Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

HOTUBA YA MBUNGE WA KIGOMA KASKAZINI NDUGU ZITTO KABWE KATIKA UZINDUZI WA JUKWAA LA VIONGOZI WA VIJIJI JIMBO LA KIGOMA KASKAZINI

with 8 comments

Kigoma, 6 Oktoba 2011

Ndugu Wenyeviti wa Vijiji vya Jimbo la Kigoma Kaskazini,

Ndugu watendaji wa Vijiji,

Viongozi wa Asasi ya Maendeleo Kigoma (KDI), Dr. Alex Kitumo – Mwenyekiti na ndugu Paul Bahemana – Mtendaji Mkuu

Afisa Miradi kutoka Taasisi ya FES Ndugu Amon Petro

Mshauri wa Mradi wa Demokrasia Vijijini, Mzee Sylvester Masinde

Wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini

Maswali na majibu

Maswali na majibu

Nachukua fursa hii kuwapongeza kwa hatua hii ya kuanzisha Jukwaa la Viongozi wa Vijiji katika Jimbo la Kigoma Kaskazini. Jukwaa ambalo litawezesha mawasiliano ya karibu miongoni mwa viongozi wa ngazi zote za Serikali Kuu (Mbunge), Halmashauri ya Wilaya (Madiwani) na ninyi Wenyeviti na Watedaji wa Vijiji.

Tulipopata wazo hili, na kwa kuzingatia kwamba katika sheria zetu za Serikali za Mitaa zinazoanzisha Mamlaka ya Serikali za Vijiji na Halmashauri za Wilaya, hakuna chombo chochote kinachokutanisha viongozi katika ngazi za vijiji, tuliona ni lazima tulitekeleze.

Katika ngazi ya Kijiji, Mwenyekiti wa Kijiji ana fursa ya kukutana na Wenyeviti wa Vitongoji katika Halmashauri ya Kijiji ambapo yeye ni Mwenyekiti wa kikao hicho. Vilevile katika ngazi ya Kata, Diwani ana fursa ya kukutana na Wenyeviti wote wa Vijiji katika Kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata ambacho yeye Diwani ni Mwenyekiti. Katika ngazi ya Jimbo, hakuna kikao chochote kwa mujibu wa Sheria ambacho kinamfanya Mbunge akutane na Viongozi wenzake waliochaguliwa kuongoza wananchi. Hata hivyo, Mbunge ni Mjumbe wa Baraza la Madiwani ambamo kunaweza kuwa na Jimbo zaidi ya Moja.

Katika hali hii na baada ya mashauriano na watu mbalimbali niliona niwaombe ndugu zetu wa KDI watusaidie kufanya utafiti wa namna bora ya kuimarisha Demokrasia katika ngazi za chini katika Jimbo letu. Moja ya mapendekezo ya Utafiti huo uliofanywa na mtaalamu wa muda mrefu katika masuala ya Serikali za Mitaa, Mzee Sylvester Masinde ilikuwa ni kuanzisha Jukwaa la Viongozi wa Vijiji katika Jimbo la Kigoma Kaskazini.

Jukwaa la Viongozi wa Vijiji

Mara mbili kila mwaka tutakuwa tunakutana kujadiliana changamoto za maendeleo katika Vijiji vyetu na Jimbo letu kwa ujumla. Tutakuwa tunapeana taarifa kuhusu miradi inayofanyika ndani ya Jimbo na kutekekelezwa katika vijiji vyetu mbalimbali. Tutakuwa tunakaguana kuhusu matumizi bora ya fedha za maendeleo katika vijiji vyetu (peer review) na pia kama tunafanya vikao vya kisheria kama Mikutano mikuu ya Vijiji na Halmashauri za vijiji. KDI itakuwa inakusanya taarifa kuhusu maendeleo ya Demokrasia katika Vijiji na Uwajibakaji katika utendaji wa shughuli zetu. Jukwaa pia litatumika kushauriana na Wabunge na Madiwani kuhusu vipaumbele vya kimaendeleo katika Jimbo letu na kuvipeleka mbele kwenye vikao vinavyogawa rasilimali kama Baraza la Madiwani na Bunge.

