Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHESHIMIWA KABWE ZUBERI ZITTO(MB) WIZARA YA MIUNDOMBINU KUHUSU MPANGO NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA BAJETI,KWA MWAKA WA FEDHA 2010/2011

with one comment

___________________

UTANGULIZI:

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kambi ya Upinzani naomba nitoe maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu hotuba ya bajeti ya Wizara ya Miundombinu kwa mwaka wa fedha 2010/2011 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kanuni ya 99(7) toleo la Mwaka 2007.

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni Mhe. Hamad Rashid Mohamed kwa kuniteua kuwa Waziri Kivuli wa Wizara ya Miundombinu kwa kipindi cha takribani miaka mitatu sasa. Namshukuru kwa miongozo yake na kuiweka kambi katika uongozi dhabiti akishirikiana na Naibu wake Dkt. Willibrod Slaa. Namshukuru pia Naibu Waziri Kivuli Mhe. Shamis Bakar Faki kwa kazi yake nzuri katika kamati ya miundombinu na vilevile kwa ushirikiano wake mkubwa name katika kuisimamia serikali kupitia Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni katika Bunge la Tisa imefanya kazi kubwa sana ya kuwasemea Watanzania na hasa Watanzania wasio na sauti na hivyo kuleta mabadiliko makubwa katika uongozi wa Taifa letu. Kambi ya upinzani Bungeni bila ya woga wala upendeleo imekuwa ikisema ukweli kuhusiana na jinsi Taifa letu linavyoongozwa na kuibua maovu yote kwa lengo la kuhakikisha kuwa mlipa kodi wa Tanzania anapata thamani ya kodi anayolipa. Kambi ya upinzani Bungeni imetimiza wajibu wake wa Kikatiba wa kuwa Serikali mbadala kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita na sasa tunatoa rai kwa Watanzania kutukabidhi serikali ili tuweze kuiongoza tofauti na ufanisi zaidi kwa kuondoa ufisadi uliokithiri, kupambana na umasikini kwa kukuza uzalishaji mali viwandani na mashambani na kujenga miundombinu imara.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwashukuru wananchi wa jimbo langu la Kigoma Kaskazini kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa katika kazi zangu. Katika kipindi cha miaka mitano tumefanya kazi kubwa sana ya kuleta maendeleo katika Mkoa wetu wa Kigoma na Jimbo letu la Kigoma Kaskazini. Mwaka 2005 kulikuwa kuna mtandao wa barabara za lami wenye kilomita 8 tu mkoa mzima wa Kigoma, leo kuna mtandao wenye kilomita 80 na ifikapo Oktoba mwaka 2010 kutakuwa na Mtandao wenye kilomita zaidi ya 100 baada ya kukamilika kwa barabara ya Mwandiga Manyovu (Asilimia 90 ya Mtanadao huu wa barabara upo katika Jimbo la Kigoma Kaskazini). Mwaka 2005, kulikuwa na uwezo wa kuzalisha 4MW za umeme pekee, leo tuna uwezo wa kuzalisha 11MW. Mwaka 2005 hapakuwa na Gati hata moja katika mwambao wa Ziwa Tanganyika, leo magati mawili yanajengwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania – moja Kigoma kusini na linguine katika Kijiji cha Kagunga jimboni Kigoma Kaskazini. Mwaka 2005 hatukuwa na Bweni hata moja la Wanafunzi wa kike katika Shule za Sekondari, leo Kigoma Kaskazini peke yake inajenga mabweni 3 katika shule tatu tofauti ili kuhakikishe mabinti wa Kigoma Kaskazini wanasoma bila matatizo. Wakati Rais Jakaya Kikwete ametembelea Mkoa wa Kigoma, ukiachana na miradi ya kimkoa aliyozindua miradi mingine yote ilizinduliwa ni ya Kigoma Kaskazini peke yake. Watu wa Kigoma Kaskazini wanajivunia sana mafanikio haya ambayo yametokea ndani ya miaka mitano tu.

Mheshimiwa Spika, Napenda kurejea kutoa shukrani zangu za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa niaba ya wakazi wote wa Kigoma, kwa kutusikiliza watu wa Kigoma na hususani kwa kunisikiliza mimi binafsi nikiwa Mbunge pekee wa Upinzani wa majimbo kutoka Mkoa wa Kigoma. Maneno aliyoyasema Rais kuwa Serikali haibagui maeneo kulingana na itikadi za vyama, alipokuwa akizindua Mitambo ya Umeme Kigoma ndio maneno ya kiungwana katika demokrasia yeyote duniani. Bado kuna changamoto nyingi sana Kigoma na tutaendelea kuzisemea ili nasi watu wa Kigoma tujione kuwa tupo sehemu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, Natambua kuwa Mkandarasi wa kujenga kipande cha Kidahwe Uvinza katika barabara ya Kigoma Tabora tayari amepatikana. Nawashukuru sana watendaji wa TANROADS na hasa Mkurugenzi Mkuu na Meneja wa Mkoa wa Kigoma kwa kuwa wepesi katika kuhakikisha miradi ya Kigoma inakwenda haraka. Natambua kuwa Fedha zimetengwa katika Bajeti kwa ajili ya kipande cha Kidahwe Kasulu katika Barabara kuu ya Kigoma Nyakanazi. Nawashukuru sana Wizara ya Miundombinu kwa kutenga fedha hizi katika Bajeti na kuwapongeza sana wabunge wote kabisa wa Mkoa wa Kigoma bila kujali itikadi za vyama kwa ushirikiano mkubwa uliopo kuhusu miradi ya miundombinu katika Mkoa wa Kigoma. Ninaiomba Serikali na hasa Wizara ya Miundombinu iharakishe mchakato wa kumalizia malipo ya fidia kwa wananchi waliobomolewa nyumba zao kupisha ujenzi wa barabara hizi.

Mheshimiwa Spika, Kwa Wabunge wa Kigoma tofauti na mimi na kwa michango yao ya kuchochea maendeleo ya mkoa wetu wa Kigoma, mungu atawalipa lakini siwaombei mrudi Bungeni kwani ni lazima kuimarisha demokrasia ya vyama vingi kwa kuchagua wabunge wengi zaidi wa Upinzani na mkoa wa Kigoma ni muhimu na lazima kupata wabunge wengi kutoka kambi ya upinzani ili kupaza sauti ya Kigoma zaidi, jambo ambalo wabunge kutoka CCM wanakwazwa. Hata hivyo tutawakumbuka katika historia kama wabunge mliokuwepo katika miaka muhimu ya mabadiliko katika mkoa wa Kigoma na Mungu awajaalie huko mwendako!

MASUALA YA JUMLA

Mheshimiwa Spika, Sekta ya Usafirishaji (Transport services) ndio sekta inayoonekana ya kimkakati katika uchumi wa Tanzania. Nafasi ya kijiografia ya Tanzania inatoa upendelea wa pekee wa sekta hii kuwa sekta chocheo kwa ukuaji wa uchumi wa Taifa letu. Sekta hii ina mahusiano mazuri na chanya (positive strong linkages) na shughuli nyingine za kiuchumi pia inagawa vizuri faida za ukuaji uchumi (strongly supportive of broad based enabling environment) na inaweza kutengeneza ajira nyingi sana. Sekta hii inajumuisha usafiri wa Reli, Barabara, Anga na usafiri wa Majini. Sekta hii kwa Tanzania ni moja ya sekta zinazokua kwa kasi na mchango wake katika pato la Taifa ni takribani asilimia 7, hii ni zaidi ya mara mbili ya mchango wa sekta ya madini katika GDP na zaidi ya mara sita ya mchango wa sekta ya umeme na gesi katika uchumi.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo sekta ya Usafirishaji imegubikwa na changamoto nyingi sana na ni moja ya sekta ambazo licha ya umuhimu wake haipewi kipaumbele kabisa katika maamuzi ya Serikali. Iliichukua serikali zaidi ya miaka 3 kupata suluhisho kuhusu kitengo cha Makontena katika Bandari ya Dar es Salaam na kusababisha usumbufu mkubwa sana kwa wateja wa bandari yetu na hivyo kupoteza biashara kwa kiwango kikubwa sana. Imeichukua serikali zaidi ya miaka 4 kushughulikia suala la Ubinafsishaji wa Uwanja wa ndege wa KIA na kuinunua kampuni ya KADCO na mpaka sasa bado menejimenti haijawa ya Shirika la Serikali. Imeichukua serikali miaka mitano bila kupata suluhisho kuhusu ubinafsishaji wa Shirika la Reli Tanzania na hata kuweza kumaliza ubinafsishaji huo na kuua kabisa usafiri wa Reli nchini. Inaendelea kuichukua serikali miaka kadhaa kumaliza tatizo la Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na kuhatarisha sana biashara ya utalii nchini.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Miundombinu imekuwa ni Wizara yenye matatizo kuliko wizara zote za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wakati gazeti la Sunday Citizen, liliita Wizara ya Nishati na Madini ‘the most corrupt ministry of the year 2007’, Wizara ya Miundombinu imekuwa ‘the most incompetent Ministry’ katika kipindi chote cha utawala wa miaka mitano ya Awamu ya nne. Hii ni kutokana na hoja kuwa katika wizara hii hakuna maamuzi yanayochukuliwa katika masuala mengi sana na hivyo kusabibisha hasara kubwa kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inamtaka  Waziri wa Miundombinu alieleze Bunge na Taifa kwa Ujumla juu ya utekelezaji wa Program ya Maendeleo ya Sekta ya Usafirishaji (TSIP). Huu ni mwaka wa tatu wa TSIP, Serikali haisemi hatua za utekelezaji ili tuweze kuipima. Kama rasilimali hazielekezwi katika ‘blue prints’ ambazo tumezipanga wenyewe, ni kwa nini tunatumia muda na fedha kuweka mipango hii?

Mheshimiwa Spika, nchi yetu imejaaliwa na Mungu kwa kuzungukwa na Bahari ya Hindi na Maziwa makuu matatu ambayo ni Ziwa Nyasa, Ziwa Tanganyika na Ziwa Victoria. Mungu angeweza kutunyima rasilimali nyingine zote na akatuacha na rasilimali hizi tu na tungeweza kukua kama Taifa kutokana na utajiri unaoweza kuzalishwa na Rasilimali hizi. Hata hivyo Mungu ametujaalia mengine mengi sana kama Madini, Mito yenye kuzalisha Umeme na Watu wapenda amani na wakarimu. Hata hivyo bado hatujaweza kutumia rasilimali hizi kujiendeleza inavyopaswa.

Mheshimiwa Spika, Usafiri wa Reli ni usafiri muhimu sana kwa nchi na hasa kuhusiana na usafiri wa mizigo yenye uzito mkubwa. Hatuwezi kuendelea kamwe kwa kutegemea usafiri wa barabara kusafirisha mizigo yenye uzito mkubwa kama Madini na bidhaa nyingine. Tanzania tuna reli mbili yaani ya TAZARA na ile ya Kati. Wabunge wamezugumza humu Bungeni kwa miaka mitano kuhusiana na adha ya usafiri wa Reli. Kimsingi hatujapata jibu kuhusu Reli ya kati. Wananchi wanaotumia reli kwa usafiri wanapata taabu kubwa. Usafirishaji wa mizigo umeporomoka kwa kiasi kikubwa sana kutoka tani 954 mpaka tani 570 ndani ya mwaka mmoja.

Mheshimiwa Spika, Reli zetu zote zinazosimamiwa na TRL na TAZARA bado zipo katika utaratibu ambao si wa kisasa.  Ukiondoa uwezo mdogo wa kuhimili mizigo yenye uzito mkubwa zaidi, bado upishanaji wa treni unategemea kufika stesheni (single track), Ni muhimu kuwa na treni zinazoweza kupishana bila kufika stesheni kwa kuongeza njia ili angalau ziwe mbili. Lazima pia uwepo mkakati wa makusudi wa kuzifanya reli zote ziwe katika mfumo wa kutumia umeme (electrified railway system) ili kuongeza ufanisi wa usafiri wa reli kwa kuongeza sana kasi, usalama na hata raha (comfortability) ndani ya mabehewa ya abiria.

Mheshimiwa Spika, Kukosekana kwa mfumo wa reli za umeme kumezuia ujio wa wawekezaji walio makini zaidi kwenye sekta ya reli.  Mifumo ya kizamani mno ya reli haivutii kuwekeza kwa faida na ni lazima kuachana nayo haraka. Treni zetu karibu zote zinatumia mifumo ya kizamani ya mawasiliano na ukiondoa simu za mikononi za abiria, wahudumu na madereva wa treni hizo, si rahisi kuona treni yenye mawasiliano bora ya redio au teknolojia.

Mheshimiwa Spika, kama ilivyo viwanja vya ndege kwa usafiri wa anga, Stesheni za Reli zina umuhimu mkubwa sana kwa usafiri wa Reli. Kwa muda mrefu sana Stesheni za Reli zimekuwa ndio maofisi ya Shirika la Reli na pia zimekuwa zinamilikiwa kwa pamoja na Reli. Stesheni za Reli, hasa zile stesheni kubwa kama vile Tabora, Kigoma, Urambo, Mpanda, Kilosa, Dodoma, Morogoro, Tanga, Mwanza na Dar es Salaam zimekuwa hazitumiki kwa asilimia 100 na kwa kweli stesheni nyingine zimekuwa chafu na hazihudumiwi ipasavyo. Nilizungumza suala hili katika hotuba zangu zote mbili zilizopita. Wizara imeweka mkakati gani wa kutumia Stesheni hizi kama vituo vya biashara na mahoteli?

Mheshimiwa Spika, nafasi ya Tanzania kijiografia inatoa fursa kubwa kwa usafiri wa anga kuwa na manufaa kwa Taifa. Hivi sasa Taifa letu lina viwanja vya ndege viwili vya kimataifa yaani Julius Nyerere International Airport na Kilimanjaro International Airport. Kiwanja cha Songwe kinamaliziwa kujengwa. Viwanja vya ndege vya Mwanza, Kigoma, Tanga, Mtwara na Mafia ni viwanja muhimu sana kwa ukuaji wa sekta na uchumi kwa ujumla. Juzi alipokuwa Kigoma Rais wa Jamhuri ya Muungano alisema hadharani na mbele ya wananchi wa Manispaa ya Kigoma kuwa Kiwanja cha ndege cha Kigoma kinajengwa kama kiwanja cha Kimataifa ili kuhudumia nchi za Kongo – Kinshasa na Burundi katika eneo la Maziwa Makuu. Natumaini kuwa watendaji wa Wizara watakumbuka kauli hii ya Rais katika mradi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma.

Mheshimiwa Spika, TCAA waliweka ushindani katika viwanja vyote vya ndege isipokuwa KIA katika suala la ‘ground handling’ ambapo ni Kampuni moja tu ya Swissport inaruhusiwa kutoa huduma. Kwa sababu ya ukiritimba ni rahisi kwa kampuni hii kukataa kutoa huduma kwa makampuni mengine yenye wateja na hata kufanya huduma hizo kuwa ghali sana. Wizara iseme ni lini itaondoa ukiritimba huu ili kuongeza ufanisi katika huduma za usafiri wa anga.

Mheshimiwa Spika, kuna hili suala la hanga pale KIA ambalo linaweza kutumika kwa ajili ya ‘hub’ ya ndege binafsi katika eneo hili la Afrika Mashariki kwa ajili ya kuweka mafuta au kwa ajili ya kuhifadhi ndege kipindi ambacho wenyewe wapo katika mapumziko. Mamlaka ya Viwanja vya ndege TAA imekodisha hanga hili kwa kampuni binafsi. Hata hivyo kampuni hii haiwezi kupeleka ndege katika eneo hili na hivyo kupunguza matumizi ambayo yangeweza kuingiza mapato zaidi kwa nchi. Wizara iondoe vikwazo hivi ili kuhakikisha kuwa nchi yetu inafaidika na uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa Hanga hii.

Mheshimiwa Spika, Kampuni yetu ya Umma ya Air Tanzania (ATCL) ambayo ilianzishwa baada ya kuvunjwa kwa mkataba na Kampuni ya South Africa Airways iliendelea kusuasua katika mwaka uliopita. ATCL ilisafirisha abiria wapatao 60,018 tu mwaka 2009 ikilinganishwa na abiria 207,305 mwaka 2008. Abiria waliosafirishwa na Kampuni binafsi ya Precision Air mwaka 2009 walikuwa 583,000 ambao ni zaidi ya nusu ya abiria wote waliosafirishwa nchini mwaka husika. ATCL haikuweza kufikia hata idadi ya abiria waliosafirshwa na Kampuni ya Coastal Travel 9141,995). Ni mategemeo ya Watanzania kuiona ATCL kama fahari ya Taifa (The National Pride). Hata hivyo hali ya ATCL inatia simanzi sana kwa sisi wapenzi wa sekta ya umma katika maeneo nyeti kama usafiri wa anga.

Mheshimiwa Spika, shirika letu la ndege limekuwa katika wakati mgumu sana kwa kipindi kirefu kutokana na ukata na ukosefu wa fedha kutokana na hali ngumu ya kiuchumi ambayo inalikumba shirika hilo , na hii inatokana na serikali kutenga kiasi kidogo sana cha fedha ili liweze kujiendesha. kitendo cha ATCL kusafirisha nusu ya abiria waliosafirishwa na kampuni moja binafsi kama Coastal Travel na moja ya Ishirini ya abiria waliosafiri kwa ndege nchi nzima ni aibu kwa shirika letu la ndege kwani kama abiria wanaongezeka ilitegemewa kuwa ni shirika letu la ndege lingeweza kujiongezea faida na mapato zaidi kutokana na ongezeko hili la wateja, ila badala yake shirika letu limekuwa na wakati mgumu zaidi kifedha. Waziri wa Miundombinu aliunda kikosi kazi cha kutazama jinsi ya kuokoa ATCL na taarifa yake tayari imekabidhiwa kwa Waziri. Hata hivyo taarifa hii imefanywa siri kubwa na utawala bora unataka taarifa hii kutolewa kwa umma ili kuweza kujua hali ya Shirika lao la umma. Kambi ya Upinzani Bungeni inatamtaka Waziri wa Miundombinu kutoa taarifa hii hapa Bungeni ili wawakilishi wa wananchi waweze kujua.

Mheshimiwa Spika, kwa ,mujibu wa Taarifa ya Msajili wa Hazina kuhusu uwekezaji wa mitaji ya Umma ya Juni 2009, Shirika la Ndege ATCL linadaiwa na kampuni ya Celtic Capital ya Miami USA kiasi cha shilingi 1.1bn kutokana na mkopo ambao haujulikani ulikuwa wa kiasi gani uliochukuliwa 15/12/2006 ili kukodisha ndege 2 Boeing 737-200. Dhamana ya serikali imekwisha na deni halijalipwa . Shirika  la ATCL pia linadaiwa na Wallis Trading Company ya Liberia USD 60,000,000 kwa kukodisha Air bus A320. Deni kwa mpaka sasa limefikia Tshs 13.3bn. Ndege hii ya Airbus ilipelekwa nchini Ufaransa kwa matengenezo na mpaka sasa haijarudi. Wakati serikali inalipa gharama za matengenezo kwa ndege hii, vile vile inatakiwa kulipa gharama za kukodisha ndege hii. Shirika limekufa na madeni yanazidi kuongezeka siku hadi siku. Naitaka Wizara ieleze kwa kina kuhusu madeni haya ya Shirika la ATCL na ni namna gani yatalipwa? Waziri wa miundombinu aeleze pia kwa nini ndege hii ya Airbus haijarudi nchini baada ya matengenezo, gharama za matenegenezo zilikuwa kiasi gani na Serikali imelipa au inadaiwa kiasi gani?

Mheshimiwa Spika, tafiti za masuala ya utalii zinaonesha kuwa kwa nchi zenye Shirika la ndege la kitaifa, asilimia 70 ya mapato yanayotokana na utalii hubakia ndani ya nchi husika ilhali kwa nchi ambazo hazina National Carriers, ni asilimia 30 tu ya mapato yanayotokana na Utalii hubakia katika nchi zao. Ndio maana nchi kama Kenya inapata watalii zaidi na mapato ya Utalii kubakia nchini humo kwa kiwango kikubwa. Hapa nchini kwa kuwa Shirika la Ndege la Taifa limekufa, ni theluthi moja tu ya mapato yanayotokana na Utalii hubakia nchini.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeshindwa kabisa kuona mahusiano haya na ndio maana imeshindwa kupata ufumbuzi kwa miaka 5 iliyopita. Kimsingi Shirika hili Serikali imeliua kwa miaka kumi sasa na kila mwaka linatokea katika ilani ya uchaguzi ya CCM kwamba litaokolewa. Mwaka 2000, ilani ya uchaguzi ya CCM ilisema ATC itabinafsishwa ili kuongeza ufanisi. Ilani ya mwaka 2005 ikasema Serikali italiondoa Shirika katika ubinafsishaji na kuliunda upya. Mwaka 2010, ilani ya CCM itasema Serikali imeamua kulifuta Shirika hili iwapo kauli ya Waziri itazingatiwa kwamba Shirika litafutwa!

Mheshimiwa Spika, ninatoa ushauri kwa Serikali kwamba iwe na mwono tofauti katika suala la Shirika la Ndege la Taifa. Kwa kuwa Utalii unategemea sana usafiri wa ndege na kwamba sekta ya utalii itafaidisha zaidi nchi iwapo kutakuwa na Shirika la Ndege la Umma lenye nguvu.

Mheshimiwa Spika, tunaitaka Serikali ihusishe mashirika ya Umma yenye kuendesha shughuli za uhifadhi katika umiliki wa Shirika la Ndege. Serikali isitoze kodi kwa TANAPA na NCA na badala yake mashirika haya yaruhusiwe kununua hisa za ATCL na kuwekeza mtaji. Sehemu ya mtaji ishikwe na Serikali na itakapofika Shirika kuanza kupata faida wananchi wauziwe sehemu ya hisa za Shirika. Uwekezaji kutoka nje sio mwarobaini wa matatizo yetu yote. Tunaweza kutumia mitaji ya ndani kimkakati ili kuimarisha Shirika la Ndege. Jambo la msingi ni serikali kusafisha vitabu vya Shirika kwa kuchukua madeni yote na kuingiza uwekezaji kutoka mashirika ya umma ya ndani ya nchi.

Mheshimiwa Spika, Ndege ya TGF aina ya Gulfstream imezungumzwa sana hapa Bungeni. Kama wote tunavyofahamu, ununuzi wa ndege hii ambayo pia inayo hadhi ya kutumiwa na Rais wa Jamhuri, ulizua malalamiko mengi mno, hasa bei yake kubwa sana ikilinganishwa na umaskini mkubwa wa Tanzania, pamoja pia na gharama zake kubwa za kimatunzo na kiuendeshaji. Ni mara chache sana Rais wa Jamhuri yetu ameitumia ndege hiyo kwa safari zake nyingi sana za kimataifa, ukiondoa zile za ndani ya nchi.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni nini kinachoendelea kuhusu uwepo mzima wa ndege hiyo na mchanganuo sahihi na wa kina wa faida zake za kiuchumi.  Je, ni faida zipi za kiuchumi nchi yetu imezipata tangu ndege hiyo inunuliwe karibu miaka sita iliyopita.  Ni kwa kiasi gani uwepo wa ndege hiyo umechangia kupungua kwa umaskini wa kupindukia wa wananchi wetu?

BARABARA

Mheshimiwa Spika, Taarifa ya hali ya uchumi inaonyesha kuwa Tanzania ina mtandao wa barabara wenye jumla  km. 85,000 ambapo asilimia 53 zipo katika hali nzuri, asilimia 33 wastani na asilimia 14 katika hali mbaya sana.  Mwaka 2008 KM. 5900 zilikuwa na hali nzuri, 2009 jumla ya KM 7400 ziko katika hali nzuri. Ongezeko hili limetokana na ukarabati wa barabara za zamani na ujenzi wa barabara mpya. Hata hivyo, licha ya juhudi za wakala wa barabara nchini kujenga barabara zaidi, mtandao wa barabara za lami nchini ni KM 5800 tu ambazo ni chini ya asilimia 10 ya mtandao wote wa barabara.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na marumbano yasiyokwisha kati ya wizara ya miundombinu na wakala wa barabara nchini kuhusu muda wa mkurugenzi mkuu. Marumbano hayo yamekuwa yakiendeshwa kupitia vyombo vya habari na masikitiko ni kwamba marumbano hayo hayahusiann na ubora wa barabara zetu. Kwa mfano kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu ya wakandarasi kuchelewa kulipwa hali inayopelekea gharama za ujenzi kuongezeka kutokana na riba au hata wakandarasi kuchelewa kuanza kazi.

Mheshimiwa Spika, taarifa ya mkaguzi na mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu ukaguzi wa barabara (value for money audit 2009), inaonyesha kwamba zaidi ya shs. 36 billioni zimelipwa kama ziada kwa mkandarasi kutokana na hali niliyoieleza hapo juu. Kumekuwa na  kurushiana mpira kati ya hazina, wizara  ya miundombinu  na TANROADS kuhusiana na malipo ya wakandarasi. Lakini ni ukweli kuwa Tanroads hawazalishi fedha bali wao ni watumiaji tu. Wenye fedha ni hazina na wizara, hivyo basi wanaosababisha hasara kwa ucheleweshaji huo ni Serikali na sote ni mashahidi wa amri za viongozi wa Serikali kuhusu kujenga barabara ambazo hazimo katika mpango wa bajeti. Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri atoe maelezo ni kwanini malumbano hayo yanaendeleo kati ya wizara na idara zilizo chini ya wizara yake? Na lini wataacha kulumbana na kufanya kazi za wananchi?

Mheshimiwa Spika, la mwisho ni kuhusu mjadala unaoendelea sasa  wa kupitisha barabara (kama 60km hivi) katikati ya Hifadhi ya Serengeti. Kumekuwa na majadiliano makali kuhusu suala hili, ambayo wakati mwingine yamezaa hali ya uzalendo na pia uzalendo upofu (blind nationalism). Napenda kunukuu maneno ya Mwalimu Nyerere kuhusu uhifadhi kama alivyoyatamka katika Arusha Manifesto mnamo Septemba mwaka 1961 “….In accepting the trusteeship of our wildlife we solemnly declare that we will do everthing in  our power  to make sure that our children’s  grandchildren will be  able to enjoy this rich and  precious hertage”. Maneno haya ya Mwalimu imekuwa ni dira ya wahifadhi wote nchini na suala la Barabara ya kupita hifadhi ya Serengeti lipimwe kutokana lengo hili la kutunza uhifadhi. Suala muhimu la kujiuliza wakati tunafikia kujenga ama kutokujenga barabara hii na hata kuweza kuhatarisha uhifadhi ni je, kama nchi tutafaidika au hatutafaidika?, na je, kuna mbadala au hakuna mbadala wa barabara hii? Tusikimbilie kupeleka lawama kwa wenzetu wa nchi jirani kwamba wanatupiga vita. Au kusema ni chaguo kati ya maendeleo ya mwananchi au wanyama, bali tuamue tukijua tunawajibu wa kiulimwengu wa kutunza utajiri uliopo Serengeti.

HITIMISHO

Mheshimiwa Spika, napenda kurejea hitimisho langu la mwezi Julai mwaka 2007. Kambi ya upinzani inatekeleza wajibu wake wa kidemokrasia wa kutoa maoni na hojaji ili Kambi ya chama kinachotawala ifanyie kazi kwa maslahi ya Taifa. Ninawatahadharisha wenzetu kuwa hali ya kisiasa ya nchi imebadilika sana na kwa kasi. Iwapo walio na serikali watashindwa kutekeleza mabadiliko muhimu ya kisera ili kuendena na upepo wa mabadiliko ya kiuchumi wananchi watawapumzisha. Sisi tunasubiri tupewe ridhaa na wananchi ili tutekeleze mipango hii ambayo wenzetu mmeshindwa kutekeleza. Mawazo mbadala tunayo, nguvu ya kutekeleza mawazo haya tunayo, nia tunayao na tunaweza!

Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa nafasi hii uliyonipa na naomba kuwasilisha.

…………………………………….

Kabwe Zuberi Zitto (Mb)

MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI-

WIZARA YA MIUNDOMBINU

29Juni, 2010

Advertisements

Written by zittokabwe

June 30, 2010 at 1:38 PM

One Response

Subscribe to comments with RSS.

 1. Ni hotuba nzuri sana kwa kweli, ya mtu aliyejipanga vema kuukabili mwanzo mpya!

  Kwa upande wa Chama Chake, ametumia maneno matamu sana ingawa kiasi fulani yamekosa uhalisia kwani ijapo amedai kufurahia mazingira ya kufanya kazi na wenzake huku wao wakiwa hawamkubali, sidhani kama hilo lina ukweli kwani ni kipindi kisichozidi miaka 5 alichofanya kazi kama CHADEMA kwa moyo wake wote!

  Kumbukumbu zinanifikisha pahala kwamba kila mara uchaguzi wa chama ulipokaribia, alikuwaaniimtu wa kuanzisha tafrani ndani ya chama kwa kutamani kugombea nafasi za juu zikiwemo Uenyekiti na Urais, licha ya kujijua kwamba umri wake haumruhusu, ili mradi akitie chama makashkash yasiyokuwa ya lazima sana.

  Kila mara hali hiyo ilipojitokeza na kusuluhishwa, iliacha makovu moyoni mwake na ndani ya chama pia, kwa kumfikiria, “Mwenzetu huyu yukoje?”

  Na mara ya mwisho ni pale alipogundulika yeye na wenzake wakijipanga, safari hii ki vingine, ili kujaribu tena kumwengua Mwenyekiti anayeendelea katika mpango wa siri, kinyume cha taratibu na kalenda ya chama inayopanga lini na namna gani wanachama kuweza kuwania nafasi za uongpzi katika chama.

  Ni kijana mzuri ‘but over ambitious’!

  Namtakia maisha mema ko kote atakakokuwa, na kwa moyo wake wa kulipigania taifa, tutakuwa pamoja, na naahidi kumpatia ushirikiano. Nimeipenda sana ile kauli ya kwamba “Ili mbegu ate kumea ni lazima ife kwanza!” Huyu ni mwanauchumi kama mwanafasihi!

  Kila la kheri Kamanda! Yaliyokutokea CHADEMA yawe fundisho uendako!

  Geoffrey Ng'humba

  March 20, 2015 at 5:26 PM


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: