Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Taifa Msibani, Umoja wetu na Utu wetu Shakani

with 8 comments

Huyu aliyelala ndio Leyla. Alikuwa na dada yake wanarudi shuleni Pemba (Wete) baada ya kula Idi Unguja. Watoto wengi sana na wanawake ndio sehemu kubwa ya waliopoteza maisha.

(Nimeandika makala hii nikiwa katika Benchi la Hospitali ya Mnazi Mmoja hapa Zanzibar. Mniwie radhi kama kuna spelling mistakes kwani nilitaka hisia zangu ziwe as raw as possible – Zitto Zitto and not Zitto a Politician).

Jana asubuhi tarehe 10 Septemba 2011 Taifa liligubikwa na habari za kushtusha za maafa. Mwanzoni taarifa zilisambaa kwamba zaidi ya watu 2000 walikuwa kwenye Boti MV Spice Islander lililopinduka na kuzama mbele kidogo ya Nungwi likielekea kisiwani Pemba. Habari hazikuwa za uhakika sana kwani vyombo vyetu vya habari na hasa Televeshini ya Taifa havikuwa vikitoa habari juu ya ajali hii.

Habari zilisambaa kupitia mitandao ya intaneti na kufuatia uchu wa habari nilianzisha #ZanzibarBoatAccident katika mtandao wa twitter ili tuweze kufuatilia kwa karibu habari zote za ajali hii.

Habari zilisambaa kuwa Televisheni ya Taifa ilikuwa inaonyesha muziki wa Taarab na Baadaye vipindi vingine vya kawaida bila kutoa habari kwa Umma kuhusu msiba huu.

Watanzania waliokoa wakiwasiliana kupitia twitter na facebook walikuwa na hasira sana na kituo cha TBC1 kutoonyesha au kupasha habari juu ya ajali hii. Mpaka saa moja jioni kituo hiki cha Televisheni ya Taifa kilikuwa kinaonyesha watu wakicheza muziki wa Kongo, wanawake wakikatika viuno na hata ngoma za asili.

‘Hallo, washa TBC1 uone Televisheni yenu inachoonyesha’ yalikuwa ni maneno ya Mwakilishi Ismael Jussa Ladhu aliponipigia kuonyesha kusikitishwa kwake na kituo hiki. Mpaka jioni tulikuwa tumepata taarifa kuwa Watanzania wenzetu 198 walikuwa wamepoteza maisha. 570 hivi walikuwa wameokolewa.

Binafsi nilipotembelea Hospitali ya Mnazi Mmoja niliweza kumwona Binti aliyeitwa Leyla, akisoma darasa la Nne huko kisiwani Pemba. Leyla alipona, aliokolewa. Nilimwambia leyla atapona na kurudi Shuleni. Mpaka ninapoandika tumeambiwa kuwa Watanzania 240 wamegundulika kupoteza maisha na zaidi ya 600 wameokolewa.

Napenda kuwapongeza sana waokoaji wetu, wavuvi wa kijiji cha Nungwi na vijiji jirani, wamiliki wa mahoteli waliojitolea vifaa vyao kwenda kuokoa watu na wanajeshi wetu wa majeshi ya ulinzi na usalama kwa kazi hii kubwa ya kuokoa. Kwa kweli tumeokoa watu wengi kuliko ilivyotarajiwa. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejitahidi sana, ilitulia na kuonyesha uongozi thabiti katika juhudi za uokoaji.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akafuta ziara yake huko Canada, ziara iliyokuwa imeandaliwa muda mrefu na kwa gharama. Lakini Rais aliona ni vema kupata hasara kuliko kuwa nje ya Nchi kipindi hiki. Hakutaka hata kumtuma Makamu wa Rais au Waziri Mkuu. Alifuta. Akatangaza siku 3 za kuomboleza.

Hata hivyo waandaaji wa Miss Tanzania waliona hasara kubwa kuahirisha shindano la Urembo usiku huo. Wangepata hasara! Hata wafadhili wao Kampuni ya simu za mkononi ya vodacom ambao miongoni mwa waliofariki wamo wateja wa vodacom, waliendelea na shindano hili.

Jumatatu, tarehe 12 Septemba 2011 ni siku ya khitma ya kuwaombea marehemu wetu.

Nimeamua kutotumia simu yangu ya Voda kwa siku nzima, sina njia ya kuiadhibu Kampuni hii isipokuwa kugoma kutumia simu yao japo kwa siku moja kuonyesha kutoridhishwa kwangu na uamuzi wao wa kutojali msiba huu kwa Taifa.

Misiba huweka jamii pamoja. Msiba huu uliotokea Zanzibar ni jaribio kubwa kwa Umoja wa Taifa letu. Shirika la Utangazaji la Taifa limeshindwa jaribio hili la kudhihirisha Umoja wetu katika kipindi hiki. Nataraji wakubwa wa Shirika hili linaloendeshwa kwa kodi watawajibika au kuwajibishwa!

Jumla ya Majeruhi na marehemu sasa inafikia zaidi ya Abiria 800! Asubuhi ya jana 10 Septemba 2011 tuliambiwa na Serikali kwamba uwezo wa Boti la MV Spice Islander ilikuwa ni abiria 500 na wafanyakazi 12. Pia tumejulishwa kuwa boti hili lilikuwa la Mizigo na sio la Abiria.

Natumai mara baada ya kumaliza maombolezo haya ya siku tatu Wakuu wa Mamlaka zinazohusika na usafiri wa Majini wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar watawajibika au kuwajibishwa. Mkuu wa Bandari ya Zanzibar Mustafa Aboud Jumbe na Waziri wa Miundombinu Hamad Masoud wanapaswa kufukuzwa kazi mara moja kama hawatawajibika wenyewe kwa kujiuzulu.

Kufukuzwa kwao kazi hakutarudisha ndugu zetu duniani bali itakuwa ni somo kuwa hatutarudia tena kufanya makosa yaliyoleteleza ajali kama hii.

Mwenyezi Mungu atupe subira wakati huu wa msiba mkubwa katika Taifa letu. Alaze roho za marehemu wetu mahala pema peponi na awape unafuu wa haraka majeruhi wetu.

Zitto Kabwe, Mb

Written by zittokabwe

September 11, 2011 at 11:21 PM

8 Responses

Subscribe to comments with RSS.

 1. Inahuzunisha sana, binafsi nawapa pole sana wote waliofikwa na msiba huu pia watanzania wenzangu wote kwa ujumla kwani sote ni ndugu……………….

  Emmanuel Mushi

  September 12, 2011 at 10:02 AM

 2. huu ni mda wa kutafakari ni mbinu gani tuzitumie ili kuzuia janga kama hili lisitokee tena, na sio sehemu ya siasa,ama kujionyesha unaweza sana kwani hili swala ni mipango ya mungu na hamna mtu wa kumpa lawama kwa kitu ambacho kishatokea…

  Victor

  September 12, 2011 at 2:30 PM

 3. Ni jambo lakusikitisha kuona utu wetu umezingwa na tamaa na ubinafsi. Sasa tunaona madhara yanayokumba wananchi ambao hatia yao ni kuiamini serikali yao na viongozi wao kuyalinda maisha yao.
  Ukiangalia mazingira yanayoizunguka ajali hii ni uzembe bila hata ya kuchimba zaidi.
  Nawaomba watanzania tuelewe kuwa vitu vidogo huleta maafa makubwa. Ajali kama hizi huepukika iwapo tutanyanyua sauti zetu kwa pamoja na kukataa uzembe wa namna hii. Tuache ubinafsi, utatumaliza!
  Nawaombea Watanzania na wageni wote waliopatwa na msiba huu. Mola azilaze pema roho za marehemu, Amina.

  susanne

  September 12, 2011 at 7:28 PM

 4. Natoa pole zangu za dhati kwa wote waliopatwa na janga hili kwa namna moja au nyingine!Pia nawaombea marehemu wote wapumzike kwa amani.Lakini ni lini serikali yetu itajifunza kuchukua tahadhari za matukio kama haya?ndugu zetu wanaendelea kupoteza maisha kila kukicha,then tunaunda kamati.Hizi kamati za kila siku ni za nini?na hivi vyombo vya habari vinavyotangaza michango,yako wapi mamilioni ya shilingi tuliyowachangia ndugu zetu wa Gongolamboto?Kweli watanzania sio wajinga tena,ipo siku.

  Lazaro Collins

  September 12, 2011 at 9:06 PM

 5. Ni kweli inasikitisha,kuna baadhi ya watanzania sio waelewa kabisa,licha ya Rais kutangaza maombolezo ya siku3 nchi nzima,kuna wafanyakazi na mindevu yao wameendelea kufanya kazi za jumuiya kama mashuleni na kuwakataza wanafunz hakuna mapumziko kwa kudai msiba ni kwa zanzibar tu,hii inaingia akilini jamani watanzania? Leo hii bila zanzibar kungekuwa na Tanzania? Hili linaboa sana.

  Paul D. Amos

  September 13, 2011 at 2:22 AM

 6. kiongozi,taifa hili hakuna uwajibikaji,hakuna wa kujiuzulu ktk hili kila moja anajali masilahi yake,tumwombe Alah atunusuru na majanga

  malula tesre

  September 13, 2011 at 11:51 AM

 7. Mungu amsaidie huyu binti apone haraka, hili ndo tatizo la kuwa na serikali ambayo haijui wajibu wake au kutokuwa na dira kamili ya Taifa. Usafiri kwa wananchi ni jambo la muhimu na msingi kabisa kwahiyo kila raia ana haki ya kusafiri popote hapa nchini, lakini serikali hii inaona kama usafiri ni zawadi kwa wananchi! Cha kushangaza eti serikali haimjui mmiliki wa meli hiyo iliyoleta maafa!!!!!!!!!!! SHAME on you JK na Shein!!

  william Jotham

  September 15, 2011 at 10:07 AM

 8. Kwakwel inauma sana kuona watanzania wanakufa kwa sababu ya uzembe wa watu wachache, nakuunga mkono zitto wote wafukuzwe

  Venance Mazebele

  September 16, 2011 at 12:44 PM


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: