Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Nitaishi kuwa Meles Zenawi

with 15 comments

 

Nitaishi kuwa Meles

 

Mwaka 1975 Mwanafunzi wa mwaka wa Kwanza wa Chuo Kikuu cha Haile Selasie (sasa Chuo Kikuu cha Addis Ababa) Legese Zenawi, akiwa na umri wa miaka 19 tu, aliacha masomo yake na kujiunga na kikundi cha Ukombozi cha watu wa Tigray (Tigray Peoples Liberation Front). Legese alikuwa anasomea shahada ya kwanza ya udaktari. Hakurudi tena Chuoni kusomea Udaktari na hakuishi tena maisha ya ujana ambayo sisi wengine wote tumeishi na kuyafurahia. Mwaka 2012 Legese akiwa na umri wa miaka 57 alifariki dunia. Lakini aliaga dunia akiwa Meles Zenawi na sio Legese Zenawi, jina alilopewa na wazazi wake huko Adwa kaskazini mwa Ethiopia.

 

Legese alibadili jina lake kwa hiari yake kufuatia kuuwawa kwa rafiki yake na mpiganaji mwenzake Meles mwaka 1975. Aliamua kumuishi mpiganaji mwenzake kwa kuchukua jina lake na kuacha jina alilopewa na wazazi wake. Meles alifanikiwa kupigana dhidi ya utawala wa kiimla wa Mengistu Haile Mariam na kumtoa madarakani na kuingiza uongozi wa kimaendeleo chini ya chama cha Kitaifa cha Ethiopian People’s Revolutionary Democratic Front (EPRDF). Meles Zenawi aliahidi kumpigania rafiki yake Meles kwa faida ya wananchi wanyonge wa Ethiopia na akatimiza ahadi hiyo kwa mafanikio makubwa sana.

 

Mwanzoni Meles alipigana kwa lengo la kutaka uhuru wa eneo la Tigray kutoka Utawala wa Mengistu na kundi la wanajeshi chini ya Derg. Meles na wenzake waliamini kabisa kwamba utawala nchini mwao chini ya Mfalme Haile Selasie na hata chini ya utawala wa Derg uligubikwa na ukabila na ueneo kwa faida ya kabila kubwa nchini humo, Amhara.Aliamini kwamba makabila madogo kama kabila lake la Tigray kutoka kaskazini mwa Ethiopia na hata makabila mengine kama Wasomali walikuwa wanakandamizwa na kunyonywa ndani ya nchi yao. Aliamini kwamba utajiri wa nchi ulikuwa unatumika kwa faida ya kundi moja lililohodhimadaraka ya nchi na kabila lao. Akiwa na umri wa miaka 19 tu na mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu aliamua kushika silaha na kupambana na ugandamizaji huu.

 

Hata hivyo Meles alibadili kabisa mtazamo wake alipogundua kuwa sio watu wa Tigray tu waliokuwa wakinyonywa na kugandamizwa na utawala wa Mengistu bali ilikuwa ni WaEthiopia wote bila kujali makabila yao. Mwaka 1985 alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama cha TPLF akiwa na umri wa miaka 29 tu.Alihakikisha anaikomboa Tigray kama mkakati wa kuikomboa Ethiopia yote. Alishirikiana na wakombozi wa Jimbo jirani la Eritrea ili kutetea Uhuru wao na kuwapa uhuru wa kuamua kama wanataka kubakia sehemu ya Ethiopia au kuwa Taifa huru ambapo waliamua kuwa Taifa huru. Akiwa kijana wa chini ya umri wa miaka 30 aliunganisha makundi mbalimbali yaliyokuwa na lengo la kuleta ukombozi na kujenga Ethiopia mpya chini ya mwavuli ya chama cha EPRDF. EPRDF ilikuwa ni umoja wa makabila yote nchini Ethiopia na walimchagua Meles kuongoza mapamabano ya ukombozi.

 

Mwaka 1991 Meles Zenawi aliongoza EPRDF kuingia Addis Ababa na kushika Dola huku Mengistu akikimbilia nchini Zimbabwe. Meles akiwa na umri wa miaka 36 tu alichaguliwa kuwa Rais wa muda wa Ethiopia na mkutano mkuu wa kitaifa ambao kwa mara ya kwanza ulikutanisha makabila yote nchini Ethiopia. Miaka mitatu baadaye kufuatia kura ya maoni Jimbo la Eritrea likajitenga kutokaEthiopia na kuunda Taifa huru. Meles alitimiza ahadi yake ya kuruhusu watu wa Eritrea kuamua kama wanataka kuwa Taifa linalojitegemea au kuwa sehemu ya Shirikisho la Ethiopia. Hata mahusiano kati ya Ethiopia na Eritrea yalipokuwa mabaya sana kiasi cha kupigana vita kugombea kijiji cha Badme, Meles hakuchukua fursa hiyo kuirudisha Eritrea kuwa mkoa ndani ya Ethiopia au hata kupata njia ya kwenda baharini, bali aliheshimu matakwa ya waEritrea ya kujitawala.

 

Ukweli ni kwamba vita kati ya Eritrea na Ethiopia ilikuwa ni vita isiyo na maana yeyote ile na itabakia kuwa doa katika historia ya uongozi wa Meles. Kitendo cha Meles kutoheshimu maamuzi ya Umoja wa Mataifa kwamba Badme ni sehemu ya Eritrea pia ni doa ambalo wafuasi wa Meles wataendelea kuwa nalo daima dumu na wakosoaji wa Meles wataendelea kujengea hoja kuonyesha kuwa Kiongozi huyu hakuwa anaheshimu maamuzi ya Taasisi za kimataifa. Hata hivyo doa hili haliwezi kufuta kabisa mafanikio makubwa ambayo kamaradi Meles ameyapata katika Ethiopia iliyokombolewa.

 

Meles alipochaguliwa kuwa Kiongozi wa chama cha TPLF mwaka 1985 Ethiopia ilikuwa kwenye ramani ya dunia kama Taifa lililoshindwa kulisha watu wake. Dunia nzima kulikuwa na kampeni za kusaidia kuondoa njaa nchini humo ambayo iliua zaidi ya watu milioni moja. Wakati mauaji ya kimbari nchini Rwanda yaliua watu milioni moja kwa mapanga na mashoka, njaa iliua watu kama hao hasa katika maeneo ya Tigray na Wollo kwa sababu ya uzembe wa Serikali ya Mengistu. Mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu wa chama cha Mengistu kilichokuwa kinatawala wakati ule (Workers Party of Ethiopia) bwana Dawit Wolde alimtahadharisha Mengistu kuhusu hali mbaya ya wananchi na kwamba Serikali ilipaswa kuchukua hatua na kujibiwa ‘kulikuwa na mabaa ya njaa miaka yote kabla sisi hatujatawala. Hiyo ni namna uasili (nature) inafanya kazi yake. Kuingilia uasili ndio maana leo tumefikia watu milioni 40’( Meredith in The State of Africa). Mengistu alilewa madaraka kiasi cha kusahau kwamba siku moja kabla ya kumvua madaraka Mfalme Haile Selasie walimwonyesha filamu (The hidden famine) ya namna yeye alivyokuwa anastarehe na pombe aghali na kulisha nyama mbwa wake ilhali wananchi wake walikuwa wanakufa kwa kukosa chakula katika baa la njaa la mwaka 1984 katika Wilaya ya Wollo. Haile Selasie baada ya kuonyeshwa filamu hiyo alipoteza fahamu kwa mawazo na siku iliyofuata tarehe 12 Septemba 1974 akavuliwa ufalme na vijana watatu wanajeshi akiwemo Mengistu Haile Mariam. Mengistu huyo huyo akiwa Rais wa Ethiopia akawa anajenga hoja kwamba njaa ni tukio la asili ili ‘kubalance’ idadi ya watu nchini mwake! Haya ndio mazingira ambayo Meles alichaguliwa kwayo kuongoza mapambano ya ukombozi akiwa na umri wa miaka 29 tu.

 

‘naomba vitabu vya Uchumi’ ndio ombi pekee Meles alilitoa kwa  mwanahabari wa kigeni aliyekwenda kumfanyia mahojiano mara baada ya kuchukua uongozi wa Taifa lake. Mwanahabari huyo alimwuliza ni msaada gani anataka kutoka kwa nchi za magharibi ili awaambie kupitia habari yake anayokwenda kuandika. Meles alijua kwamba ana ajenda moja kubwa nayo ni kuondoa njaa. Kuondoa Umasikini nchini mwake. Ajenda hii Meles aliifanyia kazi kwa nguvu zake zote kipindi chote ambacho yeye alikuwa Rais na Baadaye Waziri Mkuu wa Ethiopia.

 

Nakumbuka tulikuwa tunatania mtu yeyote aliyekondeana kwa kusema ‘ana njaa kama Ethiopia’ na hiyo ndio ilikuwa picha inayokuja machoni mwa watu wengi duniani kuhusu Ethiopia. Meles hakumaliza shida zote za Ethiopia, lakini alipambana nazo. Alizipunguza. Amelitoa Taifa lake kutoka Taifa la kupigiwa mfano kwa njaa na umasikini kwenda Taifa la kupigiwa mfano kwa maendeleo. Katika kipindi cha miaka ishirini ya utawala wake hatujasikia baa kubwa la njaa kama ilivyozoeleka kila muongo nchini humo. Mwana historia mmoja nchini humo alionyesha kuwa kila muongo ulikumbwa na njaa kali nchini Ethiopia, 1958, 1966, 1973 na 1984. Lakini toka Meles achukue uongozi wa Taifa la Ethiopia hatukusikia njaa miaka ya tisini wala miaka ya 2000. Ninaamini watakaomrithi Meles watahakikisha kuwa hakuna njaa tena ya kiwango kile nchini Ethiopia kwa miongo mingine yote ijayo. Mafanikio haya yanatokana na sera na maamuzi thabiti na ya dhati kutoka kwa kiongozi ‘Sitaki njaa nchini kwangu’. Pia usimamizi thabiti wa maamuzi sahihi yaliyotolewa.

 

Meles aliamua kupambana na umasikini na kujenga Taifa lenye nguvu za kiuchumi. Aliamua mapema kabisa kukataa ushauri wa IMF na Benki ya Dunia wa kuufungua uchumi wa Ethiopia haraka sana (liberalisation). Yeye na wenzake waliamua kuufungua uchumi kidogo kidogo kulingana na ratiba waliyojiwekea wao wenyewe. Kutokana na hali hiyo sehemu kubwa ya uchumi wa Ethiopia umeshikwa na wao wenyewe wananchi wa Ethiopia. Amejenga miundombinu kuunganisha uchumi wa nchi na hivyo kufungua masoko ya ndani licha ya yeye mwenyewe Meles kusisitiza sana mauzo ya nje. Kutokana na maamuzi yake, hivi sasa Ethiopia itaanza kuuza nje Viatu vya ngozi vilivyotengenezwa nchini humo vyenye thamani ya dola za kimarekani bilioni nne. Hii ni sawa na mara mbili ya mauzo ya dhahabu yote ya Tanzania kwenye soko la dunia. Ethiopia haina mafuta wala madini ya kutosha kama Tanzania, lakini uchumi wake umekuwa ukikua kwa zaidi ya asilimia kumi kwa miaka saba mfululizo. Ndio maana Meles ameweza kupunguza umasikini kutoka asilimia 45 ya watu waliokuwa wakiishi kwenye dimbwi la umasikini mwaka 1991 mpaka asilimia 29 mwaka 2011. Katika kipindi kama hicho (1991 – 2011) Umasikini Tanzania ulishuka kutoka asilimia 37 ya watu kuishi kwenye dimbwi la Umasikini mpaka asilimia 35 tu. Tanzania iliamua kufuata sera za kufungua uchumi wa nchi kwa haraka kama walivyoshauri Taasisi za IMF na Benki ya Dunia.

 

Wakati Meles anaaga dunia ameacha mradi mkubwa sana unatekelezwa nchini mwake. Mradi wa kuzalisha umeme 10,000 MW, Grand Millenium Project. Lengo lake ni kuzalisha umeme wa kutosha kufanya mabadiliko makubwa ya maisha ya wananchi wa Ethiopia na pia kuuza nchi jirani (Diplomasia ya Nishati). Benki ya Dunia ilikataa kufadhili mradi huu, yeye akaamua kila muEthiopia kutoa fedha za kufadhili mradi huu. Wananchi wa Ethiopia wote kila mmoja akajitolea mshahara wake wote wa Mwezi mmoja na fedha hii kugeuzwa kuwa dhamana. Pia wananchi wa Ethiopia wanaoishi nje ya nchi nao waliruhusiwa kununua dhamana hizi na kufadhili mradi huu kabambe. Mradi unatekelezwa kwa fedha za WaEthiopia wenyewe. Nina imani kuwa mradi huu utaendelezwa na viongozi wapya wa Ethiopia. Uzuri ni kwamba Meles alilea kizazi kipya cha uongozi. Aliamua kuchukua vijana wa rika mbili chini yake na kuwapa majukumu na kuwalea kiuongoni ili waweze kuwa tayari kurithi mikoba ya viongozi wanaomaliza muda wao. Waziri Mkuu mpya wa Ethiopia ana umri wa miaka kumi chini ya Meles. Meles alijua umuhimu wa kuandaa viongozi wa baadaye. Yeye hakuandaliwa. Mazingira ya ugandamizwaji, unyanyasaji na umasikini yalimwita kuchukua majukumu ya kiuongozi akiwa kijana mdogo sana wa miaka 19 alipoamua kujiunga na jeshi la ukombozi, miaka 29 alipochaguliwa kuongoza jeshi la ukombozi na miaka 36 alipochaguliwa kuwa Rais na baadaye Waziri Mkuu wa Taifa lake.

 

Meles ana makosa yake kama binaadamu. Amelaumiwa sana na mataifa ya magharibi kuhusu rekodi yake ya masuala ya haki za binaadamu na kidemokrasia. Lakini pia amelaumiwa na baadhi ya wanaharakati kwa kuuza ardhi ya wananchi kwa makampuni ya kilimo ya mashariki ya kati na mashariki ya mbali kama China. Hata hivyo sijawahi kusikia tuhuma zozote za Meles kuhusu ufisadi na kujilimbikizia mali. Siku zote aliamini kuwa cheo ni dhamana na hakutumia cheo chake  kwa faida yake tofauti na viongozi wengi sana wa kiafrika. Hapa nchini kwetu tunashuhudia watu wakitumia nafasi zao za uongozi kulimbikiza mali. Watu wana tamaa iliyokithiri ya mali. Ufisadi imekuwa ni hulka na sasa ufisadi unahusisha nafasi yeyote ya uongozi. Hata tuhuma za ufisadi na rushwa zimekuwa za kawaida mno mpaka unakuta wala rushwa wanatuhumu viongozi wenye maadili ili mradi tu ionekane rushwa ni ya kila mtu wa kila chama. Imekuwa kama Wezi kuungana kumkimbiza Polisi. Meles hakutaka Ethiopia ifikie hali hii. Alipambana na rushwa yeye mwenyewe kwa kujiwekea viwango vya kutokuwa na mawaa ya rushwa au matumizi mabaya ya Ofisi ya Umma.

 

Meles Zenawi ameacha mfumo wa Uchumi ambao haujapata fursa ya kujadiliwa vya kutosha. Mfumo ambao umeiweka Ethiopia kuwa moja ya mataifa yatakayokuwa na nguvu kubwa ya kiuchumi katika bara la Afrika ndani ya muongo mmoja na nusu ujao. Meles alipambana na umasikini kwa dhati na kwa nguvu inayostahili. Meles ametimiza wajibu wake.

 

Natamani kuwa Meles maana ameishi anachoamini kwa kupambana na ufisadi bila yeye kuwa fisadi ama kutumia vibaya Ofisi yake ya Umma. Nitaishi kuwa Meles maana adui wetu nambari moja ni Umasikini, umasikini wa vijijini. Meles alitangaza mwaka 1991 ‘our first enemy is poverty and backwardness’ na akapambana na adui umasikini kadiri ya uwezo wakeHakuna namna bora zaidi ya kumuenzi Meles zaidi ya kutenda yale mema aliyoyatenda na kurekebisha yale aliyoyakosea.

 

Nilipata fursa ya kukutana na Meles mara moja. Nilikutana naye nchini Nigeria katika mkutano kuhusu mashirikiano ya kiuchumi kati ya nchi za Ulaya na nchi za Kiafrika mwaka 2009. Baada ya mkutano ule niliamua kumsoma Meles na misingi anayosimamia. Ni kama nilimwona Mahathir Mohamad wa Malaysia ndani ya Meles Zenawi kwa namna ya utendaji wao na uwezo wao wa kujenga hoja. Isipokuwa tu Meles hakumaliza shahada yake ya udaktari na Mahathir alimaliza yake. Ni dhahiri kwamba Meles Zenawi alikuwa ni kiongozi mwenye uwezo mkubwa sana kiakili pengine kuliko viongozi wote wa kizazi cha pili barani Afrika. Uwezo wake wa Akili uliwatisha viongozi wa mataifa ya Magharibi. Walimwogopa. Wenzake wa Afrika walimheshimu. Alikuwa sauti ya Afrika kutoka Addis Ababa, Makao makuu ya Afrika.Upumzike kwa amani Meles.

Written by zittokabwe

August 28, 2012 at 2:41 PM

Posted in Uncategorized

15 Responses

Subscribe to comments with RSS.

  1. Legacy ya Meles ni haibu kwa viongozi wengi waliohai Afrika…Hasa Tanzania,Nachelea kuwaita ‘Batch of incompetent fools’

    haroun

    August 28, 2012 at 3:21 PM

  2. Well written, hongera sana kamanda1

  3. […] Alikuwa sauti ya Afrika kutoka Addis Ababa, Makao makuu ya Afrika.Upumzike kwa amani Meles. Chanzo:Zitto na Demokrasia.     Tweet   […]

  4. tuko pamoja katika kumuishi zenawi lakini ni wangapi tuna moyo kama wake

    anderson

    August 28, 2012 at 4:35 PM

  5. Kiongozi bora hufanikisha malengo akipata kuungwa mkono na wananchi anaowaongoza, kazi kubwa ya kufanya ni kuwapatia elimu wanchi juu ya mambo yanayowahusu wao binafsi na mambo yanoyoihusu nchi yao. Ndoto za kuwa kama viongozi ambao wameonyesha mafanikio makubwa katika nchi walizoongoza ni hatua moja wapo, lakini kubwa zaidi nikuwaelimisha wananci ili wajue kwa nini wapo kama walivyo sasa, ili waunge mkono wanaharakati wa ukombozi. Nidhahiri kuwa MH. ZITTO unaweza kuonyesha mabadiliko makubwa katika siasa na uongozi nchini Tanzania licha ya kuwa ZENAWI na MAHADHIR MOHAMAD hawana utofauti katika kujenga hoja na kuzitetea ili kuzifanyia kazi pia naamini kuwa upo na utakuwa mstari wa mbele katika kutetea maslahi ya watanzania. Pia ni vyema ukazielekeza nguvu nyingi katika kuwaelekeza vijana kwani wao ndo messengers kwa wazee. Tunaamini kwa pamoja kuwa Tanzania bila kupata viongozi shupavu na wapenda maendeleo ya wote hatuwezi piga hatua yoyote katika maendeleo. KEEP IT UP HM. ZITTO

    IBRAHIM HASAN NTAHONDI

    August 28, 2012 at 6:16 PM

  6. Kazi nzuri sana kaka Zitto. Naleta changamoto kwako…Tafadhali fanya uwe unaandika mara kwa mara kuhusu mashujaa wetu mbali mbali Afrika na baadae iwe kwenye mfumo wa kitabu, Bongo imepoteza ufahamu wa umajumui Afrika.

    Zavara Mponjika

    August 28, 2012 at 8:19 PM

  7. […] as I told Mr. Zitto Kabwe, Kigoma North MP-CHADEMA (Mr. Kabwe shares his views on Mr. Zenawi here), who was seated beside me, the word ‘vision’ was mentioned the most and it demonstrated that […]

  8. This is a fair analysis about Meles and the state of Ethiopia to some extent. I have read your article after reading Ahmed Salim’s.

    I have been to Ethiopia a couple of times, used their infrastructures flying and driving to the remote part of the country. It’s a country out of ruins but with a clear and eady to appreciate focus. Their airline, airports, tourism and commerce is a clear indication of a properly managed country with balanced economic strategies.

    Some criticism though, many Ethiopians were politically afraid to comment on anything linking to the government. Some severe pockets of extreme poverty can still be seen and felt in rural Ethiopia even In Addis than in a few African countries I have been.

    Whether Meles was a benevolent dictator or a cautious economic-patriot will be judged by the his legacy and events following his succession.

    Fabian

    September 4, 2012 at 5:15 AM

  9. kweli uko sawa mkuu timiza ndoto zako na iga toka kwa waliofanikiwa ili wakutie moyo.

    jasson taifa

    September 6, 2012 at 10:40 AM

  10. Zenawi a benevolent?

    Human Rights Watch (HRW) in their detailed report ‘Development without Freedom’ (DWF) quoted Meles Zenawi saying that “when Revolutionary Democracy permeates the entire society, individuals will start to think alike and all persons will cease having their own independent outlook. In this order, individual thinking becomes simply part of collective thinking because the individual will not be in a position to reflect on concepts that have not been prescribed by Revolutionary Democracy.”

    That is the true face of Zenawi

    Sabodo

    September 20, 2012 at 5:38 AM

  11. big up kaka,ive living in ethiopia 4 the past decade,am tanzaniano of somali orijin living in ogaden province,ulichoandika ni kweli naomba uige mazuri ya huyu mhe.na utakumbukwa na generations zijazo,alikuwa strict na viongozi wake sio kama tz ushikaji umezidi,ufisadi hamna kabisa na viongozi ni wafanyikazi wa raia

    ali bonge

    October 22, 2012 at 6:09 PM

  12. Zitto,

    You have over extended yourself in trying to make a comparison between Zenawi’s Ethiopia and Tanzania. In particular the comment, “Tanzania did as it was advised by the IMF and the World Bank and opened its economy,” is misleading. As you know well Tanzania under Mwalimu J.K. Nyerere DID refuse IMF and World Bank advise – we were forced to accept after our economic policies failed.

    Zenawi did what we – i.e.. CCM leadership pre:Mkapa – failed to do and that was to “read basic books on economics”. The mark of Zenawi was his willingness to engage on ideas pragmatically…this, inTanzania we have failed to do. Also, never underestimate the power of a revolutionary to start afresh and start from scratch all-over again: Tanzania never had this option. My prayer is that it never will for we will just repeat the chaos and anarchy of our neighbours let-alone the needless deaths as seen in Ethiopia itself.

    I belief through pragmatic and considered steps/change we can move forward and overtake Ethiopia…this change for us will need to see a change in the party in government for CCM do need to rest. I am not sure if Chadema will be the ones to replace them though for it could be a CCJ variety of party that needs to rise for you have internal challenges.

    Apart from that, this was an informative piece. Asante kaka.

    Barikiwa,

    Majaliwa

    Maj

    October 22, 2012 at 7:44 PM

  13. Hi there! This blog post could not be written any better!
    Going through this article reminds me of my previous roommate!
    He constantly kept preaching about this. I am going to forward this information to him.
    Pretty sure he’ll have a good read. Many thanks for sharing!

    Jade

    November 20, 2012 at 11:46 PM

  14. Asante sana kwa makala hii inavutia mno. Mimi ni mtanzania naishi USA, huu mwaka wa nne sasa kweli natamani mno kama nchi yangu ingeiga demokrasia ya USA. Hapa rais hana maguvu kama huko bongo, watu ndio wana nguvu wanalo taka linakuwa. Hii ni kinyume kabisa na huko kwetu. Maoni yangu kila mkoa Tanzania upewe haki ya kuendesha maendeleo yake, na wakuu wa mikoa wachaguliwe na wananchi wanaowaongoza. Nashangaa mno kuona mkuu wa mkoa anawatukana wananchi kuwaita wapuuzi na waziri anawasimama bila aibu kuwazodoa wananchi wa mikoa ya kusini kwa kiu yao ya mendeleo yao . Mimi nilizaliwa Lindi na kuishi Dar kwa muda mrefu kweli kama kweli tunataka Tanzania isitawi lazima tusikilize wanachotaka wananchi itapendeza mno kila mkoa uwe na katibu yake na utawala wake na kubaki nchi moja hii itasaidia kudhibiti fat cat manyang’ao mafisadi wanaotaka kuthibiti wananchi wanyonge jogoo amewika sasa tunashukuru Mr. zitto kwa kusimama na wanyonge jaj

    Maarufu

    January 19, 2013 at 8:12 PM

  15. […] as I told Mr. Zitto Kabwe, Kigoma North MP-CHADEMA (Mr. Kabwe shares his views on Mr. Zenawi here), who was seated beside me, the word ‘vision’ was mentioned the most and it demonstrated that […]


Leave a comment