Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Nyerere Wangu Mimi!

with 16 comments

nyerereMwaka 1984 nilianza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kigoma, katika mji wa Kigoma. Nakumbuka kupelekwa Shule siku ya kwanza na mama yangu mzazi Bi Shida Salum (Mungu amrehemu) nikiwa sina viatu yaani pekupeku wala begi la mkononi, nilikuwa nimebeba mfuko wa nailoni. Nakumbuka usiku wa kuamkia siku ya kwanza kwenda shule, sikulala kwa furaha na hamu ya kuwa msomi, nilijisikia fahari kuanza shule japokuwa sikuwa na kitu chochote cha zaida zaidi ya kaptula ya shule na shati liloshonwa kwa kitambaa cha sanda. Pia nilianza shule nikiwa nimechelewa kwa mwaka mmoja maana wenzangu walianza wakiwa na miaka 7. Mwaka 1983 nilipopelekwa shule mkono wangu haukuweza kushika sikio upande wa pili, ambacho kilikuwa kipimo cha kuandikishwa darasa la kwanza.

Hali ya maisha wakati huo ilikuwa mbaya sana. Nakumbuka kwenda shuleni nikiwa sina kitu tumboni au siku nzima nilikunywa uji usio na sukari. Uji wenyewe ulikuwa ni wa unga wa njano uliotokana na mahindi ya njano ambayo tuliambiwa nchi yetu ililetewa kama msaada kutoka nchini marekani.

Shule yetu kama zilivyokuwa shule nyingi za wakati huo hatukuwa na madawati ya kutosha na vyumba vya madarasa vilikuwa vichache sana. Ilikuwa ni kawaida kwa wadogo (darasa la kwanza mpaka la tatu) kusomea chini ya mwembe na kukaa juu ya matofali. Hali hiyo ilipelekea kaptura yangu ya shule kuwekwa viraka vingi maana ilikuwa inachanika mara kwa mara. Nyakati nyingine ilibidi kwenda shuleni na shati likiwa halijakauka hasa siku za alhamis, siku ya usafi na iwapo nikiwa zamu ya mchana kwani nilikuwa nina shati moja tu tena lililotokana na kitambaa cha sanda.

Kwa dhahiri, watoto wa masikini na matajiri tulikuwa shule moja, darasa moja hata wote kukaa kwenye matofali. Watoto watawala na watawaliwa tulicheza mpira pamoja, kuruka dana na hata kuruka kamba. Hatukujisikia wanyonge kwa sababu hatuna viatu au kuvaa kaptura zenye viraka na mashati ya sanda. Kamwe sikumbuki kudharauliwa shuleni sababu ya uduni wa maisha yangu. Heshima ilitokana na uwezo wako darasani na kupitia hilo nilipata marafiki wa kutoka madaraja yote ya maisha. Nakumbuka mtoto wa Mkurugenzi wa Maendeleo Mkoa wa Kigoma ndugu Daniel Masanja ndiye alikuwa rafiki yangu wa karibu na kwa kuwa sikuwa na hata pesa ya kununua bajia wakati wa mapumziko, yeye alikuwa ananinunulia.

Huko baadaye, ada yangu ya kidato cha kwanza ililipwa na Mzee Sebastian Kasomi ambaye mwanaye Kasomi Mabula alikuwa rafiki yangu mkubwa mara alipohamia shuleni kwetu akitokea mjini Shinyanga. Mzee Kasomi alikuwa Mkuu wa idara ya Kodi ya Mapato mkoani Kigoma.

Licha ya uduni wa maisha watoto wengi tuliishi kwa matumaini makubwa sana. Mwalimu wetu Mkuu ndg. Daniel Andulile alikuwa mkali sana kwa watoto wote bila kujali daraja la maisha la wazazi wao. Alikuwa anatucharaza viboko kwa makosa na utundu bila ubaguzi. Alisisitiza sana kusoma kwa bidii ili kujenga Taifa. Dhana hii ya kujenga Taifa iliingizwa kwenye akili zetu na sisi kumeza bila kujali maana yake. Wakati mwingine tulikuwa tunarudi nyumbani huku tukijadili kitoto kuwa tunajenga Taifa. Kila siku mwendo wa kilometa Sita kwenda na kurudi shuleni.

Elimu hii isiyo ya kibaguzi sasa najua ilitokana na sera za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Jitihada zangu darasani ndio ziilikuwa kipimo cha utu wangu na sio uwezo wa kiuchumi wa wazazi wangu.. Elimu iliyompa fursa sawa za kuendelea na kusonga mbele mtoto aliyekuwa kigoma, kantalamba au Dar es salaam. Elimu iliyokuza ndoto, kuinua ari na kujenga matumaini ya kila mtoto wa kitanzania. Elimu iliyovunja na kusambaratisha matabaka ya kiuchumi na dhamana. Elimu iliyojenga uzalendo na hamasa ya kutumikia taifa letu kwa misingi ya haki, uadilifu na upendo.

Sikuwahi kukutana na Mwalimu Nyerere isipokuwa niliwahi kumwona akiwa ndani ya gari nikiwa nimepanga mstari barabarani alipofanya ziara mkoani kwetu mwaka 1987 nikiwa darasa la nne. Lakini nilikuwa kama ninaishi naye kutokana na namna nilivyotaka kuwa kama yeye. Nikiwa darasa la pili nakumbuka katika mkebe wangu ( mathematical set) mkuu kuu niliweka picha ya kukatwa kutoka kwenye gazeti ya Mwalimu na Kawawa. Na nilijisikia fahari kuwa na picha zao, mara zote nilipokuwa nafungua mkebe kutoa kalamu nilijisemea kimoyomoyo, “siku moja nitakuwa kama wewe”

Licha ya maisha magumu tuliyokuwa tunaishi, maisha ya kupanga mawe kwenye mstari wa kununua mahitaji muhimu kama sukari, sabuni na mafuta kutoka duka la ushirika, maisha ya kushindia uji wa yanga na kutembea mwendo mrefu kwenda shuleni, niliishi kwa imani kubwa kuwa mimi na watoto wengine tupo sawa. Usawa katika kupata elimu, usawa katika kucheza na usawa katika ndoto na matumaini. Nimemaliza elimu ya Chuo Kikuu, ndoto niliyoruhusiwa kuwa nayo kwa sababu ya sera za Ujamaa, za Mwalimu Nyerere.

Ujamaa haukuwa katika usawa wa elimu tu ambapo kila mtoto alipata elimu bure na bora katika Shule za umma bila ubaguzi bali pia namna jamii iliishi. Mtoto alikuwa analelewa na jamii nzima. Ukifanya makosa mtaani mzazi yeyote anakuadhibu ili kukurekebisha. Ukifanya jambo jema, mzazi yeyote anakupongeza.

Mwaka 1985 mwezi Novemba nilipokuwa natoka shuleni, karibia na Benki ya Taifa ya Biashara Tawi la Obed Katikaza, nilikutana na Mama Colleta Furugunya tuliyekuwa tunaishi mtaa mmoja na nikimwita bibi Colleta. Aliponiuliza matokeo yangu ya mtihani wa kumaliza muhula wa pili wa darasa la pili kwa kujiamini nikampa karatasi yangu ya matokeo. Nilikuwa nimeshika nafasi ya tatu darasani nyuma ya Ramadhan Kalukula na Haki Manyaga. Bibi Colleta alinishika mkono mpaka duka la Viatu, Bora Shoes na kuninunulia jozi yangu ya kwanza ya viatu. Viatu vile viliitwa Asante Salim, aliyekuwa Waziri Mkuu wa mwisho wa Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa anajaribu kubadili hali mbaya iliyokuwepo. Hivyo ndivyo nilivyopata viatu vyangu vya kwanza vya shule. Shukrani kwa sera nzuri ya ujamaa, mshikamano na upendo.

Hizo ni enzi.

Advertisements

Written by zittokabwe

October 14, 2014 at 6:12 PM

Posted in Uncategorized

Tagged with , ,

16 Responses

Subscribe to comments with RSS.

 1. What a great story zitto. Umenigusa sana kaka kwani wengi tumepitia maisha hayo na kila nikisoma story zako nahamazika over and over! I wish we meet one day na ntafurahi kupata mawasiliano yako

  Salvatory Okumu

  October 14, 2014 at 6:41 PM

 2. Hizo zilikuwa enzi za ujamaa,undugu na umoja. wakati huo sote tulipoona fahari kuitwa watanzania. Zitto hali hiyo haikukupata kama bahati bali kutokana na misingi iliyojengwa na Azimio la Arusha. leo mtoto wa maskini hawezi hata kumsogelea mtoto wa mkuu wa wilaya achilia mbali kuwa rafiki. Leo wakubwa wana daraja lao na maisha yao. tuko ktk nchi moja lakini tunaishi ktk dunia mbili tofauti. Malezi ya pamoja ndio sahau. leo mtoto wa mwenzio mkubwa mwenzio na akikosea lete petrol tumchome moto. Inauma sana! Leo utovu wa nidhamu ndio dili. Nani atakemea tabia mbovu kama inalipa? Kama matusi humwezesha Mtu kupata cheo kwa nini mtoto asihimizwe kujifunza matusi? Kama matusi yanatamkwa bungeni na ktk majukwa ya siasa na watukanaji wakiwa vijana kama Mwigulu, Lusinde na Nape. au wazee kama Werema, Wassira, au wakina mama kama Sofia na Hawa Ghasia? Lakini bado liko tumaini kama liko watanzani wanyonge na maskiniutasemaBASI! Kama wanasiasa wote mnaomkumbuka Mwalimu leo (mara moja kwa mwaka) mtatubu na kurejesha misingi ya azimio la Arusha. Yawezekana, kama kila mtanzania “wa kawaida” ataamua kubeba jukumu na kufanya mabadiliko ktk familia na taifa. kwa kuacha kulia na kusema “enzi za mwalimu….” Shime tubadilike sasa. Nyerere hakuwa malaika wala watendaji au wazazi wa nyakat hizo. Bali walikuwa binadamu walioamini na kutenda walichosema.

  Lugano E.J

  October 14, 2014 at 6:56 PM

 3. Dah kumbe wa2 wametokea mbal xana! Huxuxani xuala la elimu!

  Khalid

  October 14, 2014 at 7:37 PM

 4. Mkubwa unenikumbukusha mbali sana kuhusu maisha ya Kigoma na shule yetu ya Kigoma Primary chini ya Mwalimu Mkuu Mzee Daniel Andulile akisaidiwa na Mwalimu Kapondo (Marehemu) kaka unakumbu kumbu sana.
  Sent from my BlackBerry® smartphone from Vodacom Tanzania

  slamecktz09@gmail.com

  October 14, 2014 at 8:19 PM

 5. HESHIMA KWAKO MHESHIMIWA.HAKIKA JK.NYERERE ATAKUMBUKWA KWA BUSARA NA MCHANGO WAKE KWA TAIFA.

  HUWA NAFIKIRI NA KUWAZA NINANI ANAWEZA KUWA KAMA JK.ILA MHESHIMIWA UNAZO ELEMENTS ZA JK NYERERE.
  SONGA MBELE

  edson mgomapayo

  October 14, 2014 at 9:33 PM

 6. Halafu viongozi wetu leo wanasema wanafuata maadili ya Nyerere ! Ipo siku ukweli wote utajidhihirisha.

  mntambo

  October 15, 2014 at 8:59 AM

 7. Kaka Zitto toa kitabu chako cha Historia au Autobiography yako unaweza ukawa una wa inspire vijana watu wengi kupitia maisha yako uliyopitia, kaka. Mi ni hayo nimependa story yako sana. Asante Mwalimu, asante Ujamaa.

  Amon

  October 15, 2014 at 9:10 AM

 8. Hakika wengi tumepitia huko. story yako imenifanya nitoe machozi. mungu akubariki pambana kutimiza ndoto yako,
  tunakuombea kwa mwenyezi mungu.

  AUGUSTINO MBUNDA

  October 15, 2014 at 11:33 AM

 9. Na mimi napenda sana kufikia ulipofikia wewe.

  hajy seif

  October 15, 2014 at 7:33 PM

 10. na kwa aibu kubwa cjui tunatolea wap nguvu ya kuiita tarehe 14 ni siku ya kumkumbuka mwl. ikiwa kila kitu chake kuanzia hekima yake.maneno yake.mienendo yake vyote hvyo tumeamua kuzikacha…..shame on this leaders of today waliosomeshwa na mwalimu na sasa hv wameamua kusaliti watanzania wenzao

  Hillary Ismail

  October 15, 2014 at 8:10 PM

 11. ni kwel asilimia kubwa ya watanzania tumepitia maisha ya umaskini, na tulipokuwa ndani ya uongozi wa mwalimu,tulijckia,na kujiona tuko sawa katika hali zote za kimaisha, lakini sasa ni tofauti sana katka maswala ya kimaendeleo.Wenye nacho wanaongezewa na wasiyo nacho wanabaki vile vile, hiyo ndiyo hali ya sasa Mwalimu always unforgetable on sustainable development.

  Tegemea ngobei

  October 15, 2014 at 10:57 PM

 12. natamani siku moja tanzania tufikie ktk uchumi wa hali ya juu.

  haji seiph

  October 17, 2014 at 11:20 AM

 13. Stori ina mafunzo ndani yake….Je tufanyaje tuurejeshe ujamaa ule??

  jafari

  October 20, 2014 at 8:18 AM

 14. wote wenye mafanikio wamepitia shida hongera sana mungu akuongoze utuongeze vema na kutetea haki

  laurenti dumia

  October 20, 2014 at 10:13 PM

 15. Asante Kaka Kwa Life Story Ya Maisha Yako Inayosisimua, Wengine Tumepitia Maisha Hayo, Hongera Mwl. Nyerere Kwa Sera Zake Nzuri Za Ujamaa, Mungu Ampumzishe Kwa Amani Mzee Wetu…Amen.

  Fredy Chomete

  October 24, 2014 at 12:19 PM

 16. Reblogged this on MKWELI DAIMA.

  EMANUEL HINGI

  November 6, 2014 at 4:43 PM


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: