Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Posts Tagged ‘Baadhi ya kazi za Zitto Bungeni

Baadhi ya kazi za Zitto Bungeni

with 10 comments

Baadhi ya kazi za Zitto Bungeni

Kwa uzito na mahala unapofanyika mkutano huu, naomba niwaletee kwa muhtasari kabisa baadhi ya kazi ambazo Ndugu Zitto Kabwe amezifanya katika kusukuma mbele guruduma la maendeleo katika nchi yetu.

  1. MABADILIKO SEKTA YA MADINI

Zitto alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mbunge mwaka 2005 akiwakilisha Jimbo la Kigoma Kaskazini ambalo halina mgodi hata mmoja wa madini ukiachana na wachimbaji wadogo wa udongo wa Pemba ambao una soko kubwa hapa Kariakoo jijini Dar es Salaam. Hata hivyo ajenda inayomtambulisha Zitto Kabwe kwa Taifa ni ajenda ya mabadiliko makubwa aliyoanzisha katika sekta ya Madini nyakati ambayo hakuna mwanasiasa aliyethubutu kukosoa sera za uwekezaji kwa namna aliyofanya. Baada ya kudokezwa kuwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Bwana Nazir Karamagi amesaini mkataba mpya wa Madini akiwa hotelini nchini Uingereza, Zitto alimtaka Waziri kujieleza ndani ya Bunge kuhusu mkataba huo na masharti yake ya kikodi. Waziri huyo aliposhindwa Zitto aliwasilisha Hoja Binafsi Bungeni (akiwa mbunge wa kwanza kufanya hivyo katika Bunge la Tisa na la Nane kwa pamoja). Hoja ya Buzwagi ilisababisha Zitto kusimamishwa ubunge kwa miezi 4. Hata hivyo mnamo Septemba 10, 2007 alitangaza Azimio la Songea lililomshinikiza Rais Jakaya Kikwete kuunda Kamati ya Bomani ili kupitia mikataba yote ya Madini nchini.

Kutokana na kazi yake hiyo leo Tanzania ina Sera mpya ya Madini na Sheria mpya ya Madini ambayo imeboresha nafasi ya Tanzania kufaidika na Madini, imeruhusu kisheria Serikali kuwa na hisa kwenye migodi ( na hivi tunavyoongea, kwa mfano, sasa Serikali inamiliki 50% ya Mgodi wa TanzaniteOne). Makampuni ya Madini ambayo yalikuwa yanatangaza hasara kila mwaka leo yanalipa kodi ya Mapato na Halmashauri zenye migodi zinalipwa ushuru wa huduma wa mabilioni ya fedha. Huyu ndiyo Kiongozi wetu wa ACT Wazalendo. Hawa ndio Viongozi Taifa hili linawataka. Viongozi wanaotenda na kutoa majawabu ya changamoto za nchi. Sio Viongozi wanaolaumu tu eti wakisubiri kushika dola ndio watende. Nani anayebisha rekodi hii?

 

  1. KUZUIA UBINAFSISHAJI WA SHIRIKA LA BIMA LA TAIFA (NIC) 

Zitto Kabwe alikuwa Waziri Kivuli wa Mipango na Uchumi mwaka 2006 wakati Shirika la Bima la Taifa likiwa kwenye mchakato wa Ubinafsishaji. Wafanyakazi wa TUICO Tawi la Bima walimfuata wakielezea kwa ushahidi namna mali za Shirika zilivyopangwa kuuzwa na wajanja wachache kutaka kujiuzia Shirika na Mali zake hasa jengo la kitega uchumi kwa bei ya kutupwa. Zitto aliwakilisha hoja hiyo kwenye Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi chini ya Mwenyekiti wake Ndugu Abdallah Kigoda na kuishawishi Kamati kukataa ubinafsishaji wa NIC na badala yake kuunda kikosi kazi cha kurekebisha Shirika na liendelee kuwa Mali ya Umma.

Mwezi Novemba Mwaka 2006 Baraza la Mawaziri lilikubaliana na hoja za Zitto alizotoa kwenye Kamati ya Bunge na ndani ya Bunge na kuamua kuliondoa Shirika kwenye mchakato wa ubinafsishaji na leo hii Shirika limebaki kuwa la Umma na limeanza kurudi kwenye hali yake. Aliendelea kulisaidia Shirika la Bima kwa kuagiza (akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali ) kuwa Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma yaweke Bima kupitia Shirika la Bima la Taifa na agizo hilo kutekelezwa na Mashirika mengi ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania.

Sio Bima tu, Zitto akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma aliagiza kuondolewa katika orodha ya ubinafsishaji Shirika la STAMICO ili liweze kushiriki kikamilifu katika sekta ya Madini na liliondolewa. Huo ndio Ujamaa wa kidemokrasia ambao Chama chetu cha ACT-Wazalendo kinautangaza, na huyo ndio Kiongozi wetu ambaye ana uzalendo wa dhati kwa mali za Watanzania. Nani anayebisha rekodi hii?

 

  1. SHERIA YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA

Mwaka 2008/2009 Zitto Kabwe aliweka rekodi nyingine ya kuwa Mbunge wa kwanza kuzungumzia mabadiliko ya sheria ya viongozi wa umma ili kuipa meno secretariat ya maadili ya viongozi na kutengenisha biashara na siasa. Alipeleka Bungeni Muswada Binafsi wa Sheria ili kufanya mabadiliko makubwa ya Sheria Maadili. Hata hivyo muswada ule ulizuiwa na Serikali kuingia Bungeni licha ya kukamilisha kila hatua iliyopaswa.

Leo hii Chama chetu kinazungumzia kurejesha Miiko ya Viongozi kuna watu wanadhani Zitto kaanza haya hivi sasa, la hasha. Huu ni mwendelezo wa yale aliyokuwa anaamini miaka kadhaa iliyopita na kwa kuwa yeye anapenda kutembea anayoyasema alitushawishi wenzake kufanya Miiko ya Viongozi kuwa sehemu ya Katiba ya Chama chetu. Yeye ni Kiongozi wa kwanza wa kisiasa kuweka hadharani Mali na Madeni yake hapa nchini. ACT Wazalendo ni chama pekee cha siasa hapa nchini ambacho Viongozi wake wanatakiwa kikatiba kutangaza Mali zao, Madeni yao na Maslahi yao ya kibishara. Nani anabisha rekodi hii?

 

  1. UKAGUZI WA MAHESABU WA VYAMA VYA SIASA

Katika kuhakikisha kuwa kila senti ya fedha ya umma inakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali, Ndugu Zitto Kabwe aliwasilisha Bungeni mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa, Sheria namba 5 ya Mwaka 1992 na kuwezesha CAG kukagua fedha za vyama ambazo zinatoka Serikalini kama ruzuku. Sheria ya Vyama vya siasa inataka kila Mwaka Serikali kutenga kiwango kisichozidi asilimia mbili (2%) ya Bajeti ya Serikali kama ruzuku kwa vyama vya siasa. Vyama hupewa wastani wa Shilingi bilioni 20 kila mwaka na kugawana miongoni mwao lakini fedha hizi zilikuwa hazikaguliwi kinyume na Sheria za Fedha.

Baada ya Sheria hiyo kupitishwa na Bunge mwaka 2009, Zitto alisimama kidete kuhakikisha inatekelezwa jambo ambalo lilimletea uhasama mkubwa sana na viongozi wenzake katika chama chake cha zamani akiwa Naibu Katibu Mkuu. Zitto alipigana kwa kushirikiana na Wazalendo wenzake katika Kamati ya Bunge ya PAC na kufanikiwa na hivi sasa vyama vyote vinakaguliwa na kuweka rekodi nyingine katika nchi nyingi za Afrika. Kwa kazi hii iliyotukuka Zitto Kabwe amedhibiti fedha za umma kwa vyama vya siasa na hivi sasa taarifa za mahesabu ya vyama ipo wazi, na tumeona vyama vyote vikiwa na hati chafu, vikiwemo vyama vya upinzani vya zamani. Ni wajibu wa wanachama wa vyama hivyo kuwawajibisha viongozi wao wanaogeuza fedha za ruzuku kuwa ni fedha zao binafsi. Nani anabishia rekodi hiyo ya Kiongozi wetu?

 

  1. KUFUFUA ZAO LA MKONGE

Mwaka 2012 Zitto Kabwe aliweka rekodi nyingine tena akiwa mbunge wa kwanza katika Bunge la 10 kuwasilisha Hoja Binafsi. Aliwasilisha Hoja Binafsini Bungeni akitaka Serikali kufufua Kilimo cha Mkonge kwa kuwanyanganya wawekezaji wakubwa mashamba waliyobinafsishiwa na kuyaacha bila kulimwa na badala yake mashamba yale wapewe wakulima wadogo. Zitto alitaka kubadilisha mfumo wa kulima Mkonge kutoka mashamba makubwa yanayomilikiwa na tajiri mmoja na kulimwa na manamba mamia na kwenda kwenye mfumo ambao wakulima wadogo wadogo wanalima Mkonge na hivyo kushirikisha wananchi wengi zaidi kwenye uchumi wao.

Hoja hiyo ilipingwa na Wabunge kutoka Tanga lakini iliungwa mkono sana na wananchi wa mkoa huo na hivyo kumwona Zitto kama mwakilishi wao licha ya kwamba alikuwa akiwakilisha Jimbo la Kigoma Kaskazini.

Katika Chama chetu ajenda ya kumilikisha Ardhi wananchi ni ajenda kubwa na ACT Wazalendo kimekua chama cha kwanza nchini kutangaza kinagaubaga kuwa kitazuia uporaji wa Ardhi na kumilikisha wananchi ardhi yao wenyewe. Nani anabishia rekodi hiyo?

 

  1. KURASMISHA KAZI ZA SANAA NA BURUDANI NCHINI

Kwa muda mrefu sana wadau wa tasnia ya sanaa na burudani nchini walikuwa wanalalamika kazi zao kutokuwa rasmi na hivyo kuibiwa na mchango wao katika uchumi kutotambuliwa. Mwaka 2012 Zitto Kabwe akiwa Waziri Kivuli wa Fedha alifanya kampeni maalumu ya kuhakikisha kuwa wasanii hawanyonywi na kazi zao kutambuliwa rasmi. Aliwasilisha Bungeni mabadiliko ya Sheria ya Ushuru bidhaa ili kutambua rasmi kazi za sanaa na burudani na kuhakikisha kuwa wasanii wanalipwa wanavyostahili katika biashara ya miito ya simu.

Sheria hiyo ilipitishwa na Bunge na Mamlaka ya Mapato Tanzania ikaanza kutoa stempu rasmi katika CDs za kazi za sanaa ili kudhibiti wazalishaji kuwanyonya wasanii. Katika Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2015 tasnia ya Sanaa na Burudani imekuwa sekta rasmi ya Uchumi na imeripotiwa kuwa sasa ina thamani ya shilingi 270 bilioni kama mchango wake katika Pato la Taifa. Hivi sasa Wasanii wanafaidika maradufu kwa kazi zao kuuzwa kama miito ya simu na wengine wanapata mamilioni ya shilingi na kuboresha maisha yao kwa jasho lao. Nani anabisha rekodi hii?

 

  1. KUDHIBITI UKWEPAJI KODI NA MISAMAHA YA KODI 

Wawekezaji kutoka nje wamekuwa wakiibia nchi yetu kwa kubadilisha badilisha majina ya makampuni yao na kubadili wamiliki bila ya kulipa kodi hapa nchini. Watanzania mnakumbuka jinsi majina ya mahoteli makubwa yalivyokuwa yakibadilishwa. Kwa mfano kutoka Sheraton kwenda Moevenpick na kwenda Serena sasa. Makampuni ya Simu yalivyokuwa yakibadilishwa. Kwa mfano kutoka Mobitel kwenda Buzz kwenda Tigo.

Vile vile kutoka Celtel kwenda Zain na kwenda Airtel. Haya yamekuwa yakitokea kwenye maeneo mengi zaidi ya haya. Yote haya yalitokea bila ya Serikali kupata kodi yeyote. Kwenye mauzo ya Zain kwenda Airtel Serikali ilipoteza dola za Kimarekani 312 milioni ( zaidi ya shilingi bilioni 600 kwa bei za sasa za dola ). Kwa uchungu kwa nchi yake Zitto Kabwe aliwasilisha Bungeni muswada wa sheria wa kurekebisha sheria ya kodi ya Mapato na kuanzisha tena kodi ya ongezeko la mtaji ( Capital Gains Tax ).

Marekebisho hayo yalipitishwa na Bunge kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2012 na mwaka huo huo Tanzania ilipata mapato ya shilingi bilioni 50 kwa mauzo ya Kampuni ya BP kwenda PUMA. Mwaka 2014 Tanzania ilipata dola za kimarekani 222 milioni ( zaidi ya tshs 450 bilioni )kwa mauzo ya sehemu ya vitalu vya gesi asilia vya kampuni ya Ophir kwenda kampuni ya Pavilion ya Singapore.

Zaidi ya hapo Zitto na wazalendo wenzake katika Kamati ya PAC walitoa maagizo ya kuhakikisha kuwa Misamaha ya kodi yote inakaguliwa na ukaguzi wake kuwekwa wazi ili kudhibiti mianya ya matumizi mabaya ya misamaha hiyo. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania CAG anakagua misahamaha ya kodi na PAC iliweka wazi taarifa ya kwanza ya ukaguzi wa misamaha ya kodi. Nani anabishia rekodi hizi?

 

  1. MABILIONI YA USWISS 

Mwaka 2012 mwezi Novemba Zitto Kabwe aliwasilisha Bungeni Hoja Binafsi kuhusu mabilioni ya Uswisi ikiwa na lengo la kutaka uchunguzi ufanyike kuhusu Watanzania wanaoficha fedha nje ya nchi kinyume cha sheria. Bunge lilipitisha hoja hii binafsi na kuitaka Serikali kufanya uchunguzi kuhusu Watanzania wanaotorosha fedha kwenda nje na kuchukua hatua stahiki za kisheria. Tanzania iliingia katika rekodi ya kuwa nchi ya kwanza katika nchi za Jumuiya ya SADC kupitisha Azimio la Bunge kuhusu suala la utoroshaji wa fedha. Licha ya kwamba Serikali haijatoa taarifa yake miaka miwili sasa toka Azimio la Bunge namba 9 la mwaka 2012, na baada ya danadana ya muda mrefu kutoka vyombo vinavyohusika Kiongozi wetu Zitto Kabwe ameamua leo kupasua jipu la hoja hiyo kwa kuweka wazi orodha ya kwanza ya Watanzania 99 wenye akaunti katika Benki ya HSBC ya Uswiss. Uongozi ni umakini, na sio kukurupuka na kujitafutia sifa za harakaharaka. Ilikuwa ni muhimu Ndugu Kabwe kufuata taratibu zote kabla ya kuanika majina hayo hadharani. Sasa leo baada ya kujiridhisha pasipo shaka atayaanika majina hayo hadharani na wale waliokuwa wanambeza kwamba kashindwa wanyamaze milele! Huyo ndio Zitto, mwenye uvumilivu na ujasiri usio kifani. Anatenda anayosema. Nani anabisha rekodi hii?

 

  1. KUWAJIBISHA MAWAZIRI 

Katika historia ya Tanzania ni Wabunge wawili tu walioweza kutoa hoja zilizopelekea Mawaziri wengi kuondolewa madarakani kwa mpigo. Ni Zitto Kabwe na Dkt. Harrison Mwakyembe ambaye aliongoza kamati teule ya Bunge iliyochunguza Mkataba wa kampuni feki ya kufua umeme ya Richmond. Hoja hii ilipelekea Waziri Mkuu kuwajibika kwa kujiuzulu na hivyo kumlazimisha Rais wa Jamhuri ya Muungano kuunda upya Serikali kwa kuteua Waziri Mkuu mwingine.

Zitto ana rekodi ya kipekee. Kwanza mwaka 2012 baada ya Taarifa ya CAG kuonyesha madudu katika matumizi ya fedha za umma, Zitto alikusanya sahihi za wabunge 75 na kuandika hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu. Shinikizo hili lilipelekea Rais kufukuza kazi mawaziri 8 ambao Wizara zao zilitajwa kuwa na mahesabu machafu. Pili mwaka 2013 baada ya Kamati ya Mali Asili na Mazingira kutoa taarifa yake Bungeni kuhusu Operesheni Tokomeza, Zitto alisimama ndani ya Bunge na kubadilisha mjadala kwa kutaka Mawaziri wote ambao watendaji wao walitesa wananchi kuwajibika. Mawaziri 4 waliwajibika.

Tatu, mwaka 2014 katika Taarifa Maalumu ya Kamati ya PAC kuhusu uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Escrow ya Benki ya Tanzania, Zitto na wazalendo wenzake wa kamati hiyo walipelekea Mawaziri wawili maarufu kama mawaziri wa Escrow na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwajibika. Uwajibikaji umekuwa ni ajenda kubwa ya Kiongozi wetu na amekuwa hana aibu hata kwa watu anaowaheshimu na rafiki zake. Alitaka wawajibike huku akiwatazama usoni. Ni Viongozi wachache sana wenye ujasiri wa aina hii. Huyu ndio Kiongozi wa chama chetu cha ACT Wazalendo. Nani anabisha rekodi hii?

 

  1. KUKATAA POSHO ZA KUKAA

Mwaka 2010 chama chake cha zamani waliweka katika Ilani yao ya Uchaguzi kupinga posho kama hatua ya kubana matumizi ya Serikali. Wakakubaliana kuwa wabunge wa chama chao hawatapokea posho ya kukaa (sitting allowance). Hata hivyo, ilipokuja katika utekelezaji wenzake wote wakagwaya na Ndugu Zitto Kabwe ni mbunge pekee aliyepinga posho za vikao na kuzikataa kata kata kwa miaka mitano (5) mfululizo, ambazo ni takribani shilingi milioni 21 kila mwaka. Katika kipindi hicho cha miaka mitano Zitto alikaa kuchukua jumla ya Shilingi Milioni Mia Moja na Tano (105,000,000)!! Kukataa pesa yote hii kwa sababu ya ‘principle’ tu ni jambo nadra sana kutokea katika mazingira yetu. Zitto anatembea maneno yake. Zitto anatenda anayonena. Sasa kwa yote hata kwa nini wasimchukie wenye roho zao za kwa nini?

Ndugu Wananchi,

Huyu ndio Kiongozi wa Chama chetu. Tunachoomba Watanzania mumhukumu Zitto kwa rekodi zake na si kwa propaganda za mahasimu wake.

Written by zittokabwe

July 6, 2015 at 11:12 AM