Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Ndio nataka kuwa rais

with 44 comments

Kwanza niseme wazi kabisa kabisa kuwa Urais ninautaka.

Ninaamini ninao uwezo wa kuwa Rais. Ninaamini nina uzalendo wa kutosha na utashi wa kuleta mabadiliko stahili wa namna nchi yetu inavyoongozwa. Ninajua kuwa nchi yetu imesahau maendeleo ya watu na kujikita katika maendeleo ya vitu. Ninajua kuwa hivi sasa viongozi wetu wengi wanaangalia zaidi mitindo (styles) badala ya mambo ya msingi (content). Ninajua kuwa maendeleo vijijini yamesahaulika. Ninajua nchi yetu inahitaji Uongozi wa kufanya mabadiliko makubwa (transformation) badala ya mabadiliko ya juu juu (cosmetic change). Ninajua ‘transformation’ inahitaji maamuzi magumu yatakayoudhi wengi na hasa mabwana wakubwa wa nchi za magharibi mfano kuzuia nchi yetu kuuza malighafi tu. Ninajua rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa Mali ya Umma ni kikwazo kikubwa cha maendeleo yetu na kwamba lazima hatua madhubuti zichukuliwe kuzuia na kutokomeza ufisadi. Ninajua rasilimali kama Madini, Mafuta na Gesi, Ardhi n.k. ni lazima zifaidishe wananchi wa nchi yetu.

Hivyo, nchi inahitaji Kiongozi wa juu atakayekabili changamoto hizi. Ninaamini ninaweza kuwaongoza Watanzania wenzangu kukabili changamoto hizi. Sio kazi rahisi lakini ni kazi ambayo lazima Mtanzania mmoja aifanye. Mimi nataka kuifanya. Nina uwezo wa kuifanya.

Hata hivyo kazi hii hata kama naitaka ni lazima wenye nchi waamue kunipa kazi hii. Ni lazima kwanza Chama changu kiseme wewe ndio mwanachama unaestahili kuifanya kazi hii. Ni lazima Watanzania wengi waseme wewe ndio mwananchi mwenzetu unayeweza kuchukua jukumu hili. Kuitaka tu haitoshi. Ni lazima wananchi wakuamini na kukupa jukumu hili.

Sasa kama wananchi watasema huyu Zitto anapaswa kubeba jukumu hili mwaka 2015 tuache iwe. Kama watasema hapana wewe bado mpaka mwaka 2020 au hata 2025 tuache iwe hivyo. Pia Kama hawataki kabisa tuache iwe hivyo.

Mjadala wa umri wa kugombea Urais imekuwa mjadala mkali sasa. Mjadala huu baadhi ya watu kwa sababu wanazojua wao wameamua kuita ni mjadala wa Zitto na January. Kwamba ni mjadala unaobagua Wazee. Mjadala unaopandikiza chuki na sumu za kibaguzi. Kwamba ni mjadala wa Kitabaka na kuwa Zitto na January sio tabaka stahili la vijana walio wengi. Sitamsemea January, nitajibu baadhi ya hoja za mwandishi wa makala mojawapo kama Zitto. January akitaka atamjibu naye kivyake.

Mwandishi anasema yeye hapingi hoja ya umri, bali anapinga aina ya watu wanaoshadidia hoja hiyo. Anaipenda hoja ila hapendi watoa hoja. Hoja nzuri lakini Zitto na January wabaya. Amelisema hilo mwanzo kabisa wa makala yake. Kwa hiyo kwake yeye hoja ingeletwa na vijana wengine asingekuwa na shida wala isingekuwa hoja hatari. Kwa kuwa hoja imeletwa na Zitto na January (ingawa sisi sio waanzilishi wa hoja hii) ni hoja ya kibaguzi. Nawashangaa sana wasomi wa siku hizi. Wasomi wanaojadili watu badala ya masuala.

Mwandishi anasema kwamba vyama vya siasa haviandai vijana kuwa viongozi. Nitamweleza.

Chama changu kinalea na kukuza vijana kuwa viongozi. Mimi binafsi nimejiunga na chama changu nikiwa na umri wa miaka 16, mtoto. Nimekulia ndani ya chama. Nimepewa majukumu ya kawaida kabisa ya chama kama kusimika miti ya bendera, kupokea viongozi na kuandaa mikutano. Nikiwa Chuo Kikuu Mwenyekiti wa sasa wa Chadema ndugu Mbowe alikuja kuniomba sasa nishiriki kikamilifu kukijenga upya chama. Yeye alikuwa Mbunge wa Hai akitaka chama kiwe imara zaidi, akaambiwa kuna mwanachama wenu kule Mlimani. Wakati huo CHADEMA kilikuwa chama ambacho watu wanakikimbia isipokuwa watu wa Kigoma na Kilimanjaro, Shinyanga, Karatu na Ukerewe. Vijana walikuwa wanajipambanua na CCM zaidi ama CUF au TLP kuliko hiki chama cha mabwanyenye. Huu ni mwaka 2001, muongo mmoja tu uliopita. Mimi na Freeman Mbowe ndio tumefanya mabadiliko yote yanayoonekana CHADEMA. Tumeingiza watu wapya, tumeandika Katiba upya. Ilipofika mwaka 2005 tukasema Freeman Mbowe nenda kwenye Urais, tulijuwa tunashindwa lakini tulitaka kujenga chama chetu. Tukapata Wabunge. Wabunge Wakafanya kazi. Tukaingia mwaka 2010 katika uchaguzi kama chama imara tunachokwenda kuchukua dola.

Katika mchakato huu tukaingiza vijana kwenye chama na kuwalea. John Mnyika hakuwa CHADEMA, tena alikuwa mgumu sana kuingia kwenye chama chetu. Tukampa moyo. Tukampa majukumu. Leo ni mmoja wa rasilimali watu kubwa sana katika siasa za nchi yetu. Halima Mdee hakuwa mwanasiasa kabisa. Tukampa moyo. Tukampa majukumu. Leo ni Mbunge mahiri kabisa.

Baadhi ya watu wazima waliingia CHADEMA kufuata vijana. Vijana tulifyeka pori kwanza. Nani anasema hatulei vijana kuwa viongozi wazuri? Nani haoni hazina ya viongozi vijana hivi sasa ndani ya Bunge kutoka vyama vyote? Kuna namna bora ya kulea viongozi zaidi ya kuwapa majukumu?

Mbowe alikuwa ananifuata pale Hall 1, tunakwenda kufanya kazi za chama usiku kucha, kusoma na kuchambua makabrasha ya kisera na mikakati. Ninarudi chuo usiku wa manane wakati wanafunzi wengine ama wapo wanajisomea au wamelala. Kazi ya kujenga taasisi inayoitwa chama cha siasa.

Lakini kujengwa kuwa kiongozi sio kazi ya chama pekee. Ni kazi ya jamii kwa ujumla. Wakati wanafunzi wenzangu walikuwa wanaomba kufanya kazi za mafunzo kwenye taasisi kubwa Kama Benki Kuu, nikiwa mwaka wa pili Chuo Kikuu nilikwenda kufanya internship TGNP. Kujifunza Bajeti ya kijinsia na kuipa hoja za kiuchumi. Kina mama wa TGNP wakanijenga na kunipika kiuongozi.

Chuo Kikuu sikuwa nasoma Sosholojia, lakini rafiki yangu mkubwa alikuwa Chachage. Sikuwa nasoma lugha, lakini mshauri wangu alikuwa Lwaitama. Sikuwa nasoma sheria lakini nilikuwa namwakilisha Shivji na kusoma mada zake alizopasa kuwakilisha kwenye semina kadhaa kuhusu haki za binadamu. Nimefunzwa na makundi ya watu mbalimbali na sio chama changu pekee. Jamii ndio yenye jukumu la kufunda vijana kuwa viongozi. Jamii inafanya kazi hiyo?

Inasemwa mjadala huu ni hatari kwa namna ulivyopenyezwa. Kupenyezwa? Huu mjadala wa umri umeanza kuzungumzwa mimi nikiwa nipo Chuo Kikuu. Vijana kupitia National Youth Forum Kama Taasisi ya vijana wamekuwa wakisema jambo hili toka miaka ya katikati ya tisini. Jukwaa hili la Vijana chini ya viongozi wake kina Hebron Mwakagenda wamekuwa wakitoa Maazimio na Maazimio kwamba umri wa kugombea Urais upo juu sana toka miaka ya tisini. Taasisi ya TYVA imekuwa ikijenga hoja hii toka miaka ya 2000. Hii sio hoja mpya hata kidogo. Hoja hii haijapenyezwa. Hii ni hoja ya vijana ya miaka mingi sana. Lakini sishangai kuona inaonekana ni hoja mpya kwani watanzania uwezo wetu wa kutunza kumbukumbu ni mdogo sana. Pia tunapenda kujadili mtoa hoja na sio hoja yenyewe. Mfuatiliaji yeyote makini wa siasa za vijana wa Tanzania kupitia makongamano ya vijana anajua hii sio hoja iliyopenyezwa na Zitto au January. Kuijadili kwa kumwangalia Zitto na January ni kuchoka kufikiri.

Hoja hii haina hatari yeyote inayosemwa na mwandishi. Hoja hii ni hoja kama hoja nyingine yeyote na inaweza kupita au kukataliwa. Hii sio hoja ya watu fulani. Ni hoja ya vijana ya siku nyingi sana. Vijana hawa wanajiona kupitia vijana wengine walio kwenye nafasi mbalimbali kisiasa au hata katika sekta binafsi. Mfano vijana wa Kigoma ninakotoka wakiniangalia wanajiona. Ndio wanaona tuko sawa. Wanaona mimi ni mwenzao. Nimekua miongoni mwao. Nimesoma nao. Nimecheza nao. Nimehangaika nao. Wanaona Ubunge nilionao ni Dhamana tu na hawanizungumzishi kama mtu kutoka tabaka fulani, bali kama mwenzao.

Ninaishi maisha ninayoishi. Siishi Manzese kwa Mfuga Mbwa. Siishi Masaki pia. Naishi Tabata, kwenye nyumba ya kupanga. Tabata wanaishi vijana wote wale wa tabaka la chini kama asemalo mwandishi na pia tabaka la kati na labda tabaka la juu. Najua na kusikia machungu ya vijana wasio na ajira na ndio maana nahangaika kwa kutumia nafasi ya Ubunge kujaribu kuisukuma Serikali iweke sera zinazotekelezeka za kutatua tatizo la ajira kwa vijana. Ndio maana nahangaika kila siku kujenga hoja kwamba Serikali iingilie kati ukuaji wa uchumi ili pia wanyonge wafaidike. Ninasikia machungu ya vijana wasio na ajira maana ndio walionipigia kura kuwa Mbunge. Zaidi ya hayo nakutana nao sana kuzungumza namna ya kusaidiana.

Nakutana nao mitaani kwa mijini na vijijini ninakokwenda kila wakati. Nakutana nao kwenye mitandao ya kijamii, wananiandikia na mimi ninawajibu. Nagawana nao kidogo nilichonacho ili nao waweze kijikwamua. Nawasaidia vijana wenye vipaji kukuza vipawa vyao na kupata kipato. Mwandishi anapata wapi haki ya kusema sentensi rahisi rahisi kwamba mimi sisikii machungu ya vijana wenzangu?

Ninashinda na vijana wa aina zote, ndio kazi kubwa ya Mwakilishi anayefanya kazi yake. Nina marafiki wavuvi, mafundi seremala, waimbaji wa Bongo Flava, machinga na hata wasio na ajira. Nina marafiki wenye makampuni yao, wafanyakazi wa mashirika ya Umma, wasomi wa Vyuo Vikuu na wafanyabiashara wakubwa. Mwakilishi yeyote wa wananchi lazima asikie machungu ya jamii nzima vinginevyo hatoshi.

Kijana mwenye umri wangu ana mambo mengi anayofanana nami. Ana mambo mengi ya kujifunza kutoka kwangu. Hapa katikati ilikuwa ni kama jambo lisilowezekana kijana wa aina yangu kutoka familia masikini kabisa kuwa Mbunge. Baada ya Zitto kuwa Mbunge na kutokana na kazi niliyofanya Bungeni katika Bunge la Tisa, vijana wengi walihamasika na kusema wanaweza. Leo tuna vijana wadogo kabisa kutoka familia za kawaida kabisa ni Wabunge na wanafanya vizuri. Kina Kafulila, kina Mkosamali, kina Silinde hawa ni watoto wa kimasikinj kabisa ambao ni wa kwanza kupata shahada kwenye familia zao. Hii ni nguvu ya ‘inspiration’ kutoka kwa rika linalofanana. Sugu ni mkubwa kwangu kiumri, lakini kuingia kwake siasa kumechangiwa sana na kazi zangu pamoja na wenzangu kwenye Bunge.

Kuna vijana wengi zaidi nchini kwetu wanasema ninataka niwe kama Zitto, kama January, kama Halima Mdee. Tunazungumza nao. Tunaishi nao. Ni ndugu zetu. Ni rafiki zetu. Tunaishi nao mtaani. Tunakwenda nao kwa kinyozi mmoja. Tunakwenda muziki pamoja. Ninajua machungu ya vijana. Ninafanyia kazi machungu ya vijana. Ndio kazi yangu ya kila siku kama Mbunge, kama Mwakilishi wao.

Mwandishi anasema mjadala unalenga kuleta ubaguzi. Sioni hoja yake. Wanaosema umri wa kugombea Urais ushushwe chini ya miaka 40 hawasemi wazee wasigombee. Wanasema tupanue wigo wa haki hii ya kugombea. Wanaozungumza ubaguzi ndio wenye kupenyeza mbegu za kibaguzi. Kwa kuwa wanawaza kibaguzibaguzi basi kila jambo huliangalia kibaguzi. Kama Katiba inasema yeyote mwenye haki ya kupiga kura ana haki ya kugombea nafasi yeyote ya uongozi, ubaguzi unatoka wapi? Hoja zote zinazotolewa na mtoa hoja kuhusu ubaguzi zinasambaza mbegu ya ubaguzi.

Mwandishi sasa anawaambia Watanzania waanze kufikiri sasa zamu ya nani. Mimi binafsi sijawahi kusema hii ni zamu ya vijana. Ila nimesema changamoto za sasa za nchi zinahitaji mtu mwenye uwezo wa kuzikabili, ninaamini mtu huyo ni kijana. Ninaamini kuwa kila kizazi kina ajenda zake. Kizazi chetu kina kazi ya kuhakikisha uhuru wa kiuchumi wa nchi yetu. Kizazi cha kina Mwalimu kilikuwa cha ukombozi na kujenga Taifa moja. Mwandishi hamwamini Frantz Fanon?

Hoja ya kwamba mjadala huu unataka kununua hisia za wanyonge ni hoja isiyo na [mashiko] kabisa. Mimi nimechaguliwa na wanyonge mara mbili kuwa Mbunge wao. Wanyonge wamenipa Ubunge bila kutoa rushwa. Wamenipa Ubunge kwa kuniamini. Sasa kwa nini sasa ninunue hisia zao? Hii hoja ina misingi gani? Hii ni hoja ya kubandika. Hii ni hoja ya kubumba maneno ili mwandishi aonekane kwamba anafanya uchunguzi wa kitabaka. Hakuna dhana ya tabaka katika hoja hii kama ilivyo kuwa hakuna dhana ya tabaka kwa wazee au hata wanawake. Hoja hii haizuii kwa namna yeyote ile wananchi kuhoji chanzo cha ufukara wao. Kwanza wanaosemwa kwenye hoja hii ndio wapo mstari wa mbele kuhakikisha Mali ya Nchi inatumika wa maendeleo ya wananchi. Mimi binafsi nimeanzisha mjadala wa rasilimali Madini nchini mpaka kutungwa kwa sheria mpya inayoweka misingi ya nchi kufaidika na Madini. Mimi binafsi na wenzangu tumekuwa mstari wa mbele kuhakikisha serikali inatekeleza sheria mpya.

Mwandishi amesahau Buzwagi? Mwandishi amesahau hoja ya Mkonge inayotaka wanyonge wapewe mashamba ya Mkonge na wawezeshwe na Serikali kulima Katani? Mwandishi amesahau hoja ya kusimamia sekta ya nyumba ili wanyonge wasinyonywe na wenye nyumba ambayo imetolewa na mmoja wa wanaotetea hoja ya umri kushushwa? Ama mwandishi ana wanyonge wake anaowasemea? Sio hawa manamba kwenye Mkonge. Sio hawa vijana wachimbaji wadogo. Sio hawa vijana wanaoshindwa kulipa kodi ya nyumba mwaka mzima? Wanyonge wa mwandishi ni wanazuoni wanaoishi kwa fedha za walipa kodi ambao hawana shida ya kujiuliza kama watakula au watalala maana Serikali au wafadhili wa masomo yao wanawalipia malazi na chakula. Kama wanyonge wake ni hawa waliotupigia kura sisi ili kuwawakilisha Bungeni, basi mwandishi hajui asemalo.

Hoja ya umri wa kugombea Urais, kwa kuweka pa kuanzia ama kuweka kikomo inapaswa kujadiliwa bila kuangalia majina ya wanaotetea hoja hii. Ijadiliwe kwa faida na hasara zake. Kujenga hoja kwa misingi ya kitabaka ni kuchochea ubaguzi na kunyweshea mbegu za kibaguzi. Nani ana uhakika kuwa Zitto atakuwa anaishi ifikapo mwaka 2015? Kwamba tusiandike Katiba yenye kupanua wigo wa kutoa haki ya kugombea Urais kwa sababu ya Zitto?

Huu woga dhidi ya Zitto unatoka wapi?

Written by zittokabwe

March 24, 2012 at 10:01 AM

Posted in Uncategorized

44 Responses

Subscribe to comments with RSS.

  1. Mh Zitto Kabwe,kama mwandishi hawezi kuelewe unachokieleza ,nafikiri hata uaandishi wake wa habari tutakuwa na mashaka nao. Huenda anatumiwa na watu kupotosha jamii.Ninakubaliana na wewe 100% ipo haja ya kubadilisha umri wa mgombea wa urais ,sote tunaona hilo.kushusha umri hakumpunguzii sifa mwenye umri mkubwa kugombea ,hiyo ndo “key point”-ameelewa! Nakupongeza sana mh Zitto Kabwe.

    hobidan

    March 24, 2012 at 10:40 AM

  2. Asante kwa ufafanuzi mzuri kaka Zitto,hii siyo jibu tu kwa huyo mwandishi asiyejielewa bali ni mwanga na inspiration kwa kila atakayepata hata dkk 2 za kusoma. Mimi binafsi naona kutetea hoja ya umri wa kugombea urais kupunguzwa haimaanishi kuwa lazima Zitto ugombee,inawezekana mimi Salum miaka 38 au mimi Jackson miaka 35 natamani sana kugombea na nina kila sifa na zaidi waTanzania wananihitaji ila tu sipati nafasi kama uliyonayo wewe Zitto. Umri wa kugombea hata ukiwa miaka 12 haimaniishi hata mdogo wangu wa Kata Secondary anaweza kugombea. Umeeleza vizuri hapo juu kwanini wewe unaweza kuwa rais na hilo ndilo naona hoja ya msingi kujadili.tuachane na watu wenye chuki binafsi au wanaofanya kazi kwa maslahi ya watu fulani.
    Nakutakia kila la kheri

    Raymond mauki

    March 24, 2012 at 1:52 PM

  3. Mh.Zitto binafsi nimesoma kwa makini sana posti yako hii,nimeirudia zaidi ya mara moja na kuelewa kwa undani unachokizungumza, binafsi ni kijana wa CCM, na kifupi wewe ni miongoni mwa vijana mlionivutia sana kuiamini na kujiona naweza kama kijana enzi hizo nikiwa ni makamu mwenyekiti wa serikali ya wanafunzi wa shule ya sekondari Milambo Mkoani tabora miak ya 2000s na hatimae leo nimekuwa ni miongoni mwa vijana wa kutegemewa na jamii,ni ukweli usiopingika kuwa muandishi alikuwa hajaelewa unachokusudia na kama alielewa basi hakututendea haki wananzania. katika nchi yetu na hasa maeneo ya majimbo yetu tulikuwa tukiamini kuwa ili uwe mbunge ni lazima uwe mzee wa heshima, tajiri na mwenye digrii nyingi lakini kwa muongozo wa vijana mlotangulia mmeonesha njia kuwa kumbe mambo yanawezekana. Katika suala la umri nami ningepingana na mtua mbae angeshauri kuwa kijana wa miaka 20-25 anaweza kuwa Rais lakini zaidi ya hapo ni binadamu mwingine kabisa kwani aliyokutana nayo duniani kwa miaka 30-35 ni mengi na ninaamini kwa aliyechaguliwa na Mungu kuwa Raisi anweza na akaleta matunda bora zaidi ya tunavyofikiria. binafsi haya niyatoayo si ushabiki wa kichama kwani hata itikadi yangu haifanani na yako lakini naamini kuwa kujadili hoja ndio msingi na kuachana na mambo ya kumjadili mtoa hoja.

    Imani Moshi

    March 24, 2012 at 4:11 PM

    • Mheshimiwa Zitto nakupongeza kwa kazi unazozifanya kuwasaidia wananchi wa Tanzania, na ni ukweli usiopingika kwamba wewe umeleta mchango mkubwa katika mageuzi tunayoyaona katika nchi hii leo.

      Sipingi uamzi wako wa kutangaza nia ya kugombea uongozi wa juu wa nchi hii ila nafikiri umekuwa na haraka mno ya kufanya jambo ili. Kwanza sisi kama wafuasi wako hatujajua hatima ya Mheshimiwa Dr. Slaa kama naye anahitaji kugombea au hapana. Na hatujajua chama cha CHADEMA kina mpango wa kumsimamisha mgombea yupi. Mimi nafikiri ilikuwa ni muhimu chama kwa kauli moja kupitia vikao vya ndani kuamua ni nani asimame kwenye kugombea nafasi ya urais.

      Kitu kingine kilichonishtua ni uamzi wako wa kuamua kutangaza hatua hii wakati unajua kwamba kuna shughuli pevu ya kugombania jimbo la Arumeru mashariki. Mimi nafikiri ungesubiri kwanza matokeo ya huko yakatuonyesha kama mgombea wa CHADEMA ameshinda au ameshindwa ndo ukatangaza uamzi wako. Huoni kwa kitendo chako cha kutangaza wakati kampeni ndio zimepamba moto umewafanya watu waanze kukufikiria wewe badala ya kufikiria jinsi ya kulipata jimbo la Arumeru Mashariki?

      Ushauri wangu kwako. Endelea kufanyakazi yako kwa umakini wa hali ya juu. Semea raslimali za nchi hii na hasa madini ambayo kwa sasa umekuwa kimya na mengine mengi. Jenga mtaji wa watu wa kutosha kupitia matendo yako urais upo utaupata muda ukifika.

      Utafute urais kwa njia urais kwa njia rahisi na si kwa kupnagua hoja ambazo zitakupa shida sana. Charity starts at home ukianza na upinzani ndani ya chama itakuharibia hata kwa wasio wanachama.

      NAKUAMINI, NAKUPENDA NA NINA MATUMAINI WATANZANIA WATAPATA NAFUU KUPITIA KWAKO.

      Maganga C.J

      March 25, 2012 at 6:29 PM

      • Inaonekana hujaelewa hoja soma vizuri…paragraph hii inaweza kukusaidia kidogo (kama ulisoma article vizuri utajua iko wapi) “Sasa kama wananchi watasema huyu Zitto anapaswa kubeba jukumu hili mwaka 2015 tuache iwe. Kama watasema hapana wewe bado mpaka mwaka 2020 au hata 2025 tuache iwe hivyo. Pia Kama hawataki kabisa tuache iwe hivyo”. Zitto anaongelea hoja ya umri wa mgombea wa urais lakini umelielewa kama mwandishi wa article hii soma toka kwenye link hii http://udadisi.blogspot.com/2012/03/mjadala-wa-ujana-na-urais-wazidi.html anavyotakata kuwajaza watanzania fikra zisizo na tija…si zito hata wewe pia una nafasi kama kijana..Zitto anatumia nafasi yake kama mwakilishi kutetea haki ya watanzania…Ni kama Mch Mtikila alipopigania suala la mgombea binafsi na tukalishwa maneno ya kua anapandikiza chuki na matbaka na vitu vingi vya ajabu wakati kikatiba…Kila mtanzania alifikia au zaid ya miaka 18 ana haki ya kuchagua au kuchaguliwa…mengine tuyaache ila upotoshaji kama huu ndo ulifanya hoja ya mgombea binafsi kupingwa na kufutwa na kwa upotoshaji wa waandishi kama hawa hoja ya umri wa urais nayo itazimwa tuache ushabiki wa nani kafanya tuanagalie nini anafanya…tunahitaji mabadiliko na haya wezi kuja kwa kuangalia watu nchi inajengwa na sera,mipango nausimamizi mzuri sio chama fulani..na m-support Zitto na January na mwanaharakati yeyote anaeitakia nchi hii mema…tubadilike na tujenge utamaduni wa kusoma na kua creative thinkers sio kutegemea kulishwa kila kitu…

        Gerry Bukini

        March 26, 2012 at 12:38 PM

  4. Inasikitisha sana kuona jitihada binafsi za kututoa katika dimbwi hili la kinyonyaji na jamii iliyojaa hofu, zinakandamizwa. Hoja hii, kama ulivyoeleza mheshimiwa Zitto, si ngeni, na hata usingeisema wewe kama mheshimiwa Zitto bado vijana wengine wangeipigia kelele tu. Kwani ni kigezo gani kilichotumika mwaka 2000 kumpigia Kikwete debe katika chama chake (ingawa hakupita) hata 2005, kama si ujana? Nakumbuka hoja hii tuliijadili mwaka 2001 pale Marangu TTC katika symposium ya National Youth Forum – wewe na mheshimiwa Mnyika mkiwa pia kama washiriki, wakati huo hata mlikuwa hamjagombea ubunge. Ni wazi kuwa kuna wengi katika waandishi wetu ambao ama wanatumiwa kuwachanganya watanzania – ama wamelewa ushabiki wa kimasikini wa fikra, kukumbatia fikra za chama tawala, hata pale ambapo ni dhahiri kuwa wanachoongea hakina mantiki. I think it is a high time we ignore them and move forward

    sedon

    March 24, 2012 at 4:15 PM

  5. Tanzania tunahitaji viongozi wenye maono na nchi yao! Na kama haya yote unayoyasema mheshimiwa Zitto yanatoka rohoni, nina msihi Mwenyezi Mungu atie Muhuri katika kibao cha moyo wako ili yote yatimie. Na ninakuhakikishia sisi wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tupo nyuma yako na tutakuwezesha ili ndoto yako itimie. Watanzania tumechoka kuchaguliwa viongozi wasio na vission kwa nchi yetu. Tuna utajiri wa kila aina lakini mtanzania ni masikini duniani, hata nchi za nje zinatushangaa ni jinsi gani tulivyo na aina ya viongozi wanaozunguka kuomba misaada wakati utajiri tulionao tukiusimamia sisi ndo tunapaswa kutoa misaada kwa nchi zingine kwani tutakuwa na surplus. Maisha ya mtanzania badala ya kuwa bora tunavyokwenda mbele matokeo yake yanadidimia na mtanzania anazidi kuwa masikini! Tanzania tunahitaji revolution and it is on its way, enough is enough we need creative leaders. I support u never give up! Ni kweli Tanzania inamaendeleo “cosmetic” Ni sawa na kupata rangi nzuri katika jengo lenye umri wa miaka 300 iliyopita! Tumechoka kila baada ya miaka 5 tunapaka rangi jengo lilelile wakati ukiangalia kuta zake zimejaa nyufa na misingi yake inadidimia! Its time for change!

    Stephen Mndalila

    March 24, 2012 at 5:34 PM

  6. i salute u brother..

    camillius

    March 24, 2012 at 9:28 PM

  7. This is cool and logical, I hope for more responsible responses and counter responses

    Irenei Kiria

    March 24, 2012 at 9:45 PM

  8. Kipekee kabisa nakupa heko Zitto kwa andiko hili lenye hekima na busara. Umejibu kwa unyenyekevu na uvumilivu pia. Sote tunaelewa ulikotoka na ufanisi wa kazi yako kwa ujumla. Ni ujuha tu kwa mwandishi huyo kuandika hoja za kitoto kama hizo. Anyway, tunamsamehe hajui alitendalo. Au kama anatumika kwa kusudi maalum la kuharibu nyota yetu vijana, hatafanikisha hilo.

    W

    liko tumaini

    March 24, 2012 at 10:34 PM

  9. Mh Zitto, Salaam! Nimeusoma ujumbe wako mara mbili nimeuelewa. Pia nimeyasoma maandiko ya “mwandishi.” Lakini, hapa ninapenda kuleta sura mpya katika mada inayoongelewa. Nitatumia nafasi yangu kama Mhadhiri wa Business Organisation & Administration. Organogram ya nchi haina tofauti na organogram ya taasisi baki kama vile makampuni. Katika kuwapa watendaji nafasi kwenye tasisi tunaangalia mambo makuu matatu: “experience, skills and education.” Vigezo hivi vitatu mara nyingi ndio hutumika kuamua nani alipwe kiasi gani katika ngazi gani. Kwa kuzingatia mantiki hii, kuna kila sababu ya kuweka bayana vigezo vya kitaasisi pale tunapokuwa tunaongelea kujaza nafasi za kazi zilizomo katika political organogram ya taifa kama inavyopatikana katika katiba ya nchi. Jambo hili linao msaada mkubwa sana katika kutusaidia kupambana na moral hazards, selection hazards, cognitive hazards, na matatizo kama haya kama yanayotamkwa katika mifumo ya kidemokrasia. Kama hivi ndivyo, napenda kusikia kutoka kwako kuhusumasuala haya: unataka political organogram yetu iwe na levels ngapi? Na je, ni “experience, skills and education” gani inafaa katika level ipi? Haya ni masuala ya kitaalam na yanajadilika kitaalam. Hivyo, suala la kusema kuwa katiba ikae kimya kuhusu “experience, skills and education” ya watu watakaojaza political organogram halijakaa kitaalam. Ningependa kusikia toka kwako kutokea katika perspective hii. Hata hivyo, sina mashaka na uwezo wako binafsi kama potential presidential candidate. Waiting to hear from you from this angle. Cheers!

    Deusdedit Jovin Kahangwa

    March 25, 2012 at 12:14 AM

  10. Huu ujumbe ni mzito sana Zitto, hongera kwa kuweza kuandika yote haya, naamini yamewagusa wengi. Ninaloweza kukuambia kwa sasa ni kwamba, siku zinatembea, la maana kwako kwa sasa ni kufanya kazi kwa bidii na kuyasimamia yale unayoyaamini kwa kadiri ya uwezo wako mengine yatajipanga kadiri siku zinavyokwenda, tutafika tu.

    Colly

    March 25, 2012 at 2:48 AM

  11. Kabwe nadhani mawazo yako ni sahii sana ila tu usiwe mtu wa kubadirika badirika kisa umekwazwa kama wana siasa wa kitanzania walivyo. masirahi weka mbele lakini usijiahau ahadi zako

    Sweetbirth Bruno. mbunge mtarajiwa wa jimbo jipya la Bunju

    March 25, 2012 at 7:30 AM

  12. kuna rafiki yangu amempa mtoto wake jina la Zitto kutokana na kuvutiwa kwake na juhudi za Zitto Kabwe

    Tumainiel Seria

    March 25, 2012 at 9:14 AM

  13. Mimi ni mwana CHADEMA.Mabadiliko ndani ya chama,hayafanywa na watu wawili waitwao mbowe na Zitto.Siamini kama Mbowe ana mtazamo kama wako Zitto wa kupuuza mchango wa wengine katika kuleta mabadiliko ndani ya chama

    Chama ni taasisi,mabadiliko na maendeleo yake yanatokana na jitihada za mfumo mzima na mchango na ushiriki wa kila mwanachama na viongozi.

    Kauli kwamba nyie na Mbowe ndio mmeleta mabadiliko yalilyopo ndani ya chama,ni kujidai na kuonesha kiburi dhidi wengine walioshiriki kuleta mabadiliko ndani ya chama.

    Zitto haueleweki. Nitajadili hili katika makala kwa kadiri nitakavyopata fursa.

    by kibona dickson,UDSM

    dickson Kibona.

    March 25, 2012 at 9:15 AM

  14. Maneno yako ni ukweli mtupu. Kwani viongozi waadilifu na waliokomaa walipata nafasi kubwa toka wakiwa na umri mdogo sana, mfano hai ni Dr.Salim Ahmed Salim. Akiwa kijana wa miaka 19 tu alikuwa katibu wa vijana. Na alikuwa balozi akiwa na 21au 22years old. Tunahitaji mtu mwenye uchungu na nchi hii bila kujali itikadi wala umri wake. Unaweza kuwa mtu mzima lkn ulokosa busara, sasa faida iko wapi?

    Shelly

    March 25, 2012 at 12:16 PM

  15. I am inspired! BEST ARTICLE EVER READ!! kaka mzigo unao wa nchi hii. few can sacrifise their lives for others. Am Glad we have some left in our community!

    allen mushi

    March 25, 2012 at 12:38 PM

  16. I BELIEVE MH. MBOWE CAN DO IT

    Mutoto Ya Arusha

    March 25, 2012 at 1:56 PM

  17. Subiri kwanza kijana muda bado..Muache doctor awanie tena.Maana ana akiba ya kutosha ya wananchi,tusiwachanganye.

    Alloys Machage

    March 25, 2012 at 2:26 PM

  18. Hongera sana umemjibu vizuri mwandishi na umetuelimisha na sisi nadhani kila mwenye nia nzuri amekuelewa..
    Nakuombea inshallah ufanikishe Malengo yako kwa watanzania.
    Mama.
    Kuruthum Mohamed Lwabukumba.

    Kuruthum Mohamed

    March 25, 2012 at 2:35 PM

  19. mabadiliko yaliyofanyika ndani ya chadema,hayajatokana na jitahada zenu nyie,mbowe na Zitto.Chadema ni taasisi,maendeleo na mabadiliko ndani yake yanatokana na jitihada za mfumo mzima wa utendaji wa chama kwa kuwashirikisha wanachama na viongozi wote wa chama.

    Sijasikia kutoka kwa bwana Mbowe,kama na yeye anaweaza kuwa na kauli za majivuno za kubeza kwa kiburi michango ya hali na mali ya wengine katika kujenga chama chetu na kutafuta utukufu wa kibinfsi.Mbowe hawezi kutamka upuuzi kama huu. Mara nyingi nimemsikia katika hotuba zake kama kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni,huwa anaanza kwa kuwatambua wanachama na viongozi wengine katika kujenga chama.
    Tatizo lako bwana Zitto ni kujikweza.Zitto,haueleweki

    KIBONA DICKSON.MWANACHADEMA,UDSM.

    DICKSON KIBONA

    March 25, 2012 at 4:55 PM

  20. Mkuu zitto z kabwe saruti kwako mimi ninashida binafsi kamahautajari ninaomba tuwasiliane kwa emmanuel.slyvester@yahoo.com, au 0765156828

    Emmanuel s komba

    March 25, 2012 at 5:06 PM

  21. Nimeisoma article ya Mheshimiwa Zitto,This Guy is Smart,anajua kupanga hoja na kuziteta.Naamini atafika mbali sana kisiasa na kuingia katika Vitabu vya Historia,asikate tamaa na asitegemee mafanikio ya haraka pia.

    Meinrald

    March 25, 2012 at 8:09 PM

  22. Nakutakia kila la kheri – nahamasika sana na personality, goals, ambitions pamoja na integrity yako na ya Januari. Vyama bado vinaniacha njia panda! Where I can kutakua na kiji support yangu. Tutaonana mwezi wa sita

    Ronnie Mtawali

    March 25, 2012 at 9:23 PM

  23. dissapointment, i used to look you as the only clever politician untill this, find a new advisior

    ian

    March 25, 2012 at 9:24 PM

  24. Nakubaliana na wewe kabisa Zitto kwenye suala la waandishi.Nchi hii waandishi wa kuwasemea wasio na sauti wamebaki wachache sana,wengi tuliokuwa tunadhani ni makini na wanaweza kutusemea wamebaki kutumiwa tu na mafisadi mpaka hata hawajielewi-wamepoteza utu wao na wamebaki kutanga tanga tu.Wamebaki kushambulia kila hoja inayopita mbele yao hata kama hoja hiyo inahitaji mjadala zaidi.Kimsingi mi nawaona wamefirisika sana,wanahitaji kujifikiria upya kwani nchii hii ni ya kwetu sote na mustakabali wake uko mikononi mwetu.

    Mugisha

    March 25, 2012 at 11:00 PM

  25. […] zaidi Ingia humu Be Sociable, Share! Tweet […]

  26. Binafsi nakuona unauwezo mzuri tu, ila si vema kusema nautaka Urais inapaswa watu waseme wanataka uwe Rais hapo itapendeza zaidi

    David Bassu

    March 26, 2012 at 11:31 AM

  27. nakupongeza sana mh. Zitto kwa hoja uliyojenga kuhusu urais na vijana.wanaokuza hoja hii wanahofu ya vijana kuanza kuunga mkono mabadiliko yanayoletwa na vijana baada ya wazee kwa miaka 50 bila kitu cha kujivunia.vijana tusikate tamaa,tuko nyuma yako hoja ifike kwa wananchi hasa wakati huu wa mabadiliko ya katiba mpya.

    daudi masayi

    March 26, 2012 at 1:38 PM

  28. Mhe Zitto ni heshm,a kubwa kwetu vijana wa lika lako na chini yake, kauli thabit huwa inauma sana. Najua huwa unaamini sana unachokiamini, ukweli ukiunena basi Zitto ni jadi yako kuwa tayari kuufia. Namkumbuka sana rais Mkapa kwenye moja ya hotuba zake, aliwahi kusema namnukuu,”watanzania lazima tuwe na tabia ya kufanya uchunguzi wa kina na utayari wa kukubali ukweli” Anayebeza hoja kwa kuangalia nani ametoa sauti basi arejee ushauri wa bure wa mzee Mkapa utamsaidia sana. Mhe Zitto na wenzio wa aina yako kama Mhe January tupo nyuma yenu sote kwa pamoja tuseme FORWARD EVER, BACKWARD NEVER…. Twende kwa kasi kubwa sana, asiyeweza apumzike atatukuta tumefika.

    juma kiolobele

    March 26, 2012 at 6:58 PM

  29. Zitto vijana wengi tupo pamoja na wewe binafsi nakuangalia kwa macho matatu kama mtu bora na tunu kwa taifa letu. Sina ubishi na jitihada zako kuhakikisha mnyonge wa TAnzania anapatiwa walau unafuu wa maisha kutokana
    Na uwepo wako na jinsi mnavohangaika bungeni vijana wengi tumevutika na CHADEMA maana tunaona kama Chama chenye kututoa tulipo na kutusahaulisha maumivu yanayoletwa na CCM.. Nipo pamoja nawe ktk kupunguza umri wa urais hapo sina pingamizi na sipingi kabisa wewe kuutaka uraisi! Ninachokipinga ni kauli yako umeitoa muda sio muafaka kwani inaweza kabisa kukigawa Chama na kutafsirika wengi wenu mnapenda madaraka hasa ya uraisi! Sidhani kama kingeharibika kitu Kama kauli hii ungeotoa 2015 na kuiwakilisha kwa Chama chako na muda huu kuutumia kukiimalisha Chama badala ya kuleta marumbano yasiyo na tija!

    Nicklas Mathias

    March 26, 2012 at 9:39 PM

  30. Upo sawa kwa muono wangu ila wa2 ambao ume wasaidia ni wa chache kulinganisha na weng 2liopo mitaan 2lioharibiwa tasinia ya maisha ye2 kwa mfumo wa ajabu wa elimu ya leo 2naopenda siasa ila 2naokatshwa tamaa na wanasiasa wachache. Naamin raisi mzur ni yule anaetoka ktk chama chenye uongoz bora na sera bora chadema kina cfa hzo wewe upo mwenye cfa hzo kama unania ya dhat yakusaidia wananch haswa vjana kwa faida ya nch na wananch unasapot kubwa kutoka kwa sisi haswa mimi ila usilewe cfa ukasahau wap 2nataka u2fikishe.

    Samuel mruma

    March 27, 2012 at 10:42 AM

  31. mheshimiwa kazia hapohpo maana bila kuwa na viongoz wenye upeo kama wako nchi tunaipelela kusiko. viongoz walio wengi wanajali maslahi binafsi kuliko ya umma. good job brother 2ko pamoja.

    TINKA RWEGASIRA, SUA

    March 27, 2012 at 10:35 PM

  32. SISI TUKO NYUMA YAKO WAKATI UKIFIKA LA MSINGI NI KUFAHAMU WATANZANIA WANATAKA NNI?KWA WAKATI HUO UKIFIKA NA NCHI HII HAKUNA WASIOKUJUA KWA MAGEUZI NA MABADILIKO NDANI YA SERIKALI ULIVYOWASAIDIA KWA KUANIKA BAADHI YA MAPUNGUFU KATIKA MIKATABA MBALIMBALI PIA SERA

    Masoud Kejo

    March 28, 2012 at 12:05 PM

  33. I appreciate you mr Zitto YES YOU CAN, AND TOGETHER COULD MAKE IT., kikubwa ni uhai umoja

    emmanuel mushi

    March 28, 2012 at 1:31 PM

  34. ni wazo zuri,lakini lisije kuibua malumbano ndani ya chama,na kusababisha malumbano ambayo yatakichafua chama na ccm kutumia mwanya huo kuwaangamiza,ikumbukwe kuwa wewe ni mtu wa muhimu bungeni sasa usije kujikoroga ukaukosa urais na bungeni tukose utetezi wako.kumbuka una tegemewa sana sio na wa2 wa north kigoma but all tanzanian.

    Herman Nguki

    March 28, 2012 at 3:09 PM

  35. Naamini kwamba unauwezo mkubwa wa kuiongoza nchi yetu lakini utakuwa na kazi ya ziada kuirudisha Tanzania ya zamani.

    Obadia

    March 28, 2012 at 10:23 PM

  36. Sasa mheshimiwa tumekuelewa unania na unaona kwamba unaweza kuiongoza nchi. Kwa kusema tu kwa maneno ni rahisi lakini tunachokitaka ni sera zako, na kwa kero na matatizo yote yanatukabili watanzania, utueleze kwa maandishi ni jinsi gani utainua uchumi wa nchi, utaisimamia katiba ya nchi, ni jinsi gani utawashughulikia mafisadi wanaoendelea kuimaliza nchi hii bila huruma, ni jinsi gani utainua kiwango cha elimu na mambo mengine mengi. Ili uweze kupata support toka kwetu wananchi tunahitaji sera! Asante sana mhishimiwa Zitto.

    Stephen Mndalila

    March 29, 2012 at 6:26 PM

  37. WALLAH MWISHO WA CCM HAUNA MIAKA 7 ZAIDI YA HAPO.KAMA SIO MAMBO YA NCHI YA MALI KUTOKEA NCHINI BASI TUNAMWAGA DAM HIVI KARIBUNI.YANAYO TOKEA NCHINI TUNA YAFAHAM NA HUKUM YAO IPO TAYARI.TUPO NYUMA YAKO WATANZANIA WOTE WENYE UFAHAM THABITI NA UCHUNGU WA MABADILIKO YA KWELI NDG.ZITTO.KILA LA KHERI TUNAKUUNGA MKONO

    yassin jr NTARABHANYA.

    April 5, 2012 at 5:48 PM

  38. mimi nadhani braza Zitto yako ni sahihi,ila naamini lengo lako ni kuwa kiongozi mtetezi wa wanyonge na sio lazima kuwa Rais japo naamini pia unaweza kufanya vizuri,usimpe mtu nafasi ya kutoa punje juu yako.matandiko wa mwananchi 0716186074

    9

    matandiko

    April 15, 2012 at 10:03 AM

  39. Heko braza Kabwe, ni majungu na chuki binafsi tu, vijana ndiyo chachu ya maendeleo, kwani hao wazee wamefanya lipi la ajabu sana??

    Twile Homeboy

    April 15, 2012 at 7:40 PM

  40. Hongera! Waandishi wanarudisha NYUMA maendeleo yetu. Kubwa NI UBINAFSI na KUTOJIAMINI katika kutekeleza MAJUKUMU YAO. Wanawatii WACHACHE(Mafisadi-VIGOGO) ili kutunyima HAKI & FURSA. Lazima TUWAELIMISHE mpaka WAELEWE. Hatuchoki kamwe…

    Mwl. MBAKE

    April 18, 2012 at 1:05 AM

  41. Ninaamini kuwa vijana wanao uwezo wa kuongoza nchi hii na hakuna haja ya kuhofia hilo, nchi hii iliongozwa na vijana watupu ambao ndio walijenga misingi iliyopo leo, hawa tunaowaona hawana jipya! Zito ninashukuru kwa wazo lako sidhani kama unakumbuka mwaka 2009 niliwahi kukwambia suala hilo maeneo ya masaki Dar, sasa umelifanyia kazi, pambana mkuu! lazima pawepo na nia then mengine yatafuata! aluta continua!

    Thomas Macha

    May 4, 2012 at 7:50 PM

  42. I think it was not the right time to declare his intention FOR PRESIDENTIAL RACE…………………..

    ISHMAEL LUYAGAZA

    May 11, 2012 at 1:52 PM


Leave a reply to DICKSON KIBONA Cancel reply