Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

PRESS RELEASE/TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

with one comment

Leo asubuhi Kamati ya Mashirika ya Umma imekutana na Waandishi wa Habari nakutoa taarifa yao.

****************

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

1.0 UTANGULIZI

Kamati ya kudumu ya Bunge ya kusimamia mahesabu ya Mashirika ya Umma ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Zitto Kabwe,MB (CHADEMA) ilifanya ziara ya ukaguzi wa ufanisi katika miradi ya makaa ya mawe ya Mchuchuma, Liganga,Ngaka na Kiwira kuanzia tarehe 6 – 10 Machi,2011.

Kamati ilifanya hivyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake yaliyoainishwa na kanuni ya 13 (a) – (e) ambayo miongoni mwake ni:

  • kusimamia ufanisi wa mashirika ya umma;
  • kushughulikia maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za mashirika ya umma;
  • kufuatilia sera ya ubinafsishaji wa mashirika ya umma.

Ziara ya Kamati ilifanyika katika eneo ambalo Kamati imeliita Eneo Mkakati la uzalishaji wa Megawatt 1500 za Umeme kusini mwa Tanzania (South Tanzania’s 1500MW Strategic Complex) liko katika Wilaya za Ludewa, Mbinga na Ileje/Kyela mkoani Mbeya.

2.0 KATIKA ZIARA HII KAMATI IMEBAINI YAFUATAYO:

1.      Eneo hili lina uwezo wa kuzalisha umeme wa Megawatt 1500 ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo na kuendelea na uzalishaji kwa kipindi cha miaka 150 ijayo kabla ya makaa ya mawe kwisha kabisa.

2.  Kwa mujibu wa Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Mahesabu (CAG) kwa mwaka unaoishia Juni 2009, NDC imewekeza jumla ya Shilingi 1.4 bilioni katika Mradi wa Chuma Liganga , ikiwa ni pamoja na gharama za utafiti zinazofikia Dola za Marekani 36,563.00. Mradi huu ambao bado haujaanza uzalishaji unatarajiwa kuzalisha chuma na kuongeza thamani hapa hapa nchini kabla ya kuuza nje ya nchi. NDC imepewa jukumu la kusimamia rasilimali za Chuma Liganga zinazokadiriwa kuwa Tani 1.2bn, rasilimali ambazo kama zitaendelezwa zitachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi hasa katika uzalishaji wa umeme na hivyo kusukuma mbele maendeleo ya taifa.

3. NDC wanategemea kuingia ubia na Kampuni ya Sichuan Hongda Corporation toka nchini China kuendesha Mradi wa Makaa ya mawe wa Mchuchuma na kuchimba Chuma Liganga, mradi unaotegemewa kugharimu Dola za Kimarekani 3.0 Bilioni. Mkataba wa Ubia bado haujasainiwa na unasubiri maamuzi ya Baraza la Mawaziri. Mradi wa Mchuchuma unategemea kuzalisha 600MW za Umeme. Mradi wa Liganga unatarajiwa kuzalisha Chuma kwa matumizi ya ndani na pia kuuza nje ya nchi kuliingizia Taifa fedha za kigeni.

4. NDC wameingia ubia na Kampuni ya Atomic Resources ya Australia na kuunda kampuni tanzu ya TANCOAL Energy kwa ajili ya kuchimba Makaa ya Mawe eneo la Ngaka Wilayani Mbinga kwa lengo la kuzalisha Umeme 450MW.  Mkataba wa Ubia unaonyesha kuwa NDC watakuwa na Hisa asilimia 70. Uwekezaji katika mradi huu utakuwa takribani Dola za Kimarekani 350m.

5. Kamati imefuatilia mchakato wa kurejesha Serikalini umiliki wa Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira na kubaini kuwa mchakato huo bado haujakamilika licha ya miaka miwili kupita tangu Serikali ilipotangaza azma hiyo.

6. Kamati imefuatilia utekelezaji wa agizo lake kwa Mashirika ya Hifadhi ya Jamii kuwekweza kwenye miradi ya Umeme na kubaini kuwa mchakato wake bado haujafika mbali. Shirika la NSSF kama sehemu ya utekelezaji wa agizo la Kamati limeomba kumilikishwa mgodi wa Kiwira. NSSF kwa kushirikiana na mwekezaji mwingine (strategic investor) wanatarajia kuwekeza dola za kimarekani 400m na kuzalisha 500MW katika kipindi cha miaka mitano.

7. Kamati imependekeza kwa Shirika la CHC kushirikina na ofisi ya CAG ili kuharakisha zoezi la tathmini na uchunguzi maalum (special audit) wa Mali na Madeni ya Kiwira Coal and Power Limited (KCPL). Wakati zoezi hili linaendelea Serikali (Wizara ya Fedha) Kamati inapendekeza kwamba Serikali iwape Shirika la NSSF ‘letter of intent’ ili waanze taratibu za zabuni kwa ajili ya kupata ‘strategic investor’ na masuala mengine muhimu kwa ajili ya kufufua mgodi wa Kiwira na kuzalisha umeme.

8.      Kamati imebaini kwamba mipango ya Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC)  katika miradi ya Liganga, Mchuchuma na Ngaka iwapo itatekelezwa kwa haraka na kwa umakini, na vile vile maagizo ya kuwapatia Mradi wa Kiwira Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kutazalisha 1500 MW za umeme ambazo si tu zitamaliza kabisa tatizo la umeme tulilonalo bali kuwa ni hatua ya nchi hii kuanza kuuza umeme nje ya nchi.

9. Umeme utakaozalishwa katika vyanzo hivi utatakiwa kusafirishwa kwa msongo (Transmission lines) wa 400kv kutoka Mchuchuma mpaka Mufindi (kwa mradi wa Mchuchuma) na kutoka Kyela mpaka Mbeya (kwa mradi wa Ngaka). Hii bado ni changamoto kubwa katika kufikia lengo la Taifa kujitosheleza kwa Nishati ya Umeme.

3.0 MAPENDEKEZO YA KAMATI

1.      Kamati inalipongeza Shirika la NDC kwa hatua kubwa waliofikia katika Miradi ya Mchuchuma, Liganga na South Ngaka. Hata hivyo juhudi zaidi zinatakiwa ili kuhakikisha kuwa miradi hii inatekelezwa katika muda mwafaka.

2.      Mkataba wa ubia  baina ya Shirika la NDC na  Kampuni Sichuan Hongda toka China ili kuendeleza Mradi wa Mchuchuma-Liganga ni muhimu usainiwe sasa na haraka na Serikali ishauriwe kutimiza wajibu wake kwa hatua ambayo NDC imefikia ikizingatiwa faida za kiuchumi za Mradi huu. Mazingira ya sasa ya uchumi wa Dunia na mahitaji ya Taifa ni mwafaka kwa miradi ya Makaa na Chuma. Kuchelewa kuanza kwa miradi hii kwaweza sababisha miradi isifanyike kabisa kwani uchumi wa dunia kwenye bidhaa za chuma huwa unayumbayumba sana (fluctuations).

3.      Kampuni tanzu itakayoundwa ili kuendesha miradi hii ifuate taratibu zote za uchimbaji ikiwemo kusainiwa kwa Mkataba wa Uendelezaji Migodi (Mineral Development Agreements-MDA) kwa madhumuni ya kulinda maslahi ya Serikali, Watu wa Ludewa na Kampuni yenyewe.

4.      Kwa kuwa suala la Ubia bado halijaamuliwa, Kamati inashauri kuwa ubia uzingatie kanuni ya faida (profitability and Pay Back period). Kwa mfano, NDC waweza kuanza kwa kuwa na hisa 20% lakini mara baada ya mradi kulipa (payback period) mgawo wa hisa uwe ni sawa kwa sawa. Pendekezo hili pia lizingatiwe kwa mradi wa Ngaka ambapo NDC wanahisa 30% kwenye Kampuni tanzu ya TANCOAL Energy.

5.      Wizara ya Nishati na Madini iharakishe kutoa leseni ya uchimbaji wa Makaa ya Mawe kama ilivyoombwa na kampuni ya TANCOAL ambayo inamilikiwa kwa ubia na NDC ili uchimbaji wa maakaa uanze na hivyo kuanza kuzalisha Umeme. Inapendekezwa kuwa Umeme unaotokana na Makaa ya South Ngaka uzalishwe kutokea Wilaya ya Kyela ili kurahisisha kuunganisha na gridi ya Taifa.

6.      Kamati inapendekeza kwa Kamati ya Nishati na Madini kuanza mchakato wa kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini kwa lengo la kutangaza kwamba Rasilimali za Makaa ya Mawe na Chuma kuwa ni Rasilimali za kimkakati (strategic resources) na kwamba leseni za kumiliki vitalu vya madini haya zitamilikiwa na Mahirika ya Umma tu. Pendekezo hili linatokana na ukweli kwamba kuna leseni nyingi sana za kumiliki madini haya ambazo zimemilikishwa kwa watu binafsi (speculators). Inapendekezwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba leseni zote za kumiliki vitalu vya Chuma na Makaa ya Mawe zinazomilikiwa na watu binafsi au makampuni ya nje zifutwe na kumilikishwa kwa ama STAMICO au NDC. Hata hivyo, ifikiriwe kuundwa kwa Shirika la TANZANIA IRON AND COAL CORPORATION itakayomilikiwa kwa ubia na STAMICO na NDC na Shirika lingine lolote la Umma kwa lengo la kuendeleza rasilimali ya Makaa ya Mawe na Chuma hapa nchini.

7.      Kamati inalitaka Shirika la Umeme nchini TANESCO kuanza kuwekeza katika msongo wa kusafirisha umeme (TRANSMISSION) kuelekea kwenye miradi hii ili kufanya miradi hii iwe na maana. Kamati imefurahishwa na wazo la wabia wa NDC kujenga msongo wao wa umeme. Hata hivyo, Kamati inaamini kuwa suala la msongo wa umeme liendelee kuwa chini ya Shirika la TANESCO au Serikali iunde Kampuni nyingine ya Umma kwa ajili ya Transmission peke yake. Kwa ajili ya uharaka wa msongo wa sasa Kamati inashauri kuwa wabia wa NDC wajenge msongo huu kama mkopo kwa Shirika la TANESCO.

8.      Kamati ya POAC itaandaa mkutano wa wadau kuhusu miradi ya Mchuchuma na Liganga, Nkaga na Kiwira. Lengo la mkutano huu ni kufahamu mipango ya Serikali na Mashirika katika utekelezaji wa miradi hii. Mkutano huu utahusisha Mashirika ya NDC, STAMICO, TANESCO, NSSF na CHC. Pia Makatibu wakuu wa Wizara za Viwanda na Biashara, Nishati na Madini, Kazi na Ajira na Wizara ya Fedha na Uchumi. Wenyeviti wa  Kamati za Bunge za Viwanda na Biashara  na ile ya Nishati na madini watahudhuria ili kuangalia uwezekano wa kuharakisha miradi ya Mchuchuma, kiwira na liganga kwa lengo la kuzalisha Nishati ya Umeme, kukuza Uchumi kwa kuuza nje Chuma, kutengeneza ajira na kuleta maendeleo kwa Taifa letu. Mkutano huu umepangwa kufanyika siku ya Jumatatu tarehe 21 Machi 2011.

4.0 MGODI WA MAKAA YA MAWE KIWIRA

Kwa mujibu wa Fasili ya 13 (e) ya nyongeza ya nane ya kanuni za Kudumu za    Bunge Toleo la mwaka 2007 inayosomeka” Kufuatilia sera ya Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma’’. Kwa kutumia Kanuni hii, Kamati ya POAC imetekeleza Yafuatayo;

NI MUHIMU Serikali ikatambua kwamba ni muhimu maagizo ya Kamati kwa Serikali kwamba Shirika la NSSF lipewe Mgodi wa Kiwira ili  kuweza kulikwamua shirika hilo.

HITIMISHO

Kamati inaendelea kutoa tahadhari kwamba kuchelewa kusaini mkataba wa NDC na Kampuni ya Sichuan Hongda ya kutoka China na pia kutokamilisha mchakato wa kuumilikisha mgodi wa Kiwira kwa NSSF kunachelewesha maendeleo ya Taifa.

Kamati inategemea kutumia Taarifa yake ya mwaka 2009/2010 ikijikita zaidi kwenye Mashirika ya Umma yanyojihusisha na Miundo mbinu na Nishati kama kichocheo cha Maendeleo ya Taifa.

Advertisements

One Response

Subscribe to comments with RSS.

  1. Great article keep up the spirit

    Oscar Ronald

    March 16, 2011 at 3:06 PM


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: