Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Posts Tagged ‘Wizara ya Nishati na Madini

Sera ya Gesi: Maoni ya awali #RasimuyaGesiAsilia #TanzaniaNaturalGasPolicy

with 6 comments

Jana wabunge tumegawiwa rasimu ya Sera ya Gesi Asilia. Leo Wizara ya Nishati na Madini itaendesha semina kwa wabunge kuhusu sera hiyo.

Draft 3- The Natural Gas Policy of Tanzania -2013

Draft 3- The Natural Gas Policy of Tanzania -2013(Rasimu ya Sera ya Gesi Asilia)

Nimepata muda kidogo wa kuipitia hii rasimu ya 3 nikiwa safarini kwenda Tabora kwa shughuli za chama changu cha CHADEMA , nina maoni ya awali kama ifuatavyo;

1). Kwa ujumla kupata Sera mpya ya gesi asilia ni hatua muafaka japo imechelewa sana. Hata hivyo ni bora kuchelewa kuliko kutofika kabisa. Ni vema wananchi wachukue fursa hii kuisoma na kuijadili rasimu hii na kuiboresha ili iwezeshe wananchi wenyewe kufaidika na utajiri ambao nchi yetu imejaaliwa.

2). Sera ina jumla ya sura Sita. Sura ya kwanza ya inaweka sababu na masuala ya jumla na utangulizi . Sura ya pili inaweka sababu za kuwepo kwa sera mpya na madhumuni maalumu, Sura ya tatu ndio yenye matamko ya msingi ya kisera (fundamental policy issues) ikiwemo masuala ya miundombinu ya gesi kwa ajili ya soko la ndani, usimamizi wa mapato yatokanayo na gesi asilia na masuala ya ‘’ local content’’. Sura hii pia imezungumzia masuala ya uwazi na uwajibikaji. Sura ya nne ni masuala ya mfumo wa kisheria na udhibiti na sura ya tano ni taasisi za usimamizi wa sera ya gesi asilia. Sura ya sita ni hitimisho. Kila sura imeweka matamko ya kisera.

3). Rasimu ya sera imeshindwa kutofautisha suala la Mafuta na Gesi kuwa ni suala la Muungano au sio suala la muungano katika muktadha wa Katiba mpya inayojadiliwa sasa. Hii inadhihirisha umuhimu wa kuwianisha mchakato wa katiba na michakato mingine inayoendelea nchini. Hivi sasa Zanzibar inajiandaa kuwa na sera na sheria yao ya mafuta ya gesi, iweje sera hii itamke gesi asilia ni mali ya Jamhuri ya Muungano wakati upande mmoja wa Muungano utakuwa unafaidi utajiri wake peke yake? Rasimu ya sera imeshindwa kutambua kuwa kuna vitalu vya mafuta na gesi ya (vitalu namba 9-12) vimesimamisha shughuli kwa sababu Serikali ya Zanziabar haitambui mafuta na gesi kuwa suala la muungano. Rasimu inapaswa kuzingatia jambo hili kabla ya kupata sera yenyewe.

4). Rasimu imetamka katika ukurasa wa 9 kwamba sera hii haitambui shughuli za utafutaji (‘This policy document only covers mid-and downstream segments’ ndio nukuu ya neno kwa neon ya Sera hii). Hiki ni kichekesho cha milenia .

Taifa linawezaje kuandika sera ya gesi asilia kwa upande wa uchuuzi tu (biashara) na kuacha kazi yenyewe haswa ya utafutaji na uchimbaji (exploration and exploitation are upstream). Shughuli za utafutaji na uchimbaji ndio msingi haswa wa sera ya gesi asilia.

Mikataba yote huamuliwa kwa kuzingatia kwanza utafutaji, shughuli nyingine ni biashara tu ya kitakachogunduliwa . Rasimu kuacha kabisa eneo la utafutaji na uendelezaji (upstream) ni sawa na kutokuwa na sera kabisa.

Kwa namna eneo hili lilivyoachwa kuna harufu ya mkakati wa siri wa kuwanyima wananchi msimamo wa kisera kuhusu utajiri wao unavyonyonywa . Sentensi hii yenye maneno 10 katika uk. wa 9 wa kijitabu cha rasimu ya sera unaondoa kabisa umuhimu wa sera yenyewe wakati dhumuni kuu la sera linatamkwa uk.6 kwamba Gesi asilia ni mali ya wananchi wa ‘Jamhuri ya Muungano’ wa Tanzania’’ kurasa tatu baadaye zinaiondoa sera kwenye eneo hilo la umiliki wa mali hii ( Upstream). Tumeamua kuandika sera ya uchuuzi wa gesi asilia?

5). Rasimu katika 3.2.2(uk.24) imeweka matamko ya kisera kuhusu uwazi na uwajibikaji . Uwazi ndio eneo ambalo watanzania wengi walikuwa wanasubiri kwa hamu sana . Usiri wa mikataba katika sekta mbali mbali nchini ni chanzo cha ufisadi na uporaji wa utajiri wa mali yetu. Sera hii imeJibu swala hili? HAPANA. Sera haisemi ni namna gani mikataba itakuwa wazi kwa wananchi. Sera haisemi ni namna gani wananchi wataiwajibisha Serikali na vyombo vyake (Accountability) kwenye masuala ya mafuta na gesi. Sera imepiga porojo kuhusu uwazi na uwajibikaji. Bila misingi imara ya Uwazi na Uwajibikaji katika rasilimali ya gesi asilia, sera haina maana yoyote ile.

6). Serikali ni lazima ijue kwamba hivi sasa nchi yetu nchi tajiri yenye watu masikini.[i] sera ya gesi inapaswa kutuondoa kuwa nchi yenye laana ya rasilimali. Sera hii haina mwelekeo huo kabisa . Sera inapaswa kuwezesha wananchi kupata thamani ya maliasili yetu na kuwezesha matumizi mazuri ya mapato yatokanayo na utajiri wa nchi.

Sera yetu lazima ioneshe dhahiri kwamba gesi asilia ni mali ya wananchi na uendelezaji na unyonyaji wa rasilimali hii utafaidisha wananchi kwanza na kwa ruhusa yao (Prior informed Consent Principle) sera ni lazima itamke hilo kinagaubaga.Sera ni lazima ionyeshe kuwa katika ushindani wa soko makampuni ya mafuta na gesi asilia yatapata faida ya halali ( normal retuns) ya uwekezaji wao na kwamba lolote linalozidi litabakia kuwa mali ya wananchi wa Tanzania.

Mkakati wa makampuni ya mafuta na gesi asilia ni kuhakikisha taifa linapata kiduchu na wanasaidia serikali kutoa majibu ya kipato hicho kiduchu. Watanzania hawatakubali tena.

7). Ni lazima tuseme kuwa tunataka utajiri wetu uwe neema kwa wananchi wetu, na siyo laana. Maendeleo yetu yatategemea ni namna gani tunafaidika na utajiri wetu wa maliasili kama gesi asilia. Sera ya Gesi Asilia itujengee imani hiyo. Hii Sera (Rasimu) inapaswa iangaliwe upya na hasa maeneo ya uwazi na uwajibikaji.

 

Kabwe Z. Zitto, Mb Kigoma Kaskazini

Tabora, tarehe 18 Mei 2013

Uchambuzi/Analysis: Bajeti ya Madeni

with 20 comments

Bajeti ya Mwaka huu 2012/2013 ni Bajeti ya Madeni

Serikali inapendekeza Bajeti ya TZS 15 trilioni(USD 8.75 Billion) katika mwaka 2012/13. Uchambuzi wa vitabu vya Bajeti unaonesha kwamba mafungu ya juu 5 kwenye Bajeti ni Kama ifuatavyo;

1    Huduma kwa Deni la Taifa          Tshs 2.7 trilioni(USD 1.69 Billion)
2    Wizara ya Ujenzi.                          Tshs 1 trilioni (USD 625 Million)
3    Wizara ya Ulinzi                          Tshs 920 bilioni (USD 575 Million)
4    Wizara ya Elimu                              Tshs 721 bilioni (USD 451 Million)
5    Wizara ya Nishati na Madini    Tshs 641 bilioni (USD 400 Million)
 TOTAL                                        TZS 5.982 Trilioni(USD 3.74 Billlion)
Chanzo: Vitabu vya Bajeti kwa Wabunge

Jumla ya mafungu haya ni sawa na asilimia 40% ya Bajeti. Kwa hiyo asilimia 40% ya Bajeti yote imepangwa kwa mafungu 5 tu. Fungu lenye kiwango kikubwa zaidi ya Bajeti kuliko vyote ni fungu 22 ambalo ni malipo kwa Deni la  Taifa. Pia sehemu kubwa ya fedha zilizotengwa kwa Ujenzi na Nishati ni madeni kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya miaka ya nyuma.

Hii yaweza kuwa Bajeti ya kulipa madeni zaidi kuliko Bajeti ya kuchochea maendeleo. Bajeti hii pia yaweza pia kuwa ni Bajeti ya kukopa maana jumla ya TZS 5.1 trilioni(USD 3.19 Billion) zitachukuliwa kama mikopo kwa Serikali. Mikopo ya kibiashara ambayo ni mikopo ghali sana itachukuliwa kwa wingi zaidi kuliko mwaka wa fedha uliopita.

Wabunge wanapaswa kufanya uchambuzi zaidi wa Bajeti ya mwaka huu inayopendekezwa na Serikali. Kuna haja kubwa sana ya kuharakisha kuanzishwa kwa Ofisi ya Bajeti katika Bunge na Kamati ya Bunge ya Bajeti ili kuweza kufuatilia kwa karibu, kuchunguza na kutoa taarifa kwa wabunge ili kuwezesha kuboresha Bajeti.

Misamaha yote ya Kodi na Madeni yote ambayo Serikali inaingia inabidi sasa ithibitishwe na Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi ili kuongeza udhibiti na usimamizi wa Misamaha ya Kodi na pia Deni la Taifa.