Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

KIWIRA, TANESCO na NSSF

with 5 comments

Na Zitto Kabwe

Katika gazeti la Mwananchi Jumapili la tarehe 27 Aprili 2011 ndugu yangu Lula Wa Ndali Mwananzela aliandika makala nzuri sana. Makala hiyo ilibeba kichwa cha ‘Kwa nini TANESCO isipewe Kiwira’ ikiwa kama hoja mbadala. Lula anafungua makala yake kwa kusema ‘kitu pekee ambacho hawataki kukifanya ni kuiweka Kiwira chini ya TANESCO’. Sijui kwa nini alianza na kauli hii. Hata hivyo hii ni makala ambayo ni vema ipate majibu ili kuweka sawa mjadala huu wa umiliki wa KIWIRA.

Mjadala uliopo sasa ni wa Shirika la NSSF kupewa mgodi wa KIWIRA na kuwekeza ili kuchimba makaa ya mawe na kisha kuzalisha umeme kiwango cha 200MW. Ndugu Lula pamoja na baadhi ya Watanzania wametia mashaka juu ya wazo hili na makala ninayoijadili hapa ni sehemu ya kujaribu kutafuta mbadala wa wazo hili la NSSF. Ningependa kwanza kutoa taarifa za awali ili kuhakikisha kuwa wasomaji wanaelewa nini kilipelekea wazo hili la NSSF kuingia katika uzalishaji wa umeme na hata wazo la mgodi wa KIWIRA kukabidhiwa NSSF.

Sote tunafahamu hadithi nzima ya mgodi wa KIWIRA. Kwamba mgodi ulibinafsishwa bila kufuata taratibu kwa Kampuni yenye mahusiano na Rais mstaafu Benjamin Mkapa na Waziri wake Daniel Yona, ni taariffa inayojulikana kwa umma. Mambo kadhaa hayajulikani kwa umma na hivyo wakati mwingine watu kutoa maoni bila habari kamili.

Mojawapo ya habari ambazo inawezekana hazijulikani ni kwamba kampuni ya TANPOWER RESOURCES ambayo ilimilikishwa mgodi wa KIWIRA ilichukua mikopo kutoka taasisi za kifedha ili kuanza uzalishaji kwa kuchimba makaa ya mawe na kisha kuyatumia kuzalisha umeme. Baadhi ya taasisi ambazo zilitoa mkopo huu ni pamoja na mifuko ya hifadhi ya jamii kama NSSF na PSPF. Mikopo hii ilidhaminiwa na Benki ya CRDB. NSSF pekee waliwapa Tanpower Resources jumla ya dola za kimarekani milioni 7 na mpaka sasa hazijalipwa. Serikali ilipotangaza kuuchukua mgodi huu, tukaanza kuhoji hatma ya fedha hizi za mifuko itakuwa nini.

Kutokana na hali halisi kwamba mgodi huu unaweza kuzalisha umeme wa kutosha na kwa faida na kinachotakiwa ni uwekezaji tu, baadhi yetu tukaja na wazo kwamba deni la NSSF kwa KIWIRA libadilishwe kuwa mtaji (equity) na hivyo mfuko kuwa sehemu ya wamiliki wa mgodi na kisha mgodi uanze kazi. Hili ni suala la kawaida kabisa katika biashara duniani lakini pia ni suala ambalo lingerahisisha umiliki wa Serikali kwa mgodi huu. Mimi binafsi nilitoa wazo hili ili kulinda fedha za umma katika vikao vya kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma. Ilibidi wazo hili likafanyiwe kazi na wataalamu kuweza kufahamu kama litakuwa na maslahi kwa Mfuko.

Baada ya tafiti mbalimbali kufanywa, iligundulika kuwa kote duniani, narudia, kote duniani mifuko ya hifadhi ya jamii imewekeza sana kwenye nishati. Nchini Ufaransa na Malaysia zaidi ya robo ya umeme unaozalishwa hutokana na uwekezaji uliofanywa na mifuko yao ya hifadhi ya jamii. Vile vile ilionekana kuwa licha ya faida kwa uchumi wa nchi, uwekezaji katika kuzalisha umeme una faida kubwa sana kwa mifuko yenyewe na hivyo kulinda fedha za michango ya wafanyakazi na kuwahakikishia malipo yao pindi muda wa kulipa unapofika. Hivyo, wataalamu wa uchumi, uwekezaji katika madini na umeme wakashauri kwamba NSSF wamilikishwe mgodi wote kwa asilimia 100, wawekeze, wazalishe umeme na kuuza kwa TANESCO. Ifahamike pia kuwa taasisi za fedha zilizoikopesha tanpower resources zilishatoa notice kuifilisi kampuni hii ili wauze mali na mali ya kampuni hii kisheria ni mgodi. Uuzaji wa namna hii unahatarisha azma ya Taifa ya kimkakati (strategic decision) ambayo ni kuzalisha umeme. NSSF walikuwa tayari kununua madeni yote, kulipa wafanyakazi na kuwekeza kama sehemu ya mkakati wao wa kusambaza vitega uchumi vyao (diversification of assets).

Ikumbukwe pia kwamba mnamo mwezi Mei mwaka 2010, Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma ilikutana na Mifuko yote ya hifadhi ya jamii na kuwaagiza washiriki katika juhudi za kuongeza uzalishaji wa Nishati ya Umeme ili kuepuka mikataba isiyo na maslahi ambayo kampuni binafsi zinaingia na Shirika la Umeme la TANESCO. Mikataba hii yenye ‘capacity charges’ na gharama nyingine kubwa inalitafuna Taifa kweli kweli. Sasa tunapopata Shirika la Umma lingine lenye uwezo wa kushindana na sekta binafsi, Taifa linafaidika zaidi. Baada ya maelezo haya nijaribu kuangalia hoja kadhaa za ndugu Lula ambaye anashauri kuwa TANESCO wapewe KIWIRA (ninaamini badala ya NSSF).

Ndugu Lula anasema, viongozi wanataka kujenga Taifa la wastani, yaani taifa ambalo halitaki kujaribu mambo makubwa. Moja ya mambo makubwa anayoshauri yeye ni kuiweka Kiwira chini ya TANESCO. Lula anasahau kuwa TANESCO ndiyo yenye ukiritimba wa uzalishaji umeme nchini. Wakati ‘installed capacity’ ya umeme nchini ni 1034MW, za makampuni binafsi ni takribani 180MW pekee za Songas na takribani 30 MW za makampuni mengine madogo madogo. Hata ukiweka 100MW za IPTL na baadaye 100MW za Dowans bado TANESCO watakuwa na zaidi ya 60%ya uzalishaji wa umeme. TANESCO wamekabidhiwa uhodhi kwenye usafirishaji (Transmission) na usambazaji. TANESCO ni lidubwana likubwa kweli kweli! Lula anataka tuwarundikie na KIWIRA.

Ikumbukwe KIWIRA ni 200MW pekee zinaweza kuzalishwa wakati TANESCO wana miradi mikubwa kama ule wa Kinyerezi wa 240MW na bado wanasuasua nao. Ni akili ya kawaida sana kuwa hatuwezi kuwatutika mzigo mwingine.

Lula afahamu kuwa kupewa mgodi ni jambo moja na kuwekeza ni jambo linguine. TANESCO hawana fedha za kuwekeza katika KIWIRA. Hata kama wangekuwa na fedha hizo ingekuwa bora TANESCO wawekeze kwenye njia za kusafirisha umeme ambazo zimechoka na zinapoteza 23% ya umeme wote unaozalishwa katika vyanzo vya Maji. Kiwango hiki cha umeme unaopotea ni sawa na kupoteza dola milioni 100 kila mwaka, yaani tunazalisha umeme na kuutupa! Kama TANESCO wana fedha wawekeze huko na kuachia uzalishaji wa umeme kwa wengine.

Kenya, kuna kampuni mbili za Umma – moja inazalisha tu umeme na nyingine inasafirisha na kusambaza. Ile ya kuzalisha inaitwa KenGen. Inapata faida na ipo kwenye soko la hisa la Nairobi! Ile ya kusambaza inaitwa KPLC. Inapata faida na ipo kwenye soko la hisa pia. Juzi tu KPLC wametoa ‘right issue’ ya hisa zake na Rais Kibaki alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kuuza hisa hizi kwa wakenya. Tunataka ifikie mahala ambapo TANESCO wataweza kuweka muda kwenye kusafirisha umeme unaozalishwa kwenye vyanzo mbalimbali na kuusambaza kwa Wateja.

Nikipata Mashirika ya Umma yenye kuweza kuzalisha umeme wa kutosha na kuiuzia TANESCO gharama nafuu, nitafurahi zaidi kwani Taifa litaondokana na mikataba ya kinyonyaji ambayo TANESCO imeingia na kampuni binafsi. Ndio maana ninaunga mkono NSSF kuwekeza katika uzalishaji wa umeme. Huku ndio kufikiria na kufanya mambo makubwa! Anachoshauri ndugu Lula ni ‘status quo’ ama business as usual. Ni kufikiria kwa wastani ili kujenga Taifa la wastani. Uamuzi wa kuipa NSSF mgodi wa KIWIRA ni kufikiria makubwa na kujenga Taifa linalofanya mambo makubwa. Fikra za Uongozi wa NSSF ni sawa na fikra za Dr. Mahathir Mohammed na ndio fikra ninazoamini zitaitoa nchi kutoka ilipo hivi sasa.

Ndugu Lula anasema mpango wa NSSF kumiliki KIWIRA unaacha maswali mengi. Hayataji maswali hayo na kuishia kusema ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa. Nadhani kwa faida ya wasomaji wake ni vema angeuliza maswali hayo ili aweze kupata majibu badala ya kunung’unika tu. Ninaamini kabisa kuwa maswali yote yana majibu, anaweza kuyakataa majibu hayo lakini hatakosa majibu. Kwamba kwa nini ‘hawataki kuiacha kiwira mikononi mwa TANESCO’ nimejaribu kulijibu huko juu. Kwanza sio suala la kuiacha kiwira kwa tanesco maana tanesco hawajawahi kumiliki KIWIRA. KIWIRA ilikuwa mali ya STAMICO na katika makala yake yote hazungumzii kabisa Shirika hili. KIWIRA ilijengwa wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi (Lula kasema wakati wa Nyerere, amekosea. Ilijengwa mwaka 1988) ilimilikiwa na STAMICO kabla ya kumpa Mkapa na rafiki zake. Ningemwelewa hoja yake kama angesema kiwira irudi kwa STAMICO, wazalishe makaa, wazalishe umeme na kisha wauze kwa TANESCO. Hoja hii pia nimewaambia NSSF. Kwamba Kiwira waimiliki kwa Ubia na STAMICO kwani STAMICO ndio Shirika letu la Umma kwenye uchimbaji. Hawana fedha za kuwekeza kwenye mradi mkubwa kama huu, hivyo wapate hisa ambazo watazilipa kutokana na mgawo wa faida (dividend) yao. NSSF ni mwekezaji, ana fedha. Utaalamu ataupata kwa STAMICO na menejiment watakayoiweka. NSSF haiendi kuchimba madini. Inawekeza fedha zake kwenye kampuni yake tanzu. Maana kuna maswali sasa hawa wanajua nini kuhusu umeme. NSSF ni entrepreneur! Watanzania sasa ni lazima tuelewe masuala mepesi kabisa ya uendeshaji wa uchumi wa kisasa. Dr. Ramadhani Dau haendi kushika sururu au kuendesha crane. Anawekeza na kuajiri ‘the best managers’ wa kuendesha mradi.

Ndugu Lula anasema Kiwira ni kampuni ya serikali na tanesco ni kampuni ya serikali. Anahoji kuna ugumu gani wa kuiweka kiwira chini ya tanesco. NSSF ni kampuni ya serikali pia. Kuna ugumu gani kwa NSSF kumiliki KIWIRA, kuwekeza mtaji, kuchimba makaa ya mawe na kuzalisha umeme kisha kuuza umeme huo kwa tanesco ili tanesco wabaki na jukumu la kusafirisha umeme na kusambaza kwa wateja. Kuna ugumu gani?

Lula anashauri kuwe na kampuni mbili, moja ya kuchimba makaa ya mawe na hii hana tatizo ipewe NSSF na nyingine ya kuzalisha umeme. Hana tatizo NSSF kuchimba makaa ya mawe bali tatizo lake wasizalishe umeme. Sielewi.

Hoja kwamba uchimbaji ndio unahitaji uwekezaji mkubwa. Sijui ndugu yangu ana takwimu zipi kuhusu uwekezaji katika maeneo haya. Sababu ile ile ya kuikatalia NSSF kuzalisha umeme ndiyo hiyo hiyo angeitumia kusema kuchimba makaa ya mawe waachiwe STAMICO. Isipokuwa Lula akumbuke kwamba, kuna kitu kinaitwa ‘economies of scale’, kama uchimbaji makaa na uzalilishaji umeme vikifanywa na kampuni moja, gharama za uzalishaji zinasambaa na hivyo inakuwa ni nafuu. Kuwa na wamiliki wawili tofauti ina maana kutakuwa na mikataba ya kuuziana makaa jambo ambalo yeye mwenyewe hataki mikataba ya kuuziana umeme. Uwekezaji katika KIWIRA unahitaji kuwa ‘integrated’ kwa kuchimba makaa ya mawe na kuzalisha umeme ili kuleta Tija.

Ndugu Lula anahoji kama NSSF wanataka kusaidia kuzalisha umeme kwanini hawaagizi majenereta? Hapa ndugu yangu kakosa tu taarifa. Mpango wa NSSF ni kuzalisha 500MW kwa kuanzia. Kiwira 200MW na 300MW majenereta ya gesi, 100MW itawekwa Mkuranga ili kutumia gesi ya Mkuranga na 200MW zitawekwa Dar na kutumia gesi ya Songosongo. Kuna mawazo kuwa zote hizi 300MW ziwekwe Somanga Fungu na kujenga transmission lines mpaka Dar es Salaam. Hizi jenerata za kuzalisha 300MW NSSF wapo tayari kuzinunua hata jana. Ni vizuri kabla ya kuanza kutoa shutuma mtu akapata taarifa za kina. Kuna watu hawalali wanafikiri jinsi ya kumaliza tatizo la umeme nchini. NSSF wanafuata maagizo ya Kamati ya Mashirika ya Umma kwa umakini mkubwa kwani lengo letu ni kuondokana na mzigo mkubwa wa mikataba ya kuzalisha umeme kwa kujenga uwezo wa ndani wa kuwekeza. Juhudi hizi zapaswa kuungwa mkono na sio kubezwa. Labda tatizo la ndugu Lula ni wenye kubeba ujumbe huu na sio ujumbe wenyewe!

Mwisho, ni vema Watanzania wafahamu kuwa maamuzi ya mifuko ya hifadhi ya jamii kuwekeza kwenye kuzalisha nishati ya umeme yana faida kubwa sana kwa umma na kwa mifuko yenyewe. Kwa mfano NSSF wanapata fedha kutoka kwenye michango ya wanachama. Wanachama wao ni wafanyakazi kwenye viwanda, migodi, makampuni ya huduma nk. Iwapo nchi ikikosa umeme, viwanda vikafungwa na watu kukosa kazi, maana yake mifuko inapoteza wanachama na fedha pia. Iwapo umeme wa kutosha na wa uhakika unapatikana, viwanda vikaanzishwa, watu wakaajiriwa mifuko inapata wanachama na kupata fedha pia. Ni ‘interest’ ya mifuko kama NSSF kuona uchumi unapanuka na watu wanapata ajira. Mradi wa KIWIRA peke yake utatoa ajira zaidi ya 500 na hivyo kutengeneza wanachama wa mifuko zaidi ya 500. Hapo hujaweka kampuni za huduma ambazo zitaanzishwa kama sehemu ya ‘multiplier effect’! Huku ndio kujenga Taifa linalojaribu mambo makubwa.

Vile vile, mifuko ni lazima iwekeze kwenye vitega uchumi vyenye kuleta faida ili waweze kulipa mafao kwa wanachama wao. Michango tu ya wanachama haitoshelezi kulipia mafao. Uzalishaji wa Umeme, licha ya faida kwa uchumi kwa ujumla wake, ni mradi wenye faida kubwa. Hivyo ni eneo ambalo litahakikisha kuwa fedha za wafanyakazi zinakuwa salama na hivyo kuwa tayari kulipa fidia. Kutokana na uwezekaji mbalimbali, ndio maana NSSF leo wanalipa wanachama wao tsh. 80,000 kwa mwezi wakati pensheni ya serikali ni tshs 20,000 tu. Ndio maana NSSF wana akiba ya kuwalipa wanachama wao miaka 50 ijayo bila kupokea mchango wowote kuanzia leo.

Uwekezaji wa NSSF kwenye mgodi wa KIWIRA ili kuzalisha 200MW za umeme na katika mradi wa 300MW kwa kutumia Gesi ni sehemu ya mikakati ya kuliondoa Taifa katika mikataba ya kinyonyaji na makampuni ya kigeni. Uwekezaji huu utaipunguzia TANESCO mzigo wa gharama za kuzalisha umeme na badala yake kuwekeza nguvu zake katika kusafirisha umeme (kuwekeza kwenye miundombinu) na kusambaza umeme kwa wateja. Iwapo tutawekeza vya kutosha kwenye uzalishaji wa umeme kwa kutumia mifuko yetu ya hifadhi ya jamii na TANESCO wakawekeza katika usafirishaji na usambazaji, ni dhahiri tutafikia lengo la kuunganisha zaidi ya nusu ya Watanzania kwenye mfumo wa umeme. Huko ndipo twapasa kwenda!

Written by zittokabwe

March 2, 2011 at 10:22 AM

5 Responses

Subscribe to comments with RSS.

 1. Article nzuri sana kaka, kukosekana kwa umeme kumelicost sana taifa, ivi sasa hali ni mbaya viwanda vinafungwa na watu wanakosa ajira dah, wenzetu wa uganda na kesha wameshasahau matatizo ya umeme, tuamke watanzania!

  Denis

  March 2, 2011 at 11:15 AM

 2. Well,nakushukuru sana kwa kutujuza hili. Naomba utueleze hayo maoni na maelekezo ya kamati yako kwanini hayajatekelezwa mpaka leo tunapata shida ya umeme? Je, Huyo mkapa kama alikopa hizo fedha na wenzake iweje ushauri NSSF imilikishwe mgodi na kufanya huo mkopo kama mtaji? – Hii ni kwa manufaa ya nani? Nadhani Mh. Mkapa anapaswa kulipa deni lake lote alilokopa. Afilisiwe kama anashindwa kulipa. Otherwise naunga mkono hoja zako

  Eng. Magafu

  March 3, 2011 at 12:58 PM

 3. Makala safi sana Mhe. Asante…I think the best and most articulately reasoned argument I have read on this whole matter.

  Kama ni upungufu mimi ningesema tu kwamba NSSF lazma wawe wamefikia maamuzi haya kwa kuona hakuna sekta nyingine ambazo zingewawezesha kupata faida kubwa zaida,at a lower risk, kuliko KIWIRA ( I.e.is it proven with financial modeling that this project is the best use of NSSF resouces,they could be others, including infrasctructure and housing, that could provide better,more secure results).

  Pia naona unapoongelea Malaysia na France ungetufafanulia mfumo wa sekta Yao ya umeme,imawezekana kwamba the regulatory framework and legislative environment are different. Tatizo kubwa la Tanesco ni sheria ambazo zinaibana.

  Mwisho ni kusema tu kwamba the logic kwamba kuokoa dola milioni 7 tuongeze mtaji wa milioni 200 haina mantiki. We need to weigh the risks, NSSF could end losing 200 million plus instead of 7, we need to know the profitability of current operators,hata kwa bei hiyo ya unyonyaji ili tuelewe break even point yetu. Isije huko mbele Tanesco na NSSF walete malumbano ya capacity charges huyu akimkatalia mwenzake kwa madai wote wake chini ya serikali so there’s a need for a subsidy and loss toleration (Mf. Madeni makubwa na sugu ya Tanesco ni wizara za serikali).

  Wachumi

  March 3, 2011 at 9:56 PM

  • Asante sana Wachumi

   Umenisaidia sana kupata hoja za kuuliza. Profitability ya current operators ni muhimu sana kujadiliwa kwani itasaidia kuweka idea in perspective.

   Songas kwa mfano wanasema hawapati faida kwa kuwa sehemu kubwa ya mtaji wao ni madeni. Debt to Equity ratio ni kubwa sana na hivyo they get their loans( loans from sister companies) and declare losses for years. This is massive tax planning!

   Angalizo kuhusu huko baadaye TANESCO na NSSF kugombana ni angalizo muhimu sana. Kuhusu TANESCO kuidai serikali, tumewaeleza TANESCO waweke mita za luku kwenye taasisi zote za serikali kuanzia next financial year.

   zittokabwe

   March 5, 2011 at 1:01 PM

 4. habari mheshimiwa?
  napenda kuchukua nafasi hii kupongeza hatua hiyo mnayoendelea nayo kiushauri, mwanzoni nami nilikaribia kuingia katika mjadala wa kupinga hoja hiyo ya kukabidhi mgodi wa kiwira kwa NSSF. lakini baada ya kusoma maelezo yako ya kina leo hii japo ni muda mrefu umepita lakini nimejifunza mambo mengi muhimu. la msingi mheshimiwa zito ni kuuhabarisha umma kuhusu kila hatua, nionavyo mimi hata wengi wapingao wanapinga kwa kukosa taarifa muhimu kuhusu hali ya mgodi, nishati na uwekezaji wa nje na ndani. kwa kuwa ninyi ni wawakilishi wetu mnapaswa kufanya ufuatiliaji wa kina na hatimaye kutupatia taarifa stahili bila kuzibadilisha kwa manufaa ya watu au kikundi fulani… kwa mtindo huo tunaweza kufikia hatua nzuri ya kimaendeleo… ila pia na ushauri wako ulenge katika kuleta tija ya kweli kwa taifa na hasa kwa NSSF yenyewe….. kila la heri.

  mkoba

  March 19, 2011 at 3:00 PM


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: