Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Asanteni sana Kigoma Kaskazini-Zitto Kabwe

with 9 comments

Asanteni sana Kigoma Kaskazini

HOTUBA YA MH ZITTO KABWE (MBUNGE KIGOMA KASKAZINI) ILIYOTOLEWA LEO TAREHE 15 MACHI 2015

Zitto Kabwe speaking at a rally in Karatu on September 30 2012.

Zitto Kabwe .

Mwanamapinduzi na Rais wa zamani wa Burkina Faso Thomas Sankara alisema kuwa ili kuleta mabadiliko ya kimapinduzi ni lazima kuwa na hali fulani ya uendawazimu. Ila tusiufikirie uendawazimu huu wa kuokota makopo bali ule ukichaa mzuri wa kuamini katika mambo au misingi fulani na kuisimamia kwa dhati pamoja na changamoto nyingi.

Kwa kuamini kwa dhati katika mabadiliko haya na kutaka kuboresha maisha ya wanakigoma, mwaka 2005 nilikuja kwenu kuwaomba ridhaa ya kuwatumikia kama mwakilishi wenu Dodoma. Nikiwa na umri wa miaka 29 tu. Labda ulikuwa ni msukumo wa matumaini yangu makubwa yanayoambatana na ujana yaliyowashawishi, kwani mliniamini na kunipa kazi hiyo ya heshima kubwa ya kuwawakilisha.

Mwaka 2010 mliniamini tena, naamini kutokana na utekelezaji wangu mzuri wa kazi na mafanikio tuliyoyaweza kuyapata katika jimbo letu. Hivyo kwa miaka kumi tumekuwa bega kwa bega katika safari hii ya pamoja ya kujenga na kuiendeleza jimbo letu, na leo nimekuja kuwashukuru kwa fursa mliyonipa kwani safari yetu inafikia mwisho. Fursa mliyonipa ni ya kipekee kwani ilikuwa fursa si tu ya kuwatumikia ninyi bali kulitumikia Taifa langu.

Katika miaka kumi hii kuna mambo makubwa tumeyafanya pamoja na kufanikiwa; na kuna mambo ambayo hatukuweza kuyafanya. Kwa yale ambayo hatukuweza kuyafanya naomba radhi. Kwa yale ambayo tumeweza kuyafanya naomba kuwapongeza sana kwa kufanikisha. Kwani kama Mwalimu Nyerere alivyotuambia kuhusu Uhuru na Maendeleo: “Uongozi ni kuongea na kujadili na wananchi, kuwaelewesha na kuwashawishi. Uongozi ni kufanya kazi pamoja na wananchi na kuonyesha kwa vitendo mnachotaka kufikia. Uongozi ni kuwa mmoja wa wananchi na kutambua kuwa mko sawa…. Wananchi hawawezi kuendelezwa bali wanajiendeleza.” Na ndivyo tulivyofanya kwa miaka kumi, na kwa ushirikiano wenu tumeweza kufanikisha miradi mikubwa katika Jimbo letu.

Mwaka 2005 tulikuwa hatuna barabara ya lami hata moja. Leo hii, ninapoongea nanyi tuna barabara za lami zenye zaidi ya kilomita 100 kuunganisha Jimbo letu na majimbo mengine kwa pande zote za nchi kavu. Vilevile tuna mradi mkubwa wa kuunganisha vijiji vya ufukweni mwa Ziwa Tanganyika kwa barabara. Kiujumla kwa mkoa wa Kigoma tumefanikiwa kumaliza daraja la Malagarasi na hivyo kuunganisha mkoa wetu na mkoa wa Tabora kwa lami jambo ambalo lilikuwa kilio chetu cha muda mrefu sana tokea enzi na enzi. Muhimu zaidi ni kuwa barabara hizi zinatumika na wananchi, wafanyabiashara na wakulima ili kuwasiliana, kufanya biashara na kupanua masoko.

Tumefanikiwa kuongeza huduma ya Nishati ya Umeme kwa kuunganisha vijiji zaidi ya 16 hivi sasa. Changamoto kubwa iliyobakia mkoani kwetu ni uzalishaji mdogo wa umeme na wenye gharama kubwa sana. Suluhisho la kudumu ni kufanikisha mradi wa Malagarasi wenye uwezo wa kuzalisha 44MW ambao utakuwa nafuu na kuwezesha pia kusambaza umeme mikoa jirani ya Katavi na Tabora, na hata kuuza nchi jirani ya Burundi. Viongozi wa kisiasa wa mkoa wa Kigoma watakaoingia kwenye uongozi baada ya uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka 2015 hawana budi kuweka kipaumbele kikubwa kwa mradi huu. Bila ya umeme wa uhakika na nafuu hatuwezi kupiga hatua ya kuongeza thamani ya mazao yetu kwa kujenga viwanda vya usindikaji na kuongeza ajira ya vijana wetu.

Tumefanikiwa kuanza miradi ya Bandari na Soko kubwa kijiji cha Kagunga. Lengo likiwa ni kukuza biashara ya bidhaa kati yetu na nchi ya Burundi. Kigoma ni mji wa biashara kiasili na biashara ilichukua nafasi kubwa ya uchumi wa mkoa huu kwa miaka mingi sana. Kuimarishwa kwa miundombinu ya Biashara ni sehemu ya miradi ya kimkakati katika kuuweka mkoa kuchukua nafasi yake ya kiuchumi katika nchi yetu. Katika muktadha huo ndio maana tunaendelea na miradi ya Bandari Kibirizi na Bandari ya Nchi Kavu Katosho. Ndio maana tunaendelea na mradi wa Kituo cha Usafirishaji Mwandiga ( Mwandiga International Transportation Terminal ) na eneo maalumu la kiuchumi Ujiji. Haya yote tuliyaanzisha kwa pamoja nanyi ili kuhakikisha kuwa uchumi wetu unazalisha ajira kwa watu.

Tumefanikiwa kuongeza udahili wa wanafunzi wa sekondari kwa kuwa na shule katika kata na baadhi ya kata tumejenga shule kila kijiji. Hata hivyo, tuna changamoto kubwa sana ya ubora wa elimu katika mkoa wetu. Katika jimbo la Kigoma Kaskazini zaidi ya 90% ya watahiniwa wa Kidato cha Nne wanapata madaraja ya mawili ya chini, wakati ule daraja la nne na daraja la sifuri. Tumeanzisha mradi wa majaribio ya kutoa motisha kwa Walimu ili kuona namna bora zaidi ya kuhakikisha elimu inaboreshwa. Shirika la Twaweza linaendesha mradi mkubwa wa motisha kwa walimu na baada ya mwaka huu tutakuwa tumejifunza njia bora za kuongeza ubora wa elimu kwa watoto wetu. Bila Elimu bora miradi yote niliyoeleza hapo awali haina maana yeyote. Serikali imetoa Sera mpya ya Elimu, ni wajibu wetu kuona namna ya kuitekeleza katika ngazi yetu ili kupata mafanikio. Hata hivyo, uongozi wa kisiasa utakaoingia baada ya uchaguzi mkuu mwaka huu hauna budi kujielekeza vya kutosha katika elimu ya ufundi ili kujenga stadi za kazi kwa vijana waweze kujiajiri na kuajiriwa.

Tumefanikiwa kupanua huduma ya Afya kwa kuboresha Zahanati zetu chache zilizokuwepo na kujenga zahanati kadhaa mpya na miradi ya vituo vya afya vya Mahembe na Nyarubanda. Hata hivyo nasisitiza sana umuhimu wa kinga kuliko tiba kwani gharama za afya zimekuwa kubwa sana. Ndiyo maana tulipojadili hili suala, ilionekana kuwa suluhisho linatakiwa lipatikane kwa kufanya kile ambacho hatujawahi kufanya ili kuleta maendeleo ya kweli. Na mniruhusu hapa kunukuu wosia wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alipotuasi kuwa “Maendeleo ni maendeleo ya watu. Barabara, Majengo, kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao na masuala mengi kama haya si maendeleo, bali ni vitendea kazi tu vya maendeleo” Ndiyo maana kulikuwa na umuhimu wa kutafuta njia mpya na mbadala kuboresha maisha ya mwananchi, hususan kwa upande wa afya. Uthibitisho wa ubunifu wetu ni kuwa katika kipindi hiki cha miaka 10 tumefanikiwa kuanzisha hifadhi ya jamii kwa wakulima.

Tulianza na Ushirika wa Wakulima wa Kahawa wa RUMAKU ambapo wananchi walijiunga na NSSF na hivyo kupata mikopo ya muda mfupi, huduma za afya bure na kujiwekea akiba kwa ajili ya mafao ya muda mrefu. Mafanikio makubwa yaliyopatikana yamewezesha wazo hili kusambaa nchi nzima na hivi sasa wakulima wa Korosho, Chai, Pamba, Tumbaku wanafuata nyayo za Wakulima wa Ushirika wa RUMAKU. Hapa Kigoma wazo hili sasa linatekelezwa kwa wavuvi wa mwambao mwa Ziwa Tanganyika. Ndoto yetu ni wananchi zaidi ya theluthi moja kwenye nguvu kazi wawe na Hifadhi ya Jamii. Natoa wito kwa wananchi wengine wenye uwezo wa kuchangia hifadhi ya jamii wajiunge na vikundi vya ushirika na kuchangia ili kufaidika na mafao ya muda mrefu kama pensheni lakini pia yale ya muda mfupi kama bima ya afya, mikopo kupitia SACCOS na mengine yatakayoanzishwa kama bima ya mazao.

Tumefanikiwa kujenga heshima ya watu wa Kigoma hapa nchini. Hivi sasa watu wa Kigoma tunatembea kifua mbele bila woga kuliko hapo awali. Kujiamini na kushiriki kikamilifu katika Ujenzi wa Jamhuri ya Muungano ni wajibu wetu kama raia. Changamoto za kujiona raia wa daraja la pili zimeondoka na zinaendelea kutokomezwa. Juhudi zetu ni silaha kubwa katika kuhakikisha tunakuwa sehemu ya Jamhuri yetu katika kila Nyanja za maisha yetu. Nafurahi kupata fursa ya kushiriki nanyi katika kujenga heshima hiyo ya Mkoa wetu. Nitaendelea kushiriki katika kudumisha heshima hiyo.

Nimejifunza mengi sana katika safari hii ya utumishi kwenu. Kama nilivyosema hapo awali, mliamua kufanya kile kisichozoeleka katika siasa ya nchi yetu kwa kunipa jukumu hili nikiwa kijana mdogo. Naamini kuwa ule ukichaa wangu mzuri wa kusimamia misingi ya kuleta maendeleo kwa wananchi wangu na kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia nimezipigania. Na katika safari hii nimejenga marafiki wengi sana na pengine hata maadui ingawa hao ni wachache. Lakini haijalishi kwani mi binafsi sina uhasama na binadamu mwenzangu.

Katika utumishi wangu kwenu, bungeni nimejifunza namna nchi yetu inaendeshwa. Katika kujifunza huko kuna mambo kadhaa nimefanya ya kujivunia na mengine ni makosa. Mliniruhusu kufanya makosa na kuyarekebisha makosa hayo kwa hiyo kukomaa zaidi. Shukrani za dhati ziwaendee wazee wangu ambao mliniongoza mpaka hapa tulipofika na kunishauri hata kunionya pale palipohitajika. Kwa ujumla nimejifunza kuwa mzalendo zaidi kwa nchi yangu na kuwatumikia watu wa nchi hii. Ndio maana hamkunisikia tu kutetea watu wa Kigoma pekee, bali watu maeneo mengine ya nchi yetu na makundi mbalimbali ya kijamii kama Wakulima, Wafanyakazi, Wasanii, Wavuvi, Wana michezo na wana habari.

Katika safari hii ya miaka 10 kuna watu nimewafurahisha na kuna watu nimewaudhi. Kwa wale niliowaudhi ninaomba radhi. Kwa wale niliowafurahisha ninaomba wasiache kuniongoza na kunishauri kila wakati. Haikuwa safari rahisi na sikutegemea iwe rahisi. Kiuhalisia ilikuwa safari ngumu yenye mafunzo makubwa kwangu. Ilikuwa ni safari yangu kama kiongozi na pia safari yangu binafsi ya kupevuka kifikra na kupata mafunzo kuhusu maisha. Ukifika ulikokuwa unakwenda katika safari, unaweza kutathmini mengi kuhusu safari hiyo, lakini mwisho wa siku unatakiwa ujue kama safari hii ilikuwa njema ama la. Ninajivunia safari hii na ninasema kwa dhati kabisa ilikuwa ni safari njema.

Ni wakati sasa wa kutoa nafasi kwa nguvu mpya kuongoza Jimbo letu. Kushika kijiti pale ninapoishia. Kurekebisha pale nilipokosea. Kuimarisha pale nilipofikia.

Sitakuwa mbunge wenu baada ya Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba lakini nitaendelea kutetea maslahi ya Mkoa wa Kigoma na Taifa letu kwa njia nyingine.

Sitaacha ule uendawazimu mzuri aliyoizungumzia Thomas Sankara unaoleta maendeleo ya kimapinduzi. Na misingi ni ileile na maadui ni walewale ambao mwasisi wetu Mwalimu Nyerere aliyokuwa anasema tupambane nao, yaani umaskini, ujinga, maradhi na sasa tumeongeza ufisadi. Kizazi chetu kina jukumu la kipekee kuendeleza mapambano haya na nitaendelea kuhakikisha tunafanya mapinduzi na kuwa na Taifa lenye misingi madhubuti ya uwajibikaji ili kuondoa kila aina ya ufisadi na kutumia rasilimali za nchi kuondoa umasikini, ujinga na maradhi.

Asanteni sana Kigoma Kaskazini!

Written by zittokabwe

March 15, 2015 at 5:09 PM

9 Responses

Subscribe to comments with RSS.

 1. Reblogged this on rukajuu.

  rutarakajagi

  March 15, 2015 at 5:19 PM

 2. Mr.Zito, Hakika umefanya makubwa.

  zamberi

  March 15, 2015 at 5:24 PM

 3. Hotuba nzuri yenye hisia na matumain kwa wana Kigoma Kaskazini

  Mustafa

  March 15, 2015 at 7:33 PM

 4. Hongera sana kwa hotuba nzuri yenye mafunzo makubwa sana kwa wabunge wengine wanaoomba ridhaa za wananchi na kuishia kumaliza muda wa miaka 5 bila kuleta maendeleo wala kushirikiana na wananchi ili kufikia azma ya maendeleo hayo. Pia tunaomba sisi ambao ni wafuasi wako utuweke wazi kwanini hugombei tena ubunge?

  ZAKIA SALUM

  March 15, 2015 at 7:47 PM

 5. Bw. Zitto,
  Asante sana kwa hotuba yako nzuri sana. Ni hotuba ambayo imejaa busara, ukomavu wa kisiana, umahiri katika kuwatumikia watu na mfano wa uongozi wenye kikomo. Unastahili pongezi na kuigwa kwa hili. Mimi si msemaji wa “wapiga kura” wa Kigoma kaskazini lakini naomba nitoe maoni yangu ingawaje yanaweza kureflect kwa kiasi kikubwa maoni ya wana kigoma kaskazini.
  Mosi, tunakushuru sana kwa kurudi jimboni kutuaga maana ni wana kigoma kaskazini waliokupa heshima hii and the man who you’re today.Utumishi kwa umma ni kazi ngumu na yenye vikwazo vingi. Umepambana kadri ya uwezo wako na umefikia tamati na umeona ni busara uwaachie wengine waendeleze pale ulipoishia. Uzuri ni kwamba umehighlight changamoto na matatizo ambayo yanalikabili jimbo, hivyo huyo ajaye anafahamu nini cha kufanya japo hatumjui huyu ajaye ni mtu wa namna gani.
  Pili umeomba radhi kwa wapiga kura wako, maana safari hii ya miaka 10 ni ndefu na ina uzuri na ubaya wake. Kwa yale ambayo unadhani ulitukosea “tunakusamehe” maana hata wewe ni binadamu na ukamilifu upo kwa Mungu tu peke yake. Kwa yale mazuri uliyoyafanya katika ngazi ya jimbo, mkoa na hata Taifa, tutayaenzi. Asante sana kwa kubadirisha sura ya mkoa wa kigoma kimaendeleo na kuiweka kigoma upya kwenye ramani ya Tanzania. Kabla yako, kigoma ilikuwa haisikiki na watu wa kigoma walikuwa watanzania daraja la pili. Hali hii inabadirika ingawaje haijaisha kabisa.
  Mwisho,umetuacha pia wana kigoma njia panda juu ya hatma yako ya kisiasa. Je, nyota hii ndiyo imezimika au inaenda kuzimika.. Umefukuzwa uanachama na Tanzania ili usikike na kufanya hayo uliyoyafanya ni lazima uwe na jukwaa la siasa “kwa maana ya chama cha siasa”. Wapo wengi sana wamepotea kwenye medani ya Siasa, alikuwepo Dr. Amani Kabourou hasikiki hadi leo, alikuwepo akina Thomas Ngawaiya, Masumbuko Lamwai na wengine wengi tu. Wamezima kisiana na hawapo tena kwenye printing media za taifa letu. Je, tutegmee na wewe kuzimika kama walivyozimika hawa waheshimiwa? Tulizoea kumwona Zitto kabwe kwenye kipindi cha Dakika 45 ITV, tumezoea kumwona Zitto kwenye star tv akitolea ufafanuzi maamuzi fulani, tumezoea kumsikia zitto kwenye BBC, VOA, Deutschvelle, na kwingineko. Je, ndiyo unatoweka hivyo?
  Nani atawasemea watanzani kwenye mambo ya ufisadi, rushwa, matumizi mabaya ya fedha, ubadhilifu wa mali za umma, huduma zisizofaa kwa raia na ukusanyaji wa mapato ya serikali ili kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima kama ville mashangingi wakati watu wanakosa dawa hospitalini, maji, umeme na elimu. Nani atavikagua na kuviwajibisha vyama vya siasa kwa ruzuku inayotolewa kila mwezi. Umewagusa wabadhilifu kwenye chama cha siasa “umeitwa msaliti na umekwenda na maji”. Nani atapinga posho na kuwasemea watanzania? Ni matumaini yangu kuwa utajibu maswali haya.
  Mwenyezi Mungu akujalie maisha marefu na baraka katika maamuzi utakayoyafanya siku za usoni. We’re all together in this.
  Ni mimi mkereketwa wa maendeleo
  Joshua Bukuru
  Brussels, Belgium

  Joshua Bukuru

  March 16, 2015 at 8:37 AM

  • Kweli Mkubwa

   Marunda

   March 17, 2015 at 5:38 PM

  • Mimi pia kama mmoja wa wana kigoma, napenda nikupongeze sana mheshimiwa Zitto Kabwe kwa uamuzi wa busara ulioufanya wa kiliachia jimbo la Kigoma kaskazini ili wengine nao pia washike hatamu jimboni kwetu. Hii imetuonesha jinsi usivyo na uchu wa madaraka. Big up sana. Kama vijana
   pia naamini tumejifunza kwako. Kiukweli kuagana siku zote huwa hakufurahishi masikioni mwa binadamu japo wakati mwingine lazima itokee. Mimi binafsi sikupenda hicho ulichofanya kitokee lakini baada ya kutafakari kwa undani nimeridhika. Hatua ya kuweka wazi mafanikio na changamoto zinazolikabili jimbo letu ni ya kupongezwa sana. Ni ukweli usiopingika kuwa mrithi wako umemtafunia hivyo ni yeye tu kumeza. Mwisho kabisa ni ombi kwako: mheshimiwa nyumbani ni nyumbani, hivyo usilitupilie mbali jimbo letu, hili ni jimbo lako pia hivyo katika shughuli zako jaribu kulipa kipaumbele. Ni mimi Herbert R. Ndayambuwe (makwakwa)

   Nimefurahishwa sana na hotuba yako

   nzuri sana iliyojaa busara na maelezo ya kutosha kuhusu jimbo letu la kigoma
   kaskazini. Umetueleza mafanikio
   tuliyoyapata japo pia naamini hayo ni
   kwa uchache tu na siyo tu kuyasikia
   ukiyasema ni dhahili kabisa kwamba
   yanaonekana kwa macho hasa barabara ambalo lilikuwa kilio chetu kwa

   Herbert Ndayambuwe

   March 18, 2015 at 12:32 AM

 6. Kaka, mimi ni mmoja wa wafuasi wako, mm nikijana ambae napenda kukuweka kama kioo kwenye Medani za Siasa, umefanya jambo la Busara sana kumuachia mtu mwengine kuendesha gurudumu la maendeleo ya Jimbo la Kigoma Kaskazini,
  Pia kwenye mahamuzi ya CHADEMA, nakuunga mkono kwa kauli zako, nakumbuka nilianza kuipenda CHADEMA kutoka kwa Marehem CHACHA WANGWE(R.I.P) wakati tunakaa nae Jirani Kisasa Dodoma TBA, ambako alinifanya kuona kuwa kuna chama cha watetezi wa watu, nakumbuka makala yake kwenye gazeti la Rai, lakini pia CHADEMA haikuwa na wabunge wengi, ilikuwa na wabunge wachache ila walikuwa wanafanya kazi kubwa sana na ndio muono wa watanzania juu ya uwajibikaji ulianza kuonekana, lakini wewe ukiwa mbunge kijana sana katika Bunge la 2005-2010, uulionyesha chachu ya vijana katika bunge na hiyo ndio sababu ya 2010-2015; Vijana wengi sana walipata Ubunge kwa Imani kuwa Zitto mulimuona, ingawa ndani yake wengine hadi wanamaliza awamu hii awajachangia kitu cha maana bali ni ushabiki wa uchama hama CCM au CHADEMA tu.
  Wewe ni ulikuwa ni mbunge kijana mwenye busara uliokuwa ukiweka maslai ya taifa mbele kuliko ya Chama, hili ndio lilipelekea wale wasiokuwa na busara kuunda fitna zifi yako kuwa unatumika na CCM, kwa sababu awafahamu dhumuni la siasa ni kuleta maendeleo na sio kubisha kila jambo.

  Mwisho kabisa mm nakuombea Allah akuwezeshe kutimiza ndoto zako juu ya watanzania

  Marunda

  March 17, 2015 at 5:36 PM

 7. Reblogged this on anthonymtabe.

  anthonymtabe

  March 26, 2015 at 1:13 PM


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: