Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Posts Tagged ‘nzega

Siku ya 8 Ziara CHADEMA Kanda ya Magharibi imetufikisha Jimbo la Nzega

with 2 comments

Siku ya 8 imetufikisha Jimbo la Nzega

Tumefanya mikutano 8 katika kata 8 lakini mikutano mikubwa ilikuwa kata za Puge na Ndala. Mkutano wa Nzega mjini ulikuwa mkubwa sana na umevunja rekodi ya mikutano ambayo nimewahi kufanya Nzega.

Nikiwa na viongozi wa CHADEMA mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi tumezungumza na wananchi kuhusu hali ya maisha na mabadiliko ya kisiasa yanayotakiwa. Tumeendelea kuonyesha namna nchi yetu ilivyo na mataifa 2 ndani ya nchi moja kutokana na tofauti za kimaendeleo kati ya mijini na vijijini na tofauti kubwa za kipato kati ya matajiri na masikini.

Ajenda za siku zilikuwa mabadiliko ya katiba, uwazi na uwajibikaji, siasa na vijana na hifadhi ya jamii kwa wakulima.

Nimewataka vijana waache kutumiwa na makundi ya wanasiasa kuumiza vijana wenzao na badala yake wajikite kwenye kusaidiana ili kubadili uongozi wa nchi. Nimewaambia vijana kuwa wao ni asilimia 65 ya wapiga kura wote nchini hivyo hii ni nchi yao na lazima wawe na uchu wa mabadiliko.

Nimewataka mawaziri Wassira, Lukuvi na Chikawe wajiuzulu nafasi zao kwa kushindwa kusimamia vema mchakato wa katiba na kumwambia uwongo Rais. Pia Waziri Mkuu kushindwa kuchukua hatua za kujenga mwafaka ndani ya Bunge na hivyo kila jambo kutegemea Rais aingilie kati. Kazi ya Waziri Mkuu bungeni ni nini?

Nimerejea kusisitiza Sera ya Hifadhi ya Jamii kwa Wakulima. Imefikia wakati Serikali kupitia SSRA ione umuhimu na ulazima wa kuhakikisha tunaongeza Watanzania wenye hifadhi ya jamii kwa kuanza mfumo maalumu wa hifadhi ya jamii kwa wakulima (Supplementary scheme for social security to small holder farmers). Ninapendekeza Serikali ichangie nusu kwa nusu na mkulima ili kuvutia uwekaji akiba katika nchi na kuwa na sera ya uwekezaji katika maeneo yatakayo mwinua mkulima kama miundombinu ya umwagiliaji, mikopo nafuu kwa wakulima kwenye pembejeo na nyumba na bima ya afya.

Nimezungumzia umuhimu wa uwazi katika matumizi ya fedha za umma ikiwemo malipo ya watumishi na viongozi wa umma. Nimewaeleza wananchi wa Nzega kuwa siku ya jumanne kamati ya PAC itaanza kukagua mahesabu ya vyama vya siasa nchini. Vyama vya siasa vinatumia fedha za umma takribani tshs 20bn kila mwaka kama ruzuku. Ni haki kwa wananchi kujua fedha zinatumika namna gani.

Wananchi wa Nzega wana changamoto nyingi sana. Wakulima wa Pamba walipewa madawa feki ya kuua wadudu, michango ya hovyo hovyo ni mingi mno na unyanyasi wa wana chadema ni mkubwa vijijini. Kata ya Ndala, wananchi wamejenga Kituo cha Afya lakini hakina wahudumu na mradi wa maji limeanza kuvuja kabla ya mradi kuanza. Changamoto zote hizi zinajibika, muhimu ni kufanya mabadiliko kwa kuondoa CCM madarakani na kuimarisha uwazi na uwajibikaji.

This slideshow requires JavaScript.

Written by zittokabwe

October 13, 2013 at 9:17 AM

Siku ya 7 CHADEMA Kanda ya Magharibi- Jimbo la Bukene, wilaya ya Nzega

leave a comment »

Timu ya CHADEMA kanda ya Magharibi ikijumuisha Mwenyekiti wa Kanda Ndg. Mambo na Wenyeviti wa Mikoa 3 ya Kigoma, Tabora na Katavi tumetembelea Jimbo la Bukene, wilaya ya Nzega.
Kama ilivyo kwa mikutano iliyopita tumezungumza umuhimu wa Katiba na mchakato wake kutopendelea chama chochote cha siasa kwani tunaandika katiba ya nchi, umuhimu wa mwafaka wa kitaifa na kuwapongeza viongozi wakuu wa vyama kwa kukubali kufanya mazungumzo ili kupata mwafaka. Pia tuliwaambia wananchi wasikubali mbinu chafu za kutaka kuongeza muda wa Bunge mpaka 2017 kwani itakuwa ni kinyume na katiba yenyewe.
Wananchi wa Bukene ni wakulima wa Pamba na sehemu kidogo Tumbaku. Kioja tulichokikuta Bukene ni wananchi kuuziwa dawa za Pamba feki ambazo haziui wadudu! Wananchi wa vijijini wanafanyiwa kila aina ya dhulma na kukandamizwa.
Pia tulielezwa namna watendaji wa vijiji na kata wanavyonyanyasa raia kwa kujifanya wao wakamataji, waendesha mashtaka na mahakimu. Wanatoza faini wananchi kwa kesi za kubambika. Itabidi tutafute namna ya kuhakikisha hatua zinachukuliwa dhidi ya watendaji wa kata na vijiji wanaokiuka misingi ya utawala bora. Wananchi wa vijijini wana haki ya kuishi kama raia wengine wa Tanzania. Tusiwasahau

This slideshow requires JavaScript.

Written by zittokabwe

October 12, 2013 at 9:21 AM

Ziara ya Tabora: Watu wa Mtwara wanauliza Mnatuaachaje?

leave a comment »

Written by zittokabwe

May 24, 2013 at 1:31 PM