Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Posts Tagged ‘Mtwara

“Azimio la Mtwara” Speech by Zitto Kabwe: Mtwara, 31-12-14

with 6 comments

View this document on Scribd

PICHA

"Azimio la Mtwara" tarehe 31-12-2014 Zitto Kabwe na Prof. Ibrahim Lipumba

“Azimio la Mtwara” tarehe 31-12-2014 Zitto Kabwe na Prof. Ibrahim Lipumba

 

Written by zittokabwe

December 31, 2014 at 4:10 PM

Posted in Uncategorized

Tagged with ,

Mtwara : Serikali inavunja nchi kwa kutosikiliza Wananchi

with 13 comments

Mtwara : Serikali inavunja nchi kwa kutosikiliza Wananchi

Kwa wiki ya tatu mfululizo kumekuwa na malumbano kuhusiana na suala la ujenzi wa Bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam. Kumekuwa na madai yenye nguvu ya hoja kutoka kwa wananchi wa Mtwara dhidi ya porojo kutoka kwa viongozi wenye dhamana ya kujibu madai haya ya watu wa Mtwara. Watu wa Mtwara kwa umoja wao na kwa kuungwa mkono na viongozi wa dini zote wamekuwa wakitaka Serikali ifikirie upya suala la mradi wa ujenzi wa Bomba la gesi na badala yake kujenga mitambo ya kufua umeme mkoani Mtwara na kusafirisha umeme huo kwenda maeneo mengine ya nchi. Kwenye moja ya maandishi yangu (Serikali iwasikilize watu wa Mtwara) nimeshauri kuwa Taifa liwe na gridi nyingine ya Taifa ambayo itatokana na Gesi tu na ianzie Mtwara.

Ikumbukwe kwamba katiba ya nchi, ibara ya 9 katika mabano J inataka mamlaka ya dola na vyombo vyake vyote kuhakikisha ya kwamba shughuli zote za kiuchumi zinaendeshwa kwa namna ya kwamba pasiwe mrundikano wa utajiri au shughuli za uzalishaji kwa watu wa chache. Katiba inaendela kwa kuelekeza kwamba uchumi wa nchi upangwe katika uwiano sawia (9, d). Watu wa Mtwara wanatekeleza matakwa haya ya katiba kwa kukataa mrundikano wa shughuli za kiuchumi wa nchi na utajiri wa nchi kua kwenye mikoa michache na hasa mkoa wa Dar-Es-Saalam.

Serikali imekuwa ikitoa majibu ya porojo na kuwatusi watu wa Mtwara na kama ilivyozoeleka Rais Jakaya Kikwete na Mawaziri wake wamekuwa wakisema suala la Mtwara linatumika na wanasiasa kujitafutia umaarufu. Inasikitisha sana kuona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwaambia mabalozi wa nchi za kigeni waliopo hapa nchini kuwa yanayoendelea mkoani Mtwara yanachochewa na Wanasiasa tuliosimama na wananchi wanaodai haki ya kufaidi utajiri wa nchi yetu. Rais Kikwete na Mawaziri wake wameshindwa kabisa kuonyesha uongozi katika suala hili na hatimaye kuhatarisha umoja wa kitaifa.

Kwa udhaifu wa serikali na tabia ya kutafuta mchawi badala ya kutatua tatizo la msingi, wananchi wameendelea kukutana na hata wengine sasa kuanza kusambaza ujumbe wa kukata kipande cha nchi na kuanzisha Jamhuri ya Kusini. Nimeona kwenye mabango ya mkutano wa hadhara uliofanyika 19/1/2013 wananchi wakibeba mabango yanayoaishiria kuchoka kuwa sehemu ya Tanzania na kuanzisha Jamhuri ya Makonde kuanzia jiwe la Mzungu wilayani Kilwa mpaka mto Ruvuma. Haya yanatoka na kiburi cha Serikali kujishusha na kuwasikiliza wananchi wanao dai haki yao ya kikatiba.

Ni Serikali iliyokosa uhalali wa kutawala inayoweza kudharau hisia hizi za wananchi. Serikali ielewe kwamba kamwe haitaweza kulinda kila nchi ya bomba hili iwapo italijenga kwa nguvu. Badala ya kuzungumza na vyombo vya habari Serikali ifanye mazungumzo na wananchi wa Mtwara na kukubaliana na matakwa yao. Kitendo cha Serikali kung’ang’ania msimamo wake dhidi ya watu wa mtwara ni kitendo kinacho weza kuipasua nchi na hivyo kwenda kinyume na masharti ya katiba ibara ya 28 ambayo inasema: “kila raia ana wajibu wa kulinda uhuru wa nchi, uhuru mamlaka na umoja wa taifa.”ibara ya 28, 1.

