Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Mtwara : Serikali inavunja nchi kwa kutosikiliza Wananchi

with 13 comments

Mtwara : Serikali inavunja nchi kwa kutosikiliza Wananchi

Kwa wiki ya tatu mfululizo kumekuwa na malumbano kuhusiana na suala la ujenzi wa Bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam. Kumekuwa na madai yenye nguvu ya hoja kutoka kwa wananchi wa Mtwara dhidi ya porojo kutoka kwa viongozi wenye dhamana ya kujibu madai haya ya watu wa Mtwara. Watu wa Mtwara kwa umoja wao na kwa kuungwa mkono na viongozi wa dini zote wamekuwa wakitaka Serikali ifikirie upya suala la mradi wa ujenzi wa Bomba la gesi na badala yake kujenga mitambo ya kufua umeme mkoani Mtwara na kusafirisha umeme huo kwenda maeneo mengine ya nchi. Kwenye moja ya maandishi yangu (Serikali iwasikilize watu wa Mtwara) nimeshauri kuwa Taifa liwe na gridi nyingine ya Taifa ambayo itatokana na Gesi tu na ianzie Mtwara.

Ikumbukwe kwamba katiba ya nchi, ibara ya 9 katika mabano J inataka mamlaka ya dola na vyombo vyake vyote kuhakikisha ya kwamba shughuli zote za kiuchumi zinaendeshwa kwa namna ya kwamba pasiwe mrundikano wa utajiri au shughuli za uzalishaji kwa watu wa chache. Katiba inaendela kwa kuelekeza kwamba uchumi wa nchi upangwe katika uwiano sawia (9, d). Watu wa Mtwara wanatekeleza matakwa haya ya katiba kwa kukataa mrundikano wa shughuli za kiuchumi wa nchi na utajiri wa nchi kua kwenye mikoa michache na hasa mkoa wa Dar-Es-Saalam.

Serikali imekuwa ikitoa majibu ya porojo na kuwatusi watu wa Mtwara na kama ilivyozoeleka Rais Jakaya Kikwete na Mawaziri wake wamekuwa wakisema suala la Mtwara linatumika na wanasiasa kujitafutia umaarufu. Inasikitisha sana kuona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwaambia mabalozi wa nchi za kigeni waliopo hapa nchini kuwa yanayoendelea mkoani Mtwara yanachochewa na Wanasiasa tuliosimama na wananchi wanaodai haki ya kufaidi utajiri wa nchi yetu. Rais Kikwete na Mawaziri wake wameshindwa kabisa kuonyesha uongozi katika suala hili na hatimaye kuhatarisha umoja wa kitaifa.

Kwa udhaifu wa serikali na tabia ya kutafuta mchawi badala ya kutatua tatizo la msingi, wananchi wameendelea kukutana na hata wengine sasa kuanza kusambaza ujumbe wa kukata kipande cha nchi na kuanzisha Jamhuri ya Kusini. Nimeona kwenye mabango ya mkutano wa hadhara uliofanyika 19/1/2013 wananchi wakibeba mabango yanayoaishiria kuchoka kuwa sehemu ya Tanzania na kuanzisha Jamhuri ya Makonde kuanzia jiwe la Mzungu wilayani Kilwa mpaka mto Ruvuma. Haya yanatoka na kiburi cha Serikali kujishusha na kuwasikiliza wananchi wanao dai haki yao ya kikatiba.

Ni Serikali iliyokosa uhalali wa kutawala inayoweza kudharau hisia hizi za wananchi. Serikali ielewe kwamba kamwe haitaweza kulinda kila nchi ya bomba hili iwapo italijenga kwa nguvu. Badala ya kuzungumza na vyombo vya habari Serikali ifanye mazungumzo na wananchi wa Mtwara na kukubaliana na matakwa yao. Kitendo cha Serikali kung’ang’ania msimamo wake dhidi ya watu wa mtwara ni kitendo kinacho weza kuipasua nchi na hivyo kwenda kinyume na masharti ya katiba ibara ya 28 ambayo inasema: “kila raia ana wajibu wa kulinda uhuru wa nchi, uhuru mamlaka na umoja wa taifa.”ibara ya 28, 1.

Inawezekana Serikali inaogopa kuvunja makubaliano na Wachina ya mkopo wa dola za kimarekani 1.2 bilioni ambao imeuingia bila hata kushirikisha Bunge. Inawezekana Serikali na hasa watendaji wa Serikali waliojadili mkopo huu wameshapata chao na hivyo kuogopa kusikiliza madai halali ya wananchi. Lakini yote hayo hayawezi kuwa zaidi ya Umoja wa nchi yetu. Hatuwezi kukubali nchi yetu ipasuke vipande vipande kwa sababu tu ya kulinda mkataba wa bilioni 1.2 tuliokopa China, ambayo serikali inang’ang’ania.

Tunafahamu kwamba ubalozi wa China umeandika barua serikalini kuwaondoa raia wa China waliopo Mtwara kwa hofu ya maisha yao. Serikali inaficha ukweli huu kama ilivyoficha ukweli kwamba Naibu Waziri wa Nishati na Madini bwana George Simbachawene alifukuzwa na wananchi wa Mtwara alipokwenda hivi majuzi. Serikali itaficha ukweli mpaka lini? Lazima tupate majawabu.

Kwanza Serikali iweke wazi mkataba wa ujenzi wa Bomba hili. Kamati ya Bunge ya POAC ilipokuwa inapitia mahesabu ya TPDC iliomba mkataba na kwa mshangao mkubwa wabunge wakaambiwa Mkataba haupo TPDC bali upo Wizarani. Kwa nini Mkataba huu wa matrilioni ya Fedha unafichwa? Mkataba huu ulisainiwa pamoja mikataba mingine 2, mmoja wa kujenga nyumba za wanajeshi wa thamani ya dola za kimarekani 400 milioni na mwingine wa mawasiliano jeshini wa dola za kimarekani 110 milioni, na mikataba yote mitatu imesainiwa kimya kimya bila kushirikisha wananchi kupitia Bunge. Lazima mikataba yote hii iwekwe wazi.

Pili, Mkataba huu uchunguzwe kama unalingana na thamani ya fedha maana kwa utafiti wa awali inaonyesha kuwa bei ya ujenzi wa bomba imepandishwa maradufu. Wastan wa kujenga bomba la gesi duniani ni dola za kimarekani 1.2 milioni kwa maili moja. Mradi huu wa Tanzania utagharimu dola za kimarekani 2.2 milioni kwa kilomita moja (maili 1 ni sawa na kilomita 1.6).

Tatu, Serikali ibadilishe Mkataba huu kuwa wa mkopo wa kujenga Mitambo ya kufua umeme Mtwara na ujenzi wa Msongo wa Umeme kama gridi ya pili ya Taifa. Kwa sasa Tanzania ina gridi moja ambayo inabebwa na bwawa la Mtera linalo tegemea mto Ruaha ambao hivi sasa unakauka miezi 5 katika miezi 12 ya mwaka. Ni dhahiri kwamba kwa usalama wa Taifa na hata kwa gharama Nchi itafaidika zaidi kwa kujenga gridi nyingine kutokea Mtwara badala ya kusafirisha gesi kuja Dar-Es-Salaam.

Serikali haitashinda vita hii kwa kuzusha kwamba ama wanasiasa wanaopinga wanatumika na makampuni mengine au kwa mataifa ya magharibi kutaka kuvuruga nchi. Serikali ijitazame yenyewe. Bila kufanya hayo tunayo pendekeza hapo juu, wananchi wataendelea kupigania hako yao. Hii ni vita ya uwajibikaji. Wananchi wanataka kufaidika na rasilimali za nchi yao. Kwa vyovyote vile upande wa wananchi utashinda. Vita ya uwajibikaji kwenye rasilimali za nchi sio ya vyama vya siasa, ni vita ya wananchi. Chama cha siasa kitakachokwenda kinyume na matakwa ya wananchi, kinajichimbia kaburi.

 

 

13 Responses

Subscribe to comments with RSS.

  1. Hivi mbona gesi ya Songo Songo inazalisha umeme kitambo sasa lakini hamkulalamikia hili? Pia, Zitto nikishasoma sehemu wewe mwenyewe ukipigia debe umeme wa gesi maana sio mzigo kifedha kwa Tanesco.

    Kwa kweli Watanzania tumekua wavivu kufikiria!

    Kisongo

    January 20, 2013 at 6:50 PM

  2. yani mpaka machozi ya ndani yananitoka natamani watu hawa mungu awakusanye kwa pamoja apasue ardhi iwameze kama alivyomfanya kola na nduguze kwenye biblia maana hawana huruma labda yaweza kuwa hivyo siku moja.

    nkwendamae dina

    January 20, 2013 at 6:53 PM

  3. Nafikiri watu wa mtwara wawe makini wasikurupuke kusema wanataka kuigawa nchi. Ina maana wanataka gas iwe yao pekee yao mbona mikoa mingine ina natural resources nyingi tunashare nchi nzima kama vile mlima kilimanjaro,serengeti national park,ngorongoro crater, Ruaha national park, Mikumi national park nakadharika lkn hatujawahi lalamika hata siku moja kwamba tunataka kuigawa nchi kwa vitu vidogo kama hivyo. Ninacho kifikiria mimi na ninacho washauri watu wa mtwara wasikurupuke kutoa kauli za ajabu. Wao wanachotakiwa wajaribu kuielekeza serikali ya ccm kwa utaratibu unao faa. Pale mtwara kuna wazee wenye hekima na busara zao kwanini wasimuombe rais waka kaa naye wamueleze watu wa mtwara wanataka nini ili watekelezewe kisha hiyo gas inende na kwenye maeneo mengine ya nchi. Pili kule mtwara kuna taasisi za dini kwanini hao viongozi wadini wasiombe nafasi waweze kukutana na kiongozi wa nchi kisha wakawaeleza watu wa mtwara kile wanachokidai. Tatu kuna taasisi za watu binafsi kwanni wasiyekae kwapamoja wakasema kile wanachokitaka? Kwa mfano tuna mzee wetu mkapa aende awasikilize wale watu kikubwa wanachotaka wao ni nini? Wanataka gas ije dar au hawataki? Na kama hawataki bomba la gas lisijengwe kuja dar wanasababu gani za msingi za kufanya hivyo? Na pia kama wanaruhusu ni baada ya kuridhishwa na kitu gani kutoka serikalini? Hapo nafikiri tatizo litaisha haraka sana. Lkn watu wa mtwara wasisimame kwenye misingi ya kuigawa nchi wakumbuke nao wamekula kodi za rasimali zilizotoka kwenye mikoa mingine lkn hatukuzuwia watu wa mtwara kunufaika nazo kwa sababu,tunafahamu kuwa watanzania wote ni wamoja na wala hakuna udini wala ukabila. Watu wamtwara mkumbuke kula pamoja na wenzenu cyo mwajipendelea nyinyi wenyewe na gas haipo kwenu tuu ipo na maeneo mengine ya nchi kwa maana na hao pia wajigawe kama nyie take care sana watu wa mtwara.

    Joachim Hezekiah Sajo

    January 20, 2013 at 7:02 PM

    • wewe uliye comment hapo ni kafiri hauwezi kutetea ujinga kihivo nadhani wewe umekurupuka tu kukoment hapo jipange kwanza we pumbafu acha sisi na chadema tuiokoe tanzania

      dacoda

      January 22, 2013 at 1:30 AM

  4. Sijawahi kukujibu maoni yako yoyote tangu uanzishe ukurasa wako huu. Naona leo nikujibu. Umenikuna pasipowasha lazima nikushangae.
    Tusiwe nchi inayotafuta na kuendekeza migogoro isiyoisha. Tunapojifunza Jiografia ya Darasa la tano na kidato cha tatu kuna maada inayotufundisha mahali pa kuchagua kujenga kiwanda. Moja ya sifa hizo ni uwingi wa watu wanaoweza kuajiriwa kwa urahisi kufanya kazi kiwandani, miundo mbinu kama vile usafiri, umeme na maji lakini pia soko.
    Lakini pia kuna kitu tunaita Cost and Management accounting. Somo hili linatusaidia kupembua, katika mawazo mawili yenye lengo moja, lipi ulifanye na lipi usilifanye baada ya kulinganisha gharama halisi ya mawazo hayo mawili. Hapa kabla ya kuamua ujenge kiwanda Mtwara au Dar es Salaam unapaswa kuaangalia gharama kwanza. Pale penye ghrama nafuu na faida kubwa ya muda mrefu ndipo ujenge kiwanda. Nina wasiwasi kama makundi yote yanayobishana juu ya pendekezo hili kama mmekwisha fanya upembuzi huu.
    Rasrimali zote zilizopo nchini ni za watanzania wote. Serikali yoyote halali,iliyowekwa madarakani kwa njia ya kura imepewa dhamana ya kusimamia rasirimali hizi na kuzitumia kwa maendeleo ya wananchi wote bila kujali zinapatikana mahali gani. Serikali hukusanya mapato kwa njia ya kodi na vianzo vingine vya mapato na kuziweka kwenye fuko la pamoja ( consolidated fund) na baadaye kuzigawanya kulingana na vipaumbele vyake. Mapato yaanayopatikana kwa kuwakata kodi watumishi wa serikali yanatumika kuendeleza nyanja zingine zote bila kujali kama zinatoka kwa watumishi waelimu au afya. Mapato yanayotokana na wafanya biashara halikadhalika hayarudi kwa walitozwa kodi peke yao. Kudai maadamu gesi inapatikana Mtwara basi sharti itumike Mtwara hakuna tofauti na kusema kodi ya Waheshimiwa wabunge itumike bungeni tu. Mapato yanayopatika katika sekta ya Afya yatumike kwenye Afya pekee. Dhana hii haipo duniani kote. Msingi wa kuunda serikali ni kuwa na chombo kinachosimamia rasirimali za nchi husika kwa manufaa ya wananchi wotei.
    Tuchukulie mfano mdogo : Tangu enzi kumekuwepo na maeneo yanayolima mazao ya biashara kama vile; korosho, chai, kahawa, katani, karafuu, hiliki, pamba, ng’ombe tumbaku, miwa orodha ni ndefu. Kuna maeneo ambayo hayana mazao haya, lakini fedha za kigeni zikipatikana zimekuwa zikitumika kuendeleza nchi yote bila kujali kama mahali fulani hawana mazao ya biashara. Hali kadhalkai mazao ya chakula yamekuwa yakisambazwa nchi nzima bila kujali kama eneo hili halizalishi mazao ya chakula.
    Kugawa nchi kwamisingi yoyote ile ni uhaini. Gesi sio sababu mojawapo inayohalalisha kuigawa nchi. Wewe kama mmoja wa wananchi wa Tanzania wanaotamani kugombea uraisi wa nchi usingalikuwa ni mmojawapo wa watu wanaunga mkono nchi kugawika vipande vipande. Kwa vyoyote vile Mkoa wa Mtwara ukigawika hautaweza kugombea uraisi Mtwara, utaambiwa kagombee kwenu Kigoma. Kigoma paia kukichafuka kwa sababu yoyote ile utaambiwa kagombee Kasulu. Hili tulikatae maana mwisho tutabakiwa na utawala wa mtu na mkewe.
    He who pays the piper chooses the tone ( Anayemlipa mpiga zumari ndiye huchagua wimbo) Inayotaka kujenga kiwanda ni serikali ni, vipi wananchi wa Mtwara wailazimishe serikali mahali pa kujenga?
    Busara ni kusema jengeni popote lakini mhakikishe wanachi wa mtwara hawaachwi chepwa.

    asungwile

    January 20, 2013 at 8:58 PM

    • Busara ni kusema ijengwe popote… sawa kabisa ikiwemo mkoa wa mtwara wenyewe

      Allan Anthony

      January 28, 2013 at 8:25 AM

  5. Kama wanaficha ukweli watajijua wenyewe sisi tunajiandaa kumchagua Mh.Rais wetu wa JAMUHURI YA KUSINI na tuko tayari kwa hilo kama kawaida wanavyuo wote wa kusini tutimize lengo letu kuhusu mkutano wa Febu na pia kikwete na mafisadi wenzake pamoja na askari wao wajue kua KAMA WAO WANAJIFUNZA KUUWA NA SISI TUNAJIFUNZA KUFA HADI TUISHE WOTE WA KUSINI NA WAZALENDO WA NCHI HII NDIPO WAHAMISHE GAS NA WAKISHINDWA HILO BASI TUIGAWE NCHI TU UJINGA UTUTOKE UBAKIE HUKO HUKO TANZANIA KWAO.

    AHMAD SALUM CHIBWANA

    January 20, 2013 at 10:24 PM

  6. Gezi ya Mtwara ikizalisha umeme huko Mtwara badala ya kule Dar es Salaam na njia mpya ya umeme ikajengwa kuusafirisha hadi Dar es Salaam, maeneo yote ya vijijini na mijini kwenye mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam yatakuwa yamefaidi kwani yote yatakuwa yamewezeshwa kuwa kivutio kwa uwekezaji hasa kwenye fani ya kilimo cha umwagiliaji na ufugaji wa kisasa maeneo ya vijijini. Umuhimu wa power grid badala ya gas grid umeelezewa zaidi kwenye link hii: http://db.tt/S6eMcAr3.
    Kikwazo kikubwa kwenye ujenzi wa hili bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ni kwamba bado hatujajua ni maeneo yapi yenye gesi na ni yapi hayana kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam hadi Tanga hadi mpaka wetu na Kenya kwa hiyo inawezekana kabisa tukawa tunajenga bomba kwa gharama kubwa ili kusafirisha gesi kutoka pointi moja yenye kidogo sana kwenda pointi nyingine yenye gesi yake nyingi zaidi, inayotosheleza na kubaki.
    Ujenzi wa mabomba kwa ajili ya usafirishaji wa gesi nyingi umbali mkubwa ndani ya nchi yetu ni muhimu ukawa na udhibitisho kwamba hatutoi pointi hii kupeleka pointi ile yenye gesi yake nyingi inayotosheleza na kubaki. Lakini hili halitakuwa tatizo iwapo gridi ya umeme badala ya gridi ya gesi itajengwa kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
    Gridi ya umeme utokanao na gesi asilia ikiwepo kati ya Mtwara na Dar es Salaam itakuwa kianzio kipya na itakuwa ni boresho la uhakika wa sekta ya umeme ya taifa na kwa vile inaanzia karibu sana na machimbo makubwa ya gesi huko Msumbiji basi itakuwa rahisi kuunganisha grid ya Msumbiji na ya Tanzania itakapobidi hapo baadaye.
    Mikoa ya kusini ndiyo iliyobaki bila kuunganishwa na grid ya taifa kwa muda mrefu kutokana na kutokuwa na kianzio cha umeme kinachofaa lakini kwa vile kianzio kizuri cha gesi asilia sasa kimepatikana basi umeme wa gesi uzalishwe huko Mtwara na grid ya umeme ijengwe kutoka Mtwara hadi Dar ili kuwezesha pia mikoa ya kusini kuunganishwa na gridi ya taifa. Ni vizuri ikazingatiwa kuwa umeme utokanao na gesi asilia unakuwa wa faida zaidi unapozalishwa na kutumika karibu zaidi na machimbo ya gesi.
    Gharama ya ujenzi wa gridi ya umeme ni karibu mara mbili ya gharama ya ujenzi wa bomba la gesi lakini ni kidogo sana ukilinganisha na uwingi na ukubwa wa faida zitakazotokana na kuwepo gridi ya umeme kati ya Mtwara na Dar es Salaam ambazo ni zaidi ya zitakazopatikana kutokana na kuwepo bomba la gesi kati ya Mtwara na Dar es Salaam kwa kipindi chote cha uhai wa mradi. Ukweli ni kwamba hata kama bomba lingekuwa tayari liko ardhini, bado ingekuwa faida kubwa zaidi kuliacha huko ardhini na umeme na bidhaa nyingine kutokana na gesi asilia ya Mtwara zikazalishwa huko Mtwara na grid mpya ya umeme ikajengwa kusafirisha hadi Dar es Salaam. Mabonde makubwa na mazuri mno kwa kilimo cha kisasa cha umwagiliaji kama bonde la mto Ruvu na bonde la mto Rufiji bado hayaendelezwi hasa kutokana na kukosekana kwa umeme wa uhakika.
    Kwa hiyo nakubaliana na Mh Zitto kwa hili na ni muhimu wanasiasa wakawa pamoja kwenye hili, wakakaa pembeni na kuwaachia wataalamu husika wakanya upembuzi yakinifu kuhusu manufaa ya umeme utokanao na gesi ya Mtwara ukazalishwa huko huko Mtwara badala ya Dar es Salaam na kusafirishwa kwa gridi mpya ya umeme hadi Dar eslaam.

    Dr Antipas Massawe

    January 21, 2013 at 9:55 AM

  7. NASIKITIKA KWA KUWA TAYARI NILISHAWAHI KUSIKIA KUWA KUNA ENEO LILILOPO TEMEKE LINA GESI NA INAFAHAMIKA!KWA NINI TENA ITOKE MTWARA IJE PIA HUKU?SI KILA KITU KIJE KWA WALA CHAO HAPA MJINI,NOWDAYS HAKUNA WAJINGA WAJINGA TANZANIA HII!!!!! WANAMTWARA NI WAKATI WA KUIKATAA CCM HUKO MLIKO

    Tito Mwakipesile

    January 21, 2013 at 10:37 AM

  8. Zito hajapinga kisongo ila anataka haki itendeke

    Khalid

    January 22, 2013 at 9:46 PM

  9. Jamani ndugu zanguni,
    Mnyonge mnyongeni ila haki yake mpeni,Watu wa kusini hawakatazi matumizi ya gas kwa watanzania,wanachodai nafasi yao ya kupata ajira.
    Ijengwe mitambo ya kufua gas Mtwara halafu usafilishwe umeme kugawanya mikoa yote Tanzania na kama tuna nia ya kuuza gas meli zienge zikapaki katika bandari ya mtwara kupakia mzigo.
    NB
    Haiwezekani mtu kukaa na mtungi wa pafyum ukakosa kunukia,

    Khalid

    January 22, 2013 at 9:53 PM

  10. […] tena: Tusipuuze mandamano dhidi ya Bomba la Gesi: Kilio cha Uwajibikaji; Nikaandika tena: Mtwara : Serikali inavunja nchi kwa kutosikiliza Wananchi; ni baadhi ya makala nilizoandika kuhusiana na suala la […]

  11. ukishakua kiongozi unapaswa kuchunguza matamshi yako kabla ujatamka mbele ya hadhala yaunao waongoza kiukweli kauli yakusema gesi iendee dar nisawa na mtoto umzae wewe na apewe mama mwingine ..

    omar hassan

    November 2, 2013 at 10:00 AM


Leave a comment