Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Mafuta kuwa suala la Muungano tulikosea

with 17 comments

 • Kila upande wa Muungano uchimbe Mafuta na Gesi Asili yake na Mapato yawe ya Serikali ya upande husika.
 • Shughuli za Utafutaji kwenye vitalu vyenye mgogoro ziendelee mara moja
 • Zanzibar ianzishe Shirika lake la Mafuta (PetroZan)
 • Katiba mpya itofautishe utafutaji (upstream) na Biashara (uchimbaji, midstream na downstream)

Moja ya suala linalosubiriwa kwa hamu kubwa katika mjadala na hatimaye uandishi wa Katiba mpya ni suala la Mafuta na Gesi Asilia kuwa jambo la Muungano au liondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano. Suala hili limezusha mjadala mkubwa sana mara kwa mara nchini Tanzania kiasi cha lenyewe kuwa ni hoja ya wale wasiotaka tuwe na Dola ya Jamhuri ya Muungano Tanzania.

Wakati Muungano unaanzishwa mwaka 1964 Mafuta na Gesi hayakuwa masuala ya Muungano. Nimeangalia katika Hati ya Muungano ambayo ilikuwa ni sehemu ya Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1965, suala hili halikuwamo katika orodha ya mambo Kumi na Moja ya Muungano. Nyaraka nilizoziona zinaonyesha kwamba suala la Mafuta na Gesi Asilia liliongezwa katika orodha ya Mambo ya Muungano mwaka 1968. Kuna watu wanahoji kihalali kabisa kwamba nyongeza ya jambo hili ilifanywa bila kufuata taratibu na hivyo kufanywa kinyemela na kuna wengine wanasema jambo hili lilifuata taratibu zote za kisheria ikiwemo kupigiwa kura na Bunge la Muungano na kuungwa mkono na theluthi mbili ya Wabunge kutoka pande zote za Muungano.

Katika moja ya vikao vya Bunge katika Bunge la Tisa, aliyekuwa Naibu wa Waziri wa Nishati na Madini Ndugu Adam Malima alileta kumbukumbu za mjadala Bungeni (Hansard) za mjadala wa suala la Mafuta na Gesi ili kuthibitisha kwamba jambo hili halikuuingizwa kwenye Katiba kinyemela.

Wakati umefika kwa Watafiti wa Masuala ya Muungano wakapekua nyaraka hizi na kutwambia ukweli ulio ukweli mtupu wa namna suala la Mafuta na Gesi lilivyoingizwa katika orodha ya mambo ya Muungano. Hata hivyo, jambo hili sasa ni jambo la Muungano kwa mujibu wa Katiba na ni dhahiri kuwa WaTanzania wa Zanzibar hawafurahiswhi nalo na hivyo kuazimia kupitia Azimio la Baraza la Wawakilishi kwamba jambo hili liondolewe kwenye orodha ya masuala ya Muungano. Kwa vyovote vile Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapaswa kutoa uamuzi wa mwisho utakaomaliza mjadala huu.

Jambo la kusikitisha ni kwamba licha ya Bunge la Muungano kuamua kuongeza suala la Mafuta na Gesi asilia katika masuala ya Muungano, mwaka mmoja baada ya uamuzi huo likaundwa Shirika la Maendeleo ya Mafuta Tanzania (TPDC) kwa amri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano (establishment order). Shirika hili halikuanzishwa kwa Sheria ya Bunge au kwa Sheria ya Makampuni kama yalivyo Mashirika mengi ya Umma hapa nchini bali kwa amri ya Rais ya mwaka 1960. Katika amri hii ya Rais, Shirika la TPDC halikupewa ‘mandate’ ya kimuungano. Shirika hili mipaka yake ilianishwa kuwa ni Tanzania bara peke yake. Hivyo suala la Muungano likawekewa Shirika la Tanganyika kulisimamia!

Kama ilikuwa ni bahati mbaya au makusudi au kupitiwa kwa viongozi wetu wa wakati huo ni vigumu kujua lakini huu ni mkanganyiko mkubwa ambao ulipaswa kurekebishwa mapema sana.

Shirika la TPDC limekuwa likifanya kazi ya kusimamia Sekta ya Mafuta na Gesi ikiwemo kutoa vibali vya kutafuta mafuta, kuingia mikataba na Makampuni ya kimataifa na kuisimamia mikataba hiyo. Miongoni mwa mikataba hiyo ni kwenye maeneo ambayo kama isingekuwa Muungano yangekuwa ni Maeneo ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Mbaya zaidi Mikataba yote ya utafutaji na uchimbaji Mafuta inafanywa inaingiwa na Waziri wa Nishati na Madini Wizara ambayo sio ya Muungano. Hakuna hata eneo moja ambalo taratibu zimewekwa kwamba pale ambapo eneo hilo ni eneo lilikuwa chini ya himaya ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar basi mikataba isainiwe na Mawaziri wawili wa sekta hiyo kutoka kila upande wa Muungano.

Ni dhahiri kwamba kama ni kusahau hapa kulikuwa na kusahau kukubwa ambako hakustahmiliki kwa mtu yeyote mwenye upeo achilia mbali mwananchi wa kawaida wa Zanzibar ambaye anaona anaonewa na kugandamizwa na Bara.

Mnamo miaka ya mwanzo ya 2000, Shirika la TPDC liliingia mikataba ya Vitalu kadhaa vya Mafuta miongoni vya vitalu hivyo ni vitalu nambari 9, 10, 11 na 12 mashariki ya visiwa vya Pemba na Unguja. Vile vile Shirika na Wizara ya Nishati waliingia mkataba mwingine katika Kitalu kilichopo kati ya Pemba na Tanga (mahala ambapo kumekuwa na dalili za wazi za kuwapo Mafuta kutokana na kuonekana kwa ‘Oil sips’ mara kwa mara.

Vitalu 9, 10, 11 na 12 vilipewa kampuni ya Shell ya Uholanzi na kitalu cha kati ya Tanga na Pemba walipewa Kampuni ya Antrim ya Canada ambayo baadaye waliuza sehemu ya Kampuni yao kwa Kampuni ya RAK Gas kutoka Ras Al Khaimah huko United Aarab Emirates. Kwa kuwa Vitalu hivi vipo katika eneo la iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kabla ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilikataa shughuli zozote kufanyika mpaka suala la Mafuta na Gesi kuondolewa katika orodha ya Mambo ya Muungano lipatiwe ufumbuzi.

Uamuzi huu wa Serikali ya Zanzibar ni uamuzi ambao ungechukuliwa na Serikali yeyote ile yenye mapenzi ya dhati na watu wake. Uamuzi huu ulileta mjadala mpana sana katika masuala ya Muungano na ambao hawana taarifa waliubeza sana. Hata hivyo suala hili likafanywa ajenda katika vikao vya masuala ya Muungano vinavyoitwa Vikao vya Kero za Muungano. Miaka kumi suala hili linajadiliwa na Maamuzi hayafanyiki! Hivi sasa kila suala lenye kuangukia kwenye Katiba husukumwa huko na hivyo kutoa ahueni kwa wanaogopa kufanya maamuzi.

Katika medani za uchumi kila suala lina muda wake. Masuala ya utafutaji wa Mafuta ni masuala yanayoongozwa na msimu na kuendelea kuchelewa kufanya maamuzi juu ya suala hili kunalitia hasara Taifa, Hasara ya Mabilioni ya Fedha na hasara kubwa zaidi ya kufahamu utajiri uliojificha chini ya Maji ya Bahari inayozunguka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivi sasa Pwani ya Afrika Mashariki inarindima (trending) katika utafutaji wa Mafuta na Gesi asilia. Huko Msumbiji Makampuni mbalimbali yamegundua Gesi asilia nyingi inayofikia zaidi ya futi za ujazo trillion 107 (107TCF) kwa makadirio ya chini. Hapa Tanzania utajiri wa Gesi asilia uliogunduliwa hadi hivi sasa na kutangazwa umefikia futi za ujazo trillion 20 (20TCF) ambazo ni sawa na utajiri wa thamani ya dola za kimarekani trillion 6. Makadirio yanakisiwa kuwa Tanzania kuna  futi za ujazo trillioni 85 (85TCF) za Gesi Asilia katika eneo la Kusini kuanzia vitalu namba 1 mpaka namba 5 ikiwemo vitalu vya nchi kavu na vile vya Songosongo.

Iwapo kasi ya utafutaji mafuta itaendelea kama sasa katika kipindi cha miaka 2 ijayo Tanzania itaweza kuwa kati ya nchi mbili za Afrika zenye Utajiri mwingi zaidi wa Gesi Asilia. Hivi sasa Nigeria ndio inaongoza kwa kuwa na futi za ujazo trillion 189 (189TCF) ikifuatiwa na Algeria na Angola ambazo zote zina utajiri wa juu kidogo ya 100TCF kwa Algeria na chini ya 100TCF kwa Angola. Msumbiji sasa imeifikia Algeria na kushika nafasi ya pili.

Katika masuala ya Mafuta na Gesi hatua ya kwanza ni kujua kama utajiri huu ambayo kitaalamu inaitwa gas exploration. Shughuli za utafutaji zinapandisha sana thamani ya nchi na eneo la nchi. Kwa mfano hivi sasa kitendo cha Kampuni ya Uingereza ya BG/Ophir na ile ya Norway ya StatOil kupata mafanikio makubwa katika utafutaji wa Gesi asilia kumeongeza thamani ya Pwani ya kusini ya Tanzania katika medani za utafutaji (Exploration Activities).

Hata hivyo kama ilivyogusiwa hapo juu, shughuli za Utafutaji ni shughuli za msimu. Pia huchukua muda mrefu wa kati ya miaka 5 mpaka 10 kati ya kutafuta, kupata na kuanza kuchimba. Hivi sasa ni muda wa pwani ya Afrika Mashariki. Ni lazima kuhakikisha kwamba vitalu vyote vilivyogawiwa hivi sasa vinafanyiwa kazi. Hata hivyo vitalu vingine vyovyote visigawiwe kwanza mpaka hapo matunda ya vitalu vya sasa yaonekane. Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imependekeza kusimamisha kugawa vitalu vipya. Matokeo ya utafutaji katika vitalu vya sasa yakiwa mazuri kama ilivyo sasa, thamani ya vitalu vipya itapanda sana na nchi itakuwa na nguvu ya majadiliano (strong negotiation position) dhidi ya makampuni makubwa ya mafuta. 

Tufanyaje kuhusu vitalu vilivyogawiwa katika eneo ambalo lina mgogoro kuhusu suala la Muungano? Sio kazi rahisi lakini imefikia wakati tuamue. Kwa kadri nionavyo, Itabidi kuwe na maamuzi ya mpito (interim decisions) na maamuzi ya muda mrefu.

Kwanza, ni lazima kukiri tulipokosea. Hata kama ilikuwa ni sahihi kiutaratibu kuweka suala la mafuta na Gesi katika orodha ya mambo ya Muungano, haikuwa halali Shirika la TPDC lenye mipaka ndani ya Tanzania bara kuingilia ugawaji wa vitalu na kuingia mikataba katika maeneo ambayo ni ya Muungano. Ni Taasisi ya Muungano tu ndio inaweza kushughulikia suala la Muungano na sio vinginevyo.

Ilikuwa ni dharau kubwa sana kwa Waziri wa Nishati ambayo sio Wizara ya Muungano kuingia Mikataba katika eneo la Zanzibar (ambapo kikatiba tumelifanya eneo la Muungano) bila kushauriana na kukubaliana na Waziri wa Nishati wa Zanzibar. Kukiri kosa sio unyonge, ni uungwana. Hata tukifanya vikao milioni moja chini ya Makamu wa Rais, bila kukiri kosa hili tatizo hili na mengine ya aina hii hayataisha.

Pili, ni vema kukubali kwamba shughuli za utafutaji katika vitalu vyenye mgogoro ziendelee kwenye hatua ya utafutaji tu. Kama mafuta au Gesi ikipatikana, uchimbaji usianze mpaka uamuzi wa mwisho kuhusu suala hili uwe umepatikana. Pia ninapendekeza ufumbuzi wa mwisho hapa chini. Kuchelewesha utafutaji ni hasara kwa pande zote za Muungano kutokana na taarifa za kijiolojia zitakazopatikana na hivyo kupandisha thamani ya nchi hizi mbili kijiolojia.

Hata hivyo, utafutaji huu katika eneo lenye mgogoro kati ya pande mbili za Muungano ufanyike baada ya mkataba wa PSA kufanyiwa marekebisho makubwa. Marekebisho hayo ni pamoja na Mkataba kusema wazi kwamba shughuli za uchimbaji zitafanyika iwapo tu makubaliano ya kugawana mapato ya Mafuta na Gesi kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar yamefikiwa. Pia Mkataba uzingatie maendeleo ya sasa ya kusini mwa Tanzania na hivyo mkataba uboreshwe kwa faida ya nchi ikiwemo kutolewa kwa ‘signature bonus’. Hii ni Fedha inayotolewa na Kampuni za utafutaji Mafuta kwa Serikali kabla ya utafutaji kuanza. Kiwango hutokana na majadiliano na kukubaliana. Nchi zenye jiolojia iliyopevuka hutumia njia hii kuongeza mapato ya Serikali.

Mkataba pia useme kinaga ubaga kwamba utasainiwa na Mawaziri wa pande mbili za Muungano na kwamba Kampuni inayofanya utafiti itatoa taarifa zake za Utafiti sawia kwa Mawaziri wote kwa mujibu wa vipengele vya mkataba.

Kwa upande wa maamuzi ya muda mrefu, ushauri wangu ni kwamba; kwa maana ya kuandikwa kwenye Katiba mpya ni kwamba Suala la Mafuta na Gesi Asilia liendelee kuwa suala la Muungano kwenye eneo la usimamizi wa Tasnia na leseni za utafutaji (Upstream Regulatory mechanism). Hili ni eneo linalohitaji usimamizi wa dhati kabisa na kwa pamoja pande mbili za Muungano zinaweza kufanya vizuri zaidi.

Eneo la Uchimbaji na hasa kugawana mapato ya mafuta na Gesi (Profit Oil) lisimamiwe na kila upande wa Muungano kivyake. Biashara ya Mafuta isiwe jambo la Muungano na hivyo kila Upande wa Muungano uwe na Shirika lake la Mafuta na Gesi ambalo litashiriki kama mbia wa Mashirika ya Kimataifa katika uchimbaji, usafirishaji na uuzaji wa Mafuta na Gesi Asilia. Mapato yanayotokana na Mafuta (Profit Oil) na kodi nyingine zote isipokuwa mrahaba (royalty) yawe ni masuala yanayoshughulikiwa na Serikali ya kila upande wa Muungano kwa mujibu wa Sheria ambayo Serikali hizo zimejiwekea.

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma ilipendekeza Bungeni kwamba kuwepo na Mamlaka ya Mafuta na Gesi Asilia Tanzania (Tanzania Petroleum Authority) ambayo itakuwa ni msimamizi (upstream regulator) kama suala la Muungano. Mrahaba wa Mafuta na Gesi ambao sasa ni asilimia 12 ya Mapato ya Mafuta itakusanywa na Msimamizi huyu na ndio mapato pekee katika tasnia ya Mafuta na Gesi yanapaswa kuwa mapato ya Serikali ya Muungano.

Kamati pia ilipendekeza kuanzishwa kwa Shirika la Mafuta na Gesi (Petroleum Tanzania – PetroTan) ambalo litakuwa mbia kwenye Makampuni ya utafutaji na uchimbaji wa Mafuta na Gesi kwenye Vitalu vya Tanzania bara. Mapato yote ya vitalu vya Tanzania bara na kodi zote isipokuwa Mrahaba zitakwenda kwa Mamlaka za bara tutakazo kuwa tumeamua baada ya Katiba mpya kuanza kazi. Hivi sasa TPDC inafanya kazi hii mpaka Zanzibar jambo ambalo hata kwa akili ya kawaida halipaswi kukubalika.

Aidha, napendekeza kwamba Zanzibar ianzishe Shirika lake la Mafuta sasa. Jambo hili halina haja ya kusubiri vikao vya kero za Muungano kwani ni dhahiri TPDC haina mamlaka,ushawishi na uthubutu kusema uhalali wa kusimamia vitalu vya Mafuta vilivyopo  Zanzibar.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipeleke muswada katika Baraza la Wawakilishi kuanzisha Shirika la Mafuta na Gesi la Zanzibar (Petroleum Corporation of Zanzibar – PetroZan) ili liweze kushiriki katika utafutaji na uchimbaji wa Mafuta Zanzibar. Lakini Pia PetroZan ilinde maslahi ya Zanzibar katika tasnia hii kwa kujijengea uwezo wa kusimamia ugawaji bora wa Mapato kutoka katika Mafuta na Gesi Asilia.

Kama Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inachelea kuanzishwa kwa Shirika hili, Wawakilishi wa pande zote (CCM na CUF) wapeleke muswada binafsi kuunda Shirika la Mafuta la Wazanzibari. Hawatakuwa wamevunja Katiba ya Muungano kwani hivi sasa hakuna Taasisi yenye mamlaka ya kusimamia Tasnia hii kwa Upande wa Zanzibar.

Wakati haya yote yanafanyika, shughuli za utafutaji Mafuta na Gesi katika vitalu vilivyopo katika eneo la Zanzibar na hasa vitalu namba 9,10,11 na 12 na katika kitalu cha kati ya Pemba na Tanga ziendelee kufuatia marekebisho ya Mkataba wa Utafutaji. Utafutaji wa Mafuta una faida zaidi kwa Nchi hizi mbili kuliko kwa Kampuni za Mafuta kwani uwekezaji wa Kampuni pekee na nchi zitapata taarifa za kijiolojia zitakazosaidia mikataba ya baadaye kuwa bora zaidi.

Wakati nasisitiza kwamba tuendelee na utafutaji katika vitalu tajwa, katika Katiba mpya, utafutaji wa mafuta usimamiwe na Taasisi ya Muungano. Uchimbaji na biashara ya Mafuta ufanywe na kila Serikali ya kila upande wa Muungano. Mafuta kuwa jambo la Muungano halafu kusimamiwa na Shirika la Tanganyika na Wizara ya Upande mmoja ya Muungano ndio chanzo cha mgogoro. Suluhisho sio kuifanya TPDC kuwa Shirika la Muungano, bali kila upande upewe uhuru wa kusimamia uchimbaji, Biashara na mlolongo mzima wa tasnia ya Mafuta (value chain from midstream to downstream) isipokuwa utafutaji (upstream). Hili ndio suluhisho la kudumu ninaloona linafaa. 

Uwazi (declaration):

Zitto Kabwe ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na mfuatiliaji wa karibu wa Tasnia ya Mafuta na Gesi Asilia akiwa amesomea mfumo wa uchumi wa katika tasnia ya madini na mafuta (fiscal regime in Mineral and Petroleum sector).  Zitto pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma ambayo inasimamia mahesabu na utendaji wa Shirika la TPDC. Makala hii imeandikwa baada ya ziara ya Mafunzo ya Wabunge kutembelea nchi ya Uholanzi kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo. Katika ziara hiyo Wabunge hao walikutana na Wakuu wa Shirika la Mafuta la Shell ambapo walizungumzia pia suala la vitalu namba 9, 10, 11 na 12.

17 Responses

Subscribe to comments with RSS.

 1. Tulishirikiana umememe iweje mafuta yawe pande tofauti, muhimu tusinyimane matumizi wala mapato , we need symbiotic union

  Tumaini Geofrey Temu

  May 27, 2012 at 11:46 AM

  • wewe hujui kitu kwn nyinyi mnataka mufaidike nyinyi tu mbona hio migodi na mazao yote yabiashara ni ya kwenupekeyenu????? muungano unapaswa kurekebishwa venginevo utaleta mpasuko mkubwa kwaniwazanzibari wa sasa wako macho!!

   ali saleh

   June 13, 2012 at 11:47 PM

 2. Nikweli mh…..right regards

  Dicley mlelwa

  May 27, 2012 at 11:48 AM

 3. Nakupongeza miongoni mwa watanzania wachache wanaoweza kusimama na kutetea haki za watanzania wengine bila ya kujali sehemu gani ambayo unatokea na majibu yanajieleza lakini pia ningependa kueleza pamoja na Serikali ya Tanzania kushindwa kutoa maamuzi kwa zaidi ya miaka 10 suala la mafuta kwa upande wa Zanzibar na Tanganyika lakini pia Serikali yeneywe ya Tanzania imeshindwa kuzisimamia raslimali zake na kuzitupa ovyo kwa wawekezaji wa kigeni mfano mzuri ni sekta ya madini, sasa unapong’anga’nia kuyataka mafuta yaliyopo Zanzibar na mwanao mwenyewe unamgawa bila ya uchungu ni kweli utaweza kumlea wa jirani yako. Tanzania bara imeshindwa kabisa kusimamia raslimali zake na haistahili kabisa kusimamia za wenzake

  Ahmed Juma

  May 27, 2012 at 11:49 AM

 4. nimeyakubali maoni yako.

  hakika wewe ni Mtanzania si Mtanganyika.

  naomba unisaidie kitu kimoja tu maana uelewa wangu ni mdogo…..KWA NINI MRAHABA(ROYALTY) UHUSISHWE AU UPELEKWE KTK MUUNGANO? NA MRAHABA NI NINI?

  joseph chakupewa

  May 27, 2012 at 12:01 PM

 5. Nini yalikuwa madhumuni ya mafuta kuwa ni ya Muungano? Siasa za kutaka kura au kuulinda Muungano?.kwanini mafuta yasiwe ya Muungano?

  Membe

  May 27, 2012 at 12:42 PM

 6. Nafurahi sana kuwa karibu sana nawe Mh.kila siku nikisoma vitu vyako huwa unanipanua kichwa changu nakujiona nakuwa sasa.Ni kweli ukiangalia kwa makini khsu swala la mafuta na gas Zanzibar tunawaburuza kibabe tu.huu mfumo uangaliwe upya,na kama tunashindwa kwenda sawa kwa sawa basi kila mtu achimbe yake na mikataba yake.Zanzibar tumeungana nao na sio koloni letu.

  Hancy Abby Machemba

  May 27, 2012 at 1:35 PM

 7. Mh. Zitto mimi binafsi nakubaliana na hoja hii kwa asilimia zote.Tatizo nililoliona hapa ni watawala kuhitaji kufanya kila kitu kuwa cha siri!wakati hizo watu wakizifuatilia/ama kufahamu inaonekana kwamba kuna kitu nyuma ya pazia.Naamini tangia umekuwa Mbunge hadi leo ni mda mrefu na nafikri ndiyo kwanza unalipata jambo hili,kwa kifupi jambo hili limechangia kiasi kikubwa mpasuko wa Muungano wetu ili hali kumbe jambo liko wazi.Najua uko safarini pindi ukirudi ni vema kuliweka wazi kwa Watanzania walielewe ili kuondoa mkanganyiko unao pelekea kuona Wazanzibar ni wabinafsi kumbe wako sahihi kudai mafuta yao yasiwe ya muungano.Katika kukanganyika huko naomba kufamu Je?Wizara ya Afya ni ya Mungano?na ni sahihi Mbunge kutoka Zanzibar aliye pigiwa kura Zanzibar na kuwakirisha Wazanzibar kuteuliwa kuongoza Wizara hiyo Bara?Nakutakia shughuri njema huko na urudi salama Nyumbani.

  Emmanuel Messo

  May 27, 2012 at 2:37 PM

 8. Shukran sana Mh Zitto kwa uchambuzi uliojaa umakini,ukweli na uzalendo wa Mtanzania halisi.

  mimi nina mambo mawili ningependa unisaidie.

  1.Nijuavyo mie muunganiko wa vitu viwili huzaa kimoja, lakin sijaelewa kwa muungano huu wa Tanganyika na Zanzibar ambapo majina haya mawili yalizaa jina moja la Tanzania lililo yameza majina yote mawili kisha kukawa na serekali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania na serekali ya mapinduzi ya Zanzibar pasinakua na serekali ya Tanganyika yaani naona nisawa na kuunganisha pikipiki na baiskel kisha mwenye pikipiki avute kiongoza mwendo na kupachika gia huku mwenye baiskel nae anyonge pedal zake lazima kutatokea mkanganyiko hata kama wote watakua wameelekea upande mmoja sisemi kila mmoja awe ameelekea kwake hapo sijui itakuaje!
  ni vyema tujuzwe aina ya muungano tulio nao wa kuitambua serekali ya Zanzibar huku ya Tanganyika ikiwa kapuni ili turidhike na matusi tunayo poromoshewa na wenzetu tena wakiwa katika ardhi yetu na wakizitumia fursa za kiuchumi sawa na sisi huku sisi==»next

  Mohamed A. Ferouz

  May 27, 2012 at 3:13 PM

 9. Nimekukubali kamanda unaona mbali kweli wewe ni msomi

  Bakari hassan

  May 27, 2012 at 4:08 PM

 10. Kwa kule kwao inakua ni sawa na mbwa kuingia mskitini sio tu! kwamba anaweza kufikiriwa pengine labda ni kiu ya maji ilio mpeleka humo bali hata kukanyaga kwa tambo moja haruhusiki.

  2.ningependa kujuzwa faida za mojakwamoja zitokanazo na muungano anazo zipata mtu wa bara mbali na hizi zisizo na mashiko kua eti ni ndugu kwa kuoleana na fursa za kiuchumi,
  kama hoja ni hizo pekee basi utakua hauna maana kwani watanganyika tumeoleana na wakongo,wamalawi,warundi,wanyarwanda,wakenya,waganda,wamozambiq na wengine wengi, huo uchumi ni bora waseme hao wamipakani mwa nchi jirani kulikoni huko ambako ukikamatwa hata na mche mmoja wa karafuu ni kosa la jinai

  mohamed a. ferouz

  May 27, 2012 at 4:13 PM

 11. Asante kwa taarifa hii nzuri Mh. Zitto. imenifunza mengi. Maoni yangu ni kwamba, lini tutakuwa realistic na kukubali kuwa huu muungano wa serikali mbili hautaacha kuwa na matatizo?! nadhani ungekuwa muungano wenye nguvu na tija kama tungekuwa na serikali moja tu. hapo tungeendelea ila kwa sasa tutaendelea kupoteza muda na fedha kutatua tatizo moja baada ya lingine. Tuimarishe Muungano kwa kuwa na serikali moja au tuudhoofishe kwa kuwa na serikali tatu huku serikali ya muungano ikiwa ni “ceremonial government” kwenye hiyo katiba mpya. Hivi ni kweli Wazanzibari hawafaidiki kabisa na resources za Tanganyika? Swala la maliasili na utalii kwa mfano sio swala la muungano lakini kamati ya bunge ya ardhi, maliasili na mazingira inapozungikia vituo vya maliasili wabunge kutoka Zanzibar nao wamo! nilijiuliza hivi kwanini wasingehusika kwenye zile ishu za wizara za kimuungano tu hata kwenye vikao vya bunge? wakimaliza wakaongeze nguvu baraza wa wawakilishi zanzibar? Kwenye logo ya kuitangaza Tanzania bara kiutalii ughaibuni kunakofanywa na TTB, TANAPA, nk ambayo nahakika ni mashirika yenye mamlaka Tanganyika (bara) wanaitangaza na Zanzibar sio Bagamoyo.”TANZANIA THE COUNTRY OF KILIMANJARO, ZANZIBAR & SERENGETI” kama nimekumbuka sawa sawa. Hapo Zanzibar haifaidiki bila kutoka jasho kidogo?
  Sio kwamba napinga ulichosema, bali nataka tuangalie pande zote na tuwe more holistic tunapoangalia pande gani inafaidika au inanyonywa.
  Mh. naomba nikuulize: kwanini Wazanzibar ndo wanalalamika sana kwamba wabara tunawanyonya? na kama wabara (watanganyika) hatufaidiki na chochote kwa sasa (pengine tofauti na enzi hizo) kwanini viongozi wetu wanakuwa na viapo vya kuulinda muungano kwa nguvu zote? Niliwai kumsikia Mkapa akiwa raisi na Kikwete wakitoa misimamo kama sio viapo vya kuulinda muungano kwa nguvu zote.

  HAVE A NICE TIME

  Simon S. Mrosso

  May 27, 2012 at 10:55 PM

 12. Hapo ndo tofauti ya msomi katika jamii inapopatikana nakupongeza sana Mh Zitto kwa aina hii ya shule hususan kwa sisi vijan tuko pamoja katika kulijenga taifa jipya la Tanzania lenye mafanikio

  Hussein Gama

  May 28, 2012 at 5:06 AM

 13. Nakupongeza sana mh Zitto kwani wewe sio mbinafsi nakuunga mkono. Ila mimi naona tuwe na Serikali tatu ika serikali ya Muungano iwe tu ni kwa ajili ya mambo ya Muungano kama Mafuta na Gasi na mengine. Pia iweje mafuta ya kuendesha migodi iliyowekezwa yasilipiwe kodi na huku serikali inanunua mafuta kwa makampuni kwa gharama kubwa kwani Serikali imeshindwa kuwa na visima vyake vya mafuta? Na ushauri wangu Migodi, Mafuta, Viwanda nk tusiweke tena wawekezaji tufanye kazi wenyewe zaidi tuajiri wataharamu wazungu na si kuwekeza kwani kuna mzunguko mwingi wa pesa unapotea kama vyakula, matunda na nyama vyote vinatoka Afrika Kusini kama sio kuwa masikini ni vipi tuamke. Asante

  EVODIUS

  May 29, 2012 at 4:25 PM

 14. Hapa ndipo mimi maranyingi huwa nakukubali,kwani daima huwa uko kwenye mstari wa kusimamia hoja,ukweli,ushahidi,bila katka kusimamia na kuhakikisha haki inatendeka kwa masilahi ya pande zote mbili za muungano bila ya upendeleo.kwani serekali yetu bado imebaki na mawazo mgando ya karne ya kumi na nane ya kufosi mambo yanayo wahusu wananchi badala kuwasikiliza nini wanataka kuhusu raslimali zao na kuweza kutatuwa matatizo na kero za muungano.

  MTUMWA JUMA

  June 6, 2012 at 11:59 PM


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: