Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Posts Tagged ‘Benki Kuu ya Tanzania (BOT)

Maelezo ya Gavana Prof Benno Ndulu Kuhusu Kushuka kwa Thamani ya Shilingi ya Tanzania kwa Kamati ya Fedha Uchumi na Biashara

with 5 comments

Maelezo ya Gavana Prof Benno Ndulu Kuhusu Kushuka kwa Thamani ya Shilingi ya Tanzania kwa Kamati ya Fedha Uchumi na Biashara

View this document on Scribd

Written by zittokabwe

May 3, 2015 at 4:45 PM

Yaliyojificha kuporomoka kwa shilingi dhidi ya Dola ya Marekani Shilingi inahujumiwa na Mabenki?

with one comment

Yaliyojificha kuporomoka kwa shilingi dhidi ya Dola ya Marekani

Shilingi inahujumiwa na Mabenki? – Zitto Kabwe[1]

Katika ukurasa wangu wa facebook mnamo tarehe 25 Aprili 2015 niliandika kuhusu sababu za shilingi kuporomoka thamani na majawabu ya namna ya kurejesha thamani halisi ya sarafu yetu. Nilieleza “Shilingi kuporomoka dhidi ya dola na kuvuka 1$/2000TS kunasababishwa na sababu kadhaa 1) Woga wa uchaguzi na hivyo Dola nyingi kutoingia nchini (FDI etc) kusikilizia Serikali ijayo inaundwaje 2) Woga wa uchaguzi na hivyo matajiri kununua dola kwa kasi (too many Tshs chasing too few $) ili kuzificha (hoard) nje 3) kutouza mazao nje na kuagiza bidhaa nyingi kutoka nje ( current account deficit) 4) Benki Kuu kutoachia $ nyingi kwenye soko kutokana na akiba ya fedha za kigeni kupungua 5) Kuongezeka kwa huduma ya Deni la Taifa ambapo malipo ni kwa fedha za kigeni kwa madeni yaliyo wiva.

Niliendelea kushauri majawabu “Suluhisho 1) Benki Kuu kuachia $ za kutosha kwenye soko katika muda mfupi na wa kati (Mwezi Februari BoT ilifanya hivi na kuongeza $64 milioni kwneye soko bila mafanikio[2] 2) Kuongeza mauzo nje hasa ukizingatia kwa sasa ‘our exports becomes cheaper vis a vis foreign exchange) 3) Malipo ya kodi ya Ongezeko la Mtaji kutoka BG (Shell transaction ) na Ophir (Pavilion transaction), malipo haya kwa fedha za kigeni 4) Punguza kununua vitu vya anasa kutoka nje 5) Unafuu wa huduma kwa Deni la Taifa ( Debt relief ) 6) Punguza ujazo wa fedha nchini (mop tshs out)”.

Mjadala mkali umeendelea kuhusu suala hili katika majukwaa mbali mbali. Ni dhahiri kuporomoka kwa shilingi kunaathiri sana Watanzania wa ngazi ya kati hasa wafanyabiashara wa kati wenye kununua huduma na bidhaa kutoka nje. Wenye viwanda wanaotegemea malighafi kutoka nje gharama zao za uzalishaji zimeongezeka zaidi na hivyo kuhatarisha uzalishaji mali nchini. Licha ya kwamba kuporomoka kwa shilingi kunafanya bidhaa zetu za kuuza nje kuwa rahisi, lakini huchukua muda kuzalisha bidhaa hizo na hasa kilimo kuweza kufaidika hali hiyo. Kwa hiyo ni faida kwa nchi kwa sasa kuwa na sarafu stahmilivu ( stable) iliyojengwa kwenye misingi imara ya Uchumi. Hata hivyo, inaonekana kuwa sarafu ya Tanzania inahujumiwa. Kuporomoka kwa Shilingi katika wiki za hivi karibuni sio matokeo ya nguvu za soko bali ni matokeo ya hujuma ( currency manipulations).

Mabenki makubwa ya kigeni nchini, inasemekana, katika miezi ya karibuni yamefanya currency manipulations na kupelekea dola chache kukimbizwa na shilingi nyingi na hivyo bei ya dola kupanda bei. Hii inatokana na ukweli kwamba Benki zetu kubwa tatu zinazoongoza zinaendeshwa na wageni. Inasemekana biashara hii hufanyika kati ya matawi ya Benki za kigeni hapa nchini na makao makuu yao. Kuporomoka kwa shilingi kunakotokea hivi sasa hakuendani na kuporomoka kwa miaka ya nyuma kipindi kama hiki (ambacho ki kawaida ni miezi shilingi hushuka thamani kwa sababu ya watalii kuwa wachache na mauzo ya bidhaa nje kuwa madogo sana). Wastani wa miaka 10 iliyopita inaonyesha kuwa kipindi hiki shilingi hushuka kwa kati ya 8% mpaka 13% na sio kuporomoka kwa zaidi ya 20% kulikotokea hivi sasa. Kwa mfano mwaka 2011 miezi kama hii ( Februari – Mei) Shilingi iliporomoka kutoka shs 1,380 kwa dola 1 mpaka shs 1,570 sawa na mporomoko wa 12%. Hata hivyo kuanzia mwaka huo mpaka mwaka 2014 shilingi imekuwa ikishuka thamani kwa kiwango kidogo sana. Mwaka 2013 thamani ya shilingi ilishuka kwa wastani wa asilimia 1.7 tu.

Uchambuzi huu wa thamani ya sarafu yetu unaonyesha kuwa kuna zaidi ya nguvu ya soko kunakotokana na mauzo yetu nje kuwa machache. Vile vile kupanda kwa thamani ya dola ya marekani duniani hakutoshi kuelezea mporomoko huu wa kasi wa shilingi kuanzia mwezi Disemba mwaka 2014 mpaka sasa. Tuhuma za mabenki kuwa yanahujumu shilingi (currency manipulations) zaweza kuwa na ukweli.

Vile vile, inasemekana kumekuwa na utoroshaji mkubwa wa dola kutoka nchini kwenda nje ya nchi. Utoroshaji huu unafanyika kupitia wasafiri wanaopita ukumbi wa VIP uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es Salaam. Utoroshwaji huu unatokana na hofu isiyo ya msingi kwamba uchaguzi utakuwa na vurugu. Utoroshwaji wa fedha ni kinyume sheria zetu. Sheria zetu za fedha za kigeni zinazuia mtu kubeba zaidi ya dola 10,000 za kimarekani zikiwa taslimu, kuingia nazo nchini au kutoka nazo nchini. Tafiti za haraka zinaonyesha kuwa huu umekuwa ni utaratibu wa kawaida kila mwaka wa uchaguzi tangu mfumo wa vyama vingi uanze.

Benki Kuu ya Tanzania inapaswa kuchukua hatua zifuatazo;

  1. Kufanya uchunguzi wa kushtukiza mara moja dhidi ya benki zote za kigeni zilizopo hapa nchini. Uchunguzi huu utazame biashara ya fedha za kigeni ya benki hizi kwa lengo la kuzuia ‘ currency manipulations’ na kuchukua hatua madhubuti dhidi ya Benki yeyote itakayokutwa imehujumu biashara ya fedha za kigeni kwa lengo la kushusha thamani ya shilingi dhidi ya dola za kimarekani.
  2. Jeshi la Polisi na kitengo cha kuzuia utoroshaji wa fedha ( anti money laundering unit) kufanya ukaguzi wa lazima wa watu wote wanaosafiri kwenda nje ikiwemo wanaopita sehemu ya watu mashuhuri (VIP Lounge) ili kudhibiti utoroshaji wa fedha za kigeni kwenda ughaibuni.
  3. Watanzania tufikirie upya nafasi ya Mabenki katika uchumi wa nchi na kufanya maamuzi magumu ya kurejesha baadhi ya Benki katika umiliki mpana zaidi wa Watanzania. Kwa malengo ya muda wa kati, Benki kubwa 3 nchini ilazimu kuwa na umiliki unaozidi 51% wa Watanzania. Bila ya kushika mabenki nchi itachezewa sana.
  4. Suluhiho la kudumu la sarafu stahmilivu ni kuongeza uzalishaji wa bidhaa za kuuza nje ya nchi na kupunguza manunuzi ya bidhaa kutoka nje. Urari wa Biashara wa Tanzania umepanuka kutoka $1bn mwaka 2004 mpaka $6bn mwaka 2013 (BOT 2013) kutokana manunuzi yetu nje kukua kwa kasi kutoka $2.5bn mpaka $11bn wakati mauzo yetu nje yakikua kwa kasi ndogo kutoka $1.4bn mpaka $5bn katika kipindi hicho. Isingekuwa uimara katika urari katika uwekezaji na uhamisho wa mitaji, Tanzania ingekuwa na sarafu yenye thamani sawa na takataka. Serikali ihimize uzalishaji mali mashambani na viwandani na kuuza nje biadhaa zilizoongezwa thamani. Zama za kutegemea dhahabu zimekwisha na sio endelevu. Turudi kwenye misingi: Bidhaa za Kilimo na Viwanda.

Tutaendelea kufuatilia thamani ya shilingi mpaka ifikapo mwezi Julai ambapo ndipo kipindi kigumu kwa shilingi huwa kihistoria. Hatua zilizoainishwa zisipotazamwa na mamlaka tajwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani yaweza kufikia tshs 3000!

[1] Zitto Kabwe ni Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo. Amepata kuwa Waziri Kivuli wa Fedha na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya PAC

[2] Benki Kuu kuingiza $ kwenye soko kuna hatarisha kupunguza Akiba ya fedha za Kigeni. Kutokana na ujinai unaoendelea kwenye soko la fedha za kigeni nchini, BoT kuendelea kumwaga fedha za kigeni inaweza kuwa ni mkakati wa kudumu wa wanaofaidika na ‘currency manipulations’. Kushinikiza Benki Kuu kuendelea kubomoa foreign reserve ni kutokuona mbali na kujaribu kujiridhisha kwa kutibu dalili za ugonjwa badala ya ugonjwa wenyewe.

Written by zittokabwe

May 3, 2015 at 10:40 AM

PAC imeanza uchunguzi kuhusu ukwepaji kodi unaofanywa na makampuni ya Kimataifa

leave a comment »

PAC imeanza uchunguzi kuhusu ukwepaji kodi unaofanywa na makampuni ya kimataifa.

Leo tarehe 30 Machi 2014, kamati ya BUNGE ya PAC imeanza rasmi uchunguzi kuhusu ukubwa wa tatizo la ukwepaji kodi na utoroshwaji wa fedha unaofanywa na makampuni ya kimataifa ( multinational corporations). Uchunguzi huu unatokana azimio la umoja wa kamati za PAC za nchi za SADCOPAC lilioamuliwa Arusha, Tanzania mwezi Septemba mwaka 2013 ( Azimio lilisomeka – PACs should initiate investigations on the extent of tax avoidance/evasion and illicit money transfer in their jurisdiction).

Leo PAC imekutana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Kitengo cha Fedha Haramu ( FIU) na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ajili ya majadiliano ya awali kuhusu uchunguzi huo.

Kamati imeelezwa kuwa tatizo la ukwepaji kodi ni kubwa sana na linagusa sekta zote. TRA imeieleza kamati mifano mbalimbali kwa kila sekta namna gani Taifa linapoteza kodi. Njia zinazotumika ni pamoja na udanganyifu katika mikopo, udanganyifu katika bei za mauzo ya bidhaa zinazouzwa nje na mikataba ya biashara miongoni mwa makampuni yanayohusiana. Uchunguzi uliofanywa na TRA kwa kampuni mojawapo wa uchimbaji madini unaonyesha kuwa kampuni hiyo iliyotangaza hasara mwaka 2011 iligundulika kuwa kumbe ilipata faida ya dola za kimarekani 327 milioni.

Sekta ya Utalii na mahoteli inaonyesha kugubikwa kiasi kikubwa na ukwepaji kodi kwa kampuni katika sekta hiyo kutumia mikataba na makampuni yanayohusiana yaliyokwenye Tax Havens ambayo inahamisha mapato mengi kwenda offshore (profit shifting and base erosion).
Kamati imeelezwa na BoT kuwa hivi sasa kuna uchunguzi maalumu unaoendelea kuhusu ‘illicit financial transfer’ kutoka Tanzania.

Pia ameeleza kwamba hatua zimeanza kuchukuliwa kufunga akaunti za makampuni ya madini yaliyopo offshore kwani sababu za makampuni hayo kuwa akaunti nje hazina msingi tena. Hata hivyo changamoto kubwa ni mikataba waliyoingia na Serikali ambayo inawaruhusu kufungua akaunti offshore na kuweka mapato yao yote ya mauzo ya madini huko.

Utoroshaji wa fedha kutoka Tanzania ni changamoto kubwa sana ya maendeleo ya Tanzania katika kupambana na umasikini. Utoroshwaji umekuwa ukikua mwaka hadi mwaka. Taarifa ya benki ya maendeleo Afrika inaonyesha kuwa mwaka 2010 peke yake Tanzania zilitoroshwa jumla ya dola za kimarekani bilioni 1.3 ambazo zilikuwa sawa na asilimia 5 ya Pato la Taifa (GDP) na zaidi ya asilimia 20 ya mapato ya ndani ya TRA.

Kamati ya PAC itaendesha uchunguzi na kuandaa taarifa itakayowasilishwa bungeni kwa hatua zaidi. Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa BUNGE la Tanzania kuendesha uchunguzi wa aina hii. Pia Tanzania imekuwa nchi ya kwanza katika eneo la SADC kutekeleza azimio hili. Nchini Uingereza kamati ya PAC ya BUNGE la uingereza iliendesha uchunguzi kama huu na makampuni makubwa kama google, Amazon na Starbucks waligunduliwa kukwepa kodi nchini humo. Kwa nchi za Afrika sekta yenye kutorosha fedha na kukwepa kodi kwa wingi ni sekta ya madini, mafuta na gesi. Mwaka 2013 mwezi Desemba kamati ya PAC Tanzania ilikutana na PAC – UK ili kupata uzoefu wa namna ya kuendesha uchunguzi wa aina hii.

Zitto Kabwe, MB
Mwenyekiti, PAC
Dodoma
30-03-2014

RELATED STORY: Africa’s $200 billion kept in foreign banks  (‘Rich beggar’ paradox that is Africa’s forex reserves)

Courtesy: THE EAST AFRICAN