Uwajibikaji, Changamoto na Uweledi wa Kamati ya PAC
Uwajibikaji, Changamoto na Uweledi wa Kamati ya PAC
Mfumo thabiti wa Uwajibikaji ni moja ya jawabu muhimu sana katika kuhakikisha Taifa linaondokana na ufisadi na masuala mengine yanayorudisha nyuma maendeleo ya Tanzania. Kazi za mwisho za Kamati ya PAC katika Bunge la Kumi zilisheheni mambo mengi muhimu katika mchakato endelevu wa ujenzi wa mfumo thabiti wa uwajibikaji nchini kwetu.
Taarifa ya Mwaka iliyojadiliwa na kupitishwa na Bunge wiki iliyopita ndio ilikuwa taarifa yetu ya mwisho katika Bunge hili. Kama kawaida mwaka 2015 ulianza kwa ziara za kukagua miradi na hatimaye kukutana na maafisa masuuli wa Wizara na Mashirika ya Umma ili kukagua mahesabu yao na kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya wakaguzi na Kamati.
Kipindi hiki ni muhimu sana kwangu kwani kwa vyovyote vile ni kazi yangu ya mwisho kufanya kama Mwenyekiti wa PAC, nafasi niliyoichukua mwezi Machi mwaka 2013. Kabla ya hapo nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) kuanzia Februari mwaka 2008 mpaka Februari mwaka 2013. Katika Maisha yangu ya miaka 10 Bungeni, nimetumikia uongozi wa kamati hizi kwa miaka Saba na Nusu. Hata hivyo leo natafakari kazi ya wiki nne tu na nilichojifunza katika siku hizo.
Wiki ya Kwanza, tulitembelea miradi ya njia za Reli na Mashamba ya Miwa ili kuongeza uzalishaji wa Sukari nchini. Tulikwenda mkoani Morogoro katika Wilaya za Kilosa na Kilombero. Tulijulishwa kuhusu mahitaji ya fedha nyingi katika ujenzi wa Reli ya Kati ambapo ili kukarabati mtandao Reli iliyopo zinahitajika jumla ya shilingi 500 bilioni kwa miaka mitatu mfululizo ($800m). Vilevile zinahitajika dola za Kimarekani $6 bilioni kujenga reli mpya ya kisasa (standard gauge). Wiki mbili baada ya kumaliza ziara hiyo, niliona picha ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akikagua ujenzi wa Reli ya kisasa nchini humo. Nilipoangalia picha yangu na wajumbe wenzangu katika kijireli chetu, nilicheka kicheko cha huzuni sana. Nimejifunza kwamba nchi yetu inaweza kusonga mbele iwapo tu tutaamua kujinyima baadhi ya maeneo ili kuendelea kwenye maeneo mengine. Fedha inayopotea katika kutoa misamaha ya kodi (tshs 1.9 trilioni ) peke yake, kwa mwaka mmoja inamaliza ukarabati wa Reli yote ( Kigoma – Tabora – Dar es Salaam na Tabora – Mwanza ).
Wiki hiyo pia tulitembelea kiwanda cha Sukari cha Kilombero na kukutana na Wakulima wa Miwa. Tanzania ina nakisi ya Sukari ya takribani tani 120,000 – 200,000 kwa mwaka. Uzalishaji wa ndani wa tani 300,000 hautoshelezi mahitaji ya wananchi na hivyo twalazimika kuagiza Sukari kutoka nje ya nchi ambayo husamehewa kodi. Kwa mwaka Tanzania husamehe kodi ya zaidi ya shilingi 200 bilioni katika Sukari peke yake. Fedha hii ingeweza kujenga viwanda kadhaa vya Sukari na hivyo kuachana kabisa na uagizaji na badala yake kuuza nje. Nimejifunza mengi sana katika kushughulikia suala la Sukari nchini. Nimeona namna ambavyo mfumo mzima wa Serikali ulivyo na ganzi katika kupata suluhisho la kudumu. Hivi sasa Serikali inataka uagizaji wa Sukari ufanywe na wazalishaji wa Sukari, majawabu ya namna hii ni majawabu ya kugawana pato nyemelezi (rent seeking). Jawabu la kudumu la sekta ya Sukari ni kuongeza uzalishaji wa ndani kwa kufungua viwanda vipya maeneo yenye miwa ya ziada hivi sasa, kutoa ruzuku kwa viwanda ili kupunguza gharama za uzalishaji na hatimaye kuwa na bei nafuu kwa walaji na kufungua mashamba mapya ili kuzalisha ziada na kuuza nje kwa ajili ya kupata fedha za kigeni.
Tulijadili kwa kina sana changamoto zinazoikabili sekta ndogo ya kilimo cha Korosho. Ukaguzi Maalumu ulionyesha kuwa kuna unyonyaji mkubwa wa wakulima ikiwemo kupewa pembejeo zilizoisha muda na kutofikishiwa pembejeo kabisa. Pia upotevu mkubwa sana wa Korosho na suala zima la kuuza korosho ghafi nje ya nchi. Utafiti uliofanywa na African Cashew Alliance unaonyesha kuwa Tanzania hupoteza zaidi ya dola za kimarekani 110 milioni kila mwaka kwa kuuza korosho ambazo hazijabanguliwa. Ikumbukwe kuwa Tanzania ilikuwa na viwanda 12 vya kubangua Korosho na vyote viliuzwa katika zoezi la ubinafsishaji na sasa vimekuwa ni maghala ya kuhifadhia Korosho. Tulielekeza kuwa mapato yanayotokana na tozo ya mauzo ya Korosho nje (export levy) yatumike kujenga viwanda vipya vya korosho kwa kutumia teknolojia mpya kutoka Vietnam ambapo viwanda vidogo vidogo vitajengwa kuanzia vijijini na kuzalisha ajira nyingi na kuondoa umasikini. Nimejifunza kwamba Korosho peke yake inaweza kuingiza fedha za kigeni katika nchi yetu kwa thamani ya zaidi ya dola za kimarekani 500 milioni kwa mwaka. Mwaka 2014 Tanzania imezalisha tani 200,000 za Korosho, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa tangu tupate Uhuru. Korosho inaweza kuondoa umasikini kwa watu wa mikoa ya Kusini iwapo Viongozi wakiamua iwe hivyo.
Ilituchukua siku 2 kujadiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania kuhusu mahesabu yao ya mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2013. Sababu kubwa ilikuwa ni mjadala kuhusu misamaha ya Kodi. Kama nilivyoeleza hapo juu, tulijulishwa kuhusu misamaha mingi ya kodi kuendelea kutolewa mpaka kufikia jumla ya shilingi 1.9 trilioni katika mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2014. Kamati pia ilijadili Taarifa ya ukaguzi maalumu kuhusu misamaha ya kodi na kugundua kuwa misamaha mingi inatumika ndivyo sivyo. Nimejifunza kuwa tukiendelea kusisitiza uwazi na uwajibikaji tunaweza kupunguza tatizo hili la misamaha holela ya kodi. Tuliagiza kuwa kuanzia sasa, katika kila Taarifa ya makusanyo ya TRA kila mwezi, pia taarifa ya misamaha ya mwezi huo itolewe kwa umma. Hii itasaidia kuonyesha ni mapato kiasi gani yangeweza kukusanywa bila ya misamaha na kama misamaha hiyo ni muhimu na inatumika ipasavyo.
Mifano hii michache ya Reli, Sukari, Korosho na Misamaha ya Kodi imenikumbusha changamoto nyingi ambazo nchi yetu inazo na namna bora ya kukabiliana na Changamoto hizo. Mfumo thabiti wa Uwajibikaji ni suluhisho endelevu dhidi ya changamoto hizi. Kamati ya PAC imeshiriki kikamilifu kujenga mfumo huo. Kazi bado kubwa lakini inaendelea.
Zitto Zuberi Kabwe
Hongera kwa Ripoti nzuri na mapendekezo safi ya PAC kwa Serikali.
Mchango wangu ni kwa hili la Korosho.Nakubaliana nawe na Kamati kwa ujumla.Kuwe na juhudi za dhati za kuhakikisha kuwa kunauza korosho zilizobanguliwa na kwa kufanya hivyo umaskini kwa mkulima unaweza kupungua na mapato kwa serikali yatakuwa makubwa.
pia Bodi ya korosho ma Mfuko wa wakfu wa kotosho kuna ubadhilifu mkubwa unaofanyika kutokana na mfumo na muundo wake. Bodi haimpi tija mkulima kwa kiwango tarajiwa next time muangalie hilo kwa undani wake mtabaini madudu
Ally Mshamu
February 4, 2015 at 4:10 PM
Kwanza nipongeze uwepo wenu pia na kazi nzito mnayoifanya,kimsimgi kupitia kamati hiyo tunapata kujua mwenendo wa matumizi ya rasilimali fedha kwenye mashirika ya umma.
Chagulani
February 4, 2015 at 4:27 PM
get blessed brother# mungu hamtupi mtu mwenye dhamira ya dhati## Ulu muntu mwizaaa
Edson Salvatory
February 5, 2015 at 12:24 AM
Tafakari nzuri lakini bado.
Shida ni kwamba kila jibu linaanza na “tuli” kama vile PAC – ambao wote ni wanasiasa – ndio wenye majibu ya matatizo yote, mengi hakiwa ni ya kibiashara. Tatizo kubwa la Tanzania ni kwamba wanasiasa wanaingilia masuala ya biashara na hapo ndipo suala la rent seeking linapojitokeza (mfano Tanesco,Air Tanzania nktk). Nchi kama Singapore na China zinatufundisha kwamba siasa isiingilie biashara.
Ticha
February 10, 2015 at 2:08 PM
kila la kheri ktk kutokomeza ufisadi 2po pamoja ila muende Tanga pale Handeni kuna vijiji kma mkata, komkonga, kabuku, kwamsisi, turiani, segera, kwedikwazu, kwachaga, handeni mjin nk ccm wana2tesa sna na upinzani wa chadema kule ni dhaifu sna jitahidin mfike mapema kule kabla ya uchaguz.
Miraji Jumaa
March 9, 2015 at 7:12 PM