Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Archive for the ‘Umeme Vijijini’ Category

Uchumi wa Taifa hatarini: Mfumuko wa Bei tishio kwa Serikali, Wafanyabishara na Wananchi.

with 11 comments

=PRESS RELEASE=

Uchumi wa Taifa hatarini: Mfumuko wa Bei tishio kwa Serikali, Wafanyabishara na Wananchi.

Mfumuko wa Bei umezidi kuongezeka kama taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu inavyoonesha kwamba, wakati mfumuko wa bei mwezi Julai mwaka huu (Bajeti ya mwaka wa Fedha 2011/2012 ilipokuwa inaanza) ulikuwa asilimia 13, umefikia asilimia 19.2 mwezi Novemba. Hii maana yake ni kwamba, Bajeti ya Serikali iliyopitishwa na Bunge mwezi Juni 2011, imepunguza uwezo wa kununua bidhaa na huduma kwa takribani asilimia 6. Hii ni sawa na shilingi 780 bilioni kuyeyuka katika Bajeti katika kipindi cha miezi Minne tu ya utekelezaji wa wake. Kutokana na kasi ya ukuaji wa Mfumuko wa Bei ni dhahiri kwamba, itakapofika mwisho wa mwaka wa Bajeti Serikali itakuwa imepoteza kwa kiasi kikubwa uwezo wa kununua bidhaa na huduma kwa zaidi ya robo ya Bajeti yake.

Hali ni mbaya zaidi kwa wananchi kwani Mfumuko wa Bei za vyakula umekua kwa kasi kikubwa mno. Ofisi ya Takwimu imeonesha kuwa wakati mfumuko wa Bei za vyakula ulikuwa asilimia 14.8 mwezi Julai, umefikia asilimia 24.7 mwezi Novemba 2011. Ukilinganisha na bei za vyakula mwaka 2010, mwananchi amepoteza uwezo wa kununua chakula kwa zaidi ya robo katika ya Novemba 2010 na Novemba 2011. Jumla ya vyakula ambavyo mwananchi alinunua kwa shilingi 10,000 mwaka 2010, sasa atanunua kiwango kile kile kwa shilingi 12,500. Bei za vyakula zimeongezeka kwa kiwango hiki ilhali kipato cha mwananchi aghalabu kipo pale pale. Mwathirika mkubwa ni mwananchi wa kawaida wa kijijini ambaye mapato yake ni kidogo na hivyo sehemu kubwa huyatumia kununua chakula.

Ukiangalia kwa undani utakuta mfumuko wa bei wa bidhaa kama mchele, sukari, nyama na samaki umekua maradufu. Bei ya mchele imekua kwa asilimia 50, sukari asilimia 50, nyama asilimia 30 na Samaki kwa takribani asilimia 40. Bidhaa hizi zote ni muhimu sana kwa afya ya binadaamu na hasa watoto kwa upande wa vyakula vya protini. Tusipokuwa makini na kupata majibu sahihi ya tatizo la mfumuko wa bei za vyakula, wananchi wengi na hasa watoto watapata utapiamlo na Taifa kuingia gharama kubwa katika kuwapatia huduma ya afya.

Kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula, mfumuko wa bei wa mafuta ya taa na gesi asilia unapaa kwa kasi kama moto wa nyikani. Wakati mafuta ya taa yamepanda bei kwa asilimia 71 katika ya mwezi Novemba mwaka 2010 na mwezi Novemba 2011, bei ya gesi asilia imepanda kwa asilimia 35. Madhara ya hali hii ni makubwa mno maana wananchi watakimbilia kwenye matumizi ya mkaa na kuni, hata hivyo bei za mkaa zenyewe zimepanda kwa asilimia 24. Kwa hali hii, na kutokana na ukweli kwamba wananchi wengi wa Tanzania wapo kwenye mpaka wa umasikini na daraja la kati chini, juhudi za muongo mzima za kupunguza umasikini zitafutwa ndani ya mwaka mmoja tu.

Mfumuko wa Bei unasukuma Watanzania wengi zaidi kwenye dimbwi la umasikini, unapunguza uwezo wa Serikali kutoa huduma za jamii kupitia Bajeti na hata kutimiza mipango ya miradi ya maendeleo kama miundombinu ya barabara, umeme, bomba la gesi, madaraja nk. Mkakati mahususi unatakiwa kubadili hali hii. Hatua zifuatazo zinapendekezwa ili kuuhami uchumi na kupunguza upandaji wa kasi wa gharama za maisha.

1.     Kuongeza uzalishaji wa chakula kwa kuweka mbinu za kukuza uchumi wa vijijini ni njia mojawapo endelevu ya kupunguza mfumuko wa Bei hapa nchini. Serikali sasa iache maneno matupu kuhusu sekta ya uchumi vijijini kwa kuelekeza nguvu nyingi huko. Serikali iruhusu na ivutie kwa kasi na kutoa vivutio kwa wazalishaji binafsi wa Sukari na mpunga katika mabonde makubwa. Waziri wa Kilimo na Maafisa wake watoke Ofisini na kuhimiza uzalishaji mashambani, fedha zielekezwe kujenga miundombinu ya barabara vijijini.

Vyakula vilivyolundikana mikoa ya Mbeya, Iringa na Rukwa ambapo Serikali iliahidi kununua na kutotimiza ahadi yake vinunuliwe mara moja na kusambazwa mikoa yenye shida ya chakula kama Mwanza, Mara, Kagera na mikoa ya Kaskazini. Chakula kukuta msimu mwingine katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ni kashfa kubwa kwa Serikali na inaonesha Serikali isivyokuwa makini na maisha ya wananchi.

Wakati huu ambapo tunaweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa chakula, Serikali inunue chakula cha kutosha na hasa mchele na sukari kutoka nje na kukisambaza kwenye soko ili kupunguza upungufu wa bidhaa (scarcity) katika masoko.

Mfumo uliotumika kununua Sukari tani laki moja hivi karibuni usitumike tena kwani ulizaa rushwa ya hatari na ufisadi ambao haujaripotiwa kwenye kutoa vibali. Wizara ya Kilimo iruhusu wauzaji kutoka nje walete sukari nchini moja kwa moja na kununuliwa na Bodi ya Sukari kisha kuiuza kwa wauzaji wa Jumla. Mfumo wa kutoa vibali umeonesha kutokuwa na tija na kwa kweli kunufaisha maafisa wachache wa Wizara ya Kilimo na Bodi ya Sukari.

2.     Kitengenezwe kiwanda cha kutengeneza gesi ya matumizi nyumbani (LPG extraction plant) kwa haraka ili kupunguza bei ya gesi, kuepuka kuagiza gesi kutoka nje na hivyo kuokoa fedha za kigeni na kutengeneza ajira hapa nchini. Kupanda kwa bei ya gesi asilia kunatokana na kwamba Tanzania inaagiza gesi hii yote kutoka nje ilhali malighafi ya kutengeneza gesi ipo hapa Tanzania na kwa kweli huchomwa moto (flared). Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini liingie ubia na kampuni Binafsi ili kuwekeza katika kiwanda cha kuzalisha gesi hatimaye kushusha bei na hivyo kuwezesha wananchi wengi zaidi kutumia gesi kwa matumizi ya kupikia n.k, hivyo kutunza mazingira.

3.     Ushuru wote unaokusanywa kwenye Mafuta ya Taa upelekwe Wakala wa Nishati Vijijini ili kufidia kupanda kwa bei ya mafuta ya Taa. Mfumuko wa Bei katika bidhaa ya mafuta ya taa unatokana na uamuzi wa kuwianisha bei ya mafuta ya taa na diseli ili kuondoa tatizo la uchakachuaji wa mafuta. Tatizo limeondoka (au hatulisikii tena) lakini wananchi wanaumia sana. Uamuzi sahihi wa kisera ni kupanua huduma za umeme vijijini kwa kuipa fedha zinazotokana na ushuru wa mafuta ya taa Wakala wa Umeme Vijijini. Usambazaji wa Umeme Vijijini utaongeza shughuli za kiuchumi vijijini, kukuza uchumi wa vijijini, kuongeza mapato ya wananchi kwa kuongeza thamani za mazao yao na hivyo kupunguza athari za mfumuko wa bei.

4.     Sera ya Matumizi ya Serikali iangaliwe upya kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi yasiyo ya lazima, na kuelekeza fedha nyingi zaidi katika uwekezaji umma (public investments). Matumizi Mengineyo ya Serikali yanaongeza fedha kwenye mzunguko ama kwa kulipa watu wachache stahili mbalimbali kama posho n.k au kwa kununua bidhaa na huduma bila mpango, na hivyo kusukuma bei kuwa juu kinyume na uhalisia wa soko. Tafiti za mfumuko wa Bei Tanzania zinaonyesha kwamba sera za fedha na zile za matumizi (monetary and fiscal policy) zina nafasi kubwa katika kukuza mfumuko wa bei. Hivi sasa nakisi ya Bajeti inayopelekea Serikali kukopa kwa kwa kiwango kubwa inapandisha gharama za viwanda kukopa mitaji ya muda mfupi na hivyo kuongeza gharama za uzalishaji na kasha bei za bidhaa. Wizara ya Fedha ambayo mpaka sasa imekaa kama imeishiwa namna ya kufanya, inapaswa kuamka na kutoa maelekezo mapya kwa Wizara, Idara na Wakala za Serikali kuhusu namna ya kubana matumizi na kuziba mianya yote ya kukwepa kodi.

Hitimisho

Serikali imeonesha udhaifu mkubwa sana katika kusimamia uchumi katika nusu ya kwanza ya Bajeti ya mwaka 2011/2012 ambayo pia ni Bajeti ya kwanza ya kipindi cha pili cha Serikali ya awamu wa Nne. Kuna hatari ya dhahiri kwamba ifikapo mwezi Januari 2012 tutakuwa tumerejea mfumuko wa Bei wa kiwango cha mwaka 1992 (21.9%). Tusipochukua hatua za haraka tutafikia na hata kuzidi mfumuko wa Bei kiwango cha juu kabisa ambacho kilifikiwa mwaka 1994 (33%) na hivyo viwanda kushindwa kukopa kwenye Mabenki kwa mahitaji yao ya haraka ya mitaji ya muda mfupi, wazalishaji wadogo kushindwa kulipa mikopo yao kwenye Taasisi za fedha na hivyo kufunga uzalishaji, Shirika la Umeme kushindwa kabisa kulipa gharama za mafuta ya kuendesha mitambo na kipato cha mwananchi kutomudu gharama za za kila siku. Uchumi utadorora kabisa. Taifa litakuwa hatarini.

Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania na Wizara ya Kilimo na Chakula iamke kuhami uchumi dhidi ya adui namba moja, Mfumuko wa Bei. Huu sio wakati wa kupiga porojo, viongozi wafanye kazi zao, Wananchi wajitume.

Inabidi sasa turejee kauli mbiu za miaka 50 iliyopita za Uhuru ni Kazi. Tuseme Demokrasia ni Kazi. Demokrasia sio lelemama.

Ndg. Kabwe Zuberi Zitto, Mb

Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Waziri Kivuli Fedha na Uchumi

18 Disemba 2011

Written by zittokabwe

December 18, 2011 at 12:37 PM

HOTUBA YA MBUNGE WA KIGOMA KASKAZINI NDUGU ZITTO KABWE KATIKA UZINDUZI WA JUKWAA LA VIONGOZI WA VIJIJI JIMBO LA KIGOMA KASKAZINI

with 8 comments

Kigoma, 6 Oktoba 2011

Ndugu Wenyeviti wa Vijiji vya Jimbo la Kigoma Kaskazini,

Ndugu watendaji wa Vijiji,

Viongozi wa Asasi ya Maendeleo Kigoma (KDI), Dr. Alex Kitumo – Mwenyekiti na ndugu Paul Bahemana – Mtendaji Mkuu

Afisa Miradi kutoka Taasisi ya FES Ndugu Amon Petro

Mshauri wa Mradi wa Demokrasia Vijijini, Mzee Sylvester Masinde

Wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini

Maswali na majibu

Maswali na majibu

Nachukua fursa hii kuwapongeza kwa hatua hii ya kuanzisha Jukwaa la Viongozi wa Vijiji katika Jimbo la Kigoma Kaskazini. Jukwaa ambalo litawezesha mawasiliano ya karibu miongoni mwa viongozi wa ngazi zote za Serikali Kuu (Mbunge), Halmashauri ya Wilaya (Madiwani) na ninyi Wenyeviti na Watedaji wa Vijiji.

Tulipopata wazo hili, na kwa kuzingatia kwamba katika sheria zetu za Serikali za Mitaa zinazoanzisha Mamlaka ya Serikali za Vijiji na Halmashauri za Wilaya, hakuna chombo chochote kinachokutanisha viongozi katika ngazi za vijiji, tuliona ni lazima tulitekeleze.

Katika ngazi ya Kijiji, Mwenyekiti wa Kijiji ana fursa ya kukutana na Wenyeviti wa Vitongoji katika Halmashauri ya Kijiji ambapo yeye ni Mwenyekiti wa kikao hicho. Vilevile katika ngazi ya Kata, Diwani ana fursa ya kukutana na Wenyeviti wote wa Vijiji katika Kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata ambacho yeye Diwani ni Mwenyekiti. Katika ngazi ya Jimbo, hakuna kikao chochote kwa mujibu wa Sheria ambacho kinamfanya Mbunge akutane na Viongozi wenzake waliochaguliwa kuongoza wananchi. Hata hivyo, Mbunge ni Mjumbe wa Baraza la Madiwani ambamo kunaweza kuwa na Jimbo zaidi ya Moja.

Katika hali hii na baada ya mashauriano na watu mbalimbali niliona niwaombe ndugu zetu wa KDI watusaidie kufanya utafiti wa namna bora ya kuimarisha Demokrasia katika ngazi za chini katika Jimbo letu. Moja ya mapendekezo ya Utafiti huo uliofanywa na mtaalamu wa muda mrefu katika masuala ya Serikali za Mitaa, Mzee Sylvester Masinde ilikuwa ni kuanzisha Jukwaa la Viongozi wa Vijiji katika Jimbo la Kigoma Kaskazini.

Jukwaa la Viongozi wa Vijiji

Mara mbili kila mwaka tutakuwa tunakutana kujadiliana changamoto za maendeleo katika Vijiji vyetu na Jimbo letu kwa ujumla. Tutakuwa tunapeana taarifa kuhusu miradi inayofanyika ndani ya Jimbo na kutekekelezwa katika vijiji vyetu mbalimbali. Tutakuwa tunakaguana kuhusu matumizi bora ya fedha za maendeleo katika vijiji vyetu (peer review) na pia kama tunafanya vikao vya kisheria kama Mikutano mikuu ya Vijiji na Halmashauri za vijiji. KDI itakuwa inakusanya taarifa kuhusu maendeleo ya Demokrasia katika Vijiji na Uwajibakaji katika utendaji wa shughuli zetu. Jukwaa pia litatumika kushauriana na Wabunge na Madiwani kuhusu vipaumbele vya kimaendeleo katika Jimbo letu na kuvipeleka mbele kwenye vikao vinavyogawa rasilimali kama Baraza la Madiwani na Bunge.

Jukwaa hili linakusanya viongozi wa wananchi na watendaji. Halina mwelekeo wa kichama kwani mtu yeyote aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kijiji bila kujali anatokea chama gani cha siasa  anakuwa mjumbe wa Jukwaa. Watendaji wa Vijiji wanashiriki ili sote kwa pamoja tujue masuala ya msingi ya Maendeleo ya Jimbo letu na kuweza kuwashirikisha wananchi moja kwa moja katika kujiletea maendeleo yao.

Changamoto za Maendeleo

Kipindi cha maswahil na majibu

Kipindi cha maswahil na majibu

Jimbo letu lina changamoto nyingi sana za kimaendeleo. Tupo nyuma sana katika Elimu kulinganisha na majimbo  mengine nchini, wakati tuna zaidi ya Shule za Msingi 80, Shule za Sekondari zipo 14 tu na katika hizo yenye Kidato cha Tano na Sita ni moja tu. Tumejitahidi kuwa na Zahanati takribani katika vijiji vyote lakini vituo vya Afya vipo 2 tu ukiachana na miradi inayoendelea katika kata ya Mahembe, Mukigo, Mwandiga na Kagunga. Hatujaweza kumaliza tatizo la Maji kwenye baadhi ya Vijiji vyetu. Huduma za Usafiri vijijini bado hazijatengemaa licha ya kukamilika kwa Barabara za lami za Mwandiga – Manyovu na Kigoma – Kidahwe. Hali kadhalika, ni vijiji 3 tu kati ya Vijiji vyote 32 vina huduma ya Umeme na umeme wenyewe bado haujasambazwa vya kutosha. Pamoja na kujaliwa Ziwa lenye samaki watamu (migebuka na dagaa) na wengi na hata mali asili nyingine, bado uvuvi wetu ni duni na usio nguvu ya kuondoa watu wetu kwenye umasikini. Hifadhi yetu ya Gombe haijatumika vya kutosha kukuza utalii na Ukuaji wa Sekta ya Kilimo bado si wa kiwango cha kuridhisha licha ya kuwa na michikichi mingi ambayo bei ya mawese inazidi kupanda kila mwaka katika soko la Dunia na kahawa (Gombe Coffee) bora zaidi kuliko zote Afrika kusini mwa jangwa la Sahara kwa miaka miwili mfululizo sasa.

Vyanzo vya Mapato kiduchu

Kufuatia kuanzishwa kwa Wilaya ya Uvinza, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma itakayobakia ni jimbo letu lenye kata 11 na vyanzo vichache sana vya mapato. Halmashauri yetu kwa ujumla inaweza kukusanya takribani Tshs 1.2bn pekee kwa mwaka ilhali Bajeti nzima ya Halmashauri yetu ni tshs 31bn. Zaidi ya asilimia 70 ya mapato haya yanatoka sehemu ya Kigoma Kusini ambayo sasa inakuwa ni Wilaya ya Uvinza na inakuwa na Mamlaka yake ya Serikali za Mitaa (Halmashauri ya Wilaya Uvinza).

Hivyo kuna changamoto kubwa sana katika Jimbo letu kuhakikisha tunabuni vyanzo vipya vya mapato ili Halmashauri yetu iwe endelevu. Ndio maana ni muhimu kuhakikisha kwamba (i) tunaanzisha eneo la viwanda vidogo vya kusindika mazao ya michikichi pale kijiji cha Mahembe ili kuzuia mise kupelekwa eneo la SIDO katika Manispaa ya Kigoma-Ujiji na hivyo kutengeneza ajira kwa watu wetu na kuwezesha Halmashauri kupata mapato (ii) tunaendelea kuwasukuma Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kutekeleza mradi wa Stendi ya Mabasi ya Kimataifa eneo la Mwandiga ili kukuza ajira na kupata mapato kwa Halmashauri yetu (iii) kuhakikisha Mamlaka ya Bandari nchini inamaliza mradi wa Ujenzi wa Bandari ndogo Kagunga ili kutengeneza ajira kwa watu wetu na kuleta mapato kwa Halmashauri (iv) kuwahimiza TANAPA kutangaza zaidi Hifadhi ya Gombe ili kupata watalii wengi zaidi na kujenga nyumba za wageni katika vijiji vya Mwamgongo na Mtanga ili kutengeneza ajira na kukuza mapato ya Halmashauri.

Jukumu la kukabili changamoto hizi ni letu sisi viongozi. Tumepewa ridhaa na wananchi wetu, kila mtu katika ngazi yake ili kukabili changamoto hizi kwa kushirikiana. Ni wazi tumeanza juhudi mbalimbali. Kama Mbunge wa Jimbo hili nimeajiri Mhandisi Mshauri (consultant) ambaye anatutengenezea mpango wa Maendeleo wa Jimbo letu (na baadaye Halmashauri yetu)  kwa kuibua maeneo ya kukuza uchumi wa Jimbo, kuongeza ajira na kuondoa kabisa umasikini. Mara baada mshauri huyu kumaliza kazi yake, tutawasilisha rasimu ya Mpango huu katika kikao cha Jukwaa ili kuweka maoni yenu na kupata mpango mzuri utakaotusaidia kuchochea maendeleo.

Utafutaji Mafuta (Oil exploration)

Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) limetangaza mshindi wa Zabuni ya kutafuta mafuta katika kitalu cha Ziwa Tanganyika Kaskazini. Eneo hili ni eneo lote la Kaskazini mwa Jimbo letu kuanzia Kijiji cha Kalalangabo mpaka Kijiji cha Kagunga. Kampuni ya TOTAL SA ambayo ni Kampuni tanzu ya Total ya Ufaransa ndio imeshinda zabuni hiyo na hivi sasa inajadiliana na TPDC kuhusu mkataba wa kutafuta Mafuta (PSA). Baada ya Kitalu hiki kutolewa hivi sasa kuna jumla ya Kampuni tatu zinazotafuta mafuta Mkoani Kigoma (Kampuni ya Motherland ya India eneo la Bonde la Malagarasi, Kampuni ya Beach Petroleum ya Australia katika Kitalu cha Ziwa Tanganyika Kusini na hiyo ya Total). Kutolewa kwa leseni hizi ni ama faida au laana kwetu. Ili kuepuka laana ni lazima kujipanga vizuri, kuhakikisha tunafuatilia hatua zote za mikataba na hatimaye kuwa na mikakati ya dhati ya kufaidika na rasilimali ya mafuta kama itapatikana. Hata kabla ya kupatikana kwa mafuta (ambapo wataalamu wa mafuta wanasema yapo, na hata hadithi za wazee wetu wavuvi hutwambia wamekuwa wakiona dalili) lazima tufaidike na uwekezaji katika utafutaji.

Meli yetu ya MV Mwongozo imekodishwa kwa Kampuni ya Beach Petroleum kwa mwaka mzima kufanya tafiti za mafuta. Nimeona nyaraka zinazoonyesha kuwa Kampuni hii itakuwa inalipa dola za kimarekani 900,000 kwa mwezi kwa kutumia Meli hii. Mimi kama Mbunge sijawahi kupata taarifa yeyote ya kiserikali kuhusu Jambo hili na sikumbuki kama imewahi kujadiliwa katika vikao vya Baraza la Mashauriano la Mkoa (RCC). Hata kama tozo hii ni sahihi, kwanini jambo hili limefanywa kwa siri? Lakini pia Kampuni hii itaajiri watu kutoka wapi katika utafiti wao ambao nimeambiwa tayari wamepata mikataba huko DR Congo na Burundi ambao pia wametoa leseni za kutafuta mafuta katika maeneo yao ya Ziwa Tanganyika. Tozo hii italipwa kwa Kampuni ya Meli za Taifa (MSCL) yenye makao makuu jijini Mwanza, kutakuwa na kodi yeyote ambayo Halmashauri yetu itakusanya?

Haya ni baadhi ya mambo ambayo nataka tuyajadili katika Jukwaa letu katika vikao mbalimbali. Kila jambo linalohusu maendeleo katika eneo letu ninyi viongozi wa vijiji mlijue na kuwaeleza wananchi katika mikutano mikuu ya vijiji.

Umeme Vijijini

Katika Bajeti ya mwaka huu wa fedha 2011/2012, Jimbo letu limefanikiwa kupata mradi wa mkubwa wa kusambaza umeme vijijini. Mradi huu utagharimu shilingi 5.6 bilioni na utaunganisha umeme vijiji vya Kiganza, Bitale, Mkongoro, Kalinzi, Matyazo, Mkabogo, Nyarubanda kwa kutokea Mwandiga. Waziri wa Nishati na Madini aliliambia Bunge kwamba Mradi huu utatekelezwa na Wakala wa Umeme Vijijini na utatekelezwa katika kipindi cha miezi 12 ijayo. Mradi wa kuunganisha vijiji vya Nkungwe, Kizenga na Nyamhoza tayari unatafutiwa fedha. Ni dhamira yetu kuunganisha umeme vijiji vyote vya Jimbo letu katika kipindi cha Bunge la Kumi. Ni matumaini yangu kuwa viongozi wa vijiji mtashirikiana na REA na TANESCO kuharakisha miradi hii. Muwape ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa miradi na tuwe wepesi kutatua migogoro yeyote itakayotokea kwa wananchi hasa wale watakaopaswa kuondoa mazao yao kupisha njia ya umeme. Hata hivyo ni muhimu kuhakikisha wananchi wetu wanalipwa fidia stahili.

Miradi itakayotekelezwa

Katika mwaka wa fedha 2011/2012 Halmashauri ya Wilaya Kigoma imepitisha miradi ya Maendeleo yenye thamani ya Tshs 4.5 bilioni itakayotekelezwa katika vijiji vya Jimbo la Kigoma Kaskazini. Jumla ya Bajeti nzima ya Maendeleo kwa Halmashauri nzima ni Tshs 9.5 bilioni. Miradi hii itatekelezwa katika vijiji vyenu. Tunataka ninyi muwe chachu ya kuona fedha za miradi hii zinafika vijijini na kutumika ipasavyo. Ninapendekeza kuwa kila tutakapokuwa tunakutana tuwe tunapeana taarifa kuhusu miradi hii na pale tutakapoona miradi inahujumiwa mara moja tutoe taarifa kwa Sekretariat ya Jukwaa ili kuweza kuingilia kati kuzuia hujuma. Ninawapa nakala ya miradi yote ili kila mmoja wenu awe nayo aweze kuifuatilia na pia kuwaeleza wananchi vijijini.

Miradi mingi inayokuja vijijini kwetu huhujumiwa kutokana na  ufisadi. Mfano mzuri ni ule mradi wa kutandika mabomba kule Kagunga uliofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo la Kigoma Kaskazini. Mmoja wa maafisa wa Idara ya Maji alipewa tshs 10m kwa ajili ya kununua Mabomba mapya, yeye akachukua mabomba ya zamani yaliyokuwa katika bohari yao na kuyapeleka Kagunga. Hata hivyo taarifa iliyoandikwa kwenye Kamati ya Maendeleo ya Jimbo imeonyesha kuwa Afisa huyu amenunua Mabomba mapya na hata kupata risiti kutoka Duka moja la vifaa vya Ujenzi mjini Kigoma! Nimeagiza suala hili lipelekwe katika Baraza la Madiwani na mtumishi huyu achukuliwe hatua kali za kisheria. Pili, Duka lililotoa risiti bandia kwa Afisa huyu wa Idara ya Maji lipigwe marufuku kufanya biashara na Halmashauri yetu.

Ninawataka ninyi viongozi wa Vijiji muwe mstari wa mbele kuibua ubadhirifu wa aina hii katika vijiji vyenu. Pale ambapo ninyi ni wahusika wa ubadhirifu tutakuwa tunaambiana kwenye vikao yetu na kuaibisha wenzetu watakaokutwa na kashfa za ubadhirifu. Pia tutawashitaki kwa wananchi ili kwa kutumia njia za kidemokrasia wang’olewe katika nyadhifa zao.

Kipindi cha maswahili na majibu

Kipindi cha maswahili na majibu

Hitimisho

Ninaamini Jukwaa la Viongozi wa Vijiji Kigoma Kaskazini litatumika kuimarisha mawasiliano na ushirikiano miongoni mwa viongozi bila kujali itikadi zetu za vyama, litakuza demokrasia vijijini kwetu na kuongeza uwajibikaji katika utendaji wa kazi

Natangaza rasmi sasa kwamba Jukwaa la Viongozi wa Vijiji Kigoma Kaskazini limezinduliwa rasmi.

Asanteni kwa kunisikiliza