Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

NIPITIE -Na Jacqueline Mgumia

with 7 comments

NIPITIE
Na Jacqueline Mgumia

Ndugu zangu,
 
Leo asubuhi, katika barabara ya Ali Hassani Mwinyi nikitokea Mwenge kwenda Mjini, kama kawaida watu walikuwa wengi barabarani wakisubiri mabasi kuelekea katika mihangaiko yao ya siku. Wengi wao wakiangalia muda na kusogelea mabasi kila walipoyaona. Mengi yalipita bila kusimama maana yalikuwa yamejaa, na yale yaliyosimama abiria walijaribu kujichomeka hivyo hivyo ili mradi wapate mahali pa kupenyeza mguu.
 
Lakini katika magari madogo zaidi ya ishirini niliyoweza kutayatazama, likiwemo la kwangu, ndani ya gari hakukuwa na watu zaidi ya watatu, na hivyo kuacha viti viwili hadi vinne wazi ambavyo vingeweza kubeba baadhi ya watu vituoni.
 
Nikabaki najiuliza, kwa nini hatutatui tatizo la usafiri Dar es Salaam wakati magari yapo lukuki? Sio swali geni lakini hatujalipatia ufumbuzi. Labda niulize tena, kwani kuna ugumu gani magari madogo kubeba watu walioko vituoni iwapo wote wanaelekea sehemu moja?
 
Hofu zilizopo juu ya suala hili ni bayana na zinaeleweka, “aha dunia hii haiaminiki bwana!” Kwa wale wanaokwenda na muda, wanaweza kusema ni “kazi ya ziada!” Kwa misingi ya kibepari, ‘kubebanabebana ndio maana hatuendelei Tanzania!’ Wale wanaokumbuka historia ama kuona wazo hili ni ndoto za Abunuwasi, wanasema “hadithi za ujamaa hizo!” Huku wengine wakikumbusha mabasi ya UDA na ndoto ya “mabasi ya ghorofa mbili” na “barabara za angani” – kwa namna moja au nyingine wanasema “kazi ya serikali hiyo!” SAWA.
Nafsi yangu katu haishangazwi na majibu haya, wala sina nia ya kutoa ushawishi ama kuchanganua kiini cha mitazamo hii. Yawezekana kabisa ndio sehemu ya tatizo – lakini sitozungumzia hilo leo.
 
Nia yangu haswa ni kutoa mhangaiko wa moyo wangu na kukiri kuchoshwa kuwaona watu wakigombania mabasi asubuhi, huku Serikali na sisi wananchi tukiendelea kuzoea tatizo hili.
 
Labda, pia nimechoshwa kuulizwa maswali na mwanangu nimpelekapo shule asubuhi kushindwa kuelewa kwa nini watu wazima wanaoenda kazini kama wazazi wake hawana magari na kwa nini hatuwapandishi kwenye gari letu – wakati kila siku anakumbushwa “kushare” na wenzake vitu vyake. Na leo wakati tunapita Makumbusho kaniambia, “mama mbona yule mzee mwenye shati la bluu simuoni!” Kabla sijajibu, akajijibu mwenyewe kwa swali “atakuwa amepata basi leo?”
 
Wazo langu:
Hakika Serikali ina wajibu wake na tutaendelea kuisemesha, tena kusema nayo sana tu. Ila na sisi pia, kama wananchi waungwana, tunaweza kutafuta ufumbuzi kwa nafasi zetu. Pendekezo langu tuanzishe utaratibu wa kusafirishana, tuuite “NIPITIE”. Tukimaanisha wale watu wenye magari wawe wanachukua watu wasio na magari kwenye vituo vinavyotambulika kulingana na mizunguko yao. Ili kufanikisha hilo, napendeka utaratibu ufuato:
 
1. Kwanza, wenyeviti wa mitaa waandikishe watu wote wanaohitaji usafiri, kuanzia kituo wanachoanzia kwenda kituo wanachoishia. Ili kujiandikisha mwananchi huyo lazima awe mkazi wa eneo hilo, atoe kithibitisho chake cha kazi/shughuli na barua ya kumhakikisha.
 
2. Pili, wenye magari na nia ya kutoa msaada wa usafiri, watoe ratiba ya mzunguko wao wa asubuhi, nikimaanisha – kituo wanachoanzia na kuishia – ama ambapo wangependa kuchukua watu na kuwashusha watu, na idadi yao. Pia atoe muda wa kupita njia hiyo.
 
3. Tatu, wanaopewa msaada wa gari watoe elfu 20,000 kwa mwezi – ambayo inaweza kulipwa 5,000 kwa wiki ili kukidhi mahitaji ya usimamizi wa shughuli hiyo, vilevile kutoa ajira kwa wasimamizi wa shughuli hiyo.
 
4. Nne, kila eneo liajiri mtu/watu watakoahamasisha/kusimamia na kufikiria ni jinsi gani utaratibu huo ufanyike kwa kuzingatia usalama wa wenye magari, abiria, – na kuona jinsi gani Serikali na jamii itakuwa sehemu ya mpango huu ili uendeshwe kwa amani.
Ama shughuli hii inaweza kuanzishwa na wenye magari ama wanaohitaji usafiri na wajiwekee utaratibu wao wenyewe!
 
Nyie wenzangu mwasemaje?
 
Chanzo: Blog ya Udadisi-Rethinking in Action-Chambi Chachage
Advertisements

Written by zittokabwe

May 23, 2011 at 9:27 PM

7 Responses

Subscribe to comments with RSS.

 1. Dada Jack!
  Kama ulizaliwa ukaishi kidogo kipindi cha utawala wa mwalimu Nyerere, au kama umefuatilia kwa karibu alichomaanisha Mwalimu au kama umesoma na kuelewa falksafa ya ujamaa na kujitegemea hakika unastahili kuwa mjamaaa tena wa kweli! Hicho kilichomo ndani ya moyo wako ndio utu! Wasi wasi wangu ni kuwa wangapi wanaweza kuwa na moyo kama wa kwakoaa?

  Mapendekezo yako nimeyaona, binafsi nimetatizwa na kipenghele cha pili, unajua hapa mjini watu wana ratiba tofauti hivyo huenda ikawa vigumu kwa pendekezo la pili kufanya kazi

  Jambo la msingi ni kuwa serikali kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili na siasa iwekwe pembeni katyika mambo ya msingi yanayorudisha uchumi wa nchi nyuma.

  Jefta Chaulo

  May 23, 2011 at 10:18 PM

 2. Ni wazo zuri sana na linaweza saidia kwa kiwango kikubwa sana. Changamoto ninayoona hapa ni jinsi ya kuwaelimisha wenye magari napia kuwahamasisha viongozi wa serikali za mitaa ili walipokee jukumu hili bila mizengwe. Kama kawaida watadai siyo kazi yao. Mimi naunga mkono kwa 100% – NIPITIE

  Charles Lyimo

  May 23, 2011 at 10:19 PM

 3. Bila shaka ni wazo zuri kwa vile linalenga kutatua tatizo la kijamii. Hata hivyo, utekelezaji wa mpango huo iwe umeanzishwa na wenye magari ama yeyote yule, hakika kutakuwa na tatizo la usalama (umelitaja kwenye pendekezo namba 3). Hata kama kutakuwa na utaratibu wa kuratibu mpango huo ili kuepusha masuala ya kiusalama, je, sheria za nchi zitakuwa na mtazamo gani juu ya jambo lenyewe? Kumbuka kwamba, kutekelezwa kwa mpango kama huo kutakuwa na nia nzuri, lakini kuna kundi fulani litaamua kuchukulia ni fursa kwao kutekeleza mbinu zao ovu (kuteka ikiwa ni mojawapo). Tukizingatia mfumo dhaifu tulionao (mfano uwepo wa rushwa nchini), polisi hakika hawatatoa ushirikiano wa kutosha na mpango mzima utaleta hasara kubwa katika jamii yetu. Huu ni mtazamo wangu wa haraka haraka. Tukitaka tuone kama kwa kufanya hivyo tutatatua tatizo la usafiri hasa jijini Dar es Salaam, basi tufanye utafiti wa kutosha, ili tupate taarifa za kutosha kuweza kutengeneza Sera yenye kuleza faida kwa wadau. (Conduct an Impact Evaluation under pilot study approach), kwa kuchagua barabara kadhaa zitakazohusishwa na mradi huo, vinginevyo, hatuwezi kuendelea kufanya vitu vyetu kienyeji namna hiyo tu kukisahau kwamba, tuko karne ya 21.

  Chonza, E. D.

  May 23, 2011 at 10:32 PM

 4. Jacky,

  my Cuban experience inaniambia hii haitekelezeki.

  tahir

  May 23, 2011 at 10:41 PM

 5. HIVI karibuni Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini Sumatra ilisisitiza agizo lake ililowahi kulitoa siku za nyuma kupiga marufuku mabasi kujaza mafuta yakiwa na abiria ndani.Hatua hii ya Sumatra ni nzuri kwa sababu inalenga kunusuru maisha ya watu ambao wanaweza kuteketea kwa moto endapo itatokea mlipuko wa mafuta.Hata hivyo agizo hili limeshindikana kutekelezeka kutokana na kukosa usimamizi wa sheria za usafirishaji abiria ya mwaka 1973 ambayo pamoja na mambo mengine iunaeleza uslama wa abiria wanapokuwa katika vyombo vya usafiri.Sio jambo la ajabu kuona mabasi madogo hata mabasi makubwa ya kwenda mikoani yakiwa na abiria yakiingia kujaza mafuta katika vituo vya mafuta huku askari polisi wa wakiangalia.Wakati Watanzania tumeshindwa kusimamia suala hili majirani zetu wa Kenya Uganda na Rwanda sio tu wamedhibiti mabasi kuingia vituoni kujaza mafuta yakiwa na abiria bali hata wameweza kupiga marufuku abiria kusimama linaposafiri.Faida ya kuboresha usafiri huu wa abiria hususan wa daladala ni kwamba utawafanya watu wengi wenye magari wasitumie magari yao kwenda kazini badala yake watumie usafiri wa umma.Hivi sasa usafiri wa dalalala nchini ni vurugu tupu kwa sababu mbali ya baadhi ya abiria kulazimika kuingia ndani ya basi kwa kupandia dirishani kuna adha ya kusimama huku wamebanana na baadhi ya vibaka hutumia mwanya huo kuwachomolea kuwaibia. Hata kwa nchi ambazo zimeendelea kama Marekani na Uingereza wananchi wake hutumia magari yao binafsi kwenda kwenye vituo vya usafiri wa umma wa treni na mabasi na kuyaacha hapo hadi wanaporejea kutoka kazini.Usafiri mkubwa wanaoutumia ni mabasi na treni ambayo yanabeba watu wengi kwa wakati mmoja badala ya kila mtu kuingiza gari lake barabarani kwenda kazini kwake.Tunalazimika kuhoji nini kimesababisha sisi Watanzania tushindwe kuboresha usafiri wa abiria mijini wakati wenzetu wa Uganda Kenya na Rwanda wameweza.Wenzetu hao wamesimamia ipasavyo sheria hiyo ambapo basi linalikuta limesimamisha abiri ndani kondakta na abiria wanatolewa nje na kutozwa fani wote. yaani kondakta anatozwa faini ya kurushu abiria kusimama na abiria kukubali kusimama ndani ya basi.Polisi wanashindwa nini kuwakamata madereva wanaozidisha abiria au kujaza mafuta wakiwa na abiria ndani ya mabasi?

  business daily

  May 24, 2011 at 7:23 AM

 6. Wazo jema sana, nadhani likiungwa mkono na kuboreshwa zaidi linaweza kuwa na ufumbuzi wa tabu na matatizo yetu ya kila siku hasa wakazi wa jiji la Dar.

  Saidi Msonga

  May 25, 2011 at 2:32 PM

 7. Tatizo ukiwapa lift wanakuibia laptop !

  Max

  October 14, 2011 at 4:26 PM


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: