Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Utajiri wa Gesi Asilia: Tuwasikilize Watanzania wa Mtwara na Lindi. Tusipuuze

with 15 comments

Utajiri wa Gesi Asilia: Tuwasikilize Watanzania wa Mtwara na Lindi. Tusipuuze

Maandamano ya amani yaliyofanyika mjini Mtwara siku ya alhamis wiki hii yameibua hoja mbali mbali kutoka kwa viongozi, wananchi, vyombo vya habari na mjadala wa siku nzima kwenye mitandao ya kijamii hasa facebook, twitter na JamiiForums. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ameita waandamanaji wapuuzi na Waziri wa Nishati na Madini amewaita watu hatari na wahaini. CHADEMA tumetoa kauli kupitia kwa Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwamba udhaifu wa utendaji serikalini ndio chanzo cha maandamano haya.

Lakini kuna tatizo kubwa zaidi ambalo linaonekana siyo katika sekta hii tu bali pia katika sekta nyingine ambapo tunaona matokeo yake katika maisha ya watu wetu na naweza kusema ni dalili za kushindikana kwa sera za CCM. Sera hizi ndizo ambazo zimelifikisha taifa hili hadi hapa. Kama hadi wananchi wa Mtwara ambako kwa muda mrefu imekuwa ni ngombe ya CCM wanaanza kuhoji matokeo ya sera za chama tawala basi ni dalili kuwa Watanzania wamefungua macho yao na wanaona.

Wanaona katika nishati, wanaona katika utawala bora, wanaona katia elimu (kuanzia ya msingi hadi ya juu kabisa!), wanaona katika afya, wanaona katika utendaji wa jeshi la polisi wanaona katika madini. Sera za CCM zimeshindwa. Zimeshindwa kuinua maisha yao na zinaonekana kuendelea kushindwa.

Mtwara na Lindi wanataka nini?

Watu wa Mtwara wanataka gesi isiondoke Mtwara na badala yake viwanda na mitambo ijengwe Mtwara kisha kama ni umeme au mbolea isafirishwe kupelekwa sehemu nyingine ya nchi. Watu wa Mtwara hawasemi kwamba Gesi yote na mazao yake vibaki Mtwara na Lindi. Wanasema umeme uzalishwe Mtwara usambazwe nchi nzima. Mbolea izalishwe Mtwara na kusambazwa nchi nzima. Wanataka Bandari ya Mtwara iboreshwe na kuhudumia mikoa ya Kusini. Watu wa Mtwara hawasemi kwamba mapato yote ya Gesi yatumike Mtwara tu la hasha.

Sio dhambi hata kidogo kwa watu wa Mtwara kudai masuala haya. Watu wa Mtwara wamefanya maandamano kwa amani kabisa bila kuharibu mali na kutoa maoni yao. Kwanini tuwasute na kuwasusubika kwa madai yao haya? Kwa nini tusiwasikilize? Kosa lao nini kudai viwanda ili wapate ajira? Tumesahau kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ni mikoa masikini kabisa nchini? Tumesahau kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ilitumika kwa ukombozi wa kusini mwa Afrika kiasi cha kuwa katika hatari kabisa? Tumesahau ‘sacrifice’ ya watu wa Mtwara na Lindi dhidi ya usalama wa nchi yetu? Tumesahau kuwa Korosho imekuwa zao kubwa la biashara na linaloingiza mapato mengi sana ya Fedha za kigeni? Waziri Muhongo anasema Mtwara warudishe Fedha za Mkonge na Kahawa. Mbona hataji fedha za Korosho? Mwaka 2011 Korosho ilikuwa zao la pili kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni baada ya Tumbaku.

Lakini tujiulize, watu wa Mtwara na Lindi walifadi fedha za Mkonge? Walifaidi fedha za Kahawa? Wamefaidi fedha zao za Korosho? Tumesahau hata Reli iliyoachwa na Mkoloni ya Nachingwea – Mtwara iling’olewa na Serikali huru ya Tanzania?

Tujiulize zaidi, hivi watu wa Nzega wamefaidika vipi na Mgodi wa Resolute pale Lusu? Mgodi umefungwa ukiwa umezalisha na kuuaza dhahabu ya thamani ya dola za marekani 3.3 bilioni. Hivi katika uhai wa mgodi huu Serikali Kuu imekusanya kodi kiasi gani? Halmashauri ya Wilaya ya Nzega imepata ushuru kiasi gani? Watu wa Mtwara wanayaona haya yaliyotokea Nzega na yanayotokea Tarime, Biharamulo, Kahama na Geita. Watu wa Mtwara wana Haki kuandamana kuzuia haya yaliyotokea wenzao yasiwatokee wao kwenye Gesi asilia.

Mtwara na Lindi wanakosea wapi?

Madai yao halali na mimi binafsi na chama changu tunayaunga mkono. Lakini kuna mahala lazima waelimishwe.

Watu wa Mtwara pia wanapaswa kuelewa kuwa juhudi zao zisiwatenganishe na Watanzania wengine kwani bado utajiri wa Taifa unafadisha kikundi cha Watanzania wachache sana. Watu wa Mtwara wanahitaji kuungana na watu wa Mara, watu wa Mwanza, watu wa Shinyanga na watu wa Kagera kudai utajiri wa nchi utumike kwa maendeleo ya watu badala ya kunufaisha kundi dogo la watu. Watu wa Mtwara wanapaswa kuunganisha nguvu na Watanzania wengine kuzuia uporaji wa rasilimali ya nchi dhidi ya kizazi kijacho. Watu wa Mtwara wasijitenge wakawa peke yao na Gesi yao. Nguvu ya mnyonge ni umoja.

Serikali isiyosikia

Serikali ina hoja kuhusu kujenga Bomba la Gesi kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa gharama nafuu. Umeme unaotumiwa na asilimia 14 tu ya Watanzania. Kwa kuwa hii asilimia 14 ndio wenye sauti basi watu wa Mtwara wataonekana hawana hoja kabisa. Lakini Serikali imejiuliza mara mbilimbili kuhusu mradi huu wa Bomba? Tunaambiwa na Wataalamu kwamba kuna uwezekano mkubwa mwakani gesi asilia ya kiasi cha futi za ujazo trillioni 20 itakuwa imegunduliwa katika Kitalu namba 7( block 7) ambacho kipo mkoani Dar es Salaam katika Wilaya ya Temeke. Iwapo gesi nyingi hivi itakuwa hapa Dar karibu kabisa na mitambo ya kuzalisha umeme, mradi huu wa Bomba unaojengwa kwa trillioni za shilingi utakuwa na maana tena? Huu mkopo utakuwa na tija?

Serikali imewaambia watu wa Mtwara gharama za kuleta bomba Dar dhidi ya gharama za kujenga mtambo wa kuzalisha umeme Mtwara na kuusafirisha umeme kwenda maeneo mengine ya Tanzania? Serikali imeangalia faida ya kujenga gridi nyingine badala ya kuwa na gridi moja tu yenye kushikwa na bwawa la Mtera? Leo bwawa la Mtera lisipozalisha hata megawati moja hata Dar es Salaam izalishe megawati alfu kumi umeme hautakuwapo maana uti wa mgongo wa gridi ni Mtera! Kwa nini tusiwe na gridi nyingine yenye uti wa mgongo Lindi au Mtwara?

Tuwasikilize watu wa Mtwara

Watanzania sio mabwege tena. Kuwaita watu wa Mtwara ni wahaini, wapuuzi au watu hatari haisaidii kujenga Taifa moja lenye watu huru. Serikali na wadau wote wa sekta ya Gesi likiwemo Bunge washirikiane na watu wa Mtwara kuhusu miradi ya gesi asilia. Tuwe na Azimio la Mtwara, tamko la kuelekeza namna bora ya kutumia utajiri wetu wa Gesi bila kuathiri umoja wa Taifa letu.

Ujio wa Sera, Maono na Uongozi Mbadala

Sasa hivi wananchi wa Mtwara kama wananchi wa sehemu nyingine wanahitaji maono mbadala, uongozi mbadala, sera mbadala na mwelekeo mbadala wa kitaifa ambao utaangalia mahitaji yao, utazingatia raslimali zilizopo na utaunganisha utendaji wa sekta mbalimbali katika kutengeneza mfumo wa kiutawala na kiuchumi ambao utaliinua taifa zima.

Ni kwa sababu hiyo naamini chama changu ni jibu sahihi kwa matamanio na kiu ya wananchi wa Mtwara na sehemu nyingine nchini. Ikumbukwe kuwa katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya 2010 tulielewa haja ya kuangalia mikoa hii ya Kusini kwa namna ya pekee na kuipa mwelekeo wa kipekee katika sera.  Bado tuna makusudio hayo tunapoelekea 2015 na tukishika Dola wananchi wa Mtwara na sehemu nyingine zote zilizoachwa pembezoni mwa mafanikio wajue kuwa wamepata rafiki na mshirika wa karibu wa kushirikiana nao kuleta maendeleo.

Siyo katika suala la gesi tu bali katika nishati, maji, elimu, miundombinu, kilimo, ufugaji, uvuvi, utalii. Mtwara kama ilivyo mikoa mingine ina raslimali za kutosha kuweza kuwainua wananchi wake kimaisha, na zaidi ya yote kutoa mchango mkubwa wa kiuchumi. Hili ambalo ni kweli kwa Mtwara ni kweli kwa mikoa mingine kama Kigoma, Manyara, Katavi, Lindi n.k.

 

Written by zittokabwe

December 29, 2012 at 10:57 AM

15 Responses

Subscribe to comments with RSS.

  1. together as 1

    nehemia

    December 29, 2012 at 11:11 AM

    • Tatizo si ualisia wa gesi asilia, kutafuta umaarurufu kwa upotoshaji wa mada ni kosa kubwa ambako watu wanabaki kurumbana bila positivity.Viongozi wa juu kitaifa tayari wameisha litolea ufafanuzi na kwanini gesi asilimia itasambazwa nchini kupitia dsm na asilimia nyingine itabaki Mtwara kwa ajili ya viwanda vilivyopo na ambavyo viko katika hatua ya kujengwa.Viwanda vya cement,gesi za majumbani,mitambo ya umeme,gypsum kusafirisha gesi mikoani na nje ya nchi shughuli zote zitaanzia Mtwara.Ili hayo yote yafanyike lazima kwanza gesi hiyo ichimbwe na wawekezaji washawishike kuwekeza.Ila labda kinachotakiwa ni serikali na watu wake wawe na sera za uwazi juu ya matumizzi ya nishati hiyo.Isitoshe viongozi wasipotoshe wananchi kwa kutoa majibu rahisi kwa maswali magumu.Hakuna mtanzania anayetaka vurugu kwa kuwa fahari wawili wagombanao nyasi ndo zaumia.Angalia unapokataa kutii sheria na serikali inapotumia nguvu za dola kuthibiti hali hiyo anayeumia ni nani?Mbona wanaoeneza chuki hawatangulizi familia zao kupambana na mkono wa sheria?Wanaoeneza chuki familia zao ziko njema ulaya,watoto wao wako international schools wakati unazarau shule za kata.Pamoja ya hayo wanaotia watu ujinga wa kuchochea vurugu wanatakiwa wajaribu kushawishi watanzania hasa wana Mtwara wajiandae ili kupokea ujio wa gesi.Kama hatutakuwa tumejiandaa unafikiri hata gesi ikibaki Mtwara utanufaikaje.Hata maisha bora tunayoubiriwa itakuwa ndotonna mzigo kwetu.Kama hatujaenda shule kiwanda cha gesi kitakunufaishaje.Hakuna pesa ya mgao kama Libya.Si mabaya yayodaiwa kufanywa na serikali yatangazwe,hata mazuri kidogo tuyahubiri.Mikoa ya kusini umeme gharama yake ni kidogo mbona serikali haipongezwi?Tumeambiwa Mkoa wa Pwani hadi mji wa Bungu ni umeme punguzo kwa sababu watoka Kusini na hayo si neema inaanza kuja.Tatizo sasa hatujajiandaa je nyumba zetu za faa kufungwa umeme?Kiwanda cha simenti Mtwara nacho kimeanza kuzalisha simenti na kuuza kwa bei punguzo,Kiwanda cha simenti cha Kisemvule Rhino sementi ,Mkoa wa Pwani nacho cha uza cementi kwa bei punguzo,maisha mazuri kwa kila mtanzania yaja.Isitoshe kwa watanzania ambao hawako kwenye mtandao wa gesi asilia nao neema wagusa Waziri Muhogo kaisha agiza gharama za kusambaza umeme kwa wananchi zishushwe mara moja kuanzia Jan2013.Kuhusu Dsm,ni jiji ambalo tangu awali lilitayalishwa kuwa kitovu cha uchumi wa nchi,ndo maana viwanda vingi vilijengwa hapa.Ni historia ambayo inabadilika kwa sasa kwa kuwa Tz sasa tunaelekea kuwa kama kijiji kimoja.Mkoa kwa mkoa,wilaya kwa wilaya,kijiji kwa kijiji sasa tunawasiliana kwa urahisi.Mtwara hadi Kagera ni siku moja badala ya mwezi hayo ni mabadiliko makubwa lazima kupongeza.Ndo maana inaelezwa kuwa dsm hakutegemei kujengwa viwanda badala ya Mtwara kwa kuwa bidhaa itakayozalishwa itasambazwa nchini kote kwa mtandao wa barabara na meli.Hata mali ghafi zitaenda Mtwara bila kizuizi.Gasi kuja Dsm kutaedeleza kusupport uchumi wa wakati maeneo mengine yanakua kiuchumi.Angalizo potofu karibu wasiasa wengi wahubilia kwa mitambo mikubwa ya umeme kama iliyoko Ubungo ijengwe Mtwara ili watu wapate ajira,huo ini upotoshaji,kutokana na teknologia ya sasa ilivyo vijana wengi watanufaika na kufyeka majani -vibarua ikibidi kwa sababu kazi zote zafanywa na mitambo ya ujenzi na baada ya ujenzi kukamilika operators wasomi watakuwa wachache sana je dhana ya ajira is it applicable.Mbona watu wa Tanga(Pangani,Hale falls),Iringa,Morogoro (Mtera falls ),Kilimanjaro (Nyumba ya Mungu) hawajaleta chochoko kuhusu umeme kuja Dsm.TUJITAMBUE -MPAHo

      Tadeo

      January 15, 2013 at 4:59 PM

  2. Kweli tunapaswa kuwasikiliza ili kuona tunafanyaje, it might be they have a good idea that can drugg the country out of this poverty

    Fadhili Elihudi

    December 29, 2012 at 11:28 AM

  3. Safi sana makamanda wa chadema endeleeni kutuelimisha sisi kwani asilimia kubwa 2mekweisha jitambua hongereni sana.

    Mussa

    December 29, 2012 at 12:44 PM

  4. Mie sioni ubaya kwa wao kudai hivyo wanavyodai.kulundika fursa zote za Ajira dar ndio maendeleo? ndo maana folen haiishi

    richard

    December 29, 2012 at 1:15 PM

    • HAPA NDIO NAONA UMUHIMU WA ISHU YA MAJIMBO.

      Dotto Rangimoto

      December 30, 2012 at 12:58 PM

  5. Zito usemalo ni kweli na nia yako thabiti ya kutetea uma wa watanzania inaonekana dhahiri. Kumbuka jititihada zako za leo ni hazina ya heshima ya kesho.

    Karosi Mmari

    December 30, 2012 at 1:53 PM

  6. Tunachohitaji kuhusu gas ni kuleta tija kwa wananchi wa Lindi na Mtwara na si vinginevyo tunataka viongozi waone na wajue hili hakuna blabla ktk maendeleo imani ya kuamini kua kila kitu kikiwepo Dar ndio maendeleo yatakua TZ hii ni dhana potofu yote ni Tz hivyo miundombinu ijengwe popote kwa nia ya kupanua wigo wa ajira ili kuleta maendeleo Tunatambua hali mbaya ya uchumi wa kusini,Nashukuru vyama pinzani kwa kuliona hili naomba tuungwe mkono na tukikosea basi palekebishwe SOTE NI WATANZANIA.

    AHMAD SALUM CHIBWANA

    December 31, 2012 at 7:50 AM

  7. Dirty politics undermines economic development.If every region want out because it has discovered a resourceful material we will never be the same in terms of peace and tranquility.Politicians like you Mr. Kabwe will be held responsible for damages done.

    Mohamed Sleyim

    December 31, 2012 at 12:13 PM

  8. Namwomba Mheshimiwa Zitto aendeleze uelimishaji umma wa Tanzania juu umuhimu wa kuheshimu na kufanyia kazi matarajio ya wenyeji wa Mtwara kwamba matumizi ya gesi asilia iliyopatikana kwenye ukanda wao wa Mtwara yangelenga zaidi kuupatia Ukanda wa Mtwara ile miundo mbinu muhimu kama vile bandari, reli, barabara, umeme mwingi na wa bei nafuu na maji ili kuvutia na kuongeza kasi ya uwekezaji katika uendelezaji uchumi wa kilimo, uchimbaji wa madini, viwanda na biashara ya kimataifa kati ya nchi za kusini mwa bara la Africa na zile zilizoko ndani ya bahari ya Hindi na kuizunguka kwani kupitia bandari ya Mtwara ingekuwa njia rahisi zaidi.
    Matumizi ya Gesi iliyopatikana Ukanda wa Kusini (Mtwara) yalenge zaidi kutujengea Ukanda wa maendeleo mpya tarajiwa wa Mtwara, Kusini mwa Tanzania; matumizi ya gesi itakayopatikana Ukanda wa kati (Dar es Salaam) yalenge zaidi kuendeleza ujenzi wa Ukanda wa maendeleo wa kati-Dar es Salaam; matumizi ya gesi itakayopatikana ukanda wa Kaskazini (Tanga) yalenge zaidi kuendeleza ujenzi wa ukanda wa maendeleo wa kaskazini (Tanga).
    Pia ingeweza kuwa bora zaidi kama matumizi ya gesi asilia kwa ajili ya uzalishaji umeme yangepunguzwa sana hadi kiwango cha dharura tu kwani gesi nyingi ingeweza kuuzwa na fedha zitakazopatikana zikatumika kwa manufaa zaidi kwenye kuendelezea fursa zilizopo kwa ajili ya uzalishaji wa umeme wa maji na hata wa makaa ya mawe ambao gharama za uzalishaji ni ndogo kuliko zile za uzalishaji wa umeme wa gesi.
    Matumizi ya gesi asilia inayopatikana Ukanda wa Mtwara unaolenga zaidi ukuaji wa Ukanda mpya wa meendeleo wa Mtwara,kusini mwa Tanzania utakuwa wa manufaa sio tu kwa wenyeji wa Ukanda wa Mtwara bali kwa Watanzania wote na serikali yao.
    Maamuzi ya ujenzi wa hili bomba kubwa la kusafirisha gesi asilia kutoka ukanda wa Mtwara (uliobaki nyuma sana kimaendeleo) kuja ukanda wa Dar es Salaam (unaoongoza kwa maendeleo na wenye dalili ya kuwa na gesi yake nyingi asilia) yanaashiria upendeleo katika mipango ya maendeleo kikanda na sio vizuri.

    Dr A. Massawe

    December 31, 2012 at 6:58 PM

  9. Wana haki ya kusikilizwa.madai yao ni ya msingi

    Shirikishoi nyagosaima

    December 31, 2012 at 9:41 PM

  10. Haya ndo yaleyale ya Mawese kuzalishwa kigoma kiwanda kujengwa Mwanza. Mtwara- Lindi wanahaki kusikilizwa na serikali kwani nao wanahitaji maendeleo, Dar nini bwana kila kitu? Ndiyo maana uchakachuaji mwingi. Mr Zitto sina njia nzuri ya kukufikishia ujumbe ambao binafsi naona ni kero kubwa na unachangia kupoteza mapoto ya serikali ambayo huingia mifukoni mwa watendaji warafi wa serikali. Kero hii ipo mipakani mwa Burundi na Kigoma, Kwa sisi wakazi wa kigoma unapofika mpakani unapewa karatasi yenye maandishi(visiting permit) kwa mkoni unalipa shs 10,000/ (mimi nimelipa) siku ya tarehe 28 Dec 2012 bila risiti ya serikali na hata ya Halmashauri husiki, niliporudi toka Burundi nilinyang’anywa kikaratasi na nilipo jaribu kuomba risiti, niliambiwa kuwa ni msaada wa ujirani mwema na kama wangetambua hilo wasinge niruhusu na hatasikunyingine sintaruhusiwa na wamebaki na picha yangu navyo fahamu mimi Borders hizi za manyovu na Kagunga zinapitisha zaidi ya watu 200 kila siku kuingia na kutoka na kwa makusanyo ya kati ya shs 5000-10000/. Mapato kwa siku ni kati ya 1,000,000- 2,000,000/ na kwa mwezi ni kati ya 30,000,000- 60,000,000/ Hiki ni kiwango kikubwa sana ambacho wananchi wanaibiwa na huishia mifukoni mwa waroho wachache

    baraka gilagiza

    January 3, 2013 at 10:17 AM

  11. Gesi kwa wana Mtwara kwaza kabla ya taifa kunufaika, je mtwara itafaidika na nini, Pia suala hili lisiwe kama suala ya fadhila kwa watu wabagamoyo na dar es salaam, jiulizeni kwanini sasa bandari ya Bagamoyo inajengwa, je ili isafilishe nini? pia hisitoria hinaonyesha kuwa bandari kubwa sana yenye kina kilefu ni Bandari ya Mtwara nasio nyingine

    GESI KWANZA UHAI BADAE

    January 25, 2013 at 9:13 PM

  12. […] katika magazeti kadhaa hapa nchini na kwenye blogu yangu (www.zittokabwe.com). Niliandika: Utajiri wa Gesi Asilia: Tuwasikilize Watanzania wa Mtwara na Lindi. Nikaandika tena: Tusipuuze mandamano dhidi ya Bomba la Gesi: Kilio cha Uwajibikaji; Nikaandika tena: Mtwara : Serikali inavunja […]

  13. […] Niliandika: Utajiri wa Gesi Asilia: Tuwasikilize Watanzania wa Mtwara na Lindi. Nikaandika tena: Tusipuuze mandamano dhidi ya Bomba la Gesi: Kilio cha Uwajibikaji; Nikaandika tena: Mtwara : Serikali inavunja nchi kwa kutosikiliza Wananchi; ni baadhi ya makala nilizoandika kuhusiana na suala la Mtwara. […]


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: