Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Archive for the ‘TRA’ Category

PAC imeanza uchunguzi kuhusu ukwepaji kodi unaofanywa na makampuni ya Kimataifa

leave a comment »

PAC imeanza uchunguzi kuhusu ukwepaji kodi unaofanywa na makampuni ya kimataifa.

Leo tarehe 30 Machi 2014, kamati ya BUNGE ya PAC imeanza rasmi uchunguzi kuhusu ukubwa wa tatizo la ukwepaji kodi na utoroshwaji wa fedha unaofanywa na makampuni ya kimataifa ( multinational corporations). Uchunguzi huu unatokana azimio la umoja wa kamati za PAC za nchi za SADCOPAC lilioamuliwa Arusha, Tanzania mwezi Septemba mwaka 2013 ( Azimio lilisomeka – PACs should initiate investigations on the extent of tax avoidance/evasion and illicit money transfer in their jurisdiction).

Leo PAC imekutana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Kitengo cha Fedha Haramu ( FIU) na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ajili ya majadiliano ya awali kuhusu uchunguzi huo.

Kamati imeelezwa kuwa tatizo la ukwepaji kodi ni kubwa sana na linagusa sekta zote. TRA imeieleza kamati mifano mbalimbali kwa kila sekta namna gani Taifa linapoteza kodi. Njia zinazotumika ni pamoja na udanganyifu katika mikopo, udanganyifu katika bei za mauzo ya bidhaa zinazouzwa nje na mikataba ya biashara miongoni mwa makampuni yanayohusiana. Uchunguzi uliofanywa na TRA kwa kampuni mojawapo wa uchimbaji madini unaonyesha kuwa kampuni hiyo iliyotangaza hasara mwaka 2011 iligundulika kuwa kumbe ilipata faida ya dola za kimarekani 327 milioni.

Sekta ya Utalii na mahoteli inaonyesha kugubikwa kiasi kikubwa na ukwepaji kodi kwa kampuni katika sekta hiyo kutumia mikataba na makampuni yanayohusiana yaliyokwenye Tax Havens ambayo inahamisha mapato mengi kwenda offshore (profit shifting and base erosion).
Kamati imeelezwa na BoT kuwa hivi sasa kuna uchunguzi maalumu unaoendelea kuhusu ‘illicit financial transfer’ kutoka Tanzania.

Pia ameeleza kwamba hatua zimeanza kuchukuliwa kufunga akaunti za makampuni ya madini yaliyopo offshore kwani sababu za makampuni hayo kuwa akaunti nje hazina msingi tena. Hata hivyo changamoto kubwa ni mikataba waliyoingia na Serikali ambayo inawaruhusu kufungua akaunti offshore na kuweka mapato yao yote ya mauzo ya madini huko.

Utoroshaji wa fedha kutoka Tanzania ni changamoto kubwa sana ya maendeleo ya Tanzania katika kupambana na umasikini. Utoroshwaji umekuwa ukikua mwaka hadi mwaka. Taarifa ya benki ya maendeleo Afrika inaonyesha kuwa mwaka 2010 peke yake Tanzania zilitoroshwa jumla ya dola za kimarekani bilioni 1.3 ambazo zilikuwa sawa na asilimia 5 ya Pato la Taifa (GDP) na zaidi ya asilimia 20 ya mapato ya ndani ya TRA.

Kamati ya PAC itaendesha uchunguzi na kuandaa taarifa itakayowasilishwa bungeni kwa hatua zaidi. Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa BUNGE la Tanzania kuendesha uchunguzi wa aina hii. Pia Tanzania imekuwa nchi ya kwanza katika eneo la SADC kutekeleza azimio hili. Nchini Uingereza kamati ya PAC ya BUNGE la uingereza iliendesha uchunguzi kama huu na makampuni makubwa kama google, Amazon na Starbucks waligunduliwa kukwepa kodi nchini humo. Kwa nchi za Afrika sekta yenye kutorosha fedha na kukwepa kodi kwa wingi ni sekta ya madini, mafuta na gesi. Mwaka 2013 mwezi Desemba kamati ya PAC Tanzania ilikutana na PAC – UK ili kupata uzoefu wa namna ya kuendesha uchunguzi wa aina hii.

Zitto Kabwe, MB
Mwenyekiti, PAC
Dodoma
30-03-2014

RELATED STORY: Africa’s $200 billion kept in foreign banks  (‘Rich beggar’ paradox that is Africa’s forex reserves)

Courtesy: THE EAST AFRICAN

Taarifa ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu Gesi(Ripoti ya Pan African Energy)

with one comment

Na Zitto Kabwe

Mkutano wa Tano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mambo mengine ulijadili Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Sekta ndogo ya Gesi nchini. Taarifa hii ilitokana na kazi iliyofanywa na Kamati ndogo iliyoundwa na Kamati ya Nishati na Madini chini ya uongozi wa Mbunge wa Bumbuli ndugu Januari Makamba. Miongoni mwa Hadidu rejea za Kamati ndogo zilikuwa ni kubainisha kama Mikataba, taratibu na Kanuni zinazotawala shughuli za gesi zinazingatia maslahi ya Taifa na hazitiliwi shaka na wadauna Kubainisha kama maamuzi yanayoendesha shughuli za gesi kama vile gharama za   ujenzi, uendeshaji na mambo mengine yanayoweza kuathiri gharama na usalama wa shughuli yanafikiwa kwa ufanisi na yanazingatia maslahi ya Taifa.

Taarifa ya Kamati iliwasilishwa Bungeni na kupitishwa na Bunge ili Serikali iweze kutekeleza maazimio zaidi ya ishirini na Sita yaliyopendekezwa. Miongoni mwa Maazimio hayo ni Azimio namba mbili ambalo linasema  ‘Kamati imejiridhisha bila shaka kwamba  kwa kipindi cha 2004 hadi 2009 Kampuni ya Pan African Energy Tanzania Ltd (PAT) imejirudishia isivyo halali gharama zinazofikia jumla ya dola za kimarekani milioni 28.1 sawa na fedha za kitanzania bilioni 46.3. Kutokana na kujirudishia fedha hizo isivyo halali kumefanya Serikali kukosa gawio lake linalofikia dola za kimarekani milioni 20.1.  Aidha, mpaka wakati Kamati inaandaa ripoti hii, Kampuni ya Pan African Energy Tanzania Ltd (PAT) imeshindwa kuwasilisha uthibitisho wa uhalali wa kujirudishia gharama nyingine zinazofikia jumla ya dola za kimarekani milioni 36. Hali hii inaonyesha mashaka makubwa katika uendeshaji wa sekta hii muhimu ya gesi’.

Azimio hili ni moja ya Azimio linalopaswa kuangaliwa kwa makini sana tunapojadili namna Tanzania inavyosimamia na kufaidika na Sekta ya Mafuta na Gesi. Taifa linafaidika kwa kiwango gani na Wawekezaji wanafaidika kwa kiwango gani ndio msingi wa Mikataba ya Mafuta na Gesi nchini. Hapajawa na mijadala mikali katika eneo hili kama ilivyo kwenye sekta ya Madini na hivyo kuachia kila kukicha Shirika la Maendeleo ya Mafuta Nchini (TPDC) likisaini Mikataba ya Kutafuta na kuchimba Mafuta na Gesi (Production Sharing Agreements – PSAs) bila Watanzania kujua haswa ni jambo gani linasainiwa. Hivi sasa kuna Mikataba hii 23 hapa nchini.

Duniani kote kuna familia mbili za mikataba ya Mafuta na Gesi. Familia ya kwanza inaitwa ‘concessionery’ ambapo Kampuni ya Mafuta ya Binafsi inapewa haki zote za mchakato mzima wa kutafuta, kuchimba, kusafirisha na kuuza Mafuta au Gesi. Umiliki wa Mafuta (rights) unakuwa ni wa Kampuni Binafsi na sio Serikali. Katika mfumo huu Kampuni hulipa mrahaba Serikalini na kodi zinazopaswa. Nchi kama Marekani, Uingereza na Canada hutumia mfumo huu.

Familia ya pili ni Mikataba ya Uzalishaji au kwa Kiingereza Production Sharing Agreements (PSAs). Katika mfumo huu Haki (right) inabakia kuwa mali ya Taifa husika na Kampuni ya Mafuta huwa ni kama mkandarasi tu wa kutafuta na kuchimba mafuta. Akipata mafuta, anaondoa gharama za kuzalisha na faida inagawiwa kati ya Kampuni hiyo na nchi husika kupitia Shirika la Mafuta. Huu ndio mfumo unaotumika hapa Tanzania na ulianzia huko Indonesia na Venezuela miaka ya sitini. Kutokanana mfumo huu ndio tunapata masuala haya ambayo Kamati ya Nishati na Madini imegundua kama nitakavyofafanua kwa ufupi hapa chini.

Mkataba wowote wa Mafuta na Gesi ni lazima uzingatie Uzalishaji na Mapato kwa ujumla, mrahaba kwa nchi, urejeshaji wa gharama za uzalishaji na kodi mbalimbali na namna faida inavyogawanywa. Kampuni ya Pan Africa Energy kujirejeshea gharama isizostahili za zaidi ya shilingi 46 bilioni ni sehemu ya mianya iliyopo katika mikataba yetu. Jumla ya shilingi 110 bilioni zimeonekana kuwa na mashaka makubwa katika mahesabu ya Kampuni hii.

Taarifa inaonyesha kwamba Kampuni hii imeweka pia Gharama zao za uzalishaji kwa miradi ya nje ya Tanzania. Kwa kuwa Kampuni ya Pan Africa Energy Tanzania Limited ni Kampuni Tanzu ya Pan Africa Energy iliyosajiliwa ‘offshore’ Mauritius ambayo nayo ni Kampuni tanzu ya Orca ambayo pia imesajiliwa visiwa vya Jersey, Tanzania isingekwepa kubambikiwa gharama ambazo si zake ili kupunguza mapato ya Serikali ya Tanzania. Imewahi kuelezwa huko nyuma kwamba hizi njia za kukwepa kodi zimeshamiri sana kutokana na Makampuni makubwa yanayofanya biashara hapa nchini kufanya ‘tax planning’ na hivyo kuhamisha mapato yao kwenda nchi zisizo na kodi kubwa kama Mauritius, Isle of Man, Jersey au hata City of London.

Mwaka 2009 mwezi Aprili katika Taarifa yake ya mwaka, Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma ililiambia Bunge kwamba Mkataba kati ya TPDC na Pan Africa Energy ni moja ya mikataba mibovu kuliko yote nchini. Hii ilitokana na ukweli kwamba kwa mujibu wa PSA kati ya TPDC na Pan Africa Tanzania, mrahaba wa mafuta wa asilimia 12 unalipwa na TPDC na pia Kodi ya Mapato inakokotolewa kutoka katika mrahaba huo. Kwa maana hiyo Kampuni hii hailipi Mrahaba na pia hailipi kodi ya Makampuni (corporate tax) kwa mujibu wa Mkataba. Suala hili Kamati ya Nishati na Madini haikuliangalia (labda kwa kuwa ni la kimahesabu). Kamati ya POAC ilitaka mikataba yote ya Mafuta iangaliwe upya ili kuondoa mazonge haya yanayokosesha Taifa mapato makubwa sana.

Uwezo wa TPDC kukagua mahesabu ya Kampuni za utafutaji mafuta ni mdogo au haupo kabisa. Kama TPDC wangekuwa na uwezo huu leo Kamati ya Nishati na Madini isingekuta madudu haya katika kampuni. Pia kama Kamati ya Nishati na Madini ingeangalia mikataba ya kampuni zote za kutafuta mafuta wangekuta madudu mengi zaidi. Kuna kampuni moja yenye kisima pale Mkuranga, wamesema gharama za kuchimba visima vile ni dola za Kimarekani 240 milioni ilhali gharama halisi ni dola za kimarekani 60 milioni tu. Hivyo Gesi ikianza kuchimbwa itabidi warejeshe gharama zao kwanza. Tanzania haitapata lolote mpaka Gesi ile itakwisha.

Kuna haja ya kufanya marekebisho makubwa sana katika uendeshaji na usimamizi wa sekta ya Gesi Tanzania. Shirika la TPDC lirekebishwe kwa kuanzisha Mamlaka ya Mafuta na Gesi yenye uwezo na nguvu ya kusimamia uwekezaji katika sekta hii. Vilevile kuwepo na Shirika la Mafuta na Gesi (PetroTan –National Oil and Gas Company) ambalo litashiriki katika uwekezaji  kikamilifu na kampuni binafsi. Tusiposimamia vema sekta hii Taifa letu litaingia kwenye matatizo makubwa sana huko siku za usoni.

Maneno ya Mwana Uchumi Gwiji Joseph Stiglitz ni ya kuzingatia sana. Anasema, Mara zote nchi zinazoendelea zijue, wanapojadiliana na Kampuni kubwa za Mafuta, Kampuni hizi hufikiria jambo moja tu. Jambo hilo ni kuongeza mapato yao kwa kupunguza mapato ya mataifa husika. Tanzania ni lazima ihakikishe kwamba inapangua mbinu zote za Makampuni makubwa kwa kujenga uwezo wa Wananchi wake kupitia Shirika la Mafuta na Gesi kuweza kuwa na mikataba yenye kujali faida kwa nchi. Hili la Pan Africa Energy litufumbue macho.

 FULL REPORT YA HUJUMA SEKTA YA GESI

View this document on Scribd

Walipa Kodi 15 Wakubwa Tanzania (Tanzania Top 15 Tax payers) & the missing household names

with 39 comments

Kutoka Hotuba ya Waziri Mkuu 26.08.2011 – Makampuni yanayoogoza kwa kulipa kodi

Note: (Highlights)

Only one Mining company (the smallest ie Resolute Mining), only one telecom company(Airtel Tanzania).

Household names like MeTL, Bakhresa/Azam, IPP, VodaCom, Coca cola, Pepsi(SABCO), Serengeti Breweries, Barrick Gold, AngloGold Ashanti not seen. No oil marketing companies pia.

One can conclude that, TBL is the most profitable company in Tanzania, NMB is the most profitable Bank.

 A public debate is needed.

Here under is the an extract from the Prime Minister speech;

Mheshimiwa Spika,

1. Nitumie nafasi hii kuwapongeza baadhi ya Walipakodi Wakubwa kwa Serikali na ambao wamefanya vizuri kati ya kipindi cha mwaka 2005 na 2011. Kwa kipindi hicho, Makampuni yaliyoongoza kwa kulipa kodi ni pamoja na:

i.              Tanzania Breweries Ltd. (Shilingi Bilioni 165.4);

ii.            National Microfinance Bank (Shilingi Bilioni 108.6);

iii.           Tanzania Cigarette Company (Shilingi Bilioni 92.1);

iv.            National Bank of Commerce (Shilingi Bilioni 89.9);

v.            CRDB Bank Ltd. (Shilingi Bilioni 79.2);

vi.           Tanzania Ports Authority (Shilingi Bilioni 76.8);

vii.          Tanzania Portland Cement (Shilingi Bilioni 73.4);

viii.        Airtel (T) Ltd. (Shilingi Bilioni 63.6);

ix.           Tanga Cement Company Ltd. (Shilingi Bilioni 43.6);

x.            Standard Chartered Bank Ltd. (Shilingi Bilioni 40.0);

xi.           Citibank (T) Ltd. (Shilingi Bilioni 35.7);

xii.          Resolute (T) Ltd. (Shilingi Bilioni 32.1);

xiii.        Tanzania International Container Terminal Services (Shilingi Bilioni 25.9);

xiv.         Tanzania Distillers Ltd. (Shilingi Bilioni 13.4); na

xv.          Group Five International (PTY) Ltd. (Shilingi Bilioni 9.5).

2.  Napenda kutoa rai kwa Makampuni yote Nchini kuiga mfano huu mzuri. Wito wangu kwa Makampuni, Wafanyabiashara Wakubwa kwa Wadogo na Wananchi wote ni kuongeza juhudi katika kufanya biashara zao ili zizalishe kwa wingi na kupata faida kubwa zaidi. Faida kubwa itachangia katika kuongeza Mapato ya Serikali kwa njia ya Kodi na hivyo kusaidia kukuza uchumi, kuongeza Pato la Taifa na la Mwananchi mmoja mmoja na kuondoa Umaskini. Niwadhihirishieni kwamba, Serikali inatambua umuhimu wao kwa maendeleo ya Nchi yetu na itahakikisha inaongeza juhudi zake za kuweka Mazingira Wezeshi kwa Makampuni hayo kufanya shughuli zao vizuri ili kuwezesha kulipa Kodi kwa mujibu wa Sheria.

Written by zittokabwe

August 26, 2011 at 8:29 PM