Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Muswada wa Marekebisho ya Katiba ujenge Mwafaka wa Kitaifa

with 14 comments

Zitto Kabwe[1], Mb

Kama kuna jambo moja ambalo huunganisha Taifa ni Katiba ya Taifa hilo. Katiba huweka misingi mikuu ya nchi na namna ya kujenga na kuendesha Taifa. Hivyo Katiba inapaswa kuwa ni matokeo ya mwafaka wa kitaifa kwenye masuala yote ya msingi ya nchi husika. Tanzania imekuwa ikiongozwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara. Kabla ya hapo kulikuwa na Katiba ya Uhuru ambayo ilitokana na Mwafaka wa wapigania Uhuru wa nchi yetu, baadaye Katiba ya Jamhuri ya Tangayika na kisha Katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kabla ya kubadili jina na kuitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ukiachana na Katiba ya Uhuru, Katiba nyingine zote hazikutokana na mwafaka wa kitaifa bali matakwa ya tabaka la watawala. Katiba ya kudumu ya mwaka 1977 ni zao dhahiri kabisa la utawala wa chama kimoja ambacho kilikuwa na dhamira ya kushika hatamu za uongozi. Kutokana na hali hii haikuchukua muda kwa wasomi mnamo mwaka 1983 kuanza harakati za kuifanyia mabadiliko makubwa. Mabadiliko hayo yalizaa kuwemo kwa Haki za Msingi za Binaadamu katika Katiba katika mabadiliko ya mwaka 1984, miaka saba tu toka kuandikwa kwa Katiba ya kudumu.

Takribani mwaka mzima huu kumekuwa na madai ya kuandikwa kwa Katiba mpya. Madai haya sio mapya kwani huibuka na kusinyaa kila baada ya uchaguzi Mkuu. Itakumbukwa kwamba miaka ya Tisini mwishoni kundi la vyama vya siasa liliunda Kamati ya Mabadiliko ya Katiba (KAMAKA) ili kudai kuandikwa kwa Katiba mpya. Hata hivyo safari hii sauti ya mabadiliko imekuwa ni kubwa sana kiasi cha Serikali kusikia na hivyo kupeleka Bungeni muswada wa Marejeo ya Katiba kwa lengo la kuandika Katiba mpya ya nchi yetu. Muswada huu umeleta kelele nyingi na manung’uniko mengi sana kutoka kwa makundi mbalimbali ya jamii kuanzia vyama vya siasa, viongozi wa dini na Asasi za Kijamii. Baadhi ya Asasi za Kijamii zimeunda Jukwaa la Katiba ili kuweza kuratibu vizuri juhudi za kuandikwa kwa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sababu kubwa ya kupingwa kwa muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 ni kwamba mchakato umewekwa kwenye Dola mno na hasa kwenye Urais. Rais anateua Tume ya kukusanya maoni, Rais anateua Bunge la Katiba nk. Watu wengi tungependa kuona mchakato unakuwa kwa wananchi zaidi. Serikali imefanya marekebisho kadhaa na kupanua wigo wa mjadala wa Katiba na pia kumhusisha kikamilifu Rais wa Zanzibar katika mchakato.

Baadhi yetu tunaona kama nafasi ya Zanzibar katika mchakato imepewa nguvu kubwa kupita kiasi. Ninadhani Zanzibar inastahili kupata nafasi hii katika mchakato wa Katiba. Jambo ambalo ni vizuri tulitilie maanani ni kwamba Muungano wa Mwaka 1964 ulihusisha nchi mbili huru zenye hadhi sawa mbele ya sheria za kimataifa. Linapokuja suala la kuandika Katiba ya Muungano, pande mbili za Muungano zinakuwa na hadhi sawasawa. Kwamba Zanzibar ishiriki kwenye masuala ya Muungano tu ni hoja inayojadilika iwapo tu Katiba ya Muungano ingetofautisha kinagaubaga taasisi za kimuungano na zisizo. Kwa mfano Sura ya Bunge katika Katiba ni lazima ijadiliwe na pande zote mbili ingawa Bunge wakati mwingine hupitisha miswaada ambayo sio ya masuala ya Muungano. Aina ya Muungano wetu inatulazimisha kufanya hivi tunavyofanya sasa. Mkataba wa Muungano ni lazima uheshimiwe kama ulivyo sasa.

Katiba mpya yaweza kuweka makubaliano mapya lakini muswada wa sasa ni lazima utambue nafasi halali ya Zanzibar kwa mujibu wa Katiba ya sasa na Hati za Muugano. Suala hili ni suala la kisheria na sio suala la idadi ya watu au ukubwa wa eneo la nchi husika. Nchi ya Ushelisheli yenye watu 80,000 ina nafasi sawa na Tanzania yenye watu 42 milioni katika SADC, AU na UNO. Zote zina kura moja tu. Huu ndio ukweli na hatuna budi kukubaliana nao.

Muswada unampa mamlaka Rais wa Tanzania na Rais wa Zanzibar kuteua Tume ya Katiba. Tume hii maRais hawatapata ushauri wa mtu mwingine yeyote  kwa mujibu wa kifungu cha (6) na vifungu vidogo (1), (2) na (3). Wanasiasa wakiwemo Wabunge, Wawakilishi, viongozi wa vyama wa Ngazi za Taifa, Mkoa au Wilaya hawatakuwa na sifa za kuteuliwa.

Inawezekana kabisa waandishi wa muswada walikuwa na mantiki ya kuuondoa mchakato kwenye mikono ya wanasiasa. Nia hii njema haikufikiriwa vizuri hata kidogo. Njia hii haijengi mwafaka. Tume hii sio ya Wataalamu, ni Tume inayopaswa kuwa na sura ya kitaifa. Nafasi ya wanasiasa katika mchakato wa kukusanya maoni ni muhimu sana katika kuhalalisha mchakato wenyewe. Tume lazima ionekane ni Tume ya Taifa na sio Tume ya maRais. Hivyo kipengele hiki cha kuwanyima sifa wanasiasa kinapaswa kufutwa katika muswada. Wabunge na Wawakilishi kwa kuwa ni sehemu ya Bunge la Katiba wasiwemo katika Tume, lakini viongozi wengine wa kisiasa wawe na haki ya kuteuliwa kuwa wajumbe.

Lakini pia Rais ateue Tume kutokana na maoni kutoka katika makundi yenye maslahi ya karibu na Katiba ya nchi na hivi ni vyama vya siasa. Ninapendekeza kwamba katika Wajumbe 30 wa Tume ya kukusanya maoni ya Katiba, 10 watokane na vyama vya siasa vyenye Wabunge kwa uwiano wa CCM 2, CHADEMA 2, CUF 2, NCCR 2, TLP 1 na UDP 1. Kila chama cha siasa chenye Wabunge kupitia kiongozi wake Bungeni kipeleke majina ya watu wanaowapendekeza kuwa katika Tume ya Katiba na kutokana na Mapendekezo hayo Rais atawateua kuwa wajumbe. Masharti mengine ya nusu kutoka kila upande wa Muungano yazingatiwe.

Muswada unapendekeza kuwepo kwa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume. Kifungu cha cha 7 kifungu kidogo (1), (2) na (3) kinaweka utaratibu wa kupatikana kwa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume. Muswada unasema UTEUZI wa Mwenyekiti na Makamu utazingatia kwamba mmoja atoke uapnde mmoja wa Muungano na mwingine upande wa Pili wa Muungano. Ingawa Muswada hausemi waziwazi lakini ni dhahiri kwamba Mwenyekiti wa Tume atateuliwa na Rais baada ya kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar. Sitaki kujenga hoja kwamba Mwenyekiti na Makamu wachaguliwe na wajumbe wa Tume kutoka miongoni mwao lakini ni dhahiri Mwenyekiti wa Tume anapaswa kuwa mtu mwenye heshima kubwa hapa nchini. Ningependekeza kwamba maRais wateue Wenyeviti wenza badala ya Mwenyekiti na Makamu wake ili kuweka nafasi sawa kwa pande mbili za Muungano. Hapa nchini tunao Watanzania ambao wamefanya kazi iliyotukuka katika nyadhifa mbalimbali na sasa ni wastaafu wasio na nia yeyote ya madaraka ya kisiasa wanaoweza kuongoza vizuri kabisa Tume hii. Ni pendekezo langu kwamba Dkt. Salim Ahmed Salim na Jaji Joseph Sinde Warioba wawe wenyeviti wenza wa Tume ya Katiba. Uzoefu wao katika uongozi na kuijua kwao nchi kutasaidia sana kuhakikisha kwamba mchakato wa kukusanya maoni na kisha kuandika Katiba unakuwa na mafanikio kwa kuzingatia misingi ya Taifa letu.

Muswada unapendekeza kwamba Hadidu rejea za Tume zitolewe na maRais. Kifungu cha nane na muswada kuhusu hadidu rejea nadhani hakina mantiki sana. Madhumuni ya muswada yanasema pamoja na mambo mengine muswada unaweka masharti kuhusu Hadidu rejea za Tume. Wakati huo huo muswada unasema Hadidu rejea zitakuwa ni hati ya kisheria itakayozingatiwa na Tume katika kazi zake.

Mantiki ni kwamba Hadidu rejea zinapaswa kuwa sehemu ya Muswada kama ‘schedule’ ili kuzipa nguvu ya kisheria badala ya tangazo katika gazeti la Serikali. Hadidu rejea zikiwa ni sehemu ya Muswada zitajadiliwa na Bunge na kupitishwa hivyo kuwa ni jambo ambalo limefikiwa kwa mwafaka wa wawakilishi wa wananchi.

Muswada unataka uamuzi wa kura ya maoni kuhusu Katiba uwe ni kukubaliwa na nusu ya Watanzania katika kila upande wa Muungano. Nadhani hapa tunacheza na Katiba ya nchi. Katiba ya nchi inapaswa kukubaliwa na theluthi mbili ya wapiga kura wa pande zote za Muungano yaani kila upande theluthi mbili. Hii itaipa Katiba ‘legitimacy’ na hivyo kuheshimiwa na wananchi na watawala. Kuna woga gani uliopo kutaka katika ikubalike na nusu ya wapiga kura? Mifano ya nchi nyingi duniani Katiba inapaswa kukubaliwa na theluthi mbili ya wapiga kura. Hata jirani zetu wa Kenya ilikuwa hivyo na hata kura ya maoni kuhusu mwafaka huko Zanzibar ilikuwa hivyo. Kwa kuwa Katiba ni chombo cha mwafaka wa kitaifa, muswada utamke kwamba Katiba mpya itakuwa imepita iwapo theluthi mbili ya wapiga kura watapiga kura ya ndio.

 mwisho


[1] Zitto Kabwe ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na Naibu Katibu Mkuu CHADEMA. Maoni haya ni maoni binafsi ya Zitto na kwa vyovyote vile hayawakilishi msimamo rasmi wa CHADEMA au Kambi ya Upinzani Bungeni.

Written by zittokabwe

November 7, 2011 at 11:52 AM

14 Responses

Subscribe to comments with RSS.

 1. Atakaye shindwa kuelewa maelezo haya yaliyo fasaha, basi hata angeweka uelewa kwenye ubongo hayatamkaa..
  naunga mkono hoja kaka>

 2. Ok uko right ila nina waswas kama kwel mchango wako wataupokea ukizingatia wewe upo kambi ya upinzani. Mwisho vp hali yako kiafya unaendeaje?

  Mwl.mkiza

  November 7, 2011 at 12:16 PM

 3. Uko sahihi Zitto kwani sioni haja ya rais ndoo awe mwenye mamlaka ya kial kitu kwani ndoo mwanzo wa kutunga katiba ya matakwa ya chama kimoja.

  fredy Chokela.

  November 7, 2011 at 3:22 PM

 4. Mi naunga mkono hoja hii sana sana kwenye wenyeviiti wenza ambao umetaja Jaji mstaafu Joseph Wrioba na Salim Ahmed Salim, hawa viongozi nina IMANI nao na ni wazoefu ktk uongozi wa Tz. Halafu kwanini serikali ing’ang’anie raisi awe kila kitu? Rais ni mwenyekiti wa ccm hivyo ataelemea kwenye chama chake. Jamani hii katiba tunayoitaka ni ya WATANZANIA wote ambao ni wanachama wa vyama vya siasa na wasio wanachama wa vyama vya siasa. Uwakilishi ktk tume ya kuratibu maoni ya Katiba uhusishe kila sehemu ya jamii…. wakulima,wafanyakazi,wafanyabiashara,wanasiasa,wasomi,taasisi za kidini,taasisi za kiraia,vijana na wanawake,wazee n.k MUNGU IBARIKI TANZANIA NA WATU WAKE WOTE!!!!!

  william Jotham

  November 7, 2011 at 5:36 PM

 5. Wadau wote tujitaidi kuelimisha jamii kwanza otherwise watapigia kura kitu wasichojua.

  kimali

  November 7, 2011 at 7:15 PM

 6. N kwel ndugu zito, kuna haja ya kuongeza nguvu kta wananchi kuelimisha juu ya katiba ikiwezekana tufanye mchakato wa vipepelush itasaidia kwa kila raia kufanya uhamuz sahihi tumechoka uhamuz wa m2 mmoja kuendesha serikali

  Sadick Magath

  November 9, 2011 at 10:27 PM

 7. Uko sawasawa sana kaka yangu. Nimekuunga mkono zaid kwa kuwapendekeza Warioba na Salim

  Ricardo Maftah

  November 14, 2011 at 6:42 PM

 8. kwakweli Zitto na chama chako nawapongeza sn. Ujue hawa wana2ona a2jaelimika hawajui kuwa sasa 2meelimika kweli ha2pendi vurugu lakini kwa staili hii 2nawaomba nyinyi m2komboe 2meioka kubuluzwa wakati umefika wa kuikomboa nchi kwa wanyonyaji na watemi kama nchi yao peke yao hawajui kuwa walikuja ku2omba. ila kikwete asikilize wazee wengi wa ccm hawapendi wanacho kifanya ila yataisha 2 mushimiwa Zitto 2ko nanyi nawaombea maisha marefu na afya njema

  fadhili fadhili

  November 17, 2011 at 11:16 AM

 9. Maoni ya mheshimiwa Zito kwa ujumla ni mazuri na yenye kuelimisha. Nakubaliana naye kwenye nukta ya Hadidu Rejea. Kama Bill inataja kazi za Tume pamoja na namna itakavyofanya kazi ingekuwa na mantiki zaidi kama na Hadidu Rejea zingetamkwa moja kwa moja kwenye Mswaada kwa kuwekwa sehemu ya nyongeza. Kwa hivi sasa baaada ya Bill kusheriishwa Raisi atapaswa kutoa Hadidu Rejea ambazo hazikinzani na kazi pamoja na mode of operation ya Tume inavyotamkwa katika Sheria, maana kiufundi Terms of References atakazozitoa Mh. Raisi kwa mujibu wa Sheria ya UUndwaji wa Tume zitakuwa ni mtoto wa Sheria hiyo na haziwezi kukinzana nayo zikaishi.

  Kuhusiana na Raisi Kuunda Tume mimi naona ni sahihi na utaratibu wa kawaida katika michakato ya uundwaji wa Katiba. Katika mamlaka ya kuunda Bunge la Katiba, Mswaada, kwa namna nilivyousoma mimi hayapo ka Raisi moja kwa moja. Maana, idadi ya wajumbe na namna wanavyopatikana inatajwa katika Mswaada. Kwamba, wabunge wote, ambao walichaguliwa na wananchi katika Uchaguzi Mkuu uliyopita na chaguzi ndogo zilizo/zitakazojitokeza wanakuwa moja kwa moja sehemu ya Bunge la Katiba. Na hawa ndio wengi. Raisi atachaguwa kama sikosei wajumbe 160 (sijui kama kifungu hiki kilirekebishwa) kutoka katika makundi makuu matano. Vyama vya Siasa vyenye usajili wa kudumu, Taasisi za Kidini, Taasisis zisizo za Kiserikali, Taasisi za Elimu ya Juu na Watu wenye mahitajio maalumu. Sheria haikubainisha namna wawakilishi watakavyopatikana katika makundi haya na idadi zao. Kwa ushauri wangu, 160 ingegawanywa kwa 5 kupata uwakilishi katika kila kitu na baadaye idadi ya wanachama au wahisika katika kila vikundi katika kundi vitumike kupata uwakilishi. Baadae vikundi vingependekeza majina kadhaa ya watu wenye sifa kwa Raisi naye baada ya kujiridhisha na sifa zao atawateuwa.

  George Jinasa

  November 20, 2011 at 1:37 PM

 10. hivi serikali yetu mbona ina mambo ya ajabu yaani siasa mpaka suala la wananchi wote, watoto,wazee,vijana bila kujali itikadi za vyama tunahitaji katiba bora sasa inakuwaje tena bunge lilete uccm wakati suala ni la kitaifa….!!!!!!!!!!!!!!

  lamu elizayo,p-udsm

  November 21, 2011 at 9:12 PM

 11. Kweli maoni yako ndo nazani kama yangeangaliwa zaidi!

  Luisjack mosses

  April 6, 2012 at 9:11 PM

 12. its gud,but tuwe care na watendaji

  henry wambogo

  April 7, 2012 at 2:15 PM

 13. Ambae hajaelewa hapo atakuwa kilaza ZITTO Amejaribu chambua kupitia hotuba ya TINDULISU na kumrekebisha pale anaposema ZANZIBAR imepewa nafas kubwa akiwa na maana isilingane sawa na bara, zitto anajaribu kuweka sawa na kuonesha hatari kama hawatapewa usawa kwahy muafaka wa kitaifa hautakuwepo,anaenda tena kwenye hotuba ya serikal kuwa inatakiwa wataje hadidu za rejea,kweli huyu ni kiongoz wa kitaifa na haangalii maslahi ya chama tu,kwa walioelewa hutuba ya TINDULISU ni ya kuipuza,inapinga muafaka wa kitaifa.na RAIS kasikia ushauri wake katika kuteua tume

  Hansen

  April 9, 2012 at 8:47 AM

 14. Sawa Kaka

  Mustafa Shia Shirazi

  August 23, 2014 at 7:46 AM


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: