).

Wiki hiyo pia tulitembelea kiwanda cha Sukari cha Kilombero na kukutana na Wakulima wa Miwa. Tanzania ina nakisi ya Sukari ya takribani tani 120,000 – 200,000 kwa mwaka. Uzalishaji wa ndani wa tani 300,000 hautoshelezi mahitaji ya wananchi na hivyo twalazimika kuagiza Sukari kutoka nje ya nchi ambayo husamehewa kodi. Kwa mwaka Tanzania husamehe kodi ya zaidi ya shilingi 200 bilioni katika Sukari peke yake. Fedha hii ingeweza kujenga viwanda kadhaa vya Sukari na hivyo kuachana kabisa na uagizaji na badala yake kuuza nje. Nimejifunza mengi sana katika kushughulikia suala la Sukari nchini. Nimeona namna ambavyo mfumo mzima wa Serikali ulivyo na ganzi katika kupata suluhisho la kudumu. Hivi sasa Serikali inataka uagizaji wa Sukari ufanywe na wazalishaji wa Sukari, majawabu ya namna hii ni majawabu ya kugawana pato nyemelezi (rent seeking). Jawabu la kudumu la sekta ya Sukari ni kuongeza uzalishaji wa ndani kwa kufungua viwanda vipya maeneo yenye miwa ya ziada hivi sasa, kutoa ruzuku kwa viwanda ili kupunguza gharama za uzalishaji na hatimaye kuwa na bei nafuu kwa walaji na kufungua mashamba mapya ili kuzalisha ziada na kuuza nje kwa ajili ya kupata fedha za kigeni.

Tulijadili kwa kina sana changamoto zinazoikabili sekta ndogo ya kilimo cha Korosho. Ukaguzi Maalumu ulionyesha kuwa kuna unyonyaji mkubwa wa wakulima ikiwemo kupewa pembejeo zilizoisha muda na kutofikishiwa pembejeo kabisa. Pia upotevu mkubwa sana wa Korosho na suala zima la kuuza korosho ghafi nje ya nchi. Utafiti uliofanywa na African Cashew Alliance unaonyesha kuwa Tanzania hupoteza zaidi ya dola za kimarekani 110 milioni kila mwaka kwa kuuza korosho ambazo hazijabanguliwa. Ikumbukwe kuwa Tanzania ilikuwa na viwanda 12 vya kubangua Korosho na vyote viliuzwa katika zoezi la ubinafsishaji na sasa vimekuwa ni maghala ya kuhifadhia Korosho. Tulielekeza kuwa mapato yanayotokana na tozo ya mauzo ya Korosho nje (export levy) yatumike kujenga viwanda vipya vya korosho kwa kutumia teknolojia mpya kutoka Vietnam ambapo viwanda vidogo vidogo vitajengwa kuanzia vijijini na kuzalisha ajira nyingi na kuondoa umasikini. Nimejifunza kwamba Korosho peke yake inaweza kuingiza fedha za kigeni katika nchi yetu kwa thamani ya zaidi ya dola za kimarekani 500 milioni kwa mwaka. Mwaka 2014 Tanzania imezalisha tani 200,000 za Korosho, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa tangu tupate Uhuru. Korosho inaweza kuondoa umasikini kwa watu wa mikoa ya Kusini iwapo Viongozi wakiamua iwe hivyo.

Ilituchukua siku 2 kujadiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania kuhusu mahesabu yao ya mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2013. Sababu kubwa ilikuwa ni mjadala kuhusu misamaha ya Kodi. Kama nilivyoeleza hapo juu, tulijulishwa kuhusu misamaha mingi ya kodi kuendelea kutolewa mpaka kufikia jumla ya shilingi 1.9 trilioni katika mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2014. Kamati pia ilijadili Taarifa ya ukaguzi maalumu kuhusu misamaha ya kodi na kugundua kuwa misamaha mingi inatumika ndivyo sivyo. Nimejifunza kuwa tukiendelea kusisitiza uwazi na uwajibikaji tunaweza kupunguza tatizo hili la misamaha holela ya kodi. Tuliagiza kuwa kuanzia sasa, katika kila Taarifa ya makusanyo ya TRA kila mwezi, pia taarifa ya misamaha ya mwezi huo itolewe kwa umma. Hii itasaidia kuonyesha ni mapato kiasi gani yangeweza kukusanywa bila ya misamaha na kama misamaha hiyo ni muhimu na inatumika ipasavyo.