Inawezekana Serikali inaogopa kuvunja makubaliano na Wachina ya mkopo wa dola za kimarekani 1.2 bilioni ambao imeuingia bila hata kushirikisha Bunge. Inawezekana Serikali na hasa watendaji wa Serikali waliojadili mkopo huu wameshapata chao na hivyo kuogopa kusikiliza madai halali ya wananchi. Lakini yote hayo hayawezi kuwa zaidi ya Umoja wa nchi yetu. Hatuwezi kukubali nchi yetu ipasuke vipande vipande kwa sababu tu ya kulinda mkataba wa bilioni 1.2 tuliokopa China, ambayo serikali inang’ang’ania.

Tunafahamu kwamba ubalozi wa China umeandika barua serikalini kuwaondoa raia wa China waliopo Mtwara kwa hofu ya maisha yao. Serikali inaficha ukweli huu kama ilivyoficha ukweli kwamba Naibu Waziri wa Nishati na Madini bwana George Simbachawene alifukuzwa na wananchi wa Mtwara alipokwenda hivi majuzi. Serikali itaficha ukweli mpaka lini? Lazima tupate majawabu.

Kwanza Serikali iweke wazi mkataba wa ujenzi wa Bomba hili. Kamati ya Bunge ya POAC ilipokuwa inapitia mahesabu ya TPDC iliomba mkataba na kwa mshangao mkubwa wabunge wakaambiwa Mkataba haupo TPDC bali upo Wizarani. Kwa nini Mkataba huu wa matrilioni ya Fedha unafichwa? Mkataba huu ulisainiwa pamoja mikataba mingine 2, mmoja wa kujenga nyumba za wanajeshi wa thamani ya dola za kimarekani 400 milioni na mwingine wa mawasiliano jeshini wa dola za kimarekani 110 milioni, na mikataba yote mitatu imesainiwa kimya kimya bila kushirikisha wananchi kupitia Bunge. Lazima mikataba yote hii iwekwe wazi.

Pili, Mkataba huu uchunguzwe kama unalingana na thamani ya fedha maana kwa utafiti wa awali inaonyesha kuwa bei ya ujenzi wa bomba imepandishwa maradufu. Wastan wa kujenga bomba la gesi duniani ni dola za kimarekani 1.2 milioni kwa maili moja. Mradi huu wa Tanzania utagharimu dola za kimarekani 2.2 milioni kwa kilomita moja (maili 1 ni sawa na kilomita 1.6).

Tatu, Serikali ibadilishe Mkataba huu kuwa wa mkopo wa kujenga Mitambo ya kufua umeme Mtwara na ujenzi wa Msongo wa Umeme kama gridi ya pili ya Taifa. Kwa sasa Tanzania ina gridi moja ambayo inabebwa na bwawa la Mtera linalo tegemea mto Ruaha ambao hivi sasa unakauka miezi 5 katika miezi 12 ya mwaka. Ni dhahiri kwamba kwa usalama wa Taifa na hata kwa gharama Nchi itafaidika zaidi kwa kujenga gridi nyingine kutokea Mtwara badala ya kusafirisha gesi kuja Dar-Es-Salaam.

Serikali haitashinda vita hii kwa kuzusha kwamba ama wanasiasa wanaopinga wanatumika na makampuni mengine au kwa mataifa ya magharibi kutaka kuvuruga nchi. Serikali ijitazame yenyewe. Bila kufanya hayo tunayo pendekeza hapo juu, wananchi wataendelea kupigania hako yao. Hii ni vita ya uwajibikaji. Wananchi wanataka kufaidika na rasilimali za nchi yao. Kwa vyovyote vile upande wa wananchi utashinda. Vita ya uwajibikaji kwenye rasilimali za nchi sio ya vyama vya siasa, ni vita ya wananchi. Chama cha siasa kitakachokwenda kinyume na matakwa ya wananchi, kinajichimbia kaburi.

 

 

Utajiri wa Gesi Asilia: Tuwasikilize Watanzania wa Mtwara na Lindi. Tusipuuze

with 15 comments

Utajiri wa Gesi Asilia: Tuwasikilize Watanzania wa Mtwara na Lindi. Tusipuuze

Maandamano ya amani yaliyofanyika mjini Mtwara siku ya alhamis wiki hii yameibua hoja mbali mbali kutoka kwa viongozi, wananchi, vyombo vya habari na mjadala wa siku nzima kwenye mitandao ya kijamii hasa facebook, twitter na JamiiForums. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ameita waandamanaji wapuuzi na Waziri wa Nishati na Madini amewaita watu hatari na wahaini. CHADEMA tumetoa kauli kupitia kwa Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwamba udhaifu wa utendaji serikalini ndio chanzo cha maandamano haya.

Lakini kuna tatizo kubwa zaidi ambalo linaonekana siyo katika sekta hii tu bali pia katika sekta nyingine ambapo tunaona matokeo yake katika maisha ya watu wetu na naweza kusema ni dalili za kushindikana kwa sera za CCM. Sera hizi ndizo ambazo zimelifikisha taifa hili hadi hapa. Kama hadi wananchi wa Mtwara ambako kwa muda mrefu imekuwa ni ngombe ya CCM wanaanza kuhoji matokeo ya sera za chama tawala basi ni dalili kuwa Watanzania wamefungua macho yao na wanaona.

Wanaona katika nishati, wanaona katika utawala bora, wanaona katia elimu (kuanzia ya msingi hadi ya juu kabisa!), wanaona katika afya, wanaona katika utendaji wa jeshi la polisi wanaona katika madini. Sera za CCM zimeshindwa. Zimeshindwa kuinua maisha yao na zinaonekana kuendelea kushindwa.

Mtwara na Lindi wanataka nini?

Watu wa Mtwara wanataka gesi isiondoke Mtwara na badala yake viwanda na mitambo ijengwe Mtwara kisha kama ni umeme au mbolea isafirishwe kupelekwa sehemu nyingine ya nchi. Watu wa Mtwara hawasemi kwamba Gesi yote na mazao yake vibaki Mtwara na Lindi. Wanasema umeme uzalishwe Mtwara usambazwe nchi nzima. Mbolea izalishwe Mtwara na kusambazwa nchi nzima. Wanataka Bandari ya Mtwara iboreshwe na kuhudumia mikoa ya Kusini. Watu wa Mtwara hawasemi kwamba mapato yote ya Gesi yatumike Mtwara tu la hasha.

Sio dhambi hata kidogo kwa watu wa Mtwara kudai masuala haya. Watu wa Mtwara wamefanya maandamano kwa amani kabisa bila kuharibu mali na kutoa maoni yao. Kwanini tuwasute na kuwasusubika kwa madai yao haya? Kwa nini tusiwasikilize? Kosa lao nini kudai viwanda ili wapate ajira? Tumesahau kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ni mikoa masikini kabisa nchini? Tumesahau kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ilitumika kwa ukombozi wa kusini mwa Afrika kiasi cha kuwa katika hatari kabisa? Tumesahau ‘sacrifice’ ya watu wa Mtwara na Lindi dhidi ya usalama wa nchi yetu? Tumesahau kuwa Korosho imekuwa zao kubwa la biashara na linaloingiza mapato mengi sana ya Fedha za kigeni? Waziri Muhongo anasema Mtwara warudishe Fedha za Mkonge na Kahawa. Mbona hataji fedha za Korosho? Mwaka 2011 Korosho ilikuwa zao la pili kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni baada ya Tumbaku.

Lakini tujiulize, watu wa Mtwara na Lindi walifadi fedha za Mkonge? Walifaidi fedha za Kahawa? Wamefaidi fedha zao za Korosho? Tumesahau hata Reli iliyoachwa na Mkoloni ya Nachingwea – Mtwara iling’olewa na Serikali huru ya Tanzania?

Tujiulize zaidi, hivi watu wa Nzega wamefaidika vipi na Mgodi wa Resolute pale Lusu? Mgodi umefungwa ukiwa umezalisha na kuuaza dhahabu ya thamani ya dola za marekani 3.3 bilioni. Hivi katika uhai wa mgodi huu Serikali Kuu imekusanya kodi kiasi gani? Halmashauri ya Wilaya ya Nzega imepata ushuru kiasi gani? Watu wa Mtwara wanayaona haya yaliyotokea Nzega na yanayotokea Tarime, Biharamulo, Kahama na Geita. Watu wa Mtwara wana Haki kuandamana kuzuia haya yaliyotokea wenzao yasiwatokee wao kwenye Gesi asilia.

Mtwara na Lindi wanakosea wapi?

Madai yao halali na mimi binafsi na chama changu tunayaunga mkono. Lakini kuna mahala lazima waelimishwe.

Watu wa Mtwara pia wanapaswa kuelewa kuwa juhudi zao zisiwatenganishe na Watanzania wengine kwani bado utajiri wa Taifa unafadisha kikundi cha Watanzania wachache sana. Watu wa Mtwara wanahitaji kuungana na watu wa Mara, watu wa Mwanza, watu wa Shinyanga na watu wa Kagera kudai utajiri wa nchi utumike kwa maendeleo ya watu badala ya kunufaisha kundi dogo la watu. Watu wa Mtwara wanapaswa kuunganisha nguvu na Watanzania wengine kuzuia uporaji wa rasilimali ya nchi dhidi ya kizazi kijacho. Watu wa Mtwara wasijitenge wakawa peke yao na Gesi yao. Nguvu ya mnyonge ni umoja.

Serikali isiyosikia

Serikali ina hoja kuhusu kujenga Bomba la Gesi kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa gharama nafuu. Umeme unaotumiwa na asilimia 14 tu ya Watanzania. Kwa kuwa hii asilimia 14 ndio wenye sauti basi watu wa Mtwara wataonekana hawana hoja kabisa. Lakini Serikali imejiuliza mara mbilimbili kuhusu mradi huu wa Bomba? Tunaambiwa na Wataalamu kwamba kuna uwezekano mkubwa mwakani gesi asilia ya kiasi cha futi za ujazo trillioni 20 itakuwa imegunduliwa katika Kitalu namba 7( block 7) ambacho kipo mkoani Dar es Salaam katika Wilaya ya Temeke. Iwapo gesi nyingi hivi itakuwa hapa Dar karibu kabisa na mitambo ya kuzalisha umeme, mradi huu wa Bomba unaojengwa kwa trillioni za shilingi utakuwa na maana tena? Huu mkopo utakuwa na tija?

Serikali imewaambia watu wa Mtwara gharama za kuleta bomba Dar dhidi ya gharama za kujenga mtambo wa kuzalisha umeme Mtwara na kuusafirisha umeme kwenda maeneo mengine ya Tanzania? Serikali imeangalia faida ya kujenga gridi nyingine badala ya kuwa na gridi moja tu yenye kushikwa na bwawa la Mtera? Leo bwawa la Mtera lisipozalisha hata megawati moja hata Dar es Salaam izalishe megawati alfu kumi umeme hautakuwapo maana uti wa mgongo wa gridi ni Mtera! Kwa nini tusiwe na gridi nyingine yenye uti wa mgongo Lindi au Mtwara?

Tuwasikilize watu wa Mtwara

Watanzania sio mabwege tena. Kuwaita watu wa Mtwara ni wahaini, wapuuzi au watu hatari haisaidii kujenga Taifa moja lenye watu huru. Serikali na wadau wote wa sekta ya Gesi likiwemo Bunge washirikiane na watu wa Mtwara kuhusu miradi ya gesi asilia. Tuwe na Azimio la Mtwara, tamko la kuelekeza namna bora ya kutumia utajiri wetu wa Gesi bila kuathiri umoja wa Taifa letu.

Ujio wa Sera, Maono na Uongozi Mbadala

Sasa hivi wananchi wa Mtwara kama wananchi wa sehemu nyingine wanahitaji maono mbadala, uongozi mbadala, sera mbadala na mwelekeo mbadala wa kitaifa ambao utaangalia mahitaji yao, utazingatia raslimali zilizopo na utaunganisha utendaji wa sekta mbalimbali katika kutengeneza mfumo wa kiutawala na kiuchumi ambao utaliinua taifa zima.

Ni kwa sababu hiyo naamini chama changu ni jibu sahihi kwa matamanio na kiu ya wananchi wa Mtwara na sehemu nyingine nchini. Ikumbukwe kuwa katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya 2010 tulielewa haja ya kuangalia mikoa hii ya Kusini kwa namna ya pekee na kuipa mwelekeo wa kipekee katika sera.  Bado tuna makusudio hayo tunapoelekea 2015 na tukishika Dola wananchi wa Mtwara na sehemu nyingine zote zilizoachwa pembezoni mwa mafanikio wajue kuwa wamepata rafiki na mshirika wa karibu wa kushirikiana nao kuleta maendeleo.

Siyo katika suala la gesi tu bali katika nishati, maji, elimu, miundombinu, kilimo, ufugaji, uvuvi, utalii. Mtwara kama ilivyo mikoa mingine ina raslimali za kutosha kuweza kuwainua wananchi wake kimaisha, na zaidi ya yote kutoa mchango mkubwa wa kiuchumi. Hili ambalo ni kweli kwa Mtwara ni kweli kwa mikoa mingine kama Kigoma, Manyara, Katavi, Lindi n.k.

 

Written by zittokabwe

December 29, 2012 at 10:57 AM