Posts Tagged ‘Tumbaku’
Siku ya 9 ya Ziara ya CHADEMA Kanda ya Magharibi – Jimbo la Igunga, Wilaya ya Igunga
Siku ya 9 ya Ziara ya CHADEMA kanda ya Magharibi imetufikisha Jimbo la Igunga, Wilaya ya Igunga.
Tumefanya mikutano 6 katika kata sita tofauti, tumefungua matawi ya chama na kuhutubia wananchi. Pia tumepokea kero za wananchi zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.
Tukiwa Katika kata ya Choma tumeshuhudia kiwanda cha kuchambua Pamba kilicho binafsishwa kikiwa kimetelekezwa na mwekezaji toka mwaka 1998. Ginnery hii iliyokuwa mali ya umma na kuajiri wafanyakazi 500 kwa shifti 3 kila siku (jumla 1500) nyakati za msimu imekufa na baadhi ya Mashine kuuzwa kama chuma chakavu. Kijiji cha Choma kimedorora kiuchumi kutokana na ubinafsishaji huu. Nimewaeleza wananchi kuwa nitafuatilia suala hili la Ginnery ya Manonga, katani Choma na kuwajulisha hatua mwafaka za kuchukua.
Nimependekeza pia kwamba iwe marufuku kuuza nje mazao ghafi kwani tunakuwa tunauza ajira za watu wetu. Suala hili nimekuwa nikilisema Bungeni mara kwa mara kwamba ni lazima kusafirisha mazao yaliyoongezwa thamani kwa kupiga marufuku kuuza korosho ghafi, Pamba ghafi, kahawa ghafi na Katani ghafi. Viwanda vya kilimo vinaongeza ajira sana kwa wananchi na ni suluhisho endelevu kwa tatizo la ajira na kuondoa umasikini.
Niliwapa mfano wa kiwanda kilichouzwa huko mtwara na kugeuzwa godown la kuhifadhi korosho na godown liligeuzwa kuwa kiwanda cha kubangua korosho! Niliwaeleza namna viongozi wa Serikali wanavyochanganya dhana ya uhuru wa biashara (liberalisation) na ubinafsishaji (privatisation). Dhana mbili zinazochanganya watawala wengi wa Afrika na kujikuta wakiuza mali za umma kiholela. Unaweza kuwa na Mashirika ya Umma yakishindana katika soko na makampuni binafsi. Ubinafsishaji holela unatengeneza ‘private monopolies’ na kuathiri sana ukuaji wa uchumi kutokana na ufanisi mdogo ie efficiency.
Nimerejea wito wangu wa kutaka sera ya hifadhi ya jamii kwa wakulima kupitia vikundi vyao na ushirika. Nimesisitiza umuhimu wa kuweka akiba ili kuongeza uwekezaji wa ndani na hasa uwekezaji wa miundombinu ya kilimo. Nimeonya tabia ya wananchi kukimbilia kulipwa fidia badala ya kutaka kushiriki katika miradi mikubwa ya kilimo. Kilimo endelevu ni kilimo cha wakulima wadogo wanapata huduma pamoja (integrated production schemes) badala ya wakulima wakubwa wenye kuhitaji manamba. ‘outgrower’s schemes’ ndio mwelekeo sahihi kuwafanya wananchi wamiliki ardhi, wawe na ushirika imara, wawe na hifadhi ya jamii na waondokane na umasikini.
Leo nikiwa kijijini Choma na mjini Igunga nimewaambia wananchi umuhimu uwazi wa mapato ya viongozi wa umma. Nimewaambia kuwa mishahara ya viongozi wa umma haipaswi kuwa siri na inapaswa kukatwa kodi. Kama nilivyoahidi niliokuwa mjini Mpanda, nimewaambia kuwa mshahara wa Rais wa Tanzania ni Tshs 384m kwa mwaka. Kipato hiki hakikatwi kodi na Rais hupata huduma mbalimbali bure. Niliahidi kwamba kwa kuwa gazeti la Mwananchi lilifungiwa kwa sababu ya kutaja mishahara ya watumishi wa Serikali, basi ni vema kuonyesha Serikali kuwa lile sio kosa na wananchi wana haki ya kujua. Ndio maana nikachukua hatua ya kutaja kipato cha Waziri Mkuu na Rais.
Nimemaliza awamu ya kwanza ya ziara ya kanda ya Magharibi. Nimetembelea jumla ya kata 53 katika majimbo 10 ya uchaguzi ya mikoa ya Katavi na Tabora. Siku si nyingi nitamalizia majimbo ya Urambo na Kaliua kisha Mkoa wa Kigoma. Nimefarijika sana na mwitikio wa wananchi wanaotaka mabadiliko. Wazee kwa Vijana, kina mama kwa kina baba, wanataka mabadiliko.
Nimesononeshwa na kiwango cha umasikini wa wananchi na huduma mbovu za kijamii kama Maji, Elimu na Afya.
Nimeumizwa sana na unyonyaji mkubwa dhidi ya wakulima wa Pamba na Tumbaku.
Nimekasirishwa sana na ufisadi mkubwa wa fedha za umma kupitia mbolea ya ruzuku.
Nina Hofu kubwa ya wanasiasa wengi kutojua changamoto hizi za wananchi lakini wakitaka kupewa dhamana.
Nina Hofu na wanasiasa ‘manipulative’ lakini nina matumaini kuwa viongozi ‘inspirational’ watasimama kidete kushika usukani wa jahazi letu na kulifikisha salama. Tanzania ina kila sababu ya kuendelea, hatuna cha kupoteza isipokuwa minyororo ya umasikini.
Chukua hatua!
Siku ya sita ya Ziara ya #CHADEMA imetufikisha Jimbo la Tabora Kaskazini
Siku ya sita ya Ziara ya #CHADEMA imetufikisha Jimbo la Tabora Kaskazini.
Tumefanya mkutano wetu wa mwisho kijijini Mabama. Mkutano mkubwa sana na kuingia wanachama wengi sana. Kilio kikubwa cha wananchi ni Maji na unyonyaji katika zao la Tumbaku. Kuna haja kubwa sana ya kusukuma hifadhi ya jamii kwa wakulima. Tunaweza kukoboa wakulima wengi sana kutoka kwenye unyonyaji.
Ufisadi kwenye ngazi ya kijiji unatisha.
Umewahi kusikia jengo la matofari ya saruji linajengwa kwa tope?
#CHADEMA kanda ya Magharibi leo #Bukene. Kesho 12th Oct #Nzega na keshokutwa 13th #Igunga
Siku ya 5 ya ziara ya CHADEMA Kanda ya Magharibi-Jimbo la Igalula, Wilaya ya Uyui
Siku ya 5 ya ziara ya CHADEMA Kanda ya Magharibi imetufikisha Jimbo la Igalula, wilaya ya Uyui. Tumekutana na wananchi katika vijiji vya Goweko, Loya, Miswaki, Miyenze na Kigwa.
Tumezungumza kuhusu changamoto ya usafiri wa Reli, wafugaji kunyanyaswa na watendaji wa kata na askari kwa kunyanganywa mifugo, zao la Tumbaku, maji safi na salama na suala la jumla la Katiba na mchakato wa kuandika katiba.
Kimsingi shughuli za kiuchumi za wananchi ni kubwa na hasa Kilimo na mifugo. Hata hivyo ukosefu wa miundombinu unafanya wananchi wasipate thamani ya mazao yao na jasho la kazi zao.
Nilipofika Kijiji cha Loya nimeona eneo kubwa lina miti ya mihama. Wananchi wanatumia tu mihama wakati wa njaa na mara nyingi matunda haya yanaharibika tu. Lazima matunda haya yana matumizi yake ya kiviwanda maana ‘kernel’ yake ina mafuta. Nani anajua matumizi ya Mihama?
Siku ya Nne ya ziara ya CHADEMA Kanda ya Magharibi -Wilaya ya Sikonge Mkoa wa Tabora
Siku ya Nne ya ziara ya CHADEMA Kanda ya Magharibi imetupeleka Wilaya ya Sikonge Mkoa wa Tabora.
