Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Malaysia na Tanzania: kuelekea Maisha bora dhidi ya kuelekea Ufukarishwaji kupitia Kilimo

with 8 comments

Zitto Kabwe, Mb

Malaysia na Tanzania: kuelekea Maisha bora dhidi ya kuelekea Ufukarishwaji kupitia Kilimo

Malaysia na Tanzania: kuelekea Maisha bora dhidi ya kuelekea Ufukarishwaji kupitia Kilimo

Wakati Jamhuri ya Tanganyika inapata Uhuru mwaka 1961, Nchi ya Malaya ilikuwa tayari ina uhuru miaka mine kabla. 1957. Malaya ilijiunga na Singapore, Sabah na Sarawak tarehe 16 Septemba mwaka 1963 kuunda Malaysia. Tanganyika ilijiunga na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka miezi saba baadaye. Hata hivyo Singapore ilifukuzwa kutoka katika Muungano wa Malaysia mwezi Agosti mwaka 1965 kutokana na kutofautiana kwa sera kuhusu watu wa asili na namna ya kuwalinda kiuchumi. Viongozi wa Kuala Lumper walitaka kuweka sera za kusaidia wazawa kwa kuwapa upendeleo maalumu wakati viongozi wa Singapore chini ya Lee Kuan Yew walitaka kuwepo na Malaysia moja kwa wote bila upendeleo maalumu kwa Bumiputera (son of the soil). Singapore ina wakazi wengi zaidi wahamiaji kutoka China. Tanzania imeendelea kudumu na Muungano licha ya changamoto kadha wa kadha zinazoukabili muungano huo. Tanzania na Malaysia zote zilitaliwa na mkoloni Mwingereza.

Wakati Tanzania inapata inaundwa mwaka 1964 pato la wastani la mtu mmoja lilikuwa dola za Marekani 63 wakati Malaysia ilikuwa na pato la dola za Marekani 113 Kimsingi nchi hizi zilikuwa sawa kimaendeleo ingawa Tanzania ni kubwa kwa zaidi ya mara tatu ya Malaysia. Hivi sasa Malaysia kipato cha wastani cha mwananchi ni dola za Marekani 10,000 na Tanzania ni dola za Marekani 600. Kwa Tanzania pato la wastani limeongezeka mara kumi takribani na kwa Malaysia limeongezeka mara elfu moja. Nini tofauti ya mikakati ya maendeleo ya nchi hizi mbili?

Leo tutaangalia eneo moja tu la Kilimo na namna Kilimo kilivyoweza kuivusha nchi ya Malaysia na Kilimo hicho hicho bado hakijaweza kuivusha Tanzania. Malaysia iliunda Shirika la Umma linaloitwa Federal Land Development Authority (FELDA) likiwa na wajibu mmoja mkubwa wa kuhakikisha wananchi masikini wanapata ardhi, wanalima kisasa na kuongeza uzlishaji kasha kufuta umasikini. Kila mwananchi masikini aligawiwa ardhi hekta 4.1, ardhi ikasafishwa na kuwekwa miundombinu yote muhimu, ikapandwa michikichi na Mwananchi akapata huduma za ugani ili kukuza michikichi hiyo. Shughuli zote hizi zilifanywa kwa gharama za Serikali na wananchi wale wakapewa kama mkopo ambao walikuwa wanaulipa kidogo kidogo kila wanapovuna na kuuza ngazi/mawese kwa Shirika hili la Serikali. Hivi sasa Shirika hili ni kubwa sana, lina thamani ya dola za kimarekani bilioni 3.5 na kupitia Ushirika wao wananchi hawa waliopewa ardhi ya kulipa michikichi sasa wanamiliki asilimia 20 ya Shirika hili. Malaysia iliweza kuondoa umasikini kutoka asilimia 57  ya wananchi wanaoishi kwenye dimbwi la umasikini mwaka 1965 mpaka chini ya asilimia 3 mwaka 2012. FELDA sasa ni Shirika la kimataifa maana linaanza kuwekeza duniani kote. FELDA ilipouza hisa zake kwenye masoko ya mitaji, IPO  yake ilikuwa ni ya tatu kwa ukubwa baada ya Facebook na Japanese Airlines. Shirika la Umma linalomilikiwa na Serikali, Wakulima na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (EPF) na linaloendeshwa kwa misingi ya utawala bora wa makampuni limeweza kufuta umasikini kwa zao moja tu la Michikichi. Malaysia leo inaongoza kwa kuuza Mawese duniani. Michikichi hiyo ilitoka Kigoma, Tanzania na kupelekwa Malaya na Waingereza miaka ya hamsini.

Tanzania nasi tulikuwa na Shirika la Umma kwa ajili ya Kilimo. Leo tuchukulie Shirika la NARCO. Kama FELDA, NARCO walichukua ardhi kubwa maeneo kadhaa nchini. Tofauti na FELDA wao walilima wenyewe mashamba haya na kuweka miundombinu ya kilimo. Tuchukulie mfano wa Mashamba ya mpunga kule Kapunga, wilaya ya Mbarali mkoa wa Mbeya. Mwaka 1985 NARCO walikwenda kijijini Kapunga kuwaomba wananchi wawape ardhi ya kulima mpunga. Wananchi wakawapa hekta 3000 hivi kwa mujibu wa muhtasari wa mkutano mkuu wa Kijiji nilionyeshwa mwaka 2009 nilipoenda kutembelea mashamba haya kufuatia mgogoro wa ubinafsishaji. NARCO wakapata msaada kutoka Serikali ya Japani na uwekezaji mkubwa ukafanyika ikiwemo kuweka kinu cha kukoboa mpunga cha kisasa kabisa. Hata hivyo NARCO ilijiendesha kwa hasara na ilipofika kati kati ya miaka ya 90 ikaamuriwa kubinafsishwa. NARCO ikauza mashamba yale kupitia Mpango wa ubinafsishaji kwa kampuni binafsi. Katika uuzaji huo NARCO waliuza hekta 3500 badala ya 3000 walizopewa na wananchi. Kwa maana hiyo Kijiji cha Kapunga nacho kiliuzwa!

Mifano hii miwili inaonyesha tofauti kubwa za kifikra kimaendeleo kati ya nchi zetu hizi mbili. Moja iliwezesha wananchi kumiliki ardhi na imefanikiwa. Nyingine iliamua kufanya kupitia Shirika la Umma na baada ya kushindwa, badala ya kurejesha ardhi kwa wananchi na kuwawezesha kulima, ardhi ile ikauzwa kwa kampuni ya mtu mmoja. Mfano wa Kapunga upo pia huko Wilayani Hanang kwenye mashamba ya Ngano ya Basotu nk. Hata kwenye mpango wa SACGOTT bado fikra ni za wakulima wakubwa wenye mashamba makubwa badala ya kuwezesha wananchi kumiliki ardhi na kulima kwa mfumo ambao huduma zitatolewa kwa pamoja. Ujamaa wa Malaysia ulikuwa ni wa kumilikisha wananchi wao ardhi na kuwawezesha kuzalisha. Ujamaa wetu ulikuwa ni wa kumiliki kwa pamoja na hivyo kukosa uwajibikakaji. Badala ya kuboresha tunaona bora kwenda kwa wakulima wakubwa na kugawa ardhi hovyo bila mpango.

Hatuwezi kujifunza kwa wenzetu kweli? Lini tutaacha umazwazwa?

Advertisements

Written by zittokabwe

September 24, 2013 at 10:15 AM

8 Responses

Subscribe to comments with RSS.

 1. Zitto, a good try but i think you ignore the broader issue here. Tanzania adopted Ujamaa, a policy with very specific objectives, and Malaysian didn’t. Also comparing Malaysia with a federal system to Tanzania is like comparing apples and oranges, very unscientific as very different institutions. WaTanzania huwa tunakosea tunapocompore vitu anecdotally wakati hoja kama hii inahitaji utafiti wa kina, yaani iwe PHD thesis with peer review badala ya observations za juu, juu za mwanasiasa. As such, i encourage you to use your contacts at UDSM and get a promising economics student to take this up as a thesis topic. Haya ndio maendeleo mkuu.
  Majaliwa

  Majaliwa

  September 24, 2013 at 10:24 AM

 2. Kwa jinsi viongozi wa Tanzania walivyo, taifa lipo njia panda. Tunhitaji kupata viongozi wenye mawazo na mtazamo tofauti ili kuweza kujinasua. Zito ukiwa Mbunge umeshauri mambo mengi sana yenye manufaa kwa taifa lakini kwa sababu ya watu kuwa na akili mgando wanashindwa hata kuyatekeleza kwa manufaa ya taifa. Tunahitaji muundo wa uongozi wenye fikra mpya tofauti na akina Wasira.

  Simon Nguge

  September 24, 2013 at 5:39 PM

 3. Duh!! Kweli kama ndo hivi, basi maendeleo kkwetu itakuwa ni ndoto MHESHIMIWA!! Endelea kutuelimisha ili tuwaelimishe na wengi kwa pamoja ufanye CHANGES!!

  Samsn Mazengo

  September 25, 2013 at 11:34 AM

  • Naona mh Zito umekuja na ushauri mzito unaonyesha wazi jinsi tulivyo shindwa hii ni kutokana kukoza uzalendo ndani ya nchi hii. Mimi nafikiri usikate tamaa kuendelea kuishauri serikali na wananchi wanaliona jambo unalolifanya, hivyo pia usiache kugombea kofia kubwa zaidi, tuna imani una kitu cha kuwasaidia watnzania.

   Billington Lyimo

   September 27, 2013 at 3:32 AM

 4. Mimi nakushukuru sana Mh. Zitto K.
  kwa ufahamu huu uliotuwekea mezani.

  Binafsi nachukua FURSA ya matumizi ya ARDHI ya hekari nne tu kulima matunda.

  Nitaitafuta hiyo ardhi kwa bidii sana as if ni mdeni wa Shirika fulani.
  NAAMINI nitaipata.
  Then, nitalitendea haki Kwa nguvu zangu zote.

  NAAMINI ULICHOSEMA JUU YA KUFANIKIWA.
  NA NDIVYO ITAKAVYOKUWA KWANGU.
  I’ll tell you.

  BE BLESSED SIR.

  Mr. Cliff Chief.

  September 27, 2013 at 7:45 PM

 5. Mh., tunashukuru kwa makala nzuri yenye takwimu zinazotoa picha halisi ya namna Tanzania ilivyohachwa nyuma. Licha ya baadhi ya mnyambulisho wa takwimu na mantiki kuteleza kidogo, lkn maudhui ya makala hii inasimama kuwa elimu tosha kwa viongozi wenye mamlaka ya kuwavusha Watanzania toka lindi la umasikini.

  Kuteleza kimantiki ninakokuona ni pale makala inapoamua kulinganisha umilikishwaji wa ardhi kati ya Tanzania na Malaysia licha ya utofauti wa aina za siasa zilizofatwa na haya mataifa mawili tangu awali. Pengine msukumo mkubwa umetokana na zao la mawese, lakini kimtazamo, mantiki ya makala ingekuwa bora zaidi kama ulinganifu, kwa misingi ya siasa, ungefanywa kati ya Tanzania na nchi kama China. Ujamaa wa Tanzania ulikuwa wa kumiliki mali za umma kwa pamoja, ambapo zipo ‘success story’. Hivyo, kuweka maudhui inayoelekeza kuwa Tanzania imeshindwa kufikia maendeleo kwa sababu ya siasa za umiliki wa pamoja si sahihi. China wamekuwa na umiliki wa pamoja, na hata wakati Deng Xioping (aliyeruhusu uzalishaji wa mtu mmoja kwenda sambamba na uzalishaji wa pamoja) anaingia madarakani, tayari kulikuwa na maendeleo kwenye sekta ya umma, iliyoendeshwa kwa umiliki wa pamoja, yalikuwa ya kupigiwa mfano.

  Tanzania imeshindwa kuendelea kwa sababu ya ubinafsi hasi wa viongozi, na kamwe sababu haiwezi kuwa siasa za umiliki wa pamoja. Tulikuwa na vyombo vya umma vya kupigiwa mfano, lakini vimekufa kwa sababu za ubinafsi HASI wa viongozi kulikopelekea vifo vya vyombo hivyo. Mfano mzuri na linganifu ni vyama vya ushirika ambayo vilianzishwa kuhakikisha vinaweka miundombinu ya kuwanufaisha wakulima. Tunajua mafanikio yaliyopatikana katika maeneo ambayo vyama viliongozwa vizuri, hivyo jukumu lilikuwa kutumia mafanikio ya sehemu hizo, kama darasa kwa viongozi wa ushirika uliolega. Badala yake, tulipoona tumeshindwa tukakimbia kutafuta mawazo nje na hapo ndipo viongozi wenye ubinafsi HASI walipoiingiza nchi gizani.

  Ni wazi tungeamua kufata misingi ya umiliki wa pamoja na viongozi kutokuwa na ubinafsi hasi, bado tungekuwa tumesimama mahala bora kuliko ilivyo sasa. China wamekwenda na aina hiyo ya umiliki, kiasi kwamba makampuni mengi yanayowekeza nje ya nchi yametokana na umiliki wa aina hii. Kwa mtazamo binafsi ni kwamba, tulishateleza na inabidi tukae chini kuamua tunakwenda mbele kwa staili gani. Tanzania ya leo haifahamiki inafata sera za mlengo upi wa kimaendeleo. Ni kama gari lenye sukani mbili, ambalo kila dereva anayeingia anaamua kuendesha kwa mfumo anaopenda yeye, aidha kulia (RHD) au kushoto (LHD).

  Joseph Cosmas

  September 29, 2013 at 4:14 AM

 6. Nimejifunza mengi kupitia andiko hili. Naona Tanzania tuna nafasi ya kujifunza kupitia Malaya, nchi ambayo ilikuwa katika hali ambayo naona tupo sasa. Tunaweza kufuata mfumo walioutumia ama kuuboresha zaidi kutegemeana na vile tutaona inafaa. Kikubwa katika kutekeleza hili ni kwamba, Serikali ya Tanzania iweke nguvu yake katika kuandaa mashamba na miundo mbinu na baadae kuwapatia wananchi/wazawa walime huku wakiwakata kidogokidogo mpaka gharama za maandalizi zikamilike.
  Wakati mwingine tungeweza kutengeneza mfumo ambapo serikali inawatafutia soko wakulima hawa kwa kutengeneza ghala ambazowakulima hawa watakuwa wanahifadhi na wakati mwingine kuuza mazao yao. Hili linaweza kusaidi nchi kuondokana na shida ya chakula sasa na wakati mwingine kuzuia wananchi kuuza nje ya nchi.
  Kuna mengi ya kujifunza katika hili andiko lakini pia wenzetu wanaosafiri utwa kucha kwenda Malaya, wanashindwa kuja na shauri kama hizi? Ni lini watanzania tutakuwa wazalendo kwa nchi yetu na kutaka maendeleo ya nchi zaidi ya maendeleo binafsi?

 7. Bravo, Zitto umetoa Mada inayoelimisha , lakini pia inyojaribu kufumbua macho kwa wale ambao walikuwa bado mitazamo finyu. Wakati wa Mwl. mwelekeo wetu haukuwa mbaya ila ”Approach” yetu tu ndio labda ilkuwa inahitaji marekebisho madogo ili kupata maendeleo ambayo Mwl. alilenga yawe ya jamii nzima kwa pamoja. Lakini wenzetu wameshatupozea Dira.

  Hongera Bro. Zitto.

  J. Mdeve

  Juma D. Mdeve

  October 10, 2013 at 5:08 PM


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: