Posts Tagged ‘Independent Power Tanzania Ltd (IPTL)’
Nashambuliwa, tunashambuliwa! PAC tunasema “Hatutetereki”
Nashambuliwa, tunashambuliwa! PAC tunasema “Hatutetereki”
Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya Kamati ninayoongoza ya PAC kuwasilisha Bungeni Taarifa Maalumu kuhusu ukaguzi maalumu wa akaunti ya Tegeta Escrow, kumekuwa na kampeni za chini chini zinazoendeshwa kwenye korido za Bunge na kwenye mitandao dhidi yangu binafsi na baadhi ya wabunge waliosimama kidete dhidi ya wizi wa fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania akaunti ya Escrow.
Baadhi ya tuhuma nimezipeleka kwenye vyombo vya dola ili zichunguzwe kwani zina vielelezo vya mahala pa kuanzia (kama leseni ya udereva ya mwanamke anajulikana kama Vivian Emmanuel Sirikwa na muhuri wa kampuni ya uwakili inayomilikiwa na Bwana Joseph Mkandege).
Baadhi ya tuhuma nitazijibu moja baada ya moja.
Waziri mmoja ambaye ni mtuhumiwa wa wizi wa fedha za Tegeta Escrow anazunguka kwa wabunge akisema tuhuma hizi kupikwa kama njia yake ya kuhamisha mjadala kutoka uporaji wa Tshs 200 bilioni kwenda kwenye masuala binafsi.
Tuhuma hizi zenye kichwa cha habari “Zitto na Filikunjombe wanatumiwa na Kenya na Uingereza kuvuruga na kudhoofisha Uwekezaji nchini mwetu” zinajibiwa hapa chini. Utaona ndugu Filikunjombe ametajwa kwa kichwa cha habari ili kumtaja tu bila sababu yeyote ile.
Tuhuma #1:
Zitto anaye rafiki yake Mkenya aitwae Rapahel Ongangi ambao kwa pamoja wameanzisha Gombe Advisors Co. Ltd (registered on 24 November 2011, Certificate No 87387) kwa ajili ya kufanya biashara na Makampuni ya Gesi na Mafuta yanayofanya kazi nchini hapa.
Majibu:
Gombe Advisors ni kampuni binafsi isiyofanya faida yaani ‘Company Limited by Guarantee’. Haina kazi na kampuni yoyote ya Gesi na Mafuta na wala yenyewe haijuhusishi na biashara hiyo. Gombe advisors haijafanya kazi yoyote ile na kampuni nyingine zaidi ya kusaidia wasanii wa kundi la Kigoma All stars. Upotoshaji hapa unalenga kupindisha mjadala.
Tuhuma #2:
Zitto amemsaidia Ongangi kupata uraia wa Tanzania na kwa sasa ni raia wa pasipoti. Zitto na Ongangi walimtafutia CEO wa Shell aitwae Axel Knospe nyumba na gari ya kukodi.
Majibu:
Raphael ni mtu binafsi ambaye anafanya shughuli zake hapa nchini, amesoma hapa nchini na ameoa na ana mtoto. Tuhuma hizi hazina msingi wowote ule maana ni uwongo. Wanaotoa tuhuma hizi waonyeshe hiyo pasipoti ya Bwana Ongangi kuthibitisha madai yao.
Tuhuma #3:
Mikataba ya STATOIL iliyokuwa inarushwa kwenye mitandao ya jamii na kuchapishwa kwenye magazeti ya Kenya ya hapa nchini (The Citizen na Mwananchi) mwandishi mkuu alikuwa huyo CEO wa Shell.
Majibu:
Mkataba uliovujishwa wa StatOil ulivujishwa na waandishi wa habari wa Norway. Uchambuzi wa mkataba huo nimeufanya mwenyewe kwa kutumia utaalamu wangu niliosomea wa kuchambua mifumo ya kodi kwenye sekta ya mafuta na gesi. Kwa namna yoyote ile, huyo anayetajwa kuwa CEO wa kampuni ya Shell hahusiki. Tuhuma hii wanaoitoa watoe ushahidi usio na chembe ya mashaka.
Ikumbukwe kuwa mkataba wa StatOil utaipotezea Tanzania mapato ya dola za Marekani bilioni 12 (takribani Tshs 20,400,000,000,000/=) katika kipindi cha miaka 15 baada ya gesi kuanza kuchimbwa.
Uamuzi wa Kamati ya PAC kutaka mikataba yote ya Gesi kuwa wazi una lengo la kuchambua kuona kama mikataba yote nchini haipotezi mapato kwa nchi. Uamuzi huo umewakasirisha sana baadhi ya waliohusika kuingia mikataba Serikalini maana wanajua kuna madudu kwenye mikataba na wanataka umma wa watanzania usijue!
Tuhuma #4:
Kampuni ya SHELL imechukizwa sana kucheleweshwa kwa kupata kibali cha kutafuta gesi na mafuta kule Pemba. Vilevile SHELL haina uwekezaji mkubwa Tanzania Bara kwani ilishindwa kwenye tenda zenye vitalu vyenye gesi nyingi upande wa Bara.
Majibu:
Ukweli ni kuwa Kampuni ya Shell ina vitalu 4 huko Zanzibar na tayari ina makubaliano na Serikali ya Zanzibar kuhusu utafutaji mafuta huko katika vitalu namba 9,10,11 na 12. Shell inafanya kazi na kampuni ya Petrobras ya Brazil kwenye kitalu namba 6 na namba 8. Taarifa hizi zipo wazi kwenye tovuti ya TPDC. Tuhuma nyepesi namna hii dhidi ya kampuni kubwa kama Shell zinaonyesha dharau na kiburi kinachotokana na uelewa mdogo wa mambo wa watu wanaotuhumu.
Tuhuma 5:
Ongangi anapokea maelekezo kutoka Serikali ya Kenya kuhujumu uwekezaji nchini mwetu.
Majibu:
Nazifahamu mbinu nyingi zinazotumika kufanya propaganda, lakini mbinu hii imeshindwa ikiwa mapema sana. Ni vema wanaotoa tuhuma hizi wazithibitishe vinginevyo ni mwendelezo wa propaganda zisozingatia diplomasia ndani yake dhidi ya jirani zetu wa Kenya. Hizi ni propaganda hatari ambazo hata hao wanaotuhumiwa wakisikia watatudharau sana.
Tuhuma #6 (juu ya Uingereza):
Uingereza imekuwa inamfadhili Zitto kwa miaka mingi kwa mambo yake ya kisiasa kwa hiyo sasa hivi Ubalozi wa Uingereza unamlipa Zitto na Kafulila kuhakikisha kwamba Standard Chartered ya Uingereza inalipwa deni lake lisilotambulika kisheria nchini mwetu.
Majibu:
Nimetangulia kusema hapo awali kuwa kuna propaganda ambazo haziangalii hata diplomasia; nyingine ni hii. Pamoja na kukanusha uzushi huu, ni vizuri wanaotoa tuhuma za namna hii kuthibitisha. Mimi binafsi sijawahi kufadhiliwa kisiasa na Taifa lolote lile. Inaelekea kuna wanasiasa wanaofadhiliwa na mataifa mengine ambao kwakuwa kwao ndiyo maisha wanaamini na wengine tupo kama walivyo.
Kwangu itikadi yangu ni ‘Uzalendo kwa nchi yangu’, ni jambo ambalo halina mbadala wake. Siku zote nasema “Right or wrong, my country first”.
Kurudia kurusha tuhuma kwa Ubalozi wa Uingereza nchini ni kudhihirisha kwa mara nyingine kiburi cha kuwa na mamlaka (arrogance of power) walicho nacho wanaotuma tuhuma hizi.
Aidha, wanatuhumu kuwa “Kafulila na Zitto wamehaidiwa 15% ya USD 150 million kama deni likilipwa”
Mtanzania anayeweza propaganda dhaifu kama hizi basi anatakiwa ajitafakari. Hata hivyo ni vema wanaotoa tuhuma hizi wathibitishe bila chembe ya mashaka.
Tuhuma #7:
Mbunge Mkono nae ameshikwa hasira kupoteza kazi ya uwakili pale TANESCO. Kafulila na Zitto wanalipwa na Mkono kuvuruga Serikali kwa hasira za kukosa fedha za kitapeli za TANESCO.
Majibu:
Hizi ni tuhuma ambazo sasa tumezizoea kutolewa. Mambo mepesi hayawezi kujibu mambo ya msingi kama tuhuma za wizi wa fedha zaidi ya Tshs bilioni 200 kutoka Benki kuu ya Tanzania. Kukusanya kila propaganda ili kuuhamisha umma ni kupungukiwa hekima na busara.
Aidha, wanaotuhumu wanadokeza kuwa “Naomba tuwe macho na Wabunge wetu achananeni na madai ya Zitto ya wizi. Huyu mtu anafanya biashara na Kampuni ya SHELL na inasemekana analipwa na Ubalozi wa Uingereza. Serikali ya Kenya na tapeli mkubwa Mbunge Mkono nae anawalipa Zitto na Kafulila”.
Watanzania, haya ni maneno ya hasira ya watu wanaokaribia kukamatwa kwa kushiriki wizi wa fedha katika Benki kuu ya Tanzania. Kamwe tuhuma kama hizi haziwezi kutukatisha tamaa katika kupambana ili ukweli ujulikane. Sisi tutapigana kwa ajili ya Taifa, kwa ajili ya mtanzania na tunachotaka ni umma uujue ukweli wa mambo.
Hasira hizi zinatokana na mambo mawili:
Moja ni uamuzi wa kamati ya PAC kuwasweka ndani baadhi ya watendaji wa TPDC kwa kushindwa kutekeleza maamuzi ya Kamati yanayohusu uwazi wa mikataba ya Gesi na Mafuta.
Pili, ni uamuzi wa PAC kuagiza ukaguzi maalumu wa mchakato mzima wa kuanzishwa na kufungwa kwa akaunti ya Tegeta Escrow ambapo zaidi ya shilingi bilioni 200 ziliporwa na zaidi ya shilingi bilioni 12 zinalipwa na TANESCO kila mwezi kwenda kampuni ya PAP inayomilikiwa na Harbinder Singh Seth (50%) na watu wasiojulikana kupitia kampuni ya Simba Trust iliyosajiliwa na kufichwa nchini Australia (50%).
Ieleweke kuwa PAP inalipwa shilingi milioni 400 kila siku kutoka TANESCO izalishe au isizalishe Umeme! Watanzania, PAP itaendelea kulipwa namna hiyo kwa miaka 20 ijayo. Kwa namna ambayo Seth analindwa na baadhi ya watendaji Serikalini na hasa ndani ya Wizara ya Nishati na Madini. Aidha, kuna fununu kuwa kuna maofisa serikalini wanaomiliki hizo 50% za kampuni ya PAP. Seth pia anamiliki kitalu cha gesi Mnazi bay Kaskazini kupitia kampuni ya HydroTanz.
Hasira hizi walizo nazo wanaonituhumu na Kamati yangu zimewapelekea kugushi nyaraka mbalimbali zinazonituhumu mimi na wenzangu ili kutuogopesha na kutukatisha tamaa katika kutafuta ukweli juu ya suala la uporaji wa fedha kutoka Benki kuu. Lengo lao ni kututoa kwenye mstari. Mimi na wenzangu hatutatoka kwenye mstari, tutashirikiana na wabunge wenzetu kuhakikisha ukweli unajulikana na wezi kuchukuliwa hatua kali.
Harbinder Singh Seth aliiangusha Serikali ya KANU nchini Kenya, sasa anachotaka kukifanya kinaweza kuiangusha Serikali ya CCM wakiendelea kumkumbatia.
Watanzania sio mabwege!
Zitto Kabwe
Mwenyekiti PAC
Dodoma, 9 Novemba 2014
Fedha za zilizokuwa katika akaunti maalumu ya IPTL, (Tegeta Escrow account) ni mali ya umma
Fedha za zilizokuwa katika akaunti maalumu ya IPTL, (Tegeta Escrow account) ni mali ya umma
Fedha za zilizokuwa katika akaunti maalumu ya IPTL, (Tegeta Escrow account) ni mali ya umma
Zitto Kabwe
Kwa mara nyingine serikali kupitia viongozi na watendaji wake akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wamedai kwamba kiasi cha Dola za Marekani milioni 250 zilizopaswa kuendelea kuwapo katika ‘Tegeta Escrow Account’ si mali ya serikali na hivyo si mali ya umma. Akaunti hiyo ilifunguliwa na serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) pamoja na kampuni ya Independent Power Limited (IPTL).
Kwa bahati mbaya sana viongozi wa serikali wamekuwa wakiendelea kurudia kuueneza huo uongo kwamba fedha hizo si mali ya umma. Inasikitisha pia kwamba vyombo vya habari vimekuwa navyo vikibeba na kusambaza huo uongo bila kuhoji na kuchunguza. Inashangaza sana pia asasi za kiraia nazo zimekaa kimya. Inatisha na kushangaa tena kuona wapinzani wakimwachia suala hili Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, pekee wakati mapambano dhidi ya rushwa ni ajenda kuu ya wapinzani. Kafulila amekuwa akiendelea kuhoji suala hilo bungeni peke yake bila kupata kuungwa mkono na kupewa msaada wa aina yoyote kutoka kwa wenzake wa kambi ya upinzani bungeni.
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilielekeza kuwapo kwa ukaguzi maalumu kwenye akaunti hiyo ya Tegeta escrow account iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuwa ndani yake kulikuwapo fedha za umma. PAC haina sababu yoyote ya kufuatilia fedha za watu binafsi. Mwaka 2009 iliyokuwa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ilitoa maelekezo kwa BoT kutothubutu kutoa fedha hizo. Agizo hilo la POAC lilitokana na sababu kwamba fedha hizo zilikuwa ndani ya hesabu za Tanesco.
Akaunti ya ‘Tegeta escrow’ ilifunguliwa kutokana na kuwapo kutoelewana kuhusiana na gharama halisi na halali za umeme unaozalishwa na IPTL na kuuzwa kwa TANESCO. Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICSID) katika uamuzi wake wa Februari, 2014 ilitoa hukumu kuonyesha kwamba Tanesco walitozwa kiwango cha juu zaidi ya kilichopaswa kulipwa kwa IPTL. Kwa uamuzi huo ni dhahiri kwamba fedha zilizokuwa zimehifadiwa kwenye akaunti hiyo maalumu ya escrow zilipaswa kugawanywa kwa IPTL na Tanesco baada ya hesabu kufanyiwa marekebisho upya kwa viwango halali.
Hesabu za mwaka wa fedha ulioishia Disemba 2012 za Tanesco zinaonyesha wazi kwamba fedha hizo ni mali ya shirika hilo la umma linalomilikiwa na serikali kwa asilimia mia moja. Fedha za kampuni ni suala la kisheria kama inavyobainishwa katika sheria ya kampuni ya mwaka 2002.
Kwa maelezo hayo na hoja hizo, inakuaje serikali ianze kudai kwamba fedha hizo si mali ya umma? Hivi inawezekanaje kwa fedha za mtu binafsi zikaingizwa katika hesabu za shirika la umma linalomilikiwa na serikali kwa asilimia 100? Ni lini fedha hizo zimekoma kuwa za umma? Je ni baada ya baadhi ya watendaji wa serikali kula njama za kuzichukua fedha hizo kwa kushirikiana na ‘mwekezaji’ aliyechafuka kwa ufisadi duniani?
Serikali inadanganya waziwazi kudai kwamba fedha hizo si mali ya umma. Umma una haki ya kukumbushwa kwamba madai hayo yalitolewa pia katika lile sakata la ufisadi maarufu wa EPA unaofanana kwa kila hali na huu wa sasa wa ‘Tegeta Escrow’.
Hoja nyingine ni kwamba, Mbunge Kafulila alisema kwamba Jaji Utamwa wa Mahakama Kuu ya Tanzania hakutoa uamuzi wa kuchukuliwa fedha kutoka akaunti ya ‘Tegeta Escrow’. Nimepitia kwa makini hukumu ya Jaji Utamwa na kubaini kwamba hakuna popote alipotaja akaunti ya ‘Escrow’. Hata hivyo, nilipopitia muhstasari wa kikao kati ya TANESCO, IPTL na Wizara ya Nishati na Madini, ndipo kwa mara ya kwanza nikakuta wametafsiri uamuzi wa mahakama wakidai kwamba fedha zote za ‘Tegeta Escrow’ zipewe kampuni ya PAP (inamilikiwa kwa asilimia 50 na Harbinder Singh na 50% na Simba Trust iliyosajiliwa Australia). Hiki ndicho kikao kilichofanya maamuzi ya kuiba na kugawana wenyewe fedha hizo (Hukumu ya Jaji Utamwa na muhstasari wa kikao vinaambatanishwa).
Wote waliohudhuria kikao hicho kilichojipa mamlaka ya kutafsiri hukumu ya Mahakama Kuu, wanapaswa kuchunguzwa na kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria zilizopo. Inawezekana vipi uamuzi wa mahakama ukatafsiriwa na kikao cha Wizara? Muhstasari wa kikao hicho ndio uliowasilishwa Benki Kuu (BoT) kuhalalisha madai kwamba fedha hizo lazima zitolewa kutoka akaunti ya Escrow.
Fedha zinazohusiana na akaunti ya Escrow ni Dola za Marekani milioni 250, katia ya hizo Dola milioni 122 zilizokuwa BoT zimeshatolewa na kiasi kilichosalia Dola milioni 128 zitalipwa na Tanesco kutokana na fedha zake kwa madai ya kushindwa kulipa kwa wakati. Fedha zilizolipwa ni zile ambazo zimetoka Wizara ya Nishati na Madini ambayo kisheria ndio walipaswa kulipia gharama za uzalishaji umeme (capacity charge) fedha zilizotoka kwa walipa kodi.
Ikumbukwe kwamba uhamishaji wa asilimia 70 ya hisa za IPTL kwenda PAP umeambatana na nyaraka za kughushi kutokana na kutokuwepo kabisa kwa uthibitisho wa cheti halisi cha hisa (share certificate) kutoka kampuni ya Mechmar kwenda kampuni ya Piperlink. Nyaraka za TRA zinaonyesha kwamba hisa hizo (70%) ziliuzwa kwa Shilingi za Kitanzania milioni sita (6) tu. Na bado hakuna ushahidi kuonyesha kwamba uhamishaji huo wa hisa ulipata baraka za mamlaka husika kama inavyotakiwa na sheria za nchi.
Wakati huyo anayejiita mmiliki mpya wa IPTL aliposaini mkataba wa kuchukua fedha kutoka akaunti ya Escrow zilizokuwapo BoT, hakuwa mmiliki halali kisheria kwani kodi ililipwa siku moja baada ya wao kupokea fedha kutoka BoT. Sheria inataka kutolewa kwa cheti na Kamishna wa TRA kama uthibitisho kwamba kodi yote imelipwa ipasavyo (Sheria ya Fedha ya 2012 kifungu cha 29).
Ni nani wamiliki wengine wa kampuni ya PAP? Uchunguzi ni muhimu ukawalenga vigogo na wanasiasa wakubwa wakiwamo watendaji waandamizi wa Wizara ya Nishati na Madini.
Inapaswa tutafakari kuona kwamba Harbinder Singh aliyechukua fedha za Escrow, anamiliki vitalu vya mafuta na gesi kupitia kampuni iitwayo HydroTanz ambayo nayo imesajiliwa nchini Australia, ikiwa na anwani sawa na ya kampuni ya Simba Trust. Kitalu hicho cha mafuta kinaitwa ‘Mnazi Bay North’, jirani kabisa na ugunduzi mkubwa wa hivi karibuni mkoani Mtwara.
Tunatarajia kwamba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), atafichua ukweli wa sakata hili na TAKUKURU itawafikisha mahakamani wahusika bila kujali nyadhifa zao serikalini.
Kauli ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, kwamba kuna watu waliokula rushwa na kwamba nyaraka zinazotajwa ni karatasi za kuuzia vitumbua, ni kauli zenye kuonyesha kutapatapa kwa watendaji serikalini. Hakuna hata mahali pamoja ambapo nimemtaja mtu kuwa ni mwizi zaidi ya kuwasilisha hoja zinazohitaji majibu mwafaka na si matusi, vitisho na tuhuma za kuzusha. Nyaraka za TRA haziwezi kuwa za kufungua maandazi kama ambavyo hukumu ya Jaji wa Mahakama Kuu haiwezi kuwa karatasi za kufungia maandazi na badala yake ni nyaraka halali zinazohitaji maelezo kutoka kwa viongozi na watendaji wa serikali badala ya kuropoka na kuporomosha matusi.
Hali kadhalika, Bunge lina kila sababu kupitia sheria yake ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kulinda hadhi yake kutoka kwa watendaji kama Maswi ambao wanatoa matamshi ya kuonyesha kwamba chombo hicho ni chombo cha watu wasiofaa na kwamba watu wanaofaa wanazungumza nje ya Bunge. Maswi na wengine kama wana ushahidi wa rushwa dhidi ya mbunge ama yeyote hawapaswi kupayuka ovyo bali kwa nafasi zao wanaweza kuwasiliana na vyombo vya dola kama TAKUKURU na polisi ili wachunguze na kuchukua hatua kama ambavyo vinawachunguza wao.
Kauli ya Maswi kwamba “wanaume” hawazungumzi ndani ya Bunge si tu udhalilishaji wa chombo hicho bali pia inaashiria ugonjwa wa mfumo dume uliotawala miongoni mwa viongozi wetu kwa maana kwamba wanaume ndio wenye hadhi, uwezo na heshima na wanawake ni dhaifu na wasiostahili heshima. Tufumbue macho tuone na tuondoe hisia binafsi zenye kubebwa na itikadi, chuki na misimamo yetu ya kisiasa. Tuwe wazalendo ili tuweze kusimamia utaifa.
Sent from my iPhone
Mapya IPTL: $270Million zimetokaje BoT ?
Mapya IPTL: $270m zimetokaje BoT ?
Nimesoma habari kuu ya gazeti la The Citizen la tarehe 3 Machi 2014 kuhusu mauzo ya kampuni ya IPTL kwa kampuni ya Pan Africa Power Limited (http://www.thecitizen.co.tz/News/-270m-deal–Story-of-IPTL–PAP-and-High-Court/-/1840392/2228606/-/1bddmgz/-/index.html).
THE CITIZEN 4th March 2014 How $270-million IPTL deal was planned and executed
Nimeshtushwa sana na matumizi ya fedha za akiba maalumu (escrow account) iliyokuwa benki kuu (BoT). Nikiwa mwenyekiti wa kamati ya PAC nina haya ya kusema; Mwaka 2006 Rais Jakaya Kikwete aliagiza kwamba, ili kumaliza kabisa suala la mkataba wa kuuziana Umeme wa IPTL, mitambo ya kampuni hiyo ichukuliwe na Serikali. Mwaka 2006, 2007 na 2008 Kamati ya BUNGE ya Nishati na madini imekuwa ikitoa maagizo hayo hayo kuhusu suala la IPTL. Mwaka 2009, Aprili 30 Kamati ya Bunge ya POAC ilipeleka mapendekezo bungeni kwamba IPTL ichukuliwe na serikali na fedha zilizopo katika escrow account zitumike pia kubadili mtambo ule kutoka mafuta mazito kwenda kutumia Gesi Asilia. Pendekezo hilo lilipitishwa na Bunge na POAC ikatoa maelekezo maalumu kwa Gavana wa Benki Kuu kuwa fedha zilizopo escrow account zisitumike kwa namna yeyote ile bila mitambo ya IPTL kuwa ya umma na kubadilishwa ili itumie Gesi Asilia.
Chanzo cha escrow account?
Baada ya mkataba wa IPTL kuingiwa, iligundulika kuwa kuna udanganyifu mkubwa ulifanyika katika kiwango cha mtaji wa kampuni hiyo na hivyo kufanya malipo wanayolipa tanesco kwa IPTL kuwa makubwa mno. Wakati katika kukokotoa gharama za uwekezaji (capacity charges) mtaji uliowekezwa katika IPTL ulisemwa ni dola milioni 36, ukweli ni kwamba IPTL waliweka dola 50 tu. Hivyo capacity charge ya dola milioni 3 kwa mwezi haikupaswa kulipwa yote kwani kampuni iliendeshwa kwa mkopo kuliko mtaji wa wawekezaji ( debt financed and not equity financed). Hivyo, mahakama ya kimataifa ya ICSID ikaamua kuwa, fedha zote za capacity charges ziwekwe Benki Kuu mpaka gharama halisi ziamuliwe na mahakama ndio wahusika wagawane (tanesco na IPTL). Akiba hiyo, nimeambiwa, ilifika dola 250m kabla ya kuchukuliwa na kugawanywa kwa wanahisa na wanunuzi wa IPTL. Hivyo kabla ya mgawo huu ilipaswa pesa ambazo tanesco walikuwa wanalipa kama ziada ya capacity charges kwa IPTL zirejeshwe kwanza na zinazobakia ndio zilipwe kwa wadai (creditors) na wanahisa. Kwa hali ilivyo sasa mnunuzi wa IPTL kapewa mitambo na fedha za kuinunua, ikiwemo fedha za tanesco ambazo zilipaswa kurejeshwa (Richmond cha mtoto kwa kweli).
Maswali ya kujibiwa ni haya;
Je, ziada ya fedha za malipo ya capacity charges zimerudi tanesco?
Je, mwekezaji Mpya kapewa mkataba Mpya wa kuuza Umeme (PPA) kwa utaratibu gani wa zabuni?
Je, agizo la Rais na BUNGE kwamba Mitambo iwe ya umma limetupiliwa mbali kwa vigezo gani?
Wizara ya Nishati na Madini na Benki Kuu wametoa taarifa rasmi kwa umma kuhusu masuala haya? Wizara itoe taarifa, CAG akague
Kwa namna yeyote ile CAG anapaswa kukagua mchakato huu na kuweka majibu kwa umma kupitia kamati ya PAC. Hii ndio njia bora zaidi ya kuondoa wingu katika suala la IPTL ambalo toka limeanza miaka ya tisini limegubikwa na mazongezonge ya rushwa na uvundo wa kifisadi. Uwazi utatoa ukweli na kuwezesha uwajibikaji wa fedha za umma. Wakati mchakato wa ukaguzi unafanyika ni vema Wizara ya Nishati na madini itoe tamko rasmi.
Zingatia:
Kwa mujibu wa mkataba kati ya TANESCO na IPTL capacity charge inapaswa kukokotolewa kwa kuzingatia mtaji wa asilimia 30 na mkopo wa asilimia 22.31. Mtaji wa IPTL ulikuwa $50 tu, tofauti na $36 milioni zilizotajwa kwenye mkataba na kuamuliwa na mahakama. Badala ya TANESCO kulipa ‘capacity charge’ ya dola 50,000 kila siku Umeme uzalishwe au la, udanganyifu wa mtaji ulipelekea TANESCO kuwa inalipa dola 100,000 kila siku tangu mwaka 2002. Kuanzia mwaka 2007 fedha hizo zilianza kuwekwa kwenye akaunti maalum (escrow account) BoT.
PRESS RELEASE: Shilingi Bilioni 86 zaibwa Wizara ya Nishati/TANESCO, Gridi ya Taifa hatarini
Shilingi bilioni 86 zaibwa Wizara ya Nishati/TANESCO, Gridi ya Taifa hatarini
Gazeti la The East African la Novemba 24 – 30, 2012 limetoa taarifa kwamba jumla ya dola za kimarekani milioni 54 zimegundulika kuibwa na watumishi waandamizi wa Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la TANESCO kupitia manunuzi ya Mafuta ya kuendesha mtambo wa Umeme wa IPTL. Gazeti hili limenukuu taarifa ya ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Tanzania (Controller and Auditor General). Taarifa hiyo inasema kuna kikundi (racket) ambacho kazi yake kubwa ni kujifaidisha binafsi na mpango wa umeme wa dharura kupitia manunuzi ya Mafuta mazito ya IPTL.
Itakumbukwa kwamba toka mwaka 2011 kumekuwa na shinikizo lililotolewa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwamba zabuni za ununuzi wa mafuta ya kuendesha mpango wa umeme wa dharura na mchakato mzima wa manunuzi ya mafuta haya ufanyiwe uchunguzi wa kina (forensic audit).
Katika mkutano wa 3 wa Bunge la Kumi (April 2011) niliuliza swali Bungeni kuhusu kashfa hii ya ununuzi wa mafuta ya kuendesha mtambo wa IPTL na baadaye tarehe 16 Aprili 2011 nilimwomba Spika airuhusu Kamati ya Nishati na Madini kufanya uchunguzi kuhusu kashfa hii. Kamati ya Nishati na Madini chini ya aliyekuwa Mwenyekiti ndugu January Makamba ililitaka Bunge kuazimia kufanyika kwa uchunguzi kuhusu suala hili kwenye Taarifa yake ya mwaka 2011 iliyowasilishwa Bungeni mwezi Aprili mwaka 2012. Waziri Kivuli wa Nishati na Madini ndugu John Mnyika katika Hotuba yake ya Bajeti ya Wizara hiyo mwaka 2011 alipendekeza kufanyika kwa uchunguzi kuhusu kashfa hii pia. Juhudi zote hizo hazikuzaa matunda.
Kipindi hicho kiwango kilichokuwa kinahojiwa kuibwa ni shilingi bilioni 15 tu. Taarifa ya The East African kama walivyonukuu kutoka kwenye taarifa ya CAG inaonyesha fedha zilizoibwa ni shilingi bilioni 86.
Zabuni za kununua mafuta ya kuendesha umeme wa dharura zimekuwa zikitolewa bila kufuata utaratibu wa zabuni kwa mujibu wa Sheria ya manunuzi. Hivi sasa kila mwezi Tanzania inatumia dola milioni 70 kununua mafuta ya kuendesha mitambo ya umeme. Fedha hizi zinatoka Hazina na sehemu ndogo kutoka TANESCO. Wakati fedha hizi bilioni 112 zinachomwa kila mwezi kununua mafuta mazito na dizeli ya kuendesha mitambo ya umeme, Taarifa za kitaalamu zinaonyesha kwamba Bwawa la Mtera hivi lina kina cha maji chini ya kiwango kinachotakiwa na uzalishaji wa umeme ni asilimia 20 tu ya uwezo (installed capacity). Iwapo TANESCO wataendelea kutumia zaidi maji yaliyopo Mtera, Mitambo itashindwa kazi na Gridi nzima itasimama maana Mtera ndio nguzo kuu ya Gridi ya Taifa. Hali hii ni hatari sana kwa uchumi na ulinzi na usalama wa Taifa. Kimsingi Gridi ya Taifa ipo hatarini kutokana na kiwango cha Maji kilichopo Mtera hivi sasa na kuendelea kupungua kwa kina hicho cha maji.
Wananchi wanapaswa kuelezwa kinaga ubaga nini kinaendelea katika sekta ndogo ya umeme hapa nchini;
1. Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kuhusu zabuni za manunuzi ya Mafuta ya kuendesha mitambo ya umeme wa dharura iwekwe wazi na ‘racket’ inayosemekana kuiba jumla ya shilingi bilioni 86 ionyeshwe na hatua za kisheria zichukuliwe mara moja na bila kuchelewa.
2. Waziri wa Nishati na Maadini auleze umma hali yalisi ya sekta ya umeme nchini, uzalishaji wa umeme upoje, hali ya maji katika bwawa mkakati la Mtera na nini hatma ya mitambo ya IPTL, kesi zake na utekelezaji wa mapendekezo ya Bunge kuwa kesi za kampuni hii zimalizwe nje ya mahakama. Pia Taifa lielezwe Mpango wa Dharura wa umeme unakwisha lini maana muda uliotolewa na Bunge mwezi Agosti mwaka 2011 tayari umekamilika. Waziri aeleze hatua agni amechukua baada ya kukabidhiwa taarifa na CAG kuhusu maafisa waandamizi wa Wizara waliohusika na wizi wa shilingi bilioni 86 za kununua mafuta ya IPTL.
3. Waziri wa Fedha na Uchumi aueleze umma ni kiwango gani cha fedha Hazina imetoa kununua mafuta ya kuendesha mitambo ya umeme wa dharura kati ya Mwezi Novemba mwaka 2011 na Oktoba mwaka 2012 na kama taratibu zote za zabuni zilifuatwa na pale ambapo hazikufuatwa ni hatua gani PPRA wamechukua dhidi ya waliokiuka sheria ya manunuzi na kuleta hasara ya mabilioni ya fedha kwa Serikali.
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Waziri Kivuli wa Fedha
Dar es Salaam. Novemba 25, 2012