Archive for the ‘Zitto na Demokrasia’ Category
MAELEZO BINAFSI YA MHE. ZITTO ZUBERI KABWE DHIDI YA TUHUMA ZA RUSHWA HUSUSAN KUELEKEA KATIKA KUPITISHA BAJETI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI
MAELEZO BINAFSI YA MHE. ZITTO ZUBERI KABWE DHIDI YA TUHUMA ZA RUSHWA HUSUSAN KUELEKEA KATIKA KUPITISHA BAJETI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI
Ndugu Waandishi,
Nalazimika kukutana nanyi kutoa maelezo juu ya tuhuma zenye shinikizo la kisiasa zinazoelekezwa kwangu binafsi kwamba hata mimi nimeshiriki katika vitendo vya rushwa, kwa nafasi yangu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma. Taarifa hizo, kama kawaida ya uzushi mwingine wowote zimesambazwa kimkakati na kwa kasi kubwa kiasi cha kuukanganya umma.
Nafahamu nabeba dhamana kubwa ya uongozi, taswira yangu ya uongozi daima imeakisi njozi na matumaini ya wananchi wa Kigoma Kaskazini, wananchi wanyonge na vijana kote nchini bila kujali itikadi zao za kisiasa, jinsia zao, makabila yao na rika zao. Hivyo, nawajibika kupitia kwenu kuwatoa hofu juu ya hisia potofu zinazopandikizwa kwao na wale wasiopenda kuona baadhi yetu tukiwaunganisha na kuwasemea watanzania wasio na sauti, dhidi ya vitendo vya hujuma na vyenye dhamira ovu kwa taifa.
Mkakati huo wa kuniunganisha na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanaotuhumiwa kwa kupokea Rushwa unatekelezwa kwa njia zifuatazo:
- Kumekuwa na kauli za watendaji wa serikali ambao wamekuwa wakizieneza na hususan kutoa taswira kwamba baadhi ya kauli zangu zinatokana na ushawishi wa rushwa;
- Kuna taarifa ambazo zimeandikwa tena katika kurasa za mbele za baadhi ya vyombo vya habari zikidai ’’Zitto kitanzini’’ ama ’’Zitto sawa na popo nundu’’ zikiashiria kwamba na mimi ni mla rushwa; na
- Waandishi wa habari na jamii kwa ujumla wamefikia kuaminishwa habari hizi kiasi cha wengine kuuliza kwa nini Mhe. Zitto Kabwe hakutajwa katika orodha iliyotolewa na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani.
Ndugu Waandishi,
Naomba kutoa ufafanuzi wa hicho kinachoelezwa kwamba nina ushiriki katika masuala ya rushwa hususan kwenye masuala yanayohusu sekta ya Nishati na Madini:-
- Mara baada ya bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Usambazaji wa Umeme Tanzania (TANESCO) chini ya Uenyekiti wake Meja Jenerali Mstaafu Robert Mboma kutangaza kwamba imemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Nd. William Mhando ili kupisha uchunguzi wa baadhi ya vitendo/mwenendo wake, Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ambayo mimi ni Mwenyekiti wake ilimuandikia Mhe. Spika kumuomba aridhie ili Kamati iweze kuwaita Bodi ya TANESCO, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG) na pia Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kujiridhisha na tuhuma zote zinazotajwa zinafanyiwa uchunguzi wa kina na hatua kuchukuliwa;
- Kamati ya POAC ninayoiongoza ilimuomba Mhe. Spika kuwaita wahusika tajwa kwa kuwa zilikuwapo tetesi kuwa kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi huyo siku chache kabla ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kulikuwa na lengo la kufunika ’madudu’ makubwa zaidi kwa kulichagiza Bunge na tukio hilo dogo, mkakati ambao naona umefanikiwa sana. Isitoshe, Kamati kutaka kujiridhisha na hatua za Bodi ni sehemu ya msingi ya utekelezaji wa majukumu ya Kamati yaliyowekwa kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge na pia Shirika la TANESCO ni moja kati ya mashirika ambayo yanawajibika kwetu kwa hesabu zake na pia ufanisi wake kwa ujumla. Tumefanya hivyo pia katika mashirika mengine, hili la TANESCO sio tukio la kipekee;
- Kitendo hiki cha halali na kwa mujibu wa Kanuni kilichofanywa na Kamati yangu kimetafsiriwa kwa makusudi na baadhi ya watu kwamba ni ishara ya kuwa sisi au zaidi kwamba mimi nina maslahi binafsi na TANESCO na hususan Mkurugenzi wake Injinia Mhando, ndio maana tumetaka maelezo ya Bodi. Ukweli kwamba Kamati ya POAC tumewaita pia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu (CAG) na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa jambo hilo hilo umefichwa kwa makusudi!
- Baada ya tukio hilo, nikiwa hapa Dodoma, mwandishi wa habari wa gazeti moja alinifuata akiniambia kuwa wamekutana na Mhe. Waziri Mhongo na Katibu Mkuu wake, Nd. Eliachim Maswi hapa hapa Bungeni na wamewaambia kuwa mimi nimepewa rushwa. Hakutaja nimepewa rushwa na nani, kiasi gani na wala kwa lengo gani!
- Nimejaribu kumtafuta kwa simu Mhe. Waziri Mhongo na Katibu Mkuu wake ili wanipe ufafanuzi juu ya mimi na Kamati ya POAC kuhusishwa na tuhuma hizi bila mafanikio, hali ambayo inaniondolea mashaka juu ya ushiriki wao katika kueneza au kuthibitisha uvumi huo. Najaribu sana kujizuia kutokuwa na mashaka na ushiriki wao huo ikizingatiwa uzito na taswira ya nafasi zao katika jamii, lakini wameshindwa kunidhihirishia tofauti.
Sasa naomba kutoa ufafanuzi rasmi kuhusu mlolongo wa matukio hayo tajwa ambayo yanatumiwa na baadhi ya wanasiasa kuonesha kwamba eti nimehusika na vitendo vya rushwa.
- Binafsi sijawahi kuwa na mawasiliano ya aina yeyote na uongozi wa TANESCO kushawishiwa juu ya hatua ambazo POAC ndio imezichukua za kutaka kujiridhisha juu ya utaratibu uliotumika. Ieleweke wazi kabisa kuwa, hakuna wakati wowote, popote ambapo mimi binafsi au Kamati yetu imekataa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO kuchunguzwa kwa tuhuma zozote. Ambacho tumesisitiza wakati wote ni ufuatwaji wa taratibu, kanuni na sheria, hili nitalisimamia iwe masika au kiangazi;
- Ni kwa sababu hiyo, na kwa kujiamini kabisa nimeunga mkono suala la tuhuma za rushwa zinazotajwa zichunguzwe na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kina;
- Nimekwenda mbali zaidi kukiomba chama changu CHADEMA kifanye pia uchunguzi na tathmini yake kwa kina kujiridhisha na tuhuma hizo;
- Natumia fursa hii pia kuomba vyombo vya Dola vichunguze tuhuma hizo kwa nafasi yake ili kuweza kupata ukweli;
- Ninaahidi kushiriki kikamilifu iwapo nitatakiwa katika uchunguzi wowote utakaofanywa na niko tayari kuwajibika iwapo nitakutwa na hatia yeyote.
Napenda niwatoe hofu wananchi wa jimbo la Kigoma Kaskazini walionituma kuja kuwawakilisha hapa Bungeni na Watanzania wote kwa ujumla kwamba:-
- Mimi Zitto Zuberi Kabwe sina bei, sijawahi kuwa nayo na sitarajii kuwa nayo huko mbeleni. Daima nimesimamia kidete maadili ya uongozi bora katika maisha yangu yote ya siasa, na nawaahidi sitarudi nyuma katika mapambano dhidi ya rushwa katika nchi hii pamoja na mikakati ya aina hii ya kunidhoofisha na kunivunja moyo;
- Nafarijika na salam mbali mbali zinazotolewa kunifariji na kusisitiza kuwa nisilegeze kamba katika mapambano haya, nimepokea ujumbe mwingi kwa simu, sms, tweeter na hata facebook na niko pamoja nanyi Watanzania wenzangu kamwe sitarudi nyuma hadi kieleweke. Naamini katika nchi yetu tunazo rasilimali za kutosha mahitaji/haja ya kila mmoja wetu lakini si ‘tamaa/ulafi’ wa baadhi ya watanzania wenzetu;
- Napenda kuweka rekodi sawa kwa Watanzania kwamba nimekuwa Mbunge hiki ni kipindi cha pili, Mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) huu ni takriban mwaka wa saba sasa, Kamati yangu inasimamia mashirika 259 ya Umma na si TANESCO peke yake. Mchango wa Kamati hii katika Bunge na kwa ustawi wa Mashirika ya Umma ni bayana na haujawahi kutiliwa shaka. Kamati yetu imeokoa upotevu mkubwa wa mali za umma na kuokoa fedha za umma kutokana na umakini wake. Tumefanya hivyo CHC hivi karibuni, Kiwira na kwenye mashirika mengine mengi. Kote huko uadilifu na uzalendo wa Kamati hii haujawahi kuhojiwa. Inatuwia vigumu kuona kuwa tunahojiwa katika suala hili la TANESCO. Hapa pana kitendawili.
- Zipo hoja pandikizi za kutaka Kamati ya POAC ivunjwe na haswa zikinilenga mimi binafsi. Nafahamu kiu ya wasioitakia mema nchi yetu kuiona POAC ikivunjwa au sura zikibadilishwa kwa kuwa Kamati hii imekuwa mwiba kwa mikakati yao ya kifisadi. Kwa maoni yangu, Kamati ya POAC isihusishwe na tuhuma hizi kwa vyovyote vile. Niko tayari nihukumiwe mimi kama mimi na sio kuhusisha wajumbe wengine ambao hawatajwi mahala popote katika tuhuma hizi mbaya sana katika historia ya Bunge letu. Nitakuwa tayari kunusuru Kamati ya POAC na maslahi ya taifa letu kwa kujiuzulu Uenyekiti iwapo itathibitika pasipo shaka kuwa nimehongwa. Kamati ya POAC ni muhimu zaidi kuliko mimi.
- Nafahamu pia kuwa kuna wanasiasa hasa wa Upinzani ambao wanautaka sana Uenyekiti wa POAC na wanafanya kila njia kutaka kuidhoofisha. Lakini hawajui kuwa anaepanga wajumbe wa Kamati ni Spika wa Bunge.
- Msishangae pia kuja baadae kubaini kwamba baadhi ya wanasiasa wenye midomo mikubwa ya kutuhumu wenzao wao ndio vinara wa kupokea rushwa.
- Ni lazima tufike mahali kama viongozi kwamba utaratibu unapokiukwa na yeyote yule, au uongo unapotolewa hadharani tuseme bila kuogopa. Hili ndio jukumu letu kama wabunge na viongozi. Kusimamia ufuatiliaji wa utaratibu ni jukumu letu kama Kamati ya POAC na ndio sababu ya msingi ya kuanzishwa kwa mamlaka kama CAG na PPRA. Haiwezekani, tuwe na set ya kanuni kwa kundi fulani na nyingine kwa makundi mengine, au kuhukumu ufuataji wa taratibu kwa kuangalia sura ya mtu usoni
Mwisho
Kumejengeka tabia hivi sasa ya kuwamaliza wanasiasa wenye kudai uwajibikaji na uzalendo. Kumeanzishwa kiwanda kwenye medani ya siasa cha kuzalisha majungu na fitna zenye lengo la kuwachonganisha wanasiasa wa aina hiyo na wananchi kwa kutumia vyombo vya habari na nguvu ya fedha. Naamini mbinu hizi chafu, kama nyingine nyingi zilizojaribiwa kwangu huko nyuma nazo zitashindwa.
Naamini katika kweli na kweli daima huniweka huru. Naamini kuwa mwale mdogo wa mwanga wa mshumaa hufukuza kiza. Kwa imani hiyo, sitasalimu amri mbele ya dhamira zao ovu hata nitakapobaki peke yangu katika mapambano hayo ya kulinda na kutetea rasilimali za taifa zinufaishe watanzania wote.
Daima nitaongozwa na busara ya Hayati Shabaan Robert isemayo, ‘Msema kweli huchukiwa na marafiki zake, nitakapofikwa na ajali hiyo, sitaona wivu juu ya wale wawezao kudumu na marafiki zao siku zote, siwezi kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa kitambo, nikajitenga na furaha ya kweli itakayotokea pale uwongo utakapojitenga”.
Ahsanteni sana.
TAARIFA YA KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA MASHIRIKA YA UMMA #POAC #KamatiMashirikaUmma @teamzitto

KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA MASHIRIKA YA UMMA
TAARIFA YA KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA MASHIRIKA YA UMMA KWA MWAKA WA FEDHA UNAOISHIA JUNI 30, 2010
HIGHLIGHTS
Maoni na Mapendekezo ya Kamati
Baada ya mjadala wa maudhui na uchambuzi wa Taarifa hii hapo awali, Kamati ina maoni na mapendekezo mahususi yafuatayo:
7.1 Maoni ya Kamati
Mheshimiwa Spika, ni maoni ya Kamati kuwa , Ofisi ya Msajili wa Hazina bado inatakiwa kuimarisha usimamizi katika Mashirika ya Umma kwa niaba ya Serikali, aidha Kamati inaamini kuwa iwapo Mashirika ya Umma yatasimamiwa vema , yana nafasi kubwa ya kusaidia ukuaji wa pato la taifa na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaendelea kusisitiza kuwa katika uchumi mchanganyiko (mixed economy), ambao Sekta binafsi haijakuwa sana na hivyo kuihitaji Sekta ya Umma katika kutengeneza miundo mbinu na mazingira bora ya uchumi, ni wajibu wa Serikali kwa kupitia Mashirika ya Umma kuendelea kutoa baadhi ya huduma za muhimu kwa Wananchi wake kwa gharama nafuu zaidi bila kulenga kupata faida kubwa. Ni kwa mantiki hiyo, Kamati ina maoni kuwa huduma za afya, pensheni kwa wazee, huduma za nishati na uinuaji wa kiuchumi kwa Wananchi wa kawaida zitabaki kutegemea kwa kiasi kikubwa mashirika ya Umma hapa Nchini.
7.2 Mapendekezo ya Kamati
Mheshimiwa Spika,kwa kuzingatia kanuni za kudumu za Bunge Toleo la mwaka 2007, Naomba kuwasilisha Mapendekezo ya Kamati kama ifuatavyo;
7.2.1 Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Kamati imebainisha kuwa Mashirika mengi ya Umma hayana mitaji ya kutosha kujiendesha, na kwa kuwa kutokuwepo kwa mitaji kunasababishwa zaidi na kutokuwepo kwa mfuko wa uwekezaji wa Umma ( Public Investment Fund), kwa hiyo Kamati inaendelea kupendekeza kuwa Mfuko wa uwekezaji wa Umma uanzishwe mara moja ili kwa utaratibu utakaoonekana unafaa baadhi ya Mashirika ya Umma yenye kupata faida yaanze kuweka fedha katika mfuko huo ili kusaidia Mashirika ya Umma yasiokuwa na mitaji ila ni strategic kwa Taifa letu.
7.2.2 Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Kamati imebaini viashiria vya Fedha za kufidia wakulima wa Pamba kutokana na anguko la uchumi duniani, kutowafikia walengwa kupitia kwenye Bodi ya Pamba Tanzania, na kwa kuwa viashiria hivyo vinatokana na ukaguzi wa Hesabu za Bodi kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30,2010 ambao umeonyesha kuwa baadhi ya walengwa wa fedha za kunusuru bei ya Pamba wamekiri kutopewa fedha hizo na hivyo Mkaguzi kutoa hati yenye shaka kwa Bodi ya Pamba. Kwa hiyo Kamati inapendekeza kuwa, Kamati inapendekeza kuwa Bodi ya Pamba, iliyopo sasa hivi, ivunjwe na iundwe upya. Aidha Kamati inaitaka Serikali ifanye ukaguzi na uchunguzi maalumu ili kubaini iwapo fedha za kufidia anguko la bei ya Pamba ziliwafikia walengwa kama ilivyokusudiwa na kisha kuchukua hatua stahili kutokana na uchunguzi huo na Bunge lipewe Taarifa ya matokeo ya Uchunguzi huo.
7.2.3 Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika tathmini yake ya viwanda vilivyobinafsishwa vya ubanguaji Korosho, imebainika kuwa baadhi ya wawekezaji wamekiuka kwa makusudi mikataba ya uendeshaji wa Viwanda hivyo, na kwa kuwa kwa kufanya hivyo wamesababisha Taifa kuendelea kusafirisha korosho ghafi kwenda Nje ya Nchi na hivyo kuondoa fursa ya wakulima kupata faida ya kutosha na kupunguza ajira Nchini, kwa hiyo Kamati inapendekeza kuwa Serikali ichukue uamuzi wa kuvirejesha viwanda vyote vya kubangua Korosho vilivyobinafsishwa na wawekezaji wake kushindwa kuviendeleza ili kuona namna bora ya kuwekeza kwenye ubanguaji wa korosho ikiwa na pamoja na Serikali kusisitiza umuhimu wa kuuza Korosho iliyobanguliwa Nje ya Nchi kwa kuwajengea uwezo wakulima wa kubangua Korosho.
7.2.4 Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Kamati imebaini kuwa Bodi ya Madawa Tanzania (MSD) inatumia takribani siku 21 ili kukamilisha mchakato wa kuondoa dawa bandarini , na kwa kuwa ucheleweshaji huo una athiri usambazaji wa dawa hapa Nchini kwa wakati muafaka na muda mwingine kusababisha dawa kuharibika kabla ya kuwafikia walengwa na hivyo kusababisha Hoja kadhaa za Ukaguzi wa Hesabu, Kamati inapendekeza kuwa Bodi ya madawa ianze mchakato wa kuwa na ghala maalum (bonded ware house) ili kurahisisha utoaji wa dawa bandarini mapema iwezekanavyo na zikaguliwe huko na Mamlaka zinazodhibiti ubora kama Shirika la Viwango la Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA). Kamati inapendekeza kwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha na TRA kuharakisha jambo hili kabla mwaka wa fedha haujakamilika.
7.2.5 Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Kamati imebaini na kuthibitisha ukosefu wa mitaji ya kutosha na uwekezaji mdogo wa serikali katika baadhi ya Mashirika ya Umma ili yatekeleze mipango mikakati muhimu kwa manufaa ya Umma na baadhi ya Mashirika hayo ya Umma ni yale ambayo ni chachu ya maendeleo ya Taifa (strategic parastatals) , na kwa kuwa ukosefu wa fedha na mitaji unazorotesha juhudi za Taifa letu kupata maendeleo, kwa hiyo Kamati inapendekeza kuwa Serikali itoe bajeti ya kutosha kwa Mashirika yafuatayo, Baraza la Taifa la uwezeshaji kiuchumi ( NEEC) ambalo linahitaji kiasi cha shilingi bilioni 25.5 kutekeleza majukumu yake ya kisheria, Shirika la Tija la Taifa (NIP) na Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO) ili Mashirika haya yaweze kutekeleza mipango yake ipasavyo ambayo mingi imelenga kuinua Maisha ya Watanzania wa kawaida waweze kushiriki shughuli za kiuchumi ipasavyo.
7.2.6 Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Taifa linakabiliwa na Changamoto kubwa zinazohusiana na shughuli za usimamizi wa Nishati ya Gesi asilia na Mafuta na hasa uchimbaji na usimamizi wa mapato yatokanayo na gesi asilia, na kwa kuwa tunalo Shirika la Umma la Mafuta na Petroli (TPDC) ambalo ndilo lenye jukumu la kuendeleza Sekta hiyo hapa Nchini, na kwa kuwa Shirika hilo linakabiliwa na changamoto kubwa ikiwamo kutojiendesha kwa mujibu wa Amri ya Uanzishwaji wake (establishment order) na hivyo kukwama kutekeleza majukumu yake ipasavyo, kwa hiyo basi Kamati inapendekeza kuanzia sasa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) lijiendeshe kwa mujibu wa Amri (order) ya uanzishwaji wake[1] ( TPDC Establishment Order of 1969 na pia Public Corporation Act of 1992) ikiwa ni pamoja na kubaki na fedha zote inazokusanya kama Mashirika mengine (retention) badala ya kurudishwa Wizara ya Nishati na Madini. Aidha Kamati inasisitiza kuwa, Wizara ya Nishati na Madini isiingilie utendaji kazi wa kila siku wa TPDC, ili Shirika hili lifanye kazi kwa ufanisi, kwa uhuru na kwa misingi ya uanzishwaji wake.
7.2.7 Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kumedhihirika wazi ukosefu wa ufanisi katika uendeshaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kulikosababishwa na matatizo ya Menejimenti iliyokuwepo na mikataba mibovu (mfano ukodishwaji wa ndege ya Air bus), Kamati inapendekeza hatua za kisheria zichukuliwe kwa wote waliohusika na uingiaji wa mikataba hiyo, lakini pia kamati inapendekeza Serikali ifikirie uundwaji upya wa Shirika la Ndege la Taifa.
7.2.8 Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tathmini ya ubinafsishaji wa Mashamba ya Mkonge imedhihirisha kuwa, Hali ya mashamba mengi siyo nzuri. Kati ya mashamba yote yaliyobinafsishwa, ni mashamba mawili tu ya Mkambara na Mwelya yanayoridhisha kwa namna yanavyohudumiwa. Kamati inashauri serikali ifuatilie kwa ukaribu uendelezaji wa mashamba ili sera ya ubinafsishaji iwe na matunda yaliyokusudiwa. Aidha ili kuepuka migogoro na Wananchi, Maeneo ya mashamba yaliyovamiwa na wananchi yaachiwe kwa wananchi hao na mipaka ya mashamba ilindwe ipasavyo, na kwa wawekezaji walioshindwa kuendeleza mashamba ya Mkonge, Serikali iyarudishe na kuyagawa upya ikiwezekana hata kwa Wakulima wadogo. Fikra kwamba Mkonge lazima ulimwe na Wakulima wakubwa imepitwa na Wakati, Serikali iwawezeshe Wakulima wadogo kupitia Taasisi za fedha walime Mkonge katika Mashamba hayo.
7.2.9 Mheshimiwa Spika, Kutokana na ongezeko la riba inayotokana na Mkopo ambao Serikali imechukua kutoka kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii kugharimia ujenzi wa Chuo Kikuu Dodoma, Kamati inatoa pendekezo mahsusi kwa Serikali kutia saini Makubaliano ya Mkopo baina yake na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Nchini kwa fedha walizotoa kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma. Ni vema ikafahamika kuwa Fedha hizi ni mali ya Wanachama na hivyo ni lazima zilindwe ipasavyo. Itakumbukwa kuwa pendekezo hili limetolewa kwa mara ya tatu mfululizo na Kamati kwenda Serikalini na hadi sasa halijatekelezwa; Kamati inataka kupata maelezo ya Serikali juu ya jambo hili, kwa hiyo Kamati inaliomba Bunge liazimie sasa, na kuitaka Serikali kutia saini makubaliano hayo ili madeni ya Mifuko ya Jamii yawe salama kwa mujibu wa Sheria ya Dhamana, mikopo na ruzuku. Kamati inasisitiza kuwa madeni ambayo hayana Mashaka yaanze kulipwa mara moja.
7.2.10 Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mkataba baina ya Shirika la Utangazaji Tanzania ( TBC) na Star Times International Communication una mapungufu kadhaa ya kisheria na ambayo yamebainishwa na Mkaguzi wa Hesabu wa TBC baada ya kuchambua Mkataba na Taarifa ya Hoja za Ukaguzi,na kwa kuwa mapungufu hayo yanaweza kuwa na athari katika utendaji wa TBC kwa siku zijazo , kwa hiyo basi Kamati inapendekeza kuwa, Serikali iupitie upya Mkataba huo ili kuainisha maeneo ya maboresho, aidha Serikali ifanye utaratibu wa kuangalia namna nzuri ya kutoa fedha kwa uendeshaji wa TBC ili kiwe chombo cha utangazaji wa Umma chenye kujiendesha kwa uhuru na kwa maslahi ya Umma.
7.2.11 Mheshimiwa Spika, kwa kuwa suala zima la ubinafshaji wa yaliokuwa Mashirika ya Umma limekuwa na changamoto kubwa, zaidi kutokana na baadhi ya mali za Mashirika kuuzwa kwa bei isiyolingana na thamani , pia Mikataba mingi ya ubinafsishwaji kukiukwa na wawekezaji, na kwa kuwa kwa kiasi kikubwa zoezi hili halikufanikiwa katika maeneo mengi, na kwa kuwa Bunge kama mwakilishi wa Wananchi lingependa kufahamu faida na changamoto ya zoezi zima la ubinafsishaji ili Waheshimiwa Wabunge wapate nafasi ya kujadili zoezi hilo kwa uwazi, hivyo, Kamati inapendekeza Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuendesha Uchunguzi Maalum ( inquiry on Privatisation Policy in Tanzania ) kwa kushirikiana na Shirika Hodhi la yaliyokuwa Mashirika ya Umma ( CHC) , Taarifa ya uchunguzi huo iwasilishwe na kujadiliwa ndani ya Bunge mapema iwezekanavyo. Kamati inaazimia kufanyika kwa “ public inquiry” katika zoezi la ubinafsishaji, uchunguzi huu utakuwa wazi na Taarifa yake itajadiliwa Bungeni na kuwa wazi kwa Wananchi.
7.2.12 Mheshimiwa Spika, kwa kuwa changamoto zinazolikabili Taifa katika Sekta ya mafuta na gesi ni kubwa na hivyo kuhitaji Mkakati wa Makusudi wa muda mrefu wa kukabiliana nazo, na kwa kuwa Mashirika ya Umma ikiwa ni pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli( TPDC) ndio wadau wakubwa wa kuhakikisha Nchi inanufaika ipasavyo na Sekta ya gesi na Mafuta, na kwa kuwa Makampuni yanayotafuta mafuta na gesi hapa Nchini yamekuwa yakipeleka fedha TPDC ili ziweze kutoa mafunzo kwa watumishi ili kuongeza uelewa katika Sekta hiyo, kwa hiyo Kamati inapendekeza kuwa, kuanzishwe Mfuko Maalumu (Trust Fund) ili fedha zote za Mafunzo ziwekwe humo ili kupanua wigo kwa watanzania wote ambao wangependa kusomea fani za gesi na mafuta waombe ufadhili katika Mfuko huo wapate mafunzo badala ya fedha za mafunzo kutumika kwa watumishi wachache wa TPDC na Wizara ya Nishati na Madini na muda mwingine kutumika kwa shughuli zisizo za Mafunzo kama ilivyobainishwa na Kamati ya Nishati na Madini.
7.2.13 Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) linakabiliwa na hali mbaya ya kifedha unaotokana na gharama kubwa za kununua umeme kutoka kwenye makampuni binafsi (kwa mfano IPTL pekee wanalipwa shilingi bilioni 64.2 kwa mwaka), na kwa kuwa gharama za ununuzi wa umeme ndio zinasababisha TANESCO iendelee kupata hasara kila mwaka (kwa mfano hasara ya shilingi bilioni 47.3 kwa mwaka 2009/2010) na hata kuongeza gharama za umeme kwa Wananchi, Kamati inapendekeza kuwa, katika muda mfupi baada ya mtambo wa TANESCO wa ( jacobsen) kuanza kazi waachane na kununua umeme wa gharama kubwa kama ule wa IPTL, na katika muda mrefu Kamati inasisitiza kufanyike uwekezaji wa kutosha katika kuzalisha umeme. Miradi ya Umeme inayopendekezwa kufanywa na Mshirika ya Umma ipewe kipaumbele sana ili kuwepo na mchanganyiko sawia (right balance) kati ya uwekezaji binafsi na ule wa Umma.
7.2.14 Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Taarifa za uchunguzi kuhusiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) uliofanywa na Kamati Ndogo ya POAC ulikamilika na Taarifa kuwasilishwa kwako, na kwa kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali pia amekamilisha uchunguzi kuhusu TBS na utekelezaji wa majukumu yake ya kisheria, Kamati inapendekeza sasa Serikali ilete Taarifa ya utekelezaji na majibu ya Hoja za Taarifa hizo mbili ili Bunge liweze kupata nafasi ya kuzijadili kwa kina.
[1] TPDC Establishment Order of 1969 and Public Corporation Act, 1992
TAARIFA YA KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA MASHIRIKA YA UMMA KWA MWAKA WA FEDHA UNAOISHIA JUNI 30, 2010