Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Posts Tagged ‘bajeti

BAJETI MBADALA 2012-2013

with 18 comments

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI NDUGU KABWE ZUBERI ZITTO (MB), WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI, KUHUSU MAPENDEKEZO YA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013

View this document on Scribd

PRESS RELEASE: On Government Austerity Measures-Cut Re-current Expenditure Not Development Expenditure

with 15 comments

PRESS RELEASE

MPANGO WA SERIKALI KUPUNGUZA MATUMIZI

Punguza Matumizi ya Posho SIYO Matumizi ya Reli, Barabara, Elimu na Afya

Mwezi Disemba mwaka 2011 Waziri wa Fedha na Uchumi alimwandikia barua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) kumwahidi mambo yepi Serikali ya Tanzania itafanya ili kurekebisha Bajeti yake. Utaratibu huu hufanyika kila mwaka kupitia mpango unaoitwa ‘Policy Support Instrument (PSI). Katika barua hiyo Waziri wa Fedha wa Tanzania ameahidi kwamba Serikali itafanya juhudi kupunguza matumizi ili kuweza kupunguza uwiano wa nakisi ya Bajeti na Pato la Taifa (fiscal deficit to GDP ratio) kutoka asilimia 7.2 mpaka asilimia 6.6 ya Pato la Taifa.

Waziri wa Fedha na Uchumi ameiambia IMF kwamba ifikapo mwisho wa Mwezi Disemba mwaka 2011 (wiki mbili zilizopita) Baraza la Mawaziri la Tanzania limefikia maamuzi ya kupunguza nakisi ya Bajeti kwa kiwango kilichotajwa. Maeneo yanayotajwa ni Pamoja na Miradi ya Maendeleo ambapo jumla ya miradi yenye thamani ya Tshs 157bn itakatwa. Waziri
wa Fedha ametaja miradi hiyo katika Ukarabati na Ujenzi wa Miundombinu.

Kambi ya Upinzani Bungeni inapinga kuondolewa kwa miradi ya maendeleo ili kupunguza matumizi ya Serikali. Kimsingi wakati kama huu ambapo hali ya uchumi ni mbaya na vijana wengi vijijini na mijini hawana ajira tunasisitiza umuhimu wa kutumia zaidi kwenye miradi ya maendeleo.

Punguza matumizi ya kawaida

Kambi ya Upinzani Bungeni inarejea wito wake kwa Serikali kupunguza matumizi ya kawaida ili kupata fedha za kutosha kwa ajili ya maendeleo. Haiwezekani kamwe tukawa Taifa huru iwapo miradi yetu yote ya maendeleo inafadhiliwa na wahisani. Kiwango kidogo tulichokiweka katika Bajeti ya mwaka huu ndicho hicho sasa kinakatwa na hivyo miradi yote ya maendeleo kubakia kwa wahisani ama kwa mikopo au misaada. Kiwango cha Tshs 203bn sawa na 0.5% ya Pato la Taifa ambacho Serikali imeahidi kupunguza ni kidogo mno na kinalenga kuumiza watumishi wa kada ya chini ya Serikali na sio viongozi wakubwa. Bajeti ya Mafunzo inayoenda kukatwa itaumiza Manesi na Walimu au watumishi wanaoongeza ujuzi ili kuboresha kazi zao. Serikali ikate matumizi yote yasiyo ya lazima na hasa posho (360bn), ipunguze matumizi ya magari na yale yasiyo na uhitaji yapigwe mnada na viongozi wote isipokuwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika na Jaji Mkuu washushwe madaraja ya kusafiria kwenye ndege. Safari zote ambazo hazina mahusiano na miradi ya maendeleo zipigwe marufuku kwa muda wote wa miezi sita ya Bajeti iliyobakia.

Serikali ihakikishe matumizi katika Sekta ya Elimu na Afya hayakatwi kabisa ili kuhakikisha tunalinda mafanikio kiduchu ya upanuzi wa sekta hizi na kuongeza uwezo wa Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi hasa wa vijijini.

Matumizi ya Maendeleo yasiguswe, yaongezwe

Tayari imeonekana kwamba katika kipindi chote cha nusu ya Bajeti Halmashauri za Wilaya hazijapata fedha za maendeleo. Mfano Halmashauri ya Wilaya Kigoma imepata asilimia 0.3 tu ya Bajeti ya Maendeleo ilhali Halmashauri ya Mji wa Mpanda imepata asilimia 4 tu. Ni dhahiri miradi ya maendeleo kwa maeneo mengi ya vijijini itakwama kwani ni wazi kabisa kwamba Halmashauri hazipati fedha zote za Bajeti ya Maendeleo. Serikali itambue kwamba miradi ya maendeleo sio anasa bali ndio vyanzo vya baadaye vya mapato ya serikali. Miradi ya maendeleo hutoa ajira kwa wananchi na hivyo kuwapunguzia umasikini wa kipato. Jumla ya Tshs 157bn zinazotakiwa kukatwa zisikatwe bali ziongezwe ili kupata fedha za kurekebisha miundombinu kama Reli ya Kati.Kwa mfano Reli ya Kati inahitaji Tshs 200bn katika kipindi cha miaka 3 ili iweze kusafirisha mizigo tani 1.5m kwa mwaka kila siku na kuzalisha faida.

Ongeza Mapato ya Ndani

Inashangaza kwamba katika mpango wa Serikali kupunguza nakisi ya Bajeti mkazo umewekwa kwenye kuondoa miradi ya maendeleo badala ya kuongeza mapato. Nakisi hupunguzwa ama kwa kupunguza matumizi au kwa kuongeza Mapato. Serikali katika Taarifa yake kwa IMF imeibua njia moja tu ya kuongeza mapato, kodi ya mapato kutoka Kampuni ya Geita Goldmine. Huu ni uvivu wa kufikiri.

Serikali imeambiwa mara kadhaa suala la kuanza kutumika kwa sheria mpya ya madini kwa Kampuni za Madini zilizokuwapo. Makusanyo ya Mrahaba peke yake kwa sheria mpya, kiwango kipya na kanuni mpya ya kukokotoa ingeongeza mrahaba mpaka Tshs 203bn kutoka Tshs 99bn za sasa. Kwanini Serikali ianvuta miguu katika kutekeleza hili? Waziri wa Nishati na Madini aliahidi Bungeni kwamba mazungumzo na Kampuni za Madini yanaisha Mwezi Septemba. Mbona Serikali imekuwa BUBU katika hili?

Serikali iliahidi kuangalia suala la mauzo ya mali za makampuni zilizoko Tanzania na kodi ambayo tunapaswa kukusanya, Serikali imekuwa kimya kabisa katika suala hili. Marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa kuondoa msamaha kwenye ‘deemed capital goods yangeongeza mapato ya Serikali kwa kiwango kikubwa na kupunguza mzigo wa
misamaha ya Kodi.

Uwajibikaji kwa Bunge

Inashangaza zaidi kwamba sasa imekuwa ni mtindo kwa Serikali kutoa ‘commitments’ muhimu za kibajeti kwa Shirika la IMF badala ya wananchi kupitia Bunge. Bunge limepitisha Bajeti, mapitio yeyote ya Bajeti yanapaswa kuidhinishwa na Bunge. Bila kufanya hivyo maana ya Bunge kupitisha Bajeti inakuwa haina mantiki na uhuru wa Taifa letu unakuwa haupo kwetu.

Umuhimu wa Bunge kutunga haraka Sheria ya Ofisi ya Bajeti ya Bunge (Parliamentary Budget Act) sasa unaonekana waziwazi. Muswada umewasilishwa Bungeni na Wabunge binafsi kutaka kuundwa kwa mfumo wa kuisimamia Serikali katika Bajeti. Ofisi ya Spika wa Bunge ihakikishe muswada huu unachapishwa katika Gazeti la Serikali mara moja ili usomwe kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Sita wa Bunge na kutungwa kuwa sheria katika mkutano wa Saba.

Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ilete mpango wa kupunguza matumizi Bungeni ili ujadiliwe na kuidhinishwa na Bunge kabla ya kuanza kutumika. Vinginevyo Mpango wa Serikali kwa IMF utakuwa ni kudharau wananchi na kuuza uhuru wetu kwa Shirika la Fedha la Kimataifa. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema mwishoni mwa miaka ya Sabini ‘toka lini Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limekuwa Wizara ya Fedha ya Kimataifa (International Ministry of Finance)?’

Kabwe Zuberi Zitto, Mb

Waziri Kivuli Fedha na Uchumi

Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni (NKUB)

Dar es Salaam, 10 Januari 2012.

Uchumi wa Taifa hatarini: Mfumuko wa Bei tishio kwa Serikali, Wafanyabishara na Wananchi.

with 11 comments

=PRESS RELEASE=

Uchumi wa Taifa hatarini: Mfumuko wa Bei tishio kwa Serikali, Wafanyabishara na Wananchi.

Mfumuko wa Bei umezidi kuongezeka kama taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu inavyoonesha kwamba, wakati mfumuko wa bei mwezi Julai mwaka huu (Bajeti ya mwaka wa Fedha 2011/2012 ilipokuwa inaanza) ulikuwa asilimia 13, umefikia asilimia 19.2 mwezi Novemba. Hii maana yake ni kwamba, Bajeti ya Serikali iliyopitishwa na Bunge mwezi Juni 2011, imepunguza uwezo wa kununua bidhaa na huduma kwa takribani asilimia 6. Hii ni sawa na shilingi 780 bilioni kuyeyuka katika Bajeti katika kipindi cha miezi Minne tu ya utekelezaji wa wake. Kutokana na kasi ya ukuaji wa Mfumuko wa Bei ni dhahiri kwamba, itakapofika mwisho wa mwaka wa Bajeti Serikali itakuwa imepoteza kwa kiasi kikubwa uwezo wa kununua bidhaa na huduma kwa zaidi ya robo ya Bajeti yake.

Hali ni mbaya zaidi kwa wananchi kwani Mfumuko wa Bei za vyakula umekua kwa kasi kikubwa mno. Ofisi ya Takwimu imeonesha kuwa wakati mfumuko wa Bei za vyakula ulikuwa asilimia 14.8 mwezi Julai, umefikia asilimia 24.7 mwezi Novemba 2011. Ukilinganisha na bei za vyakula mwaka 2010, mwananchi amepoteza uwezo wa kununua chakula kwa zaidi ya robo katika ya Novemba 2010 na Novemba 2011. Jumla ya vyakula ambavyo mwananchi alinunua kwa shilingi 10,000 mwaka 2010, sasa atanunua kiwango kile kile kwa shilingi 12,500. Bei za vyakula zimeongezeka kwa kiwango hiki ilhali kipato cha mwananchi aghalabu kipo pale pale. Mwathirika mkubwa ni mwananchi wa kawaida wa kijijini ambaye mapato yake ni kidogo na hivyo sehemu kubwa huyatumia kununua chakula.

Ukiangalia kwa undani utakuta mfumuko wa bei wa bidhaa kama mchele, sukari, nyama na samaki umekua maradufu. Bei ya mchele imekua kwa asilimia 50, sukari asilimia 50, nyama asilimia 30 na Samaki kwa takribani asilimia 40. Bidhaa hizi zote ni muhimu sana kwa afya ya binadaamu na hasa watoto kwa upande wa vyakula vya protini. Tusipokuwa makini na kupata majibu sahihi ya tatizo la mfumuko wa bei za vyakula, wananchi wengi na hasa watoto watapata utapiamlo na Taifa kuingia gharama kubwa katika kuwapatia huduma ya afya.

Kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula, mfumuko wa bei wa mafuta ya taa na gesi asilia unapaa kwa kasi kama moto wa nyikani. Wakati mafuta ya taa yamepanda bei kwa asilimia 71 katika ya mwezi Novemba mwaka 2010 na mwezi Novemba 2011, bei ya gesi asilia imepanda kwa asilimia 35. Madhara ya hali hii ni makubwa mno maana wananchi watakimbilia kwenye matumizi ya mkaa na kuni, hata hivyo bei za mkaa zenyewe zimepanda kwa asilimia 24. Kwa hali hii, na kutokana na ukweli kwamba wananchi wengi wa Tanzania wapo kwenye mpaka wa umasikini na daraja la kati chini, juhudi za muongo mzima za kupunguza umasikini zitafutwa ndani ya mwaka mmoja tu.

Mfumuko wa Bei unasukuma Watanzania wengi zaidi kwenye dimbwi la umasikini, unapunguza uwezo wa Serikali kutoa huduma za jamii kupitia Bajeti na hata kutimiza mipango ya miradi ya maendeleo kama miundombinu ya barabara, umeme, bomba la gesi, madaraja nk. Mkakati mahususi unatakiwa kubadili hali hii. Hatua zifuatazo zinapendekezwa ili kuuhami uchumi na kupunguza upandaji wa kasi wa gharama za maisha.

1.     Kuongeza uzalishaji wa chakula kwa kuweka mbinu za kukuza uchumi wa vijijini ni njia mojawapo endelevu ya kupunguza mfumuko wa Bei hapa nchini. Serikali sasa iache maneno matupu kuhusu sekta ya uchumi vijijini kwa kuelekeza nguvu nyingi huko. Serikali iruhusu na ivutie kwa kasi na kutoa vivutio kwa wazalishaji binafsi wa Sukari na mpunga katika mabonde makubwa. Waziri wa Kilimo na Maafisa wake watoke Ofisini na kuhimiza uzalishaji mashambani, fedha zielekezwe kujenga miundombinu ya barabara vijijini.

Vyakula vilivyolundikana mikoa ya Mbeya, Iringa na Rukwa ambapo Serikali iliahidi kununua na kutotimiza ahadi yake vinunuliwe mara moja na kusambazwa mikoa yenye shida ya chakula kama Mwanza, Mara, Kagera na mikoa ya Kaskazini. Chakula kukuta msimu mwingine katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ni kashfa kubwa kwa Serikali na inaonesha Serikali isivyokuwa makini na maisha ya wananchi.

Wakati huu ambapo tunaweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa chakula, Serikali inunue chakula cha kutosha na hasa mchele na sukari kutoka nje na kukisambaza kwenye soko ili kupunguza upungufu wa bidhaa (scarcity) katika masoko.

Mfumo uliotumika kununua Sukari tani laki moja hivi karibuni usitumike tena kwani ulizaa rushwa ya hatari na ufisadi ambao haujaripotiwa kwenye kutoa vibali. Wizara ya Kilimo iruhusu wauzaji kutoka nje walete sukari nchini moja kwa moja na kununuliwa na Bodi ya Sukari kisha kuiuza kwa wauzaji wa Jumla. Mfumo wa kutoa vibali umeonesha kutokuwa na tija na kwa kweli kunufaisha maafisa wachache wa Wizara ya Kilimo na Bodi ya Sukari.

2.     Kitengenezwe kiwanda cha kutengeneza gesi ya matumizi nyumbani (LPG extraction plant) kwa haraka ili kupunguza bei ya gesi, kuepuka kuagiza gesi kutoka nje na hivyo kuokoa fedha za kigeni na kutengeneza ajira hapa nchini. Kupanda kwa bei ya gesi asilia kunatokana na kwamba Tanzania inaagiza gesi hii yote kutoka nje ilhali malighafi ya kutengeneza gesi ipo hapa Tanzania na kwa kweli huchomwa moto (flared). Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini liingie ubia na kampuni Binafsi ili kuwekeza katika kiwanda cha kuzalisha gesi hatimaye kushusha bei na hivyo kuwezesha wananchi wengi zaidi kutumia gesi kwa matumizi ya kupikia n.k, hivyo kutunza mazingira.

3.     Ushuru wote unaokusanywa kwenye Mafuta ya Taa upelekwe Wakala wa Nishati Vijijini ili kufidia kupanda kwa bei ya mafuta ya Taa. Mfumuko wa Bei katika bidhaa ya mafuta ya taa unatokana na uamuzi wa kuwianisha bei ya mafuta ya taa na diseli ili kuondoa tatizo la uchakachuaji wa mafuta. Tatizo limeondoka (au hatulisikii tena) lakini wananchi wanaumia sana. Uamuzi sahihi wa kisera ni kupanua huduma za umeme vijijini kwa kuipa fedha zinazotokana na ushuru wa mafuta ya taa Wakala wa Umeme Vijijini. Usambazaji wa Umeme Vijijini utaongeza shughuli za kiuchumi vijijini, kukuza uchumi wa vijijini, kuongeza mapato ya wananchi kwa kuongeza thamani za mazao yao na hivyo kupunguza athari za mfumuko wa bei.

4.     Sera ya Matumizi ya Serikali iangaliwe upya kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi yasiyo ya lazima, na kuelekeza fedha nyingi zaidi katika uwekezaji umma (public investments). Matumizi Mengineyo ya Serikali yanaongeza fedha kwenye mzunguko ama kwa kulipa watu wachache stahili mbalimbali kama posho n.k au kwa kununua bidhaa na huduma bila mpango, na hivyo kusukuma bei kuwa juu kinyume na uhalisia wa soko. Tafiti za mfumuko wa Bei Tanzania zinaonyesha kwamba sera za fedha na zile za matumizi (monetary and fiscal policy) zina nafasi kubwa katika kukuza mfumuko wa bei. Hivi sasa nakisi ya Bajeti inayopelekea Serikali kukopa kwa kwa kiwango kubwa inapandisha gharama za viwanda kukopa mitaji ya muda mfupi na hivyo kuongeza gharama za uzalishaji na kasha bei za bidhaa. Wizara ya Fedha ambayo mpaka sasa imekaa kama imeishiwa namna ya kufanya, inapaswa kuamka na kutoa maelekezo mapya kwa Wizara, Idara na Wakala za Serikali kuhusu namna ya kubana matumizi na kuziba mianya yote ya kukwepa kodi.

Hitimisho

Serikali imeonesha udhaifu mkubwa sana katika kusimamia uchumi katika nusu ya kwanza ya Bajeti ya mwaka 2011/2012 ambayo pia ni Bajeti ya kwanza ya kipindi cha pili cha Serikali ya awamu wa Nne. Kuna hatari ya dhahiri kwamba ifikapo mwezi Januari 2012 tutakuwa tumerejea mfumuko wa Bei wa kiwango cha mwaka 1992 (21.9%). Tusipochukua hatua za haraka tutafikia na hata kuzidi mfumuko wa Bei kiwango cha juu kabisa ambacho kilifikiwa mwaka 1994 (33%) na hivyo viwanda kushindwa kukopa kwenye Mabenki kwa mahitaji yao ya haraka ya mitaji ya muda mfupi, wazalishaji wadogo kushindwa kulipa mikopo yao kwenye Taasisi za fedha na hivyo kufunga uzalishaji, Shirika la Umeme kushindwa kabisa kulipa gharama za mafuta ya kuendesha mitambo na kipato cha mwananchi kutomudu gharama za za kila siku. Uchumi utadorora kabisa. Taifa litakuwa hatarini.

Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania na Wizara ya Kilimo na Chakula iamke kuhami uchumi dhidi ya adui namba moja, Mfumuko wa Bei. Huu sio wakati wa kupiga porojo, viongozi wafanye kazi zao, Wananchi wajitume.

Inabidi sasa turejee kauli mbiu za miaka 50 iliyopita za Uhuru ni Kazi. Tuseme Demokrasia ni Kazi. Demokrasia sio lelemama.

Ndg. Kabwe Zuberi Zitto, Mb

Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Waziri Kivuli Fedha na Uchumi

18 Disemba 2011

Written by zittokabwe

December 18, 2011 at 12:37 PM