Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Posts Tagged ‘uwajibikaji

Uwajibikaji, Changamoto na Uweledi wa Kamati ya PAC

with 5 comments

Uwajibikaji, Changamoto na Uweledi wa Kamati ya PAC

Mfumo thabiti wa Uwajibikaji ni moja ya jawabu muhimu sana katika kuhakikisha Taifa linaondokana na ufisadi na masuala mengine yanayorudisha nyuma maendeleo ya Tanzania. Kazi za mwisho za Kamati ya PAC katika Bunge la Kumi zilisheheni mambo mengi muhimu katika mchakato endelevu wa ujenzi wa mfumo thabiti wa uwajibikaji nchini kwetu.

Taarifa ya Mwaka iliyojadiliwa na kupitishwa na Bunge wiki iliyopita ndio ilikuwa taarifa yetu ya mwisho katika Bunge hili. Kama kawaida mwaka 2015 ulianza kwa ziara za kukagua miradi na hatimaye kukutana na maafisa masuuli wa Wizara na Mashirika ya Umma ili kukagua mahesabu yao na kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya wakaguzi na Kamati.

Kipindi hiki ni muhimu sana kwangu kwani kwa vyovyote vile ni kazi yangu ya mwisho kufanya kama Mwenyekiti wa PAC, nafasi niliyoichukua mwezi Machi mwaka 2013. Kabla ya hapo nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) kuanzia Februari mwaka 2008 mpaka Februari mwaka 2013. Katika Maisha yangu ya miaka 10 Bungeni, nimetumikia uongozi wa kamati hizi kwa miaka Saba na Nusu. Hata hivyo leo natafakari kazi ya wiki nne tu na nilichojifunza katika siku hizo.

Wiki ya Kwanza, tulitembelea miradi ya njia za Reli na Mashamba ya Miwa ili kuongeza uzalishaji wa Sukari nchini. Tulikwenda mkoani Morogoro katika Wilaya za Kilosa na Kilombero. Tulijulishwa kuhusu mahitaji ya fedha nyingi katika ujenzi wa Reli ya Kati ambapo ili kukarabati mtandao Reli iliyopo zinahitajika jumla ya shilingi 500 bilioni kwa miaka mitatu mfululizo ($800m). Vilevile zinahitajika dola za Kimarekani $6 bilioni kujenga reli mpya ya kisasa (standard gauge). Wiki mbili baada ya kumaliza ziara hiyo, niliona picha ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akikagua ujenzi wa Reli ya kisasa nchini humo. Nilipoangalia picha yangu na wajumbe wenzangu katika kijireli chetu, nilicheka kicheko cha huzuni sana. Nimejifunza kwamba nchi yetu inaweza kusonga mbele iwapo tu tutaamua kujinyima baadhi ya maeneo ili kuendelea kwenye maeneo mengine. Fedha inayopotea katika kutoa misamaha ya kodi (tshs 1.9 trilioni ) peke yake, kwa mwaka mmoja inamaliza ukarabati wa Reli yote ( Kigoma – Tabora – Dar es Salaam na Tabora – Mwanza ).

Wiki hiyo pia tulitembelea kiwanda cha Sukari cha Kilombero na kukutana na Wakulima wa Miwa. Tanzania ina nakisi ya Sukari ya takribani tani 120,000 – 200,000 kwa mwaka. Uzalishaji wa ndani wa tani 300,000 hautoshelezi mahitaji ya wananchi na hivyo twalazimika kuagiza Sukari kutoka nje ya nchi ambayo husamehewa kodi. Kwa mwaka Tanzania husamehe kodi ya zaidi ya shilingi 200 bilioni katika Sukari peke yake. Fedha hii ingeweza kujenga viwanda kadhaa vya Sukari na hivyo kuachana kabisa na uagizaji na badala yake kuuza nje. Nimejifunza mengi sana katika kushughulikia suala la Sukari nchini. Nimeona namna ambavyo mfumo mzima wa Serikali ulivyo na ganzi katika kupata suluhisho la kudumu. Hivi sasa Serikali inataka uagizaji wa Sukari ufanywe na wazalishaji wa Sukari, majawabu ya namna hii ni majawabu ya kugawana pato nyemelezi (rent seeking). Jawabu la kudumu la sekta ya Sukari ni kuongeza uzalishaji wa ndani kwa kufungua viwanda vipya maeneo yenye miwa ya ziada hivi sasa, kutoa ruzuku kwa viwanda ili kupunguza gharama za uzalishaji na hatimaye kuwa na bei nafuu kwa walaji na kufungua mashamba mapya ili kuzalisha ziada na kuuza nje kwa ajili ya kupata fedha za kigeni.

Tulijadili kwa kina sana changamoto zinazoikabili sekta ndogo ya kilimo cha Korosho. Ukaguzi Maalumu ulionyesha kuwa kuna unyonyaji mkubwa wa wakulima ikiwemo kupewa pembejeo zilizoisha muda na kutofikishiwa pembejeo kabisa. Pia upotevu mkubwa sana wa Korosho na suala zima la kuuza korosho ghafi nje ya nchi. Utafiti uliofanywa na African Cashew Alliance unaonyesha kuwa Tanzania hupoteza zaidi ya dola za kimarekani 110 milioni kila mwaka kwa kuuza korosho ambazo hazijabanguliwa. Ikumbukwe kuwa Tanzania ilikuwa na viwanda 12 vya kubangua Korosho na vyote viliuzwa katika zoezi la ubinafsishaji na sasa vimekuwa ni maghala ya kuhifadhia Korosho. Tulielekeza kuwa mapato yanayotokana na tozo ya mauzo ya Korosho nje (export levy) yatumike kujenga viwanda vipya vya korosho kwa kutumia teknolojia mpya kutoka Vietnam ambapo viwanda vidogo vidogo vitajengwa kuanzia vijijini na kuzalisha ajira nyingi na kuondoa umasikini. Nimejifunza kwamba Korosho peke yake inaweza kuingiza fedha za kigeni katika nchi yetu kwa thamani ya zaidi ya dola za kimarekani 500 milioni kwa mwaka. Mwaka 2014 Tanzania imezalisha tani 200,000 za Korosho, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa tangu tupate Uhuru. Korosho inaweza kuondoa umasikini kwa watu wa mikoa ya Kusini iwapo Viongozi wakiamua iwe hivyo.

Ilituchukua siku 2 kujadiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania kuhusu mahesabu yao ya mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2013. Sababu kubwa ilikuwa ni mjadala kuhusu misamaha ya Kodi. Kama nilivyoeleza hapo juu, tulijulishwa kuhusu misamaha mingi ya kodi kuendelea kutolewa mpaka kufikia jumla ya shilingi 1.9 trilioni katika mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2014. Kamati pia ilijadili Taarifa ya ukaguzi maalumu kuhusu misamaha ya kodi na kugundua kuwa misamaha mingi inatumika ndivyo sivyo. Nimejifunza kuwa tukiendelea kusisitiza uwazi na uwajibikaji tunaweza kupunguza tatizo hili la misamaha holela ya kodi. Tuliagiza kuwa kuanzia sasa, katika kila Taarifa ya makusanyo ya TRA kila mwezi, pia taarifa ya misamaha ya mwezi huo itolewe kwa umma. Hii itasaidia kuonyesha ni mapato kiasi gani yangeweza kukusanywa bila ya misamaha na kama misamaha hiyo ni muhimu na inatumika ipasavyo.

Mifano hii michache ya Reli, Sukari, Korosho na Misamaha ya Kodi imenikumbusha changamoto nyingi ambazo nchi yetu inazo na namna bora ya kukabiliana na Changamoto hizo. Mfumo thabiti wa Uwajibikaji ni suluhisho endelevu dhidi ya changamoto hizi. Kamati ya PAC imeshiriki kikamilifu kujenga mfumo huo. Kazi bado kubwa lakini inaendelea.

Zitto Zuberi Kabwe

Written by zittokabwe

February 4, 2015 at 3:45 PM

Azimio la Mtwara -Uwajibikaji katika Uvunaji wa Maliasili ya Nchi yetu

with 5 comments

Azimio la Mtwara

Uwajibikaji katika Uvunaji wa Maliasili ya Nchi yetu.

"Azimio la Mtwara" tarehe 31-12-2014 Zitto Kabwe na Prof. Ibrahim Lipumba

“Azimio la Mtwara” tarehe 31-12-2014 Zitto Kabwe na Prof. Ibrahim Lipumba

Tanzania kama zilivyo nchi nyingi za bara la Afrika imejaaliwa kuwa na Rasilimali mbali mbali za asili. Miongoni mwa rasilimali hizo ni pamoja na Madini na Gesi Asilia. Usimamizi wa uvunaji wa rasilimali hizi umegubikwa na manung’uniko makubwa ya wananchi hususan kutokana na usiri mkubwa uliopo kwenye mikataba ya uvunaji wa Maliasili hizi za Taifa. Mikataba yote 6 ya uvunaji wa Dhahabu bado ni Siri kubwa na vile vile mikataba yote 26 ya utafutaji na uvunaji wa Gesi Asilia na Mafuta. Mikataba miwili imevuja mpaka sasa na yote imeonyesha tofauti kubwa sana na mikataba ya mfano ambayo Serikali imeweka wazi. Mikataba ya mfano hutumika kujadiliana na makampuni ya uwekezaji katika utafutaji na uchimbaji wa Gesi na Mafuta hapa nchini. Mageuzi katika sekta ndogo ya gesi na mafuta yamekuwa hayashirikishi wananchi na hufanywa kwa usiri mkubwa na hivyo kusababisha wananchi kutokuwa na taarifa kabisa na kinachoendelea katika utajiri wao wa asili.

Mwaka 2007 nilitangaza Azimio la Songea lililokuwa na malengo makuu manne

1) kutokuwa na mikataba mipya ya madini mpaka mikataba iliyokuwepo ipitiwe. Mikataba yote ya madini ilipitiwa na Kamati ya Bomani na tangu mwaka 2007 hapajawa na mkataba Mpya wa madini ulioingiwa na Serikali.

2) kufanya mabadiliko ya sheria zote za kodi ambazo ni kikwazo katika kukusanya kodi katika sekta ya madini. Sheria husika zimefanyiwa marekebisho ikiwemo kupandisha mrahaba, kufuta nafuu ya kodi ya ongezeko la thamani kwa kampuni za madini na kuirejesha kodi ya ongezeko la mtaji.

3) Serikali kumiliki sehemu ya hisa katika migodi ya madini. Kwa mujibu wa sera Mpya ya madini ya mwaka 2009 na sheria Mpya ya madini ya mwaka 2010 Serikali itakuwa na hisa katika kila mgodi Mpya unaoanza nchini.

4) Halmashauri za Wilaya zenye migodi kupata mgawo wa theluthi ya mrahaba unaokusanywa katika madini yanayovunwa nchini. Pamoja na kwamba hivi sasa Halmashauri zinakusanya kodi ya ‘ cess’ lakini bado Serikali Kuu inabeba fedha yote ya mrahaba.

Malengo haya yaliongoza mjadala wa masuala ya madini mwaka 2007 mpaka 2010 sheria Mpya ya madini ilipotungwa. Utekelezaji wa Azimio la Songea ni wa zaidi ya 75% lakini bado kilio cha wananchi kipo pale pale. Hii inatokana na usiri mkubwa wa mikataba na hususan mikataba ya gesi na miundombinu yake. Usiri huu unasababisha ukosefu mkubwa wa uwajibikaji kwa upande wa watendaji wa Serikali. Usiri hupelekea rushwa na ufisadi. Moja ya sababu kubwa zinazotolewa na watetezi wa usiri wa mikataba ni kwamba mikataba ile ina Siri za kibiashara na hivyo washindani wa kibiashara wataiba Siri za wenzao. Hoja hii ni nyepesi sana kwani makampuni yote makubwa yanayowekeza nchini yamesajiliwa katika masoko ya hisa kwenye nchi za magharibi na katika masoko hayo mikataba yao hulazimika kuwekwa wazi. Hivyo usiri huo ni kwa wananchi tu na sio kwa hao washindani. Makampuni mengi yaliyopo nchini yanamilikiwa na watu wale wale kupitia masoko ya hisa. Vile vile majirani zetu kama Msumbiji wameweka mikataba yao yote wazi.

Ni dhahiri kwamba moja ya sababu kubwa ya kushamiri kwa rushwa nchini kwetu ni ukosefu wa mfumo thabiti wa uwajibikaji. Ndio maana katika mkutano wa kufunga mwaka 2014 na kuukaribisha mwaka 2015 uliofanyika mjini Mtwara tarehe 31 Desemba 2014, niliwaomba wananchi wa Mtwara kuufanya mwaka 2015 kuwa ni mwaka wa kuwajibishana. Hivyo Azimio la Mtwara ni wito wa kutaka Uwazi na Uwajibikaji katika utafutaji na uvunaji wa mali asili za nchi yetu. Azimio la Mtwara lina malengo yafuatayo

1 kutaka mikataba yote inayohusu uvunaji wa rasilimali za nchi iwekwe wazi kwa wananchi na Bunge liipitie kuidhia kabla ya kuingiwa kwa mikataba hiyo

2 kutaka haki ya wananchi kuruhusu utafutaji wa madini au gesi na mafuta katika maeneo yao ( right of free prior informed consent )

3 kutaka sehemu ya mrahaba unaotokana na uvunaji wa Maliasili ya nchi kugawanywa kwa maeneo yanayovunwa rasimali hizo

4 kutaka mfumo wa mapato na matumizi ya mapato yasiyo ya kikodi ( rents ) yanayotokana na uvunaji wa Maliasili za nchi kuwa wazi kwa wananchi na kushirikisha wananchi katika kupanga matumizi husika kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo

Azimio hili ni wito tu utakaotusaidia kuiwajibisha Serikali katika masuala ya utajiri wa Taifa.

Zitto Kabwe, Mb

Mtwara 31-12-2014

Mada yangu kwenye mafunzo ya Kamati za Mahesabu #PAC #Uwajibikaji #denilataifa #utoroshajiwafedha

leave a comment »

Leo tumeanza Mafunzo ya kamati za Bunge zinazosimamia fedha za Umma na Bajeti (PAC, LAAC, BC) kuhusu Uwajibikaji, Rushwa, Deni la Taifa na Utoroshaji wa fedha (illicit money transfer) hapa Bagamoyo.  Wiki yote hii.

Mada yangu kwenye mafunzo ya Kamati za Mahesabu niliyotoa asubuhi hii.

View this document on Scribd

Maandamano dhidi ya Bomba la Gesi: Kilio cha Uwajibikaji

with 24 comments

Maandamano dhidi ya Bomba la Gesi: Kilio cha Uwajibikaji

Maandamano dhidi ya Bomba la GesiPicha Hisani ya: Mtwara Kumekucha Blog by Baraka Mfunguo

Maandamano dhidi ya Bomba la Gesi
Picha Hisani ya: Mtwara Kumekucha Blog by Baraka Mfunguo

‘Dar inachangia asilimia 80 ya mapato. Kitovu cha Uchumi. Dar inachangia 90% ya ufisadi. Uti wa mgongo wa ufisadi nchini’

Malumbano kati ya wananchi wa Mtwara na Serikali kuhusu matumizi bora ya utajiri wa nchi yameendelea kwa takribani wiki moja sasa. Baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara na Waziri wa Nishati na Madini kuwaita Watanzania wa Mtwara Wahaini, wapuuzi na watu hatari, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naye aliingia kwenye mjadala huo kwa kuonya watu wanaowaunga mkono watu wa Mtwara na kuwaita watu wanaotafuta umaarufu wa kisiasa na wanaotaka kugawa nchi. Siku moja baada ya hotuba ya Rais, Waziri wa Nishati na Madini alifanya mkutano na waandishi wa habari kueleza suala lile lile ambalo bosi wake alilielezea usiku wa kuamkia mwaka mpya 2013. Hii ni dalili ya Serikali kuweweseka.

Katika kauli ya Serikali, ambayo haikuwa na jipya zaidi ya wimbo ule ule wa ‘kugawa nchi’ ‘umaarufu wa kisiasa’ nk, Serikali ilitaka kuonyesha umma kuwa watu wa Mtwara hawana shukurani. Kwamba miaka yote toka Uhuru watu wa Mtwara wamekuwa wakilishwa na Pamba, Kahawa, Chai, Tumbaku, Sukari, Kidatu nk. Kwamba watu wa Mtwara na Lindi hawakuchangia hata kidogo kwenye hazina ya Taifa. Hivyo wao kupigia kelele gesi yao ni uchoyo na roho mbaya na kukosa shukurani. Kauli ya Serikali ni kauli ya chombo kinachoendelea kukosa ‘legitimacy’ ya kuongoza taifa. Ni kauli ya kukata tamaa. Ni kauli hatari sana dhidi ya Watanzania waliojitolea damu kulinda uhuru wa nchi yetu.

Moja, Serikali katika kauli yake haitaji kabisa kwamba toka Uhuru watu wa Mtwara na Lindi wamekuwa wachangiaji wakubwa sana katika uchumi wa Taifa kupitia zao la Korosho. Takwimu za Uzalishaji wa Korosho zinaonyesha kwamba kuanzia mwaka 1965 mpaka 2011 Korosho imeliingizia Taifa fedha kigeni jumla ya dola za Kimarekani 4.58 bilioni ( Cashewnuts Sub-sector study 2003, Hali ya Uchumi 2012, Cashewnuts Tanzania Report 2010). Katika Mwaka wa Uchumi unaoishia Novemba 2012, Korosho imeliingizia Taifa jumla ya dola za Kimarekani 151 milioni. Katika mwaka 2011 zao hili liliingiza dola 130 milioni wakati Pamba iliingiza dola 53 milioni tu. Licha ya Zao la Korosho kuingiza fedha hizi za kigeni  (sawa ni shilingi trilioni 7.2) kwa nchi mikoa ya Lindi na Mtwara ipo miaka 50 nyuma kimaendeleo kulinganisha na mikoa mingine ya Tanzania. Serikali inataka kufuta historia ya mchango wa zao la Korosho kwenye uchumi wa nchi yetu kwa sababu ya uroho wa gesi asilia. Kwa nini kauli rasmi ya Serikali haijataja Korosho kabisa? Kauli hii ilipitishwa na ngazi zote za Serikali? Mawaziri wa Serikali wanaotoka mikoa ya Lindi na Mtwara walikubali kauli kama hii itoke dhidi ya wananchi wao wanaoteseka na zao la Korosho miaka nenda miaka rudi?

Pili, Serikali imesahau kabisa mchango wa watu wa Lindi na Mtwara katika ulinzi wa Taifa letu. Moja ya sababu ya mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa nyuma kimaendeleo ni juhudi za ukombozi wa kusini mwa Afrika. Kambi ya wapigania uhuru wa Msumbiji ilikuwa Nachingwea. Kambi ya Frelimo iliwekwa kwenye Shamba la Mkonge kilometa 17 tu kutoka mjini Nachingwea ambapo ilikuwa makao makuu ya ukombozi wa Msumbiji. Rais Samora Machel, Rais Joaqim Chissano na Rais Guebuza waliendesha mapambano kutoka kusini mwa Tanzania. Makaburu wa Afrika Kusini na Wareno walikuwa wanashambulia nchi yetu na mikoa hii miwili ya Lindi na Mtwara ikawa ‘buffer zone’. Wakati Dar es Salaam inaendelea kwa kila aina ya maendeleo, mikoa ya Lindi na Mtwara ilikuwa inalinda ili wanaoishi Dar es Salaam na mikoa mingine waishi wa amani na starehe. Serikali inapimaje mchango huu wa mikoa hii? Tunaipima kwa fedha? Uroho wa gesi asilia kuzalisha umeme wa kufurahisha walalaheri asilimia 14 nchini ndio inaifanya Serikali kusahau kabisa ‘sacrifice’ ya watu wa Mtwara katika kulinda uhuru wa Taifa letu?

Tatu, Serikali inasema lazima bomba lije Dar es Salaam kwa sababu Dar ndio inazalisha asilimia 80 ya Mapato ya Serikali. Kwanza huu ni uwongo. Ni aibu Serikali kujitetea kwa uwongo. Dar es Salaam ni kituo tu cha kukusanyia mapato ya Serikali. Uzalishaji mkubwa wa nchi yetu wenye kuzalisha kodi unafanyika nje ya Dar es Salaam. Walipa kodi wakubwa wengi Ofisi zao Kuu zipo Dar es Salaam lakini uzalishaji wao unafanyika nje ya Dar es Salaam. Serikali itoe orodha ya walipa kodi wakubwa 100 tuone uzalishaji halisi wa mapato hayo unafanyika wapi. Hata hivyo inawezekana kuwa ikawa kweli Dar es Salaam inakusanya asilimia 80 ya mapato ya nchi. Basi na tuseme Dar es Salaam inachangia asilimia 90 ya ufisadi wote nchini. Kashfa zote kubwa za Ufisadi zinafanyika Dar es Salaam na fedha nyingi za ufisadi zinatumika Dar es Salaam.

Mwisho, maandamano ya watu wa Mtwara ni kielelezo tosha kwamba watu wa mikoa ya Lindi na Mtwara wamechoshwa na longolongo za Serikali. Wananchi wa Mtwara na Lindi wanataka Uwajibikaji wa Serikali kuhusu utajiri wa nchi. Mtanzania yeyote mwenye tahadhari ya nchi yetu kutokuwa na laana ya rasilimali ataungana mkono na watu wa Lindi na Mtwara kudai maendeleo. Nilitoa mfano wa Mgodi wa Golden Pride ambao umemaliza dhahabu yote tani 76 katika eneo la Lusu wilayani Nzega. Kampuni ya Resolute ya Australia iliwekeza dola 370 milioni kuanzia mwaka 1998 (mkataba wao ulisainiwa 25th June 1997). Katika kipindi cha uhai wa mgodi, miaka 14,  Kampuni hii imeuza dhahabu ya thamani ya dola za kimarekani 3.3 bilioni. Kabla Serikali haijawaita watu Mtwara wahaini, wapuuzi na watu hatari, iwaambie watu Watanzania kodi kiasi gani imekusanywa kutoka mgodi huu katika kipindi cha miaka 14. Mpaka mwaka 2008, kwa mujibu wa Taarifa ya Kamati ya Bomani, kampuni hii ilikuwa imelipa mrahaba wa dola 11 milioni na kodi nyingine dola 16 milioni. Serikali itwambie ilipofika Disemba 2012 kodi kiasi imekusanywa kutoka kampuni hii?

Pia watu wa Mtwara na Lindi wameona historia ya bomba la Songosongo. Hata kodi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa (0.3%) ilikuwa inalipwa Halmashauri ya Manispaa Ilala na kampuni ya Pan Africa Energy. Ilichukua juhudi za mbunge wa Kilwa Kaskazini Murtaza Mangungu kuingilia kati ndio kodi ikaanza kulipwa Kilwa ambapo uzalishaji unafanyika. Watu wa Mtwara ni werevu, wanajua wafanyalo. Wanataka utajiri wa nchi unufaishe nchi kwa kuanzia kule utajiri ulipo. Kuna dhambi gani?

Uwajibikaji katika uvunaji wa Rasilimali ya Gesi ndio chanzo cha maandamano ya watu wa Mtwara. Serikali isikimbilie kulaumu wanasiasa kwamba ndio wamechochea maandamano haya. Haya ni maandamno ya wananchi wakitaka Serikali yao iwajibike kwao. Serikali ithubutu kufanya ubabe wa kujenga bomba la gesi bila ridhaa ya Wananchi wa Lindi na Mtwara. Wananchi wanapohitaji uwajibikaji ni wajibu wa Serikali kuwajibika kwao ni sio kuwaita wahaini, wachochezi, watu hatari, wapuuzi. Watu wa Mtwara wamechangia maendeleo ya Taifa letu kwa jasho na damu. Serikali ina wajibu wa kuwasikiliza, kuwaelimisha na kupata mwafaka. Kauli ya Serikali imewatukana watu wa Mtwara na Lindi. Hawatakubali kudhalilishwa. Hawatakubali historia yao kufutwa. Hawatakubali waendelee kubaki nyuma kimaendeleo. Serikali ifikirie tena.

Written by zittokabwe

January 3, 2013 at 2:10 PM

ONE WORD: Uwajibikaji/Accountability

with 6 comments

Nikiwatania wabunge wa CCM kufuatia habari za Mawaziri Nane(8) kuwajibika kwa kujiuzulu nafasi zao

Nikiwatania wabunge wa CCM kufuatia habari za Mawaziri Nane(8) kuwajibika kwa kujiuzulu nafasi zao.
Teasing CCM Mps about news of 8 Ministers resigning on accountability grounds.

Written by zittokabwe

April 22, 2012 at 11:34 AM