Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

HOTUBA KWA MASHIRIKA YA HIFADHI YA JAMII KUHUSIANA NA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA UZALISHAJI WA UMEME

with one comment

MAELEZO YA UFUNGUZI YA MWENYEKITI WA KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA MASHIRIKA YA UMMA, ZITTO KABWE KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO KATI YA KAMATI NA WAKUU WA MASHIRIKA YA HIFADHI YA JAMII KUHUSIANA NA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA UZALISHAJI WA UMEME ULIOFANYIKA APRILI 6, 2010 KATIKA HOTELI YA PARADISE CITY, DAR ES SALAAM

1. Tangu Taifa letu lipate uhuru tukikaribia miaka Hamsini, tumekuwa katika jitihada za kuboresha maisha ya Mtanzania kwa kupigana na umasikini, maradhi, ujinga na matatizo mengine ya kijamii. Juhudi hizi zote zinategemea kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kiuchumi ambayo ndiyo msingi wa nyanja zingine za maendeleo. Shughuli za kiuchumi zikiongezeka, uchumi wa nchi unapanuka na maisha ya wananchi yanaboreka. Vile vile shughuli za uchumi zikidumaa, maisha ya wananchi
yanadumaa pia.

2. Maendeleo ya kiuchumi yanaenea katika masuala ya viwanda, kilimo, usafirishaji, uchimbaji wa madini na huduma nyingine za kiuchumi na kijamii. Ufanisi katika sekta hii unategemea huduma wezeshaji(enablers) kuu za miundombinu, nishati na teknolojia ya habari na mawasiliano. Taasisi wa Economic Intelligence Unit, katika Taarifa yake ya mwezi Machi mwaka 2010 inakadiria kuwa uchumi wa Tanzania utapanuka maradufu katika ya mwaka 2005 na 2011 (GDP doubles from 14bn USD in 2005 to 28bn USD in 2011). Huu ni ukuaji mkubwa sana wa uchumi wa nchi katika kipindi kifupi. Huduma wezeshi nazo zinapaswa kukua kuwiana na kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.

3. Sisi sote tutakubaliana kuwa nishati ya umeme in nafasi kubwa sana katika ufanisi wa maendeleo ya viwanda, huduma zote za kiuchumi,mawasiliano na maisha ya kijamii. Pamoja na umuhimu huu, bado huduma hii ya umeme haijawafikia wananchi walio wengi na haiaminiki katika zile sehemu ambazo huduma imefika. Matokeo yake ni kuwa maendeleo ya Taifa letu yako katika shaka kubwa. Uwezo wa sasa (installed capacity) ni wa kuzalisha 900MW. Hata hivyo, ni 600MW peke yake ndio zinazalishwa hapa nchini. Hii inapelekea kuwapo kwa nakisi (deficit) ya zaidi ya 300MW za umeme.

Mazingira ya sasa ya uzalishaji wa umeme hapa nchini ni hatarishi kwa Taifa kwani hakuna umeme wa akiba na matokeo yake ni njia za kusafirisha umeme kuzidiwa na hivyo kupoteza umeme mwingi sana katika usafirishaji. Takwimu zinaonesha kuwaasilimia 24 ya umeme unaozalishwa hupotea katika usafirishaji, hii ni sawa na kuendesha mashine moja ya Kituo cha Kidatu, yenye uwezo wa kuzalisha 50MW, kwa mwaka mzima bure. Kifedha hii ni sawa na kupoteza shs 100bn kila mwaka.

Upotevu huu wa umeme unaosababishwa na uchakavu wa njia zakusafirisha umeme na kuzidiwa kwa gridi kwa kutokuwepo na umeme waakiba, haukubaliki hata kidogo katika Taifa lenye kujali maendeleo ya kiuchumi.

4. Shirika letu la TANESCO limejitahidi sana kutoa huduma ya umeme hapa nchini licha ya changamoto mbalimbali. Changamoto hizi zimepelekea Shirika kufikisha umeme kwa Watanzania asilimia 14 tu na wazalishaji wengi wa Viwandani wanalalamika juu ya ubora wa umeme na uhakika wake. Miongoni mwa sababu za TANESCO kushindwa kukidhi mahitaji ya umeme ni ukosefu wa mtaji wa kutosha katika kuzalisha na kutawanya umeme.

Tunaelewa kuwa taasisi za hifadhi za jamii zimetoamchango mkubwa kwa TANESCO kwa kutoa mkopo wa shilingi bilioni 300 kwa ajili ya kurekebisha mtaji wa TANESCO. Kumekuwa na juhudi kwa upande wa TANESCO katika kusafisha vitabu vya hesabu na hata kuweza kupunguza hasara kutoka Tshs. 162bn mwaka 2006, Tshs. 67bn mwaka 2007 na mpaka Tshs. 21bn mwaka 2008. Tumetaarifiwa kuwa, kufuatia mgawo wa umeme wa mwezi Oktoba mwaka 2009 na sababu nyinginezo, Shirika limeongeza hasara na hata kufuta ‘operating profit’ iliyokuwa imeanza kupatikana. Sababu kubwa sana ya hasara kwa TANESCO ni gharama kubwa sana za mauzo ya umeme (Cost of sales) na hii inatokana hasa na gharama za kununua umeme kutoka Wawekezaji binafsi (IPPs). Nimejulishwa pia kuwa kun achangamoto ya uchache wa Gesi kwa ajili ya kuzalisha Umeme hapa nchini. Ninaamini kuwa uwepo wa Shirika la TPDC katika mkutano huu utasaidia sana kupata ufafanuzi wa jambo hili na kuona njia za kutatua.

5. Kwa upande mwingine, taasisi za hifadhi ya jamii zina kiasi kikubwa cha fedha ambazo huwekeza katika miradi mbalimbali ili kuboresha mafao ya wanachama wake. Tumeelezwa kuwa taasisi za hifadhiya jamii zina aina ya miradi inayofahamika kama Socially Responsible investments (yaani miradi yenye faida kwa jamii) na Economically Targeted Investments, (yaani miradi yenye kuchochea uchumi). Ninaamini kuwa uwekezaji katika uzalishaji wa umeme ni mojawapo ya miradi hii tuliyoitaja.

Taarifa ya Shirika la OECD ya mwaka 2009 (OECD working paper on Insurance and Pensions no. 32 – Pension FundsInvestment in Infrastructure) inaonesha kuwa Ulimwenguni kote mifuko ya hifadhi ya Jamii sasa inaelekeza uwekezaji katika, pamoja na miradi mingine ya miundombinu, uzalishaji na usambazaji wa umeme. Mwelekeo huu unatokana na ukweli uliothibitishwa kisayansi kwamba uwekezaji katika maeneo haya unalipa (Higher and stable returns), ulinzi dhidi ya kuyumbayumba (protection against volatility), ulinzi dhidi ya mfumuko wa bei na kusambaza uwekezaji (diversification of portfolios). Hivyo, uwekezaji katika uzalishaji wa umeme hutoa mapato na faida ya muda mrefu ambayo inaendana kabisa na madai ya muda mrefu ya mifuko ya Pensheni (Yield Long-term predictable revenue stream that match liability of a Pension Fund). Nchi za Jumuiya ya Ulaya kama Uholanzi,Uingereza nk, na vile vile nchi za Mashariki ya mbali kama vile Malaysia sasa zinafaidika na uzalishaji mkubwa wa umeme kutokana na uwezekaji wa mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Ninaamini kuwa Tanzania inaweza kufaidika sana na uwekezaji katika eneo hili kutokana na fedha za ndani na hivyo kupunguza gharama za kununua umeme na hasa ‘capacity charges’.

6. Ninachukua nafasi hii kuzishukuru taasisi zote za hifadhi ya jamiikwa michango yake katika kuendeleza miradi mbalimbali ya nchini, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, nyumba za TPDF, Polisi n.k.

Uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma unaokaribia zaidi ya Tshs 800bn hauna mfano katika eneo lote la Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara. Uwekezaji huu uliofanywa kwa miaka mitatu ni sawa na Uwekezaji wa kutoka nje (FDI) hapa nchini wa miaka kumi ya 1995 – 2005. Vile vile ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ni uwekezaji mkubwa na wapekee tangu ujenzi wa Reli ya TAZARA mwaka 1975. Ninawashukuru sana kwa kutimiza wajibu wenu huo kwa Taifa letu.

7. Sasa, ninachukua fursa hii kwa niaba ya Kamati ya POAC kuziomba Taasisi hizi za Pensheni zielekeze vitega uchumi vyao katika uzalishaji wa umeme ili kulipunguzia Taifa adha ya nishati ya umeme. Mwakani Taifa letu linafikisha miaka 50 toka Uhuru. Tungependa kuona kuwa wakati tunasherehekea miaka 50 ya uhuru tusherehekee tukiwa naangalau zaidi ya 1000MW za umeme zinazozalishwa na kutumika na Wananchi, Viwanda na Migodi. Ingekuwa ni heshima kubwa kwa Waasisi wa Taifa letu kama moja ya miradi itakayozinduliwa katika sherehe za nusu karne ya Uhuru uwe ni mradi mkubwa wa kuzalisha umeme unaomilikiwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

8. Ninavyofahamu mimi ni kuwa miradi hii ni mizuri kibiashara na Taasisi hazitafanya makosa kuwekeza katika sekta hii. Ninaiomba Serikali kupitia Wizara zake mbalimbali, hasa Wizara ya Nishati na Madini na Wizara ya Fedha na Uchumi, kutoa vivutio na ushirikiano wake mkubwa kuziwezesha Taasisi hizi kufanya hivyo.

9. Ninafungua rasmi kikao hiki cha mashauriano kati ya Kamati ya POAC, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, TANESCO, TPDC na Serikali.

Asanteni kwa kunisikiliza.

Zuberi Zitto Kabwe (MB)
Mwenyekiti,Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma
Dar es Salaam, Aprili 6, 2010

Advertisements

Written by zittokabwe

May 25, 2010 at 5:37 PM

One Response

Subscribe to comments with RSS.

  1. […] This post was mentioned on Twitter by Thisyear Magazine, Zitto Zuberi Kabwe. Zitto Zuberi Kabwe said: HOTUBA KWA MASHIRIKA YA HIFADHI YA JAMII KUHUSIANA NA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA UZALISHAJI WA UMEME: http://wp.me/pRboX-l […]


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: