Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Posts Tagged ‘POAC

Extending Social Security to the excluded: A Personal Tour of Duty

with 4 comments

Written by zittokabwe

October 3, 2013 at 12:51 PM

Posted in Uncategorized

Tagged with , ,

Kufutwa kwa #POAC: #AnnaMakinda adhibitiwe au tusahau Uwajibikaji nchini

with 33 comments

Katika mkutano wa Kumi wa Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Spika wa Bunge ndugu Anna Makinda alitangaza mabadiliko kadhaa ya muundo wa Bunge katika Kamati mbalimbali za Bunge. Moja ya maamuzi ya Spika yalikuwa ni kufutwa kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma ambayo inajulikana kifupi kama POAC. Maamuzi haya yameleta sintofahamu kwa wananchi wengi na wafuatiliaji wa masuala ya Bunge na Uwajibikaji katika nchi yetu. Ni muhimu tufahamu uundwaji wa POAC ulitokana na misingi gani na kwamba Uamuzi wa Spika unarudisha nyuma maendeleo makubwa ya kujenga Bunge imara na lenye meno. Maamuzi ya Spika ni kinyume cha kanuni za Bunge, sheria ya Ukaguzi na Katiba ya nchi. Maamuzi ya Spika yanavuruga Bunge,ni ya hovyo na yanapaswa kupingwa na kila mdau wa Uwajibikaji nchini.

Baada ya Tanzania kuingia kwenye zoezi la Ubinafsishaji, mashirika mengi ya Umma yaliuzwa na mengine kufa kabisa. Wakati huo kulikuwa na chombo kinaitwa SCOPO (Standing Committee on Parastatal Organisations) kwa madhumuni ya kusimamia uendeshaji wa Mashirika ya Umma. Bunge lilikuwa na Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma na kamati hiyo ilifutwa mwaka 1997 kufuatia hatua za ubanifsishaji na ukweli kwamba Mashirika ya Umma hayatakuwapo na hivyo hapakuwa na haja ya kuwapo kwa kamati hiyo. Mwenyekiti wa mwisho wa Kamati hiyo alikuwa ni Mzee William Shelukindo wakati huo akiwa Mbunge wa Jimbo la Bumbuli wilayani Lushoto mkoani Tanga.

Mwaka 2007, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alifanya mkutano wa Uwajibikaji na kueleza Taifa kuwa kimsingi Mashirika ya Umma bado yapo na mahesabu yao, kwa kuwa hayaangaliwi, ni mabaya sana nafedha za umma zinapotea. Pia alieleza kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 143(5) inamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kutoa taarifa za Ukaguzi za Mashirika ya Umma (Public Authorities and Other Bodies). Hivyo aliomba Bunge liunde Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma ili liweze kupokea, kujadili na kutoa maelekezo kuhusu mahesabu ya Mashirika ya Umma na kusimamia ufanisi wa Mashirika ya Umma. Vile vile alishauri Kamati hiyo isimamie sera ya  Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma. Spika wa Bunge wa wakati huo, kupitia Kamati aliyoiunda chini ya Job Ndugai (wajumbe wengine walikuwa dkt Willibrod Slaa, Beatrice Shelukindo, Hamad Rashid Mohammed na Nimrod Mkono) wakaunda Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma kwa mujibu wa Kanuni za Bunge za Mwaka 2007. Kamati ya POAC iliundwa rasmi mwaka 2008 mwezi Februari. Nilipewa dhamana ya kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Kamati hii. Sababu za kuanzishwa kwa kamati ya POAC bado zipo na kimsingi sababu hizo ni za maana sana sasa kuliko ilivyokuwa kabla.

Majukumu ya POAC yaliainishwa na sehemu ya tatu ya nyongeza ya nane ya Kanuni za Bunge toleo la mwaka 2007, kanuni ya 115 (13)(a-e). Majukumu hayo ni pamoja na kushughulikia mahesabu yaliyokaguliwa ya Mashirika ya Umma, kuainisha maeneo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za Umma, kutathmini ufanisi wa Mashirika ya Umma na kufuatilia utekelezwaji wa sera ya ubinafsishaji wa mashirika ya Umma. Kuanzia mwaka 2008 Mdhibiti na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali amekuwa akitoa taarifa za mahesabu ya mashirika kama Katiba ya nchi inavyomtaka na sheria ya ukaguzi ya mwaka 2008. Sheria hii imeitaja kamati ya POAC kama moja ya kamati zenye majukumu ya kuwasilisha Bungeni taarifa ya mwaka ya mahesabu ya Mashirika ya Umma.

Katika kipindi cha miaka mitano POAC imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa umahiri na kwa kweli kwa uwazi sana kuliko kamati nyingine zote za Bunge. Taarifa ya mwisho ya POAC katika Bunge iliyowasilishwa katika mkutano wa saba wa Bunge, mwezi Aprili mwaka 2012 ulipelekea kutolewa kwa hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu ambayo ilisababisha mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri. Hatua hii ilikuwa ni hatua muhimu sana katika kuweka mizizi ya utamaduni wa uwajibikaji nchini kwetu. Wakati Kamati inajiandaa na Taarifa yake ya Mwaka 2012 kwenye Mkutano wa Kumi na Moja, Spika ameivunja. Ikumbukwe maagizo ya mwisho ya Kamati ya POAC yalikuwa ni kuzuia mifuko ya hifadhi ya jamii kutoa mikopo kwa Serikali bila ya kuwapo kwa mikataba. Hivi sasa Serikali imekopa zaidi ya shilingi 1.2 trilioni kutoka mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa ajili ya miradi mbalimbali, mikopo hiyo ya fedha za wafanyakazi haina mikataba yeyote na POAC iliona hatari ya fedha za wafanyakazi kupotea na kuleta madhara makubwa kwa wastaafu nchini.

Katika maelezo yake Spika amesema nchi nyingine duniani hazina kamati kama ya POAC. Nadhani waliomshauri Spika waliamua kumdanganya na yeye akadanganyika. Nchi zote za Afrika Mashariki zina Kamati ya kusimamia Mashirika ya Umma. Kenya inaitwa Public Investments Committee, Uganda inaitwa State Corporations Committee na hata nchi nyingine kama India ambazo zinafuata utamaduni wa kibunge kama wetu wanayo na wanaita Public undertakings Committee. Nchini Afrika Kusini sio tu kuna Kamati ya Mashirika ya Umma bali pia kuna Wizara inayosimamia Mashirika ya Umma (Ministry of Public Entreprises). Kimsingi Kamati ya POAC ilipaswa kuongezewa nguvu zaidi ili kufikia uwezekaji wa Serikali kwenye makampuni binafsi badala ya kuifuta. Uwezekaji wa Serikali kwenye makampuni kama BP, AirTel, Kilombero Sugar, SonGas nk hauna uangalizi wowote.

Uamuzi wa Spika wa Bunge kuifuta Kamati ya POAC ni uamuzi unaorudisha nyuma juhudi za nchi kujenga asasi za uwajibikaji, ni kinyume cha sheria ya ukaguzi wa umma inayotaja Kamati tatu za Bunge za kusimamia fedha za Umma na ni kinyume cha Katiba ya nchi. Spika wa Bunge anasema kazi za Kamati ya POAC zitafanywa na Kamati ya PAC; Tanzania ina jumla ya Mashirika ya Umma 258 yenye thamani ya shilingi trilioni 10.2 mpaka mwezi Juni mwaka 2012, hata kamati ya POAC ilikuwa haiwezi kushughulikia Mashirika yote ya Umma katika mwaka mmoja, PAC itawezaje kusimamia Wizara za Serikali, Mikoa na wakala za Serikali na wakati huo huo Mashirika ya Umma 258? Kwa vyovyote vile Taifa linarudi miaka ya kabla ya 2008 ambapo Mashirika ya Umma yalikuwa kichaka cha kuiba fedha za Umma. Hivi karibuni Kamati ya POAC iligundua mtindo wa Wizara za Serikali kupeleka fedha Serikali kwenye Mashirika na kutumia kifisadi ili kukwepa ukaguzi kwenye Wizara (Wizara ya Utalii ilipeleka zaidi ya shilingi 600 milioni Bodi ya Utalii mwaka 2010/2011). Ikumbukwe pia wizi wa EPA, MEREMETA na hata uuzaji holela wa baadhi ya mali za Serikali kupitia ubinafsishaji ulifanyika nyakati ambazo Bunge halina kamati inayosimamia Mashirika ya Umma.

Kwa vyovyote vile Spika wa Bunge amedhihirisha namna ambavyo anafanya maamuzi bila kuzingatia maslahi ya nchi wala kuzingatia historia ya uwajibikaji katika nchi. Namna mijadala ya Bunge inavyoendeshwa, namna anavyobeba ajenda za Serikali katika kujenga Bunge kibogoyo na namna anavyofanya maamuzi kwa kukurupuka, inahitaji hatua za kuokoa misingi ya uwajibikaji wa nchi. Ni lazima Spika wa Bunge adhibitiwe kwa kuondolewa katika nafasi hiyo haraka iwezekanavyo. Spika lazima ajue kwamba Mamlaka yapo kwa wananchi na yeye ni msimamizi tu wa vikao vya Baraza la wananchi liitwalo Bunge. Anna Makinda lazima adhibitiwe, vinginevyo nchi yetu itaumia.

Written by zittokabwe

February 10, 2013 at 11:24 AM

RASIMU YA RATIBA YA SHUGHULI ZA KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA MASHIRIKA YA UMMA (POAC)

with 4 comments

LENGO: KUCHAMBUA NA KUJADILI TAARIFA YA HESABU ZILIZOKAGULIWA ZA MASHIRIKA YA UMMA KWA MWAKA WA FEDHA UNAOISHIA JUNI 30, 2010

S/N

TAREHE

SHIRIKA

MHUSIKA

1 Jumamosi na Jumapili 22 -23 Oktoba Wajumbe kuwasili Dar es salaam  

 

 

 

 

 

  • WAJUMBE WA KAMATI
  • OFISI YA CAG
  • WENYEVITI WA BODI ZA MASHIRIKA HUSIKA
  • WATENDAJI WA MASHIRIKA
  • MSAJILI WA HAZINA

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

2 Jumatatu 24 Oktoba
  1. Bodi ya Utalii Tanzania ( TTB)
  2. Benki ya Posta Tanzania ( TPB)
3 Jumanne 25 Oktoba  

  1. kituo cha uwekezaji Tanzania ( TIC)
  2. Mfuko wa Pensheni ya Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa ( LAPF)
4 Jumatano 26 Oktoba
  1. Mamlaka ya Ufundi stadi Tanzania ( VETA)
  2. Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma ( PPF)
5 Alhamisi 27 Oktoba
  1. Shirika la Mafuta Tanzania ( TPDC)
  2. Chuo cha Uhasibu Arusha
  3. Chuo kikuu cha Ardhi
6 Ijumaa 28 Oktoba
  1. Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji ( EWURA)
  2. Shirika la Madini Tanzania ( STAMICO)

 

 

7 Jumamosi na Jumapili 29 – 30 Oktoba Mapumziko ya Mwisho mwa wiki

 

 

8 Jumatatu 31 Oktoba        1.   Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ( HESLB)

2.  Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania ( TANESCO)

 

9 Jumanne 01 Novemba
  1. Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)
  2. Maktaba kuu ya Taifa

 

10 Jumatano Novemba 02
  1. Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano ( TCRA)
  2. Tume ya Taifa ya Mipango ya Ardhi
  3. Chuo kikuu Dodoma
11 Alhamisi Novemba 03       1.Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB)

2. Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini ( IRDP)

 

12 Ijumaa Novemba 04
  1. Benki ya Twiga ( TWIGA BANCORP)
  2. Bodi ya Pamba Tanzania
  3. Chuo cha Taifa cha usafirishaji ( NIT)

 

13 Jumamosi na Jumapili 05 – 06 Novemba Kuelekea Dodoma Katibu wa Bunge

 

TANBIHI          

  • Saa 3:00 Asubuhi: kuanza Kwa kikao
  • Saa 4:00 Asubuhi: chai

 

Written by zittokabwe

October 25, 2011 at 12:40 PM

Press Release: Mkulo apishe uchunguzi

with 4 comments

 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri wa Fedha ndugu Mustafa Mkulo akae pembeni kupisha uchunguzi dhidi yake kuhusu Shirika la CHC.

Katika Mkutano wa Nne wa Bunge la Kumi kulitokea malumbano makali kati ya  Serikali na Wabunge wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma kuhusu kuongezwa muda wa Shirika la CHC. Wakati Waziri wa Fedha alileta Azimio la kulivunja Shirika hili lenye taarifa nyingi na nyeti kuhusu zoezi la Ubinafsishaji, Kamati ya Bunge ya POAC kutokana na uzoefu wake wa kukagua mahesabu ya Mashirika ya Umma na kufuatilia zoezi la Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma, ilipinga hatua hii na kulitaka Bunge kukataa Azimio la Serikali na kulifanyia marekebisho makubwa. Hatimaye Bunge liliridhia kufanya mabadiliko makubwa katika Azimio la CHC, kwa kuamuru Shirika lipewe uhai wa miaka 3 na kuagiza uchunguzi wa namna bora ya kuendesha shughuli za Shirika la Consolidated Holdings. Mapendekezo ya Kamati ya POAC ni kulifanya Shirika hili kuwa la kudumu na kulipa jukumu la kumiliki na kusimamia uwekezaji wa Serikali kwenye kampuni binafsi (National Investment Agency) kama ilivyo Shirika la Tamasek ya Singapore na Shirika la Khazana ya Malaysia. Kwa sasa Uwekezaji wa Serikali katika Kampuni binafsi unasimamiwa na Hazina na usimamizi wake ni mbovu na hauleti tija kwa Taifa.

Kitendo cha kushindwa kwa hoja Bungeni kiliifedhesha Serikali na hivyo kwa kupitia Wizara ya Fedha kuamua kulihujumu Shirika kwa kumsimamisha Mkurugenzi wake Mkuu kwa makosa ya kimajungumajungu na kwa kuzusha kwamba CHC iliwahonga wabunge ili kuitetea.  Waziri wa Fedha ndugu Mustafa Mkulo alilitaarifu Bunge kuwa Bodi ya CHC imeomba ukaguzi maalumu kuhusu tuhuma za ubadhirifu ndani ya Shirika hilo. Niliitaka Serikali ichunguze pia tuhuma kwamba Kamati ya POAC ilihongwa na kuahidi kuahidi kujiuzulu nyadhifa zangu zote ikithibitika.

Katika Uchunguzi wake Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Heabu za Serikali kwa kupitia Kampuni ya Ernest and Young walitaka kufanya mahojiano na Waziri wa Fedha juu ya tuhuma mbalimbali zinazomkabili ndani ya CHC. Waziri Mkulo alikataa kuhojiwa na wakaguzi na badala yake akaandika barua (kumb TYC/B/70/2/03 ya Oktoba 8, 2011) yenye kujibu tuhuma moja, tena kwa juu juu, kuhusu yeye kuliamuru Shirika kuuza kiwanja cha Shirika bila kufuata taratibu za sheria. Wakati Waziri anakanusha kuliagiza Shirika kuuza kiwanja kwa mtu aliyemtaka yeye, mimi nina ushahidi tosha wa Nyaraka kutoka Hazina, kwa mfano barua TYC/A/290/13/4 ya Machi 9, 2011 ambayo inawagiza CHC kutekeleza agizo la Waziri la Fedha kuhusu kiwanja na. 10 barabara ya Nyerere. Vilevile, nina ushahidi wa mkutano uliofanyika huko Morogoro Hotel kati ya Waziri wa Fedha na Mwenyekiti wa Bodi ya CHC kuhusu jambo hilo.

Siku mbili baada ya kumjibu CAG, Waziri wa Fedha ndugu Mustafa Mkulo aliamua kutengua uamuzi wake wa kuongeza muda wa Bodi ya Shirika la CHC mpaka mwezi Disemba 2011 na hivyo kuivunja. Uamuzi huu wa Waziri una lengo la kuficha ukweli kwani CHC bila Bodi ya Wakurugenzi inaendeshwa na Hazina na hivyo taarifa ya ukaguzi itabidi ipelekwe Hazina ambayo Waziri wake ni mtuhumiwa.

Uchunguzi wa kina

Ninapendekeza uchunguzi wa kina ufanyike kwa kutumia vyombo vya dola na hasa TAKUKURU kuhusu tuhuma hizi dhidi ya Waziri wa Fedha na alazimishwe  kisheria kujibu maswali ya wakaguzi (Auditors) kuhusu tuhuma dhidi yake.

Wakati uchunguzi unaendelea ndugu Mustafa Mkulo asimamishwe kazi ya Uwaziri wa Fedha hadi hapo uchunguzi utakapokamilika. Kitendo chake cha kuiamuru Bodi kumsimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu kwa tuhuma za kutunga na majungu na baadaye kuvunja Bodi ya CHC wakati inasubiri taarifa ya uchunguzi kutoka kwa CAG ni kuingilia uchunguzi na pia ni matumizi mabaya ya Ofisi ya Umma ili kulinda maslahi binafsi. Ni dhahiri akiendelea kuwa Waziri wa Fedha ataharibu uchunguzi.

Vilevile, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndugu Jakaya Kikwete aangalie kama anaitendea haki nchi na Uchumi wa nchi kwa kuwa na Waziri wa Fedha ambaye anasema uwongo Bungeni bila kuogopa na mwenye kutumia Ofisi yake vibaya kwa kuchukua maamuzi yanayoingilia uchunguzi unaomhusu ili kujilinda.

Taarifa ya Uchunguzi ikabidhiwe kwa Spika

Kutokana na ukweli kwamba suala la CHC lilianzia Bungeni na hata Waziri mwenyewe kukiri kuwa taarifa ya uchunguzi inapaswa kuwekwa wazi. Kutokana na matokeo ya sasa ambapo Waziri wa Fedha mwenyewe ana tuhuma za kujibu na kwamba hivi sasa hakuna Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika na hata itakayoundwa itateuliwa na Waziri mtuhumiwa ninashauri kuwa taarifa ya uchunguzi wa Shirika la CHC sasa ipelekwe kwa Spika wa Bunge kwa hatua zaidi.

Kabwe Zuberi Zitto, Mb

Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi

Dar es Salaam, 13 Oktoba, 2011.