Mifano hii michache ya Reli, Sukari, Korosho na Misamaha ya Kodi imenikumbusha changamoto nyingi ambazo nchi yetu inazo na namna bora ya kukabiliana na Changamoto hizo. Mfumo thabiti wa Uwajibikaji ni suluhisho endelevu dhidi ya changamoto hizi. Kamati ya PAC imeshiriki kikamilifu kujenga mfumo huo. Kazi bado kubwa lakini inaendelea.

Zitto Zuberi Kabwe

Written by zittokabwe

February 4, 2015 at 3:45 PM

Taarifa ya PAC 2014

with 4 comments

Written by zittokabwe

January 29, 2015 at 6:19 PM

Posted in Uncategorized

Tagged with , ,

Tunaweza kujitosheleza kwa Sukari

with 2 comments

Tunaweza kujitosheleza kwa Sukari

Leo siku nzima kamati ya PAC ilikuwa inazungumza na Bodi ya Sukari, Wizara ya Kilimo na Wakulima wa Miwa Wilayani Kilombero. Tanzania huzalisha wastani wa tani 300,000 za Sukari kwa mwaka ilhali mahitaji ni tani 420,000 kwa mwaka. Hii hupelekea uagizaji wa Sukari kutoka nje ambao umekumbwa na malalamiko makubwa sana kutoka kwa wadau mbalimbali.

Masuala kadhaa yameibuliwa katika kikao cha leo

  1. Wakulima wamelalamikia sana uingizaji holela wa Sukari nchini. Bei ya Miwa imeshuka kutoka tshs 69,000 kwa tani mpaka tshs 55,000 sababu ya Sukari ya ndani kukosa soko.
  2. Wakulima wamelalamikia viwanda kwa kujipangia bei bila kuwashirikisha wao na pia viwanda ndio vinapima Miwa na ubora wa mua wa mkulima hivyo kuleta mgongano mkubwa wa MASLAHI kwa mwekezaji
  3. Wakulima wametaka hisa 25% za Serikali katika viwanda vya Sukari wapewe wao ili waweze kushiriki katika Uchumi wa nchi
  4. Bodi ya Sukari imeshindwa kuendeleza mradi wa RUIPA kwa sababu ya kutokuwa na Fedha tshs 11 bilioni za kulipa fidia ya Wananchi katika eneo la mradi. Mradi huu ungeweza kuzalisha tani 244,000 za Sukari kwa mwaka
  5. Wakulima wamelalamikia sana tabia ya viwanda kushindwa kununua Miwa yote ya Wakulima na hivyo kupelekea takribani nusu tu ya Miwa kutumika na nusu nyingine kubaki mashambani na kuharibika. Wastani wa tani 400,000 za Miwa huharibika Wilayani Kilombero peke yake. Hii ni sawa na tani 50,000 za Sukari

PAC imetoa ufafanuzi wa masuala yafuatayo

  1. Kamati ilikwishaiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania kufanya uchunguzi wa kikodi katika Sekta nzima ya Sukari nchini. TRA wameijulisha kamati kwamba wanafanyia kazi suala hilo na wameomba muda zaidi ili kukamilisha kazi hiyo. PAC imekubaliana na ombi hilo na pia kwamba inasubiri Taarifa ya kikosi kazi kilichoundwa na Katibu Mkuu Kiongozi ili kupata suluhisho la kudumu la Changamoto zinazokabili Sekta ya Sukari. Kamati ikishapata taarifa zote hizo itazifanyia kazi na kuziwasilisha Bungeni.
  2. Kamati imeielekeza Bodi ya Sukari kuhakikisha inaendeleza mradi wa RUIPA kwa kutangaza zabuni ya kumpata mwekezaji ambaye atalima sehemu ya shamba na kumilikisha kwa hati Wakulima ( outgrowers) sehemu nyingine ya shamba. Mradi wa RUIPA uwe mfano wa ushiriki wa wananchi katika Kilimo cha kisasa. Wakulima wamilikishwe Ardhi ya kulima Miwa na kuuza kwenye kiwanda, wasikodishiwe Ardhi hiyo. Bodi ya Sukari ipate FEDHA tshs 11 bilioni za fidia ya wananchi kutokana na zabuni ya kupata mwekezaji na malipo tangulizi ya mwekezaji.
  3. Modeli ya Malaysia yaweza kutumika katika mradi wa RUIPA, kwa kuwagawia wananchi ( households ) 1500 wanaoathiriwa na mradi kila mmoja hekta 5 ( 4 za kulima Miwa na 1 ya makazi yake ) na hekta zinazobakia katika jumla ya hekta 14700 ziwe nucleus. Ushiriki wa wananchi katika uzalishaji wa Ndio njia endelevu ya kutokomeza umasikini nchini.
  4. Kamati imeelekeza kuwa Bodi ya Sukari iwe na mamlaka ya kuwa mdhibiti ( regulator ) kwa kutoa bei elekezi za mauzo ya Miwa na Sukari nchini ili kulinda Wakulima dhidi ya unyonyaji wa wawekezaji. Bodi pia ihusike na udhibiti katika upimaji wa Miwa na kiwango cha Sukari katika Miwa ( sucrose ) ili kujibu Changamoto ya Wakulima kupunjwa.
  5. Kamati imeelekeza kuwa vianzishwe viwanda vya ngazi ya kati vya Sukari ili kutumia Miwa ya ziada na kuzalisha Sukari na hivyo kuongeza uzalishaji. Vyama vya Wakulima wa Sukari vimehamasishwa kuanzisha viwanda vidogo hivyo na Bodi ya Sukari imeelekezwa kulegeza masharti ya uanzishaji wa viwanda vya ngazi ya kati.
  6. PAC imepingana na Wakulima kwamba hisa za Kampuni 25% wapewe wao na badala yake PAC imeelekeza Msajili wa Hazina aangalie uwezekano wa kuorodhesha hisa za Serikali katika soko la hisa la Dar Es Salaam na vyama vya Wakulima vipewe fursa kununua sehemu ya hisa hizo ( angalau 5%).
  7. Wakulima wa Miwa wamehamasishwa kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili wafaidike na mafao ya muda mrefu na muda mfupi ikiwemo Bima ya Afya, mikopo katika SACCOS zao na pensheni uzeeni. Tanzania ina jumla ya Wakulima wa Miwa ( out-growers ) 19,000 wenye kuzalisha nusu ya Sukari inayozalishwa nchini.

Tukipunguza upotevu wa Miwa ya Sukari ( wastage ) nchi nzima kwa kuanzisha viwanda vya Kati vya kusindika Miwa, tunaweza kuongeza uzalishaji kwa zaidi ya tani 80,000 za Sukari na kupunguza Sukari inayoagizwa kutoka nje. Tukitekeleza mradi wa RUIPA, tutakuwa na Sukari ya ziada tani 200,000 ambazo tunaweza kuuza nje na kupata fedha za kigeni.

Hii iwe mikakati ya muda mfupi. Tunaweza tukiamua na kashfa za Sukari zitakuwa Historia. Tufanye sasa

Written by zittokabwe

January 9, 2015 at 7:15 AM

Posted in Uncategorized

Tagged with , , ,