Jukwaa hili linakusanya viongozi wa wananchi na watendaji. Halina mwelekeo wa kichama kwani mtu yeyote aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kijiji bila kujali anatokea chama gani cha siasa  anakuwa mjumbe wa Jukwaa. Watendaji wa Vijiji wanashiriki ili sote kwa pamoja tujue masuala ya msingi ya Maendeleo ya Jimbo letu na kuweza kuwashirikisha wananchi moja kwa moja katika kujiletea maendeleo yao.

Changamoto za Maendeleo

Kipindi cha maswahil na majibu

Kipindi cha maswahil na majibu

Jimbo letu lina changamoto nyingi sana za kimaendeleo. Tupo nyuma sana katika Elimu kulinganisha na majimbo  mengine nchini, wakati tuna zaidi ya Shule za Msingi 80, Shule za Sekondari zipo 14 tu na katika hizo yenye Kidato cha Tano na Sita ni moja tu. Tumejitahidi kuwa na Zahanati takribani katika vijiji vyote lakini vituo vya Afya vipo 2 tu ukiachana na miradi inayoendelea katika kata ya Mahembe, Mukigo, Mwandiga na Kagunga. Hatujaweza kumaliza tatizo la Maji kwenye baadhi ya Vijiji vyetu. Huduma za Usafiri vijijini bado hazijatengemaa licha ya kukamilika kwa Barabara za lami za Mwandiga – Manyovu na Kigoma – Kidahwe. Hali kadhalika, ni vijiji 3 tu kati ya Vijiji vyote 32 vina huduma ya Umeme na umeme wenyewe bado haujasambazwa vya kutosha. Pamoja na kujaliwa Ziwa lenye samaki watamu (migebuka na dagaa) na wengi na hata mali asili nyingine, bado uvuvi wetu ni duni na usio nguvu ya kuondoa watu wetu kwenye umasikini. Hifadhi yetu ya Gombe haijatumika vya kutosha kukuza utalii na Ukuaji wa Sekta ya Kilimo bado si wa kiwango cha kuridhisha licha ya kuwa na michikichi mingi ambayo bei ya mawese inazidi kupanda kila mwaka katika soko la Dunia na kahawa (Gombe Coffee) bora zaidi kuliko zote Afrika kusini mwa jangwa la Sahara kwa miaka miwili mfululizo sasa.

Vyanzo vya Mapato kiduchu

Kufuatia kuanzishwa kwa Wilaya ya Uvinza, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma itakayobakia ni jimbo letu lenye kata 11 na vyanzo vichache sana vya mapato. Halmashauri yetu kwa ujumla inaweza kukusanya takribani Tshs 1.2bn pekee kwa mwaka ilhali Bajeti nzima ya Halmashauri yetu ni tshs 31bn. Zaidi ya asilimia 70 ya mapato haya yanatoka sehemu ya Kigoma Kusini ambayo sasa inakuwa ni Wilaya ya Uvinza na inakuwa na Mamlaka yake ya Serikali za Mitaa (Halmashauri ya Wilaya Uvinza).

Hivyo kuna changamoto kubwa sana katika Jimbo letu kuhakikisha tunabuni vyanzo vipya vya mapato ili Halmashauri yetu iwe endelevu. Ndio maana ni muhimu kuhakikisha kwamba (i) tunaanzisha eneo la viwanda vidogo vya kusindika mazao ya michikichi pale kijiji cha Mahembe ili kuzuia mise kupelekwa eneo la SIDO katika Manispaa ya Kigoma-Ujiji na hivyo kutengeneza ajira kwa watu wetu na kuwezesha Halmashauri kupata mapato (ii) tunaendelea kuwasukuma Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kutekeleza mradi wa Stendi ya Mabasi ya Kimataifa eneo la Mwandiga ili kukuza ajira na kupata mapato kwa Halmashauri yetu (iii) kuhakikisha Mamlaka ya Bandari nchini inamaliza mradi wa Ujenzi wa Bandari ndogo Kagunga ili kutengeneza ajira kwa watu wetu na kuleta mapato kwa Halmashauri (iv) kuwahimiza TANAPA kutangaza zaidi Hifadhi ya Gombe ili kupata watalii wengi zaidi na kujenga nyumba za wageni katika vijiji vya Mwamgongo na Mtanga ili kutengeneza ajira na kukuza mapato ya Halmashauri.

Jukumu la kukabili changamoto hizi ni letu sisi viongozi. Tumepewa ridhaa na wananchi wetu, kila mtu katika ngazi yake ili kukabili changamoto hizi kwa kushirikiana. Ni wazi tumeanza juhudi mbalimbali. Kama Mbunge wa Jimbo hili nimeajiri Mhandisi Mshauri (consultant) ambaye anatutengenezea mpango wa Maendeleo wa Jimbo letu (na baadaye Halmashauri yetu)  kwa kuibua maeneo ya kukuza uchumi wa Jimbo, kuongeza ajira na kuondoa kabisa umasikini. Mara baada mshauri huyu kumaliza kazi yake, tutawasilisha rasimu ya Mpango huu katika kikao cha Jukwaa ili kuweka maoni yenu na kupata mpango mzuri utakaotusaidia kuchochea maendeleo.

Utafutaji Mafuta (Oil exploration)

Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) limetangaza mshindi wa Zabuni ya kutafuta mafuta katika kitalu cha Ziwa Tanganyika Kaskazini. Eneo hili ni eneo lote la Kaskazini mwa Jimbo letu kuanzia Kijiji cha Kalalangabo mpaka Kijiji cha Kagunga. Kampuni ya TOTAL SA ambayo ni Kampuni tanzu ya Total ya Ufaransa ndio imeshinda zabuni hiyo na hivi sasa inajadiliana na TPDC kuhusu mkataba wa kutafuta Mafuta (PSA). Baada ya Kitalu hiki kutolewa hivi sasa kuna jumla ya Kampuni tatu zinazotafuta mafuta Mkoani Kigoma (Kampuni ya Motherland ya India eneo la Bonde la Malagarasi, Kampuni ya Beach Petroleum ya Australia katika Kitalu cha Ziwa Tanganyika Kusini na hiyo ya Total). Kutolewa kwa leseni hizi ni ama faida au laana kwetu. Ili kuepuka laana ni lazima kujipanga vizuri, kuhakikisha tunafuatilia hatua zote za mikataba na hatimaye kuwa na mikakati ya dhati ya kufaidika na rasilimali ya mafuta kama itapatikana. Hata kabla ya kupatikana kwa mafuta (ambapo wataalamu wa mafuta wanasema yapo, na hata hadithi za wazee wetu wavuvi hutwambia wamekuwa wakiona dalili) lazima tufaidike na uwekezaji katika utafutaji.

Meli yetu ya MV Mwongozo imekodishwa kwa Kampuni ya Beach Petroleum kwa mwaka mzima kufanya tafiti za mafuta. Nimeona nyaraka zinazoonyesha kuwa Kampuni hii itakuwa inalipa dola za kimarekani 900,000 kwa mwezi kwa kutumia Meli hii. Mimi kama Mbunge sijawahi kupata taarifa yeyote ya kiserikali kuhusu Jambo hili na sikumbuki kama imewahi kujadiliwa katika vikao vya Baraza la Mashauriano la Mkoa (RCC). Hata kama tozo hii ni sahihi, kwanini jambo hili limefanywa kwa siri? Lakini pia Kampuni hii itaajiri watu kutoka wapi katika utafiti wao ambao nimeambiwa tayari wamepata mikataba huko DR Congo na Burundi ambao pia wametoa leseni za kutafuta mafuta katika maeneo yao ya Ziwa Tanganyika. Tozo hii italipwa kwa Kampuni ya Meli za Taifa (MSCL) yenye makao makuu jijini Mwanza, kutakuwa na kodi yeyote ambayo Halmashauri yetu itakusanya?

Haya ni baadhi ya mambo ambayo nataka tuyajadili katika Jukwaa letu katika vikao mbalimbali. Kila jambo linalohusu maendeleo katika eneo letu ninyi viongozi wa vijiji mlijue na kuwaeleza wananchi katika mikutano mikuu ya vijiji.

Umeme Vijijini

Katika Bajeti ya mwaka huu wa fedha 2011/2012, Jimbo letu limefanikiwa kupata mradi wa mkubwa wa kusambaza umeme vijijini. Mradi huu utagharimu shilingi 5.6 bilioni na utaunganisha umeme vijiji vya Kiganza, Bitale, Mkongoro, Kalinzi, Matyazo, Mkabogo, Nyarubanda kwa kutokea Mwandiga. Waziri wa Nishati na Madini aliliambia Bunge kwamba Mradi huu utatekelezwa na Wakala wa Umeme Vijijini na utatekelezwa katika kipindi cha miezi 12 ijayo. Mradi wa kuunganisha vijiji vya Nkungwe, Kizenga na Nyamhoza tayari unatafutiwa fedha. Ni dhamira yetu kuunganisha umeme vijiji vyote vya Jimbo letu katika kipindi cha Bunge la Kumi. Ni matumaini yangu kuwa viongozi wa vijiji mtashirikiana na REA na TANESCO kuharakisha miradi hii. Muwape ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa miradi na tuwe wepesi kutatua migogoro yeyote itakayotokea kwa wananchi hasa wale watakaopaswa kuondoa mazao yao kupisha njia ya umeme. Hata hivyo ni muhimu kuhakikisha wananchi wetu wanalipwa fidia stahili.

Miradi itakayotekelezwa

Katika mwaka wa fedha 2011/2012 Halmashauri ya Wilaya Kigoma imepitisha miradi ya Maendeleo yenye thamani ya Tshs 4.5 bilioni itakayotekelezwa katika vijiji vya Jimbo la Kigoma Kaskazini. Jumla ya Bajeti nzima ya Maendeleo kwa Halmashauri nzima ni Tshs 9.5 bilioni. Miradi hii itatekelezwa katika vijiji vyenu. Tunataka ninyi muwe chachu ya kuona fedha za miradi hii zinafika vijijini na kutumika ipasavyo. Ninapendekeza kuwa kila tutakapokuwa tunakutana tuwe tunapeana taarifa kuhusu miradi hii na pale tutakapoona miradi inahujumiwa mara moja tutoe taarifa kwa Sekretariat ya Jukwaa ili kuweza kuingilia kati kuzuia hujuma. Ninawapa nakala ya miradi yote ili kila mmoja wenu awe nayo aweze kuifuatilia na pia kuwaeleza wananchi vijijini.

Miradi mingi inayokuja vijijini kwetu huhujumiwa kutokana na  ufisadi. Mfano mzuri ni ule mradi wa kutandika mabomba kule Kagunga uliofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo la Kigoma Kaskazini. Mmoja wa maafisa wa Idara ya Maji alipewa tshs 10m kwa ajili ya kununua Mabomba mapya, yeye akachukua mabomba ya zamani yaliyokuwa katika bohari yao na kuyapeleka Kagunga. Hata hivyo taarifa iliyoandikwa kwenye Kamati ya Maendeleo ya Jimbo imeonyesha kuwa Afisa huyu amenunua Mabomba mapya na hata kupata risiti kutoka Duka moja la vifaa vya Ujenzi mjini Kigoma! Nimeagiza suala hili lipelekwe katika Baraza la Madiwani na mtumishi huyu achukuliwe hatua kali za kisheria. Pili, Duka lililotoa risiti bandia kwa Afisa huyu wa Idara ya Maji lipigwe marufuku kufanya biashara na Halmashauri yetu.

Ninawataka ninyi viongozi wa Vijiji muwe mstari wa mbele kuibua ubadhirifu wa aina hii katika vijiji vyenu. Pale ambapo ninyi ni wahusika wa ubadhirifu tutakuwa tunaambiana kwenye vikao yetu na kuaibisha wenzetu watakaokutwa na kashfa za ubadhirifu. Pia tutawashitaki kwa wananchi ili kwa kutumia njia za kidemokrasia wang’olewe katika nyadhifa zao.

Kipindi cha maswahili na majibu

Kipindi cha maswahili na majibu

Hitimisho

Ninaamini Jukwaa la Viongozi wa Vijiji Kigoma Kaskazini litatumika kuimarisha mawasiliano na ushirikiano miongoni mwa viongozi bila kujali itikadi zetu za vyama, litakuza demokrasia vijijini kwetu na kuongeza uwajibikaji katika utendaji wa kazi

Natangaza rasmi sasa kwamba Jukwaa la Viongozi wa Vijiji Kigoma Kaskazini limezinduliwa rasmi.

Asanteni kwa kunisikiliza

Advertisements

8 Responses

Subscribe to comments with RSS.

 1. Kiongozi, tunashukuru. jukwaa lina manufaa mengi sana na kurahisisha mawasiliano baina ya viongozi, kuhusisha, kuinua matatizo ya maendeleo ya kijamii na matatizo ya miundombinu katika jamii. tunakutakia mafanikio mema sana.

 2. Hongera sana mh. kwa kuanzisha hilo baraza na inatakiwa na wah. wengine waige mfano huu, ni jambo la kutia moyo kwasababu halihusishi itakadi za kichama. Halafu inakuwaje kampuni inapewa mkataba wa kutafuta mafuta mradi wa mabilioni ya pesa halafu wewe mbunge hauna taarifa. Sasa hiyo ni serikali gani imbayo haiwahusishi wadau ambao ni wananchi. Mh. fuatilia mradi huo ili jimbo lenu lifaidi.

  william Jotham

  October 8, 2011 at 12:26 PM

 3. Nimeyapenda sana haya mawazo na ungezaliwa mapema basi tz tungekuwa mbele ya china kiuchumi angarizo wazo zuri ziwia siasa isiingie kabisa maana kuna watu wanamawazo hasi na wengine wanataka wakuzofishe wewe hongera na simamia hilo.

  Ally lilangela hamis

  October 9, 2011 at 10:10 PM

 4. Na kuhusu mikataba fuatilia kwa makini kwani matatizo ya maliasili za tz ni mikataba sisi tunatajka tufaidi mafuta yetu pigania hilo mpaka dakika ya mwisho tuko pamoja na tunaomba feedback

  Ally lilangela hamis

  October 9, 2011 at 10:17 PM

 5. Mr Kabwe you so bright, Ni fahari kuwa na kiongozi kama wewe, kigoma si maskini kama wengine wanavyodhani kuwa ni mkoa maskini, Kiogoma imefanywa maskini na watawala mbalimbali, LAKINI MIMI HUWA NAAMINI HUWEZI SHINDANA NA NGUVU ZA WAKATI, NI WAKATI WA KIGOMA SASA KUIBUKA NA KUWA MKOA WENYE NGUVU SANA HAPA NCHINI, FURSA TULIZO NAZO HAZIPO POPOTE PALE TANZANIA NA SASA WAKATI UMEFIKA WA KIGOMA YENYE KUTAMANIKA KUIBUKA NA KUWA JUU KABISA

  Sila

  October 10, 2011 at 4:39 PM

 6. Kwa hotuba yako hiyo,Mhesh.Zitto, Mungu akuinue na kukujalia.Sina mengi.

  Fidelis kulolwa.

  October 10, 2011 at 6:05 PM

 7. Ni kitendo cha busara sana cha kuwaunganisha viongozi na watendaji kutoka katika kata 11 zenye vijiji zaidi ya 30, lengo kuu likiwa ni kuwaomba, kwa umoja wao, kujadili changamoto mbali mbali zilizomo jimboni na kuzitafutia ufumbuzi.

  Ni hatua ya kupongezwa kwani huwaweka wadau hao pamoja bila kujali itikadi za vyama vyao, dini zao na mahali watokako.

  Kitendo hicho, kwa namna moja ama nyingine, kinatoa fursa ya kukupatia (mb) taarifa ya huduma za maendeleo ya vijiji jimbo zima. Kwa maana hiyo kuna uwezekano kuwa tukio hili linakusaidia pia kutambua mapungufu na kukusaidia kufanya tathmini ya nini kifanyike na kwa wakati gani kwa mustakabali wa jimbo na taifa kwa ujumla.

  Tunazidi kuomba kwamba mwanzo huu uwe ni endelevu pale inapobidi!

  Amini, shoka moja huweza kunolewa kwa masaa 7584 na kisha kuangusha gogo kwa masaa 24 tu.

  Tunakuomba usichoke mh. Zitto!

  Paulus

  October 13, 2011 at 12:52 PM

 8. Kaka hakika wewe ni kiongozi na sio mtawala, kweli jimbo lako ni la mfano katika mkna wa kigoma, ni sehemu pekee ambayo hakika vijana wake wote wanajituma, kaka sijasikia juu ya wawekezaji katika sekta ya uvuvi katika jimbo lako hasa baada ya vijiji vingi kuunganishwa na umemd pamoja na ujenzi wa barabara kwenda gombe, hii itasaidia kuwashawishi TANAPA kuitangaza gombe kwa nguvu na kutuongezea mapato

  Isack

  October 15, 2011 at 3:53 PM


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: