Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Posts Tagged ‘Wizara ya Ujenzi

Tamko la Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo ndg. Zitto Kabwe kuhusu Ripoti ya CAG mwaka 2013/2014

with 7 comments

Tamko la Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo ndg. Zitto Kabwe kuhusu Ripoti ya CAG mwaka 2013/2014

1) Taarifa nyingine ya CAG imetoka, kwa mujibu wa Katiba ya JMT na kwa mujibu wa sheria za nchi. Taarifa hii imechelewa kutolewa kulingana na mabadiliko ya Ratiba za Bunge ambapo hapo awali taarifa ilikuwa ikitoka mwezi Aprili na kuwezesha kuchangia katika mchakato wa Bajeti ya nchi. Taarifa ya mwaka huu na ile ya mwaka Jana imetoka wakati wa Bunge la Bajeti na hivyo Bajeti ya Serikali haijazingatia hoja za ukaguzi ili kuboresha mfumo wa matumizi ya fedha za umma. Ni vema utaratibu wa zamani wa ripoti kutolewa mwezi Aprili urejewe ili wabunge waweze kutumia ripoti hizo wakati wa kamati katika kujadili makadirio ya Bajeti za Wizara mbalimbali.

2) Taarifa kama miaka iliyopita bado sio nzuri. Mapato mengi ya Serikali bado yanapotea. Uk. 53 wa Taarifa unaonyesha kuwa mizigo inayoingizwa nchini kupita kwenda nchi jirani zinazotumia bandari zetu hubakia nchini na kuingizwa sokoni hivyo kukwepa kodi. Mwaka 2013/2014 mizigo ya transit iliyobaki nchini kiudanganyifu ilikuwa zaidi ya bidhaa 6000 kwa mujibu wa Taarifa ya CAG. Hivyo kodi ya tshs 836 bilioni haikulipwa kwa mizigo hiyo sawa sawa na 10% ya makusanyo yote ya kodi za ndani. Tshs 836 bilioni ilipotea mwaka 2013/14 peke yake. Wakati hili linatokea Serikali ipo ukata mkubwa na kushindwa kuendesha miradi yake mbalimbali. Fedha iliyokwepwa idara ya forodha peke yake inalipa Madeni yote ya wakandarasi wa barabara wanaoidai TANROADS na riba kulimbikizwa kila mwaka. Fedha hii ingelipa Madeni yote ya mfuko wa PSPF wanayoidai Serikali. Fedha hizi zingeweza kulipia miradi 2 mikubwa nchini ya BVR na vitambulisho vya Taifa ambayo inasuasua kutokana na ukata.

Natoa wito kwa CAG kwanza kuweka wazi orodha ya bidhaa hizo zilizobakia nchini na kuingizwa nchini bila kulipa kodi. Vile vile CAG aweke wazi wafanyabiashara wote walioagiza bidhaa hizi na vyombo vya kiuchunguzi vichukue hatua za kuwashtaki wafanya biashara hawa mara moja.

Natoa wito kwa Kamati ya Bunge ya PAC kuwaita mara moja maafisa wa TRA kujieleza mbele ya kamati kuhusu suala hili na kuandaa taarifa maalumu bungeni ili kuanika uoza huu unaopoteza mapato mengi sana ya Serikali.

3) CAG kaonyesha kuwa kuna ubadhirifu mkubwa sana kitengo cha maafa cha ofisi ya Waziri Mkuu ambapo tshs 163 billioni za chakula cha maafa hazikukusanywa katika kipindi cha miaka 5 iliyopita. Huu ni kama mrija wenye wastani wa tshs 32 bilioni kuchotwa kwa kisingizio cha chakula cha maafa kwa wananchi. Kwa malezo ya CAG ni kwamba Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wamekula fedha za chakula cha misaada. Maana hakuna uthibitisho wa kuwa mahindi yaliyogawanywa na taarifa kutolewa na Wakala wa Akiba ya Chakula (NFRA). Kitengo cha maafa ofisi ya PM kimekuwa mrija wa wizi wa fedha za umma, wizi ambao umekuwa ukifanyika bila ya kugunduliwa kwa miaka 5 sasa. ACT Wazalendo inaisihi Kamati ya Bunge ya PAC kufanya uchunguzi maalumu kwenye kashfa hii ya tshs 163 bilioni katika Ofisi ya Waziri Mkuu na Wakala wa Hifadhi ya Chakula ( NFRA).

4) ACT Wazalendo inalitaka Bunge kuchukua stahiki dhidi ya Wizara ya Ujenzi kufuatia ripoti ya CAG kuonyesha kuwa Wizara ilidanganya Bunge katika kupitisha Bajeti ya tshs 252 bilioni ambapo kati yake tshs 87 bilioni ziliibiwa au matumizi yake kutoeleweka.

5) ACT Wazalendo inampongeza CAG kwa kuendelea na zoezi la kisheria la kukagua mahesabu ya vyama vya siasa. Hii inaweka misingi ya uwajibikaji kuanzia kwenye vyama vya siasa, taasisi muhimu sana katika ujenzi wa demokrasia. Vyama vya siasa vichukulie ripoti ya CAG kama changamoto ya kutoa kwanza kibanzi kwenye macho yao ili kuwa na ‘ moral standing’ ya kupambana dhidi ya ubadhirifu wa fedha za umma nchini.

Zitto Kabwe

Kiongozi wa Chama ACT Wazalendo

 

 

RATIBA YA PAC KUJADILI HESABU ZILIZOKAGULIWA ZA SERIKALI KUU NA MASHIRIKA YA UMMA

leave a comment »

Uchambuzi/Analysis: Bajeti ya Madeni

with 20 comments

Bajeti ya Mwaka huu 2012/2013 ni Bajeti ya Madeni

Serikali inapendekeza Bajeti ya TZS 15 trilioni(USD 8.75 Billion) katika mwaka 2012/13. Uchambuzi wa vitabu vya Bajeti unaonesha kwamba mafungu ya juu 5 kwenye Bajeti ni Kama ifuatavyo;

1    Huduma kwa Deni la Taifa          Tshs 2.7 trilioni(USD 1.69 Billion)
2    Wizara ya Ujenzi.                          Tshs 1 trilioni (USD 625 Million)
3    Wizara ya Ulinzi                          Tshs 920 bilioni (USD 575 Million)
4    Wizara ya Elimu                              Tshs 721 bilioni (USD 451 Million)
5    Wizara ya Nishati na Madini    Tshs 641 bilioni (USD 400 Million)
 TOTAL                                        TZS 5.982 Trilioni(USD 3.74 Billlion)
Chanzo: Vitabu vya Bajeti kwa Wabunge

Jumla ya mafungu haya ni sawa na asilimia 40% ya Bajeti. Kwa hiyo asilimia 40% ya Bajeti yote imepangwa kwa mafungu 5 tu. Fungu lenye kiwango kikubwa zaidi ya Bajeti kuliko vyote ni fungu 22 ambalo ni malipo kwa Deni la  Taifa. Pia sehemu kubwa ya fedha zilizotengwa kwa Ujenzi na Nishati ni madeni kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya miaka ya nyuma.

Hii yaweza kuwa Bajeti ya kulipa madeni zaidi kuliko Bajeti ya kuchochea maendeleo. Bajeti hii pia yaweza pia kuwa ni Bajeti ya kukopa maana jumla ya TZS 5.1 trilioni(USD 3.19 Billion) zitachukuliwa kama mikopo kwa Serikali. Mikopo ya kibiashara ambayo ni mikopo ghali sana itachukuliwa kwa wingi zaidi kuliko mwaka wa fedha uliopita.

Wabunge wanapaswa kufanya uchambuzi zaidi wa Bajeti ya mwaka huu inayopendekezwa na Serikali. Kuna haja kubwa sana ya kuharakisha kuanzishwa kwa Ofisi ya Bajeti katika Bunge na Kamati ya Bunge ya Bajeti ili kuweza kufuatilia kwa karibu, kuchunguza na kutoa taarifa kwa wabunge ili kuwezesha kuboresha Bajeti.

Misamaha yote ya Kodi na Madeni yote ambayo Serikali inaingia inabidi sasa ithibitishwe na Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi ili kuongeza udhibiti na usimamizi wa Misamaha ya Kodi na pia Deni la Taifa.