Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

NAKUAGAJE REGIA?

with 59 comments

Mh. Regia Mtema

 

Siku zote ninaamini katika sera za vizazi kufundana na kukabidhiana majukumu. Katika maisha ya kijamii ninaumizwa sana na kupotea kwa utamaduni wa wazazi kurithisha watoto wao masuala kama ufundi na hata majukumu ya kitamaduni kwenye mila na desturi zetu. Ndio maana hivi sasa kwenye vijiji vingi hapa nchini imekuwa nadra kupata mafundi Seremala wa kurithi ama Waashi pia. Kwenye Siasa Kizazi kinaposhindwa kuandaa kizazi kingine kuchukua jukumu la kuongoza kuna hatari kubwa ya Taifa kukosa viongozi walioandaliwa vema na hivyo kuongoza inavyopasa. Taifa huumia sana linapopoteza viongozi wanaoandaliwa kubeba majukumu mazito ya kitaifa.

Dada Regia Estelatus Mtema, Mbunge wa Viti Maalumu, Waziri Kivuli wa Kazi na Ajira na Mjumbe wa Kamati Kuu CHADEMA ni mmoja wa wanasiasa vijana waliokuwa wanafundwa kuchukua majukumu zaidi ya Taifa letu. Alikuwa anafundwa na Chama chake. Alikuwa anafundwa na Bunge (mafundo kutoka kwa vyama vyote na hasa Spika Anna Simamba Makinda). Alikuwa anafundwa na marafiki zake. Alikuwa anafundwa na Chama cha Walemavu Tanzania (CHAWATA). Alifundwa na Shirika la FES. Dada Regia alikuwa anafundika. Alikuwa ni Hazina kubwa kwa Taifa letu. Alikuwa na sifa za peke yake kabisa kulinganisha na wanasiasa wengine na hasa wanasiasa vijana. Nitaeleza.

Sijui ni kwa nini mama yangu Bi Hajjat Shida Salum amekuwa sasa anapata habari kwanza kabla yangu (yeye ndiye aliyenipa habari za msiba wa Mwenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga na Rafiki yangu kipenzi Shelembi).

Nikiwa nimepumzika sebuleni, nyumbani kwetu Tabata Bi Shida ghafla ananiuliza, umeongea na dada yako? Ilikuwa kama saa sita mchana hivi, yeye kasimama upenoni mwa ukuta ananiangalia macho makali. Nikashtuka kidogo maana amekuwa mgonjwa mgonjwa toka amerejea toka Hijja miezi kadhaa iliyopita. Najua akiniuliza hivyo ana maanisha nani (Mhonga Said Ibrahim Ruhwanya), nikamjibu sijazungumza naye, kunani? Akaniambia piga simu makao makuu nasikia kuna Mbunge wetu wa Viti Maalumu amepata ajali. Mara moja nikashika simu kumpigia ndugu Msafiri Mtemelwa. Alichoniambia sikuamini. Eti kwamba Regia amepata ajali na amefariki muda mfupi uliopita. Nikamwita rafiki yangu Hatibu Mchange anayeishi jirani yetu kumwambia aje ili anisindikize makao makuu ya chama. Kisha nikamjulisha Bi Shida kuhusu msiba wa rafiki yake na mwanae Regia. Nikamwacha akilia sana. Sikumpa pole wala kumtaka asilie maana kwanza sikuamini kabisa kwamba ni kweli Regia ametutoka. Nikasema mpaka nikamwone mwenyewe kwa macho yangu.

Siku nne kabla ya kifo chake Regia alikuja nyumbani kumsalimu mama yetu (Bi Shida siku zote alimwona Regia kama mwanaye na yeye Regia alimheshimu mama yangu kama mama yake mzazi kabisa). Wakati namsindikiza akaniambia, ‘ naona umeshikia bango suala la ajira kwa vijana. Nakuunga mkono na unipe ‘data’ za kutosha ili kupitia Wizara yangu nilisukume suala hilo kwa nguvu zaidi’. Tukakubaliana. Tukakumbatiana na kuagana. Yeye alikuwa ameambatana na kulwa wake Remija. Kumbe ndio nilikuwa namuaga moja kwa moja dada yangu Regia Estelatus Mtema, mwanasiasa kijana asiye na woga na jasiri haswa. Hii ndio sifa yake kubwa kuliko wanasiasa wengi vijana. Ujasiri!

Regia hakuwa mwanasiasa wa asili ama kurithi. Aliamua kuingia kwenye siasa kwa kwanza ushahiwishi wa ndugu David Kafulila ambaye walikutana huko kwenye Programu ya Mafunzo kwa vijana (YLTP) inayoendeshwa na Shirika la Friedrich Ebert Foundation (FES), mimi ni mwanzilishi wa Programu hii katika YLTP 1. David akiwa mwakilishi wa CHADEMA na Regia akiwa Mwakilishi wa CHAWATA katika YLTP 6. Regia alishawishika na kuingia CHADEMA, chama kikamweka kitengo cha Vijana kama Afisa. Wakati fulani kukatokea matatizo kati yake na Afisa mwenzake ndugu Ali Omar Chitanda kuhusu namna ya kufanya kazi. Regia akiwa na hoja kwamba chama kinajenga ushawishi kwa wasomi na hivyo vijana wasomi tu ndio waendeshe kitengo kile. Wakawa hawawezi kufanya kazi na mwenzake kabisa. Nikiwa Naibu Katibu Mkuu wa chama nikachukua maamuzi ya kumhamisha Regia na kumpeleka kuwa Afisa wa Mafunzo chini ya Kurugenzi ya Mafunzo na Oganaizesheni inayoongozwa na ndugu Benson Kigaila Masalamakali. Regia kwa ujasiri akaniandikia ujumbe mfupi wa simu ‘uamuzi wako sio sahihi’. Sikumjibu bali nikamwita Ofisini siku ya Pili yake. Nikamweleza namna ambavyo chama kinahitaji kada zote na kwamba wasomi wa vyuo vikuu waje kwenye chama wakijua pia kuna maafisa ambao si wasomi na wana mchango mkubwa katika harakati za kidemokrasia. Nikampa mifano ya namna mtu Kama Samora Machel alivyochaguliwa kiongozi wa FRELIMO ilhali kulikuwa na wasomi zaidi yake kama Joachim Chisano au hata mkewe Graca Machel. Regia alinielewa vizuri sana na mkutano ukaishia kutaniana kuhusu namna ya mitindo ya uongozi. Regia hakuficha kama hakupenda jambo na wala hakuwa anaangalia cheo cha mtu. Alisema anachokiamini na mengine yatabaki mjadala wa baadaye.

Ujasiri wake wakati mwingine ulimletea shida kwa wakubwa zake lakini hakuna hata mmoja aliyetilia shaka mapenzi yake kwa chama chetu. Hakujali kuudhiwa na alikuwa tayari kukilinda chama muda wote. Huu ni mfano wa pili wa Ujasiri wake kisiasa.

Wakati wa uchaguzi Mkuu wa nchi mwaka 2010 Regia alikwenda kugombea Ubunge katika Wilaya ya nyumbani kwao Kilombero. Watu wengi hawakumpa nafasi kubwa ya kushinda. Aliliandaa jimbo lake kwa mikutano ya mara kwa mara. Alishinda kura za maoni katika mchakato wa ndani ya chama. Katika kikao cha Kamati Kuu mmoja wa Wakurugenzi wa Chama akasema tunaye mgombea mwingine mzuri sana, Mwanasheria. Regia akaombwa kukaa pembeni. Akakubali. Kamati Kuu ikampitisha mtu ambaye hakwenda kwenye kura za maoni na wala hatukuwa tunamjua maana tuliambiwa na mtu tunayemwamini kwamba ni mgombea mzuri. Regia hakufurahishwa na uamuzi ule lakini kwa heshima na utiifu wa hali ya juu akakubali kutogombea. Siku za kurejesha fomu za kugombea zilipokuwa zinakwisha yule mgombea akatoa nje. Hakuonekana, kwa sababu mbalimbali ambazo sisi tuliokuwa mbali na Dar es Salaam na Morogoro hatuzijui. Chama hakikuwa na namna isipokuwa kurudi kwa Regia kumwomba aokoe jahazi. Regia hakusita. Akaendesha kampeni za uhakika akiwa hana mali wala jina kisiasa. Akaaminiwa na watu wa Kilombero. Akapata kura nyingi sana ambazo hata zilileta utata wa uhalali wa matokeo ya uchaguzi katika Jimbo lile. Ujasiri na nidhamu ya namna hii ni nadra sana kwa wanasiasa sio tu vijana hata waliobobea kwenye siasa. Huyu ndio Regia. Ndiye tunamsindikiza kwenye nyumba yake ya milele. Regia mwenye upendo wa dhati kwa watu aliowapenda. Regia aliyekuwa tayari kusaidia kwa hali na mali wenzake wanapohitaji msaada. Hii ni sifa yake ya nyingine ya kipekee.

Mara baada ya Uchaguzi Mkuu na yeye kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Spika alitugawa kwenye Kamati Wabunge wote. Kazi ya kwanza ya Kamati hizi ilikuwa ni kuchagua wenyeviti na makamu wao. Regia alijua mimi napenda kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (uwekezaji umma). Hata hivyo alijua nina wakati mgumu sana kutokana na mazingira ya kisiasa yaliyokuwapo wakati ule kati ya Wabunge wa CCM na CHADEMA. Regia ni Mbunge pekee (ukiachana na wajumbe wa kamati ya POAC kutoka CHADEMA) aliyezunguka nami usiku kucha na kupiga simu kwa kila Mbunge mjumbe wa Kamati yangu kuniombea kura. Mbunge mwenzangu na Rafiki yangu wa karibu kutoka Ludewa Deo Filikunjombe atamkumbuka Regia kwa aina ya kampeni aliyopiga. Deo aliniambia kwamba alipokea simu ya mwanamke anaongea Kipangwa (moja ya Lugha ya watu wa Ludewa). Mwanamke yule mwenye sauti nyembamba na ya kutulia alikuwa anamwombea kura Zitto kuwa mwneyekiti wa POAC. Deo alifurahishwa na namna Regia alivyoweza kutumia lugha ya nyumbani kwao kuniombea kura. Hata tulipopata taarifa kwamba Kamati ya Wabunge wa CCM imeamua kwamba atakayepewa kura sio mimi, Regia alinitia moyo na kuendelea na kampeni. Asubuhi ya siku ya kura alimpitia kila mjumbe wa Kamati POAC aliyemwona na kumkumbusha kunipa kura hata kama CCM imewakataza. Nilimcheka sana Regia kwa kumwambia wewe sio mzoefu hapa. Hao wakishakaa ndio maamuzi hayo. Akaniambia hapana watabadilika. Ghafla Waziri Mkuu akatangaza kikao kingine cha Wabunge wa CCM na huko wakaelezwa kwamba kamchagueni Zitto. Ningekata tamaa bila kuendelea na juhudi usiku kucha kama nilivyoshauriwa na regia kwa kweli nisingeshinda nafasi ile. Regia alikuwa mtu wa kwanza kumjulisha matokeo ya uchaguzi nilipopata kura 13 kati ya 15 zilizopigwa. Huyu ndiye Regia ambaye alikuwa na uwezo wa kufanya kila mbinu ili mwenzake apate msaada. Ni lazima watu watoe machozi. Ni lazima Wabunge watoe machozi. Ni lazima wana CHADEMA wamlilie. Mimi sitawafuta machozi na nimekataa kulia.

Kikao cha mwisho cha chama ambacho nilishiriki na Regia nilihudhuria kwa muda mfupi sana. Wenzangu watakumbuka mengine katika kila kikao kile. Mimi ninakumbuka moja tu ambalo ni moja ya sifa pekee aliyokuwa nayo na wanayo wanasiasa wachache sana na hasa wanasiasa vijana (ambao hupenda zaidi siasa za kuridhisha kwa kusema watu wapendacho). Regia alikuwa na uwezo mkubwa wa kusema usichopenda kusikia. Alisema tu. Katika kikao kile wajumbe na Wabunge walikuwa katika ‘emotion’ sana kuhusiana na muswada wa mchakato wa kuandika Katiba. Mjadala ulikuwa mkali sana. Mwenyekiti wetu akampa nafasi Regia aseme. ‘mimi nashauri tuombe kuonana na Rais Kikwete’ yalikuwa ni maneno yake makali kupenya kwenye ngome za masikio ya wengi na yalipokelewa kwa mguno mkubwa. Mwenyekiti akaamrisha wajumbe na Wabunge watulie kwani Regia ana haki ya kutoa maoni yake. Mimi niliondoka baada ya muda mfupi maana nilikuwa ndio nimetoka nchini India kwa matibabu na nilikuwa na masharti ya kupumzika muda mrefu. Ushauri wa Regia (pamoja na wajumbe na viongozi wengine wa chama walioshauri ama waziwazi au kwa chinichini) ndio uliofuatwa na sasa kumekuwa na mazungumzo ya mara kwa mara ya viongozi kuhusu sheria ile ya mchakato wa kuandika Katiba. Huyu ndio dada Regia. Maisha mafupi lakini mafunzo makubwa katuachia vijana wenzake kwenye medani ya siasa.

Nakuagaje Regia?

Nilikataa kuamini kuwa umekufa. Nikasema mpaka nikuone.

Nilipofika Tumbi, nikasema hujafa na wala siingii ‘motury’ kukuona.

Sasa eti nakuandikia Tanzia . Kwa nini nikuage?

Halafu nakuagaje REGIA?

Ukikutana na Shelembi Magadula, mwambie kile kiti chake cha udiwani tulikitunza, akija atakikuta. Ukikutana na Chacha Wangwe Mwambie bado tunaendelea na harakati Nyamongo. Ukikutana na Amina mwambie asilie tena vijana wengi wameingia Bungeni na sasa wanaelekea Ikulu.

Ukikutana na Bibi Titi mwambie sasa wanawake hata wanawake walemavu wanaweza bila hata kuwezeshwa, wanajiwezesha.

Nakuagaje dada yangu mpenzi? Haya.

Mungu atupe subira.

 

Kabwe Zuberi Zitto, Mb

DSM, 16 Januari 2012.

Written by zittokabwe

January 17, 2012 at 8:56 AM

59 Responses

Subscribe to comments with RSS.

 1. pengo lake sijui ni nani wa kuliziba

  munga (@munga2)

  January 17, 2012 at 9:20 AM

  • Nimeguswa na Tanzia yako Mhe. Zitto, mimi pia namlilia Regia kama kiongozi kijana lakini zaidi ni School mate wangu Forodhani Secondary School nikiwa nimemtangulia darasa moja ila tulikuwa shifti moja na kila siku ilikuwa lazima nimuone. Wakati ule nilikuwa Katibu Mkuu wa Serikali ya wanafunzi alikua mpole na mtiifu hakupenda makundi ila alikuwa mcheshi na alijichanganya na wenzake pasi kujali ulemavu wake. Mungu ailaze roho ya Regia Mtema peponi, Amina.

   Christopher Stephen Njau
   Mwenyekiti wa UVCCM – Kata ya Miburani
   Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam.

   Christopher S. Njau

   January 18, 2012 at 3:52 PM

 2. Pole sana my brother,bwana alitoa na bwana ametwaa jina lake lihimidiwe.apumzike kwa amani.Amina

  Oscar george

  January 17, 2012 at 9:20 AM

 3. This is very touching… May her beautiful soul rest in enternal peace. AMEEN

  Teddyliscious Kaegele

  January 17, 2012 at 9:24 AM

 4. Pole sana Chadema, pole sana Tanzania na pole sana familia ya marehemu Regia. Inaumasana kupoteza kiongozi ambeye bado ana nguvu za kulitumikia taifa. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi

  Sarah Tesha

  January 17, 2012 at 9:27 AM

 5. Ni kweli tumempoteza mtu muhimu

  Ezra kavana

  January 17, 2012 at 9:28 AM

 6. Nimeguswa na maneno yako.hatuna zaid la kupinga..Mola ndio mjuzi wa kila kitu..tumuombe dada yetu Mbunge wetu hapumzike kwa amani…Inna li llah wa inna illah rajiun

  Fatma

  January 17, 2012 at 9:35 AM

 7. Zitto Kifo cha dada Regia kimetupa majonzi mengi Mungu atusaidie katika wakati huu ambao tunawaza juu ya harakati zake za mapinduzi ya kisiasa.R.I.P

  Elias Chausi

  January 17, 2012 at 9:37 AM

 8. inauma sana kumpoteza kijana mahiri kama huyu, tena mwenzetu na dada yetu Regia, Mungu ailaze roho yake pema tena peponi japo pengo lake ni vigumu kuzibika lakini Mungu mkubwa atatenda.

  Oscar Baruti

  January 17, 2012 at 9:47 AM

 9. mmm mungu ailaze roho yake mahali pema peponi…………..ameeeeeeeeeeeeeeeeeen

  MSEMO RAMLA

  January 17, 2012 at 9:52 AM

 10. Rest in peace mpambanaji wetu

  Edson Z Mushumbusi

  January 17, 2012 at 9:59 AM

 11. Nataman nisingesoma hapa,inaniumiza kumjua vizuri wakati ndo hayupo tena imeniumiza lakini nashukuru nini ntasema kitakachofaa zaidi ya kumwomba mungu akupokee kwenye raha ya milele,tunajua kimwili hatupo nawe lakini ki roho tupo pamoja na kwa sababu kiroho tupo pamoja basi roho yako iendelee kututia nguvu na ujasiri kama wako kama ambavyo kaka zitto ameweza kutanabaisha,TUTAKUPENDA NA KUKUKUMBUKA DAIMA PUMZIKA KWA AMAN NA USIJALI ZITTO ATAKUAGA TU,BYE DA REGIA byeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeee!.

  John Rogath Xavery Nguzo

  January 17, 2012 at 10:04 AM

 12. Ni ngumu sana kuamini, lakini ndio hivyo tena. Pole sana Ziito.
  Mimi naamini kila mtu ni pekee na hakuna atakayeweza kuziba pengo la mwingine anapoondoka. Tulimpenda sana Regia, tunaamini Mungu atakupa tumziko la Milele

  Colly

  January 17, 2012 at 10:24 AM

 13. RIP jemedari! Njia yetu ni moja!

  DAniel

  January 17, 2012 at 10:43 AM

 14. Muheshimiwa kiukweli nimesoma kwa utuluvi sana ulichokiandika juu ya dada yetu REGIA mpaka nimejikuta nadondokwa na chozi. Ila katika hali ya kiubinaadam mwenzako anapotangulia mbele ya haki cha kwanza kabisa ni kumshukuru Mungu na kumuombea kwani ni maombi tu peke yake ndiyo yanayoweza kumsaidia kwa wakati hu. Nihitimishe kwa kusema “INA LILAH WA INA ILAIH RAJ UN”

  Chapa S. Magotti

  January 17, 2012 at 10:45 AM

 15. jamani, machozi yananitoka

  masai

  January 17, 2012 at 10:45 AM

 16. Kweli dada Regia tutakukumbuka daima,,,,tutaendelea kufuata harakati zako ipo siku tutakutana tena……

  Keneth Runji

  January 17, 2012 at 10:52 AM

 17. Mungu amrehemu

  Thomas B Mwamfupe

  January 17, 2012 at 11:04 AM

 18. Pole sana Mh. tuzidi kumuombea apumzike kwa aman kwani wote tupo safari moja!! Let her soal Rest in Peace!! tutamkumbuka daima..

  Jane Mwangomale

  January 17, 2012 at 11:08 AM

 19. sisi tulikupenda ila Mungu amekupenda zaidi

  Winner

  January 17, 2012 at 11:09 AM

 20. Pole sana kaka zito na watanzania,kwani tumepoteza moja kati ya viongozi vijana mwenyeu uwezo na ujasiri mkubwa katika kusimamia mambo ya msingi katika taifa.mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.amina

  Robert l mollel

  January 17, 2012 at 11:09 AM

 21. Kifo cha mwanadamu hakika kitaacha simanzi hasa ukikumbuka mazuri yake. Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi.

  Mvumo A. Balati

  January 17, 2012 at 11:10 AM

 22. Kwa uzuni na majonzi, nasema ”Pole” kwa familia, ndugu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo, pia kwa waTanzania wote wanaogusa na kupotelewa mwanasiasa wetu wa Mrengn wakati Dada Regia.

  Mjema Abdalah A.

  January 17, 2012 at 11:23 AM

 23. it pain ,let us recur and do on it to her good she left.

  philipo msengi

  January 17, 2012 at 11:34 AM

 24. It is turf to swallow But God has made his mark to be know..

  Rest in Peace dada yetu… Tutafuata njia zako..

  Martin Kessy

  January 17, 2012 at 11:36 AM

 25. wewe ndio shujaa wa kweli, hakika sisi na chama chetu tutakukumbuka daima. ushauri wangu kwa chama ni kwamba tutenge siku maalum ya kuwakumbuka mashujaa wetu hasa waliokitetea chama kwa nguvu zao, akili zao na hata mali zao. Ikiwezekana kabisa Jan 14 iwe siku ya kumuenzi dada yetu na kipenzi chetu kwa Taifa na chama chetu pia. Buriani Regia Mtema. Bwana ametoa na bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Kwa tunaosoma Bible maanadiko yanasema ….kufa ni faida na kuishi ni Kristo. Amen

  Winner

  January 17, 2012 at 11:38 AM

 26. KWELI NI MSIBA WETU WOTE POLENI SANA FAMILIA YA MBUNGE WETU TUKO NYUMA YAKO DADA REGIA TUTAYAUNGA MKONO NAKUYAENDELEZA YALE YOTE ULIYO TUACHIA DADA REGIA MUNGU AILAZE MAALI PEMA PEPONI DADA YETU

  ALFRED SWAI

  January 17, 2012 at 11:38 AM

 27. R.I.P R. MTEMA.

  philipo msengi

  January 17, 2012 at 11:44 AM

 28. Da nimesoma kwa makini sana kaka ZITTO huzuni imeongezeka sana juu ya kumpoteza dada yangu Regia basi haina jinsi make wote ni safari moja ila….

  Andrew Richard Lwanda

  January 17, 2012 at 11:59 AM

 29. Hakika Kizuri hakiishi maana jinsi dada huyu alivyokuwa anashika kasi katika siasa ilikuwa hakuna upinzani kwa kushika jimbo 2015,lakini pia ni moja kati ya wabunge wachache wa viti maalumu waliokuwa wana tabia ya kuchangia hoja mara kwa mara bungeni hivyo alikuwa na ujasiri wa pekee kidogo.

  Kazi ya Mungu haina makosa,Mungu ailaze roho ya marehemu peponi,Ameni.

  Alex Ntegeye
  Kiganza-Kigoma

  Alex Ntegeye

  January 17, 2012 at 12:39 PM

 30. Nilipokuona Karimjee sikutaka hata kukusalimia Zitto maana nilikuwa na simanzi sana. Regia ndiyo huyo tumemuaga. Tusonge mbele!

  Harry James

  January 17, 2012 at 12:44 PM

 31. Very emotional! Inauma lakini lazima tukubali mapenzi ya Mungu

  Shagihilu

  January 17, 2012 at 12:54 PM

 32. haya ni maisha kaka angu! kweli 2mepoteza jembe la ukweli kwasisi 2limfahamu kwa jina la mama wa koo saba ndani ya serikali! 2nawaomba viongozi we2 wa chadema muwe na moyo wa uvumiliv hasa kwa kipind hiki kigumu 2lichokuwa nacho! ”RAHA YA MILELE UMPE EE BWANA NA MWANGA WA MILELE UMWANGAZIE APUMZIKE KWA AMANI AMINA”

  Floritha osward

  January 17, 2012 at 1:49 PM

 33. Mh. Zitto, binafsi, niungane nawe kukiri kwa dhati ya moyo wangu kwamba kwa hakika huu ni msiba mkubwa kwa taifa, kwa chama na kwa familia ya Mbunge shupavu marehemu Regia Mtema. Taifa limepoteza kiongoz mahiri ambaye alikuwa na mchango mkubwa kwa ustawi wa watanzania wa leo na kizazi kijacho. Kadhalika Chama kimepoteza mchezaji muhimu ambaye wakati wote hakusita kutumia muda wake, juhudi na maarifa katika kujenga, kuimarisha na kuendeleza chama kwa maslai ya taifa. Mchango wake ulikuwa ni nguzo muhimu kwa wakati tulionao na kwa maendeleo ya baadae ya chama. Aidha kwa familia yake, ninashindwa kupata neno ambalo litabeba uzito wa pigo lililowapata. Dada Regia kwao alikuwa ni msaada na nguzo muhimu ya familia. Hivyo, kwa namna ulivyojitahid kuonesha umahiri, ushupavu na uzalendo wa dada Regia, sina budi kusema pengo la dada Regia halitaweza kuzibika. Ijapokuwa kimwili hauko nasi tena ila kiroho tutakuwa nawe. Daima watanzania watayaenzi na kuendeleza mawazo yako chanya ili yawe msaada kwa ujenzi wa jamii ya watanzania. MUNGU AILAZE MAHALA PEMA PEPONI ROHO YA MAREHEMU MH. REGIA: AMEEN.

  Jabiri Omari

  January 17, 2012 at 2:40 PM

 34. Hakika taifa limepoteza nguvu kazi ambayo ndio kwanza ilikua imeanza kujidhihirisha ni kiasi gani inahitajika kwa taifa. Mimi naona msiba huu si wa familia na ukoo wa Mtema na CHADEMA tu, bali ni taifa lote; tena hususani vijana ambao walikua wanajifunza mengi sana kutoka kwa Regia.

  Mwanadamu unaweza kusema mambo mengi sana pale unapoondokewa na ndugu, jamaa na marafiki, lakini jambo la kuzingatia ni kutokumkufuru Mungu; nami naomba niishie hapa.

  Ninachoweza kusema ni dada Regia endelea kupumzika kwa amani katika makao yetu ya kudumu. Ninatumai siku moja nitaungana nawe huko.

  Amina.

  Mathew Bukhi

  January 17, 2012 at 3:17 PM

 35. umenitoa machozi mheshimiwa! R.I.P Regia Mtema!

  Elia Kisigila

  January 17, 2012 at 3:23 PM

 36. Inauma sana lakini sisi hatuwezi kupinga, ombi langu naomba watanzania wote tumuenzi dada Regia kwa yote alio tutendea na mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi bwana alitoa na bwana ametwaa jina la bwana libarikiwe.amina

  david simwimba

  January 17, 2012 at 3:26 PM

 37. RIP

  DOTTO MONDO

  January 17, 2012 at 3:40 PM

 38. Bwana ni mwema wakati wote,tulimpenda sana dada Regia kwa msimamo wake aliokuwa nao katika chama lakini mungu amempenda zaidi,tunamwomba mungu aweze kutupa viongozi bora vijana kama dada Regia maana ameliacha pengo kubwa sana katika nchi hii.jina la bwana lihimidiwe milele Amina.

  HAPPINESS COSMAS

  January 17, 2012 at 3:41 PM

 39. INAUMA LAKINI HATUWEZI KUPINGA ,OMBI LA KWA WATANZANIA ,KATIKA KIPINDI HIKI CHA MAJONZI TUMUOMBE MUNGU ATUSAIDIE NI KWELI TULIMPENDA LAKINI MUNGU KAMPENDA ZAIDI, MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU MAHALI PEMA PEPONI,BWANA AMETOA NA BWANA AMETWAA JINA LA BWANA LIBARIKIWE.

  David Simwimba

  January 17, 2012 at 3:57 PM

 40. Pole sana kaka ama hakika umeonesha upendo wa dhati kwa mpendwa wetu dada Regina mungu ailaze roho yake kwa aman BWANA AMETOA NA BWANA ATWAA JINA LAKE LIHIMIDIWE

  Allan Shemahimbo

  January 17, 2012 at 3:57 PM

 41. May your soul rest in peace Regia,Mema ulofanya kwa nchi hii Utalipwa na Mwenyezi Mungu!

  Concessa

  January 17, 2012 at 4:55 PM

 42. mungu ailaze roho ya marehemu pema peponi

  hosea joseph

  January 17, 2012 at 5:19 PM

  • Pole sana kaka haya ndo mapenzi ya mungu ampe mapumziko ya milele amina

   Joseph Masaga

   January 18, 2012 at 1:26 AM

 43. Siwezi tena kuisoma message hii, maana sipo tayari kutokwa machozi kwa kazi ya Bwana!!
  Bwana ametoa, Bwana ametwaa na jina lake lihimidiwe. Mungu akupokee katika nuru ya uso wake na kuirehemu roho yako Amen!!

  Dennis Sasabo

  January 17, 2012 at 6:28 PM

 44. Zitto, umenigusa. Regia ametoa mchango mkubwa tumwombea dua RIP Regia

  Dan Welwel

  January 17, 2012 at 6:54 PM

 45. R.I.P Regia…gone too soon!

  Emmanuel

  January 17, 2012 at 9:41 PM

 46. R.I.P hon REGIA !!amen

  trishabellemarry

  January 18, 2012 at 8:52 AM

 47. Kweli ni vigumu kuamini na uchungu wake hausimuliki,Mungu anajua yote na yatupasa kumshukuru kwa kila jambo,Mungu ailaze roho ya marehemu Regia mahali pema peponi Amina.

  Benedict

  January 18, 2012 at 9:41 AM

 48. Sio rahisi kuamini Ndugu yangu mpendwa na Mheshimiwa wangu Mbunge Zitto Z. Kabwe. Imeishatokea. Naomba tufute majonzi na tufikirie kuziba hilo pengo. Tuko pamoja na tunaamini mabadiliko yataletwa na mawazo mapya ya wabunge vijana bila kujali itikadi za vyama vyao. Si vibaya mkiteuwa mtu mwengine wa jimbo la marehemu aendeleze mapambano. Poleni sana familia ya Regia Mtema, marehemu. Poleni sana CHADEMA. Poleni sana wapendwa wananchi wenzangu kwa ujumla. REGIA E. MTEMA pumzika salama. Lawama hazitatusaidia, tuungane na tuzidi kuomba. William Johnsami Mmanyema.

  WILLIAM Johnsami Mmanyema

  January 18, 2012 at 12:02 PM

 49. Inauma,ila ipo siku atafurahi huko alipo, tunakutegemea Zito na Vijan a wote!Mchange na wengine>

  abdu twaha

  January 18, 2012 at 1:02 PM

 50. Nilianza kumfahamu Regia katika kipindi cha kampeni ambapo kulikuwa na Kongamano la wagombea vijana kutoka vyama vyote pale Moven pick,alidraw attention za wote waliohudhuria kwa jinsi alivyoweza kujieleza.
  Nakumbuka mara nyingine nilikutana na mama Shida salum dodoma hotel akiwa amekaa na Mh Regia pamoja na mdogo wako wa Kike[simkumbuki jina lake] katika kipindi cha bunge mwanzoni tu baada ya Uchaguzi.Walinikaribisha kwenye kikao hicho nilivutiwa na maongezi yao.Hakika nilijiuliza mama zitto na Regia ni ndugu au marafiki?nikakumbuka labda wamekutana kwenye chama cha walemavu.Lakini hiyo haitoshi kuweka ukaribu waliokuwa nao.
  Kaka yangu ZITTO tumlilie lakini tukumbuke kumuombea kheri katika makazi yake ya milele lakini pia tuziandae nafsi zetu kwani ni safari yetu sote hasa ukichukulia mfano wa dada yako wa karibu bi Regia ambae ameondoka bila kuuguzwa na mtu yeyote,NI GHAFLA MNO.INA LILAH WA INA ILAIH RAJ UN”
  “Hakika sisi ni wake na kwake yeye tutarejea”

  Fatma..

  January 18, 2012 at 3:12 PM

 51. Pole Chadema, pole kambi ya upinzania Bungeni, poleni wabunge wanawake Bungeni, poleni wabunge vijana Bungeni, tulimpenda Regia lakini Mungu amempenda zaidi, kalale pema peponi, Amina.

  Christopher S. Njau

  January 18, 2012 at 3:56 PM

 52. hapo kaka umeongea

  noel nicholaus

  January 18, 2012 at 8:52 PM

 53. mheshimiwa Zitto nimeusoma utenzi wako kwa marehemu Regia, mifereji ya machozi inatililika machoni pangu, mwenyezi mungu amlaze mahali pema peponi amina

  Frank Theodory

  January 19, 2012 at 8:40 AM

 54. very sory brother.

  todo

  January 20, 2012 at 12:44 PM

 55. tanzia hii kaka Zitto,imenitoa machozijapo umesema umekataa kulia.Najua kwako kilio ni tanzia hii ndefu>M<ungu amlaze pema peponiAmen

  deusdedith kivyiro

  January 20, 2012 at 2:20 PM

 56. Pole sana Zitto kwa kumpoteza mwanasiasa, mwanachama mwenzio na na mtu wako wa karibu. Haikuumizi wewe pekee ingawa kwa kuwa ulikuwa naye karibu unaumia zaidi. Hilo ni pigo kubwa kwa taifa letu sisi kama vijana tunakila sababu ya kusikitika kwa kupotelewa na kiongozi muhimu kijana mwenzetu. Taifa lilimhitaji sana. Jambo la muhimu kukumbuka ni kwamba tunaishi muda mfupi tufanye kila lililo jema kwa Taifa letu katika siku tulizopewa na Mungu kuwa hapa duniani. Tusichoke kuandaa vijana kwani Mwenyezi Mungu haishiwi na vipaji kama hivyo atawainua wengine watakaoendeleza yale aliyoyapigania dada yetu mpendwa Regia.

  AUDRONICUS KIVYIRO

  January 20, 2012 at 3:26 PM

 57. umeonyesha hisia kali mheshimiwa. Bigup nasi tuko nawe

  Emmanuel Mayaya

  February 2, 2012 at 11:37 PM


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: