Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

UDINI: UCHAFU CHINI YA KAPETI. TUNAJIDANGANYA WASAFI

with 19 comments

Peace. Photo: Dunia Duara

Peace. Photo: Dunia Duara

Mheshimiwa Spika,  nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Wizara hii ambayo ni muhimu sana na ni moja ya Wizara ambazo ni andamizi katika uendeshaji wa Serikali yetu kwa sababu ndiyo Wizara ambayo inasimamia administration of justice. Kwa   hiyo, nafurahi sana kuzungumza leo hii.

Mheshimiwa Spika, nina kitabu cha survey ambayo imefanywa na watu wa REPOA lakini ni kazi ya Serikali na kwa sababu ni kazi ya Serikali, kitabu hicho kinaitwaViews of the People 2007. Kitabu hiki ni sehemu ya shughuli za utekelezaji wa kila mwaka wa Mkakati Wa Kupunguza Umaskini na Kukuza Uchumi yaani MKUKUTA. Katika kitabu hiki, inaonyesha kwamba level ya kutoaminiana mistrusts kati ya Watanzania imefikia 78%, kwa maana ya kwamba katika kila Watanzania 10 ni Watanzania 8 tu ndiyo wanaoaminiana na kuaminika. Kwa hiyo, katika kila Wabunge 10 ndani ya Bunge hili ni Wabunge 2 tu ambao akisimama akizungumza unaweza ukaamini maneno yake, hii ni hali mbaya sana katika taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nimeanza hili kwa sababu ya mjadala ninaouona wa suala la Mahakama ya Kadhi. Mjadala huu ukiangalia tu mtiririko wa watu wanavyochangia, umeligawa Bunge kwa misingi ya dini. Wabunge Waislam wanatoa sababu zao za kwa nini Mahakama ya Kadhi iwepo na Wabunge Wakristo wanatoa sababu zao kwa nini Mahakama ya Kadhi isiwepo na inafikia mpaka kutumia lugha ambazo watu wanaotusikiliza huko nje na wao wanagawanyika.

Mheshimiwa Spika, sasa sisi wengine tumekuta nchi hii ikiwa united, nchi ambayo watu wote tunaishi pamoja na kwa kuangalia level ya ujana, wengine tunaamini tutaishi muda mrefu zaidi ya wengine, kwa hiyo, tusingependa kuona taifa linaparaganyika na wengine tusingependa kuona kwa macho yetu wenyewe na kwa kweli wengine tupo tayari kusimama kuona kwamba taifa hili haligawanyiki.  Mjadala huu unahitaji tolerance ya hali ya juu sana kwa sababu ni mjadala wa imani, mnapoanza kujibizana kwa imani ni kama wengine wanavyosema uvumilivu utaondoka, tunahitaji tolerance ya hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bahati mbaya sana haujaja Muswada, kuna maelezo, kwa wale ambao wanasema kwamba Mahakama ya Kadhi iwepo, ni haki yao kusema kwamba Mahakama ya Kadhi iwepo, tutakuja kukubali au kukataa tutakapoona kwamba Muswada huu unakidhi haja. Lakini majibizano ambayo yanaendelea sasa hivi siyohealth hata kidogo kwa sababu akisimama Mbunge Salum akamjibu Mbunge Paul, Paul na Salum ambao si Wabunge wataendelea kujibizana huko nje.

Mheshimiwa Spika, mimi nadhani tuwe watulivu na tuwe tolerant, tusikilize hoja za kila upande kwa sababu hata baadhi ya lugha ambayo inatumika si nzuri, kwa sababu atasimama mtu atasema wenzetu wanasema hivi, Mheshimiwa Spika ukisema wenzetu kwa mfano Mheshimiwa Godfrey Zambi amesimama anasema wenzetu wanasema hivi maana yake ni kwamba tayari kuna makundi kwamba kuna hawa wenzetu na hawa si wenzetu.

Mheshimiwa Spika, mimi nisingependa tufikie katika hali ya namna hiyo ningependa mjadala huu uwe mpana zaidi, uwe mjadala wa hoja zaidi, tusikilizane, tuangalie imani za kila mtu na tuweze kuona na wala sio kwamba mimi niseme tu kwa sababu limekuwa likizungumzwa, hujibu hoja ya kwamba ni lazima Mahakama ya Kadhi iwepo kwa kusema ikiwepo na hao wengine wataanzisha Mahakama yao, inawezekana hao wengine hawana utaratibu wa aina hiyo. Ndiyo maana ni lazima na ni muhimu sana tuweze kuhakikisha kwamba mjadala wa namna hii hautugawi bali unakuwa ni mjadala ambao ni health vinginevyo hali ilivyo sasa tumehama Bunge la kuwa Bunge la Vyama Vingi tumekuwa Bunge la dini mbili. Maana tumezoea mijadala ni Kambi hii ya Upinzani inapingana na Kambi ya Chama Tawala lakini toka jana naona mjadala ni kambi ya wanaotaka Mahakama ya Kadhi na kambi ya wasiotaka Mahakama ya Kadhi. Mimi nadhani tusubiri hiyo report ambayo Waziri ameizungumzia na ijadiliwe kwa mapana na tusiingie katika lugha ambazo zinaweza zikatufanya kama taifa tuweze kugawanyika. (Makofi)’

Haya ni baadhi ya maneno niliyoyasema tarehe 14 Agosti 2008 wakati nachangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria. Bunge lilikuwa limewaka moto. Wabunge Waislam wakijenga hoja za kiislam kutaka mahakama ya kadhi na wabunge wakristo wakijenga hoja za kikristo kukataa mahakama ya Kadhi. Kulikuwa na Umoja wa Wabunge Waislam na Umoja wa Wabunge wakristo. Wakikaa kwenye vikao na kupanga namna ya kujenga na kupangua hoja. Hali ilikuwa mbaya sana. Nikawatazama Wabunge wazee rafiki zangu na kuwaandikia wasimame kuonya hali ile, hawakusimama. Nikaomba nafasi kusema. Hali ikatulia na nilipotoka Mzee Kingunge Ngombale Mwiru akaniita kunishukuru sana. Mzee Malecela alikuwapo Bungeni lakini akanitumia ujumbe wa kunipongeza kwa maneno yangu yale. Lakini mpasuko wa nchi kwa misingi ya dini bado ni dhahiri kabisa.

Tumeshudia vitendo vya watu kuchukua sharia mkononi na kufanya mauaji dhidi ya watu wengine kwa misingi ya dini zao. Leo Mtanzania mwenzetu Padri Everist Mushi anapumzishwa kwenye nyumba yake ya milele. Ameuwawa kwa kupigwa risasi. Kosa lake nini? Kundi la wahuni wachache limetoa roho ya Mtanzania kwa sababu tu Mtanzania huyu ni Mkristo. Tumeshuhudia mauaji pia kwa sababu ya ugomvi wa kuchinja.

Eti sisi Watanzania leo tunagombana kwa sababu ya kuchinja.

Bora sisi wengine tunakula majani tu na hivyo magomvi haya ya kuchinja, ambayo kwa kweli kwa muda mrefu jamii ilijiwekea utaratibu wake bila kuingiliwa na serikali, hayatusumbui sana. Hata hivyo yanasumbua jamii zetu na ni suala la ibada kwa baadhi ya Watanzania. Kugombana kwa sababu ya kuchinja ni dalili tosha kuwa sasa uzi wa uvumilivu wa kidini uliokuwa umeshika Taifa hili umekatika. Ni kweli umekatika, wala tusishtuke.

Tatizo kubwa Tanzania ni utamaduni wa kuficha uchafu. Majumbani kwetu tunafagia na kuweka uchafu chini ya kapeti na kujidai tu wasafi. Namna hiyo hiyo ndio tunavyoangalia matatizo yetu ya kijamii na hasa kiimani. Nimesema hapo juu kwenye hotuba yangu hiyo ya mwaka 2008, Watanzania hatuaminiani kabisa kabisa. Tunadanganyana sana tunapokutana na tunapoona tatizo cha kwanza tunakimbilia kutafuta ‘jamii gani ya kulaumu’ na kulaumu kwa ujumla. Waislam kadhaa wanasema eti nchi inaendeshwa kwa mfumo kristo hivyo kupendelea wakristo. Wakristo kadhaa wanasema Waislam wanapendelewa na kulindwa na dola. Lakini hawa waislam na wakristo wanaolalamika hawakai kuoanisha hayo malalamiko yao ili kupata suluhisho. Hawataki  kwa sababu pakiwa hakuna ‘tension’ watapata ajenda? Kuna watu wanaishi kwa migogoro tu.

Suala la udini lipo, linakomaa. Badala ya kulitatua kwa kuchukua hatua kali za kisheria kwa watu wote wanaosambaza jumbe za chuki tunabaki kulaumulaumu na kuguguna tu. Udini upo na ni kansa inatula kidogo kidogo. Nitawapa mfano wa udini dhahiri niliyokutana nao kwenye uchaguzi jimboni kwangu mwaka 2010.

Jimbo langu lina vijiji 33. Kuna vijiji viwili vilikuwa vina mvuto tofauti kwangu. Kijiji cha Kagunga kilinipokea vizuri sana mwaka 2005, wakanipa kura nyingi sana (nilishinda kwa tofauti ya kura 600 dhidi ya mpinzani wangu Helimenshi Mayonga). Kwa kweli niliwapenda watu wa Kagunga na kufanya kazi nyingi za maendeleo kule ikiwemo kushawishi miradi mikubwa ya maendeleo kama ujenzi wa bandari, ujenzi wa soko na hata kupeleka umeme na kujenga barabara kuunganisha kijiji hiki na mji wa Kigoma. Kijiji hiki kina wakazi wengi ambao ni waumini wa kikristo.

Kijiji cha Bubango kina waislamu wengi. Mwaka 2005 Kijiji hiki wakazi wake walinikataa kabisa na kuunga mkono mgombea kutoka chama cha CUF kwamba eti ni chama cha Waislamu. Ilifikia wakati nilikuwa wala siwezi kufanya mkutano wa kampeni katika kijiji hiki kwa sababu hawakutaka hata kuniona. Nilishindwa vibaya sana katika kijiji hiki. Kuna vituo vya kupigia kura nilipata kura 4 kati ya kura 280 zilizopigwa. Katika kipindi cha miaka 5 ya ubunge wangu, niliwakasirikia watu wa Bubango na sikwenda kabisa kuwatembelea licha ya kutuma ujumbe wazee kunitaka radhi. Sasa tazama nini kilitokea mwaka 2010?

Siku moja nikiwa katika kampeni kijijini Bubango, nikaitwa msikitini na waumini wakaelekezwa wanipe kura kwa sababu mimi ni mwislamu mwenzao. Sheikh aliyekuwa anatoa mawaidha akasema msijali Zitto hakufanya lolote lile hapa kijijini lakini mpeni kura tu kwa sababu ni Mwislamu mwenzetu. Nikaenda kwenye mkutano wa Hadhara nikawaambia wale watu kuwa sitaki kura zenu kama mnanipa kwa sababu ya uislamu wangu. Nikaondoka. Nilishinda katika kijiji hiki. Nilipewa kura kwa sababu ya uislam wangu.

Ngome yangu ya kampeni ilikuwa Kagunga. Ndipo nilipoweka nguvu zangu maana ninapendwa na nilifanya mambo makubwa. Siku chache kabla ya kampeni, ilikuwa siku ya jumanne nikaitwa kwenda Kagunga kwamba mambo yameharibika sana. Nikataharuki na kupanda boti la kukodi na kwenda Kagunga nikafika saa nne usiku. Wenyeji wangu wakaniambia kuwa wametangaziwa kanisani kwamba Zitto asipewe kura kwa sababu akienda Bungeni ataleta mahakama ya kadhi. Nikaomba kuongea na viongozi wa dini kesho yake asubuhi, wakaja wachungaji 11 (Kagunga kuna makanisa mengi sana). Nikawauliza ni kweli kwamba mimi nisipewe kura kwa sababu ya uislamu wangu? Wakasema hayo ndio maagizo na wameshawaambia waumini. Nikawauliza mnaamini katika hayo? Wachungaji wanne wakasema, mheshimiwa mbunge sisi tupo na wewe. Nikapiga ngoma kuitisha mkutano wa hadhara saa nne asubuhi pale ziwani Kagunga. Nikawaambia watu wa Kagunga, anayetaka kuninyima kura kwa sababu ya uislamu wangu aendelee na uamuzi wake. Nikaorodhesha nini tumefanya Kagunga. Nikasema kama hayo hayatoshi kuwafanya kuchagua mbunge, basi amueni kwa kutumia imani za dini yenu. Nikashuka, nikapanda boti na kuondoka. Matokeo yalipotoka, Kagunga nilishinda kwa tofauti ya kura tisini tu (kutoka kura 600 mwaka 2005).

Toka matukio haya mawili nikasema moyoni mwangu hatuna nchi tena. Viongozi wamekuwa wakitoa kauli za kugawa wananchi. Kiongozi wa CCM kwa mfano anaposema CUF ni chama cha Waislam, anawaambiwa waislam nendeni huko ndio chama chenu. Kiongozi wa CCM anaposema CHADEMA ni chama cha kikristo, anawaambia wakristo nendeni huko ndio chama chenu. Mwanachama wa CHADEMA anapotoa taarifa kuonyesha kuwa CCM inapendelea waislamu, anadhihirisha kuwa kweli chama chake hakipendi waislamu. Viongozi wa kisiasa wanatoa kauli majukwaani bila kuzipima na kugawa wananchi. Baadhi ya taasisi za kidini zimekuwa zikutumiwa na vyama vya siasa kusambaza chuki hizi kwenye jamii.

Mimi ni Mtanzania. Taifa ambalo limejengwa kwenye misingi ya usawa na haki. Misingi ya Umoja na mshikamano. Tunu zetu ni hizo na sio dini zetu. Viongozi wanapoendelea kulea upuuzi huu wa udini Taifa litapasuka vipande vipande. Kwenye masuala ya udini watu hawaweki akili, wanaongozwa na imani. Mijadala inayoendelea sasa inatugawa sana. Lazima tukatae. Tuseme udini sio tunu ya Taifa letu, inaweza kuwa tunu ya mtu binafsi lakini Utanzania wangu ni utu, umoja, uzalendo, uwajibikaji na uadilifu.

Mtu yeyote yule anayepanda mbegu za udini asionewe aibu. Ashughulikiwe haraka sana. Wapuuzi Fulani wanasema kwa kuwa Mkuu wa Polisi ni wa dini Fulani basi ndio maana hachukui hatua. Huyu sio Mkuu wa polisi wa kwanza nchini wa dini hiyo, kuna aliyekuwepo na akaingiza msikitini askari polisi na viatu. Tusiruhusu kabisa upuuzi huu kwamba watu wenye dini Fulani hawachukui hatua dhidi ya watu wa dini zao. Vyombo vya usalama vijue, mtu anayeua ni muuaji tu na lazima achukuliwe hatua kwa uuaji wake. Tena uuaji mbaya unaojenga chuki kwa nchi yetu. Mtu anayetamka maneno ya chuki dhidi ya dini nyingine achukuliwe hatua bila kujali hadhi yake.

Mwisho hatuna namna, ni lazima Taifa liongee. Lazima tuwe na mjadala wa wazi na wa kuheshimiana kuhusu masuala ya udini na kuvumiliana kidini. Hatuwezi kuweka rehani amani ya nchi yetu kwa suala la kuswali au kusali. Badala ya kurushiana lawama, tuzungumze kwa uwazi. Makundi ya wananchi wenye kuona uonevu wa kidini waje waseme kwa uwazi na masuala hayo kujadiliwa kwa uwazi. Muhimu tupate mwafaka na kujenga Taifa imara na lenye mshikamano.

Kwa nchi yenye utajiri wa rasilimali kama yetu udini ni kichocheo tosha cha vita ya wenyewe kwa wenyewe na migogoro isiyokwisha. Ni lazima tuchukue hatua sasa. Tuache unafiki wa kunyoosheana kidole. Kila mtu atazame nafsi yake na aseme ukweli wake kwa uwazi kabisa. Tusifukie uchafu chini ya kapeti.

Advertisements

Written by zittokabwe

February 21, 2013 at 11:33 AM

Posted in Anne Makinda

19 Responses

Subscribe to comments with RSS.

 1. Mhe.natambua juhudi zako za dhati kabisa na kiu ya kutaka mabadiliko katika nchi hii..sina budi kukupongeza na kukuombea kheri na afya stamilivu katika mapambano haya mpaka kieleweke!

  Alphonce Kazimzuri

  February 21, 2013 at 11:52 AM

 2. Kweli kaka tena km mtu anakuwa chanzo apewe onyo kali kwa kuambiwa wewe ndio chanzo cha haya, km utapata muda angali hotuba ya ustadh Ilunga Hasan youtube halafu pima mwenyewe km kweli kiongozi mkubwa wa dini na anaaminika halafu anakuwa mstari wa mbele kuchochea ghasia. All the best brother.

  Amwesiga Mgoha

  February 21, 2013 at 12:05 PM

 3. Hii ni moja ya makala nzuri iliyoshoheni ukweli mtupu wa hali halisi ilivyo hapa nchini.Ni ukweli usiopingingika kuwa wakuu wa nchi wajua hali halisi sababu wana vyombo vilivyowekwa kuwapasha habari sahihi.

  Tuondoe ukimya katika kujenga na uimarisha amani ya nchi hii kwa kuweka mijadala huru ya kusikiliza kero za kila upande tukiwa na lengo na nia ya dhati ya kuzitatua.Vinginevyo jahazi litazidi kutota na tutagawana bao kwa aibu na fedhea mbele ya Mungu.

  habayu

  February 21, 2013 at 12:05 PM

 4. Kama watanzania wa madhehebu yote pamoja na viongozi wa vyama vyote vya siasa pamoja na wale wa serikali watasoma walaka wa Mh ZITTO kwa makini basi hakutakuja tokea vita ya wenyewe kwa wenyewe itakayosababishwa na na udini lakini kwa hali ilivyo walaka wa Zitto umetabili vita huko mbeleni na waasa viongozi hasa wale wa serikali wanaosimamia dora watafakali kwa makini yaliyo andikwa ndani ya walaka huu na wayafanyie kazi.Mfano mzuri ni mauaji ya albino watu wanapelekwa mahakamani mahakama inatenda haki kwa kutoa hukumu ya kifo kwa walio husika cha ajabu albino na watanzania kwa ujumla tunasubiri adhabu itolewe cha ajabu tunaona kimya matokeo yake albino wametoa ujumbe kuwa watahamia ikulu ili kushinikiza serikali itekeleze amri ya mahakama.

  paul c.mhumba

  February 21, 2013 at 12:38 PM

 5. You are one of my heroes

  maisonafricane

  February 21, 2013 at 1:28 PM

 6. Ni kweli kabisa hoja zilizomo ndani ya waraka huu kama zikipata nafasi sahihi katika fikra za watu wetu, na wakikubaliana kuzipokea kwa unyenyekevu, wakaacha kiburi na majivuno ya kujidhania kuwa wao wanajua,hapana shaka maudhui ya waraka huu yatakuwa ni kidonge cha tiba dhidi ya madhaifu na mawazo manyonge yanayotupelekea kuona amani yetu ikitoweka kwa visingizio vya udini. Wasalaam.

  Zephaniah Nyambele

  February 21, 2013 at 2:47 PM

 7. Zito unakili wazi tatizo la udini, unazaliwa hujalikuta, unakuwa pia hujaliona. Sasa unaliona likinyemelea Taifa letu. Hupendi kulipalilia ili liendelee kuwepo. Unaendelea kusema udini ni uchafu chini ya zulia.
  Uchafu?
  Kwa nini dini ifananishwe na uchafu?
  Chini ya zulia?
  Zulia la nani?
  Nani kaweka?
  Kwa nini kaweka?
  Kwa mdhumuni gani?
  Ndugu zangu maswali haya yasipojibiwa, kwa ufasaha, ni ndoto kutatua tatizo la udini. Wote tunakubali kuwa aliyeliunganisha Taifa la Tanzania ni mtu mmoja tu kwa nafasi yake ya uongozi katika Taifa hili. Wadini walikuwepo tangu zama, lakini walikosa mpenyo. Walijaribu kwa makusudi kupenyeza udini wakakemewa, wakatishika, wakanyamaza. Eneo la siasa ni eneo analoweza kuingia mtu yeyote, hata mwendawazimu. Nyerere aliwahi kusema’ kuna siku tunaweza tukampata Raisi kichaa. Akaitumia vibaya Katiba ya nchi’. Leo yametukuta. Nyerere pia aliwahi kusema ‘ Amani sio kitu cha kuchezea. Msidhani mataifa mengine wanayopigana wenyewe kwa wenyewe ni watu wa tofauti sana! Hapana ni sawa tu na watanzania. Watanzania amani ikiondoka watapigana sawa tu na Warundi.’ Akafananisha amani na mtu uliopandwa, unaostahili kumwagiliwa maji kila siku ili uzidi kukua.
  Sasa hivi wanaopaswa kumwagilia, wanauong’oa, wanakung’uta udongo, wanauanika ili ukauke.
  Raisi anayepatikana kwa rushwa,akiingia atataka arudishiwe kwanza hela zake alizotoa kwa njia ya rushwa wakati wa kampeni. Hawezi kununua watu kabla yeye hajanunuliwa. Pia anayeingia kwa misingi ya udini kwa uwazi au kwa kificho hawezi kukemea udini hadharani kwa kuwa anaofanya nao udini kifichoni watamsuta.
  Watamsuta wakisema ‘Unatuambia udini wewe?’

  Kuna watumishi wa usalama wa Taifa walionyesha wasiwasi wao kuwa, raisi asipofuata misingi ya usalama wa Taifa, Tasisi ya Usalama wa Taifa haiwezi kufanya kazi kitaaluma. Wengine wakajiuzulu.
  Zulia ni nini na ni nani?

  asungwile

  February 21, 2013 at 3:10 PM

 8. MIMI binafsi naomba nikusifu ndugu yangu Zito, kilichokusukuma kuandika makala hiyo ni uzalendo wa nchi yako wala si dini yako, mm ni mkristu naomba nikuombe radhi kuwa sikuipigia cdm 2005 ambayo wewe pamoja na Mbowe ambaye ni mkristu ndio chama chenu, nilimchagua Kikwete ambaye ni muislam kwa kuwa niliamini ataisaidia TZ. 2010 sikuweza kumpigia kwa sababu ya kushindwa kuniletea maisha bora aliyoyaahidi na juhudi zenu vyama vya upinzani zaidi CDM (ukiwa wewe mwenyewe, Slaa na Mdee) mkiitumia nafasi ya uchache wenu kuleta mabadiliko ya kifikra ndani ya bunge la Tz. Ktk kufanya hivyo nikajikuta niko ndani ya dimbwi la kidini! Tatizo liko hapa mimi napenda nimchague mtu mwenye sifa njema kwa taifa, lkn wakristu tukimchagua muislam, waislam wanasema hilo sio chaguo letu kiasi cha huyo kiongozi kuchukiwa na waislam wenzie. Hata waislam wenye mlengo mkali wa dini wakiisoma makala yako ninahisi watakujibu kwa namna ulivoiandika. Kibaya zaidi mm rafiki zangu wengi ni waislam, kwa bahati mbaya mambo haya yalivyojitokeza mahusiano yetu si kama huko nyuma. Kama hoja hiyo binafsi utaisoma bungeni nitakusifu zaidi. Tatizo letu sisi wakristu na waislam tumewasahau watu wasio na dini kama Kingunge, wenye majina yenye kusadifu dini kumbe si waumini. Mm niko pamoja na wewe tushirikiane kujenga taifa. Ahsante!!!!

  GWAKISA

  February 21, 2013 at 3:42 PM

 9. Nikweli uyasemayo mheshimiwa Zitto, but watanzania wengi wanaangalia sana image ya viongozi wao! ( gate keepers ) please speak for!

  Justin Silas

  February 21, 2013 at 4:24 PM

 10. Kaka Zitto Mimi ni mmoja wa vijana ambao nipo CHADEMA lakini nakuelewa sana unapotoa hoja zako. Nimekuwa mtafakuri mzuri sana pale ninaposoma makala zako. hakika unakipaji kikubwa sana na mara nyingi nawaambia vijana wenzangu, wewe huna haiba za kupendwa hovyohovyo ila unapendwa na watu makini na wanaopenda kusikiliza na kujua ukweli, hutoi kauli katika ombwe la bongo yako bali wewe ni mdadisi na mpenda kujifunza, hakika darasa la leo limekuwa chakula bora katika fikra zangu. wewe mara nyingi huzungumza kifalsafa, Mungu akupe maisha marefu.

  Philemon Mtoi

  February 22, 2013 at 12:53 PM

 11. chanzo cha udini kwani ni nini au nani? Tanzania?

 12. Nachoweza kusema kwa dhati kabisa ni kwamba muheshimiwa zitto kabwe ukithubutu kugombea urais basi kura yangu halali yako.

  Abdallah Zatty

  February 22, 2013 at 11:39 PM

 13. Lakini pia chokochoko hizi za kidini zinachochewa kwa kiasi kikubwa na watanzania wasiojua matumizi mema ya mitandao ya kijamii.Kuna watu wamefungua facebook ama twitter accounts kwa minajili ya kushadadia masuala ya dini.Malumbano,matusi na majibizano yasiyo ya msingi yametawala sana katika kurasa hizo.Wako waliofungua blogs kwa minajili hiyohiyo.KWELI MAENDELEO HUJA NA MAMBO LEO.Hatuna budi wakristo na waislamu wenye mapenzi mema na nchi yetu kufunga kwa maombi kuliombea taifa letu.

  Erick Machua

  February 24, 2013 at 6:00 PM

 14. HONGERAA! MH. ZITTO, Ni kauli nzito inayopaswa kutiliwa maanani na kila MTANZANIA ambae anaitakia kheri nchi yetu. Tupime kauli zetu kabla ya kuzungumza tusiwe kama mchangiaji ASENGWILE, yy badala ya kukemea anaanza kunyoosheana vidole, huu c wakati muafak

  YUSUPH A. MKWAYU,

  February 26, 2013 at 12:25 AM

 15. Muheshimiwa zito

  Mimi naunga mkono ka kiasi kikubwa maelezo uliyoyatoa kuhusu suala la udini na mustakabali wa taifa letu. Ila naomba nikukosoe kidogo pale ulipoteleza na kuchochea udini ule ule tunaouchukia, kwa kusema kwamba

  “Tumeshudia vitendo vya watu kuchukua sharia mkononi na kufanya mauaji dhidi ya watu wengine kwa misingi ya dini zao. Leo Mtanzania mwenzetu Padri Everist Mushi anapumzishwa kwenye nyumba yake ya milele. Ameuwawa kwa kupigwa risasi. Kosa lake nini? Kundi la wahuni wachache limetoa roho ya Mtanzania kwa sababu tu Mtanzania huyu ni Mkristo”.

  Je wewe umejuaje kwamba Padre Mushi aliuliwa kwasababu ya ukristo wake? Hapana shaka Padre alikuwa mkristo lakini sababu za kuuwawa kwake wanazijua wauwaji (na labda yeye marehemu). Nafikiri kabla kukamilika kwa uchunguzi tusije kufikia hitimisho la namna hii kwa kadhia hii na nyengine, mpaka pale tutakapokuwa na ushahidi kamili.

  Tumuombe mungu atulinde na mgawanyiko huu usizidi kutuumiza, na sote tuwe waadilifu wa kweli tusiuendekeze an tuukemee udini kwa namna yoyote ile.

  Abdalla Said

  March 1, 2013 at 12:00 AM

 16. naomba kutoa pendekezo moja kuwa: waislam wote waishio tz bara wahamie zenj na wakristo wote waishio zenj wahamie bara maana waislaw ni wagomvi sijui wana wivu kutokana na idadi yao ndogo,hata wakristo wakiamua kuwapiga watakwisha kwa dk moja

  musa kulwa

  March 19, 2013 at 9:26 PM

 17. […] aseme ukweli wake kwa uwazi kabisa. Tusifukie uchafu chini ya kapeti. extract from his article UDINI: UCHAFU CHINI YA KAPETI. TUNAJIDANGANYA WASAFI | Zitto na Demokrasia Great spirits have always encountered violent opposition from mediocre minds Albert Einstein […]

 18. Broo ZZ Kabwa co cr unadeserve hiyo nafac uliyo nayo wala hukuptshwa kwa pesa.

  jasam

  May 8, 2013 at 11:30 AM

 19. viongozi wote wangekua km ZZ Kabwe wenye uzalendo na nchi yao nadhan tungefika mbali japo kila mmoja atachukulia kwa mtazamo wake coz true dat agent wa udini ni govt ktk maamuzi yake, cc wananchi kwani huku street mbaka sasa tunaishi kwa amani baina ya dini zote tunashirikiana ktk raha na shida cristians wamepanga kwenye majumba ya muslims n muslims wamepanga kwenye majumba ya cristians na hata kuoleana baina ya dini zote dat meens hatujafikia kitaani kubaguana kiukwel hivyo viongoz, govt, na taacc zote za dini tuangalie kwa makini UFA uooo.. tusije tukashindwa kuuziba BUT mbona cmpo tu Govt jaman kama jumuiya za kidin zipo kisheria kwa kutambua serikari haina dini bt raia wake wanadini bas mcpende kuwaingilia ktk mambo yao km hakuna uvunjifu wa sheria eg km alivyo sema mh ZZK waislam wenyewe hawataki bakwata nyie mnawalazimisha kwa nn? waachien wenyewe waunde jumuiya wanayoitaka nyie km govt mletew habal kwmba jumiya hiyo na kiongoz ni huyo km kuna ulazima lkn huko kulazmishana ndio kuonekana kunaleta mambo km hayo kwan hii ni sawa na casa wananch wanamtaka mbunge fulan nyie mnalazimisha mbunge fulan mnaemtaka nyie ni kutokana na pesa zenu pamoja na interest zenu binafc end of the day vuruguUUUU, iz not fair jaman hii n nchi huru kila mmoja anauhuru wa kumchagua amtakayee WAKRISTO wakiamua kufanya yao pasipo uvunjifu wa sheria au waislam wameamua kufanya yao pocpo uvunjif wa sheria waachen MCWARAZIMISHE MTAKAYO NINYI. Leo hii kiongoz wa waislam akifanyiwa ualifu moja kwa moja hica za majibu ya takwenda kuwa ni mkristo kafanya hivyo na kiongoz wa wakristo akifanyiwa uhalifu bac moja kwa moja hica ni waislam wamefanya hivyo TUACHE HIYOO DHANA JAMANIIIII kwani huo ndio UFA wenyewe watu wanapenya kufanya yao kwa faida zao kwa kujua mwanvuli wa kujfichia ni UDINI upo. GOVT, VIONGOZI BALANCE KTK DINI ZOTE BILA KUJAL UCHACHE WA WAUMINI NI MUHIM SANA NAAMINI 100% MKIZINGATIA YA ZITO KABWE HILI SWALAAA LITAISHA LKN KM MKITAKA YENU NDIO YAFANYIKE NYIE KM GOVT. BASI UFA UTAKUA MLANGO. NI HAYO TU………

  jasam

  May 8, 2013 at 12:23 PM


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: