Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Uchumi wa Taifa hatarini: Mfumuko wa Bei tishio kwa Serikali, Wafanyabishara na Wananchi.

with 11 comments

=PRESS RELEASE=

Uchumi wa Taifa hatarini: Mfumuko wa Bei tishio kwa Serikali, Wafanyabishara na Wananchi.

Mfumuko wa Bei umezidi kuongezeka kama taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu inavyoonesha kwamba, wakati mfumuko wa bei mwezi Julai mwaka huu (Bajeti ya mwaka wa Fedha 2011/2012 ilipokuwa inaanza) ulikuwa asilimia 13, umefikia asilimia 19.2 mwezi Novemba. Hii maana yake ni kwamba, Bajeti ya Serikali iliyopitishwa na Bunge mwezi Juni 2011, imepunguza uwezo wa kununua bidhaa na huduma kwa takribani asilimia 6. Hii ni sawa na shilingi 780 bilioni kuyeyuka katika Bajeti katika kipindi cha miezi Minne tu ya utekelezaji wa wake. Kutokana na kasi ya ukuaji wa Mfumuko wa Bei ni dhahiri kwamba, itakapofika mwisho wa mwaka wa Bajeti Serikali itakuwa imepoteza kwa kiasi kikubwa uwezo wa kununua bidhaa na huduma kwa zaidi ya robo ya Bajeti yake.

Hali ni mbaya zaidi kwa wananchi kwani Mfumuko wa Bei za vyakula umekua kwa kasi kikubwa mno. Ofisi ya Takwimu imeonesha kuwa wakati mfumuko wa Bei za vyakula ulikuwa asilimia 14.8 mwezi Julai, umefikia asilimia 24.7 mwezi Novemba 2011. Ukilinganisha na bei za vyakula mwaka 2010, mwananchi amepoteza uwezo wa kununua chakula kwa zaidi ya robo katika ya Novemba 2010 na Novemba 2011. Jumla ya vyakula ambavyo mwananchi alinunua kwa shilingi 10,000 mwaka 2010, sasa atanunua kiwango kile kile kwa shilingi 12,500. Bei za vyakula zimeongezeka kwa kiwango hiki ilhali kipato cha mwananchi aghalabu kipo pale pale. Mwathirika mkubwa ni mwananchi wa kawaida wa kijijini ambaye mapato yake ni kidogo na hivyo sehemu kubwa huyatumia kununua chakula.

Ukiangalia kwa undani utakuta mfumuko wa bei wa bidhaa kama mchele, sukari, nyama na samaki umekua maradufu. Bei ya mchele imekua kwa asilimia 50, sukari asilimia 50, nyama asilimia 30 na Samaki kwa takribani asilimia 40. Bidhaa hizi zote ni muhimu sana kwa afya ya binadaamu na hasa watoto kwa upande wa vyakula vya protini. Tusipokuwa makini na kupata majibu sahihi ya tatizo la mfumuko wa bei za vyakula, wananchi wengi na hasa watoto watapata utapiamlo na Taifa kuingia gharama kubwa katika kuwapatia huduma ya afya.

Kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula, mfumuko wa bei wa mafuta ya taa na gesi asilia unapaa kwa kasi kama moto wa nyikani. Wakati mafuta ya taa yamepanda bei kwa asilimia 71 katika ya mwezi Novemba mwaka 2010 na mwezi Novemba 2011, bei ya gesi asilia imepanda kwa asilimia 35. Madhara ya hali hii ni makubwa mno maana wananchi watakimbilia kwenye matumizi ya mkaa na kuni, hata hivyo bei za mkaa zenyewe zimepanda kwa asilimia 24. Kwa hali hii, na kutokana na ukweli kwamba wananchi wengi wa Tanzania wapo kwenye mpaka wa umasikini na daraja la kati chini, juhudi za muongo mzima za kupunguza umasikini zitafutwa ndani ya mwaka mmoja tu.

Mfumuko wa Bei unasukuma Watanzania wengi zaidi kwenye dimbwi la umasikini, unapunguza uwezo wa Serikali kutoa huduma za jamii kupitia Bajeti na hata kutimiza mipango ya miradi ya maendeleo kama miundombinu ya barabara, umeme, bomba la gesi, madaraja nk. Mkakati mahususi unatakiwa kubadili hali hii. Hatua zifuatazo zinapendekezwa ili kuuhami uchumi na kupunguza upandaji wa kasi wa gharama za maisha.

1.     Kuongeza uzalishaji wa chakula kwa kuweka mbinu za kukuza uchumi wa vijijini ni njia mojawapo endelevu ya kupunguza mfumuko wa Bei hapa nchini. Serikali sasa iache maneno matupu kuhusu sekta ya uchumi vijijini kwa kuelekeza nguvu nyingi huko. Serikali iruhusu na ivutie kwa kasi na kutoa vivutio kwa wazalishaji binafsi wa Sukari na mpunga katika mabonde makubwa. Waziri wa Kilimo na Maafisa wake watoke Ofisini na kuhimiza uzalishaji mashambani, fedha zielekezwe kujenga miundombinu ya barabara vijijini.

Vyakula vilivyolundikana mikoa ya Mbeya, Iringa na Rukwa ambapo Serikali iliahidi kununua na kutotimiza ahadi yake vinunuliwe mara moja na kusambazwa mikoa yenye shida ya chakula kama Mwanza, Mara, Kagera na mikoa ya Kaskazini. Chakula kukuta msimu mwingine katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ni kashfa kubwa kwa Serikali na inaonesha Serikali isivyokuwa makini na maisha ya wananchi.

Wakati huu ambapo tunaweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa chakula, Serikali inunue chakula cha kutosha na hasa mchele na sukari kutoka nje na kukisambaza kwenye soko ili kupunguza upungufu wa bidhaa (scarcity) katika masoko.

Mfumo uliotumika kununua Sukari tani laki moja hivi karibuni usitumike tena kwani ulizaa rushwa ya hatari na ufisadi ambao haujaripotiwa kwenye kutoa vibali. Wizara ya Kilimo iruhusu wauzaji kutoka nje walete sukari nchini moja kwa moja na kununuliwa na Bodi ya Sukari kisha kuiuza kwa wauzaji wa Jumla. Mfumo wa kutoa vibali umeonesha kutokuwa na tija na kwa kweli kunufaisha maafisa wachache wa Wizara ya Kilimo na Bodi ya Sukari.

2.     Kitengenezwe kiwanda cha kutengeneza gesi ya matumizi nyumbani (LPG extraction plant) kwa haraka ili kupunguza bei ya gesi, kuepuka kuagiza gesi kutoka nje na hivyo kuokoa fedha za kigeni na kutengeneza ajira hapa nchini. Kupanda kwa bei ya gesi asilia kunatokana na kwamba Tanzania inaagiza gesi hii yote kutoka nje ilhali malighafi ya kutengeneza gesi ipo hapa Tanzania na kwa kweli huchomwa moto (flared). Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini liingie ubia na kampuni Binafsi ili kuwekeza katika kiwanda cha kuzalisha gesi hatimaye kushusha bei na hivyo kuwezesha wananchi wengi zaidi kutumia gesi kwa matumizi ya kupikia n.k, hivyo kutunza mazingira.

3.     Ushuru wote unaokusanywa kwenye Mafuta ya Taa upelekwe Wakala wa Nishati Vijijini ili kufidia kupanda kwa bei ya mafuta ya Taa. Mfumuko wa Bei katika bidhaa ya mafuta ya taa unatokana na uamuzi wa kuwianisha bei ya mafuta ya taa na diseli ili kuondoa tatizo la uchakachuaji wa mafuta. Tatizo limeondoka (au hatulisikii tena) lakini wananchi wanaumia sana. Uamuzi sahihi wa kisera ni kupanua huduma za umeme vijijini kwa kuipa fedha zinazotokana na ushuru wa mafuta ya taa Wakala wa Umeme Vijijini. Usambazaji wa Umeme Vijijini utaongeza shughuli za kiuchumi vijijini, kukuza uchumi wa vijijini, kuongeza mapato ya wananchi kwa kuongeza thamani za mazao yao na hivyo kupunguza athari za mfumuko wa bei.

4.     Sera ya Matumizi ya Serikali iangaliwe upya kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi yasiyo ya lazima, na kuelekeza fedha nyingi zaidi katika uwekezaji umma (public investments). Matumizi Mengineyo ya Serikali yanaongeza fedha kwenye mzunguko ama kwa kulipa watu wachache stahili mbalimbali kama posho n.k au kwa kununua bidhaa na huduma bila mpango, na hivyo kusukuma bei kuwa juu kinyume na uhalisia wa soko. Tafiti za mfumuko wa Bei Tanzania zinaonyesha kwamba sera za fedha na zile za matumizi (monetary and fiscal policy) zina nafasi kubwa katika kukuza mfumuko wa bei. Hivi sasa nakisi ya Bajeti inayopelekea Serikali kukopa kwa kwa kiwango kubwa inapandisha gharama za viwanda kukopa mitaji ya muda mfupi na hivyo kuongeza gharama za uzalishaji na kasha bei za bidhaa. Wizara ya Fedha ambayo mpaka sasa imekaa kama imeishiwa namna ya kufanya, inapaswa kuamka na kutoa maelekezo mapya kwa Wizara, Idara na Wakala za Serikali kuhusu namna ya kubana matumizi na kuziba mianya yote ya kukwepa kodi.

Hitimisho

Serikali imeonesha udhaifu mkubwa sana katika kusimamia uchumi katika nusu ya kwanza ya Bajeti ya mwaka 2011/2012 ambayo pia ni Bajeti ya kwanza ya kipindi cha pili cha Serikali ya awamu wa Nne. Kuna hatari ya dhahiri kwamba ifikapo mwezi Januari 2012 tutakuwa tumerejea mfumuko wa Bei wa kiwango cha mwaka 1992 (21.9%). Tusipochukua hatua za haraka tutafikia na hata kuzidi mfumuko wa Bei kiwango cha juu kabisa ambacho kilifikiwa mwaka 1994 (33%) na hivyo viwanda kushindwa kukopa kwenye Mabenki kwa mahitaji yao ya haraka ya mitaji ya muda mfupi, wazalishaji wadogo kushindwa kulipa mikopo yao kwenye Taasisi za fedha na hivyo kufunga uzalishaji, Shirika la Umeme kushindwa kabisa kulipa gharama za mafuta ya kuendesha mitambo na kipato cha mwananchi kutomudu gharama za za kila siku. Uchumi utadorora kabisa. Taifa litakuwa hatarini.

Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania na Wizara ya Kilimo na Chakula iamke kuhami uchumi dhidi ya adui namba moja, Mfumuko wa Bei. Huu sio wakati wa kupiga porojo, viongozi wafanye kazi zao, Wananchi wajitume.

Inabidi sasa turejee kauli mbiu za miaka 50 iliyopita za Uhuru ni Kazi. Tuseme Demokrasia ni Kazi. Demokrasia sio lelemama.

Ndg. Kabwe Zuberi Zitto, Mb

Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Waziri Kivuli Fedha na Uchumi

18 Disemba 2011

Written by zittokabwe

December 18, 2011 at 12:37 PM

11 Responses

Subscribe to comments with RSS.

 1. hii nchi sasa inaelekea pabaya tatizo n kwamba serikali yetu inapoambiwa k2 na wapinzani wao wanachukulia ka n upuuzi. Kwa hali 2liyofika serikali inatakiwa kushukua hatua madhubuti juu ya kuokoa uchumi wa nchi

  Danson Gadson

  December 18, 2011 at 1:26 PM

 2. That is very true Zitto..

  We all need to pull up together to address and achieve this.

  Martin

  December 18, 2011 at 1:47 PM

 3. Kamanda umezungumza hadi umenitisha, hawa jamaa (CCM) Me siwaelewi kabisa, hii siyo mara ya kwanza ya wewe kuwapa ushauri wa nn cha kufanya. Katika bajeti ya TAIFA ya 2011-2012 uliwashauri wakakataa ushauri wako. Nadhan hata leo huu ushauri ulioutoa hawatausikiliza. Hawa jamaa bila viboko hawaendi. Kilichobaki tuwabadilishie lugha tu. /kamanda ZITTO tupo pamoja/

  Mwanawavitto Kiraro

  December 18, 2011 at 2:03 PM

 4. Shukran kiongoz bora ndan ya karwne ye2 bal nasikitika kuwa ndan ya nchi ambayo ina wa2 wenye mchango mzur wa mawazo bt serikal yangu kuwa c sikivu kwa kujifanya inaøa kumbe kipofu,mawazo yako mazur na umewapa solutions za kutosha na pia usichoke kuwakilisha mawazo ya wananch nas ä pamoja nawe kuwaslisha mawazo mawazo ya kujenga nch

  Mwaipopo dickson

  December 18, 2011 at 2:31 PM

 5. Kwakweli hali nimbaya sana kwa ss kwawatanzania wote kama sisi wanafunzi wa vyuo vikuu tunaogitegemea wenyewe ombao serikali imetunyima mkupo huku tukishuhudia serikali ikichezea pesa zetu kwa matanuzi ya kawaida it real pain. what if we will react tz ppl!

  Emmanuel mtui

  December 18, 2011 at 2:49 PM

 6. Tuache longolongo tufanye maamuzi yetu kwa vitendo ili kuondoa umaskin kwa wananchi uliokithiri. Kweka sera katika mafaili haitoshi bila kuyafanyia kazi.

  Kaboyoka joseph

  December 18, 2011 at 3:15 PM

 7. Mhe.umeweza kuonyesha takwimu makini,maisha magumu kupindukia.Tena viongozi wasipolitazama suala hili vizuri,tunaenda kuliangamiza taifa,kwani nguvu kazi ya taifa hili(VIJANA) wameshindwa kupewa kipaumbele licha ya serikali kutoa ahadi lukuki ikiwemo kila kijana wa kitanzania atapata elimu lakini si kweli.mimi ni mmoja wapo wa wanafunzi walionyimwa mkopo,wakati nina sifa zote nasomea uhandisi,inatisha kama tunakosa elimu maisha yanapanda kiasi hiki what next?.wazazi wetu wanajifungulia kwenye sakafu,so painful.GO AHEAD LORD WILL BLESS YOU.

  JOSIAH I KAYENZEMALE

  December 18, 2011 at 11:21 PM

 8. Asante sana comrade zitto kwa kuzidi kuishauri serkal yetu hii yenye viongozi na watendaji wengi walioishiwa fikra. Hakika watz tunamshukuru mungu kwa kutupatia wazalendo kama wewe na wengine kibao ambao imani yangu inanituma kuamini kwamba mngepatiwa nafasi kuiongoza serikali ya tz hata kwa kipindi cha miaka mitatu, lazima mafanikio (au japo “dalili za mafanikio”) zingeonekana wazi. Hongera sana na Mungu akupe nguvu na moyo wa ujasiri ili kwa busara na ujuzi wako tuijenge Tz.

  Comrade zitto pamoja na hayo mm nahisi ripoti hii haijaosomwa na wengi. Ningeshauri utafute namna ya kupata jukwaa la kuweza kujadili ripoti yako hii ili watu waweze kupata mwamko na kujadili kwa pamoja juu ya nini kifanyike endapo halii hii ya mfumuko wa bei itazidi kuendelea ilihali upo uwezekano wa kuzuia au japo kupunguza mfumuko huu na ugumu wa maisha kwa wananchi endapo serikali itatimiza wajibu wake kwa kuyafanyia kazi maeneo uliyoyatolea ufafanuzi.

  Niwaombe watanzania wenzangu tuzidi kuchapa kazi kwa bidii kila mmoja ktk nafasi yake. Tusiishie kulalamika tu kuhusu ugumu wa maisha. Tuwajibike kwa nafasi zetu ikiwa ni pamoja na kuwahoji hawa wenzetu wa aina ya Ngd Zitto tuliowatuma waisimamie serikali kuhakikisha watz tuanaishi maisha tunayostahili kuishi ktk nchi yetu yenye rasilimamali lukuki. Wataznania tunapaswa kuamka, tumesinzia vya kutosha. Tuchape kazi kwa bidii LAKINI nashauri kwa MSISITIZO: Pamoja na sisi kuwajibika, Lazima tujijengee tabia na udhubutu wa kuwawajibishe viongozi wetu wa ngazi zote ili watimize wajibu wao. KAMA HAWAWEZI tuhakikishe wanakaa pembeni wanakaa watu walio na upeo wa nini kifanye ili kuisaidia nchi yetu. Mimi nimechoka, haya sio maisha hata kidogo. Hatuwezi kuwa tunataabika afu serikali na baadhi ya watendaji wake wanakula kuku kwa mrija bila hata kufanya kazi yenye tija.

  Mungu ibariki TZ, Mungu Mbariki Zitto na watu wote wote wa aina yake…

  Richard

  December 19, 2011 at 10:27 AM

 9. TANZANIA TUMEKWISHA. BADO TUNAHITAJI MAAMUZI MAGUMU. SERIKALI IMESHINDWA, SO TUAMUE SS WANANCHI WENYEWE. TUIGE MFANO WA MISRI NA KWINGINEKO

  Edgar V.K

  December 19, 2011 at 10:46 AM

 10. Chadema mnanini cha kuwafanyia watanzania ndani ya miaka 10 kama mtachukua nchi 2015??

  twihesage

  December 24, 2011 at 11:50 AM

 11. Naam kamanda 2napaswa kufanya maamuzi ye2 kwa vitendo

  Emmanuel Mayaya

  February 3, 2012 at 10:24 AM


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: