Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Posts Tagged ‘Mwadhama Polycap kardinali Pengo

PASAKA YA KATIBA

with 2 comments

PASAKA YA KATIBA

“Sote tuwe na umoja” (Yn. 17:21)

Nimesoma kwa kina Tamko la Maaskofu Thelathini na Wawili wa Kanisa Katoliki Tanzania. Pia nimepitia taarifa za magazeti yote nchini yaliyoandika kuhusu salamu za Sikukuu ya Pasaka kwa Wakristo nchini na Watanzania kwa ujumla. Mwenendo wa Bunge la Katiba umeshamiri katika matamko ya Viongozi wetu wa Dini katika mahubiri yao ya Sikukuu ya Pasaka.

Napenda kuwashukuru kwa Maaskofu wetu kwa Hekima na Busara ya hali ya juu katika matamko yao na wito wa kutaka mchakato wa Katiba uendelee kwa kuheshimu maoni ya Wananchi na kuboresha inapobidi ili kupata Katiba bora. Kama nilivyopata kusema hapo awali, Katiba ni Mwafaka wa Taifa kwa hiyo ni lazima kila mmoja wetu awe na moyo wa maridhiano. Makundi makubwa ya Kisiasa nchini yanapasa kuunga mkono kwa vitendo Tamko hili la Maaskofu pamoja na rai mbali mbali ambazo Viongozi wetu wa kiroho wametoa wakati huu wa Sikukuu ya Pasaka.

Maaskofu wanatukumbusha Nanukuu; “Tulichukua hatua kubwa kuunganisha nchi mbili huru, Tanganyika na Zanzibar, na kuifanya kuwa nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa kielelezo kwa Bara la Afrika cha kujenga umoja”. Wanaendelea “Pamoja na mafanikio hayo makubwa, zimejitokeza dosari kadhaa katika umoja zilizofanya umoja wetu upoteze baadhi ya sifa zake za awali. Kupungua kwa hisia za kujisikia watu wote ni taifa moja, ni dosari iliyoanza kukua taratibu na sasa inaonekana kuwa ndio ukweli. Baadhi ya Watanzania wanafikiri kuwa umoja unaofuta tofauti haufai ila umoja unaosisitiza tofauti kama ulivyo umoja wa kikanda (kama ilivyo SADC, ECOWAS, n.k) ndio unafaa! Wakati mataifa mengine yanatamani umoja unaofanana na ule umoja wetu wa awali, baadhi yetu tunatamani kurudi nyuma kwenye umoja wa mpito!”

Ni dhahiri viongozi wetu wa kiroho wanaumizwa na juhudi zinazoendelea za kuuzongazonga Muungano na hata kuhoji uhalali wake kiasi cha baadhi ya Watanzania kutaka tuwe Jumuiya ya Kiuchumi tu. Tunaonywa pia kuhusu Muungano wenye Serikali ya Muungano ‘egemezi na tegemezi’ iwapo hatutaboresha Rasimu ya Katiba. Vilevile viongozi wetu wa dini wanasikitikia uwezekano wa Muungano kuvunjika. Hata hivyo wanaonyesha kwamba Rasimu ya Katiba imeweka misingi mizuri ya kuendeleza Mshikamano na Umoja wetu. Wanasema;

“Vigezo vyote muhimu kwa maisha ya mshikamano kitaifa vimeandikwa katika Rasimu ya Katiba Sura ya 1 hadi ya 5. Tukisha kukubaliana na yaliyomo katika sura hizo, muundo wowote wa Serikali unawezekana kwa kuzingatia kanuni za uwiano wa madaraka na wajibu wa mihimili mitatu ya Dola kwa mujibu wa Sura za 8 hadi 15”. Wanaendelea, “Chaguo la muundo wa Dola, sharti liongozwe na malengo na madhumuni ya umoja wetu wa kutaka tuishi kwa mshikamano wa dhati. Uchaguzi wa muuungano wa serikali moja, mbili au tatu sharti ufanywe kwa dhamiri safi iliyo na uelewa uliochambua matatizo yaliyopo ya Muungano na kuridhia mfumo utakaosuluhisha matatizo hayo pasipo mashaka yoyote”

Katika Salamu zake na Pasaka, Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam Dkt. Valentino Mokiwa naye pamoja na kulaani vikali mwenendo wa Bunge la Katiba ametaka pia Muundo Muungano ikibidi uwe na Rais mmoja tu na wengine wawe wasaidizi wake. Hii inarutubisha hoja ya kuboresha Rasimu ya Katiba ili kupata Katiba inayopendekezwa itakayopelekwa kwa Wananchi na kuamuliwa kwa kura. Kwa maoni yangu, ni vema Wajumbe wote wa Bunge la Katiba kuweka mawazo yao wazi badala ya kung’ang’ania misimamo ya Vyama vyao vya siasa au Makundi yao. Wanaotaka Serikali Mbili (S2) wawasikilize wanaotaka Serikali Tatu (S3) kama zilivyo kwenye Rasimu na vilevile wanaotaka Tatu zilizoboreshwa (S3z) nao pia wasikilizwe. Hatimaye tupate Katiba bora inayopendekezwa. Neno Dhamira Safi ni neno la msingi na la kuzingatia sana katika mchakato huu. Ni vema wenzetu wasiotaka Muungano wawe wazi badala ya kujificha kwenye miundo.

Maaskofu wetu wanatusihi nanukuu, “Tunalisihi na kulishauri Bunge Maalum la Katiba kuheshimu mawazo yaliyowasilishwa na kutumia busara zilizopendekezwa za kujenga muundo wa Muungano utakaokidhi mahitaji ya utangamano, mshikamano, amani, maadili, uhuru na uwajibikaji wa viongozi na raia wa Tanzania”. Kwa upendo kabisa viongozi wa Dini wanatuombea, “Wakati huu wa Pasaka, tuendelee kuliombea Bunge Maalumu la Katiba ili wajumbe wawe wazingatifu wa matakwa na matarajio ya Watanzania yalivyoainishwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba na Tume ya mabadiliko ya Katiba kwa kuheshimu maoni ya Watanzania na kuboresha maoni hayo kwa hekima na busara ili kulinda mstakabali wa Taifa letu”.

Licha ya kuombewa na viongozi wetu hatuna budi sote kwa pamoja kulaani na kukataa lugha za matusi na kibaguzi zilizogubika majadiliano ya Bunge Maalumu la Katiba. Askofu Mkuu wa KKKT Dkt. Alex Malasusa amekemea vitendo vya kibaguzi na kusisitiza umuhimu wa kusikilizana, kuheshimiana na kuridhiana. Wakati Kardinali Pengo anasihi Wajumbe waliotoka nje kurejea Bungeni ni vema basi viongozi wa dini zetu zote kuu, Waislam na Wakristo, pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wachukue wajibu wa kwanza, kuendelea kukemea vikali lugha za kibaguzi, matusi na kejeli. Viongozi wa Bunge la Katiba wachukue jukumu la kuwaadhibu Wajumbe wanaotoa lugha za namna hii wakati wa mijadala na viongozi wa vyama vya siasa waweke nidhamu kwa wanachama wao. Ninashauri Viongozi wetu wa Dini kukaa pamoja na Viongozi wa makundi ya kisiasa katika Bunge Maalumu ili kupata maridhiano, kujenga kuaminiana na kusonga mbele. Ni vema mkutano huu wa maridhiano chini ya Viongozi wakuu wa Dini zetu ufanyike kabla ya Sikukuu ya Muungano. Nawasihi viongozi wetu wa kisiasa kukubali maridhiano kupitia kwa viongozi wa dini zetu kwani maridhiano yanajenga Mwafaka na Katiba ni Mwafaka Mkuu wa Kitaifa.

Maaskofu wamenena. Tusikie. Pasaka iwe ya Maridhiano katika kuandika Katiba. Mateso aliyopata Bwana Yesu na kisha kufufuka kwake iwe rejea yetu na kusameheana pale tulipokoseana na kuweka misingi ya kuheshimiana, kusikilizana na kuridhiana.

 

Zitto Kabwe, MB

Dar-es-Salaam,

Jumatatu 21/04/2014

 

 

 

Written by zittokabwe

April 21, 2014 at 5:45 PM