Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Posts Tagged ‘katiba

PASAKA YA KATIBA

with 2 comments

PASAKA YA KATIBA

“Sote tuwe na umoja” (Yn. 17:21)

Nimesoma kwa kina Tamko la Maaskofu Thelathini na Wawili wa Kanisa Katoliki Tanzania. Pia nimepitia taarifa za magazeti yote nchini yaliyoandika kuhusu salamu za Sikukuu ya Pasaka kwa Wakristo nchini na Watanzania kwa ujumla. Mwenendo wa Bunge la Katiba umeshamiri katika matamko ya Viongozi wetu wa Dini katika mahubiri yao ya Sikukuu ya Pasaka.

Napenda kuwashukuru kwa Maaskofu wetu kwa Hekima na Busara ya hali ya juu katika matamko yao na wito wa kutaka mchakato wa Katiba uendelee kwa kuheshimu maoni ya Wananchi na kuboresha inapobidi ili kupata Katiba bora. Kama nilivyopata kusema hapo awali, Katiba ni Mwafaka wa Taifa kwa hiyo ni lazima kila mmoja wetu awe na moyo wa maridhiano. Makundi makubwa ya Kisiasa nchini yanapasa kuunga mkono kwa vitendo Tamko hili la Maaskofu pamoja na rai mbali mbali ambazo Viongozi wetu wa kiroho wametoa wakati huu wa Sikukuu ya Pasaka.

Maaskofu wanatukumbusha Nanukuu; “Tulichukua hatua kubwa kuunganisha nchi mbili huru, Tanganyika na Zanzibar, na kuifanya kuwa nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa kielelezo kwa Bara la Afrika cha kujenga umoja”. Wanaendelea “Pamoja na mafanikio hayo makubwa, zimejitokeza dosari kadhaa katika umoja zilizofanya umoja wetu upoteze baadhi ya sifa zake za awali. Kupungua kwa hisia za kujisikia watu wote ni taifa moja, ni dosari iliyoanza kukua taratibu na sasa inaonekana kuwa ndio ukweli. Baadhi ya Watanzania wanafikiri kuwa umoja unaofuta tofauti haufai ila umoja unaosisitiza tofauti kama ulivyo umoja wa kikanda (kama ilivyo SADC, ECOWAS, n.k) ndio unafaa! Wakati mataifa mengine yanatamani umoja unaofanana na ule umoja wetu wa awali, baadhi yetu tunatamani kurudi nyuma kwenye umoja wa mpito!”

Ni dhahiri viongozi wetu wa kiroho wanaumizwa na juhudi zinazoendelea za kuuzongazonga Muungano na hata kuhoji uhalali wake kiasi cha baadhi ya Watanzania kutaka tuwe Jumuiya ya Kiuchumi tu. Tunaonywa pia kuhusu Muungano wenye Serikali ya Muungano ‘egemezi na tegemezi’ iwapo hatutaboresha Rasimu ya Katiba. Vilevile viongozi wetu wa dini wanasikitikia uwezekano wa Muungano kuvunjika. Hata hivyo wanaonyesha kwamba Rasimu ya Katiba imeweka misingi mizuri ya kuendeleza Mshikamano na Umoja wetu. Wanasema;

“Vigezo vyote muhimu kwa maisha ya mshikamano kitaifa vimeandikwa katika Rasimu ya Katiba Sura ya 1 hadi ya 5. Tukisha kukubaliana na yaliyomo katika sura hizo, muundo wowote wa Serikali unawezekana kwa kuzingatia kanuni za uwiano wa madaraka na wajibu wa mihimili mitatu ya Dola kwa mujibu wa Sura za 8 hadi 15”. Wanaendelea, “Chaguo la muundo wa Dola, sharti liongozwe na malengo na madhumuni ya umoja wetu wa kutaka tuishi kwa mshikamano wa dhati. Uchaguzi wa muuungano wa serikali moja, mbili au tatu sharti ufanywe kwa dhamiri safi iliyo na uelewa uliochambua matatizo yaliyopo ya Muungano na kuridhia mfumo utakaosuluhisha matatizo hayo pasipo mashaka yoyote”

Katika Salamu zake na Pasaka, Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam Dkt. Valentino Mokiwa naye pamoja na kulaani vikali mwenendo wa Bunge la Katiba ametaka pia Muundo Muungano ikibidi uwe na Rais mmoja tu na wengine wawe wasaidizi wake. Hii inarutubisha hoja ya kuboresha Rasimu ya Katiba ili kupata Katiba inayopendekezwa itakayopelekwa kwa Wananchi na kuamuliwa kwa kura. Kwa maoni yangu, ni vema Wajumbe wote wa Bunge la Katiba kuweka mawazo yao wazi badala ya kung’ang’ania misimamo ya Vyama vyao vya siasa au Makundi yao. Wanaotaka Serikali Mbili (S2) wawasikilize wanaotaka Serikali Tatu (S3) kama zilivyo kwenye Rasimu na vilevile wanaotaka Tatu zilizoboreshwa (S3z) nao pia wasikilizwe. Hatimaye tupate Katiba bora inayopendekezwa. Neno Dhamira Safi ni neno la msingi na la kuzingatia sana katika mchakato huu. Ni vema wenzetu wasiotaka Muungano wawe wazi badala ya kujificha kwenye miundo.

Maaskofu wetu wanatusihi nanukuu, “Tunalisihi na kulishauri Bunge Maalum la Katiba kuheshimu mawazo yaliyowasilishwa na kutumia busara zilizopendekezwa za kujenga muundo wa Muungano utakaokidhi mahitaji ya utangamano, mshikamano, amani, maadili, uhuru na uwajibikaji wa viongozi na raia wa Tanzania”. Kwa upendo kabisa viongozi wa Dini wanatuombea, “Wakati huu wa Pasaka, tuendelee kuliombea Bunge Maalumu la Katiba ili wajumbe wawe wazingatifu wa matakwa na matarajio ya Watanzania yalivyoainishwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba na Tume ya mabadiliko ya Katiba kwa kuheshimu maoni ya Watanzania na kuboresha maoni hayo kwa hekima na busara ili kulinda mstakabali wa Taifa letu”.

Licha ya kuombewa na viongozi wetu hatuna budi sote kwa pamoja kulaani na kukataa lugha za matusi na kibaguzi zilizogubika majadiliano ya Bunge Maalumu la Katiba. Askofu Mkuu wa KKKT Dkt. Alex Malasusa amekemea vitendo vya kibaguzi na kusisitiza umuhimu wa kusikilizana, kuheshimiana na kuridhiana. Wakati Kardinali Pengo anasihi Wajumbe waliotoka nje kurejea Bungeni ni vema basi viongozi wa dini zetu zote kuu, Waislam na Wakristo, pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wachukue wajibu wa kwanza, kuendelea kukemea vikali lugha za kibaguzi, matusi na kejeli. Viongozi wa Bunge la Katiba wachukue jukumu la kuwaadhibu Wajumbe wanaotoa lugha za namna hii wakati wa mijadala na viongozi wa vyama vya siasa waweke nidhamu kwa wanachama wao. Ninashauri Viongozi wetu wa Dini kukaa pamoja na Viongozi wa makundi ya kisiasa katika Bunge Maalumu ili kupata maridhiano, kujenga kuaminiana na kusonga mbele. Ni vema mkutano huu wa maridhiano chini ya Viongozi wakuu wa Dini zetu ufanyike kabla ya Sikukuu ya Muungano. Nawasihi viongozi wetu wa kisiasa kukubali maridhiano kupitia kwa viongozi wa dini zetu kwani maridhiano yanajenga Mwafaka na Katiba ni Mwafaka Mkuu wa Kitaifa.

Maaskofu wamenena. Tusikie. Pasaka iwe ya Maridhiano katika kuandika Katiba. Mateso aliyopata Bwana Yesu na kisha kufufuka kwake iwe rejea yetu na kusameheana pale tulipokoseana na kuweka misingi ya kuheshimiana, kusikilizana na kuridhiana.

 

Zitto Kabwe, MB

Dar-es-Salaam,

Jumatatu 21/04/2014

 

 

 

Written by zittokabwe

April 21, 2014 at 5:45 PM

Inyonga, Mpanda Magharibi- Ziara Kanda ya Magharibi

with 2 comments

Jana nimefanya mikutano 6 katika jimbo la Mpanda Magharibi, nimepewa heshima ya utemi wa Ukonongo pale Inyonga, tumezungumza na wananchi wakulima wa tumbaku na madhila yao.

Wananchi wanadhulumiwa kwenye bei ya dola za kimarekani katika kila kilo ya tumbaku ambapo wanapewa bei ya tshs 1400 kwa dola $1 moja! Makato ya pembejeo makubwa na wanashindwa kutoka kwenye umasikini. Tukiwa Sikonge tutatoa kauli kuhusu Wakulima wa Tumbaku na namna ya kuwakomboa.

Tumezugumza umuhimu wa Katiba mpya ya wananchi na namna ya kuepusha mchakato kutekwa na kundi dogo la watu wasiotaka mabadiliko. Tumezungumza kuhusu umuhimu wa mwafaka wa kitaifa katika kuandika katiba ya nchi yetu. Kuweka maslahi ya Taifa mbele ya maslahi ya vyama vya siasa.

Leo tunakwenda Mpanda Magharibi kuanzia Mpanda ndogo mpaka Ikola, Mwambao mwa Ziwa Tanganyika.

Mtemi wa Ukonongo, Inyonga

Mtemi wa Ukonongo, Inyonga

 

IMG-20131005-WA0002

Kulia mwenyekiti wa chadema kanda ya magharibi, kushoto mwenyekiti wa chadema mkoa wa Katavi mara baada ya kutawazwa kuwa Mtemi wa Ukonongo eneo la Inyonga Wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi.

IMG-20131005-WA0005 IMG-20131005-WA0006 IMG-20131005-WA0011

Written by zittokabwe

October 6, 2013 at 9:29 AM

Katiba ni Mwafaka wa Kitaifa. Viongozi zungumzeni

with 3 comments

Kwa takribani wiki tatu sasa kumekuwa na sintofahamu kuhusu muswada wa sheria uliopitishwa na Bunge ili kufanya marekebisho ya sheria ya marekebisho ya Katiba ya mwaka 2011. Mjadala na upitishaji wa sheria hii uliweka rekodi ya pekee katika nchi yetu kwa vitendo vya kihuni kutokea Bungeni ambavyo nisingependa kuvirejea kutokana na aibu kubwa ambayo Bunge liliingia. Kiukweli kuna sintofahamu katika nchi kuhusu kuandikwa kwa Katiba mpya. Hii imechangiwa na kurushiana maneno miongoni mwa wanasiasa wa pande zote mbili, wanaopinga muswada ulivyo na wanaounga mkono muswada ulivyo. Masuala ya Tume imalize kazi yake lini, ushiriki wa Zanzibar na idadi ya wajumbe kutoka Zanzibar kwenye Bunge la Katiba, Wajumbe wa Bunge Maalumu wanapatikanaje na kadhalika ni masuala ambayo yanaweza kupatiwa mwafaka kwa viongozi kukaa na kuzungumza. Haya sio masuala ya kushindwa kujenga mwafaka labda kuwe na nia mbaya dhidi ya mchakato wa kuandika Katiba mpya. Katiba sio suala la kufanyia siasa. Katiba ni uhai wa Taifa.

Ni wazi kuna kundi kubwa ambalo halijitokezi waziwazi ambalo lingependa pasiwe na katiba mpya ya Wananchi. Kuna kundi lingine ambalo lingependa mchakato wa kuandika Katiba uendelee kwa miaka mingine zaidi ili kuweza kupata Katiba bora. Kuna kundi la Wabunge ambao kwa chinichini wanataka mchakato uendelee, uchaguzi uahirishwe mpaka mwaka 2017 na wao waendelee kuwa wabunge. Naamini watu hawa wanaota ndoto za mchana kwani hakuna mahusiano yeyote kati ya uchaguzi mkuu na kuandika katiba mpya. Kama Bunge hili la sasa na Serikali hii itashindwa kukamilisha zoezi hili, Bunge linalokuja na Serikali itakayoingia madarakani itaendelea nalo. Hivyo sio lazima kupata Katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015. CHADEMA imependekeza kuwepo na marekebisho ya mpito kwenye Katiba ya sasa ili kuwezesha Tume huru ya Uchaguzi, masuala ya wagombea binafsi na kadhalika. Vyama vingine vya siasa vinaweza kuwa na mapendekezo yao ya mpito na hivyo kutoa nafasi ya kutosha kabisa wa kuandika Katiba makini.

