Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Posts Tagged ‘Wakulima

HIFADHI YA JAMII KWA SEKTA ISIYO RASMI[1]

with 2 comments

HIFADHI YA JAMII KWA SEKTA ISIYO RASMI[1]

Zitto Kabwe[2]

Hifadhi ya Jamii ni sera ya Maendeleo. Ni sera inayolenga kuendeleza Maisha ya Watu na kuhakikisha kuwa Watu wanaofaidika na sera hiyo kutotumbukia kwenye dimbwi la Umasikini. Ni kinga dhidi ya kuporomoka kwa kipato kutokana na kifo, ulemavu au Umri. Wanazuoni wanahusisha Hifadhi ya Jamii na tafsiri ya Maendeleo ambayo inajikita kwenye uwezo (capability) ambapo maendeleo yanahakikishwa hata kama mtu hana uwezo wa kufanya kazi. Kwenye mada iliyowalishwa kuhusu uzoefu wa Ghana tumeona namna sekta ya Hifadhi ya Jamii ya Nchi hiyo ilivyoasisiwa kwa kuanzia akiba ya lazima mwaka 1960 mpaka mfumo wa pensheni mwaka 2010 kupitia Shirika la Umma lililoundwa mwaka 1972 (Social Security and National Insurance Trust – SSNIT). Tanzania ilianza mfumo wa Akiba ya Wafanyakazi mwaka 1964 kama tulivyoelezwa katika historia ya Shirika la Hifadhi ya Jamii nchini (NSSF) na kuingia kwenye mfumo wa pensheni mwaka 2001. Nchini Ghana mfumo wa kujiwekea akiba kwa hiari (voluntary scheme) umewekwa kwenye sheria zao mbali mbali. Hata hivyo, wakati asilimia 86 ya nguvu kazi ya Ghana ipo katika sekta isiyo rasmi, ushiriki wa wananchi wa nchi hiyo katika Hifadhi ya Jamii ni mdogo kwa kiwango cha 1.23% ya wanachama wote wa mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini humo. Kwa kuwa mada ya uzoefu wa Ghana na changamoto zake imezungumzwa tayari, tutaona ni namna gani Tanzania inaweza kupanua wigo wa Hifadhi ya Jamii kwa kuhakikisha kuwa wananchi wengi Zaidi wanafikiwa.

Katika kipindi cha miongo miwili sasa maendeleo makubwa yamefanyika katika sekta ya Hifadhi ya Jamii nchin katika sera na sheria. Hifadhi ya Jamii imetoka mifuko ya Akiba mpaka mifuko ya Pensheni. Hata hivyo kama ilivyo kwa Ghana bado Hifadhi ya Jamii kwa Tanzania ni uwanja wa Wafanyakazi wa sekta rasmi, waajiriwa wa serikali, mashirika ya umma na makampuni binafsi. Watanzania wengi waliojiajiri na walio katika sekta isiyo rasmi hawamo katika mfumo wa Hifadhi ya Jamii. Takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa Watanzania wengi wapo kwenye sekta isiyo rasmi. Takribani asilimia 70 wapo kwenye ukulima mdogo mdogo (vibaku kwa lugha ya Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi) na wengine asilimia 10 wamejiajiri kwenye shughuli mbalimbali kama biashara ndogondogo, madini, Sanaa, michezo na uchuuzi mwingine. Watanzania wenye ajira rasmi ni sehemu ndogo sana ya nguvu kazi ya Tanzania. Ni dhahiri kuwa Hifadhi ya Jamii Tanzania inawahusu watu kiduchu sana, takribani asilimia 6 tu ya nguvu kazi ya nchi na asilimia 3 tu ya Watanzania wote. Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2013 inaonyesha kuwa wanachama wa mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii nchini ni takribani 1.1 milioni.

Hili ni janga la Taifa. Rundo kubwa la wananchi hawachangii katika kapu la pensheni hivi sasa, hii maana yake ni kwamba huu ni mzigo mkubwa sana na usiokwepeka kwa Taifa pindi idadi ya wazee itakavyoongezeka katika kipindi cha miaka michache ijayo. Tusifumbwe na muundo wetu wa idadi ya watu hivi sasa ambapo Zaidi ya nusu ya Watanzania wana umri chini ya miaka 18 na asilimia 72 wana umri chini ya miaka 30. Hili kundi la watoto linaweza kuwa gawio (demographic dividend) iwapo tutajipanga vizuri. Tusipojipanga hili ni bomu ambalo likilipuka tutatafutana. Ipo siku itafika ambapo hili kundi la watoto halitakuwa na uwezo wa kufanya kazi tena lakini itabidi livishwe na kulishwa. Viongozi wenye maono mapana ya nchi lazima wawe na matayarisho katika masuala kama haya ya nchi. Majawabu yapo nayo ni kuhakikisha kuwa Hifadhi ya Jamii inahusisha watu wengi Zaidi kwa kuandikisha watu katika sekta isiyo rasmi na hasa wakulima na wafugaji, wavuvi na wachimbaji madini, wafanya biashara ndogondogo na wengineo. Huko ndipo pa kuelekea kama kweli tunataka kuwa na Tanzaia imara, bora na yenye neema. Hata hivyo suala hili linahitaji utashi wa kisiasa na maamuzi.

Kuna watu wanaweza kudhani kuwa jambo hili ni ndoto za alinacha. Linawezekana sio tu kwa sekta isiyo rasmi bali kila mwananchi mwenye uwezo wa kufanya kazi ataona umuhimu wa Hifadhi ya Jamii. Hata kwa nchi kama Tanzania jambo hili linawezekana. Kuna mifano kadhaa ya nchi ambazo zimefanikiwa katika jambo hili na kupiga hatua kubwa. Nchi hizi ni kama vile Korea ya Kusini, Thailand na China. Nchi ya China imepata mafanikio makubwa sana kwa kufikisha hifadhi ya jamii kwa wakulima vijijini. Serikali za nchi hizo zimeshikiriana na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuhakikisha raia wao wengi wanapata ulinzi wa kijamii ili kupambana na umasikini.

Mkutano na Wakulima wa Kahawa

Mkutano na Wakulima wa Kahawa

Hapa Tanzania tumejaribu katika Mkoa wa Kigoma, Jimbo la Kigoma Kaskazini ambapo wakulima 750 wa Kahawa kupitia chama cha Ushirika cha Msingi kinachoitwa RUMAKO walijiunga na NSSF mwaka 2013 mwezi Machi. Katika mkutano huu tulishuhudia Mwenyekiti wa Ushirika huo Mzee Yahaya Mahwisa akitoa ushuhuda mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndugu Jakaya Kikwete namna RUMAKO ilivyofaidika baada ya kujiunga na hifadhi ya jamii. Hivi sasa wakulima hawa wana bima ya afya kupitia mpango wa SHIB wa NSSF, wanapata mikopo ya riba nafuu ili kununua Kahawa kwa ajili ya kuuza kwenye mnada na mikopo ya kuboresha mashamba yao na kuongeza ubora wa kahawa na hivyo mapato yao. Kutokana na mafanikio makubwa ya ya RUMAKO vyama vingine 11 vya Ushirika vya Msingi vimejiunga na NSSF katika mkoa wa Kigoma. Vilevile tumeshuhudia Shirika la NSSF likiingia makubaliano ya kikazi na Tume ya Ushirika nchini ambapo Zaidi ya wakulima 400,000 wataandikishwa kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Vile vile tumeshuhudia wachimbaji wadogo wadogo wa madini wakijiunga na Hifadhi ya Jamii. Hatua zote hizi zinatokana na ukweli kwamba RUMAKO imewafungua macho NSSF na sasa inapasa kufungua macho mifuko mingine yote nchini na Serikali ili kufanya mapinduzi makubwa sana katika sekta ya Hifadhi ya Jamii nchini Tanzania.

Sekta ya Kilimo na Sekta ya Madini ni mwanzo mzuri kwa sababu licha ya kwamba ni sekta zisizo rasmi lakini pia ni sekta zenye historia ya kuwa na vyama vya ushirika. Kwa kuwa itakuwa ni changamoto kubwa sana kuandikisha mwanachama mmoja mmoja kwani utawala wake utakuwa mgumu sana, kuandikisha kupitia vyama vya ushirika kutasaidia kuondoa changamoto hizo. Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ikiwafikia wakulima ni kama imelifikia Taifa zima maana wao ndio wengi na kwa kweli wakiwa na taarifa za kutosha watafurahia mipango hii. Hata hivyo maeneo mengine kama michezo yanaweza kuwa rahisi kuandikisha kwa Serikali kuweka kanuni kwamba mikataba ya wachezaji na Timu zao ni lazima iwe na kipengele cha Hifadhi ya Jamii. Hii itaondoa kabisa tatizo kubwa la wachezaji wetu hasa wa soka kuishi maisha hohe hahe baada ya kustaafu. Upande wa Sanaa pia na hasa kwa wanamuziki jambo hili linaweza kutekelezwa. Muhimu ni ni kwa mifuko ya Hifadhi ya Jamii kufikisha ujumbe huu kwa wananchi na Serikali kuweka vivutio kwa watu kuweka akiba.

Msingi wa ukuaji wa uchumi wa nchi ni akiba. Uwekezaji wa ndani unahusiana kabisa na uwekaji akiba wa nchi, ndio nadharia za uchumi zinasema. Nchi haiwezi kutegemea tu uwekaji kutoka nje kwani uhuru wa nchi unakuwa hatarini. Nchi zilizoendelea zinaita mitaji kutoka nje kwa sababu tayari mitaji ya ndani imezidiwa. Sisi Tanzania mitaji ya ndani wala hatuna mipango nayo. Hivyo Serikali yeyote makini ni lazima ihamasishe wananchi wake kuweka akiba ili kutumia akiba hiyo kuongeza uzalishaji wa ndani na kuondoa umasikini. Hifadhi ya Jamii ni jawabu la kukuza utamaduni wa kuweka akiba na kutumia akiba hiyo kuwekeza katika sekta zinazokuza ajira na kuchochea uchumi kukua. Kwa wakulima, mifuko ya Hifadhi ya Jamii inaweza;

–  Kuandikisha kwenye Hifadhi ya Jamii wakulima ambapo watakuwa wamehamasishwa kujiunga kupitia vyama vya msingi vya ushirika. Vivo hivyo hili linawezekana kwa wafugaji na wavuvi. Wachimbaji wadogo wadogo wa madini na pia wafanyabiashara wadogo kupitia vyama vyao wanaweza kuandikishwa pia.

–   Michango kwenye mifuko ambapo wakulima watachangia kulingana na kipato chao kwa kuweka kiwango cha chini kabisa cha mfanyakazi. Kwa kuwa mapato ya wakulima ni ya msimu mifuko itaweka mfumo ambao wakulima watachangia baada ya mavuno yao mara moja. Hata hivyo, kivutio cha Serikali kinatakiwa ili mfumo huu kufikia watu wengi Zaidi. Kwa mfano kama kima cha chini ni shs 20,000 kwa mwezi, basi Serikali itachangia shilingi 10,000 na Mkulima tshs 10,000. Hili linawezekana pia kwa wafugaji, wavuvi na hata wafanyabiashara ndogo ndogo. Iwapo Serikali itaweka kivutio hiki, utamaduni wa kuweka akiba nchini utaongezeka sana na Taifa linaweza kutumia sehemu ya akiba hiyo kufanya uwekezaji katika maeneo yatakayokuza tija kwenye kilimo, kwa mfano uwekezaji kwenye viwanda vya mbolea, viwanda vya kuongeza thamani kwenye mazao na hata mikopo kwa wakulima yenye kuwaongezea kipato na hata kuboresha mashamba yao.

–    Mafao ya wakulima aghalabu hayawi sawa na mafao ya wafanyakazi. Baadhi ya mafao kama Bima ya Afya yatafaidisha wakulima na wafanyakazi. Kwa mfumo wa sasa iwapo Wakulima milioni moja tu watajiunga na Hifadhi ya Jamii, watanzania milioni sita watakuwa wamefadika na Bima ya Afya. Hayo ni mapinduzi makubwa. Taifa linataka nini Zaidi ya kuwa na watu wenye afya? Gharama ya Afya kwa wananchi inaongezeka sana na wananchi wengi wakiwa na Hifadhi ya Jamii tutakuwa tumeondoa mzigo huu kwao na hata kwa Serikali.

Wakulima na hata wafugaji wana changamoto zao. Kwa mfano ukame ukitokea wanashindwa kupata mavuno na hivyo kuingia kwenye dimbwi la umasini kwa sababu wanakosa ‘coverage’. Hasara za namna hii sasa zinaonekana kama ni agenda ya kimaendeleo (see World Bank- World Development Report- Risk and Opportunities, Managing Risk for Development, 2014). Ushahidi wa kisayansi unaonyesha kuwa wakulima na wafugaji wakiwa na uhakika wa kutoathiriwa na matendo kama ukame nk huwa wanafanya kazi kwa bidii na jamii kupata maendeleo endelevu. Hifadhi ya Jamii ina majawabu kwa masuala haya kwa kuwa na sera zifuatazo:

Bima ya Ukame/Mvua ambapo wakulima wataweza kufidiwa iwapo kukitokea ukame uatakaoharibu mazao yao au mvua kubwa yenye madhara kama hayo. Sehemu ya mchango wa mwanachama kwenye mfuko wa Hifadhi ya Jamii inaweza kuwekwa pembeni kununulia bima hiyo. Mfuko wa Hifadhi ya Jamii unaweza kuingia makubaliano na makampuni ya Bima kufanya kazi hii. Tunaweza kujifunza Zaidi eneo hili kutoka nchi za Ghana na India ambazo zimeanza skimu za namna hii.

Mfuko wa Bei ambapo wakulima wanaathirika sana na kupanda na kushuka kwa bei za mazao yao. Hivyo fao hili linaweza kuwekwa katika moja ya mafao ambayo wakulima watapata kwa kujiunga na mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Katika mfumo wa namna hii wakulima watalima Zaidi kwani wana uhakika kuwa hata bei zikishuka sana kwenye soko la dunia angalau gharama zao za uzalishaji zitarudi kwa kupitia fao hili. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imetangaza kuanzisha ‘Stabilization fund’ kuchukua nafasi ya mbolea ya ruzuku baada ya mfumo huo kugubikwa na ufisadi wa kutisha ambapo katika ruzuku za tshs 584 bilioni zilizotolewa kati ya mwaka 2008/2009 na 2012/2013 ni asilimia 40 tu ndio iliwafikia walengwa na asilimia 60 ililiwa na wajanja wachache haswa mawakala wa mbolea na viongozi wa vijiji. Badala ya Serikali kuweka fedha huko ni vema ikubaliane kuchangia katika michango ya wakulima watakaojiunga na mifuko ya Hifadhi ya Jamii na kauchia mifuko kuwa na ‘Fao la Bei’. Ninashauri Wananchi wote kukataa Fedha za umma kupelekwa kwenye miradi ya majaribio ambayo inatufanya kuongeza Deni la Taifa na badala yake tuisukume serikali kuchangia katika Michango ya wakulima (matching) na hivyo kuongeza uwekezaji wa akiba nchini. Mifuko ya Hifadhi ya jamii itasimamia vizuri zaidi ‘price stabilization fund’ kama ‘Fao la Bei’ kuliko Serikali kwa kufanya uwekezaji makini wenye kulipa (good returns) tena kwenye kuboresha miundombinu ya kilimo, uongezaji wa thamani wa mazao yetu na uboreshwaji wa masoko.

Hifadhi ya Jamii kwa sekta isiyo rasmi, na hapa nimeonyesha kwa wakulima, inawezekana. Hifadhi ya Jamii ni suala la kimaendeleo na ni moja ya dawa ya kuondokana na umasikini ambayo hatukuwa tumeitilia maanani. Jambo bora Zaidi kuliko yote ni kuwa suala hili hatuletewi na wazungu bali ni mawazo yetu wenyewe ya kuhakikisha watu wetu wanakuwa na maendeleo na umasikini unaondoshwa. Hifadhi ya Jamii ni kidonge dhidi ya ufukara na ufukarishwaji. Wito kwangu kwa mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii ni kuweka skimu za kuwafikia watu walio kwenye sekta isiyo rasmi na kuweka mafao yanayoendana na hali halisi zao. Wito wangu kwa Serikali ni kuweka vivutio kwa wananchi ili waweze kuweka akiba. Mpango wa kuanzisha ‘price stabilization fund’ uliotangazwa na Serikali hivi majuzi Bungeni wakati wa Bajeti ya Wizara ya Kilimo ubadilishwe na kuwa ‘matching’ ya Serikali kwa wakulima wanaoweka akiba katika mifuko ya hifadhi ya jamii.

Nimalizie mada yangu hii kwa kurudia mapendekezo ya Kamati ya Bunge ya PAC kwa takribani miaka 3 sasa ( kabla yake POAC), kwamba hakuna haja ya kuwa na mifuko lukuki nchini. Mifuko iunganishwe na kuwa Mfuko 1 utakaohusika na watumishi wa Serikali, Mfuko 1 utakaohusika na wafanyakazi wa sekta binafsi na kwa kuwa tumeanza skimu za sekta isiyo rasmi basi zikikomaa kuwe na mfuko 1 utakaohusika na sekta isiyo rasmi. Tunaweza kwa mfano kuunganisha NSSF na PPF kuwa mfuko mmoja kwa sekta binafsi, LAPF na PSPF kuwa mfuko wa sekta ya umma na GEPF kujikita kwenye sekta isiyo rasmi.

Vile vile nadhani ni vema badala ya mifuko kuendesha Bima zao za Afya basi zikasimu uendeshaji huo kwa Mfuko wa Bima ya Afya kwa kuchangia kile kiasi ambacho wataalamu wa actuarials wanaonesha kinapaswa kutumika kwa gharama za afya. Hii itaondoa tatizo lililopo la wanachama kuchangia mara mbili kwa gharama za Afya.

Asanteni kunisikiliza

[1] Mada iliyowasilishwa katika Mkutano Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii Tanzania (NSSF) jijini Arusha 13 -15 Mei 2014.

[2] Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali na Mbunge wa Kigoma Kaskazini

 

Written by zittokabwe

May 15, 2014 at 11:23 AM

Siku ya 8 Ziara CHADEMA Kanda ya Magharibi imetufikisha Jimbo la Nzega

with 2 comments

Siku ya 8 imetufikisha Jimbo la Nzega

Tumefanya mikutano 8 katika kata 8 lakini mikutano mikubwa ilikuwa kata za Puge na Ndala. Mkutano wa Nzega mjini ulikuwa mkubwa sana na umevunja rekodi ya mikutano ambayo nimewahi kufanya Nzega.

Nikiwa na viongozi wa CHADEMA mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi tumezungumza na wananchi kuhusu hali ya maisha na mabadiliko ya kisiasa yanayotakiwa. Tumeendelea kuonyesha namna nchi yetu ilivyo na mataifa 2 ndani ya nchi moja kutokana na tofauti za kimaendeleo kati ya mijini na vijijini na tofauti kubwa za kipato kati ya matajiri na masikini.

Ajenda za siku zilikuwa mabadiliko ya katiba, uwazi na uwajibikaji, siasa na vijana na hifadhi ya jamii kwa wakulima.

Nimewataka vijana waache kutumiwa na makundi ya wanasiasa kuumiza vijana wenzao na badala yake wajikite kwenye kusaidiana ili kubadili uongozi wa nchi. Nimewaambia vijana kuwa wao ni asilimia 65 ya wapiga kura wote nchini hivyo hii ni nchi yao na lazima wawe na uchu wa mabadiliko.

Nimewataka mawaziri Wassira, Lukuvi na Chikawe wajiuzulu nafasi zao kwa kushindwa kusimamia vema mchakato wa katiba na kumwambia uwongo Rais. Pia Waziri Mkuu kushindwa kuchukua hatua za kujenga mwafaka ndani ya Bunge na hivyo kila jambo kutegemea Rais aingilie kati. Kazi ya Waziri Mkuu bungeni ni nini?

Nimerejea kusisitiza Sera ya Hifadhi ya Jamii kwa Wakulima. Imefikia wakati Serikali kupitia SSRA ione umuhimu na ulazima wa kuhakikisha tunaongeza Watanzania wenye hifadhi ya jamii kwa kuanza mfumo maalumu wa hifadhi ya jamii kwa wakulima (Supplementary scheme for social security to small holder farmers). Ninapendekeza Serikali ichangie nusu kwa nusu na mkulima ili kuvutia uwekaji akiba katika nchi na kuwa na sera ya uwekezaji katika maeneo yatakayo mwinua mkulima kama miundombinu ya umwagiliaji, mikopo nafuu kwa wakulima kwenye pembejeo na nyumba na bima ya afya.

Nimezungumzia umuhimu wa uwazi katika matumizi ya fedha za umma ikiwemo malipo ya watumishi na viongozi wa umma. Nimewaeleza wananchi wa Nzega kuwa siku ya jumanne kamati ya PAC itaanza kukagua mahesabu ya vyama vya siasa nchini. Vyama vya siasa vinatumia fedha za umma takribani tshs 20bn kila mwaka kama ruzuku. Ni haki kwa wananchi kujua fedha zinatumika namna gani.

Wananchi wa Nzega wana changamoto nyingi sana. Wakulima wa Pamba walipewa madawa feki ya kuua wadudu, michango ya hovyo hovyo ni mingi mno na unyanyasi wa wana chadema ni mkubwa vijijini. Kata ya Ndala, wananchi wamejenga Kituo cha Afya lakini hakina wahudumu na mradi wa maji limeanza kuvuja kabla ya mradi kuanza. Changamoto zote hizi zinajibika, muhimu ni kufanya mabadiliko kwa kuondoa CCM madarakani na kuimarisha uwazi na uwajibikaji.

This slideshow requires JavaScript.

Written by zittokabwe

October 13, 2013 at 9:17 AM

Siku ya sita ya Ziara ya #CHADEMA imetufikisha Jimbo la Tabora Kaskazini

leave a comment »

Siku ya sita ya Ziara ya #CHADEMA imetufikisha Jimbo la Tabora Kaskazini.

Tumefanya mkutano wetu wa mwisho kijijini Mabama. Mkutano mkubwa sana na kuingia wanachama wengi sana. Kilio kikubwa cha wananchi ni Maji na unyonyaji katika zao la Tumbaku. Kuna haja kubwa sana ya kusukuma hifadhi ya jamii kwa wakulima. Tunaweza kukoboa wakulima wengi sana kutoka kwenye unyonyaji.
Ufisadi kwenye ngazi ya kijiji unatisha.

Umewahi kusikia jengo la matofari ya saruji linajengwa kwa tope?

#CHADEMA kanda ya Magharibi leo #Bukene. Kesho 12th Oct #Nzega na keshokutwa 13th #Igunga

This slideshow requires JavaScript.

Written by zittokabwe

October 11, 2013 at 12:32 PM