Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Posts Tagged ‘BoT

Mapya IPTL: $270Million zimetokaje BoT ?

with 5 comments

Mapya IPTL: $270m zimetokaje BoT ?

THE CITIZEN (Courtesy MillardAyo Blog)

THE CITIZEN
(Courtesy MillardAyo Blog)

THE CITIZEN (Courtesy MIllardAyo Blog)

THE CITIZEN
(Courtesy MIllardAyo Blog)

Nimesoma habari kuu ya gazeti la The Citizen la tarehe 3 Machi 2014 kuhusu mauzo ya kampuni ya IPTL kwa kampuni ya Pan Africa Power Limited (http://www.thecitizen.co.tz/News/-270m-deal–Story-of-IPTL–PAP-and-High-Court/-/1840392/2228606/-/1bddmgz/-/index.html).

THE CITIZEN 4th March 2014 How $270-million IPTL deal was planned and executed

Nimeshtushwa sana na matumizi ya fedha za akiba maalumu (escrow account)  iliyokuwa benki kuu (BoT). Nikiwa mwenyekiti wa kamati ya PAC nina haya ya kusema; Mwaka 2006 Rais Jakaya Kikwete aliagiza kwamba, ili kumaliza kabisa suala la mkataba wa kuuziana Umeme wa IPTL, mitambo ya kampuni hiyo ichukuliwe na Serikali. Mwaka 2006, 2007 na 2008 Kamati ya BUNGE ya Nishati na madini imekuwa ikitoa maagizo hayo hayo kuhusu suala la IPTL. Mwaka 2009, Aprili 30 Kamati ya Bunge ya POAC ilipeleka mapendekezo bungeni kwamba IPTL ichukuliwe na serikali na fedha zilizopo katika escrow account zitumike pia kubadili mtambo ule kutoka mafuta mazito kwenda kutumia Gesi Asilia. Pendekezo hilo lilipitishwa na Bunge na POAC ikatoa maelekezo maalumu kwa Gavana wa Benki Kuu kuwa fedha zilizopo escrow account zisitumike kwa namna yeyote ile bila mitambo ya IPTL kuwa ya umma na kubadilishwa ili itumie Gesi Asilia.

Chanzo cha escrow account?

Baada ya mkataba wa IPTL kuingiwa, iligundulika kuwa kuna udanganyifu mkubwa ulifanyika katika kiwango cha mtaji wa kampuni hiyo na hivyo kufanya malipo wanayolipa tanesco kwa IPTL kuwa makubwa mno. Wakati katika kukokotoa gharama za uwekezaji (capacity charges) mtaji uliowekezwa katika IPTL ulisemwa ni dola milioni 36, ukweli ni kwamba IPTL waliweka dola 50 tu. Hivyo capacity charge ya dola milioni 3 kwa mwezi haikupaswa kulipwa yote kwani kampuni iliendeshwa kwa mkopo kuliko mtaji wa wawekezaji ( debt financed and not equity financed). Hivyo, mahakama ya kimataifa ya ICSID ikaamua kuwa, fedha zote za capacity charges ziwekwe Benki Kuu mpaka gharama halisi ziamuliwe na mahakama ndio wahusika wagawane (tanesco na IPTL). Akiba hiyo, nimeambiwa, ilifika dola 250m kabla ya kuchukuliwa na kugawanywa kwa wanahisa na wanunuzi wa IPTL. Hivyo kabla ya mgawo huu ilipaswa pesa ambazo tanesco walikuwa wanalipa kama ziada ya capacity charges kwa IPTL zirejeshwe kwanza na zinazobakia ndio zilipwe kwa wadai (creditors) na wanahisa. Kwa hali ilivyo sasa mnunuzi wa IPTL kapewa mitambo na fedha za kuinunua, ikiwemo fedha za tanesco ambazo zilipaswa kurejeshwa (Richmond cha mtoto kwa kweli).

Maswali ya kujibiwa ni haya;

Je, ziada ya fedha za malipo ya capacity charges zimerudi tanesco?

Je, mwekezaji Mpya kapewa mkataba Mpya wa kuuza Umeme (PPA) kwa utaratibu gani wa zabuni?

Je, agizo la Rais na BUNGE kwamba Mitambo iwe ya umma limetupiliwa mbali kwa vigezo gani?

Wizara ya Nishati na Madini na Benki Kuu wametoa taarifa rasmi kwa umma kuhusu masuala haya? Wizara itoe taarifa, CAG akague

Kwa namna yeyote ile CAG anapaswa kukagua mchakato huu na kuweka majibu kwa umma kupitia kamati ya PAC. Hii ndio njia bora zaidi ya kuondoa wingu katika suala la IPTL ambalo toka limeanza miaka ya tisini limegubikwa na mazongezonge ya rushwa na uvundo wa kifisadi. Uwazi utatoa ukweli na kuwezesha uwajibikaji wa fedha za umma. Wakati mchakato wa ukaguzi unafanyika ni vema Wizara ya Nishati na madini itoe tamko rasmi.

Zingatia:

Kwa mujibu wa mkataba kati ya TANESCO na IPTL capacity charge inapaswa kukokotolewa kwa kuzingatia mtaji wa asilimia 30 na mkopo wa asilimia 22.31. Mtaji wa IPTL ulikuwa $50 tu, tofauti na $36 milioni zilizotajwa kwenye mkataba na kuamuliwa na mahakama. Badala ya TANESCO kulipa ‘capacity charge’ ya dola 50,000 kila siku Umeme uzalishwe au la, udanganyifu wa mtaji ulipelekea TANESCO kuwa inalipa dola 100,000 kila siku tangu mwaka 2002. Kuanzia mwaka 2007 fedha hizo zilianza kuwekwa kwenye akaunti maalum (escrow account) BoT.

Written by zittokabwe

March 4, 2014 at 3:51 PM

Benki Kuu: Hazina ya Taifa imekauka?

with 35 comments

 Zitto Kabwe, Mb.

Benki Kuu ya Taifa lolote ndio taasisi pekee yenye takwimu zote nyeti na za uhakika zinazohusu uchumi wa Taifa hilo. Katika tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania eneo la Machapisho kuna Taarifa nyeti sana mbili, Mapitio ya Uchumi ya Mwezi (Monthly Economic Review) inayotoka kila Mwezi katika Mwaka na Mapitio ya Uchumi ya Robo Mwaka (Quarterly Economic Bulletin). Taarifa hizi hutoa taarifa kuhusu masuala yote muhimu yanayohusu Uchumi wa Jamhuri ya Muungano na Uchumi wa Zanzibar ikiwemo taarifa za Mfumuko wa Bei, Mapato na Matumizi ya Serikali, Mwenendo wa Biashara ya Kimataifa na Deni la Taifa.

Ukienda kwenye tovuti ya Benki Kuu leo utakuta Taarifa hizi. Lakini Taarifa hizi zimeishia Desemba mwaka 2011 zikitaarifu masuala ya Uchumi ya Mwezi Novemba na robo ya mwaka inayoishia Desemba. Ukitaka kujua Bajeti ya Serikali na mwenendo wake hutapata taarifa za sasa bali za Mwezi Novemba mwaka 2011, miezi sita nyuma. Huu sio utendaji uliotukuka. Hii ni kuficha taarifa kwa wananchi. Taarifa zinafichwa ili iwe nini? Nani anafaidika na kufichwa kwa taarifa muhimu kama hizi?

Kuna tetesi kwamba Hazina ya Taifa (Hifadhi ya Fedha za kigeni – foreign reserve) inakauka, kwamba tuna hifadhi ya kuagiza bidhaa nje kwa mwezi mmoja tu. Niliposikia tetesi hizi sikuamini. Nilipoenda katika tovuti ya Benki Kuu ili kuweza kuwa na habari rasmi (authoritative) nimekuta takwimu za Novemba 2011.

Takwimu ya Mfumuko wa Bei iliyoko kwenye tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania ni ya mwezi Novemba mwaka 2011!

Ukitaka kujua mwenendo wa Bajeti ya Serikali kama makusanyo ya Kodi na Matumizi utapata Taarifa ya Mwezi Novemba mwaka 2011.

Ukitaka kujua manunuzi ya Mafuta (fuel imports) kwa miezi 3 ya mwanzo ya mwaka 2012 ili kuweza kuona namna Umeme wa dharura umeathiri urari wetu wa Biashara ya Nje hupati taarifa hiyo katika tovuti ya Benki Kuu.

Taarifa zinafichwa.

Ndio. Zinafichwa tena makusudi maana taarifa hizi zipo Benki Kuu. Huu ni uzembe maana Nchi inawalipa wafanyakazi wa Benki Kuu mishahara minono ili wafanye kazi hizi. Benki Kuu pia imetoa zabuni kwa Kampuni Binafsi kuchapisha Taarifa hizi. Kama Taarifa hazitoki kwa wakati ni wizi. Wizi ambao haupaswi kufumbiwa macho.

Benki Kuu ya Tanzania ipo miezi Sita nyuma. Aibu kubwa sana.

Wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano akihakikishia mataifa duniani kuhusu uwazi Serikalini (#OGP), Taasisi kubwa kama Benki Kuu inaficha Taarifa ambazo ni nyeti kwa wananchi na muhimu kwa wafuatiliaji wa sera za Serikali. Rais wa nchi anaongea Buluu, Gavana wa Benki Kuu anasimamia Kijani!

Inaudhi na kukera sana kwenda kwenye tovuti ya Benki Kuu na kukuta taarifa za miezi Sita iliyopita. Benki Kuu hamstahili kuitwa Benki Kuu, labda benki kuu kuu. Rekebisheni jambo hili haraka sana maana kuficha taarifa kwa Umma ni ufisadi. Haki ya kupata taarifa ni haki ya msingi katika Katiba yetu.  Hatutaki kushtukizwa na kuambiwa Hazina ya Taifa imekauka.

Prof. Ndulu hakikisha Taarifa ya Mapitio ya Uchumi wa kila Mwezi imewekwa kwenye tovuti kwa muda mwafaka. Ifikapo mwisho wa Wiki inayoanzia Jumatatu Mei 14, tovuti ya Benki Kuu iwe na Taarifa za miezi yote (Desemba, Januari, Februari, Machi na Aprili). Taarifa hizi ni muhimu ili nasi tutekeleze majukumu yetu ya Kikatiba kama Wabunge, Mawaziri vivuli na Wananchi wa Tanzania.