Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Posts Tagged ‘afya

Siku ya 9 ya Ziara ya CHADEMA Kanda ya Magharibi – Jimbo la Igunga, Wilaya ya Igunga

with one comment

Siku ya 9 ya Ziara ya CHADEMA kanda ya Magharibi imetufikisha Jimbo la Igunga, Wilaya ya Igunga.

Tumefanya mikutano 6 katika kata sita tofauti, tumefungua matawi ya chama na kuhutubia wananchi. Pia tumepokea kero za wananchi zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.

Tukiwa Katika kata ya Choma tumeshuhudia kiwanda cha kuchambua Pamba kilicho binafsishwa kikiwa kimetelekezwa na mwekezaji toka mwaka 1998. Ginnery hii iliyokuwa mali ya umma na kuajiri wafanyakazi 500 kwa shifti 3 kila siku (jumla 1500) nyakati za msimu imekufa na baadhi ya Mashine kuuzwa kama chuma chakavu. Kijiji cha Choma kimedorora kiuchumi kutokana na ubinafsishaji huu. Nimewaeleza wananchi kuwa nitafuatilia suala hili la Ginnery ya Manonga, katani Choma na kuwajulisha hatua mwafaka za kuchukua.

Nimependekeza pia kwamba iwe marufuku kuuza nje mazao ghafi kwani tunakuwa tunauza ajira za watu wetu. Suala hili nimekuwa nikilisema Bungeni mara kwa mara kwamba ni lazima kusafirisha mazao yaliyoongezwa thamani kwa kupiga marufuku kuuza korosho ghafi, Pamba ghafi, kahawa ghafi na Katani ghafi. Viwanda vya kilimo vinaongeza ajira sana kwa wananchi na ni suluhisho endelevu kwa tatizo la ajira na kuondoa umasikini.

Niliwapa mfano wa kiwanda kilichouzwa huko mtwara na kugeuzwa godown la kuhifadhi korosho na godown liligeuzwa kuwa kiwanda cha kubangua korosho! Niliwaeleza namna viongozi wa Serikali wanavyochanganya dhana ya uhuru wa biashara (liberalisation) na ubinafsishaji (privatisation). Dhana mbili zinazochanganya watawala wengi wa Afrika na kujikuta wakiuza mali za umma kiholela. Unaweza kuwa na Mashirika ya Umma yakishindana katika soko na makampuni binafsi. Ubinafsishaji holela unatengeneza ‘private monopolies’ na kuathiri sana ukuaji wa uchumi kutokana na ufanisi mdogo ie efficiency.

Nimerejea wito wangu wa kutaka sera ya hifadhi ya jamii kwa wakulima kupitia vikundi vyao na ushirika. Nimesisitiza umuhimu wa kuweka akiba ili kuongeza uwekezaji wa ndani na hasa uwekezaji wa miundombinu ya kilimo. Nimeonya tabia ya wananchi kukimbilia kulipwa fidia badala ya kutaka kushiriki katika miradi mikubwa ya kilimo. Kilimo endelevu ni kilimo cha wakulima wadogo wanapata huduma pamoja (integrated production schemes) badala ya wakulima wakubwa wenye kuhitaji manamba. ‘outgrower’s schemes’ ndio mwelekeo sahihi kuwafanya wananchi wamiliki ardhi, wawe na ushirika imara, wawe na hifadhi ya jamii na waondokane na umasikini.

Leo nikiwa kijijini Choma na mjini Igunga nimewaambia wananchi umuhimu uwazi wa mapato ya viongozi wa umma. Nimewaambia kuwa mishahara ya viongozi wa umma haipaswi kuwa siri na inapaswa kukatwa kodi. Kama nilivyoahidi niliokuwa mjini Mpanda, nimewaambia kuwa mshahara wa Rais wa Tanzania ni Tshs 384m kwa mwaka. Kipato hiki hakikatwi kodi na Rais hupata huduma mbalimbali bure. Niliahidi kwamba kwa kuwa gazeti la Mwananchi lilifungiwa kwa sababu ya kutaja mishahara ya watumishi wa Serikali, basi ni vema kuonyesha Serikali kuwa lile sio kosa na wananchi wana haki ya kujua. Ndio maana nikachukua hatua ya kutaja kipato cha Waziri Mkuu na Rais.

Nimemaliza awamu ya kwanza ya ziara ya kanda ya Magharibi. Nimetembelea jumla ya kata 53 katika majimbo 10 ya uchaguzi ya mikoa ya Katavi na Tabora. Siku si nyingi nitamalizia majimbo ya Urambo na Kaliua kisha Mkoa wa Kigoma. Nimefarijika sana na mwitikio wa wananchi wanaotaka mabadiliko. Wazee kwa Vijana, kina mama kwa kina baba, wanataka mabadiliko.

Nimesononeshwa na kiwango cha umasikini wa wananchi na huduma mbovu za kijamii kama Maji, Elimu na Afya.

Nimeumizwa sana na unyonyaji mkubwa dhidi ya wakulima wa Pamba na Tumbaku.

Nimekasirishwa sana na ufisadi mkubwa wa fedha za umma kupitia mbolea ya ruzuku.

Nina Hofu kubwa ya wanasiasa wengi kutojua changamoto hizi za wananchi lakini wakitaka kupewa dhamana.

Nina Hofu na wanasiasa ‘manipulative’ lakini nina matumaini kuwa viongozi ‘inspirational’ watasimama kidete kushika usukani wa jahazi letu na kulifikisha salama. Tanzania ina kila sababu ya kuendelea, hatuna cha kupoteza isipokuwa minyororo ya umasikini.

Chukua hatua!

This slideshow requires JavaScript.

Written by zittokabwe

October 14, 2013 at 8:42 AM

MKULIMA hana Pensheni? RUMAKO, Kigoma wamekataa

with 3 comments

MKULIMA hana Pensheni? RUMAKO, Kigoma wamekataa

Mkutano na uongozi wa chama cha RUMAKO

Mkutano na uongozi wa chama cha RUMAKO

Jumapili ilio pita, tarehe 25 Agosti 2013, nilikutana na wanachama wa Chama cha Ushirika cha Rumako, chama cha msingi cha Ushirika kinachojumuisha wakulima wa Kahawa wa Vijiji vya Matyazo na Mkabogo katika Halmashauri ya Wilaya Kigoma na Rusaba katika Halmashauri ya Wilaya Buhigwe. RUMAKO ni sehemu ya Ushirika wa Kanyovu ambao wanachama wake ni vyama vya Ushirika vya msingi katika Mkoa wa Kigoma. Huu ulikuwa ni Mkutano Mkuu wa RUMAKO kujadili kuhusu maswala ya hifadhi ya jamii, afya, pembejeo na maendeleo yao kiuchumi.

Mapema mwaka huu nilizungumza na wanachama wa RUMAKO ambao walinipa malalamiko yao kuhusiana na mfumo mzima wa ulimaji na uuzaji kahawa katika jimboni Kigoma Kaskazini. Wakulima hawa walikua na changamoto nyingi za kiuchumi.

Kwanza hali ya maisha ya mkulima ni ya ufukara mno, na kwa hapa Tanzania tunaweza kusema ni kundi la wasio nacho kiuhalisia ingawa kuna baadhi yao kipato chao kinaweza kuwaweka kama watu wenye kipato cha kati kwa tafsiri za Benki ya Dunia. Mfumo wa Ukulima Kahawa unawaacha wakulima wakiwa katika mzunguko wa umasikini (vicious cycle of poverty) kwani hutumia fedha nyingi kuandaa shamba na kununua pembejeo na kwa kuwa hawana fedha hukopa na baada ya kuuza mazao takribani fedha yote hulipia mikopo yao. Zinazo baki ndio za matumizi ya kawaida. Wanapofika miaka ya kustaafu, wakulima hawa hawana hifadhi yoyote sababu asilimia 100 ya kipato hiki hutumika kwa matumizi yao ya nyumbani, matumizi ya afya, ununuzi wa pembejeo, ununuzi  wa mbolea nk. Ule msemo wa ‘Mkulima hana pensheni’ unadhihirishwa na mfumo huu nilioueleza.

Upande wa afya napo hali ya wananchi hawa wa Ushirika wa RUMAKO ni mbaya sana. Magonjwa mengi yanawakabili wakati hawana bima yoyote. Tafiti mbali mbali zimeoneya uhusiano mkubwa kati ya Afya na Tija , pia kati ya Afya bora na muda wa kuishi. Vile vile ule msemo wa ‘mkulima hana Bima’ nao unadhihirishwa na hali hii ambapo Mkulima inabidi awe ana akiba ya kutosha kuweza kumudu matibabu, vinginevyo hupoteza maisha. Hivyo kwa kuwa Wananchi hawa hawana Bima ya Afya, Tija yao inakuwa chini na hatimaye maisha yao yanakuwa dhaifu.

Suala la Pembejeo ni nimewahi kuzungumzia mara nyingi ndani na nje ya Bunge. Pembejeo zinazo tolewa na wizara ya Kilimo kupitia mfumo wa ‘ruzuku ya pembejeo’ zinamfikia mkulima wa RUMAKO na wakulima wengine nchini kwa kuchelewa sana kiasi kwamba hazina kabisa kazi wakati zinapo fika. Pia wananchi wamejikuta mara kwa mara waki saini fomu za kupokea pembejeo bila kuzipokea. Niliwahi kuambiwa kijijini Bitale kuwa mawakala wa pembejeo za ruzuku hulipa wananchi shilingi 2000 ili kununua ‘vocha; zenye thamani ya shilingi 37,000. Pale Matyazo niliambiwa kuwa walisainishwa kupokea mbegu za Mahindi za ruzuku na hazikufika! Jitihada za RUMAKO kuwa wakala wa kugawa pembejeo hazikufanikiwa na badala yake pembejeo huuzwa katika maduka ya watu binafsi. Kuna mtandao mkubwa sana wa kifisadi wa utoroshaji pembejeo nchini. Kwa upande wa Kigoma Kaskazini pembejeo hizo zimeonekana zikivushwa mpaka wa Tanzania na Burundi. Bungeni mara kadhaa nimeomba kufutwa kwa mfumo huu wa kifisadi lakini wenye ‘vested interests’ hawataki kabisa licha ya wao wenyewe kujua kuwa mbolea ya ruzuku ni wizi. Kila mwaka katika muda wa miaka saba iliyopita Serikali inagawa fedha za ruzuku ya mbolea wastani wa shilingi sitini bilioni. Asilimia hamsini ya Fedha hizi huibwa na wajanja kuanzia Wizarani mpaka vijijini. Huko Iringa marehemu walionekana kwenye orodha ya watu waliopewa mbolea ya ruzuku.

Ule msemo wa ‘benki sio rafiki wa masikini’ unadhihirishwa na wakulima hawa. Kwa miaka 10 wamekuwa wakipata mkopo wa kununua Kahawa kutoka katika Moja ya Mabenki hapa nchini. Riba imekuwa ya wastani wa asilimia 15 – 18. Wakulima hawa hukopa mwezi Septemba na hurudisha mkopo mwezi Januari baada ya kuuza Kahawa yao mnadani Moshi. Katika hali ya kushangaza sana Benki hiyo ilikuwa inawatoza riba ya mwaka mzima hata kama mkopo wamekaa nao kwa miezi minne tu! Hii ndio ‘vicious cycle of poverty’ haswa. Mkulima anabaki pale pale mwaka hadi mwaka. Akiumia kazini hana fao la ajali wala fao la matibabu. Akizeeka hana pensheni. Mfumo wetu wa fedha unamfanya mkulima aendelee kuwa hohe hohe. RUMAKO imeamua kujikomboa.

RUMAKO kupitia mkutano wake mkuu iliamua kuwaita watu wa NSSF ili wawaeleze kama Mkulima anaweza kuwa mwanachama. Waliniomba kuwafikishia ujumbe wao kwa Shirika hilo. Ni ndoto yangu ya miaka mingi sana kuona mtanzania wa kawaida anakuwa na hifadhi ya jamii. Watanzania wanao jiunga NSSF hadi sasa ni waajiriwa wa serikali au wa makampuni binafsi, na sio wakulima. NSSF ilitaka mazungumzo ya moja kwa moja na bodi ya RUMAKO kuhusu hifadhi ya jamii na faida zake zote, huku wanachama wa RUMAKO wakiwaelewesha pia wawakilishi wa NSSF kuhusu mfumo wa ulimaji kawaha. Wanachama wa RUMAKO waliamua kwa kauli moja kujiunga na NSSF na wakalipia michango kwa miezi sita kwa walikuwa kwenye mfumo wa mavuno. Hata hivyo ni wanachama 700 tu wa RUMAKO waliojiunga mpaka ninapoandika makala hii.

Ukombozi wa Mkulima

Mkutano na Wakulima wa Kahawa

Mkutano na Wakulima wa Kahawa

Huu ni msimu wa Kununua Kahawa. RUMAKO wameachana na ile Benki iliyokuwa inawatoza riba ya asilimia 15-18 kwa mwaka wakati wao wanakaa na mkopo chini ya nusu mwaka. NSSF inawatoza riba kulingana na muda ambao wakulima hukaa na mkopo. RUMAKO ina rekodi isio tia shaka kuwa huuza kahawa yao na kulipa mkopo ndani ya miezi 3-4. Kwa uamuzi huu tu RUMAKO itaokoa zaidi ya shilingi milioni mia tatu kwa mwaka. Fedha hii inayookolewa kutokana na riba peke yake inaweza kulipia michango ya wakulima hawa kwa NSSF kwa mwaka mzima na wakulima kuwa na Bima ya Afya na mafao mengine ambayo NSSF hutoa. Mkopo huu utahusu mambo matatu ambayo ni Mkopo wa malipo ya awali kwa wakulima kwa kahawa iliyokusanywa ili kuuzwa, mkopo wa pembejeo na hivyo kuondokana kabisa na utegemezi wa pembejeo za ruzuku ambazo hazifiki kwa wakati, Mkopo wa kuandaa mashamba ili kuongeza uzalishaji (tija kwa ekari).

Kujiunga huku kwa wakulima wa RUMAKO katika NSSF kuna matokeo gani kwao wenyewe na kwa jamii zao? Faida kubwa ni kuAa wanachama hawa sasa wamepata bima ya afya. Bima hii ni kuhusu matibabu ya magonjwa yao wote pamoja na familia zao, ikiwemo fao la ajali kazini na fao la kujifungua kwa kina mama wajawazito. Uamuzi huu pekee umehakikisha Hifadhi ya Jamii kwa wakulima 700 na wategemezi wao 5 (Baba, Mama na Watoto 4). Wakulima wa Ushirika wa RUMAKO sasa wana uhakika na maisha yao ya uzeeni maana wanajiwekea akiba ambayo ina faida kubwa sana. Ule msemo wa ‘Mkulima hana Pensheni’ unaanza kufutwa na wakulima hawa wa vijiji vya Matyazo, Mkabogo na Rusaba. Kufikisha hifadhi ya Jamii kwa mkulima ni mapinduzi tosha ambayo wengi hawaamini kama inatokea.

Ni faida gani kwa mfuko wa hifadhi ya jamii NSSF? Licha ya kusuasua kuingia katika sekta inayoitwa isiyo rasmi, mifuko ya Hifadhi ya Jamii imethibitishiwa kuwa wanaweza kufikisha huduma zao kwa watu masikini. NSSF sasa imepata wanachama 700 kwa mkupuo katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja. Wanachama hawa wamelipa michango yao sio tu kwa wakati bali wamelipa kwa miezi sita mbele kwani kipato chao kinatokana na  msimu kwa hiyo wana uhakika wa kulipa. Kwa kuwa wakulima hawa wanalipa sawa na michango ya watu wa kima cha chini cha mshahara, viwanda vingapi hapa tayari kwa ujumla wa wanachama hawa? Tayari mkoani Kigoma, hasa Halmashauri ya Wilaya Kigoma na Uvinza wameanza mkakati wa kupanua suala hili mpaka kwa wakulima wa Michikichi na Tumbaku. Kuna mkakati wa kufikia wakulima 100,000 katika kipindi cha miaka mitano. Hii itakuwa sawa asilimia 10 ya wanachama wa mifuko ya hifadhi ya Jamii waliopo nchini hivi sasa. Mapinduzi yanatokea magharibi mwa Tanzania. Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ifungue macho. Wakulima wanakopesheka. Wakulima wanaweza kuwa na pensheni. Inatokea Matyazo.

Itokee Tandahimba pia!

Written by zittokabwe

August 28, 2013 at 12:12 PM