Nikiwa na Wenyeviti wa chama wa mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora pia Mwenyekiti wa Kanda ya Magharibi Ndg. Mambo tumefanya mikutano 4.
MAJI
Kata ya Kitunda nilivunjika moyo sana baada ya kushuhudia wananchi wakichota maji ya Kunywa kwenye dimbwi ambamo Ng’ombe anakunywa maji. Maji yana rangi kama chai ya maziwa. Nimevunjika moyo sana sababu kwa umri huu wa Taifa letu Maji safi na salama haipaswi kuwa ni jambo la kukampenia tena au kufanyia siasa. Kina mama wanatembea kilometa nyingi kwenda kuchimba maji kwenye madimbwi. Watanzania hawastahili kabisa maisha ya namna hii. Nimepata uchungu sana sababu hizi ndio kazi wanasiasa tunapasa kufanya kusaidia wananchi na kwa kweli kukutana na hali kama hii kunavunja moyo sana.
Baadhi ya Wabunge tulisimama kidete kuhakikisha bajeti ya Wizara ya Maji inaongezwa na ikaongezwa TZS185 bilioni kwa ajili ya Maji vijijini. Ni wajibu wetu wabunge kuhakikisha fedha hii inafika kwa wananchi ili kuwaondolea madhila haya wasiostahili. Changamoto kama hizi za wananchi masikini wa vijijini zinanifanya nifikirie sana nafasi yangu binafsi katika siasa za nchi yetu, siasa za masuala na majawabu.
Kero ya Wakulima wa Tumbaku
Kero ya wakulima wa Tumbaku bado ni kubwa sana na tumekuwa tunaelezwa kila tunapokwenda. Hapa Sikonge mwaka 2012/13 Chama Kikuu cha Ushirika kimewakata wananchi fedha za mbolea ambayo wananchi hawakupata. Wananchi wanakaa msimu mpaka msimu kupata fedha za mauzo ya Tumbaku. Makato ni mengi na kufanya mkulima ashindwe kuvunja mzunguko wa umasikini.
Nimetoa mawazo ya kisera kwamba imefikia wakati wakulima kupitia vyama vya msingi wajiunge na mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuweza kwanza kuweka akiba, pili kupata mikopo nafuu kupitia vyama vyao vya kuweka na kukopa na hivyo kuweza kuwalipa wakulima pindi wauzapo tumbaku.
Nimetoa wito kwa SSRA waangalie uwezekano wa kuanzisha scheme maalumu ya hifadhi ya jamii kwa wakulima ambapo Serikali ishiriki kwa kuchangia kiwango maalumu katika kila michango ya wakulima. Hii itawezesha wakulima kupata mafao kama bima ya afya, bima ya mazao, mikopo midogo midogo, tofauti za bei na hata elimu kwa watoto wategemezi. Hili ni wazo jipya lakini linapaswa kutazamwa ni kuinua wakulima wa Tanzania. Tusiendelee kuwasahau wakulima. Watanzania wapo Vijijini, tusiwasahau. Umasikini wa Tanzania unaonekana vijijini (rural phenomenon), tutokomeze umasikini kwa kuwekeza kwa mkulima.
Inyonga, Mpanda Magharibi- Ziara Kanda ya Magharibi
Wananchi wanadhulumiwa kwenye bei ya dola za kimarekani katika kila kilo ya tumbaku ambapo wanapewa bei ya tshs 1400 kwa dola $1 moja! Makato ya pembejeo makubwa na wanashindwa kutoka kwenye umasikini. Tukiwa Sikonge tutatoa kauli kuhusu Wakulima wa Tumbaku na namna ya kuwakomboa.
Tumezugumza umuhimu wa Katiba mpya ya wananchi na namna ya kuepusha mchakato kutekwa na kundi dogo la watu wasiotaka mabadiliko. Tumezungumza kuhusu umuhimu wa mwafaka wa kitaifa katika kuandika katiba ya nchi yetu. Kuweka maslahi ya Taifa mbele ya maslahi ya vyama vya siasa.
Leo tunakwenda Mpanda Magharibi kuanzia Mpanda ndogo mpaka Ikola, Mwambao mwa Ziwa Tanganyika.