Posts Tagged ‘KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI (PAC)’
Uwajibikaji, Changamoto na Uweledi wa Kamati ya PAC
Uwajibikaji, Changamoto na Uweledi wa Kamati ya PAC
Mfumo thabiti wa Uwajibikaji ni moja ya jawabu muhimu sana katika kuhakikisha Taifa linaondokana na ufisadi na masuala mengine yanayorudisha nyuma maendeleo ya Tanzania. Kazi za mwisho za Kamati ya PAC katika Bunge la Kumi zilisheheni mambo mengi muhimu katika mchakato endelevu wa ujenzi wa mfumo thabiti wa uwajibikaji nchini kwetu.
Taarifa ya Mwaka iliyojadiliwa na kupitishwa na Bunge wiki iliyopita ndio ilikuwa taarifa yetu ya mwisho katika Bunge hili. Kama kawaida mwaka 2015 ulianza kwa ziara za kukagua miradi na hatimaye kukutana na maafisa masuuli wa Wizara na Mashirika ya Umma ili kukagua mahesabu yao na kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya wakaguzi na Kamati.
Kipindi hiki ni muhimu sana kwangu kwani kwa vyovyote vile ni kazi yangu ya mwisho kufanya kama Mwenyekiti wa PAC, nafasi niliyoichukua mwezi Machi mwaka 2013. Kabla ya hapo nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) kuanzia Februari mwaka 2008 mpaka Februari mwaka 2013. Katika Maisha yangu ya miaka 10 Bungeni, nimetumikia uongozi wa kamati hizi kwa miaka Saba na Nusu. Hata hivyo leo natafakari kazi ya wiki nne tu na nilichojifunza katika siku hizo.
Wiki ya Kwanza, tulitembelea miradi ya njia za Reli na Mashamba ya Miwa ili kuongeza uzalishaji wa Sukari nchini. Tulikwenda mkoani Morogoro katika Wilaya za Kilosa na Kilombero. Tulijulishwa kuhusu mahitaji ya fedha nyingi katika ujenzi wa Reli ya Kati ambapo ili kukarabati mtandao Reli iliyopo zinahitajika jumla ya shilingi 500 bilioni kwa miaka mitatu mfululizo ($800m). Vilevile zinahitajika dola za Kimarekani $6 bilioni kujenga reli mpya ya kisasa (standard gauge). Wiki mbili baada ya kumaliza ziara hiyo, niliona picha ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akikagua ujenzi wa Reli ya kisasa nchini humo. Nilipoangalia picha yangu na wajumbe wenzangu katika kijireli chetu, nilicheka kicheko cha huzuni sana. Nimejifunza kwamba nchi yetu inaweza kusonga mbele iwapo tu tutaamua kujinyima baadhi ya maeneo ili kuendelea kwenye maeneo mengine. Fedha inayopotea katika kutoa misamaha ya kodi (tshs 1.9 trilioni ) peke yake, kwa mwaka mmoja inamaliza ukarabati wa Reli yote ( Kigoma – Tabora – Dar es Salaam na Tabora – Mwanza ).
Wiki hiyo pia tulitembelea kiwanda cha Sukari cha Kilombero na kukutana na Wakulima wa Miwa. Tanzania ina nakisi ya Sukari ya takribani tani 120,000 – 200,000 kwa mwaka. Uzalishaji wa ndani wa tani 300,000 hautoshelezi mahitaji ya wananchi na hivyo twalazimika kuagiza Sukari kutoka nje ya nchi ambayo husamehewa kodi. Kwa mwaka Tanzania husamehe kodi ya zaidi ya shilingi 200 bilioni katika Sukari peke yake. Fedha hii ingeweza kujenga viwanda kadhaa vya Sukari na hivyo kuachana kabisa na uagizaji na badala yake kuuza nje. Nimejifunza mengi sana katika kushughulikia suala la Sukari nchini. Nimeona namna ambavyo mfumo mzima wa Serikali ulivyo na ganzi katika kupata suluhisho la kudumu. Hivi sasa Serikali inataka uagizaji wa Sukari ufanywe na wazalishaji wa Sukari, majawabu ya namna hii ni majawabu ya kugawana pato nyemelezi (rent seeking). Jawabu la kudumu la sekta ya Sukari ni kuongeza uzalishaji wa ndani kwa kufungua viwanda vipya maeneo yenye miwa ya ziada hivi sasa, kutoa ruzuku kwa viwanda ili kupunguza gharama za uzalishaji na hatimaye kuwa na bei nafuu kwa walaji na kufungua mashamba mapya ili kuzalisha ziada na kuuza nje kwa ajili ya kupata fedha za kigeni.
Tulijadili kwa kina sana changamoto zinazoikabili sekta ndogo ya kilimo cha Korosho. Ukaguzi Maalumu ulionyesha kuwa kuna unyonyaji mkubwa wa wakulima ikiwemo kupewa pembejeo zilizoisha muda na kutofikishiwa pembejeo kabisa. Pia upotevu mkubwa sana wa Korosho na suala zima la kuuza korosho ghafi nje ya nchi. Utafiti uliofanywa na African Cashew Alliance unaonyesha kuwa Tanzania hupoteza zaidi ya dola za kimarekani 110 milioni kila mwaka kwa kuuza korosho ambazo hazijabanguliwa. Ikumbukwe kuwa Tanzania ilikuwa na viwanda 12 vya kubangua Korosho na vyote viliuzwa katika zoezi la ubinafsishaji na sasa vimekuwa ni maghala ya kuhifadhia Korosho. Tulielekeza kuwa mapato yanayotokana na tozo ya mauzo ya Korosho nje (export levy) yatumike kujenga viwanda vipya vya korosho kwa kutumia teknolojia mpya kutoka Vietnam ambapo viwanda vidogo vidogo vitajengwa kuanzia vijijini na kuzalisha ajira nyingi na kuondoa umasikini. Nimejifunza kwamba Korosho peke yake inaweza kuingiza fedha za kigeni katika nchi yetu kwa thamani ya zaidi ya dola za kimarekani 500 milioni kwa mwaka. Mwaka 2014 Tanzania imezalisha tani 200,000 za Korosho, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa tangu tupate Uhuru. Korosho inaweza kuondoa umasikini kwa watu wa mikoa ya Kusini iwapo Viongozi wakiamua iwe hivyo.
Ilituchukua siku 2 kujadiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania kuhusu mahesabu yao ya mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2013. Sababu kubwa ilikuwa ni mjadala kuhusu misamaha ya Kodi. Kama nilivyoeleza hapo juu, tulijulishwa kuhusu misamaha mingi ya kodi kuendelea kutolewa mpaka kufikia jumla ya shilingi 1.9 trilioni katika mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2014. Kamati pia ilijadili Taarifa ya ukaguzi maalumu kuhusu misamaha ya kodi na kugundua kuwa misamaha mingi inatumika ndivyo sivyo. Nimejifunza kuwa tukiendelea kusisitiza uwazi na uwajibikaji tunaweza kupunguza tatizo hili la misamaha holela ya kodi. Tuliagiza kuwa kuanzia sasa, katika kila Taarifa ya makusanyo ya TRA kila mwezi, pia taarifa ya misamaha ya mwezi huo itolewe kwa umma. Hii itasaidia kuonyesha ni mapato kiasi gani yangeweza kukusanywa bila ya misamaha na kama misamaha hiyo ni muhimu na inatumika ipasavyo.
Mifano hii michache ya Reli, Sukari, Korosho na Misamaha ya Kodi imenikumbusha changamoto nyingi ambazo nchi yetu inazo na namna bora ya kukabiliana na Changamoto hizo. Mfumo thabiti wa Uwajibikaji ni suluhisho endelevu dhidi ya changamoto hizi. Kamati ya PAC imeshiriki kikamilifu kujenga mfumo huo. Kazi bado kubwa lakini inaendelea.
Zitto Zuberi Kabwe
RATIBA -KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI (PAC) JANUARI 2015
KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI (PAC)
RASIMU YA RATIBA YA UKAGUZI WA MIRADI NA KUJADILI HESABU ZILIZOKAGULIWA ZA SERIKALI KUU NA MASHIRIKA YA UMMA KUANZIA TAREHE 05 HADI 24 JANUARI 2015,
MKOA WA MOROGORO NA OFISI NDOGO YA BUNGE, DAR ES SALAAM
Fedha za zilizokuwa katika akaunti maalumu ya IPTL, (Tegeta Escrow account) ni mali ya umma
Fedha za zilizokuwa katika akaunti maalumu ya IPTL, (Tegeta Escrow account) ni mali ya umma
Fedha za zilizokuwa katika akaunti maalumu ya IPTL, (Tegeta Escrow account) ni mali ya umma
Zitto Kabwe
Kwa mara nyingine serikali kupitia viongozi na watendaji wake akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wamedai kwamba kiasi cha Dola za Marekani milioni 250 zilizopaswa kuendelea kuwapo katika ‘Tegeta Escrow Account’ si mali ya serikali na hivyo si mali ya umma. Akaunti hiyo ilifunguliwa na serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) pamoja na kampuni ya Independent Power Limited (IPTL).
Kwa bahati mbaya sana viongozi wa serikali wamekuwa wakiendelea kurudia kuueneza huo uongo kwamba fedha hizo si mali ya umma. Inasikitisha pia kwamba vyombo vya habari vimekuwa navyo vikibeba na kusambaza huo uongo bila kuhoji na kuchunguza. Inashangaza sana pia asasi za kiraia nazo zimekaa kimya. Inatisha na kushangaa tena kuona wapinzani wakimwachia suala hili Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, pekee wakati mapambano dhidi ya rushwa ni ajenda kuu ya wapinzani. Kafulila amekuwa akiendelea kuhoji suala hilo bungeni peke yake bila kupata kuungwa mkono na kupewa msaada wa aina yoyote kutoka kwa wenzake wa kambi ya upinzani bungeni.
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilielekeza kuwapo kwa ukaguzi maalumu kwenye akaunti hiyo ya Tegeta escrow account iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuwa ndani yake kulikuwapo fedha za umma. PAC haina sababu yoyote ya kufuatilia fedha za watu binafsi. Mwaka 2009 iliyokuwa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ilitoa maelekezo kwa BoT kutothubutu kutoa fedha hizo. Agizo hilo la POAC lilitokana na sababu kwamba fedha hizo zilikuwa ndani ya hesabu za Tanesco.
Akaunti ya ‘Tegeta escrow’ ilifunguliwa kutokana na kuwapo kutoelewana kuhusiana na gharama halisi na halali za umeme unaozalishwa na IPTL na kuuzwa kwa TANESCO. Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICSID) katika uamuzi wake wa Februari, 2014 ilitoa hukumu kuonyesha kwamba Tanesco walitozwa kiwango cha juu zaidi ya kilichopaswa kulipwa kwa IPTL. Kwa uamuzi huo ni dhahiri kwamba fedha zilizokuwa zimehifadiwa kwenye akaunti hiyo maalumu ya escrow zilipaswa kugawanywa kwa IPTL na Tanesco baada ya hesabu kufanyiwa marekebisho upya kwa viwango halali.
Hesabu za mwaka wa fedha ulioishia Disemba 2012 za Tanesco zinaonyesha wazi kwamba fedha hizo ni mali ya shirika hilo la umma linalomilikiwa na serikali kwa asilimia mia moja. Fedha za kampuni ni suala la kisheria kama inavyobainishwa katika sheria ya kampuni ya mwaka 2002.
Kwa maelezo hayo na hoja hizo, inakuaje serikali ianze kudai kwamba fedha hizo si mali ya umma? Hivi inawezekanaje kwa fedha za mtu binafsi zikaingizwa katika hesabu za shirika la umma linalomilikiwa na serikali kwa asilimia 100? Ni lini fedha hizo zimekoma kuwa za umma? Je ni baada ya baadhi ya watendaji wa serikali kula njama za kuzichukua fedha hizo kwa kushirikiana na ‘mwekezaji’ aliyechafuka kwa ufisadi duniani?
Serikali inadanganya waziwazi kudai kwamba fedha hizo si mali ya umma. Umma una haki ya kukumbushwa kwamba madai hayo yalitolewa pia katika lile sakata la ufisadi maarufu wa EPA unaofanana kwa kila hali na huu wa sasa wa ‘Tegeta Escrow’.
Hoja nyingine ni kwamba, Mbunge Kafulila alisema kwamba Jaji Utamwa wa Mahakama Kuu ya Tanzania hakutoa uamuzi wa kuchukuliwa fedha kutoka akaunti ya ‘Tegeta Escrow’. Nimepitia kwa makini hukumu ya Jaji Utamwa na kubaini kwamba hakuna popote alipotaja akaunti ya ‘Escrow’. Hata hivyo, nilipopitia muhstasari wa kikao kati ya TANESCO, IPTL na Wizara ya Nishati na Madini, ndipo kwa mara ya kwanza nikakuta wametafsiri uamuzi wa mahakama wakidai kwamba fedha zote za ‘Tegeta Escrow’ zipewe kampuni ya PAP (inamilikiwa kwa asilimia 50 na Harbinder Singh na 50% na Simba Trust iliyosajiliwa Australia). Hiki ndicho kikao kilichofanya maamuzi ya kuiba na kugawana wenyewe fedha hizo (Hukumu ya Jaji Utamwa na muhstasari wa kikao vinaambatanishwa).
Wote waliohudhuria kikao hicho kilichojipa mamlaka ya kutafsiri hukumu ya Mahakama Kuu, wanapaswa kuchunguzwa na kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria zilizopo. Inawezekana vipi uamuzi wa mahakama ukatafsiriwa na kikao cha Wizara? Muhstasari wa kikao hicho ndio uliowasilishwa Benki Kuu (BoT) kuhalalisha madai kwamba fedha hizo lazima zitolewa kutoka akaunti ya Escrow.
Fedha zinazohusiana na akaunti ya Escrow ni Dola za Marekani milioni 250, katia ya hizo Dola milioni 122 zilizokuwa BoT zimeshatolewa na kiasi kilichosalia Dola milioni 128 zitalipwa na Tanesco kutokana na fedha zake kwa madai ya kushindwa kulipa kwa wakati. Fedha zilizolipwa ni zile ambazo zimetoka Wizara ya Nishati na Madini ambayo kisheria ndio walipaswa kulipia gharama za uzalishaji umeme (capacity charge) fedha zilizotoka kwa walipa kodi.
Ikumbukwe kwamba uhamishaji wa asilimia 70 ya hisa za IPTL kwenda PAP umeambatana na nyaraka za kughushi kutokana na kutokuwepo kabisa kwa uthibitisho wa cheti halisi cha hisa (share certificate) kutoka kampuni ya Mechmar kwenda kampuni ya Piperlink. Nyaraka za TRA zinaonyesha kwamba hisa hizo (70%) ziliuzwa kwa Shilingi za Kitanzania milioni sita (6) tu. Na bado hakuna ushahidi kuonyesha kwamba uhamishaji huo wa hisa ulipata baraka za mamlaka husika kama inavyotakiwa na sheria za nchi.
Wakati huyo anayejiita mmiliki mpya wa IPTL aliposaini mkataba wa kuchukua fedha kutoka akaunti ya Escrow zilizokuwapo BoT, hakuwa mmiliki halali kisheria kwani kodi ililipwa siku moja baada ya wao kupokea fedha kutoka BoT. Sheria inataka kutolewa kwa cheti na Kamishna wa TRA kama uthibitisho kwamba kodi yote imelipwa ipasavyo (Sheria ya Fedha ya 2012 kifungu cha 29).
Ni nani wamiliki wengine wa kampuni ya PAP? Uchunguzi ni muhimu ukawalenga vigogo na wanasiasa wakubwa wakiwamo watendaji waandamizi wa Wizara ya Nishati na Madini.
Inapaswa tutafakari kuona kwamba Harbinder Singh aliyechukua fedha za Escrow, anamiliki vitalu vya mafuta na gesi kupitia kampuni iitwayo HydroTanz ambayo nayo imesajiliwa nchini Australia, ikiwa na anwani sawa na ya kampuni ya Simba Trust. Kitalu hicho cha mafuta kinaitwa ‘Mnazi Bay North’, jirani kabisa na ugunduzi mkubwa wa hivi karibuni mkoani Mtwara.
Tunatarajia kwamba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), atafichua ukweli wa sakata hili na TAKUKURU itawafikisha mahakamani wahusika bila kujali nyadhifa zao serikalini.
Kauli ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, kwamba kuna watu waliokula rushwa na kwamba nyaraka zinazotajwa ni karatasi za kuuzia vitumbua, ni kauli zenye kuonyesha kutapatapa kwa watendaji serikalini. Hakuna hata mahali pamoja ambapo nimemtaja mtu kuwa ni mwizi zaidi ya kuwasilisha hoja zinazohitaji majibu mwafaka na si matusi, vitisho na tuhuma za kuzusha. Nyaraka za TRA haziwezi kuwa za kufungua maandazi kama ambavyo hukumu ya Jaji wa Mahakama Kuu haiwezi kuwa karatasi za kufungia maandazi na badala yake ni nyaraka halali zinazohitaji maelezo kutoka kwa viongozi na watendaji wa serikali badala ya kuropoka na kuporomosha matusi.
Hali kadhalika, Bunge lina kila sababu kupitia sheria yake ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kulinda hadhi yake kutoka kwa watendaji kama Maswi ambao wanatoa matamshi ya kuonyesha kwamba chombo hicho ni chombo cha watu wasiofaa na kwamba watu wanaofaa wanazungumza nje ya Bunge. Maswi na wengine kama wana ushahidi wa rushwa dhidi ya mbunge ama yeyote hawapaswi kupayuka ovyo bali kwa nafasi zao wanaweza kuwasiliana na vyombo vya dola kama TAKUKURU na polisi ili wachunguze na kuchukua hatua kama ambavyo vinawachunguza wao.
Kauli ya Maswi kwamba “wanaume” hawazungumzi ndani ya Bunge si tu udhalilishaji wa chombo hicho bali pia inaashiria ugonjwa wa mfumo dume uliotawala miongoni mwa viongozi wetu kwa maana kwamba wanaume ndio wenye hadhi, uwezo na heshima na wanawake ni dhaifu na wasiostahili heshima. Tufumbue macho tuone na tuondoe hisia binafsi zenye kubebwa na itikadi, chuki na misimamo yetu ya kisiasa. Tuwe wazalendo ili tuweze kusimamia utaifa.
Sent from my iPhone
Ukaguzi Maalumu akaunti ya Tegeta Escrow-Hadidu Rejea-PAC
Ukaguzi Maalumu akaunti ya Tegeta Escrow
Hadidu rejea
1) Kuchunguza uendeshaji wa mkataba wa kuzalisha Umeme kati ya kampuni ya IPTL na TANESCO
2) Kuchunguza kama wakati escrow inafunguliwa kampuni ya mechmar ilikuwa inamiliki IPTL, kama ilikuwa imefilisiwa na kama ilikuwa imehamisha umiliki wake kwa kampuni ya PAP.
3) Kuchunguza na kuthibitisha ushahidi wa kampuni ya PAP kununua kampuni ya mechmar na kumiliki IPTL
4) Kuchunguza chanzo cha mgogoro kuhusu tozo kati ya TANESCO na IPTL na kuthibitisha ushahidi wowote kuwa mgogoro uliamuliwa kwa faida ya IPTL
5) Kuchunguza kama ilikuwa sahihi kwa mwanasheria mkuu wa Serikali kusamehe kodi ya VAT ya jumla ya tshs 26 bilioni kutokana na tozo ya capacity charges na TRA wachukue hatua gani kuhakikisha kodi hiyo inakusanywa
6) Kuchunguza kiwango cha fedha kilichopaswa kuwemo katika akaunti ya escrow, kiwango gani kilikuwepo wakati IPTL wanalipwa na kiwango gani kitapaswa kulipwa zaidi kutoka tanesco
7) Kuchunguza madai ya benki ya standard chartered kwa tanesco na madai mengine yeyote yanayohusiana na mkataba wa kuzalisha Umeme wa IPTL na iwapo Serikali imejihadhari na uwezekano wa madai yanayoweza kufunguliwa, nafasi na heshima ya nchi katika kuheshimu mikataba ya kimataifa na ya uwekezaji.
8) Kuchunguza iwapo Wizara ya Nishati na madini ambayo ni mhusika Mkuu wa akaunti ya tegeta escrow ilifanya ‘due diligence’ ya kutosha kabla ya kuingia makubaliano ya kutoa fedha zilizopo akaunti ya tegeta escrow. Kupata Maelezo ya Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na madini ni kwa nini aliagiza ukaguzi maalum wakati yeye ni mhusika Mkuu kwenye mchakato mzima na ilhali akijua PAC tayari imeanza mchakato wa ukaguzi.
9) Kutoa mapendekezo ya njia bora za kisheria kulinda Taifa kutoingia hasara zaidi katika mkataba wa IPTL chini ya wamiliki wapya
10) Kutoa ushauri kwa kamati ya PAC juu ya mapendekezo ya hatua ambazo Bunge linapaswa kuchukua kuhusu matokeo ya ukaguzi huu maalumu
Imetolewa na;
KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI (PAC)