Vitabu 23 nilivyosoma mwaka 2015(The 23 Books I read in 2015) #letsread
Vitabu 23 nilivyosoma mwaka 2015
Zitto Kabwe
Nimesoma vitabu 23 tu mwaka huu unaoisha leo.
Mwaka 2015 ulikuwa mwaka wa uchaguzi, nimesoma zaidi kidogo ya nusu ya https://zittokabwe.wordpress.com/2014/12/27/vitabu-nilivyosoma-2014-books-i-have-read-in-2014-booksread2014-letsread/ .
Katika mwaka 2015 niliweza kufanya uchambuzi wa vitabu 4 tu kwani ilipofika mwishoni mwa mwezi Machi, 2015 nilianza kazi mpya kabisa ya kujenga Chama kipya cha Siasa chenye kufuata mrengo wa kushoto – ACT Wazalendo.
Niliweza kuchambua 1. The Establishment, Owen Jones 2. The Alchemist, Paulo Coelho 3. The Last Banana, Shelby Tucker na 4. Act of Treason, Vince Flynn. Natumai nitarejesha safu yangu ya Kitabu na Kalamu ya gazeti la #RaiaTanzania kuanzia Januari, 2016.
Baadhi ya vitabu nilivyosoma mwaka huu ni marudio ya vitabu nilivyosoma zamani ili kujikumbusha mambo Fulani Fulani. Mfano hivi sasa najitahidi sana kusoma vitabu nilivyosoma shule ya sekondari katika ‘literature’ ili kuelewa zaidi na kulinganisha na hali ya sasa. Ndio maana mwaka huu nilirudia kitabu cha A Man of the People cha Chinua Achebe mara tu baada ya uchaguzi. Kiukweli huwa narudia rudia sana vitabu vya Achebe kutafuta ulinganisho wa hali ya siasa ya miaka ya sitini na miaka hii ya sasa. Vile vile najaribu kuelewa suala la #Biafra kutoka katika jicho la mwandishi.
Mwaka huu nimejitahidi sana kusoma ‘fiction’ na nimefurahia sana juhudi hizo japo niliuweka kando ushairi na sikuweza kabisa kumaliza The Capital, Thomas Piketty. Kwa kuwa nimedhamiria kujikita tena kwenye taalumu yangu ya Uchumi na kutumia taaluma hiyo kwenye siasa za Bunge, nitamaliza The Capital In’Sha Allah. Ninataraji kufungua mwaka na The Courage to Act: A Memoir of a crisis and its aftermath, Ben S. Bernanke. Kitabu hiki nililetewa kama zawadi na @Ritaupara, mmoja wa rafiki zangu wanaopenda kusoma vitabu pia. Kitabu changu bora cha mwaka kilikuwa Ujamaa, Ralph Ibbot. Napendekeza kila Mtanzania anayethamini historia ya nchi yetu miaka ya mwanzo ya Uhuru asome kitabu hiki.
Karibu kuona orodha ya Vitabu nilivyosoma mwaka 2015;
- The Alchemist – Paulo Coelho
- Deng Xiaoping: The Man who Made Modern China – Michael Dillon
- Ujamaa: The hidden story of Tanzania’s socialist villages – Ralph Ibbot
- Race, Revolution, and the Struggle for Human Rights in Zanzibar: The Memoirs of Ali Sultan Issa and Seif Sharif Hamad – G. Thomas Burgess
- Home and Exile – Chinua Achebe
- My Watch – Olesegun Obasanjo
- How Much Land Does A Man Need? – Leo Tolstoy
- Facing Mount Kenya – Jomo Kenyatta
- The Tipping Point – Malcolm Gladwell
- Chinua Achebe: Tributes and Reflections – Ed. Nana Ayebia Clarke & James Currey
- A Man of The People – Chinua Achebe
- Believer: My 40 Years in Politics – David Axelrod
- Politics – David Runciman
- The Man from Beijing – Henning Mankell
- The Establishment – Owen Jones
- 50 Years of Development Partnership – The World Bank
- Adultery – Paulo Coelho
- The Zahir – Paulo Coelho
- Growing Up With Tanzania – Karim Hirji
- The Governance of China – Xi Jinping
- The Last Banana – Shelby Tucker
- Act of Treason – Vince Flynn
- In the Footsteps of the Prophet – Tariq Ramadhan
Baadhi ya kazi za Zitto Bungeni
Baadhi ya kazi za Zitto Bungeni
Kwa uzito na mahala unapofanyika mkutano huu, naomba niwaletee kwa muhtasari kabisa baadhi ya kazi ambazo Ndugu Zitto Kabwe amezifanya katika kusukuma mbele guruduma la maendeleo katika nchi yetu.
- MABADILIKO SEKTA YA MADINI
Zitto alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mbunge mwaka 2005 akiwakilisha Jimbo la Kigoma Kaskazini ambalo halina mgodi hata mmoja wa madini ukiachana na wachimbaji wadogo wa udongo wa Pemba ambao una soko kubwa hapa Kariakoo jijini Dar es Salaam. Hata hivyo ajenda inayomtambulisha Zitto Kabwe kwa Taifa ni ajenda ya mabadiliko makubwa aliyoanzisha katika sekta ya Madini nyakati ambayo hakuna mwanasiasa aliyethubutu kukosoa sera za uwekezaji kwa namna aliyofanya. Baada ya kudokezwa kuwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Bwana Nazir Karamagi amesaini mkataba mpya wa Madini akiwa hotelini nchini Uingereza, Zitto alimtaka Waziri kujieleza ndani ya Bunge kuhusu mkataba huo na masharti yake ya kikodi. Waziri huyo aliposhindwa Zitto aliwasilisha Hoja Binafsi Bungeni (akiwa mbunge wa kwanza kufanya hivyo katika Bunge la Tisa na la Nane kwa pamoja). Hoja ya Buzwagi ilisababisha Zitto kusimamishwa ubunge kwa miezi 4. Hata hivyo mnamo Septemba 10, 2007 alitangaza Azimio la Songea lililomshinikiza Rais Jakaya Kikwete kuunda Kamati ya Bomani ili kupitia mikataba yote ya Madini nchini.
Kutokana na kazi yake hiyo leo Tanzania ina Sera mpya ya Madini na Sheria mpya ya Madini ambayo imeboresha nafasi ya Tanzania kufaidika na Madini, imeruhusu kisheria Serikali kuwa na hisa kwenye migodi ( na hivi tunavyoongea, kwa mfano, sasa Serikali inamiliki 50% ya Mgodi wa TanzaniteOne). Makampuni ya Madini ambayo yalikuwa yanatangaza hasara kila mwaka leo yanalipa kodi ya Mapato na Halmashauri zenye migodi zinalipwa ushuru wa huduma wa mabilioni ya fedha. Huyu ndiyo Kiongozi wetu wa ACT Wazalendo. Hawa ndio Viongozi Taifa hili linawataka. Viongozi wanaotenda na kutoa majawabu ya changamoto za nchi. Sio Viongozi wanaolaumu tu eti wakisubiri kushika dola ndio watende. Nani anayebisha rekodi hii?
- KUZUIA UBINAFSISHAJI WA SHIRIKA LA BIMA LA TAIFA (NIC)
Zitto Kabwe alikuwa Waziri Kivuli wa Mipango na Uchumi mwaka 2006 wakati Shirika la Bima la Taifa likiwa kwenye mchakato wa Ubinafsishaji. Wafanyakazi wa TUICO Tawi la Bima walimfuata wakielezea kwa ushahidi namna mali za Shirika zilivyopangwa kuuzwa na wajanja wachache kutaka kujiuzia Shirika na Mali zake hasa jengo la kitega uchumi kwa bei ya kutupwa. Zitto aliwakilisha hoja hiyo kwenye Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi chini ya Mwenyekiti wake Ndugu Abdallah Kigoda na kuishawishi Kamati kukataa ubinafsishaji wa NIC na badala yake kuunda kikosi kazi cha kurekebisha Shirika na liendelee kuwa Mali ya Umma.
Mwezi Novemba Mwaka 2006 Baraza la Mawaziri lilikubaliana na hoja za Zitto alizotoa kwenye Kamati ya Bunge na ndani ya Bunge na kuamua kuliondoa Shirika kwenye mchakato wa ubinafsishaji na leo hii Shirika limebaki kuwa la Umma na limeanza kurudi kwenye hali yake. Aliendelea kulisaidia Shirika la Bima kwa kuagiza (akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali ) kuwa Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma yaweke Bima kupitia Shirika la Bima la Taifa na agizo hilo kutekelezwa na Mashirika mengi ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania.
Sio Bima tu, Zitto akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma aliagiza kuondolewa katika orodha ya ubinafsishaji Shirika la STAMICO ili liweze kushiriki kikamilifu katika sekta ya Madini na liliondolewa. Huo ndio Ujamaa wa kidemokrasia ambao Chama chetu cha ACT-Wazalendo kinautangaza, na huyo ndio Kiongozi wetu ambaye ana uzalendo wa dhati kwa mali za Watanzania. Nani anayebisha rekodi hii?
- SHERIA YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA
Mwaka 2008/2009 Zitto Kabwe aliweka rekodi nyingine ya kuwa Mbunge wa kwanza kuzungumzia mabadiliko ya sheria ya viongozi wa umma ili kuipa meno secretariat ya maadili ya viongozi na kutengenisha biashara na siasa. Alipeleka Bungeni Muswada Binafsi wa Sheria ili kufanya mabadiliko makubwa ya Sheria Maadili. Hata hivyo muswada ule ulizuiwa na Serikali kuingia Bungeni licha ya kukamilisha kila hatua iliyopaswa.
Leo hii Chama chetu kinazungumzia kurejesha Miiko ya Viongozi kuna watu wanadhani Zitto kaanza haya hivi sasa, la hasha. Huu ni mwendelezo wa yale aliyokuwa anaamini miaka kadhaa iliyopita na kwa kuwa yeye anapenda kutembea anayoyasema alitushawishi wenzake kufanya Miiko ya Viongozi kuwa sehemu ya Katiba ya Chama chetu. Yeye ni Kiongozi wa kwanza wa kisiasa kuweka hadharani Mali na Madeni yake hapa nchini. ACT Wazalendo ni chama pekee cha siasa hapa nchini ambacho Viongozi wake wanatakiwa kikatiba kutangaza Mali zao, Madeni yao na Maslahi yao ya kibishara. Nani anabisha rekodi hii?
- UKAGUZI WA MAHESABU WA VYAMA VYA SIASA
Katika kuhakikisha kuwa kila senti ya fedha ya umma inakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali, Ndugu Zitto Kabwe aliwasilisha Bungeni mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa, Sheria namba 5 ya Mwaka 1992 na kuwezesha CAG kukagua fedha za vyama ambazo zinatoka Serikalini kama ruzuku. Sheria ya Vyama vya siasa inataka kila Mwaka Serikali kutenga kiwango kisichozidi asilimia mbili (2%) ya Bajeti ya Serikali kama ruzuku kwa vyama vya siasa. Vyama hupewa wastani wa Shilingi bilioni 20 kila mwaka na kugawana miongoni mwao lakini fedha hizi zilikuwa hazikaguliwi kinyume na Sheria za Fedha.
Baada ya Sheria hiyo kupitishwa na Bunge mwaka 2009, Zitto alisimama kidete kuhakikisha inatekelezwa jambo ambalo lilimletea uhasama mkubwa sana na viongozi wenzake katika chama chake cha zamani akiwa Naibu Katibu Mkuu. Zitto alipigana kwa kushirikiana na Wazalendo wenzake katika Kamati ya Bunge ya PAC na kufanikiwa na hivi sasa vyama vyote vinakaguliwa na kuweka rekodi nyingine katika nchi nyingi za Afrika. Kwa kazi hii iliyotukuka Zitto Kabwe amedhibiti fedha za umma kwa vyama vya siasa na hivi sasa taarifa za mahesabu ya vyama ipo wazi, na tumeona vyama vyote vikiwa na hati chafu, vikiwemo vyama vya upinzani vya zamani. Ni wajibu wa wanachama wa vyama hivyo kuwawajibisha viongozi wao wanaogeuza fedha za ruzuku kuwa ni fedha zao binafsi. Nani anabishia rekodi hiyo ya Kiongozi wetu?
- KUFUFUA ZAO LA MKONGE
Mwaka 2012 Zitto Kabwe aliweka rekodi nyingine tena akiwa mbunge wa kwanza katika Bunge la 10 kuwasilisha Hoja Binafsi. Aliwasilisha Hoja Binafsini Bungeni akitaka Serikali kufufua Kilimo cha Mkonge kwa kuwanyanganya wawekezaji wakubwa mashamba waliyobinafsishiwa na kuyaacha bila kulimwa na badala yake mashamba yale wapewe wakulima wadogo. Zitto alitaka kubadilisha mfumo wa kulima Mkonge kutoka mashamba makubwa yanayomilikiwa na tajiri mmoja na kulimwa na manamba mamia na kwenda kwenye mfumo ambao wakulima wadogo wadogo wanalima Mkonge na hivyo kushirikisha wananchi wengi zaidi kwenye uchumi wao.
Hoja hiyo ilipingwa na Wabunge kutoka Tanga lakini iliungwa mkono sana na wananchi wa mkoa huo na hivyo kumwona Zitto kama mwakilishi wao licha ya kwamba alikuwa akiwakilisha Jimbo la Kigoma Kaskazini.
Katika Chama chetu ajenda ya kumilikisha Ardhi wananchi ni ajenda kubwa na ACT Wazalendo kimekua chama cha kwanza nchini kutangaza kinagaubaga kuwa kitazuia uporaji wa Ardhi na kumilikisha wananchi ardhi yao wenyewe. Nani anabishia rekodi hiyo?
- KURASMISHA KAZI ZA SANAA NA BURUDANI NCHINI
Kwa muda mrefu sana wadau wa tasnia ya sanaa na burudani nchini walikuwa wanalalamika kazi zao kutokuwa rasmi na hivyo kuibiwa na mchango wao katika uchumi kutotambuliwa. Mwaka 2012 Zitto Kabwe akiwa Waziri Kivuli wa Fedha alifanya kampeni maalumu ya kuhakikisha kuwa wasanii hawanyonywi na kazi zao kutambuliwa rasmi. Aliwasilisha Bungeni mabadiliko ya Sheria ya Ushuru bidhaa ili kutambua rasmi kazi za sanaa na burudani na kuhakikisha kuwa wasanii wanalipwa wanavyostahili katika biashara ya miito ya simu.
Sheria hiyo ilipitishwa na Bunge na Mamlaka ya Mapato Tanzania ikaanza kutoa stempu rasmi katika CDs za kazi za sanaa ili kudhibiti wazalishaji kuwanyonya wasanii. Katika Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2015 tasnia ya Sanaa na Burudani imekuwa sekta rasmi ya Uchumi na imeripotiwa kuwa sasa ina thamani ya shilingi 270 bilioni kama mchango wake katika Pato la Taifa. Hivi sasa Wasanii wanafaidika maradufu kwa kazi zao kuuzwa kama miito ya simu na wengine wanapata mamilioni ya shilingi na kuboresha maisha yao kwa jasho lao. Nani anabisha rekodi hii?
- KUDHIBITI UKWEPAJI KODI NA MISAMAHA YA KODI
Wawekezaji kutoka nje wamekuwa wakiibia nchi yetu kwa kubadilisha badilisha majina ya makampuni yao na kubadili wamiliki bila ya kulipa kodi hapa nchini. Watanzania mnakumbuka jinsi majina ya mahoteli makubwa yalivyokuwa yakibadilishwa. Kwa mfano kutoka Sheraton kwenda Moevenpick na kwenda Serena sasa. Makampuni ya Simu yalivyokuwa yakibadilishwa. Kwa mfano kutoka Mobitel kwenda Buzz kwenda Tigo.
Vile vile kutoka Celtel kwenda Zain na kwenda Airtel. Haya yamekuwa yakitokea kwenye maeneo mengi zaidi ya haya. Yote haya yalitokea bila ya Serikali kupata kodi yeyote. Kwenye mauzo ya Zain kwenda Airtel Serikali ilipoteza dola za Kimarekani 312 milioni ( zaidi ya shilingi bilioni 600 kwa bei za sasa za dola ). Kwa uchungu kwa nchi yake Zitto Kabwe aliwasilisha Bungeni muswada wa sheria wa kurekebisha sheria ya kodi ya Mapato na kuanzisha tena kodi ya ongezeko la mtaji ( Capital Gains Tax ).
Marekebisho hayo yalipitishwa na Bunge kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2012 na mwaka huo huo Tanzania ilipata mapato ya shilingi bilioni 50 kwa mauzo ya Kampuni ya BP kwenda PUMA. Mwaka 2014 Tanzania ilipata dola za kimarekani 222 milioni ( zaidi ya tshs 450 bilioni )kwa mauzo ya sehemu ya vitalu vya gesi asilia vya kampuni ya Ophir kwenda kampuni ya Pavilion ya Singapore.
Zaidi ya hapo Zitto na wazalendo wenzake katika Kamati ya PAC walitoa maagizo ya kuhakikisha kuwa Misamaha ya kodi yote inakaguliwa na ukaguzi wake kuwekwa wazi ili kudhibiti mianya ya matumizi mabaya ya misamaha hiyo. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania CAG anakagua misahamaha ya kodi na PAC iliweka wazi taarifa ya kwanza ya ukaguzi wa misamaha ya kodi. Nani anabishia rekodi hizi?
- MABILIONI YA USWISS
Mwaka 2012 mwezi Novemba Zitto Kabwe aliwasilisha Bungeni Hoja Binafsi kuhusu mabilioni ya Uswisi ikiwa na lengo la kutaka uchunguzi ufanyike kuhusu Watanzania wanaoficha fedha nje ya nchi kinyume cha sheria. Bunge lilipitisha hoja hii binafsi na kuitaka Serikali kufanya uchunguzi kuhusu Watanzania wanaotorosha fedha kwenda nje na kuchukua hatua stahiki za kisheria. Tanzania iliingia katika rekodi ya kuwa nchi ya kwanza katika nchi za Jumuiya ya SADC kupitisha Azimio la Bunge kuhusu suala la utoroshaji wa fedha. Licha ya kwamba Serikali haijatoa taarifa yake miaka miwili sasa toka Azimio la Bunge namba 9 la mwaka 2012, na baada ya danadana ya muda mrefu kutoka vyombo vinavyohusika Kiongozi wetu Zitto Kabwe ameamua leo kupasua jipu la hoja hiyo kwa kuweka wazi orodha ya kwanza ya Watanzania 99 wenye akaunti katika Benki ya HSBC ya Uswiss. Uongozi ni umakini, na sio kukurupuka na kujitafutia sifa za harakaharaka. Ilikuwa ni muhimu Ndugu Kabwe kufuata taratibu zote kabla ya kuanika majina hayo hadharani. Sasa leo baada ya kujiridhisha pasipo shaka atayaanika majina hayo hadharani na wale waliokuwa wanambeza kwamba kashindwa wanyamaze milele! Huyo ndio Zitto, mwenye uvumilivu na ujasiri usio kifani. Anatenda anayosema. Nani anabisha rekodi hii?
- KUWAJIBISHA MAWAZIRI
Katika historia ya Tanzania ni Wabunge wawili tu walioweza kutoa hoja zilizopelekea Mawaziri wengi kuondolewa madarakani kwa mpigo. Ni Zitto Kabwe na Dkt. Harrison Mwakyembe ambaye aliongoza kamati teule ya Bunge iliyochunguza Mkataba wa kampuni feki ya kufua umeme ya Richmond. Hoja hii ilipelekea Waziri Mkuu kuwajibika kwa kujiuzulu na hivyo kumlazimisha Rais wa Jamhuri ya Muungano kuunda upya Serikali kwa kuteua Waziri Mkuu mwingine.
Zitto ana rekodi ya kipekee. Kwanza mwaka 2012 baada ya Taarifa ya CAG kuonyesha madudu katika matumizi ya fedha za umma, Zitto alikusanya sahihi za wabunge 75 na kuandika hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu. Shinikizo hili lilipelekea Rais kufukuza kazi mawaziri 8 ambao Wizara zao zilitajwa kuwa na mahesabu machafu. Pili mwaka 2013 baada ya Kamati ya Mali Asili na Mazingira kutoa taarifa yake Bungeni kuhusu Operesheni Tokomeza, Zitto alisimama ndani ya Bunge na kubadilisha mjadala kwa kutaka Mawaziri wote ambao watendaji wao walitesa wananchi kuwajibika. Mawaziri 4 waliwajibika.
Tatu, mwaka 2014 katika Taarifa Maalumu ya Kamati ya PAC kuhusu uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Escrow ya Benki ya Tanzania, Zitto na wazalendo wenzake wa kamati hiyo walipelekea Mawaziri wawili maarufu kama mawaziri wa Escrow na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwajibika. Uwajibikaji umekuwa ni ajenda kubwa ya Kiongozi wetu na amekuwa hana aibu hata kwa watu anaowaheshimu na rafiki zake. Alitaka wawajibike huku akiwatazama usoni. Ni Viongozi wachache sana wenye ujasiri wa aina hii. Huyu ndio Kiongozi wa chama chetu cha ACT Wazalendo. Nani anabisha rekodi hii?
- KUKATAA POSHO ZA KUKAA
Mwaka 2010 chama chake cha zamani waliweka katika Ilani yao ya Uchaguzi kupinga posho kama hatua ya kubana matumizi ya Serikali. Wakakubaliana kuwa wabunge wa chama chao hawatapokea posho ya kukaa (sitting allowance). Hata hivyo, ilipokuja katika utekelezaji wenzake wote wakagwaya na Ndugu Zitto Kabwe ni mbunge pekee aliyepinga posho za vikao na kuzikataa kata kata kwa miaka mitano (5) mfululizo, ambazo ni takribani shilingi milioni 21 kila mwaka. Katika kipindi hicho cha miaka mitano Zitto alikaa kuchukua jumla ya Shilingi Milioni Mia Moja na Tano (105,000,000)!! Kukataa pesa yote hii kwa sababu ya ‘principle’ tu ni jambo nadra sana kutokea katika mazingira yetu. Zitto anatembea maneno yake. Zitto anatenda anayonena. Sasa kwa yote hata kwa nini wasimchukie wenye roho zao za kwa nini?
Ndugu Wananchi,
Huyu ndio Kiongozi wa Chama chetu. Tunachoomba Watanzania mumhukumu Zitto kwa rekodi zake na si kwa propaganda za mahasimu wake.
Tamko la Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo ndg. Zitto Kabwe kuhusu Ripoti ya CAG mwaka 2013/2014
Tamko la Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo ndg. Zitto Kabwe kuhusu Ripoti ya CAG mwaka 2013/2014
1) Taarifa nyingine ya CAG imetoka, kwa mujibu wa Katiba ya JMT na kwa mujibu wa sheria za nchi. Taarifa hii imechelewa kutolewa kulingana na mabadiliko ya Ratiba za Bunge ambapo hapo awali taarifa ilikuwa ikitoka mwezi Aprili na kuwezesha kuchangia katika mchakato wa Bajeti ya nchi. Taarifa ya mwaka huu na ile ya mwaka Jana imetoka wakati wa Bunge la Bajeti na hivyo Bajeti ya Serikali haijazingatia hoja za ukaguzi ili kuboresha mfumo wa matumizi ya fedha za umma. Ni vema utaratibu wa zamani wa ripoti kutolewa mwezi Aprili urejewe ili wabunge waweze kutumia ripoti hizo wakati wa kamati katika kujadili makadirio ya Bajeti za Wizara mbalimbali.
2) Taarifa kama miaka iliyopita bado sio nzuri. Mapato mengi ya Serikali bado yanapotea. Uk. 53 wa Taarifa unaonyesha kuwa mizigo inayoingizwa nchini kupita kwenda nchi jirani zinazotumia bandari zetu hubakia nchini na kuingizwa sokoni hivyo kukwepa kodi. Mwaka 2013/2014 mizigo ya transit iliyobaki nchini kiudanganyifu ilikuwa zaidi ya bidhaa 6000 kwa mujibu wa Taarifa ya CAG. Hivyo kodi ya tshs 836 bilioni haikulipwa kwa mizigo hiyo sawa sawa na 10% ya makusanyo yote ya kodi za ndani. Tshs 836 bilioni ilipotea mwaka 2013/14 peke yake. Wakati hili linatokea Serikali ipo ukata mkubwa na kushindwa kuendesha miradi yake mbalimbali. Fedha iliyokwepwa idara ya forodha peke yake inalipa Madeni yote ya wakandarasi wa barabara wanaoidai TANROADS na riba kulimbikizwa kila mwaka. Fedha hii ingelipa Madeni yote ya mfuko wa PSPF wanayoidai Serikali. Fedha hizi zingeweza kulipia miradi 2 mikubwa nchini ya BVR na vitambulisho vya Taifa ambayo inasuasua kutokana na ukata.
Natoa wito kwa CAG kwanza kuweka wazi orodha ya bidhaa hizo zilizobakia nchini na kuingizwa nchini bila kulipa kodi. Vile vile CAG aweke wazi wafanyabiashara wote walioagiza bidhaa hizi na vyombo vya kiuchunguzi vichukue hatua za kuwashtaki wafanya biashara hawa mara moja.
Natoa wito kwa Kamati ya Bunge ya PAC kuwaita mara moja maafisa wa TRA kujieleza mbele ya kamati kuhusu suala hili na kuandaa taarifa maalumu bungeni ili kuanika uoza huu unaopoteza mapato mengi sana ya Serikali.
3) CAG kaonyesha kuwa kuna ubadhirifu mkubwa sana kitengo cha maafa cha ofisi ya Waziri Mkuu ambapo tshs 163 billioni za chakula cha maafa hazikukusanywa katika kipindi cha miaka 5 iliyopita. Huu ni kama mrija wenye wastani wa tshs 32 bilioni kuchotwa kwa kisingizio cha chakula cha maafa kwa wananchi. Kwa malezo ya CAG ni kwamba Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wamekula fedha za chakula cha misaada. Maana hakuna uthibitisho wa kuwa mahindi yaliyogawanywa na taarifa kutolewa na Wakala wa Akiba ya Chakula (NFRA). Kitengo cha maafa ofisi ya PM kimekuwa mrija wa wizi wa fedha za umma, wizi ambao umekuwa ukifanyika bila ya kugunduliwa kwa miaka 5 sasa. ACT Wazalendo inaisihi Kamati ya Bunge ya PAC kufanya uchunguzi maalumu kwenye kashfa hii ya tshs 163 bilioni katika Ofisi ya Waziri Mkuu na Wakala wa Hifadhi ya Chakula ( NFRA).
4) ACT Wazalendo inalitaka Bunge kuchukua stahiki dhidi ya Wizara ya Ujenzi kufuatia ripoti ya CAG kuonyesha kuwa Wizara ilidanganya Bunge katika kupitisha Bajeti ya tshs 252 bilioni ambapo kati yake tshs 87 bilioni ziliibiwa au matumizi yake kutoeleweka.
5) ACT Wazalendo inampongeza CAG kwa kuendelea na zoezi la kisheria la kukagua mahesabu ya vyama vya siasa. Hii inaweka misingi ya uwajibikaji kuanzia kwenye vyama vya siasa, taasisi muhimu sana katika ujenzi wa demokrasia. Vyama vya siasa vichukulie ripoti ya CAG kama changamoto ya kutoa kwanza kibanzi kwenye macho yao ili kuwa na ‘ moral standing’ ya kupambana dhidi ya ubadhirifu wa fedha za umma nchini.
Zitto Kabwe
Kiongozi wa Chama ACT Wazalendo
Maelezo ya Gavana Prof Benno Ndulu Kuhusu Kushuka kwa Thamani ya Shilingi ya Tanzania kwa Kamati ya Fedha Uchumi na Biashara
Maelezo ya Gavana Prof Benno Ndulu Kuhusu Kushuka kwa Thamani ya Shilingi ya Tanzania kwa Kamati ya Fedha Uchumi na Biashara
Yaliyojificha kuporomoka kwa shilingi dhidi ya Dola ya Marekani Shilingi inahujumiwa na Mabenki?
Yaliyojificha kuporomoka kwa shilingi dhidi ya Dola ya Marekani
Shilingi inahujumiwa na Mabenki? – Zitto Kabwe[1]
Katika ukurasa wangu wa facebook mnamo tarehe 25 Aprili 2015 niliandika kuhusu sababu za shilingi kuporomoka thamani na majawabu ya namna ya kurejesha thamani halisi ya sarafu yetu. Nilieleza “Shilingi kuporomoka dhidi ya dola na kuvuka 1$/2000TS kunasababishwa na sababu kadhaa 1) Woga wa uchaguzi na hivyo Dola nyingi kutoingia nchini (FDI etc) kusikilizia Serikali ijayo inaundwaje 2) Woga wa uchaguzi na hivyo matajiri kununua dola kwa kasi (too many Tshs chasing too few $) ili kuzificha (hoard) nje 3) kutouza mazao nje na kuagiza bidhaa nyingi kutoka nje ( current account deficit) 4) Benki Kuu kutoachia $ nyingi kwenye soko kutokana na akiba ya fedha za kigeni kupungua 5) Kuongezeka kwa huduma ya Deni la Taifa ambapo malipo ni kwa fedha za kigeni kwa madeni yaliyo wiva.
Niliendelea kushauri majawabu “Suluhisho 1) Benki Kuu kuachia $ za kutosha kwenye soko katika muda mfupi na wa kati (Mwezi Februari BoT ilifanya hivi na kuongeza $64 milioni kwneye soko bila mafanikio[2] 2) Kuongeza mauzo nje hasa ukizingatia kwa sasa ‘our exports becomes cheaper vis a vis foreign exchange) 3) Malipo ya kodi ya Ongezeko la Mtaji kutoka BG (Shell transaction ) na Ophir (Pavilion transaction), malipo haya kwa fedha za kigeni 4) Punguza kununua vitu vya anasa kutoka nje 5) Unafuu wa huduma kwa Deni la Taifa ( Debt relief ) 6) Punguza ujazo wa fedha nchini (mop tshs out)”.
Mjadala mkali umeendelea kuhusu suala hili katika majukwaa mbali mbali. Ni dhahiri kuporomoka kwa shilingi kunaathiri sana Watanzania wa ngazi ya kati hasa wafanyabiashara wa kati wenye kununua huduma na bidhaa kutoka nje. Wenye viwanda wanaotegemea malighafi kutoka nje gharama zao za uzalishaji zimeongezeka zaidi na hivyo kuhatarisha uzalishaji mali nchini. Licha ya kwamba kuporomoka kwa shilingi kunafanya bidhaa zetu za kuuza nje kuwa rahisi, lakini huchukua muda kuzalisha bidhaa hizo na hasa kilimo kuweza kufaidika hali hiyo. Kwa hiyo ni faida kwa nchi kwa sasa kuwa na sarafu stahmilivu ( stable) iliyojengwa kwenye misingi imara ya Uchumi. Hata hivyo, inaonekana kuwa sarafu ya Tanzania inahujumiwa. Kuporomoka kwa Shilingi katika wiki za hivi karibuni sio matokeo ya nguvu za soko bali ni matokeo ya hujuma ( currency manipulations).
Mabenki makubwa ya kigeni nchini, inasemekana, katika miezi ya karibuni yamefanya currency manipulations na kupelekea dola chache kukimbizwa na shilingi nyingi na hivyo bei ya dola kupanda bei. Hii inatokana na ukweli kwamba Benki zetu kubwa tatu zinazoongoza zinaendeshwa na wageni. Inasemekana biashara hii hufanyika kati ya matawi ya Benki za kigeni hapa nchini na makao makuu yao. Kuporomoka kwa shilingi kunakotokea hivi sasa hakuendani na kuporomoka kwa miaka ya nyuma kipindi kama hiki (ambacho ki kawaida ni miezi shilingi hushuka thamani kwa sababu ya watalii kuwa wachache na mauzo ya bidhaa nje kuwa madogo sana). Wastani wa miaka 10 iliyopita inaonyesha kuwa kipindi hiki shilingi hushuka kwa kati ya 8% mpaka 13% na sio kuporomoka kwa zaidi ya 20% kulikotokea hivi sasa. Kwa mfano mwaka 2011 miezi kama hii ( Februari – Mei) Shilingi iliporomoka kutoka shs 1,380 kwa dola 1 mpaka shs 1,570 sawa na mporomoko wa 12%. Hata hivyo kuanzia mwaka huo mpaka mwaka 2014 shilingi imekuwa ikishuka thamani kwa kiwango kidogo sana. Mwaka 2013 thamani ya shilingi ilishuka kwa wastani wa asilimia 1.7 tu.
Uchambuzi huu wa thamani ya sarafu yetu unaonyesha kuwa kuna zaidi ya nguvu ya soko kunakotokana na mauzo yetu nje kuwa machache. Vile vile kupanda kwa thamani ya dola ya marekani duniani hakutoshi kuelezea mporomoko huu wa kasi wa shilingi kuanzia mwezi Disemba mwaka 2014 mpaka sasa. Tuhuma za mabenki kuwa yanahujumu shilingi (currency manipulations) zaweza kuwa na ukweli.
Vile vile, inasemekana kumekuwa na utoroshaji mkubwa wa dola kutoka nchini kwenda nje ya nchi. Utoroshaji huu unafanyika kupitia wasafiri wanaopita ukumbi wa VIP uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es Salaam. Utoroshwaji huu unatokana na hofu isiyo ya msingi kwamba uchaguzi utakuwa na vurugu. Utoroshwaji wa fedha ni kinyume sheria zetu. Sheria zetu za fedha za kigeni zinazuia mtu kubeba zaidi ya dola 10,000 za kimarekani zikiwa taslimu, kuingia nazo nchini au kutoka nazo nchini. Tafiti za haraka zinaonyesha kuwa huu umekuwa ni utaratibu wa kawaida kila mwaka wa uchaguzi tangu mfumo wa vyama vingi uanze.
Benki Kuu ya Tanzania inapaswa kuchukua hatua zifuatazo;
- Kufanya uchunguzi wa kushtukiza mara moja dhidi ya benki zote za kigeni zilizopo hapa nchini. Uchunguzi huu utazame biashara ya fedha za kigeni ya benki hizi kwa lengo la kuzuia ‘ currency manipulations’ na kuchukua hatua madhubuti dhidi ya Benki yeyote itakayokutwa imehujumu biashara ya fedha za kigeni kwa lengo la kushusha thamani ya shilingi dhidi ya dola za kimarekani.
- Jeshi la Polisi na kitengo cha kuzuia utoroshaji wa fedha ( anti money laundering unit) kufanya ukaguzi wa lazima wa watu wote wanaosafiri kwenda nje ikiwemo wanaopita sehemu ya watu mashuhuri (VIP Lounge) ili kudhibiti utoroshaji wa fedha za kigeni kwenda ughaibuni.
- Watanzania tufikirie upya nafasi ya Mabenki katika uchumi wa nchi na kufanya maamuzi magumu ya kurejesha baadhi ya Benki katika umiliki mpana zaidi wa Watanzania. Kwa malengo ya muda wa kati, Benki kubwa 3 nchini ilazimu kuwa na umiliki unaozidi 51% wa Watanzania. Bila ya kushika mabenki nchi itachezewa sana.
- Suluhiho la kudumu la sarafu stahmilivu ni kuongeza uzalishaji wa bidhaa za kuuza nje ya nchi na kupunguza manunuzi ya bidhaa kutoka nje. Urari wa Biashara wa Tanzania umepanuka kutoka $1bn mwaka 2004 mpaka $6bn mwaka 2013 (BOT 2013) kutokana manunuzi yetu nje kukua kwa kasi kutoka $2.5bn mpaka $11bn wakati mauzo yetu nje yakikua kwa kasi ndogo kutoka $1.4bn mpaka $5bn katika kipindi hicho. Isingekuwa uimara katika urari katika uwekezaji na uhamisho wa mitaji, Tanzania ingekuwa na sarafu yenye thamani sawa na takataka. Serikali ihimize uzalishaji mali mashambani na viwandani na kuuza nje biadhaa zilizoongezwa thamani. Zama za kutegemea dhahabu zimekwisha na sio endelevu. Turudi kwenye misingi: Bidhaa za Kilimo na Viwanda.
Tutaendelea kufuatilia thamani ya shilingi mpaka ifikapo mwezi Julai ambapo ndipo kipindi kigumu kwa shilingi huwa kihistoria. Hatua zilizoainishwa zisipotazamwa na mamlaka tajwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani yaweza kufikia tshs 3000!
[1] Zitto Kabwe ni Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo. Amepata kuwa Waziri Kivuli wa Fedha na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya PAC
[2] Benki Kuu kuingiza $ kwenye soko kuna hatarisha kupunguza Akiba ya fedha za Kigeni. Kutokana na ujinai unaoendelea kwenye soko la fedha za kigeni nchini, BoT kuendelea kumwaga fedha za kigeni inaweza kuwa ni mkakati wa kudumu wa wanaofaidika na ‘currency manipulations’. Kushinikiza Benki Kuu kuendelea kubomoa foreign reserve ni kutokuona mbali na kujaribu kujiridhisha kwa kutibu dalili za ugonjwa badala ya ugonjwa wenyewe.
TAMKO LA RASILIMALI NA MADENI-ZITTO ZUBERI KABWE(KIONGOZI WA CHAMA ACT-WAZALENDO) @ACTWazalendo
TAMKO LA RASILIMALI NA MADENI LA NDUGU ZITTO ZUBERI KABWE (KIONGOZI WA CHAMA ACT-WAZALENDO) KWA MUJIBU WA KATIBA YA ACT-WAZALENDO
WEALTH DECLARATION FORMS FOR ZITTO ZUBERI KABWE-PARTY LEADER ACT-WAZALENDO
Katiba ya ACT-Wazalendo Kama Ilivyopitishwa Na Mkutano Mkuu 29Machi15
Alliance for Change and Transparency
(ACT-Wazalendo)
Chama cha Wazalendo
KATIBA
TOLEO LA 2015
Turejeshe nchi yetu Tanzania!-Hotuba ya Mzalendo Zitto Kabwe #ACTWazalendo @ACTWazalendo
Turejeshe nchi yetu Tanzania!
Watanzania wenzangu, wageni waalikwa
Nawashukuru kwa kuwa pamoja nasi siku hii ya kihistoria.
Karibu Miaka 54 iliyopita tulipopata uhuru, Muasisi na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa kijana mwenye umri wa miaka 39, mwenye matumaini makubwa na taifa jipya na alikuwa na ndoto! Ndoto yake ilikuwa imejikita katika kuhakikisha taifa letu litakuwa taifa lisilo na umaskini, dhiki, ufukara; taifa lisilo na tofauti kubwa kati ya maskini na tajiri; taifa lenye usawa, haki na maendeleo, ambapo watoto wote wanasoma shule bila kujali kipato cha mzazi; taifa ambalo wananchi wake wanamiliki uchumi wao.
Ndoto hii aliiamini kwa dhati na wananchi wote walikubali na kuota nae ndoto hii. Alilisimamia kwa maneno na vitendo kupitia Azimio la Arusha, sera zake na uongozi wake wa kizalendo. Mpaka mauti ilipomkuta aliamini katika misingi hii aliyojitahidi kuturithisha. Lakini miaka 16 baada ya kifo chake, ndoto yake imeyeyuka!
Tulilonalo ni jinamizi alilolihofu Nyerere.
Leo hii:
Watanzania wachache wameondoka katika unyonge na dhiki.
Watanzania wengi bado wapo katika hali ya dhiki.
Watanzania wachache wameshikilia uchumi: Warasimu, Wanasiasa na Matajiri wachache wenye mitaji.
Watanzania wengi bado kama Mwalimu Nyerere alivyosema “wananyonywa kiasi cha kutosha; wanapuuzwa kiasi cha kutosha”.
Ndoto ya Mwalimu Nyerere bado haijawafikia wananchi.
Sasa ndio wakati wa mabadiliko ya kimapinduzi.
Sasa ndio wakati wa kujenga Uchumi shirikishi ambao utaruhusu kila mwananchi kupata fursa ya kuboresha maisha yake;
Sasa ndio wakati dola imara ipate nafasi ya kusimamia uchumi;
Sasa ndio wakati kwa wananchi kuwa na uhuru wa kweli wa mawazo, fikra, kushirikiana, kuabudu;
Sasa ndio wakati wananchi kuwa na nguvu ya kuwawajibisha viongozi wao;
Sasa ndio wakati wetu watanzania kujirithisha upya nchi yetu!
Huu ndio wakati wa kubomoa uchumi wa kinyonyaji na kifisadi na kujenga uchumi wa wananchi. Haya ndio mabadiliko ya kimapinduzi tunayoyataka. Hii ndiyo ilikuwa ndoto ya Mwalimu Nyerere, na muda umefika wananchi turejeshe nchi mikononi mwetu!
Haya yamekuwa mawazo yangu kwa muda mrefu kwa sababu mimi ni zao la ndoto ya Mwalimu Nyerere. Nililelewa na mama yangu mzazi pekee mwenye ulemavu; nimeanza kusoma shule ya msingi nikiwa naenda peku. Lakini kutokana na kufaulu mitihani vizuri, sikuhitaji kuwa tajiri kusoma mpaka chuo kikuu. Leo hii kutokana na elimu bora niliyoipata bure, nimesafiri na kufika katika nchi zaidi ya 70; nikiwa kama kiongozi nimekutana na kubadilishana mawazo na watu muhimu duniani kama vile wakuu wa nchi. Sio mimi peke yangu bali tupo maelfu tuliofaidika na mfumo huu. Lakini muhimu kupita yote, nimeweza kutumikia wananchi wa Kigoma na watanzania bungeni kwa miaka 10. Kama hii si ndoto iliyokuja kuwa kweli, ni nini?
Zitto Zuberi Kabwe angezaliwa mwaka 2000, angekuwa kijana ambaye hajakamilisha elimu yake, haelewi lugha za kigeni kama kiingereza, hana ujuzi wowote na kama Mungu angeendelea kuninyima kipaji cha kuimba kama sasa ningeshindwa hata kutoka kama Diamond na Mwana FA! Mwalimu Nyerere asingepigania ndoto yake miaka ya 60 na 70, ningekuwa kama mamilioni ya vijana leo ambao wanahangaika kutafuta ajira na kipato bila ujuzi na elimu.
Na ndiyo maana siku ya leo ni muhimu kwangu. Nina furaha na heshima kubwa kuwa katika familia yangu mpya ya kisiasa. Familia inayoaamini katika itikadi, misingi na tunu ninazoziamini.
Nimezungumza mara kadhaa kuhusu sababu za kujiunga na chama hiki. Chama cha Wazalendo ACT- Tanzania inaongozwa na misingi ya Uzalendo, Demokarsia, Uhuru wa fikra na matendo, Utu, Usawa, Uadilifu, Uwazi, Uwajibikaji na Umoja katika kila kitu. Chama hiki ni cha wananchi si wenyenchi wa sasa waliojimilikisha taifa. Chama hiki ni cha watanzania wote bila kujali kabila, dini, jinsia, rangi ya ngozi au hali ya ulemavu!
Tunapojadili wananchi kujimilikisha upya nchi yetu ni kupitia usimamizi wa sheria utakaohakikisha kuwa kuna uwazi na uwajibikaji wa viongozi. Uwazi tunaouamini ni ule utakaohakikisha kila mwananchi anapata taarifa za fedha zao, mikataba ambayo Serikali inaingia kwa niaba yao na taarifa za maslahi, mali na madeni ya viongozi wao. Tunataka uwazi katika uendeshaji wa Serikali na sisi tutaanza na uwazi katika uendeshaji wa chama chetu. Tunataka wananchi sio tu wajione kuwa sehemu ya uendeshaji wa nchi yao, bali pia wawe sehemu ya uendeshaji wa nchi yao.
Tunataka uwazi utakaoruhusu uhuru wa mawazo na uhuru wa wananchi kujieleza bila kuhofu Serikali kuwachukulia hatua kwa kutoa mawazo yao. Ndio maana ACT Wazalendo tunapinga vikali miswada ya sheria ambayo Serikali ya CCM imeiwasilisha bungeni katika mkutano unaoendelea. Miswada hii kama vile muswada wa Haki ya kupata taarifa, vyombo vya habari na ule wa makosa ya mtandao, inalenga kuminya na kunyima haki za wananchi kuwasiliana kwa uhuru na kutoa mawazo yao kama inavyoainishwa katika katiba ya nchi.
Tunapojadili wananchi kurejesha taifa mikononi mwao tunazungumzia uwajibikaji. Ripoti ya Tume ya Marekebisho ya Katiba ilieleza moja ya sababu kubwa ya kushamiri rushwa, ufisadi na ubadhirifu nchini ni nanukuu ‘kukosekana kwa mfumo madhubuti wa uwajibikaji’ nchini kwetu. Sababu kubwa ya ACT Wazalendo kupinga Katiba inayopendekezwa ni kwamba Katiba hiyo imechakachua nia hii ya kuweka mfumo wa uwajibikaji. Ndio maana tunawaambia wananchi waikatae Katiba hiyo kwa nguvu zao zote! Katiba inayoepndekezwa inastahili kadi nyekundu, tuikatae na kura ya hapana!
Iwapo wananchi hawawezi kuwawajibisha viongozi kwa matendo yao hatuwezi kujenga jamii ya watu wanaoheshimiana na kutii sheria za nchi.
Kila Mtanzania bila ya kujali cheo chake ni lazima awe chini ya sheria. Uwajibikaji ni lazima uanze na viongozi. Mnajua kuwa katika maisha yangu ya kisiasa hili ndio limekuwa jukwaa langu. Kwa bahati mbaya tunaishi katika kipindi ambacho wanasiasa wengi wamekuwa wakikumbwa na kashfa mbalimbali za kifisadi na matokeo yake inajengwa picha kuwa kila mwanasiasa ni fisadi. Mfumo wa Uwajibikaji wenye uwazi utasaidia wananchi kutofautisha wanasiasa wanaosimamia maslahi ya umma na wale wanaosimamia maslahi yao binafsi na vyama vyao vya siasa.
Mwungwana ni vitendo; nimewajibisha watu kwenye Buzwagi na mikataba ya madini, kwenye matumizi mabaya ya fedha za umma na juzi juzi kwenye akaunti ya Tegeta Escrow. Lakini matukio haya machache hayatoshi kujenga mfumo madhubuti wa Uwajibikaji. Ni lazima kufanya mapinduzi ya mfumo mzima wa uchumi wa nchi yetu na kujenga mfumo mpya unaohudumia kila Mtanzania na ambao kila Mtanzania anajivunia kuujenga. Hatuwezi kuwa Taifa linaloshikiliwa na vikundi vya wafanyabishara wachache na wanasiasa wanaofadhiliwa na wafanyabishara hao.
ACT Wazalendo inataka kujenga Taifa ambalo viongozi wake wanawajibika kwa wananchi. Hii ndio fikra tunayotaka kurejesha. Hizi ndizo siasa zilizoasisi Taifa letu. Hatuna budi, ni lazima kurudi kwenye misingi na kuanza upya!
Kwa sababu ACT Wazalendo imejikita kwenye misingi hii, tumelihuisha Azimio la Arusha.
Sio tu tumeweka miiko ya uongozi lakini pia tumetunga kanuni za kutekeleza miiko hiyo na kuifanya kuwa sehemu ya Katiba ya chama chetu. Hitaji moja kubwa la Kanuni zetu za Maadili ni kutaka kila Kiongozi wa ACT Wazalendo kuweka hadharani Maslahi yake, Mali na Madeni yake.
Katika chama hiki huo ndio utamaduni wa kisiasa tunaotaka kuujenga. Kutenda tunachohubiri hata kabla ya kuingia kwenye uongozi wa Dola.
Chama cha ACT Wazalendo kimeelekeza kikanuni kwamba kila Kiongozi wa chama lazima atangaze Mali zake na Madeni yake. Kila Kiongozi lazima aweke wazi maslahi yake ya kibiashara na mengineyo wazi ili kila anapotenda au kusema jambo wananchi wajue maslahi aliyonayo au la katika suala husika. Viongozi wote wa kitaifa wa ACT Wazalendo wamefanya hivyo na tutaweka saini zetu mbele yenu kama mashahidi. Naomba Mwanasheria wetu aje hapa tutekeleze matakwa haya ya kikanuni.
Fomu hizi zitakuwa kwenye tovuti ya chama ndani ya muda mfupi ujao ili kila mtanzaina aone. Kila Kiongozi wa Chama ambaye Miiko ya Uongozi inamtaja anapaswa kuwa amejaza fomu hizi na kuziwasilisha kwa Katibu wa Kamati ya Uadilifu katika ifikapo tarehe 30 Juni 2015. Tunapopinga Viongozi wa Umma kufanya Biashara na Serikali na hivyo kuwa na mgongano wa kimaslahi na kushamiri kwa ufisadi, hivyo hivyo tunapinga Viongozi wa Chama chetu kufanya Biashara na Chama. Ni Marufuku Serikali kugeuzwa kuwa genge la watu wachache wanaopora rasilimali za Umma. Uadilifu tunaoutaka Serikalini ni lazima uanzie kwetu tunaohubiri.
Tutafanya haya kwa kubadilisha siasa zetu kuelekea kwenye masuala yanayowahusu wananchi; Wakulima, Wafanyakazi, Wafanyabiashara ndogo ndogo, Vijana, Wanawake na Wazee wetu.
Tunataka kurejesha nchi yetu Tanzania kwa kujenga uchumi wa wote. Tunaporejea kwenye Azimio, hatusemi tunakwenda kutaifisha kila kitu na Serikali kuendesha shughuli zote za kiuchumi. Tunaheshimu na kuthamini sekta binafsi na mchango wake katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo. Tunamaanisha kuwa ni lazima Dola isimamie uchumi. Sio kazi ya Serikali kufanya biashara. Lakini tunamaanisha kuwa ni lazima kurekebisha baadhi ya makosa yaliyofanyika kwenye ubinafsishaji na hususan ubinafsishaji holela uliofanyika kwenye sekta ya Kilimo na kupora ardhi ya wananchi wetu na kuwageuza kuwa manamba kwenye ardhi yao wenyewe.
Tunataka kutomokeza ukwepaji kodi.
Tanzania inapoteza 15% ya makusanyo katika forodha kwa sababu ya ukwepaji wa kodi. Hii ni sawa na tshs 490 bilioni kwa mwaka, fedha ambazo zingeweza kuchangia wananchi milioni 4 kwenye hifadhi ya Jamii. Tanzania inapoteza takribani tshs 2 trilioni kila mwaka kwenye misamaha ya kodi. Hii ni fedha ambayo ingeweza kujenga reli mpya ya kati ya kisasa kutoka Dar mpaka Mwanza na Kigoma ndani ya miaka mitatu. Ili kuondoa upotevu huu ni lazima kupanua wigo wa kodi, kurahisisha kodi, kupunguza baadhi ya kodi kama ( PAYE) na kutumia teknolojia kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi.
Vile vile ni muhimu kuimarisha mfumo wetu wa kodi za kimataifa ili kuzuia utoroshaji mkubwa unaofanywa na makampuni ya kigeni. Ili tujitegemee kama Taifa ni lazima kukusanya mapato ya ndani ya kutosha. Ili kukusanya mapato ya ndani ya kutosha ni lazima kuweka mazingira mazuri ya biashara hasa kwa wafanyabishara ndogo ndogo kwani ndio wazalishaji wakubwa wa ajira.
Kwa Vijana, Taifa hili ni lenu. Asilimia 75 ya Watanzania wapo chini ya miaka 40. Asilimia 65 ya wapiga kura wapo chini ya miaka 40. Nusu ya Watanzania ni watoto chini ya miaka 18. Kurejesha nchi kwenye misingi ni wajibu wa kujenga maisha yenu. Haikubaliki Vijana kuwa mzigo kwa wazazi kwa sababu tu uchumi hauzalishi ajira za kutosha. ACT Wazalendo ndio jukwaa lenu la kufanya mapinduzi ya mfumo wa uchumi ili kujenga uchumi shirikishi unaozalisha ajira. ACT Wazalendo inataka kuwajengea mfumo wa hifadhi ya jamii ambapo mtakapokuwa Wazee msipate tabu za pensheni na matibabu wanazopata Wazee wetu hivi sasa. Shiriki kujijengea Taifa litakalohakikisha maisha yako ya sasa nay a baadae na ya kizazi kijacho.
Kwa Wanawake, Ninyi ndio mhimili wa Taifa hili, wazalishaji wakuu na walezi wa Taifa letu. Kurejesha nchi kwenye misingi ni wajibu wa kutambua nafasi yenu stahili katika jamii. Nikiwa nimelelewa na Mwanamke mwenye ulemavu na mpiganaji wa kweli wa haki za wananchi walio pembezoni, sina namna kutoa heshima yangu zaidi ya kuongoza chama chenye misingi thabiti ya kumkomboa mwanamke. Msitarajie watu wengine kuwapigania mnapaswa kuchukua hatua kupitia jukwaa hili la ACT Wazalendo.
Kwa wafanyabishara, ninyi ndio mnachochea shughuli za Uchumi na kuzalisha ajira. Kuanzia kwa wamiliki wa maduka madogo mitaani mpaka kwa mameneja wa maduka makubwa; kutoka kwa wachuuzi na mama lishe mpaka kwa wamiliki wa viwanda na biashara; mnaamka kila siku asubuhi kujenga Taifa hili kwa kuzalisha mali na huduma. Baadhi yenu ambao mnamiliki viwanda, mashirika makubwa na kutoa ajira kwa maelfu ya wananchi, mmeanza mkiwa mnashona viatu na sare za shule, au mkitengeneza na kuuza mkate. Mmepata utajiri wenu na mali zenu kwa juhudi na jasho lenu na kutokana na fursa za kiuchumi zilizokuwepo kipindi hicho ambacho hakikuangalia dini, kabila, uwezo wa kifedha au rangi ya ngozi. ACT Wazalendo inataka kuwawekea mazingira bora ya biashara halali lakini pia kuhakikisha mnalipa kodi zenu na kutonyonya wafanyakazi wenu. Tunataka kuwawekea mfumo rahisi wa kodi, wenye kueleweka na unaowapa motisha kuzalisha zaidi ili kuongeza ajira zaidi na kupanua Pato la Taifa. Msipotimiza wajibu wenu biashara zenu hazitashamiri. Kurudi kwenye misingi ya Taifa hili ni kurejesha maadili katika biashara zenu.
Kwa Wakulima, Wafugaji na Wavuvi, ninyi ndio mnaolilisha Taifa letu na kuleta fedha nyingi za kigeni kupitia mauzo nje. Kwa miongo mitatu sera za nchi zimewaweka pembeni na hivyo uchumi wenu kusinyaa. Viwanda vyote vya kusindika mazao yenu vimeuzwa kwa bei ya kutupwa licha ya kwamba jasho lenu ndio lilitumika kuvijenga. Miundombinu ya barabara, maji, umeme na mawasiliano haiwafikii ili muweze kupata masoko. Hamna hifadhi ya jamii wala bima ya mazao yenu. Ardhi yenu wamepewa wawekezaji na mnakodishiwa, mnapanga kwenye ardhi yenu wenyewe. Mmeachwa mkijihangaikia. Kurejesha nchi kwenye misingi kutawarudishia heshima yenu katika nchi yetu. ACT Wazalendo ndio jukwaa sahihi kwenu kuhakikisha kuwa tunajenga uchumi shirikishi ambao mtafaidika na jasho lenu. Hamna cha kupoteza isipokuwa minyororo ya kinyonyaji.
Kwa Watanzania wote mnaonisikiliza leo, katika ukumbi huu na popote mlipo kupitia vyombo vya habari, mnamo mwaka 1978 Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitangaza vita dhidi ya nduli Idi Amini na kusema;
“Tutampiga. Sababu za kumpiga tunazo, nia tunayo, uwezo wa kumpiga tunao”.
Tanzania ipo katika vita hivi sasa.
Vita dhidi ya Ufisadi,
vita dhidi ya uporaji wa rasilimali zetu,
vita dhidi ya Siasa chafu.
Vita dhidi ya Uchumi wa kinyonyaji.
Vita dhidi ya kuporomoka kwa Utaifa wetu.
Tunapaswa kufanya jambo moja tu, nalo ni kupigana vita hizi. Ni vita kwa ajili ya kurejesha ndoto tuliyoota miaka 54 iliyopita na Muasisi wetu Mwalimu Julius Nyerere. Tunataka kurejesha nchi kwa wananchi, tunataka kujimilikisha nchi yetu. Wananchi wawe WENYE nchi! Tutimize ndoto yetu ya kuona;
Tanzania yenye Dola madhubuti,
Tanzania yenye Wananchi wenye mwamko,
Tanzania yenye sekta binafsi iliyochangamka,
Tanzania yenye uchumi unaonufaisha watu wote.
Sababu tunazo, nia tunayo na uwezo tunao. Twendeni tukajenge Chama kitakachorejesha misingi ya Taifa letu.
Asanteni sana
Mzalendo Zitto Kabwe