Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Posts Tagged ‘Kamati ya Mishati na Madini

Taarifa ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu Gesi(Ripoti ya Pan African Energy)

with one comment

Na Zitto Kabwe

Mkutano wa Tano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mambo mengine ulijadili Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Sekta ndogo ya Gesi nchini. Taarifa hii ilitokana na kazi iliyofanywa na Kamati ndogo iliyoundwa na Kamati ya Nishati na Madini chini ya uongozi wa Mbunge wa Bumbuli ndugu Januari Makamba. Miongoni mwa Hadidu rejea za Kamati ndogo zilikuwa ni kubainisha kama Mikataba, taratibu na Kanuni zinazotawala shughuli za gesi zinazingatia maslahi ya Taifa na hazitiliwi shaka na wadauna Kubainisha kama maamuzi yanayoendesha shughuli za gesi kama vile gharama za   ujenzi, uendeshaji na mambo mengine yanayoweza kuathiri gharama na usalama wa shughuli yanafikiwa kwa ufanisi na yanazingatia maslahi ya Taifa.

Taarifa ya Kamati iliwasilishwa Bungeni na kupitishwa na Bunge ili Serikali iweze kutekeleza maazimio zaidi ya ishirini na Sita yaliyopendekezwa. Miongoni mwa Maazimio hayo ni Azimio namba mbili ambalo linasema  ‘Kamati imejiridhisha bila shaka kwamba  kwa kipindi cha 2004 hadi 2009 Kampuni ya Pan African Energy Tanzania Ltd (PAT) imejirudishia isivyo halali gharama zinazofikia jumla ya dola za kimarekani milioni 28.1 sawa na fedha za kitanzania bilioni 46.3. Kutokana na kujirudishia fedha hizo isivyo halali kumefanya Serikali kukosa gawio lake linalofikia dola za kimarekani milioni 20.1.  Aidha, mpaka wakati Kamati inaandaa ripoti hii, Kampuni ya Pan African Energy Tanzania Ltd (PAT) imeshindwa kuwasilisha uthibitisho wa uhalali wa kujirudishia gharama nyingine zinazofikia jumla ya dola za kimarekani milioni 36. Hali hii inaonyesha mashaka makubwa katika uendeshaji wa sekta hii muhimu ya gesi’.

Azimio hili ni moja ya Azimio linalopaswa kuangaliwa kwa makini sana tunapojadili namna Tanzania inavyosimamia na kufaidika na Sekta ya Mafuta na Gesi. Taifa linafaidika kwa kiwango gani na Wawekezaji wanafaidika kwa kiwango gani ndio msingi wa Mikataba ya Mafuta na Gesi nchini. Hapajawa na mijadala mikali katika eneo hili kama ilivyo kwenye sekta ya Madini na hivyo kuachia kila kukicha Shirika la Maendeleo ya Mafuta Nchini (TPDC) likisaini Mikataba ya Kutafuta na kuchimba Mafuta na Gesi (Production Sharing Agreements – PSAs) bila Watanzania kujua haswa ni jambo gani linasainiwa. Hivi sasa kuna Mikataba hii 23 hapa nchini.

Duniani kote kuna familia mbili za mikataba ya Mafuta na Gesi. Familia ya kwanza inaitwa ‘concessionery’ ambapo Kampuni ya Mafuta ya Binafsi inapewa haki zote za mchakato mzima wa kutafuta, kuchimba, kusafirisha na kuuza Mafuta au Gesi. Umiliki wa Mafuta (rights) unakuwa ni wa Kampuni Binafsi na sio Serikali. Katika mfumo huu Kampuni hulipa mrahaba Serikalini na kodi zinazopaswa. Nchi kama Marekani, Uingereza na Canada hutumia mfumo huu.

Familia ya pili ni Mikataba ya Uzalishaji au kwa Kiingereza Production Sharing Agreements (PSAs). Katika mfumo huu Haki (right) inabakia kuwa mali ya Taifa husika na Kampuni ya Mafuta huwa ni kama mkandarasi tu wa kutafuta na kuchimba mafuta. Akipata mafuta, anaondoa gharama za kuzalisha na faida inagawiwa kati ya Kampuni hiyo na nchi husika kupitia Shirika la Mafuta. Huu ndio mfumo unaotumika hapa Tanzania na ulianzia huko Indonesia na Venezuela miaka ya sitini. Kutokanana mfumo huu ndio tunapata masuala haya ambayo Kamati ya Nishati na Madini imegundua kama nitakavyofafanua kwa ufupi hapa chini.

Mkataba wowote wa Mafuta na Gesi ni lazima uzingatie Uzalishaji na Mapato kwa ujumla, mrahaba kwa nchi, urejeshaji wa gharama za uzalishaji na kodi mbalimbali na namna faida inavyogawanywa. Kampuni ya Pan Africa Energy kujirejeshea gharama isizostahili za zaidi ya shilingi 46 bilioni ni sehemu ya mianya iliyopo katika mikataba yetu. Jumla ya shilingi 110 bilioni zimeonekana kuwa na mashaka makubwa katika mahesabu ya Kampuni hii.

Taarifa inaonyesha kwamba Kampuni hii imeweka pia Gharama zao za uzalishaji kwa miradi ya nje ya Tanzania. Kwa kuwa Kampuni ya Pan Africa Energy Tanzania Limited ni Kampuni Tanzu ya Pan Africa Energy iliyosajiliwa ‘offshore’ Mauritius ambayo nayo ni Kampuni tanzu ya Orca ambayo pia imesajiliwa visiwa vya Jersey, Tanzania isingekwepa kubambikiwa gharama ambazo si zake ili kupunguza mapato ya Serikali ya Tanzania. Imewahi kuelezwa huko nyuma kwamba hizi njia za kukwepa kodi zimeshamiri sana kutokana na Makampuni makubwa yanayofanya biashara hapa nchini kufanya ‘tax planning’ na hivyo kuhamisha mapato yao kwenda nchi zisizo na kodi kubwa kama Mauritius, Isle of Man, Jersey au hata City of London.

Mwaka 2009 mwezi Aprili katika Taarifa yake ya mwaka, Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma ililiambia Bunge kwamba Mkataba kati ya TPDC na Pan Africa Energy ni moja ya mikataba mibovu kuliko yote nchini. Hii ilitokana na ukweli kwamba kwa mujibu wa PSA kati ya TPDC na Pan Africa Tanzania, mrahaba wa mafuta wa asilimia 12 unalipwa na TPDC na pia Kodi ya Mapato inakokotolewa kutoka katika mrahaba huo. Kwa maana hiyo Kampuni hii hailipi Mrahaba na pia hailipi kodi ya Makampuni (corporate tax) kwa mujibu wa Mkataba. Suala hili Kamati ya Nishati na Madini haikuliangalia (labda kwa kuwa ni la kimahesabu). Kamati ya POAC ilitaka mikataba yote ya Mafuta iangaliwe upya ili kuondoa mazonge haya yanayokosesha Taifa mapato makubwa sana.

Uwezo wa TPDC kukagua mahesabu ya Kampuni za utafutaji mafuta ni mdogo au haupo kabisa. Kama TPDC wangekuwa na uwezo huu leo Kamati ya Nishati na Madini isingekuta madudu haya katika kampuni. Pia kama Kamati ya Nishati na Madini ingeangalia mikataba ya kampuni zote za kutafuta mafuta wangekuta madudu mengi zaidi. Kuna kampuni moja yenye kisima pale Mkuranga, wamesema gharama za kuchimba visima vile ni dola za Kimarekani 240 milioni ilhali gharama halisi ni dola za kimarekani 60 milioni tu. Hivyo Gesi ikianza kuchimbwa itabidi warejeshe gharama zao kwanza. Tanzania haitapata lolote mpaka Gesi ile itakwisha.

Kuna haja ya kufanya marekebisho makubwa sana katika uendeshaji na usimamizi wa sekta ya Gesi Tanzania. Shirika la TPDC lirekebishwe kwa kuanzisha Mamlaka ya Mafuta na Gesi yenye uwezo na nguvu ya kusimamia uwekezaji katika sekta hii. Vilevile kuwepo na Shirika la Mafuta na Gesi (PetroTan –National Oil and Gas Company) ambalo litashiriki katika uwekezaji  kikamilifu na kampuni binafsi. Tusiposimamia vema sekta hii Taifa letu litaingia kwenye matatizo makubwa sana huko siku za usoni.

Maneno ya Mwana Uchumi Gwiji Joseph Stiglitz ni ya kuzingatia sana. Anasema, Mara zote nchi zinazoendelea zijue, wanapojadiliana na Kampuni kubwa za Mafuta, Kampuni hizi hufikiria jambo moja tu. Jambo hilo ni kuongeza mapato yao kwa kupunguza mapato ya mataifa husika. Tanzania ni lazima ihakikishe kwamba inapangua mbinu zote za Makampuni makubwa kwa kujenga uwezo wa Wananchi wake kupitia Shirika la Mafuta na Gesi kuweza kuwa na mikataba yenye kujali faida kwa nchi. Hili la Pan Africa Energy litufumbue macho.

 FULL REPORT YA HUJUMA SEKTA YA GESI

View this document on Scribd