Changamoto kubwa sana ya siasa za Tanzania ni kelele. Wanasiasa hatuzungumzi kwenye masuala yanayohusu uhai wa Taifa. Kila chama kinakuwa na misimamo yake na kuishikilia na hatimaye kujikuta tunapoteza fursa ya kuzungumza na kujadiliana kama Watanzania. Mwaka 2011 hali ilikuwa hivi hivi mpaka kundi la Wazee viongozi wastaafu walipoingilia kati na kupelekea wanasiasa kukaa na kuzungumza. Bahati mbaya sana viongozi wale ndio sasa wamepewa usukani wa kuandika Katiba kwa kuwa kwenye Tume. Hawawezi tena kufanya kazi ile ya kutafuta suluhu iliyopelekea Rais kuzungumza na viongozi wa vyama vyote vya siasa ikulu jijini Dar es Salaam.

Vyama vya Upinzani nchini sasa vimeungana kupinga muswada wa marekebisho ya Sheria ya Marekebisho ya Katiba ya mwaka 2011. Waziri wa Sheria na Katiba, Waziri wa Nchi ofisi ya Rais mahusiano na Uratibu, viongozi waandamizi wa CCM wote nao wameungana kuunga mkono muswada kama ulivyo. Badala ya kutafuta mwafaka, kumekuwa na kurushiana maneno ya kejeli na kadhalika. Taifa halijengwi namna hii. Taifa linajengwa kwa mwafaka na Katiba ni moja ya nyenzo wa Mwafaka wa Taifa. Niliwahi kuandika huko nyuma kuwa Katiba haiandikwi barabarani bali huandikwa mezani kwa watu kukaa na kukubaliana masuala ya Taifa dhidi ya maslahi ya kivyama ya wanasiasa.

Hakuna kilichoharibika. Bado tunayo nafasi kama Taifa kukaa na kukubaliana. Kwa hali ya sasa nafasi hii ipo mikononi mwa Mkuu wa Nchi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais ana wajibu wa kikatiba wa kuhakikisha umoja wa kitaifa unaendelea kuongoza mchakato huu wa katiba ya nchi yetu. Hata hivyo ni vizuri kutahadharisha kuwa sio sahihi kwa wanasiasa wa pande zote kujaribu kumlazimisha Rais kuridhia ama kutoridhia sheria hiyo. Si sawa kisiasa kwa wanasiasa wa upinzani kujaribu kumlazimisha Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama chenye wabunge wengi bungeni kwenda tofauti na wabunge wake na wakati huohuo ni utovu wa nidhamu kwa Waziri wa Sheria kujaribu kumshauri hadharani Rais wake kuridhia sheria hiyo kwani ni kinyume cha misingi ya uongozi na pia kinatafsirika kama kumshurutisha (blackmail) Rais wake.

Kutosaini muswada huu kunaweza kuleta mgongano kati ya Wabunge wa CCM na Rais. Hata hivyo Rais lazima aweze kushawishi chama chake kwamba umoja wa kitaifa ni muhimu ziadi kuliko maslahi ya kisiasa ya chama chao. Pia kikatiba Rais anasaini miswada kuwa sheria akiwa Mkuu wa Nchi na sio Mkuu wa Serikali ya Jamhuri. Akiwa Mkuu wa Nchi maslahi mapana ni kuweka mwafaka wa pamoja miongoni mwa wananchi. Rais Jakaya Kikwete anapaswa kutumia mamlaka yake kama Mkuu wa Nchi kuiweka nchi pamoja kwa kuurejesha muswada bungeni ili uweze kujadiliwa upya na wadau wote na kupitishwa tena na Bunge. Ibara ya 97 ya Katiba ya sasa imeweka masharti ya utaratibu wa kutunga sheria na iwapo Rais ataurudisha muswada huu Bungeni pamoja na maelezo ya hatua hii, upitishwaji wake utahitaji theluthi mbili ya wabunge wote. Hii itakuwa hatua muhimu sana katika historia ya demokrasia yetu. Rais afuate ushauri huu kwani una manufaa makubwa.

Hata hivyo, ni lazima pawepo na mazungumzo miongoni mwa wanasiasa na makundi ya kijamii kuhusu Katiba. Katiba nzuri itapatikana pale tu ambapo mazingira ya kisiasa yanaonyesha nia njema kwa pande zote kisiasa. Kukwepa kuangaliana machoni na kuzungumza tofauti zetu za kimitazamo ni hatari zaidi. Juzi ngumi zimerushwa Bungeni. Kesho zitakua mitaani na vijijini kwetu. Tunataka kujenga Taifa la namna hiyo?

Written by zittokabwe

September 28, 2013 at 3:28 PM

Posted in Tanzania, Zitto Kabwe

Tagged with , , , , ,