Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Kuundwa Kamati teule kuchunguza Malipo ya TZS 216bn kwa niaba ya Meremeta

leave a comment »

MHE. ZITTO Z. KABWE:

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kukushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia asubuhi hii katika Wizara yetu muhimu sana, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Napenda na mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine, kulipongeza Jeshi letu kwa kazi ambayo wanafanya ya kulinda mipaka ya nchi yetu na kuiepusha na maadui na kuiweka tayari kwamba wakati wowote ambapo tunaweza tukavamiwa, Jeshi letu litakuwa liko tayari.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili napenda kuwapongeza vijana wetu, in uniforms, walioko Darfur, walioko Lebabon, kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya ya kulinda heshima ya nchi yetu huko waliko. Jambo la msingi na la kusisitiza ni kuhakikisha kwamba vifaa ambavyo wanajeshi wetu walioko katika mission hizi za kulinda amani, vinakuwa ni vifaa ambavyo ni vizuri na vinavyoendana na hadhi ya nchi yetu. Lakini pia nimepata taarifa kule Darfur, kuanzia mwezi ujao, Naibu Kamanda atakayeongoza Kikosi cha African Union kule Darfur, atakuwa ni Kamanda kutoka Tanzania. Kwa hiyo, napenda kupongeza sana jambo hili. 

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimpongeze kwa dhati kabisa Naibu Waziri Kivuli wa Wizara ya Ulinzi, kwa hotuba yake nzuri sana. Ameongea vitu vizuri sana na ameonesha ni namna gani ambavyo Kambi ya ilivyojipanga na kuweza kuhakikisha kwamba tunaisimamia vizuri Serikali. Lakini pia napenda nitoe shukrani zangu za dhati kwa Waziri wa Ulinzi, kwa Hotuba yake nzuri na Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. 

Mheshimiwa Naibu Spika, JKT. Kwa muda mrefu sana tumekuwa tukizungumzia suala la kurejeshwa kwa JKT na Serikali imekuwa ikiahidi kwamba JKT itarudi. Lakini nimeangalia bajeti ambayo imepangwa kwa ajili ya maendeleo, Vote 39, Development. Zimepangwa takribani shilingi bilioni 3 tu, kwa ajili ya JKT. Na tunafahamu kwamba ili hao vijana 20,000 waweze kuingia kwenye Makambi, ni lazima Makambi haya yasafishwe, Makambi haya yakarabatiwe, nk. Siamini kwamba shilingi bilioni 3 zinaweza zikatosha kwa ajili ya kazi hii. Kwa hiyo nilikuwa ninapata wasiwasi kama kuna committment ya dhati ya kuweza kuhakikisha kwamba JKT inarudi na inafanya jinsi ambavyo inavyotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama unavyofahamu mara baada ya JKT kuwa imevunjwa, yaani imesimamishwa mwaka 1994, hapa kati akati kumekuwa na vijana wengi sana ambao wanamaliza kidato cha VI, wanamaliza Vyuo Vikuu na hawaendi JKT. Baadhi ya vijana hao, mimi nikiwemo, tumefanikiwa mpaka kuingia kwenye siasa na kuwa Wabunge, hatujapita JKT. Nilikuwa naomba na ninatoa rai, nililisema hili mwaka 2006 halijafanyiwa kazi naomba lirejewe, vijana wote ambao ni viongozi wa kisisasa ambayo hawakupita JKT, waandaliwe mafunzo maalum ya JKT kuanzia sasa. Hili lifanywe ndani ya mwaka huu, mara baada ya Bunge la mwezi Novemba, voluntary, wasilazimishwe, lakini voluntary wale ambao wanataka, mimi nitakuwa tayari, mara baada ya Bunge la mwezi Novemba, wiki 8 vijana ambao wana nyadhifa za kisiasa waende JKT, ni muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni muhimu sana kwa sababu ya vijana, Viongozi wa kisiasa kujua historia ya nchi, kuwa na ukakamavu, kujifunza mbinu za kijeshi na kuweza kujua ni mambo yepi ambayo yanapaswa kufanywa kama kiongozi. Kwa hiyo, nilikuwa ninashauri kwamba hili lifanywe, liandaliwe na ninaamini kwamba itakuwa ni motisha kubwa. Vijana ambao hawajaenda JKT, wakiwaona vijana wanasiasa na magwanda ya JKT wanapiga kwata, in-take ijayo, vijana wengi sana watajitokeza kwenda. Kwa hiyo, nilikuwa ninaomba hili liweze kuchukuliwa kwa uzito wake unavyotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, National Defence College, hili ni jambo ambalo lilichelewa. Nchi kutokuwa na National Defence College, ilikuwa ni makosa makubwa. Kwa hiyo, ninapenda nishauri kwamba mchakato wa National Deffence College, uweze kuharakishwa ili kuhakikisha kwamba watu waweze kujiunga. Na mimi nilishamwambia Mnadhimu Mkuu wa Jeshi kwamba, nitaomba rasmi katika in-take ya mwanzo kabisa National Deffence College, kwa ajili ya Masters of Strategic Studies niweze ku-join ili niweze kwenda na kujifunza na kuweza kuona ni namna gani ambavyo kama mtanzania ninaweza nikailinda nchi yangu kupitia taaluma.

Mheshimiwa Naibu Spika, Msemaji Mkuu wa Upinzani, amezungumzia masuala ya assets au biashara ambazo Jeshi linafanya. Jambo hili ni jambo la kutilia mkazo sana, Majeshi mengi duniani yanafanya biashara. Mheshimiwa Sanya, ametolea mfano wa Jordan, ametolea mfano wa Egypt, yanafanya biashara. Contracts kubwa kubwa zote, ambazo zinafanyika Egypt leo, zimeshikwa na Majeshi. Lakini wanakuwa makini sana na aina ya biashara ambazo wanazifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, huko nyuma tumefanya makosa. Kwamba tumejikuta tunaliingiza Jeshi letu katika shughuli za kibiashara, deal za kibiashara na makampuni off show, makampuni ambayo yanakuwa yameundwa kwa ajili ya kufanya wizi. Na kumekuwa kuna ripoti nyingi sana, nilikuwa nasona kitabu hapa cha Nicholous Saxon, Treasure Islands; kinazungumzia off show companies na namna gani ambavyo zinaiba kutoka Bara la Africa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1997 Jeshi letu liliunda kampuni ya Meremeta. Kampuni hii ikaungana na kampuni nyingine kutoka Afrika ya Kusini, inaitwa Trinex, wakawa na 50%, 50%. Uchunguzi ambao nimeufanya umeonesha kwamba Trinex wala sio Kampuni kwa ajili ya kufanya biashara, ni Financial Adviser. Ambayo kazi yake ni ku-trot from one African Country to another African Country, kutengeneza deals mbalimbali. Na ninaripoti hapa, Namibia waliwafukuza Trinex. Sisi tukawakumbatia Trinex! Wakaingia makubaliano na Meremeta. Wakatusababishia mkopo kutoka NEDCO Trade Services ya South Africa, ambayo ni kampuni tanzu ya Ned Bank ya South Africa. Mkopo wa $10,000,000 takribani shilingi bilioni 16 kwa exchange rate ya sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi Meremeta wakashindwa kuzilipa. Baada ya Meremeta kushindwa kuzilipa, Serikali ikalichukua lile deni. Baada ya Serikali kuchukua lile deni, inapofikia wakati wa kulipa, tumeilipa Ned Bank ya South Africa $ 132,000,000! Tumekopa $ 10,000,000 tumelipa $ 132,000,000. Na Mheshimiwa Waziri, nitakupa barua ya Serikali ambayo ina-comfirm huo mkopo kutoka NEDCO ni barua ambayo ilikuwa inaenda Deustche Bank AG ya London, ambayo ni Banker wa NEDCO Trade Services, kwa ajili ya mkopo huo wa $ 10,000,000. Lakini pili, nilifanya uchunguzi wangu binafsi nikawatafuta watu wa Ned Bank, kuwauliza, inakuwaje mtukope $ 10,000,000 tuwalipe $ 132,000,000? Ambayo ni sawasawa na zaidi ya shilingi bilioni 216? Yaani kwamba, tunakopa bilioni 16 tunalipa bilioni 216! Mpaka sasa, hawajatoa hayo majibu! Lakini nitakupatia pia mawsiliano yote ambayo nimefanya na hao watu wa Ned Bank, li uweze kuona.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, rais aliunda Kamati ya Bomani, ambayo ilifanya uchunguzi kuhusiana na sekta ya madini. Katika one of the conclusion yake kuhusiana na suala la Meremeta, walisema, Serikali ifanye uchunguzi wa kina juu ya uanzishwaji wa kampuni za Meremeta na Tan Gold, umiliki wa Serikali katika kampuni hizo na uhalali wa malipo ya dola za Marekani milioni 132, yaliyofanywa na Benki Kuu kwa Benki ya Ned Bank ya Afrika ya Kusini. Ripoti hii ilitolewa mwezi Aprili, 2008. Mpaka sasa hakuna uchunguzi ambao umefanyika!

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, baada ya kuwa Treasury Registreer ame-list Tan Gold kama sehemu ya Makampuni yanayomilikiwa na Serikali, tukaagiza, mwezi Juni 2009, tarehe 8 nakumbuka; tukamuandikia barua Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, kwamba sasa fanya uchunguzi kuhusu transaction iliyotoka Meremeta, Benki Kuu na hawa watu wa South Africa. Mpaka sasa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, ameshindwa kufanya huo uchunguzi, kwa sababu amefanya mawasiliano na watu wa Treasury Registrar, hamna lolote ambalo wamelijibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sisi tunajua, sisi ni wazalendo! Tunajua kwamba kwa njia moja ama nyingine, kuna mambo ambayo Jeshi letu lilifanya ambayo labda hayapaswi kwenda kwenye Public. Mambo haya yanaeleweka na tunaelewa! Na kuna kipindi hapa tuli-offer, basi Serikali iende kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge ika-explain suala hili. Lakini Serikali imekuwa kila siku inaweka jambo hili under the carpert! Lakini haliwezi kwisha bila suala hili kufanyiwa uchunguzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 117, kama sijakosea, baada ya hoja hii kwisha, nitatoa hoja, kwamba Bunge liunde kamati Teule, kufanya uchunguzi wa malipo ya dola milioni 132 kutoka Benki Kuu, kwenda Ned Bank ya South Africa, wakati mkopo ambao tulichukua kutoka Meremeta ulikuwa ni dola milioni 10 peke yake. na wala haitasaidia kusema kwamba jambo hili ni la usalama wa Taifa! Haitasaidia kusema kwamba jambo hili ni la ulinzi wa nchi yetu! Jambo hili lisipopatiwa ufumbuzi litaendelea kupaka matope Jeshi letu. Na sisi hatuwezi kukubali Jeshi letu liendelee kupakwa matope, tunataka Jeshi letu liwe ni taasisi safi, taasisi ambayo haihhusiki kabisa na ufisadi wa aina yoyote, taasisi ambayo watanzania wataendakwayo ikitokea nchi inapata matatizo yoyote. Na tumeona nchi mablimbali kwamba we want to rely on our army!

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tulikuwa tunaomba jambo hili liweze kupatiwa ufumbuzi wa mwanzo na wa mwisho! Lifanyiwe uchunguzi, tuone hizo transactions zilizofanywa ni kwa ajili ya nini? Na kama kuna mambo ambayo ni kwa maslahi ya umma, Bunge lielezwe. Kama haliwezi kuelezwa in a plainary, Kamati ya Ulinzi na Usalama ielezwe. Kama Kamati hiyo itakuwa ni kidogo sana, Kamati ya Uongozi ya Bunge, ielezwe. Hatuwezi kuwa miaka mitano tunazungumzia jambo moja, sisi tunasema hivi, Serikali inasema hivi, halipati ufumbuzi!

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilikuwa ninaomba kama nilivyokwambia, mwishoni kabisa, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, nitaomba Bunge lako liridhie, tuweze kufanya uchunguzi huu. Haiwezekani mabilioni ya fedha hizi za umma yapotee, halafu sisi wawakilishi wa wananchi tukae kimya bila kusema. Kwa hiyo hayo ndio niliyokuwa napenda kuyazungumza. JKT irudi, Wabunge Vijana waingie JKT haraka iwezekanavyo. National Defence College iwe fast track na uchunguzi wa malipo kutoka Benki Kuu, wa dola milioni 132 kwenda Ned Bank ya South Africa kupitia kampuni yake tanzu ya NEDCO ambayo ni off show company, imesajiliwa Mauritius, iweze kufanywa ili tuweze kulimaliza suala hili kwa kuwa na uchunguzi wa mwanzo na wamwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: