Posts Tagged ‘Mafuta na Gesi Asilia’
Mtwara : Serikali inavunja nchi kwa kutosikiliza Wananchi
Mtwara : Serikali inavunja nchi kwa kutosikiliza Wananchi
Kwa wiki ya tatu mfululizo kumekuwa na malumbano kuhusiana na suala la ujenzi wa Bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam. Kumekuwa na madai yenye nguvu ya hoja kutoka kwa wananchi wa Mtwara dhidi ya porojo kutoka kwa viongozi wenye dhamana ya kujibu madai haya ya watu wa Mtwara. Watu wa Mtwara kwa umoja wao na kwa kuungwa mkono na viongozi wa dini zote wamekuwa wakitaka Serikali ifikirie upya suala la mradi wa ujenzi wa Bomba la gesi na badala yake kujenga mitambo ya kufua umeme mkoani Mtwara na kusafirisha umeme huo kwenda maeneo mengine ya nchi. Kwenye moja ya maandishi yangu (Serikali iwasikilize watu wa Mtwara) nimeshauri kuwa Taifa liwe na gridi nyingine ya Taifa ambayo itatokana na Gesi tu na ianzie Mtwara.
Ikumbukwe kwamba katiba ya nchi, ibara ya 9 katika mabano J inataka mamlaka ya dola na vyombo vyake vyote kuhakikisha ya kwamba shughuli zote za kiuchumi zinaendeshwa kwa namna ya kwamba pasiwe mrundikano wa utajiri au shughuli za uzalishaji kwa watu wa chache. Katiba inaendela kwa kuelekeza kwamba uchumi wa nchi upangwe katika uwiano sawia (9, d). Watu wa Mtwara wanatekeleza matakwa haya ya katiba kwa kukataa mrundikano wa shughuli za kiuchumi wa nchi na utajiri wa nchi kua kwenye mikoa michache na hasa mkoa wa Dar-Es-Saalam.
Serikali imekuwa ikitoa majibu ya porojo na kuwatusi watu wa Mtwara na kama ilivyozoeleka Rais Jakaya Kikwete na Mawaziri wake wamekuwa wakisema suala la Mtwara linatumika na wanasiasa kujitafutia umaarufu. Inasikitisha sana kuona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwaambia mabalozi wa nchi za kigeni waliopo hapa nchini kuwa yanayoendelea mkoani Mtwara yanachochewa na Wanasiasa tuliosimama na wananchi wanaodai haki ya kufaidi utajiri wa nchi yetu. Rais Kikwete na Mawaziri wake wameshindwa kabisa kuonyesha uongozi katika suala hili na hatimaye kuhatarisha umoja wa kitaifa.
Kwa udhaifu wa serikali na tabia ya kutafuta mchawi badala ya kutatua tatizo la msingi, wananchi wameendelea kukutana na hata wengine sasa kuanza kusambaza ujumbe wa kukata kipande cha nchi na kuanzisha Jamhuri ya Kusini. Nimeona kwenye mabango ya mkutano wa hadhara uliofanyika 19/1/2013 wananchi wakibeba mabango yanayoaishiria kuchoka kuwa sehemu ya Tanzania na kuanzisha Jamhuri ya Makonde kuanzia jiwe la Mzungu wilayani Kilwa mpaka mto Ruvuma. Haya yanatoka na kiburi cha Serikali kujishusha na kuwasikiliza wananchi wanao dai haki yao ya kikatiba.
Ni Serikali iliyokosa uhalali wa kutawala inayoweza kudharau hisia hizi za wananchi. Serikali ielewe kwamba kamwe haitaweza kulinda kila nchi ya bomba hili iwapo italijenga kwa nguvu. Badala ya kuzungumza na vyombo vya habari Serikali ifanye mazungumzo na wananchi wa Mtwara na kukubaliana na matakwa yao. Kitendo cha Serikali kung’ang’ania msimamo wake dhidi ya watu wa mtwara ni kitendo kinacho weza kuipasua nchi na hivyo kwenda kinyume na masharti ya katiba ibara ya 28 ambayo inasema: “kila raia ana wajibu wa kulinda uhuru wa nchi, uhuru mamlaka na umoja wa taifa.”ibara ya 28, 1.
Inawezekana Serikali inaogopa kuvunja makubaliano na Wachina ya mkopo wa dola za kimarekani 1.2 bilioni ambao imeuingia bila hata kushirikisha Bunge. Inawezekana Serikali na hasa watendaji wa Serikali waliojadili mkopo huu wameshapata chao na hivyo kuogopa kusikiliza madai halali ya wananchi. Lakini yote hayo hayawezi kuwa zaidi ya Umoja wa nchi yetu. Hatuwezi kukubali nchi yetu ipasuke vipande vipande kwa sababu tu ya kulinda mkataba wa bilioni 1.2 tuliokopa China, ambayo serikali inang’ang’ania.
Tunafahamu kwamba ubalozi wa China umeandika barua serikalini kuwaondoa raia wa China waliopo Mtwara kwa hofu ya maisha yao. Serikali inaficha ukweli huu kama ilivyoficha ukweli kwamba Naibu Waziri wa Nishati na Madini bwana George Simbachawene alifukuzwa na wananchi wa Mtwara alipokwenda hivi majuzi. Serikali itaficha ukweli mpaka lini? Lazima tupate majawabu.
Kwanza Serikali iweke wazi mkataba wa ujenzi wa Bomba hili. Kamati ya Bunge ya POAC ilipokuwa inapitia mahesabu ya TPDC iliomba mkataba na kwa mshangao mkubwa wabunge wakaambiwa Mkataba haupo TPDC bali upo Wizarani. Kwa nini Mkataba huu wa matrilioni ya Fedha unafichwa? Mkataba huu ulisainiwa pamoja mikataba mingine 2, mmoja wa kujenga nyumba za wanajeshi wa thamani ya dola za kimarekani 400 milioni na mwingine wa mawasiliano jeshini wa dola za kimarekani 110 milioni, na mikataba yote mitatu imesainiwa kimya kimya bila kushirikisha wananchi kupitia Bunge. Lazima mikataba yote hii iwekwe wazi.
Pili, Mkataba huu uchunguzwe kama unalingana na thamani ya fedha maana kwa utafiti wa awali inaonyesha kuwa bei ya ujenzi wa bomba imepandishwa maradufu. Wastan wa kujenga bomba la gesi duniani ni dola za kimarekani 1.2 milioni kwa maili moja. Mradi huu wa Tanzania utagharimu dola za kimarekani 2.2 milioni kwa kilomita moja (maili 1 ni sawa na kilomita 1.6).
Tatu, Serikali ibadilishe Mkataba huu kuwa wa mkopo wa kujenga Mitambo ya kufua umeme Mtwara na ujenzi wa Msongo wa Umeme kama gridi ya pili ya Taifa. Kwa sasa Tanzania ina gridi moja ambayo inabebwa na bwawa la Mtera linalo tegemea mto Ruaha ambao hivi sasa unakauka miezi 5 katika miezi 12 ya mwaka. Ni dhahiri kwamba kwa usalama wa Taifa na hata kwa gharama Nchi itafaidika zaidi kwa kujenga gridi nyingine kutokea Mtwara badala ya kusafirisha gesi kuja Dar-Es-Salaam.
Serikali haitashinda vita hii kwa kuzusha kwamba ama wanasiasa wanaopinga wanatumika na makampuni mengine au kwa mataifa ya magharibi kutaka kuvuruga nchi. Serikali ijitazame yenyewe. Bila kufanya hayo tunayo pendekeza hapo juu, wananchi wataendelea kupigania hako yao. Hii ni vita ya uwajibikaji. Wananchi wanataka kufaidika na rasilimali za nchi yao. Kwa vyovyote vile upande wa wananchi utashinda. Vita ya uwajibikaji kwenye rasilimali za nchi sio ya vyama vya siasa, ni vita ya wananchi. Chama cha siasa kitakachokwenda kinyume na matakwa ya wananchi, kinajichimbia kaburi.
Mchango wangu Bungeni-Hotuba ya Waziri Mkuu: Haki za Uraia, Mafuta/Gesi Asilia na Uwajibikaji
MHE. ZITTO Z. KABWE:
Unyanyasi wa Watu wa Kigoma
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia Hotuba hii ya Waziri Mkuu. Jana Mheshimiwa Waziri amekuja kuomba Bunge limuidhinishie jumla ya shilingi trilioni 3.8 kwa ajili ya Ofisi yake na taasisi zote zilizo chini ya Ofisi yake pamoja na takribani shilingi bilioni 113 kwa ajili ya Bunge. Fedha zote hizi takribani shillingi trilioni 3.2 zinakwenda Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla hatujaweza kumuidhinishia Mheshimiwa Waziri Mkuu fedha hizi na yeye kama Mkuu wa Shughuli za Serikali, msimamizi wa kazi za Serikali za kila siku na ambaye anaangalia utendaji wa takribani Mawaziri, wote ni vizuri aweze kutoa majibu kwa baadhi ya masuala ambayo mengine ameyaainisha kwenye hotuba yake, lakini mengine hakuyaainisha katika hotuba yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na Kigoma. Mheshimiwa Waziri Mkuu katika ukurasa wa 51 wa Hotuba yake amezungumzia masuala ya ulinzi na usalama lakini hakugusia kabisa operesheni ambazo zinaendelea hivi sasa katika Mkoa wa Kigoma nadhani na Mkoa wa Kagera kuhusiana na masuala ya wahamiaji haramu. Hivi tunavyozungumza ni kwamba mamia ya watu wa Kigoma wameonyeshwa kwamba siyo raia wa Tanzania. Utaratibu huu umekuwa ukiendelea mwaka hadi mwaka. Napenda Mheshimiwa Waziri Mkuu akumbuke historia baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia kati ya mwaka 1918 na mwaka 1924 Kigoma haikuwa sehemu ya Tanganyika. Kigoma ilikuwa inatawala kama inavyotawaliwa tofauti sasa hivi Burundi kama inavyotawaliwa sasa tofauti Rwanda. Kwa muda mrefu sana Mkoa wa Kigoma umeachwa nyuma katika kila kitu eneo la maendeleo.
Mimi nimeona lami ya kwanza ya highway mwaka 2008. Miaka zaidi ya 40 baada ya uhuru. Leo hii watu wa Kigoma wa maeneo ya Kusini mwa Kigoma wa maeneo ya Kaskazini mwa Kigoma wanasombwa kwenye maboti, wanasomwa kwenye magari wakiambiwa kwamba siyo raia wa Tanzania. Hatuwaoni Wamakonde wakiambiwa kwamba siyo raia wa Tanzania na wanapakana na Msumbiji. Hatuwaoni Wamasai wanaambiwa siyo raia wa Tanzania na wanapakana na Kenya. Hatuwaoni Wachaga wanaambiwa siyo raia wa Tanzania wanapakana na Kenya. Hatuwaoni Wanyakyusa wanaambiwa siyo raia wa Tanzania wanapakana na Zambia na vile vile wanapakana na Malawi.
Kwa nini suala hili liwe ni kwa watu wa Kigoma na watu wa Katavi peke yake? Kwa nini tunatumia fedha za nchi, polisi wa nchi kwenda kusumbua watu wa Kigoma. Nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu operesheni inaendelea sasa hivi katika Mkoa wa Kigoma kuwanyanyasa Raia wa Kigoma waonekane ni Raia wa Tanzania wa daraja B ikome mara moja na viongozi wa Kisiasa, Wabunge wote wa Mkoa wa Kigoma na Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa tukae tuweze kuangalia kwa sababu kuna uonevu wa hali ya juu sana katika operesheni ambayo inaendelea hivi sasa.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba niyaseme hayo vizuri na ninarejea kwamba tumefundishwa na wazee wetu kwamba sisi kati ya mwaka 1918 na mwaka 1924 hatukuwa sehemu ya Tanganyika iliyokuwa inatawaliwa na Mwingereza. Ninaomba nirejee sisi ni watu wa Kigoma kwanza kabla hatujawa wa Tanganyika, kabla hatujawa Watanzania. Ninaomba nilisisitize hili na watu wa Kigoma wananisikia kwa sababu tumenyanyaswa sana. Ninaomba masuala ya uraia yaangaliwe kwa karibu sana. Huu ni ujumbe ambao nimepewa na watu wa Kigoma nimeombwa niueleze na naomba Ofisi ya Waziri Mkuu, Mkuu wa Kigoma yupo hapa, Wakuu wa Wilaya, Kamanda Mkuu wa Mkoa wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma na IGP waweze kuliangalia jambo hili kuweza kuhakikisha kwamba tunawalinda raia wa Kigoma.
Wenye Mabilioni Uswisi(Switzerland)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Mheshimiwa Waziri Mkuu kumekuwa na taarifa ambazo zimeandikwa katika vyombo vya habari toka wiki iliyopita. Lilianza Gazeti la The East African baadaye wakaja Gazeti la The Citizen na leo nimesikia kwamba Gazeti la Mwananchi limezungumza kwamba kuna Watanzania 6 wana fedha katika akaunti kule Uswisi zaidi ya shilingi bilioni 303. India walipopata taarifa hizi kutoka Benki ya Uswisi waliwataja majina watu wote wana siasa na wafanyabiashara wenye fedha nje na fedh zile zikachunguzwa zile ambazo zimepatikana kwa haramu zikarejeshwa India. Nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu uagize TAKUKURU na vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama kwanza tutambue ni Watanzania gani hawa na fedha hizi zimepatikana kwa njia zipi na zile ambazo zimepatikana kwa njia ya wizi na ufisadi zirejeshwe nchini mara moja. Kwa sababu hatujaanza kunyonya utajiri huu wa gesi tayari kuna watu ambao wameshaanza kutajirika nao.
Tutakapoanza kunyonya hali itakuwaje? Kwa hiyo, nilikuwa naomba suala hili Serikali ilichukulie kwa uzito mkubwa ili itume salaam kwa mtu yeyote ambaye anatarajia kwamba atafaidika na utajiri wa rasilimali ya nchi kama gesi na madini na kadhalika ajue kwamba kokote atakapoficha fedha zake tutazifuata na zitarudi katika nchi hii. Nilikuwa naomba Waziri Mkuu aweze kuliangalia jambo hili kwa ukaribu sana.
Zuia Makampuni ya Kigeni kwenye Ulinzi
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu hivi sasa Kiongozi wa Upinzania amezungumza jana kuna meli ziko Pwani ya Mkoa wa Pwani, Lindi na Mtwara zinatafuta mafuta. Mheshimiwa Waziri Mkuu hakuna kampuni hata moja ya mafuta inayonunua hata mchicha kutoka Tanzania. Meli zote ambazo ziko Bandari Mtwara zinakwenda kupeleka huduma kwenye maeneo ambayo yanatafuta mafuta yanapata mchele, nyanya, vitunguu, mchicha, mafuta ya kula na kadhalika kutokea Kenya kwa sababu hatujaweka utaratibu wa kufanya nchi yetu iweze kufaidika na utaraji huu mwanzoni. Kwa sababu hatua hizi za mwanzoni hakuna kodi ambayo tunapata kwa sababu mafuta bado yanatafutwa.
Hatua hizi za mwanzoni tunatakiwa tufaidike na fedha inayokuja, watu waweze kutumia fedha za kutoka ndani. Lakini hali ilivyo hivi sasa ni kwamba makampuni ya mafuta yanatumia zaidi ya dola milioni 161 kwa ajili ya shughuli za ulinzi na makampuni yanayolinda, ni makampuni ya nje. Yanabeba silaha kubwa kubwa, siku yakiamua kutugeuka na Navy yetu ilivyo tutapata shida. Nilikuwa naomba tutenge resources za kutosha na hata kama hatujaziweka kwenye bajeti sasa hivi, tuangalie, tuimarishe Navy na tupige marufuku, tuandike sheria kabisa kwamba itakuwa ni marufuku kwa raia yeyote wa kigeni kubeba silaha zozote kubwa ili kuweza kuhakikisha kwamba ulinzi ama unafanywa na watu wa ndani au unafanywa na Navy yetu tuweze kulinda mipaka yetu vizuri.
Utafutaji Mafuta Zanzibar Uendelee
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili kuna suala ambalo halijaisha na Kiongozi wa Upinzani Bungeni jana amelizungumzia la mafuta na gesi katika masuala ya muungano. Nilikuwa naomba jambo hili tulimalize kwa haraka. tulimalize kwa haraka na mimi sioni ubaya kwa kweli, sioni ubaya hata kidogo kama tukiamua kwamba shughuli zote commercial not upstream, sio masuala ya regulation, sio masuala ya vibali, sio masuala ya kutoa leseni, masuala yote commercial yanayohusiana na mafuta na gesi, kila upande wa muungano ushughulike na masuala yake.
Hakuna sababu ya kunga’gania jambo hili kama sisi tuna dhahabu, tuna tanzanite, tuna madini hayapo sehemu ya muungano, kwa nini mafuta na gesi yawe sehemu ya muungano? Hili ni jambo ambalo tulimalize, liishe tuimalize hii kero, vikao na vikao havitasaidia, tuimalize hii kero, tu-move forward watu wa Zanzibar waanze utaratibu wao wa kufanya utafutaji wao, waangalie kama watayapata hayo mafuta au hawatayapata, sisi tayari huku Bara tumeshapata, tuna matrilioni ya gesi, basin a wenyewe tuwaache waendelee na utaratibu wao. Hakuna sababu ya kuchelewesha jambo hili tuweze kulimaliza mapema.
TZS 40 Bilioni kwa Kiwira
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni suala la Kiwira na baadae nitakuwa na mazungumzo na baadhi ya Mawaziri kuhusiana na suala hili tuliangalie kwa makini. Tumetenga shilingi bilioni 40 kwenye fedha ya maendeleo Wizara ya Nishati na Madini kwa ajili ya nini? Kuna fedha ambayo tunaenda kuwalipa watu ambao wameuharibu mgodi. Kwa nini tulipe watu ambao wameuharibu mgodi?
Lakini tunaenda kulipa bilioni 40 sio kwa Kiwira nzima..
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
******
Related Story in THE Citizen(Wednesday, 27 June 2012): Zitto wants Swiss bank accounts investigated probed