Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Katiba ni Mwafaka wa Kitaifa. Viongozi zungumzeni

with 3 comments

Kwa takribani wiki tatu sasa kumekuwa na sintofahamu kuhusu muswada wa sheria uliopitishwa na Bunge ili kufanya marekebisho ya sheria ya marekebisho ya Katiba ya mwaka 2011. Mjadala na upitishaji wa sheria hii uliweka rekodi ya pekee katika nchi yetu kwa vitendo vya kihuni kutokea Bungeni ambavyo nisingependa kuvirejea kutokana na aibu kubwa ambayo Bunge liliingia. Kiukweli kuna sintofahamu katika nchi kuhusu kuandikwa kwa Katiba mpya. Hii imechangiwa na kurushiana maneno miongoni mwa wanasiasa wa pande zote mbili, wanaopinga muswada ulivyo na wanaounga mkono muswada ulivyo. Masuala ya Tume imalize kazi yake lini, ushiriki wa Zanzibar na idadi ya wajumbe kutoka Zanzibar kwenye Bunge la Katiba, Wajumbe wa Bunge Maalumu wanapatikanaje na kadhalika ni masuala ambayo yanaweza kupatiwa mwafaka kwa viongozi kukaa na kuzungumza. Haya sio masuala ya kushindwa kujenga mwafaka labda kuwe na nia mbaya dhidi ya mchakato wa kuandika Katiba mpya. Katiba sio suala la kufanyia siasa. Katiba ni uhai wa Taifa.

Ni wazi kuna kundi kubwa ambalo halijitokezi waziwazi ambalo lingependa pasiwe na katiba mpya ya Wananchi. Kuna kundi lingine ambalo lingependa mchakato wa kuandika Katiba uendelee kwa miaka mingine zaidi ili kuweza kupata Katiba bora. Kuna kundi la Wabunge ambao kwa chinichini wanataka mchakato uendelee, uchaguzi uahirishwe mpaka mwaka 2017 na wao waendelee kuwa wabunge. Naamini watu hawa wanaota ndoto za mchana kwani hakuna mahusiano yeyote kati ya uchaguzi mkuu na kuandika katiba mpya. Kama Bunge hili la sasa na Serikali hii itashindwa kukamilisha zoezi hili, Bunge linalokuja na Serikali itakayoingia madarakani itaendelea nalo. Hivyo sio lazima kupata Katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015. CHADEMA imependekeza kuwepo na marekebisho ya mpito kwenye Katiba ya sasa ili kuwezesha Tume huru ya Uchaguzi, masuala ya wagombea binafsi na kadhalika. Vyama vingine vya siasa vinaweza kuwa na mapendekezo yao ya mpito na hivyo kutoa nafasi ya kutosha kabisa wa kuandika Katiba makini.

Changamoto kubwa sana ya siasa za Tanzania ni kelele. Wanasiasa hatuzungumzi kwenye masuala yanayohusu uhai wa Taifa. Kila chama kinakuwa na misimamo yake na kuishikilia na hatimaye kujikuta tunapoteza fursa ya kuzungumza na kujadiliana kama Watanzania. Mwaka 2011 hali ilikuwa hivi hivi mpaka kundi la Wazee viongozi wastaafu walipoingilia kati na kupelekea wanasiasa kukaa na kuzungumza. Bahati mbaya sana viongozi wale ndio sasa wamepewa usukani wa kuandika Katiba kwa kuwa kwenye Tume. Hawawezi tena kufanya kazi ile ya kutafuta suluhu iliyopelekea Rais kuzungumza na viongozi wa vyama vyote vya siasa ikulu jijini Dar es Salaam.

Vyama vya Upinzani nchini sasa vimeungana kupinga muswada wa marekebisho ya Sheria ya Marekebisho ya Katiba ya mwaka 2011. Waziri wa Sheria na Katiba, Waziri wa Nchi ofisi ya Rais mahusiano na Uratibu, viongozi waandamizi wa CCM wote nao wameungana kuunga mkono muswada kama ulivyo. Badala ya kutafuta mwafaka, kumekuwa na kurushiana maneno ya kejeli na kadhalika. Taifa halijengwi namna hii. Taifa linajengwa kwa mwafaka na Katiba ni moja ya nyenzo wa Mwafaka wa Taifa. Niliwahi kuandika huko nyuma kuwa Katiba haiandikwi barabarani bali huandikwa mezani kwa watu kukaa na kukubaliana masuala ya Taifa dhidi ya maslahi ya kivyama ya wanasiasa.

Hakuna kilichoharibika. Bado tunayo nafasi kama Taifa kukaa na kukubaliana. Kwa hali ya sasa nafasi hii ipo mikononi mwa Mkuu wa Nchi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais ana wajibu wa kikatiba wa kuhakikisha umoja wa kitaifa unaendelea kuongoza mchakato huu wa katiba ya nchi yetu. Hata hivyo ni vizuri kutahadharisha kuwa sio sahihi kwa wanasiasa wa pande zote kujaribu kumlazimisha Rais kuridhia ama kutoridhia sheria hiyo. Si sawa kisiasa kwa wanasiasa wa upinzani kujaribu kumlazimisha Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama chenye wabunge wengi bungeni kwenda tofauti na wabunge wake na wakati huohuo ni utovu wa nidhamu kwa Waziri wa Sheria kujaribu kumshauri hadharani Rais wake kuridhia sheria hiyo kwani ni kinyume cha misingi ya uongozi na pia kinatafsirika kama kumshurutisha (blackmail) Rais wake.

Kutosaini muswada huu kunaweza kuleta mgongano kati ya Wabunge wa CCM na Rais. Hata hivyo Rais lazima aweze kushawishi chama chake kwamba umoja wa kitaifa ni muhimu ziadi kuliko maslahi ya kisiasa ya chama chao. Pia kikatiba Rais anasaini miswada kuwa sheria akiwa Mkuu wa Nchi na sio Mkuu wa Serikali ya Jamhuri. Akiwa Mkuu wa Nchi maslahi mapana ni kuweka mwafaka wa pamoja miongoni mwa wananchi. Rais Jakaya Kikwete anapaswa kutumia mamlaka yake kama Mkuu wa Nchi kuiweka nchi pamoja kwa kuurejesha muswada bungeni ili uweze kujadiliwa upya na wadau wote na kupitishwa tena na Bunge. Ibara ya 97 ya Katiba ya sasa imeweka masharti ya utaratibu wa kutunga sheria na iwapo Rais ataurudisha muswada huu Bungeni pamoja na maelezo ya hatua hii, upitishwaji wake utahitaji theluthi mbili ya wabunge wote. Hii itakuwa hatua muhimu sana katika historia ya demokrasia yetu. Rais afuate ushauri huu kwani una manufaa makubwa.

Hata hivyo, ni lazima pawepo na mazungumzo miongoni mwa wanasiasa na makundi ya kijamii kuhusu Katiba. Katiba nzuri itapatikana pale tu ambapo mazingira ya kisiasa yanaonyesha nia njema kwa pande zote kisiasa. Kukwepa kuangaliana machoni na kuzungumza tofauti zetu za kimitazamo ni hatari zaidi. Juzi ngumi zimerushwa Bungeni. Kesho zitakua mitaani na vijijini kwetu. Tunataka kujenga Taifa la namna hiyo?

Written by zittokabwe

September 28, 2013 at 3:28 PM

Posted in Tanzania, Zitto Kabwe

Tagged with , , , , ,

3 Responses

Subscribe to comments with RSS.

 1. Tunakukubali mawazo yako kaka

  bachudi

  September 28, 2013 at 3:59 PM

 2. Nakubaliana nawe kabisa,Rais hapaswi Shurutishwa “Blackmail” aidha na Vyama vya Upinzani wala Chama chake kama kinafanyana hivyo pia.
  Kama Taifa tunapaswa Kuheshimu Utawala wa sheria na Kuheshimu KATIBA iliyopo kwani Bado I Halali na Rais wetu ALIAPA KUILINDA HIYO,kutoitii ama Kutoifuata KATIBA iliyopo ni sawa na UHAINI kwa Nchi.
  Tujiulize Sana na Kuweka “HISIA” pembeni Je Taratibu za Kisheria,Kanuni Kuhusu UUNDWAJI WA SHERIA ulifuatwa ama La??
  Tujiulize Mathalani Je BUNGE letu Kama Chombo cha KUTUNGA SHERIA lilikuwa na Uwezo wa Kupitisha MUSWADA ule ili Hatimaye Rais Akiuridhia Iwe Sheria??
  Tujiulize Pia Kuna Kosa Chama cha Siasa kuwa na Majority(Wabunge wengi zaidi) Waliochaguliwa kwa Kura za WANANCHI ktk katika Bunge ,je hii ni Dhambi??
  Tuumize Vichwa kuangalia sio KIITIKADI NA HISIA bali kwa Dhana Pana ya Demokrasia Chama Kuwa na Wabunge Wengi Maana Yake KIDEMOKRASIA YA UWAKILISHI NI NINI??
  Mwisho Tujiulize kama kwa Kuacha Kanuni za Kupitisha Sheria na Kuongozwa na Hisia za KIITIKADI kuwa mfano hawa Wameshinda na Sisi Tumeshindwa TUTAFIKIA MUAFAKA WA KIMAAMUZI???
  Nauliza hivi sababu Hata Siku Moja ktk Ulimwengu Haitotokea Binadamu wote ktk Nchi Moja Wakawa na SAUTI/MAWAZO fulani Kuhusu Jambo fulani Hata Ndani ya Dini Ambamo kuna VITABU VYA MWENYEZI MUNGU kuna Tafsiri Tofauti za Maandiko.
  Je Mnafikiri Kuaccommodate Mawazo ya Watu Wasiokubali badala ya Kufuata Kanuni ya KIDEMOKRASIA YA WENGI WAPE lakini KUHESHIMU UHURU WA CHOMBO CHA KIKATIBA BUNGE WA KUTUNGA SHERIA ndio Suluhu???
  Tukijenga Precedent Hii ya KULIPOKA BUNGE MAMLAKA yake ya Kutunga Sheria na sasa kuvipa Vyama vya Siasa,Wanaharakati nk nk itakuwaje Huko Mbele???
  Mwishoni itakuwa Kuingilia Uhuru wa Mahakama,Dola ktk shughuli zake Endapo tutaona Maamuzi yake Baadhi yetu Hatuyapendi kwa “HISIA” kulikoni UHALISIA.
  Rais anapaswa kufanya Uamuzi Independently baada ya Kujiridhisha kuwa Uamuzi ama ulifuata taratibu zote ama La na Siyo Kutishwa kuwa USIPOFUATA YETU ITAKUWA HIVI.
  Kamwe Haitotokea Kukubaliana Kila Jambo hata hiyo KATIBA nina Uhakika HAITOKUWA IMECHUKUA MAAMUZI YA WATANZANIA WOOTE! Kuna baadhi Yataachwa na Hawa Walioachwa Mawazo yao Wana HAKI LAKIN hatutosimamisha KATIBA Ajili mawazo yao Yameachwa Yatachukuliwa ya Walio wengi hata kama Wanatoka Chama Kimoja YA WENGI SIO SABABU NI YA CHAMA CHAO BALI NI YA WENGI na hii ndio DEMOKRASIA.

  Benedict Felician

  September 28, 2013 at 5:09 PM

 3. Mimi nionavyo ni kwamba suala la katiba mpya ccm hawataki lifanikiwe, kuna aina ya ujanja ambao ccm wanadhani haujulikani– ambao ni mkakati wao wa kuhakikisha serikali 2 zinabaki zilivyo. Hili ndiyo linaleta utata kwa ccm. Na kwakuwa wametangaza hadharani juu ya jambo hili, watahakikisha inakuwa hivyo. Pendekezo la viongozi kukaa na kuzungumza ni zuri, lakini ccm watakuwa tayari? Kitu pekee kinachotutesa Tanzania ni mawazo mgando ya wanaccm(walio wengi), hawaamini kwamba wanasiasa wa upinzani na wananchi kwa ujumla ni sawa na wao!

  Simon Nguge

  September 29, 2013 at 10:16 PM


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: