Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

Zitto ‘amgeuzia kibao’ CAG(Gazeti la Mwananchi)

with 3 comments

RUZUKU VYAMA VYA SIASA

*ADAI AMESHINDWA KUKAGUA SH83 BILIONI

Kizitto Noya

WAZIRI Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe ametaka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ichunguzwe kwa uzembe wa kushindwa kukagua hesabu za ruzuku za vyama vya siasa kwa muda wa miaka mitatu.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Kabwe alisema CAG ameshindwa kukagua ruzuku ya Sh83 bilioni iliyotolewa kwa vyama vya siasa nchini tangu mwaka 2005 hadi 2010.

Alisema ingawa kuna tatizo katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, CAG hawezi kumtupia mzigo huo pekee yake kwani naye anahusika.

“Nikiwa Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, ninamwomba CAG afanye audit (ukaguzi) kwa vyama vyote vya siasa kwa miaka mitatu iliyopita sasa na siyo baada ya miezi sita,” alisema Kabwe na kuongeza:

“Ruzuku ya vyama vya siasa ni eneo ambalo huwa haliangaliwi kabisa na fedha nyingi ya walipa kodi inakwenda katika vyama. Kuanzia mwaka 2005 mpaka 2010 jumla ya Sh 83 bilioni zimetolewa kama ruzuku kwa vyama vya siasa,” alisema Kabwe na kuongeza:

“Fedha zote hizi kwa miaka yote hii, hazikuwa zinakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, (CAG).”

Kwa mujibu wa Kabwe, ubadhirifu unaoweza kujitokeza kwenye fedha za ruzuku zinazotolewa kwa vyama vya siasa, unatokana pamoja na mambo mengine na CAG kushindwa kukagua ruzuku hizo tangu vyama vianze kuipata mwaka 1996.

“Ndiyo maana kumekuwa na ubadhirifu mwingi wa fedha za ruzuku kwenye vyama takriban vyote hapa nchini,” alisema Zitto.

Alisema mwaka 2008, alipeleka pendekezo la mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa katika Bunge la Novemba kutaka vyama vikaguliwe na CAG.

Alisema pendekezo lake lilisomeka: “Vyama vyote vitakaguliwa na CAG na itakuwa ni jukumu la vyama vya siasa kupeleka taarifa zao kwa CAG kwa mujibu wa sheria.”

“Hivyo tangu mwaka 2008 vyama vinatakiwa vikaguliwe na CAG kwa mahesabu yao lakini mpaka sasa hakuna chama ambacho kimeshakaguliwa,” alisema Zitto na kuongeza:

“CAG mwaka huu amelalama tu kwenye taarifa yake kuwa vyama havikupeleka taarifa zao kwa Msajili. Ametoa miezi sita ili wasahihishe makosa? miezi sita ili watafute nyaraka za kugushi ili kuyaweka mahesabu sawa?” alihoji.
Kabwe alisema kauli ya CAG kwamba hahusiki kuvikagua vyama vya siasa ni kukwepa majukumu kwani sheria ya sasa inamtaka afanye hivyo kwa kuteua wawakilishi.

“Hakuna sababu kwa CAG kutoa miezi sita kwa vyama, bali vyama sasa viheshimu Public Audit Act,(Sheria ya Ukaguzi wa Fedha za Umma), Public Finance Act (Sheria ya Fedha za Umma) and (na) Political Parties Act (Sheria ya Vyama vya Siasa)”

Kwa mujibu wa Kabwe, CAG anapaswa kudai mahesabu kutoka kwa vyama na wala si kusema kuwa hahusiki na watu binasi. “Vyama siyo ‘individuals’, vyama ni taasisi,” alisema.

“Kwa sheria mpya, wakaguzi wa vyama wanapaswa kuteuliwa na CAG na siyo vyama kwenda kuokota wakaguzi na kuweka hesabu zao kama ambavyo imezoeleka,” alisema.

Zitto alisema vyama vya siasa ndivyo vinavyounda Serikali, hivyo iwapo haviheshimu fedha za walipa kodi, Serikali wanazounda haziwezi kuheshimu fedha za walipa kodi.

“Ruzuku iliyotolewa kwa vyama mwaka 2010 ilikuwa ni mara tatu ya Bajeti ya Wizara ya Afrika Mashariki au ni zaidi ya Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara. CAG ni lazima afanye kazi yake,” alisema na kuongeza:

“Msajili wa Vyama naye achunguzwe, ofisi yake inafanya kazi kwa mujibu wa sheria, kwa nini hakuwa na taarifa za vyama vya siasa wakati yeye ndiye mwenye jukumu la kusimamia vyama.”
“Iwapo anashindwa kusimamia ruzuku kukaguliwa atawezaje kusimamia matumizi ya fedha kwenye uchaguzi wakati uchaguzi uligubikwa na matumizi ya fedha nyingi za kifisadi,” alidai Zitto.

Ripoti ya CAG iliyoishia Juni 30 mwaka 2010, imeeleza kuwa vyama sita vyenye wawakilishi bungeni vimeshindwa kuonyesha taarifa za matumizi ya ruzuku ya Sh17.14 bilioni.

Vyama hivyo ni CCM, CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi, TLP na UDP. Katika hesabu za kawaida kuhusu fedha hizo, chama hicho tawala kimepata mgawo wa Sh12 bilioni kutokana na asilimia 70 ya mgawo.

CUF kinachopata asilimia 20 ya ruzuku kimepata mgawo wa Sh3.43 bilioni, Chadema chenye asilimia nane Sh1.37 bilioni na vyama vitatu vinavyoshikilia asilimia mbili Sh343 milioni.

Akijibu Madai hayo, Utouh alisema: “Sijakwepa majukumu. Fedha zinatoka serikalini, zinakwenda kwa Msajili wa Vyama.”

“Yeye (Msajili), ndiye mwenye kazi ya kuvigawia vyama fedha hiyo na sheria inataka baada ya matumizi, vyama vinapaswa kutengeneza hesabu zake na kuziwakilisha kwa Msajili. Siyo kazi yangu kuvitengenezea mahesabu vyama vya siasa.”

Kuhusu madai ya Zitto kwamba utaratibu huo wa Msajili kukagua vyama uko kwenye sheria ya zamani ambayo Zitto alidai kwamba alishatoa mapendekeza bungeni na kufanyiwa marekebisho, yanayomtaka CAG kuteua wakaguzi wa hesabu za vyama vya siasa, Utouh alisema:

“Mwulize yeye (Zitto) chama chake kilishanipelekea mahesabu ili niyakague kama anajua hivyo ndivyo inavyotakiwa? Tupo hapa kufanya kazi. Hatupo kukwepa majukumu. Mwulize kama hivyo ndivyo sheria inavyotaka Chadema ilishawahi kuniletea mahesabu yake?”

Chanzo: Gazeti la Mwananchi

Written by zittokabwe

April 21, 2011 at 9:14 AM

3 Responses

Subscribe to comments with RSS.

 1. […] Zitto ‘amgeuzia kibao’ CAG(Gazeti la Mwananchi) (via Zitto na Demokrasia) April 21, 2011 Sajjo L.M. Leave a comment Go to comments RUZUKU VYAMA VYA SIASA *ADAI AMESHINDWA KUKAGUA SH83 BILIONI Kizitto Noya WAZIRI Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe ametaka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ichunguzwe kwa uzembe wa kushindwa kukagua hesabu za ruzuku za vyama vya siasa kwa muda wa miaka mitatu. Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Kabwe alisema CAG ameshindwa kukagua ruzuku ya Sh83 bilioni iliyotolewa kwa vyama vya siasa nchini tangu m … Read More […]

 2. Kwanza hongera sana Mh.Zitto kwa kutoa taarifa muhimu ya kinachoendelea juu ya siasa ya Tanzania.kwa sisi tulioko nje na Tanzania inatusaidia sana.Nichangie kuhusu hii repoti.Itawezekanaje kweli nchi kukosa statistic kamili kutoka ktk idara husika kwa wakati na kwa usahihi.Inamaana viongozi husika ni kweli hawafanyi wajibu wao.Huwa sielewagi kabisa kabisaa.Ukiachana na hii report ,ukitaka kujua tuna mapungufu makubwa katika kutoa statistic za ukweli.Hembu jaribu kumuuliza Mkuu wa police Tanzania Je ni watanzania wangapi wanakufa kwa siku kwa uzembe barabarani mfano amelewa na kuendesha gari au kuchomokea au kupita taa nyekundu n.k .Naamini atasema apewe muda ndio aweze kuwa na jibu.Swali,Je siku zote anafanya nini ofisini?Nionavyo mimi viongozi wengi ila sio wote hapo nyumbani ni wavivu na wazembe.Lakini naamini tukiamua Inawezekana kujenga Tanzania bora.
  Mdau toka USA

  vabisay

  April 21, 2011 at 6:31 PM

 3. Vyama vya siasa ni jukumu lenu kupeleka taarifa za fedha kwa CAG.Mnaonesha kidole kimoja kwa mwingine vinne vinakuoneshea wewe.Tuanzie kuondoa ufisadi kwenye vyama bila kuangalia CHADEMA,CCM wala CHAUSTA

  Makaya

  April 26, 2011 at 6:43 PM


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: