Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Ukiukwaji wa Kanuni za Bodi ya Kahawa Nchini

with 2 comments

MHE. SAID A. ARFI (k.n.y. MHE. KABWE Z. ZITTO) aliuliza:-

 Kwa mujibu wa Kanuni za Bodi ya Kahawa nchini, ni marufuku Kahawa kuondolewa kutoka Mkoa wenye kiwanda cha kukoboa ikiwa ghafi; Bodi iliagiza Kahawa ibanguliwe kwenye viwanda vilivyopo kwenye Mikoa ilikozalishwa na kuhifadhiwa, lakini Bodi hiyo imekuwa ikikubali kupokea Kahawa kutoka Kigoma bila kubanguliwa na hivyo kuvunja Kanuni zake:-

Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya ukiukwaji huo ambao unahujumu ushirika mkoani Kigoma?

 

NAIBU WAZIRI WA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Kabwe Zitto, namwombea Mheshimiwa Zitto na wote wanaougulia huko India, Mwenyezi Mungu abariki dawa zinazowahudumia.

Mheshimiwa Spika, sasa napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kabwe Zuberi Zitto, Mbunge wa Kigoma Kaskazini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tangu kilimo cha kahawa kianze mkoani Kigoma, kahawa yao ilisafirishwa kubanguliwa mjini Moshi kwenye kiwanda cha Tanganyika Coffee Curing Company (TCCCO). Mwaka 2004/2005 Chama cha Msingi cha Ushirika cha Kanyovu kilijenga kiwanda chake cha kubangulia kahawa huko Matiyazo ambacho kilikidhi ubanguaji wa kahawa yote ya Kigoma. Hata hivyo baadhi ya wanachama wa Kanyovu walijiengua kutoka katika ushirika huo na kuunda umoja wao kwa jina la KACOFA. Wilaya ya Kigoma ilitoa kibali kwa wakulima wanachama wa KACOFA kusafirisha kahawa yao kwenda kubanguliwa TCCCO Moshi. Hali kadhalika, TCCCO pia KACOFA wanapata huduma za mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani ambao haupo mkoani Kigoma.

Mheshimiwa Spika, ili kulinda uasili wa kahawa, Bodi ya Kahawa Tanzania inasimamia na kuhakikisha kwamba kahawa hiyo ya KACOFA inauzwa kama kahawa ya Kigoma bila kuchanganywa na kahawa ya Kilimanjaro kwa kutumia mfumo maalum wa ufuatiliaji yaani traceability.

Mheshimiwa Spika, wakulima wa Kigoma wanashauriwa kuanzisha mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani na kupunguza gharama za uzalishaji katika kiwanda chao ili kuwavuta KACOFA sasa kurudi kukoboa kahawa yao mkoani Kigoma.

 

MHE. SAID A. ARFI:

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ambayo hayakukidhi swali lililoulizwa; swali lilikuwa Serikali inatoa kauli gani juu ya ukiukwaji wa taratibu za Bodi ya Kahawa. Lakini, umetoa maelezo na hukutoa kauli ya Serikali juu ya ukiukwaji huo. Hawa viongozi wa Serikali wa Wilaya ya Kigoma waliotoa kibali kinyume na taratibu na kanuni za Bodi wanachukuliwa hatua gani?

Swali la pili; ikiwa hivyo ndivyo, je, sasa Wizara yako iko tayari mahala popote pale wakulima wanapotaka kujitenga na Chama Kikuu cha Ushirika wanaweza kufanya hivyo?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA:

Mheshimiwa Spika, suala la kahawa linatawaliwa na sheria ya kahawa ya mwaka 2001 pamoja na marekebisho yake, na utaratibu wake ni mrefu. Wadau wanaohusika hapo ni wengi; Halmashauri za Wilaya zinahusika. Na nimeeleza katika majibu yangu kwamba Halmashauri ya Wilaya ndiyo iliyotoa kibali na yenyewe nayo ina mamlaka yake ya kufanya hivyo. Lakini pamoja na hayo ni kwamba, nikijibu kwa pamoja na swali la pili lile la wanaotaka kujiengua katika ushirika ni hiyari, hakuna kulazimishwa kwamba wewe lazima uwe ushirika huu, sheria ya ushirika ndivyo inavyosema.

Sasa wale wanapoona kwamba sisi haturidhiki katika ushirika huu, wako huru kabisa kwa mujibu wa sheria kutafuta wanakoona kuna green pasture. Kwa hiyo, kwa maelezo yangu hayo, ninachotaka kusema ni kwamba ukitizama vizuri, hakuna waliokiuka hapa, hakuna makosa makubwa yaliyofanyika. Wale baada ya kuamua kujitenga, Halmashauri ilisoma sheria ikaona hapa tunaweza tukawaruhusu wakaenda, na wakaenda wakakuta mambo ni mazuri kule. Sasa ninachosema ni kwamba kule Kigoma tuboreshe utaratbu huu, tuweke utaratibu wa stakabadhi ghalani, tuwavutie KACOFA ili waweze kurejea kukobolea kahawa yao. Lakini, msimamo wetu ni huo kwamba kahawa ikobolewe katika eneo lile inapozalishwa ili kuweza kuwanufaisha wakulima.

Written by zittokabwe

November 12, 2011 at 2:11 PM

2 Responses

Subscribe to comments with RSS.

 1. Hapa Naibu Waziri yuko sahihi kabisa kwasababu mkulima yeye anachoangalia ni bei nzuri na mazingira mazuri ya kuuza kahawa yao. Mi nasema hivi kutokana na uzoefu wa kutoka wilayani Ngara. Kule wakulima wa kahawa hawafaidi bei ya kahawa na matokeo yake kahawa inaishia aidha Burundi,Rwanda au Uganda. Chama cha Msingi kipo na waliisha nunua mashine ya kukoboa kahawa lakini tangu ifungwe hakuna juhudi zozote za kununua kahawa kwaajili ya kuzikoboa. Ni miaka kama mitatu chama hakinunui kahawa na wakulima wanapewa ahadi hewa kuwa kahawa yao itanunuliwa na chama hicho. Lakini msimu ukifika hakuna kunachoendelea.
  Serikali inapoteza mapato kutokana na wakulima wa kahawa wilayani ngara kuuza kahawa yao burundi, rwanda na uganda.

  william Jotham

  November 13, 2011 at 6:53 AM

  • Serikali inapoteza mapato kwa kuwa imetelekeza vyama vya ushirika. Vimeachwa yatima kwa sababu viongozi hawaoni faida mifukoni mwao. wengi wa viongozi wa halmashauri za wilaya na wakuu wa wilaya hawasimamii ukuaji wa maendeleo ya ushika nchini kama sera ya maendeleo ya ushirika inavyoelekeza, na kwa manufaa binafsi, wana wanavunja sheria na kanuni zilizowekwa.

   Kuna faida kubwa kwa kahawa kukobolewa kwenye maeneo iliko zalishwa kwa mfano, gharama ya usafirishaji inakuwa imepungua sana, na zaidi sana inatoa ajira zaidi kwa wananchi wa maeneo husika katika ukoboaji.

   changamoto iliyotolewa na Naibu waziri haina budi kuchukuliwa kwa umakini na uharaka na mhe Zitto na wabunge wenzako, “Mheshimiwa Spika, wakulima wa Kigoma wanashauriwa kuanzisha mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani na kupunguza gharama za uzalishaji katika kiwanda chao ili kuwavuta KACOFA sasa kurudi kukoboa kahawa yao mkoani Kigoma.”

   LET US SHAME THE DEVIL JAMANI. WALE JAMAA WA KANYOVU WAKO SO COMMITTED, SERIKALI LAZIMA IBANWE KUWASAIDIA.

   Adam

   November 25, 2011 at 11:27 AM


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: