Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Posts Tagged ‘maji

Siku ya 9 ya Ziara ya CHADEMA Kanda ya Magharibi – Jimbo la Igunga, Wilaya ya Igunga

with one comment

Siku ya 9 ya Ziara ya CHADEMA kanda ya Magharibi imetufikisha Jimbo la Igunga, Wilaya ya Igunga.

Tumefanya mikutano 6 katika kata sita tofauti, tumefungua matawi ya chama na kuhutubia wananchi. Pia tumepokea kero za wananchi zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.

Tukiwa Katika kata ya Choma tumeshuhudia kiwanda cha kuchambua Pamba kilicho binafsishwa kikiwa kimetelekezwa na mwekezaji toka mwaka 1998. Ginnery hii iliyokuwa mali ya umma na kuajiri wafanyakazi 500 kwa shifti 3 kila siku (jumla 1500) nyakati za msimu imekufa na baadhi ya Mashine kuuzwa kama chuma chakavu. Kijiji cha Choma kimedorora kiuchumi kutokana na ubinafsishaji huu. Nimewaeleza wananchi kuwa nitafuatilia suala hili la Ginnery ya Manonga, katani Choma na kuwajulisha hatua mwafaka za kuchukua.

Nimependekeza pia kwamba iwe marufuku kuuza nje mazao ghafi kwani tunakuwa tunauza ajira za watu wetu. Suala hili nimekuwa nikilisema Bungeni mara kwa mara kwamba ni lazima kusafirisha mazao yaliyoongezwa thamani kwa kupiga marufuku kuuza korosho ghafi, Pamba ghafi, kahawa ghafi na Katani ghafi. Viwanda vya kilimo vinaongeza ajira sana kwa wananchi na ni suluhisho endelevu kwa tatizo la ajira na kuondoa umasikini.

Niliwapa mfano wa kiwanda kilichouzwa huko mtwara na kugeuzwa godown la kuhifadhi korosho na godown liligeuzwa kuwa kiwanda cha kubangua korosho! Niliwaeleza namna viongozi wa Serikali wanavyochanganya dhana ya uhuru wa biashara (liberalisation) na ubinafsishaji (privatisation). Dhana mbili zinazochanganya watawala wengi wa Afrika na kujikuta wakiuza mali za umma kiholela. Unaweza kuwa na Mashirika ya Umma yakishindana katika soko na makampuni binafsi. Ubinafsishaji holela unatengeneza ‘private monopolies’ na kuathiri sana ukuaji wa uchumi kutokana na ufanisi mdogo ie efficiency.

Nimerejea wito wangu wa kutaka sera ya hifadhi ya jamii kwa wakulima kupitia vikundi vyao na ushirika. Nimesisitiza umuhimu wa kuweka akiba ili kuongeza uwekezaji wa ndani na hasa uwekezaji wa miundombinu ya kilimo. Nimeonya tabia ya wananchi kukimbilia kulipwa fidia badala ya kutaka kushiriki katika miradi mikubwa ya kilimo. Kilimo endelevu ni kilimo cha wakulima wadogo wanapata huduma pamoja (integrated production schemes) badala ya wakulima wakubwa wenye kuhitaji manamba. ‘outgrower’s schemes’ ndio mwelekeo sahihi kuwafanya wananchi wamiliki ardhi, wawe na ushirika imara, wawe na hifadhi ya jamii na waondokane na umasikini.

Leo nikiwa kijijini Choma na mjini Igunga nimewaambia wananchi umuhimu uwazi wa mapato ya viongozi wa umma. Nimewaambia kuwa mishahara ya viongozi wa umma haipaswi kuwa siri na inapaswa kukatwa kodi. Kama nilivyoahidi niliokuwa mjini Mpanda, nimewaambia kuwa mshahara wa Rais wa Tanzania ni Tshs 384m kwa mwaka. Kipato hiki hakikatwi kodi na Rais hupata huduma mbalimbali bure. Niliahidi kwamba kwa kuwa gazeti la Mwananchi lilifungiwa kwa sababu ya kutaja mishahara ya watumishi wa Serikali, basi ni vema kuonyesha Serikali kuwa lile sio kosa na wananchi wana haki ya kujua. Ndio maana nikachukua hatua ya kutaja kipato cha Waziri Mkuu na Rais.

Nimemaliza awamu ya kwanza ya ziara ya kanda ya Magharibi. Nimetembelea jumla ya kata 53 katika majimbo 10 ya uchaguzi ya mikoa ya Katavi na Tabora. Siku si nyingi nitamalizia majimbo ya Urambo na Kaliua kisha Mkoa wa Kigoma. Nimefarijika sana na mwitikio wa wananchi wanaotaka mabadiliko. Wazee kwa Vijana, kina mama kwa kina baba, wanataka mabadiliko.

Nimesononeshwa na kiwango cha umasikini wa wananchi na huduma mbovu za kijamii kama Maji, Elimu na Afya.

Nimeumizwa sana na unyonyaji mkubwa dhidi ya wakulima wa Pamba na Tumbaku.

Nimekasirishwa sana na ufisadi mkubwa wa fedha za umma kupitia mbolea ya ruzuku.

Nina Hofu kubwa ya wanasiasa wengi kutojua changamoto hizi za wananchi lakini wakitaka kupewa dhamana.

Nina Hofu na wanasiasa ‘manipulative’ lakini nina matumaini kuwa viongozi ‘inspirational’ watasimama kidete kushika usukani wa jahazi letu na kulifikisha salama. Tanzania ina kila sababu ya kuendelea, hatuna cha kupoteza isipokuwa minyororo ya umasikini.

Chukua hatua!

This slideshow requires JavaScript.

Written by zittokabwe

October 14, 2013 at 8:42 AM

Siku ya sita ya Ziara ya #CHADEMA imetufikisha Jimbo la Tabora Kaskazini

leave a comment »

Siku ya sita ya Ziara ya #CHADEMA imetufikisha Jimbo la Tabora Kaskazini.

Tumefanya mkutano wetu wa mwisho kijijini Mabama. Mkutano mkubwa sana na kuingia wanachama wengi sana. Kilio kikubwa cha wananchi ni Maji na unyonyaji katika zao la Tumbaku. Kuna haja kubwa sana ya kusukuma hifadhi ya jamii kwa wakulima. Tunaweza kukoboa wakulima wengi sana kutoka kwenye unyonyaji.
Ufisadi kwenye ngazi ya kijiji unatisha.

Umewahi kusikia jengo la matofari ya saruji linajengwa kwa tope?

#CHADEMA kanda ya Magharibi leo #Bukene. Kesho 12th Oct #Nzega na keshokutwa 13th #Igunga

This slideshow requires JavaScript.

Written by zittokabwe

October 11, 2013 at 12:32 PM

Ardhi, Maji na Ajira kuamua Ubunge Arumeru Mashariki

with 4 comments

Ardhi, Maji na Ajira kuamua Ubunge AruMeru Mashariki

“Uchaguzi wa Ubunge Arumeru Mashariki ni kipimo cha namna wananchi mnavyoridhika na watawala, namna mnavyoridhika na mgawo wa Ardhi na namna mnavyoridhika na mgawanyo wa Maji katika Wilaya yenu”. Haya yalikuwa baadhi ya maneno yangu katika hotuba ya kumkaribisha Mwenyekiti wa Taifa CHADEMA ndugu Freeman Mbowe kuzindua kampeni za chama chetu katika viwanja vya Leganga katika mji mdogo wa USA River wilayani Arumeru.

Siku moja kabla ya siku ya uzinduzi nilikuwa najisomea makala mbalimbali kuhusu Wilaya ya Arumeru. Pia nilitumia muda mrefu kuzungumza na wananchi wa Meru ili kujua uchaguzi huu una maana gani kwao. WaMeru wengi niliozungumza nao waliniambia namna wanavyochukizwa na ukosefu wa Ardhi kwa wananchi. Baadhi waliniambia kwamba Kama Serikali haitachukulia suala la Ardhi kwa uzito wake Meru kutatokea vurugu kubwa sana.

Vurugu Meru sio Jambo jipya kabisa. Inakumbukwa kwamba miaka ya 1950 kulitokea fujo na wananchi kuchomewa nyumba zao ili kupisha wakulima wakubwa kutoka Afrika Kusini (makaburu) katika eneo la Engarananyuki. Vurugu hizi ndio zilipelekea WaMeru kuchanga fedha kumpeleka ndugu Jafet Kirilo huko Umoja wa Mataifa kutetea Ardhi ya Wameru mwaka 1952 kufuatia vurugu za mwaka 1951. Licha ya juhudi hizo bado Ardhi ni tatizo kubwa kwa wananchi wa Meru.

Mashamba makubwa ambayo walipewa walowezi wakati wa Uhuru yaligawiwa kwa familia chache sana Meru. Wanasiasa walijipa mashamba makubwa na mengine mpaka Leo hayakugawiwa. Ujamaa na utaifishaji wa mashamba haukufanyika Meru kwa mshangao mkubwa sana na hata mashamba ambayo Serikali ya Mwalimu Nyerere iliagiza wapewe wananchi walipewa Wabunge, Madiwani, Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri (soma Brian Cooksey kuhusu uwekezaji katika Maua, June 2011).

Hivi Leo Ardhi kubwa ya Meru imeshikwa na matajiri na kulimwa Maua. Kilimo hiki cha Maua mwaka 2008 kiliingizia Taifa fedha za kigeni takribani tshs 150bn. Hata hivyo kuna malalamiko makubwa sana ya wananchi wanaofanya kazi katika mashamba haya kuhusu malipo duni na nyenzo za kufanyia kazi. Kuna malalamiko kuhusu kemikali na madawa yanayotumika na  afya ya mfanyakazi kutozingatiwa.

Ifahamike kwamba Benki ya Rasilimali Tanzania inasimamia mikopo ya zaidi ya tshs 50bn ambazo kampuni za Maua zilipewa kwa Dhamana ana ya Serikali. Katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, suala hili liliibuliwa na Mkurugenzi Mkuu wa TIB kukiri kwamba hakuna kampuni umeanza kulipa mikopo hii. Ni dhahiri Serikali itajikuta inalipa madeni haya yaliyokopeshwa kwa kampuni binafsi! Hii pia inaonyesha namna amabvyo serikali inafanya haraka na wepesi kusaidia wawekezaji kuliko wananchi wanaoteseka na kukosa Ardhi ya kulima na kujipatia ruziki.

Wawekezaji wanapewa Ardhi na mtaji!
Haya ndio yanajenga hasira ya wananchi wa Meru. Hasira hii kwa vyovyote itahamishiwa katika sanduku la kura ili kumpata Mbunge kutoka miongoni mwao atakayeweza kusimama kidete kuhakikisha Ardhi inapatikana kwa wananchi wa Meru. Kwa nini huko nyuma, katika chaguzi zilizopita Jambo hili halikuwapa hasira wananchi? Ni dhahiri hapakuwa na Mwanasiasa ambaye ana uwezo mkubwa wa kulieleza na kuwapa imani wananchi. Ndugu Joshua Nassari amedhihirisha kwamba analijua tatizo hili kwa dhati kabisa. Nilivyomsikiliza akiongea katika kampeni, na pia katika mazungumzo yetu binafsi amenithibitishia kuwa ni mwanasiasa kijana mwenye kipaji kikubwa katika kujenga hoja na ku articulate masuala ya msingi.
Changamoto nyingine kubwa kwa Meru ni haki ya kupata Maji. Meru kuna Maji mengi sana lakini matajiri wenye mashamba wameyazuia Maji hayo na hivyo wananchi wa kawaida hawapati Maji ya kumwagilia mazao Yao na pia kwa matumizi ya nyumbani. Hili nalo linajenga hasira kubwa sana kwa wananchi wa kawaida. Ardhi na Maji ni masuala yanayokwenda pamoja wilayani Meru.

Mwisho kabisa nimeona makundi ya vijana wasio na ajira na hivyo kukosa Kipato. Vijana wengi wanashinda kwenye stendi za mabasi na kuita abiria. Ukosefu wa Ajira kwa vijana Kama tusemavyo kila wakati ni changamoto kubwa sana kwetu viongozi na hasa viongozi vijana. Natumai ndugu Joshua Nassari atahusisha suala la Ardhi na Maji katika muktadha mzima wa Ajira na Kipato kwa wananchi wa Arumeru Mashariki. Uchaguzi wa Arumeru ni uchaguzi kati ya kuwa na Ardhi au kuendelea kutokuwa nayo. Ni uchaguzi muhimu kwa watu wa Meru. Wasio na Ardhi watamchagua mgombea atakayesimamia mgawo wa Ardhi unaozingatia haki. Mgombea huyo ni mgombea wa CHADEMA ndugu Joshua Nassari.

This slideshow requires JavaScript.

Written by zittokabwe

March 11, 2012 at 3:47 PM