Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Posts Tagged ‘Deni la taifa

Deni la Taifa: Wafaidi wachache, twalipa wote #DeniLaTaifa

with 2 comments

Deni la Taifa: wafaidi wachache, twalipa wote

denilataifaLeo nimeandika kuhusu Deni la Taifa kukua kwa kasi na kufikia tshs 27 trilioni mpaka Desemba 2013 kutoka tshs 10 trilioni mwaka 2005. Baadhi ya Watalaamu wanajenga hoja kuwa kukopa sio shida, bali kukopa kwa ajili ya nini. Nikakumbuka mzigo wa madeni ambao Taifa lilibeba miaka ya sabini na themanini kiasi cha Tanzania kukoswa koswa kuwa nchi ya Kwanza duniani kushindwa kuhudumia madeni yake. ‘heshima’ hiyo ilikwenda kwa nchi ya Nicaragua mwaka 1982. Mikopo ya nini?

Mwishoni mwa miaka ya sabini Tanzania ilikopa dola za kimarekani milioni sitini (USD 60m) kwa ajili ya mradi wa Kiwanda cha viatu Morogoro. Lengo la kiwanda kiwanda kile ilikuwa ni kuuza viatu nchini Italia. Mwaka mmoja baada ya kiwanda kuzinduliwa kilikuwa na uwezo wa kuzalisha kwa ufanisi wa asilimia 4 tu ya uwezo wake na hakikuweza kuuza hata jozi moja ya kiatu nje ya nchi. Miaka ya tisini kiwanda kile kiliuzwa katika mpango wa ubinafsishaji na hivi sasa kimegeuzwa kuwa ghala. Hata hivyo Deni hili lilipwa na kila Mtanzania kupitia kodi.

Kesho Jumanne tarehe 28 Januari, 2014 Kamati ya Bunge ninayoongoza ya Hesabu za Serikali (PAC) inapokea taarifa ya ukaguzi maalumu uliofanywa kuhusu Mfumo na Mchakato wa kusambaza pembejeo za ruzuku kwa wakulima. Ukaguzi huu umefanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG). Nimeipitia Taarifa hii na kukumbuka habari ya ‘Morogoro Shoe Factory’.

Bajeti ya pembejeo za ruzuku ya mwaka 2011/12 ilikuwa tshs 122.4 bilioni, kati ya hizo tshs 88.9 bilioni ni mkopo kutoka Benki ya Dunia. Taarifa ya CAG inaonyesha uvundo wa ufisadi katika mfumo mzima wa pembejeo za ruzuku. Katika kijiji cha Lunyala wilayani Nkasi mkoa wa Rukwa asilimia 70 ya wananchi waliorodheshwa kupata mbolea walikuwa bandia, hata hao waliopata mbolea walidai mbolea ilikuwa haina ubora stahili na matokeo yake uzalishaji wa mazao ulikuwa mdogo. Hata hivyo wasambaji wa mbolea walilipwa fedha zao zote. Afisa mmoja mwandamizi wa Benki ya Dunia alipata nukuliwa kusema kuwa asilimia 60 ya Bajeti ya pembejeo za ruzuku iliporwa na wajanja wachache.

Deni hili nalo litalipwa na Watanzania wote japo waliofadika ni wezi wachache. Kinachosikitisha ni kwamba masuala haya yanayohusu wananchi hayapati msukumo kwenye mijadala ya kitaifa. Tusipobadilika tutajikuta tuna madeni mpaka kwenye kope za macho yetu.

…mikopo haisaidii, hata tukiitumia kujenga shule au hospitali au viwanda lazima ilipwe. Mlipaji ni mkulima wa vijijini…” Azimio la Arusha, 1967.

Written by zittokabwe

January 27, 2014 at 3:52 PM

Posted in Uncategorized

Tagged with , ,

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Shilingi bilioni 620 za Deni la Taifa hazina maelezo

with 21 comments

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Shilingi bilioni 620 za Deni la Taifa hazina maelezo

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ametoa taarifa yake ya mwaka 2011/2012 na kuonyesha kuwa kuna skandali kubwa sana katika akaunti ya Deni la Taifa. Nanukuu

‘Uhakiki wa mchanganuo wa madeni ya Taifa kama ulivyokuwa tarehe 30 Juni, 2012 ulibaini kuwepo kwa marekebisho ya deni ya shilingi 619,803,554,183.91 ambayo uongozi haukuweza kutoa maelezo ya kuridhisha.’ (Taarifa ya CAG, Ripoti ya Serikali Kuu 2011/2012 uk 158). Mwisho wa Kunukuu

Katika Taarifa yake hiyo CAG anaendelea kuonyesha kuwa Deni la Taifa linazidi kukua na mwaka unaoishia mwezi Juni 2012 deni lilikuwa kwa asilimia 17 kutoka mwaka unaoishia mwezi Juni 2011.

Kukosekana kwa maelezo ya kuridhisha kuhusu zaidi ya nusu trilioni za Deni la Taifa ni jambo linalopaswa kutiliwa mashaka makubwa, kuchunguzwa na kupata majawabu stahiki. Tafiti mbalimbali duniani zinaonyesha kuwa kuna mahusiano makubwa sana kati ya Deni la Taifa la utoroshaji wa fedha kwenda kwenye mabenki ya ‘offshore’. Katika kitabu cha ‘Africa’s Odious Debts: How Foreign Loans and Capital flight bled a continent’ kilichoandikwa mabwana Leonce Ndikumana na James Boyce imeonekana kwamba Deni la Taifa huchochea utoroshwaji wa Fedha kwenda kuficha nje ya Tanzania.

Mabilioni haya kwenye akaunti ya Deni la Taifa yanashtusha sana. Kambi ya Upinzani Bungeni kwa miaka miwili mfululizo imekuwa ikitaka ukaguzi maalumu kwenye akaunti za Deni la Taifa lakini Serikali imeshindwa kufanya hivyo. Nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya PAC pia nimemtaka CAG afanye ukaguzi huu maalumu.

Kambi ya upinzani Bungeni ilisema hivi katika Bajeti yake kivuli 2012/13:

DENI LA TAIFA

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasikitika kwa serikali kuendelea kutengeneza madeni kwa Taifa kwa kuendelea kukopa zaidi kwa matumizi ya kawaida ya serikali. Wakati Serikali inasisitiza kwamba Deni letu linastahmilika, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali anaonyesha mashaka makubwa sana kutokana na kasi ya kukua kwa Deni la Taifa. Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonyesha  kuwa Deni la Taifa linazidi kuongezeka kwa asilimia 38% kutoka shilingi trillion 10.5 mwaka 2009/2010 hadi shilingi trillion 14.4 mwaka 2010/2011. Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha Deni la Taifa limefikia shilingi trillion 20.3 mpaka ilipofika mwezi Machi mwaka 2012. Ukisoma taarifa ya Mwezi wa Mei 2012 ya Benki Kuu ya Tanzania, Deni la Taifa sasa limefikia shilingi trillion 22.

Mheshimiwa Spika, Suala hapa sio ustahmilivu wa Deni kama inavyodai Serikali bali ni kwamba tunakopa kufanyia nini? Bajeti ya Mwaka 2012/13 inayopendekezwa inaonyesha kwamba Serikali itakusanya shilingi trilioni 8.7 kama makusanyo ya ndani na itatumia shilingi trilioni 10.6 kama matumizi ya kawaida. Ni dhahiri kwamba sehemu ya mikopo ambayo serikali inachukua sasa itakwenda kwenye matumizi ya kawaida. Hatutaki mikopo kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya posho, kusafiri, magari nk. Tuchukue mikopo kuwekeza kwenye miradi itakayokuza uchumi na kuzalisha kodi zaidi. Bajeti inaonyesha kwamba Serikali itakopa shilingi takribani trillion 5 mwaka 2012/13.  Serikali ikubalikutekeleza mapendekezoya Kambi ya Upinzani ya kuimarisha ukusanyaji  wa kodi na kupanua wigo wa kodi katika maeneo muhimu kama sekta ya madini na mawasiliano, kuzuia misamaha ya kodi, kutokomeza ukwepaji kodi, na kuepuka matumizi mabaya ili kuepuka madeni yasiyo ya lazima.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapenda kusisitiza kwamba Bunge lifanye ukaguzi maalumu kuhusu akaunti ya Deni la Taifa ili kuweza kubaini ukweli kuhusu ustahmilivu wa Deni na mikopo ambayo Serikali inachukua kama inakwenda kwenye Maendeleo na miradi ipi na kama miradi hiyo ina tija. Vilevile tumependekeza kwamba Mikopo yote ambayo Serikali inachukua iwe inapata idhini ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi au Bunge litunge sharia ili kiwango cha juu cha kukopa ambacho Serikali haipaswi kuvuka. Kuiacha Serikali inaendelea kukopa bila mpango ni kuliweka Taifa rehani na kupeleka mzigo wa kulipa madeni haya kwa kizazi kijacho. Hatuwezi kukubali Wazee wetu waishi maisha yao, waishi maisha yetu na pia wakope maisha ya watoto wetu. Mwisho wa kunukuu.

Kambi ya Upinzani inarejea kutaka ukaguzi maalumu kuhusu akaunti za Deni la Taifa na maelezo ya kina ya Serikali kuhusu shilingi 620 bilioni ambazo hazina maelezo kwenye Deni la Taifa. Hatuwezi kukaa kimya kuona Watanzania wanabebeshwa madeni ambayo kimsingi ni madeni bandia yanayotajirisha watu wachache wenye uwezo na ujasiri mkubwa wa kuiba, kupora nakufisidi hazina ya Taifa letu.

Kabwe Zuberi Zitto,Mb

Waziri Kivuli Fedha na Uchumi

Written by zittokabwe

April 13, 2013 at 5:00 PM